Header

Hatua ambazo Mungu anachukua anapomwokoa mwenye dhambi

Biblia inafundisha wazi kwamba tunazaliwa tukiwa wenye dhambi na tukiwa hatuwezi kuyaelewa mambo ya kiroho na bila kutamani kabisa wokovu. Kwa hivyo ni jukumu la Mungu mwenyewe katika neema yake kufanya kazi ndani ya mioyo yetu na kutuleta kwa Yesu Kristo ambaye ndiye Mwokozi pekee wa wenye dhambi. Katika sehemu hii tutaona ni namna gani Mungu anamwokoa mwenye dhambi.

1. Jamabo la kwanza ambalo Mungu anafanya ili amwokoe Mwenye dhambi ni kuangaza mwanga katika mawazo yake ya giza. Biblia inasema, “Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang’aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso ya Yesu Kristo” (2 Wakorintho 4:6). Katika kila hali, Roho Mtakatifu hutumia neno la Mungu kufanya mambo haya yote (Zaburi 119:130). Pia wakati huo huo pazia unaondolewa kutoka moyoni mwa mtu (2 Wakorintho 3:15,16) na halafu Bwana anafungua moyo wake ili alipokee neno lake (Matendo 16:14). Mambo haya yanapofanyika mtu huona hali yake ya kweli ambayo ni mbaya sana kwa sababu ya dhambi zake. Kabla ya kuonyeshwa dhambi zake, mtu huyu inawezakuwa alikuwa amebatizwa na kuwa mshirika wa kanisa, ama inawezekana alikuwa mhubiri. Mambo ya kuona hali yake ya dhambi yanamfanya kuona jinsi alivyo mwenye dhambi na jinsi moyo wake ulivyo mwovu (Yeremia 17:9) na kwamba yeye hafai kamwe kusimama mbele za Mungu mtakatifu. Huu ndiyo wakati mtu anaelewa kwamba kazi zake zote ambazo alikuwa anadai kwamba ni nzuri, anatambua kwamba ni takataka tupu (Isaya 64:6) na kwamba yeye anafaa kuwa jahanum kwenye moto unaowaka milele. Mambo haya yote anayaona kwa sababu amefunuliwa jinsi yeye alivyo na kuonyeshwa kwamba hakuna chochote ndani yake ambacho anaweza kutumainia.

Kwa sababu ya mwanga ambao Mungu ameugaza ndani ya mtu huyu na kwa usaidizi wa Roho Mtakatifu mtu huyu anaelewa sasa kwamba yeye ni mwenye dhambi mkuu sana na anahitaji tu Mwokozi Yesu Kristo. Roho Mtakatifu huwa anamwongoza mtu huyu kwa Bwana Yesu Kristo ili aweze kuomba msamaha wa dhambi zake, kuoshwa dhambi zake, kupewa amani, kupewa haki na pia kupewa nguvu. Mambo yanayofuata kutokana na tukio hili ni kutubu dhambi, kubadilika kwa maisha kwa sababu yeye sasa ni kiumbe kipya.

Je, katika maisha yako umewahi kuhisi jambo kama hilo ambalo nimeeleza? Ikiwa jibu lako ni la, inawezekana kuwa wewe bado hujaokoka. Mwombe Mungu akuonyeshe dhambi zako saa hii.

2. Jambo la pili ambalo Mungu anafanya anapomwokoa mtu ni kwamba Yeye anadhibiti maisha yake yote. Kwa kawaida wanadamu wanajipenda sana na wanapenda mambo ya ulimwengu huu sana kuliko Mungu (2 Timotheo 3:2,4). Mtu ambaye ameokoka huwa anabadilishwa tamaa zake kwamba mambo ya Mungu ndiyo yanampendeza zaidi kuliko mambo ya ulimwengu. Yeye anapewa tamaa ya kupenda mambo ya Mungu sana kuliko mambo mengine. Kwa hivyo upendo wa Mungu kwake unakuwa ndiyo kitu muhimu sana kwa moyo wake. Mtu ambaye ameokoka, moyo wake unavutiwa sana kwa watu wote wa jamii ya Mungu bila kujali uraia wao, kabila lao ama kanisa lao. Hii ndiyo inakuwa dhihirisho kwamba kweli mtu huyu ametoka katika giza la dhambi na ameingia uzimani kwa sababu anawapenda mandugu zake (1 Yohana 3:14).

Je, wewe unahisi hivyo kuwahusu wakristo wenzako kila mahali? Jichunguze kuambatana na chaguo ambazo unafanya: jinsi unachagua kazi utakayoifanya, mahali unakoishi, shule ambayo utapeleka watoto wako kusoma ama marafiki wako.

3. Jambo la tatu ambalo Mungu anafanya wakati anamwokoa mtu ni kumwezehesha mtu kuamua. Kwa kawaida uamuzi wa mwanadamu umefungwa kwa sababu ya utumwa wa dhambi. Baada ya kuzaliwa mara ya pili, uamuzi wa mtu unabadilika na mtu anaanza kushughulika na mambo ya Mungu. Mungu anapomwokoa mtu kwa neema yake, huwa anampatia moyo mpya na roho mpya ambayo itamwongoza katika kutii sheria zake. Hizi zote ni baraka za Agano Jipya ambazo Mungu aliahadi watu wake (Ezekieli 36:26-27). Kwa sababu mtu huyu amewekwa huru kutoka kwa dhambi, sasa yeye anaanza kufurahia kutii sheria za Mungu. Yeye sasa anaamua kwamba atamtii Kristo katika kila jambo hata ikiwa itamgharimu.

Je, wewe unafurahia sana kumtii Mungu katika kila jambo kila wakati? Kwa mfano, wewe unaiweka siku ya Sabato kuwa takatifu na kuwa siku ya kumtumikia Mungu tu, ama unatumia wakati fulani wa siku hiyo kufanya mambo yako ya kujifurahisha mwenyewe?

4. Jambo la nne ambalo Mungu anafanya anapomwokoa mtu ni kubadilisha tabia ya mtu huyo kabisa na kumfanya kuwa kiumbe kipya (2 Wakorintho 5:17). Kama vile mti unavyojulikana kwa matunda yake, imani ya mtu ambaye ameokoka inajulikana kwa sababu ya tabia yake njema. Baada ya kuzaliwa mara ya pili mtu hubadilika na kuanza kuishi maisha ya kumtumikia Mungu. Biblia inasema, “Kama mkijua kwamba Yeye ni mwenye haki, mwajua kwamba kila atendaye haki amezaliwa na Yeye” (1 Yohana 2:29). Lengo kuu la kila mtoto wa Mungu ni kumpendeza Baba yake wa mbinguni kila wakati hata ikiwa lengo hili halionekani na watu katika maisha yake. Hata ikiwa lengo lake la kumpendeza Mungu halionekani na watu, yeye anaendelea tu kukaza mwendo ili aweze kufikia ile alama ya ushindi iliyowekwa ili aweze kupata tuzo ambayo ameitiwa huko juu mbinguni katika Kristo Yesu (Wafilipi 3:12,14).

Je, umeelewa ya kwamba nilikuwa ninaeleza kuhusu mkristo wa kweli katika kifungu hiki? Na je, wewe ni mkristo? Ikiwa wewe ni mkristo, mshukuru Mungu sana. Ikiwa wewe si mkristo mwombe Mungu akuokoe saa hii.

Mungu alipanga ndoa kwa ajili ya utukufu wake katika maisha ya watu wake

Nimechukua fursa hii kuandika kuhusu ndoa kwa sababu ninapotazama nchini mwetu na ulimwenguni kote, watu wengi hawafahamu kabisa ndoa ni nini na ni kwa nini Mungu alianzisha ndoa. Ni jambo la kuhuzunisha kwamba watu wengi huwa hawaheshimu ndoa kwa sababu wao wenyewe huwa hamheshimu Mungu.

Katika sura hii tutatazama ni nani aliyeanzisha ndoa na ni kwa nini alianzisha ndoa. Haya ndiyo yatakuwa mafundisho ya kwanza ambayo yataendelea katika matoleo mengine kuhusu ndoa na kuishi maisha ya ndoa.

Je, ni nani aliyeanzisha ndoa na ni kwa nini alianzisha ndoa?

“Bwana Mungu akasema, 'Si vema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa. “Kisha Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanamume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanamume.” (Mwanzo 2:18,22).

1. Bwana Mungu aliona kwamba mwanamume alikuwa na hitaji la msaidizi: “Bwana Mungu akasema, 'Si vema huyu mtu awe peke yake.”

Bwana Mungu ambaye ndiye mwumba wa mbingu na nchi anaona kila kitu na anafahamu kila jambo katika kila hali. Katika kitabu cha Mwanzo sura ya 2, tunasoma kwamba Mungu aliumba kila kitu na akampa Adamu jukumu ya kupatia kila kiumbe jina. Miongoni mwa viumbe hivi hakuna hata kimoja ambacho kilipatikana kuwa na uwezo wa kumsaidia Adamu. Mungu aliona hivi na kwa hivyo tunasoma kwamba alimwumba Hawa na akamleta kwa Adamu.

Hii inatufundisha kwamba watu wa Mungu kila wakati wanafaa kuwa na imani ndani ya Mungu kwamba atawatosheleza wakati wa mahitaji yao. Ni lazima tumwamini Mungu katika uamuzi wetu kuhusu ndoa. Ni lazima kila wakati tutafute kuongozwa na kushauriwa Mungu wakati tunataka kuoa au kuolewa. Tusiwahi kuwaza kwamba Mungu huwa hatuelewi na kwamba pia huwa hataki tuwe katika ndoa. Hakuna mtu ambaye anaweza kuwaleta pamoja watu katika ndoa isipokuwa Mungu. Mungu anajua ni nani ambaye anafaa katika maisha yetu kuwa mke au mume. Mungu anajua kwamba unataka mke au mume na kwa wakati ufao, atamleta yule ambaye anakufaa.

Usitegemee yale ambayo unayaona kwa macho yako ya kiasili kama urembo, maumbile ya mwili, kabila au rangi. Tegemea tu Mungu. Usikimbilie kuwa katika uhusiano na mtu yeyote. Tafuta kuongozwa na kusaidiwa na Mungu. Usianzishe uhusiano wa mapenzi kama wakati wako bado haujafika. Je, unataka kuepuka matatizo mengi na machozi mengi? Tafuta ushauri wa Mungu. Usikate tamaa, endelea kumwomba Mungu na kwa wakati ufao, atakujibu.

Hii inatuonyesha jinsi Mungu anavyojali sana watu wake.

2. Mungu alimleta mwanamke kwa sababu yeye ndiye alifaa kuwa msaidizi wa mwanamume: “Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa mwanamume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanamume.”

Miongoni mwa viumbe vya Mungu ambavyo Mungu aliumba, hakukuwa na msaidizi aliyefaa kwa Adamu. Kwa hivyo alimwumba mwanamke kutoka kwa ubavu ambao alitoa kwa mwanamume. Baada ya kumwumba mwanamke, Mungu alimleta kwa Adamu. Adamu alipewa mke bila matatizo yoyote na bila yeye kulipa lolote au kutoa chochote.

Mke mwema ni zawadi kutoka kwa Mungu. Adamu sasa hakuwa peke yake. Mungu alikuwa ameshughulikia upweke wake. Biblia inasema kwamba kila zawadi nzuri inatoka kwa Mungu. Wakati huu, Mungu alikuwa ameanzisha ndoa ya kwanza ulimwenguni na ndoa hii ilikuwa imekamilika kwa sababu ilitendeka kabla ya dhambi kuingia ulimwenguni.

Kusudi la ndoa ni urafiki wa ndani sana. Ni aibu sana na huzuni mkubwa sana wakati tunawasikia na kuwaona watu ambao hawana shukurani kwa Mungu kwa kuanzisha ndoa. Watu hawa, huwapiga na wanawatesa mabibi wao na mabwana wao. Watu wengi katika ulimwengu huu huwafahamu kwamba ndoa ni kitu kitakatifu. Wao huoa leo na kesho wao huachana. Wao huzungumza vibaya kuhusu ndoa kana kwamba ni mwanadamu ambaye aliianzisha. Unapotazama nchini mwetu na ulimwenguni leo, utaona kwamba katika ndoa hakuna urafiki kamwe. Watu wengi wanaoa na kuolewa kwa sababu zisizofaa. Kwa mfano wengine wanaoa na kuolewa kwa sababu ya tamaa mbaya, wengine kwa sababu ya kulazimishwa na watu wa jamii zao, wengine nao kwa sababu wanataka waonekane kwamba wameolewa au wameoa, wengine kwa sababu ya pesa na mali, wengine pia wako na sababu nyingi ambazo msingi wake si neno la Mungu. Hii ndiyo sababu ndoa mingi za leo ni mahali pa vita. Katika ndoa hizi hakuna amani, furaha wala urafiki. Ndoa hizi ni kinyume na jinsi Mungu alivyopanga toka mwanzoni.

Biblia inatupatia mfano mkuu wa ndoa ya kweli na huu ni Kristo Yesu akiwa Bwana arusi na kanisa lake likiwa bibi arusi. Kristo Yesu ndiye rafiki mwema ambaye tunafaa kufuata na kujifunza kutoka Kwake. Kristo Yesu alikufa kwa ajili ya kanisa lake, Yeye anaishi akiliombea kanisa lake na Yeye anarudi kulipeleka kanisa lake nyumbani. Mtazame Kristo Yesu pekee kwa sababu Yeye ndiye mfano ambao tunafaa kuufuata.

3. Mungu alipanga ndoa kati ya mume mmoja na mke mmoja pekee: “Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanamume, akaleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume.”

Ni mwanamke mmoja ambaye aliletwa kwa Adamu na siyo wanamwake wengi. Mwanamke aliletwa kwa mume mmoja na siyo kwa waume wengi. Kuwa na zaidi ya mke mmoja au kuwa na zaidi ya mume mmoja ni dhambi machoni pa Mungu. Wewe usimtazame Daudi au Solomoni au wengine katika Agano la Kale bali tazama mpango wa Mungu katika ndoa ya Adamu na Hawa. Kuwa na wake au waume wengi ni kisingizio cha wale ambao wana tamaa mbaya na hawana tunda la Roho Mtakatifu ambalo linajumlisha kuwa na kiasi (Wagalatia 5:22-25).

Ndoa pia si kati ya watu wawili wa jinsia moja: “Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta mwanamke kwa huyo mwanamume.” Mungu alimleta mwanamke kwa Adamu, si mwanamume. Ni uovu wa hali juu sana kwamba watu wameamua kuenda kinyume na mpango wa Mungu wa ndoa na wale ambao wanafanya mambo haya, wasipotubu, wataenda jahanum. Mungu atawahukumu na hasira Yake itawamwagikia ikiwa wataendelea kukataa kutubu dhambi zao.

Je, tunafaa kuishi aje kulingana na mafundisho haya.

1. Ni lazima kwanza tutafute wokovu kupitia kwa Kristo Yesu.

Mtu ambaye hajaokoka, hawezi kamwe kumpendeza Mungu katika ndoa yake. Ikiwa tunataka kumpendeza Mungu, ni lazima tumwamini yule ambaye amemtuma ambaye ni Kristo Yesu. Mungu anapendezwa tu wakati tunafanya kazi zetu zote ndani ya Kristo. Hakuna yeyote ambaye anaweza kumpendeza Mungu asipokuja kwake kupitia kwa Kristo Yesu. Ni Kristo ambaye Mungu Baba amemtia muhuri (Yohana 6:27).

Njoo kwa Kristo leo, kwa sababu bila Yeye, huwezi kumpendeza Mungu kwa matendo yako mazuri katika ndoa yako au katika jambo lingine lolote.

2. Ni lazima tutafute kumletea Mungu utukufu kupitia kwa Kristo Yesu.

Katika kila jambo kwa gharama yoyote ile, lazima tutafute kumtukuza Mungu kupitia kwa Kristo. Hatuwezi kuwa na ndoa mzuri ikiwa ndoa haimletei Mungu utukufu. Usitafute kuufurahisha ulimwengu kwa sababu hautawahi kufurahishwa nawe. Usitafute kufurahisha watu wa jamii yako katika ndoa yako, kwa sababu ndoa ni kati ya watu wawili tu, mume mmoja na mke mmoja. Tafuta kumfurahisha Mungu pekee. “Ye yote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Ye yote ahudumuye maneno hana budi kuhudumu kwa nguvu zile apewazo na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo” (1 Petro 4:11).

Ishara za Mkristo wa Kweli.

1. Yule ambaye anamwamini Yesu Kristo ako na amani na tumaini.

Biblia inasema, “Kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo; Sasa sisi ambao tumeamini tunaingia katika ile raha” (Warumi 5:1; Waebrania 4:3). Yule ambaye ameokoka, dhambi zake zote zimesamehewa na hatia yake yote imeondolewa. Dhamira yake sasa haina mzigo wa dhambi. Yeye sasa ako na ushirika na Mungu na ni rafiki ya Mungu. Yeye sasa haogopi kifo, bali anaweza kungojea ile siku atakufa bila uoga. Mafundisho ya siku ya hukumu na maisha ya milele hayana taabu kwake sasa. Kifo sasa si kitu cha kuogopa kwake. Ile siku Yesu Kristo atarudi na vitabu vitafunguliwa, hakuna dhambi yoyote ambayo itapatikana katika kitabu chake. Yeye atakuwa na Mungu milele, tumaini lake ni la mbinguni, yaani mji ambao hauwezi kutingishwa.

Pengine yeye hafahamu kamili haya mambo yote, na pengine kuna wakati maishani mwake ambapo yeye ako na shaka kama kweli ameokoka. Yeye ni kama mtoto mchanga ambaye baba yake ni tajiri sana na yeye ni mrithi wa utajiri huu. Lakini hata kama yeye haelewi mambo haya yote na hata kama kuna wakati ambapo yeye ako na shaka, bado yeye anaweza kusema, “mimi niko na tumaini ambalo halitanikatisha tamaa” (Warumi 5:5).

2. Yule ambaye anamwamini Yesu Kristo ana moyo mpya.

Biblia inasema, “Kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya; Wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio Jina Lake. Hawa watoto wamezaliwa si kwa damu wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu; Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ndiye Kristo amezaliwa na Mungu” (2 Wakorintho 5:17; Yohana 1:14-15; 1 Yohana 5:1). Yule ambaye ameokoka sasa hana ule utu ambao alizaliwa nao. Yeye amebadilishwa na kufanywa mpya na kugeuzwa katika mfano wa Yesu Kristo mwenyewe. Yule ambaye anajali tu vitu vya dunia na hajali hata kidogo vitu vya ufalme wa Mungu hana imani ya ukweli.

3. Yule ambaye anamwamini Yesu Kristo ni mtu mtakatifu katika moyo wake na katika maisha yake.

Biblia inasema kwamba Mungu anatakasa mioyo ya watu wake kwa imani na kwamba watu wake Mungu wanatakaswa kupitia kwa imani na kwamba, “Kila mmoja mwenye matumaini haya katika Yeye hujitakasa, kama vile Yeye alivyo mtakatifu” (Matendo ya Mitume 15:9; 26:18; 1 Yohana 3:3). Yule ambaye anamwamini Yesu Kristo anapenda vile vitu ambavyo Kristo anavipenda na anavichukia vile vitu Kristo anavichukia. Upendo wa moyo wake ni kutii amri zake na kupuuza kila dhambi. Tamaa yake ni kutafuta vile vitu ambavyo ni vya haki na kweli na safi na vyema; na kujitakasa kutoka kwa uchafu wa aina yoyote. Yeye anajua kwamba yeye bado hajakamilika na kwamba maisha yake ya kila siku ni maisha ya vita dhidi ya dhambi ambayo imebaki ndani mwake. Lakini kila siku yeye hupigana vita na dhambi na hukataa kutumikia dhambi. Ikiwa mtu hana utakatifu moyoni mwake na maishani mwake, tunaweza kujua kwa hakika kwamba yeye hana imani ya kweli ndani mwake. Yule ambaye anaishi maisha ya dhambi bila kupigana na dhambi, hajaokoka!

4. Yule ambaye anamwamini Yesu Kristo hutenda mambo mema.

Biblia inasema kwamba imani ambayo ni ya kweli itazaa matunda mema kwa njia ya upendo (Wagalatia 5:6). Yule ambaye ako na imani ya kweli ndani yake hawezi kuwa mtu mnyonge au mtu wa kukaa-kaa tu na kusema yeye ameokoka. Imani yake itamwongoza kutembea katika nyayo za Bwana wake ambaye alienda “huku na huko akitenda mema” (Matendo ya Mitume 10:38). Imani yake bila kukosa itamwongoza mtu katika maisha ya ukristo. Ile kazi ambayo atafanya, pengine watu wengine wa dunia hawataona, na pengine kazi yake njema itakuwa si mambo makubwa kama kutoa pesa nyingi kanisani. Lakini Mungu anaona kila kitu ambacho anafanya katika ufalme wake na Yeye hatasahau kazi yake. Mtu akisema ako na imani lakni awe hana matendo mema ambayo imani yake imezaa, basi imani yake si ya kweli. Mtu ambaye anajijali tu na ni mnyonge hana haki ya kusema ameokoka!

5. Yule ambaye anamwamini Yesu Kristo atashinda ulimwengu.

Biblia inasema, “Kwa maana kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Huku ndiko kuushinda kuushindako ulimwengu, yaani, hiyo imani yetu” (1 Yohana 5:4). Yule ambaye ameokoka hatafuata mawazo ya dunia kuhusu ni nini uongo na ni nini ukweli. Yeye hafuati nyayo za dunia katika mambo kama ni nini mtu anapaswa kufanya katika kazi yake na biashara yake. Pia yule ambaye ameokoka hatafuti utukufu kutoka kwa watu wa dunia na hajali hata kama watu wa dunia wanamdharau. Yeye hafuati anasa za dunia hii au vitu vya dunia hii. Yeye anatazama vile vitu ambavyo macho ya wanadamu hayawezi kuviona. Yeye hutazama Mwokozi wake ambaye wakati hu haonekani lakini siku moja atarudi na kuonekana na watu wote wa ulimwengu. Ikiwa mtu ako na upendo wa dunia moyoni mwake, basi yeye hana imani ya ukweli. Yule ambaye anapenda sana dunia na vitu vyake na anasa zake, hajaokoka.

6. Yule ambaye anamwamini Yesu Kristo ana ushuhuda ndani mwake kwamba kweli yeye ni mtoto wa Mungu.

Biblia inasema, “Kila mtu amwaminiaye Mwana wa Mungu anao ushuhuda ndani mwake” (1 Yohanna 5:10). Tunapaswa kuwa waangalifu sana kuhusu jambo hili kwa sababu hili jambo la ushuhuda wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu si jambo rahisi kuelewa. Lakini Biblia inatufundisha kwamba yule ambaye ameokoka kwa ukweli na ana imani ya ukweli ndani mwake atahisi mambo haya moyoni mwake. Atahisi mambo haya kwa sababu ana imani ndani ya Yesu Kristo na imani hii ndiyo chanzo cha hisia hizi. Yule ambaye hajaokoka anaweza kusema kwa mdomo wake kwamba yeye ana imani, lakini moyoni mwake atajua kwamba kuna makosa hapa, na kwamba yeye kwa ukweli hana imani. Yule ambaye ameokoka atakuwa na Roho Mtakatifu ndani mwake na yeye atajua ndani ya moyo wake kwamba yeye amefanywa mtoto wa Mungu. Yeye ndani mwake atajua bila shaka kwamba ana ushirika wa kweli na Mungu Baba na kwa hivyo hatakuwa na hofu mbele za Mungu.

7. Yule ambaye anamwamini Yesu Kristo atamheshimu sana.

Biblia inasema, “Kwa ninyi mnaoamini, Yeye ni wa thamani” (1 Petro 2:7). Katika mstari huu Biblia haisemi kwamba kwa wale ambao wanaamini ukristo ni wa thamani au injili ni ya thamani au wokovu ni wa thamani, bali inasema kwamba kwao Kristo mwenyewe ni wa thamani. Yule ambaye ameokoka anamwamini Kristo mwenyewe na imani yake iko ndani ya Kristo na haiko ndani ya vitu vingine. Yeye sasa ni mtu wa Kristo na ana uhusiano na Kristo na anashiriki naye Kristo kila wakati. Maisha yake ni maisha ya imani ndani ya Yesu Kristo mwenyewe. Kristo ni hakikisho lake na yeye anatumaini Kristo pekee kwa wokovu wake. Kila siku ataongea na Kristo katika maombi na kumtumikia Kristo na kumpenda Kristo na kutarajia kwa moyo wake wote kurudi kwake. Haya ni maisha ya yule ambaye ana imani ndani ya Kristo na anamwammini. Yule ambaye hathamini Kristo hajaokoka.

Msomaji, ninaweka hizi ishara saba mbele yako na ninakusihi ujichunguze vizuri kulingana na ishara hizi saba. Ikiwa wewe umeokoka basi kwa ukweli utakuwa na ishara hizi saba ndani mwako. Na ikiwa ukijichunguza na kupata kwamba wewe huna ishara hizi saba, basi ni lazima ufahamu kwamba wewe hujaokoka, ingawa unawaza kwamba umeokoka.

Ni namna gani watu wa Mungu wanaweza

kusahau Ufalme wa Mungu.

Sura hii ni ufafanuzi wa Hagai 1:1-11. Tafadhali hakikisha kwamba umesoma kifungu hiki kabla ya kusoma sura hii. Katika kifungu hiki, tunapata mahubiri ya kwanza ambayo Mungu aliwapatia watu wa Israeli kupitia kwa nabii Hagai. Watu wa Israeli walikuwa wamerudi nchini mwao baada ya kukaa miaka 70 katika nchi ya Babeli. Wakati walirudi Yerusalemu, walipata kwamba hekalu liliangamizwa kabisa na watu wa Babeli. Watu wa Israeli walianza kazi ya kulijenga tena hekalu lakini walikufa moyo kwa sababu maadui wao waliwapinga sana. Kwa miaka 16, hekalu lilikuwa limejengwa nusu tu, lakini watu wa Israeli walikuwa na manyumba mazuri. Katika mahubiri haya, Mungu anaongea na Zerubabeli, ambaye alikuwa kiongozi wa Wayahudi, kupitia kwa nabii Hagai.

1. Vijisababu vya watu (mstari wa 2).

Kwa miaka 16 kazi ya kujenga hakalu ilisimama na hekalu lilijengwa nusu tu. Wakati watu wa Israeli walikumbushwa jambo hili, wao walisema, “Wakati haujawadia wa kujenga nyumba ya Bwana” (mstari wa 2). Inaonekana kwamba watu walisema, “Tunajua kwamba ni jukumu letu kujenga hekalu hili, na siku moja hakika tutamaliza kazi hii, lakini wakati huu haufai.” Pengine wao walikuwa na sababu ya kutoa vijisababu hivi: “Sisi hatuna pesa ya kulijenga hekalu; maadui wa Mungu bado wako hapa, wacha tungoje hadi wao waondoke; hatuna wale mafundi ambao tunawahitaji,” na kadhalika.

Ni jambo la kutuhuzunisha wakati watu wa Mungu wanatoa vijisababu badala ya kuwa na moyo wa kufanya kazi ya Ufalme wa Mungu. Kuna watu wengi katika nchi yetu ambao wameokoka lakini hawana moyo wa kufanya kazi ya Ufalme wa Mungu. Kuna wale ambao wanasema, “Sijafundishwa vizuri katika chuo cha Biblia na kwa hivyo siwezi kumtumikia Mungu. Kwanza ninahitaji kufundishwa vizuri, halafu nitamtumikia Mungu.” Pia, kuna wengine ambao wanasema, “Ninafanya kibarua au afisini fulani, na kazi yangu ni ngumu sana. Ninahitaji kufanya masaa mengi kila siku na jioni huwa nimechoka kabisa, na kwa hivyo siwezi kufanya kazi ya Ufalme wa Mungu. Wacha kwanza nipate pesa nyingi, halafu nitamtumikia Mungu kwa moyo wangu wote.” Lakini hivi vijisababu ni vya bure. Yesu alisema, “Utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake na haya yote mtaongezewa” (Mathayo 6:33). Wakati wa kumtumikia Mungu kwa mioyo yetu yote ni sasa.

2. Malalamishi ya Mungu (mistari 3-4).

Mungu aliwaambia watu wa Israeli, “Je, ni wakati wenu ninyi wa kuishi katika nyumba zenu zilizojengwa vizuri, wakati hii nyumba ikibaki, gofu?” Hapa tunaona ni kwa nini hawa watu wa Israeli waliacha kazi ya kujenga hekalu. Ilikuwa si kwa sababu ya maadui wao au kwa sababu wakati haukuwa umefaa. Wao waliacha kazi ya kujenga hekalu kwa sababu walijali sana starehe zao na vitu vyao kuliko Ufalme wa Mungu. Wao walitaka pesa na starehe na vitu, na kwa hivyo walivifuata vitu hivi na walisahau kazi ya kujenga hekalu la Mungu.

Hatari hii sisi sote tunaweza kuanguka ndani yake. Anasa za ulimwengu na vitu vya dunia vinaweza kutuvuta. Shetani anaviweka vitu vya dunia kama elimu na starehe mbele zetu na kutujaribu tuvifuate. Yeye hutukumbusha kwamba kufuata elimu si dhambi na kupata vitu vya dunia si dhambi. Yeye anajua kwamba mioyo yetu inaweza kuvutwa na vitu hivi na tunaweza kusahau kazi ya Ufalme wa Mungu.

3. Hukumu ya Mungu (mistari 5-6; 9-11).

Kwa sababu watu wa Israeli hawakumtumikia Mungu kwa mioyo yao yote, Mungu aliwahukumu. Hukumu ya Mungu ilikuja kwa njia mbili.

(i) Kulikuwa na wakati wa njaa nchini mwao (mistari 9-11). Ni Mungu ambaye anatupatia mvua (Mathayo 5:44-45), na ni Mungu ambaye anasimamisha mvua (Kumbukumbu la Torati 28:24). Kwa hivyo kulikuwa na wakati ambapo watu wa Israeli hawakupata mvua: “Kwa hiyo, kwa sababu yenu mbingu zimezuia umande wake na ardhi mavuno yake” (mstari 10).

(ii) Watu hawakutosheka na vitu vya dunia (mistari 5-6). Hata ile miaka ambayo mvua ilinyesha na watu waliweza kuvuna, wao bado hawakutosheka na vitu vya dunia: “Mmepanda vingi, lakini mmevuna haba. Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa, lakini hamtosheki” (mstari 6). Jambo hili linatukumbusa kwamba anasa za dunia na vitu vya dunia haviwezi kututosheleza. Tunaweza tu kuwa na furaha hapa duniani wakati tuko na amani na Mungu: “Afadhali chakula cha mboga mahali palipo na upendo kuliko nyama ya ndama iliyonona pamoja na chuki” (Mithali 15:17).

4. Amri ya Mungu (mistari 7-8).

Mungu aliwaamrisha watu, “Pandeni milimani mkalete miti na kujenga nyumba, ili nipata kuifurahia nitukuzwe” (mstari 8). Amri za Mungu si ngumu kuelewa; amri zake ni rahisi: sisi tunapaswa kutumia vipawa vyetu kufanya kazi ndani ya Ufalme wake na kujenga Ufalme wake. Sisi tunapaswa kuhubiri injili kwa dunia yote na kuyafanya mataifa yote yawe watu wake Mungu. Hii ni kazi ambayo Mungu ametupatia, na hii ni kazi ambayo tunapaswa kufanya kwa mioyo yetu yote.

Maombi ya Daudi

Mafundisho haya ni ufafanuzi wa kifungu cha 2 Samweli 7:18-29. Hakikisha kwamba unasoma kifungu hiki kabla ya kuendelea kusoma mafundisho haya.

Katika kifungu hiki tunasoma kuhusu maombi ya Daudi baada ya Mungu kumwahidi mambo makuu (2 Samweli 7:11-16). Ni maombi ambayo yana mafundisho muhimu sana kwetu. Tumeamrishwa na Mungu tuombe. Je, tunafaa kuomba kwa njia gani? Je, mioyo yetu inafaa kuwa aje wakati tunakuja kwa Mungu kwa maombi? Haya ndiyo mambo tunasoma katika kifungu hiki.

1. Daudi aliomba kwa unyenyekevu.

Kumbuka kwamba Daudi alikuwa mfalme wa nchi ya Israeli. Chini yake, taifa la Israeli lilikuwa na jeshi zuri na uchumi wa taifa hili ulikuwa mzuri sana. Daudi alikuwa mtu ambaye aliheshimiwa na watu wake sana. Yeye alikuwa kiongozi mashuhuri sana.

Lakini hata hivyo, Daudi wakati alikuja kwa Mungu kwa maombi, hakuja kama mfalme bali alikuwa kama mtumishi ambaye alimtegemea Mungu kwa kila jambo. Aliomba, “Ee Bwana mwenyezi, mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo?” (mstari 18). Daudi haanzi maombi yake kwa kumweleza Mungu kwamba yeye ni mfalme mashuhuri wa Israeli na mtu ambaye alikuwa wa kiroho sana. Bali yeye alijua kwamba, yeye pamoja na jamii yake hawakuwa kitu mbele za Mungu mwenye mamlaka na nguvu zote ambaye anatawala mbingu na duniani.

Hili ni funzo ambalo tunafaa kujifunza kutoka kwa Daudi. Biblia inasema kwamba, “Mungu huwapinga mwenye kiburi lakini huwapa neema wale ambao wamejinyenyekeza” (1 Petro 5:5). Bwana Yesu Kristo alitoa mfano ambapo Mfarisayo mmoja mwenye kiburi aliomba, “Mungu, ninakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine: wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma, natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu” (Luka 18:9-14). Yesu Kristo alisema, mtu huyu hakukubalika machoni pa Mungu. Bali yule ambaye aliomba, “Mungu nihurumie, mimi mwenye dhambi” (Luka 18:13), ndiye aliyekubalika machoni pa Mungu. Ikiwa kweli tunataka kukubalika machoni pa Mungu, lazima tuwe wanyenyekevu. Ikiwa tunataka maombi yetu yakubalike kama yale ya Daudi, lazima tuombe kwa unyenyekevu.

2. Daudi katika maombi yake, alimtukuza Mungu.

Daudi aliomba, “Tazama jinsi ulivyo mkuu, Ee, Bwana Mwenyezi! Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe” (mstari wa 22). Tazama sababu ya Daudi kumtukuza na kumsifu Mungu: ni kwa sababu ya jinsi Mungu mwenyewe alivyo. Hapa Daudi alikuwa anawaza kuhusu jinsi Mungu alivyo na kwa sababu hii, alimtukuza na akamsifu na pia alitoa shukurani zake kwa jinsi Mungu alivyo.

Tazama pia kile Daudi anasema kumhusu Mungu: “Jinsi ulivyo mkuu.” Daudi alitambua kwamba Mungu ni mkuu, “jinsi ulivyo mkuu Ee Bwana Mwenyezi.” Daudi alijua kwamba Mungu ambaye aliabudu alikuwa mtawala wa kila kitu. Yeye ni mkuu na anatawala kila kitu. Hii ndiyo sababu Daudi anaendelea na kusema, “Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe.” Daudi alijua kwamba kuna Mungu mmoja wa kweli, mwumba wa mbingu na dunia, ambaye ni Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hii ndiyo sababu alikuja mbele za Mungu kwa moyo mnyenyekevu. Daudi alijua kwamba Mungu ni mkuu na anatawala kila kitu.

Wakati tunaomba, ni lazima tutilie maanani Mungu ni nani kwa sababu tunafaa kujua tunamwomba nani. Wakati tunamjua Mungu ni nani, ndipo tutaweza kuomba vyema. Ikiwa kila wakati tutafahamu kwamba Yule ambaye tunaomba kwake ni Mkuu na kwamba ni Yeye ambaye anatawala kila kitu na anathibiti kila kitu, ndipo tutaweza kuja Kwake katika maombi kwa unyenyekevu tukimsifu na kumtukuza kama tu jinsi Daudi alifanya.

3. Daudi aliomba kulingana na mapenzi ya Mungu.

Wakati tunasoma 2 Samweli 7, tunasoma kwamba lilikuwa kusudi la Daudi kujenga hekalu katika mji wa Yerusalemu. Daudi alimwambia nabii Nathani, “Mimi hapa ninaishi katika jumba la kifalme la mierezi, wakati sanduku la Mungu limebaki katika hema” (2 Samweli 7;2). Ni wazi kwamba Daudi alikuwa na kusudi la kumjengea Mungu hekalu kubwa katika mji wa Yerusalemu. Lakini usiku huo, Mungu alimwambia nabii Nathani aende na amwambie Daudi, “Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu” (2 Samweli 7:12-13).

Ilikuwa tamaa ya Daudi kumjengea Mungu nyumba lakini yalikuwa mapenzi ya Mungu kwamba nyumba hiyo ijengwe na Solomoni. Katika maombi haya hatuoni Daudi akibishana na Mungu au kujaribu kumshawishi Mungu afanye jinsi yeye alitaka. Yeye alikuwa amesikia maneno ya Mungu kutoka kwa nabii Nathani na aliomba kulingana na yale alikuwa ameambiwa na Mungu. Aliomba, “Basi sasa, Bwana ukaitimize ahadi uliyosema kuhusu mtumishi wako na nyumba yake milele. Ukafanye kama ulivyoahidi, ili kwamba Jina Lako litukuke milele” (2 Samweli 7:25-26).

Daudi alijua mapenzi ya Mungju na aliyakubali yafanyike kwa kuomba kulingana na mapenzi hayo. Maombi yake hakuongozwa na yale ambayo yeye mwenyewe alitaka, bali yaliongozwa na mapenzi ya Mungu kwake. Yeye aliomba mapenzi ya Mungu yatimike wala siyo yake. Hili lilikuwa ombi la unyenyekevu.

Jinsi ya kuomba kulingana na mafundisho haya.

Maombi haya ya Daudi ni ya muhimu sana kwetu leo kuwaza juu yake. Tumeamrishwa na Mungu tuombe na tunahitaji kujifunza kuomba kutoka kwa neno Lake jinsi tunafaa kuomba.

1. Tukumbuke kila wakati kwamba Mungu ni mkuu na anatawala viumbe vyote wakati tunakuja kwake katika maombi.

Kwa hivyo tuje Kwake na moyo ambao umenyenyekea na uko tayari kukubali mapenzi yake. Tuhakikishe kwamba hatuji mbele za Mungu tukimshawishi atimize mapenzi yetu.

2. Pili tuhakikishe kwamba wakati tunakuja mbele za Mungu, hatuji na moyo ambao haujanyenyekea na unalalamika.

Mara mingi kuna mambo ambayo sisi hutaka, lakini haya yawe si mapenzi ya Mungu kwetu. Daudi alitaka kumjengea Mungu nyumba, lakini haya hayakuwa mapenzi ya Mungu. Mapenzi ya Mungu yalikuwa kwamba Solomoni aijenga nyumba hiyo. Wakati tunasoma maombi ya Daudi, hatusomi popote kwamba alilalamika au alikataa mapenzi ya Mungu. Bali Daudi alikubali mapenzi hayo ya Mungu kwa moyo wenye furaha na mnyenyekevu. Tuhakikishe kwamba tunafuata mfano huu wa Daudi.

3. Tuhakikishe kwamba tunaongozwa na neno la Mungu katika maombi yetu.

Daudi alisikiza vyema kabisa yale ambayo Nathani alimwambia na akaomba kulingana na mapenzi ya Mungu. Mapenzi ya Mungu ambayo alielezwa na nabii Nathani, yalimwongoza katika maombi yake. Tuhakikishe kwamba tunasoma na kufuata Biblia ili tuweze kufahamu mapenzi ya Mungu ambayo yatatuwezesha kuomba vyema. Tusiombe jinsi wale ambao hawamjui Mungu wala mapenzi yake wanavyoomba. Tukumbuke kwamba katika Biblia, Mungu ametuonyesha wazi mapenzi Yake kwetu. Tuhakikishe kwamba tunaongozwa na Biblia katika maisha yetu yote.

*********

Mchungaji anapaswa kuhakikisha kwamba

yeye mwenyewe ameokoka

“Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe (Matendo ya Mitume 20:28).

Ikiwa wewe ni mchungaji, hakikisha kwamba unachunga hali yako ya kiroho. Hakikisha kwamba wewe mwenyewe umeokoka. Hakikisha kwamba wewe si yule ambaye anawahubiria wengine Kristo lakini yeye mwenyewe hana Kristo. Mungu amewaahidi wachungaji wote zawadi kuu, lakini ni yule tu ambaye ameokoka ndiye atapata zawadi hii. Kuna wachungaji wengi ambao leo wako jahanum ambao waliwaonya watu kuhusu jahanum. Usiwaze kwamba kwa sababu wewe ni mchungaji, basi wewe kwa hakika umeokoka. Mungu hataruhusu yeyote kuingia mbinguni kwa sababu yeye alikuwa mhubiri, hata kama alikuwa na vipawa vingi. Ukitaka kuingia mbinguni, hakikisha kwamba wewe mwenyewe umeokoka.

Kuwa mtu bila wokovu ni jambo mbaya sana, lakini kuwa mchungaji bila wokovu na mbaya zaidi. Kila wakati unasoma Biblia, unasoma kuhusu hukumu yako. Kila wakati unahubiri injili unaongeza hukumu yako kwa sababu wewe unamkataa yule Mwokozi ambaye unawahubiria wengine.

Kwa kawaida, yule mchungaji ambaye hajaokoka hajui hali yake ya kweli. Kila siku yeye husoma Biblia, na kwa nje huishi maisha matakatifu mbele za watu wa dunia. Yeye huhubiri kuhusu dhambi na anawahimiza wengine kuishi maisha matakatifu. Lakini wakati huu wote yeye mwenyewe hajaokoka na anaenda jahanum. Yeye ni kama mtu ambaye anawalisha wengine mkate na wakati huo huo anakufa njaa.

Ikiwa hii ni kweli kwako, basi sikia shauri langu: ujihubirie kabla ya kuwahubiria wengine. Usiwe kama wale ambao siku ya hukumu watasema, “Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako na kwa jina lako kutoa pepo na kufanya miujiza mingi?”. Ikiwa wewe hujaokoka, utasikia maneno haya ya Yesu Kristo, “Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!” (Mathayo 7:21-23). Ninakushauri kiri dhambi zako mbele za watu wa kanisa lako na uwaambie wakuombee uokoke!

Kupata mchungaji ambaye hajaokoka si jambo la kushangaza sana. Mahubiri yako hayatakuwa na uhai ikiwa Kristo hayumo moyoni mwako. Wote ambao wanataka kuwa wachungaji wanapaswa kujua hii. Je, ni faida gani kuwa mchungaji ikiwa wewe hujui Mungu na neema yake na wokovu wake? Lakini ukiokoka, utamjua Mungu na neema yake na wokovu wake na utakuwa na furaha nyingi sana. Wewe huwezi kujua chochote ulimwenguni hadi umjue Mungu.

Wakati Mungu alimwumba mwanadamu, mwanadamu alikuwa amekamilika na aliishi katika ulimwengu ambao umekamilika. Viumbe vyote vilifunua utukufu wa Mungu. Mwanadamu hangetenda dhambi, fahamu yake kumhusu Mungu ingeendelea kuongezeka. Lakini mwanadamu alianguka dhambini na alipoteza fahamu yote kumhusu Mungu.

Kazi ya Kristo ni kuturejesha kupitia kwa imani katika ile hali ya usafi, kutii na upendo ambayo sisi tuliumbwa ndani. Kwa hivyo wale ambao ni watakatifu wanafahamu ni kwa nini Mungu aliumba viumbe. Wakati tunawaza juu ya viumbe, tunahitaji kufahamu kwamba viumbe viliumbwa kuonyesha utukufu wa Mungu. Hii ndiyo sababu sisi sote tunapaswa kumpenda Mungu na kumtumikia, hii ndiyo hekima ya kweli.

Wale ambao ni walimu wa shule wanapaswa kuwafundisha watoto kuhusu wokovu kwanza, na halafu kuwafundisha mambo yote mengine ya shule. Usiwaze kwamba watoto ni wadogo sana na kwa hivyo hawawezi kufahamu neno la Mungu. Fundisha watoto Biblia ili wao waweze kumfuata Mungu.

*******

Kristo amewaweka huru watu wa Mungu kutoka kwa nguvu za dhambi

“Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli” (Yohana 8:36).

Haya ni maneno ya Kristo Mwana wa Mungu kwa wale Wayahudi ambao walikuwa wamemwamini. Alizungumza maneno haya kwao, kwa sababu wao waliwaza kwamba kwa sababu wao ni uzao wa Abrahamu, basi walifaa kuitwa wana wa Mungu (Yohana 8:33). Yesu aliwajibu kwa kuwaeleza kwamba, hata kama wao ni uzao wa Abrahamu, wao walikuwa watende dhambi wakuu: “Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Abrahamu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno la Mungu” (Yohana 8:37).

Tunajifunza mambo haya kutoka kwa mstari huu wa Yohana 8:36.

1. Wale ambao Mwana amewaweka huru, wakati moja walikuwa watumwa.

Yesu alisema, “kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi” (Yohana 8:34). Huu ni ukweli ambao Biblia inaeleza kwa wazi kabisa. “Sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina” (Tito 3:3). Kila mmoja wetu amezaliwa akiwa mtenda dhambi na mtumwa wa dhambi na mtumwa wa shetani. Kwa sababu tulikuwa watenda dhambi, hatukuwa na ushirika na Mungu na hatukuwa na tumaini wala Mungu mwenyewe.

Hatukuwa tu watenda dhambi, bali tulikuwa watumwa wa dhambi na tulikuwa tumenaswa na kila aina ya tamaa za ulimwengu. Kila mtu ambaye ameokoka alikuwa hivi kabla ya kuokoka. Yeye alikuwa mtumwa wa shetani na dhambi. Hakuna lolote zuri ndani mwetu ambalo lilimfurahisha Mungu ndipo atuokoe. Sisi tulikuwa maadui wake na hatima yetu ilikuwa jahanum katika moto mkali.

Shukurani kwa Mungu kwa sababu ametukomboa kutoka kwa nguvu za dhambi na shetani kupitia kwa Kristo Yesu. Yesu alisema, “sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi” (Mathayo 9:13). Yesu Kristo anatuonyesha wazi hapa kwamba alikuja kuwaweka huru watu wake kutoka katika utumwa wa dhambi. Yesu Kristo alikufa msalabani Kalvari kuwaweka huru wenye dhambi na alifufuka kutoka kwa wafu kuwawezesha watu wake kumwabudu Mungu anaye ishi.

Wale wote ambao hawajaokoka, bado wako katika utumwa wa shetani na dhambi. Hawawezi kufanya lolote kumpendeza Mungu; wao hawana tumaini na hawana Mungu katika ulimwengu huu. Watakapokufa, watatupwa katika jahanum milele.

Wewe ambaye hujaokoka, hutawahi kupata amani na uhuru hadi Kristo mwenyewe akuweke huru kutoka kwa utumwa wa dhambi. Njoo Kwake leo kwa sababu yuko tayari kukuweka huru na kukuhakikishia nafasi mbinguni.

2. Ni Mwana pekee ambaye anazo nguvu za kuwaweka huru wenye dhambi kutoka kwa nguvu za dhambi.

Yesu alisema, “Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli” (Yohana 8:36). Pia alisema, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia Kwangu” (Yohana 14:6). Paulo naye alisema, “Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi” (1 Timotheo 1:15). Huu ndiyo ujumbe wa Biblia na msingi wa kweli zote ambazo mwanadamu amepokea kutoka kwa Mungu. Bwana Yesu Kristo alitoka mbinguni kwa kusudi moja tu: kuwaokoa wenye dhambi. Nguvu za kuokoa ziko mikononi mwa Kristo Yesu peke yake wala si kwa mwingine yeyote.

Wakristo wote waliokolewa na wameokolewa kupitia kwa Kristo peke yake. Kristo Yesu alipokuwa amebatizwa, sauti ilisikika kutoka mbinguni ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ambaye ninapendezwa sana naye” (Mathayo 3:17). Sauti hiyo hiyo ilisikika tena ikisema, “Huyu ni Mwanangu, nimpendaye, msikilizeni Yeye” (Marko 9:7). Kile Mungu Baba alikuwa akisema ni kwamba, hakuna yeyote ambaye anaweza kumwokoa mwanadamu kutoka kwa nguvu za dhambi isipokuwa Kristo Yesu pekee.

Wengi wamewaamini watu wengine na wengi wametafuta wokovu katika mambo mengine na wametumia njia zingine wakiwaza kwamba kwa kufanya hivyo, wataokolewa. Hakuna yeyote ambaye alifaulu. Wengi wamekufa wakijaribu na mwishowe wameenda jahanum. Kuna njia moja tu ya kupokea msamaha wa dhambi zetu na kuokolewa kutoka kwa utumwa wa dhambi, na hii ni kupitia kwa Kristo Yesu pekee. Usimalize wakati wako ikijaribu kutumia njia zingine. Njoo kwa Kristo Yesu kwa sababu Yeye ndiye anazo nguvu za kukuokoa na hakuna mwingine.

Kwa sisi sote ambao tumemwamini Kristo pekee kwa ajili ya wokovu wetu, tufurahie na tuendelee kufurahia kwa yale ambayo Mungu ametufanyia ndani ya Kristo. Tujitolee kabisa kwa kumtumikia Mungu wakati wowote na katika hali zote. Furahieni mandugu.

3. Kwa sababu Mwana ametuweka huru, hatuwezi kuwa watumwa tena; milele tuko huru ndani ya Mwana.

Yesu alisema, “Mtakuwa huru kweli kweli” (Yohana 8:36). Kwa sababu Mwana wa Mungu amekufa na akafufuka, minyororo ya utumwa ilivunjwa: “Ondoka, angaza, kwa kuwa nuru yako imekuja na utukufu wa Bwana unaangaza juu yako” (Isaya 60:1). Sasa Kristo Yesu amewaleta wote ambao wameokoka katika Ufalme wa Mungu na hakuna yeyote ambaye anaweza kuwapokonya kutoka katika mikono Yake. Wao sasa wako salama mikononi Mwake.

Watoto wote wa Mungu wako huru ndani ya Kristo na sasa wanaweza kumtumikia kwa ujasiri kwa sababu wamewekwa huru milele kutoka kwa utumwa wa dhambi. Kuna wengi ambao wanakataa kuamini kwamba wakati wameokolewa na Kristo, milele wao wameokoka ndani ya Kristo. Wao huwaza kwamba mtu anaweza kuokoka na siku moja apoteze wokovu wake na aende jahanum. Huu si ukweli kwa sababu Mwana akikuweka huru, utakuwa huru kweli kweli. Biblia haisema kwamba utakuwa huru kwa wakati fulani tu. Wokovu wetu umehakikishwa na Mwana wa Mungu na hakuna siku ambapo mtu anaweza kupoteza wokovu wake. Yesu mwenyewe alisema, “Haya ndiyo mapenzi yake Yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho” (Yohana 6:39).

Jambo hili ni la furaha kuu kwa watu wa Mungu wote na ni la huzuni mkubwa sana kwa wale ambao hawajaokoka. Ikiwa wewe hujaokoka, wewe bado uko chini ya ghadhabu ya Mungu. Wewe huna tumaini, huna Mungu na huna maisha ndani ya Kristo. Maisha yako, yamo hatarini kwa sababu wewe huko ndani ya Kristo. Wewe huko huru, wewe bado ni mtumwa ambaye amefungwa minyororo na uko karibu kutupwa jahanum. Wewe uko na tumaini moja la kuepuka jahanum, na hili ni Kristo Yesu Mwana wa Mungu.

Njoo kwa Kristo Yesu sasa kwa sababu yuko tayari kukupokea na kukuokoka.

*******

Je, Utakatifu ni Nini?

Je, utakatifu ni nini? Jibu ni kwamba utakatifu ni kazi ambayo Mungu anafanya ndani ya moyo wa mwanadamu ili yule mwanadamu awe mtu wa kiroho na si mtu wa dhambi. Hii ni kazi ya Mungu kumfanya mtu hai na wa kiroho, ili huyu mtu sasa hajali mambo ya dunia,bali anajali sana mambo ya mbinguni.

1. Utakatifu unajengwa juu ya neno la Mungu. Utakatifu wa ukweli si hisia ndani ya moyo, bali ni njia ya ukweli (Zaburi 119:30). Utakatifu unatoka kwa Mungu, hautoki kwa moyo wa mwanadamu.

2. Utakatifu unapatikana ndani ya moyo wa mwanadamu (Warumi 2:29). Kuna wale ambao kwa nje wanaonekana kuwa watakatifu, lakini kwa ukweli mioyo yao ni mioyo ya dhambi. Lakini yule ambaye ni mtakatifu ako na maisha ya Mungu ndani mwake. Yeye haishi maisha ya utakatifu kuwaonyesha tu watu, bali ako na utakatifu ndani mwake.

3. Utakatifu ni kazi ya Mungu, si kazi ya mwanadamu. Wakati tunazaliwa hapa ulimwenguni, tunazaliwa wenye dhambi. Biblia inatuambia kwamba dhambi inafanya kazi ndani yetu tangu tuzaliwe (Warumi 7:5), lakini utakatifu unatoka kwa Mungu (Yakobo 3:17). Yule ambaye hajaokoka hana utakatifu ndani mwake, utakatifu ni mwangaza ndani ya moyo wa mwanadamu, ni kitu ambacho Mungu anapanda ndani mwetu, ni tunda la Roho Mtakatifu (Wagalatia 5:22). Bila kazi hii ya Mungu hakuna yeyote ambaye anaweza kuwa mtakatifu.

4. Utakatifu unapatikana katika kila sehemu ya mwanadamu. Paulo aliandika, “Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa” (1 Wathesalonike 5:23). Mtu ambaye ni mtakatifu anafahamu vitu vya Mungu na anavipenda vitu hivi kwa moyo wake. Yeye ana tamaa ya kuvifuata vitu hivi na anaishi yale maisha ambayo yanampendeza Mungu. Yeye sasa ni mtu mpya (Wakolosai 3:10). Si kwamba yeye ni mtakatifu hapa na pale tu, bali ni mtakatifu katika kila sehemu.

5. Utakatifu unaonekana maishani. Hii ni kazi ya Mungu ambayo inaonekana katika maisha ya mwanadamu. Yeye haongei tu kuhusu utakatifu, bali anaishi maisha matakatifu.

6. Utakatifu ni jambo nzuri. Utakatifu ni kama dhahabu: inaonekana kuwa kitu kizuri. Yule ambaye ako na utakatifu wa ukweli hapa ulimwenguni ni kama malaika hapa ulimwenguni: yeye anaonyesha utukufu wa Mungu.

7. Utakatifu ni jambo la milele. Mungu anapanda utakatifu ndani ya moyo wa mwanadamu na hii inambadilisha yule mtu, na yeye anaanza kuwa mtakatifu jinsi Mungu alivyo mtakatifu. Wakati mtu anaokoka, hatapoteza wokovu wake: mti wa utakatifu umepandwa ndani yake na mti huu hauwezi kung’olewa.

Waraka wa Paulo kwa Wafilipi

Wafilipi 1:3-11

Katika kifungu hiki mtume Paulo anatufundisha mambo matatu muhimu: anatufundisha kuhusu ushirika wa wakristo, hakikisho la wakristo na pia maombi yake kwa sababu ya kanisa la Filipi.

Katika mstari wa 3-4 Paulo anamshukuru Mungu kwa sababu ya ushirika aliokuwa nao na kanisa hili la Filipi. Yeye anasema kwamba kanisa hili lilikuwa likishirikiana naye katika kueneza injili. Katika sehemu hii ya kifungu hiki tutaona ni ushirika wa namna gani uliokuwa kati ya Paulo na kanisa la Filipi na ulikuwa unahusu nini haswa.

1. Ushirika huu ulihusu upendo wa mandugu.

Paulo anasema, “Ninyi mko moyoni mwangu” (mstari wa 7), na katika mstari wa 8, anaongeza kusema, “Mungu ni shahidi yangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Yesu Kristo.” Mistari hii inatuonyesha ushirikiano uliokuwa kati ya Paulo na kanisa hili. Hapa tunaona kwamba mtume Paulo aliwakumbuka wapendwa hawa katika moyo wake kila wakati. Yeye hakuwakumbuka tu wakati alisikia ripoti ya jinsi kanisa hili linavyoendelea, bali alikuwa anawakumbuka kila siku. Wao walikuwa sehemu yake na pia walikuwa ndani ya moyo wake. Upendo wa mtume Paulo kwa kanisa la Filipi unatuonyesha jinsi upendo wa kweli wa wakristo unapaswa kuwa. Hii inamaanisha kwamba ikiwa hakuna upendo miongoni mwa wakristo, ni vigumu sana kuwa na ushirika. Kumpenda mtu kunamaanisha kumfanyia mtu huyo yale mambo ambayo ni mema na kushiriki naye katika mambo mema. Kumpenda mtu ni kumfanyia yale mambo ambayo ni ya faida kwake kwanza kabla ya kushughulikia mahitaji yetu. Huu ndiyo unaitwa upendo wa kujitolea, yaani upendo ambao unakufanya ufikirie kuhusu ndugu yako mkristo kwanza kabla ya kuanza kujali mambo ambayo yanakuhusu. Katika injili ya Yohana, Bwana Yesu Kristo anatuonyesha mfano wa upendo huu. Bwana Yesu anasema, “Hakuna upendo ulio mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yohana 15:13). Huu ndiyo upendo ambao kila mkristo anapaswa kuwa nao kwa wakristo wenzake. Kila mshirika wa kanisa anapswa kuwajali mandugu wenzake na kushughulikia mahitaji yao.

2. Ushirika huu ulihusu kuombeana.

Mtume Paulo anasema hapa kwamba alikuwa anawakumbuka wakristo hawa wa kanisa la Filipi na alikuwa akiwaombea. Wakati wakristo wanapoombeana, hii ni dhihirisho ya kwamba wao wana ushirika. Ikiwa tunasema kwamba tuna ushirika na wakristo wenzetu, basi tunapaswa kuombeana. Pia ni vizuri sana kanisa fulani kuyaombea makanisa mengine ambayo wanashirikiana pamoja katika kazi ya kueneza injili.

3. Ushirika huu ulihusu kusaidiana.

Paulo anasema kwamba anaomba kwa furaha sana kwa sababu ya ushirika wake na kanisa la Filipi katika kazi ya kueneza injili. Zaidi ya kuombeana, kanisa la Filipi lilimtumia Paulo zawadi. Hii intuonyesha kwamba tunaposhiriki pamoja na wakristo wenzetu hata katika kutumia pamoja mali na vitu vya dunia ambavyo Mungu ametubariki navyo, tunahimizana sana katika Bwana.

Katika mstari wa 6 Paulo anaeleza kuhusu hakikisho la wokovu wetu. Anasema, “Nina hakika kwamba, Yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataindeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.” Hapa tunasoma kwamba, yule ambaye ameokoka amehakikishiwa maisha ya milele mbinguni. Mtume Paulo anawaeleza wakristo wa kanisa hili la Filipi kwamba anajua hawatakata tamaa kuhusu imani yao hata ikiwa watapata taabu. Hii ni kwa sababu ni Mungu mwenyewe ambaye ameanzisha hii kazi ya wokvu ndani mwao. Hivi ndivyo anawaambia Wafilipi, “Yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu ataiendeleza na kuikamilisha.” Maneno ya Paulo hapa yanatukumbusha kwamba wokovu ni kazi ya Mungu mwenyewe. Mtu hapati wokovu kwa sababu amefanya uamuzi wa kumkubali Yesu Kristo. Wokovu wa mtu hautengemei bidii yake kamwe ama matendo yake. Ni Mungu mwenyewe ambaye anamwonyesha mtu dhambi zake kwa kufanya kazi yake ndani ya moyo wa mtu. Katika kitabu cha Waefeso 1:4, Biblia inasema, “Mungu alituchagua katika Yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake.” Hii inatuonyesha wazi kwamba kabla ya Mungu kuumba ulimwengu alipanga mpango wake wa kuwaokoa wenye dhambi. Hii ndiyo sababu Paulo anawaeleza wakristo wa Filipi kwamba wanapaswa kuwa na hakikisho kwamba baada ya maisha ya hapa ulimwenguni wao watakuwa na Kristo milele mbinguni. Tunapaswa kujua kwamba Mungu hatazuiliwa na chochote, chochote ambacho alipanga kitatimika.

Tena Paulo anawaeleza Wafilipi kwamba Mungu ataikamilisha kazi ambayo ameanza ndani mwao. Wokovu ni kazi kuu ya Mungu. Katika kazi hii Mungu anampatia uzima mtu ambaye alikuwa amekufa katika dhambi na makosa. Pia Mungu anamwonyesha huyu mtu uovu wa dhambi zake. Halafu, Mungu anampatia mtu toba na imani ndani ya Yesu Kristo na anamhesabia haki. Baada ya kufanya haya yote, Mungu anaanzisha kazi ya kumtakasa mtu ili afanane na Kristo mwenyewe. Hii kazi ya kumtakasa mtu ili afanane na Kristo Yesu ni kazi ya maisha yote wakati mtu ako hapa ulimwenguni. Mungu mwenyewe ataendelea kufanya kazi hii katika mioyo ya wale ambao wameokoka hadi siku ile watatoka humu duniani. Mungu ataendelea kufanya kazi hii katika mioyo ya watu wake hadi siku ile wataingia mbinguni.

Maombi ya Paulo kwa Wafilipi (mistari 9-11).

Kuna mambo mawili ambayo Mtume Paulo anaomba kwa ajili ya kanisa la Filipi katika hii barua yake.

(i) Upendo. Paulo anasema, “Haya ndiyo maombi yangu kwamba upendo wenu uongezeke zaidi katika maarifa na ufahamu wote.” Kanisa la Filipi lilikuwa kanisa ambalo washirika wake walipendana sana, kwa hivyo Paulo anawaeleza waendelee kuwa na huu upendo wa mandugu zaidi na zaidi. Paulo anawaombea kwamba upendo wao kwa mandugu wenzao uwe ni wa kujua zaidi neno la Mungu ili washirika wote waweze kujua ni mambo gani yaliyo mazuri ya kufanyiana katika kila hali.

(ii) Maisha matakatifu. Katika mistari ya 10-11 Paulo anasema, “Ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ile ya Kristo, mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu.” Ishara ya mkristo wa kweli ni maisha matakatifu. Biblia inasema kwamba Mungu “Alituchagua katika Yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake” (Waefeso 1:4). Yesu mwenyewe alisema, “Ni heri walio na moyo safi, kwa maana hao watamwona Mungu” (Mathayo 5:8). Pia tunasoma katika kitabu cha Waebrania kwamba bila kuwa na utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu (Waebrania 12:14). Ikiwa mtu anasema kwamba ameokoka lakini anaishi maisha ya dhambi, basi ukristo wake si wa kweli. Yeye hajaokoka kwa sababu ishara kubwa ya wokovu, yaani kuishi maisha matakatifu haionekani ndani mwake.