Header

Funzo la Kwanza, 1 Timotheo 3:15, Je, Kanisa ni nini?

 

Katika mstari huu, Paulo anasema, “Kama nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa  kweli.”  Katika mstari huu Paulo anaongea kuhusu kanisa.  Anasema mambo matatu kuhusu kanisa.  Anasema kwamba kanisa ni jamii ya Mungu, ni kanisa la Mungu aliye hai na pia kanisa ni nguzo na msingi wa kweli.  Kwa hivyo Paulo anatufundisha mambo matatu hapa kuhusu kanisa.

 

I.  Kanisa ni Nyumba ya Mungu.

 

Hili ndilo jambo la kwanza Paulo anazungumza kuhusu kanisa katika kifungu hiki, kwamba kanisa ni nyumba ya Mungu.  Je, hii inamaanisha nini?  Agano Jipya linatueleza jambo hili zaidi.

 

1.  Kanisa ni nyumba ya Mungu (1 Timotheo 3:15).

 

Nyumba ni jamii.  Kwa hivyo Paulo anasema kwamba kanisa ni jamii ya Mungu.  Kama vile baba ndiye kichwa cha nyumba, vivyo hivyo Mungu ndiye kichwa cha kanisa.  Kanisa silo la mchungaji, ama kasisi, ama mtu yeyote yule, bali ni la Mungu, ni nyumba yake, yaani ni jamii yake.  Nyumba inajumlisha watoto ambao kiongozi wa jamii amewaleta hapa ulimwenguni.  Hawa ni watoto wake mwenyewe ambao wako na sura yake.  Vivyo hivyo kanisa linajumlisha watu ambao Mungu amewaleta katika ufalme wake.  Sisi ni watoto wa Mungu, Yeye ndiye ametuokoa na ametuleta katika ufalme wake, tumezaliwa mara ya pili tukiwa na sura yake.  Kama vile Mungu ni wa huruma, neema na ni mtakatifu, vivyo hivyo wale wamezaliwa mara ya pili, ambao ni watoto wake wako na sura yake.  Sura hii ya Mungu ndani yetu bado hijakamilika.  Sisi bado hatujakuwa wenye huruma, wazuri na watakatifu jinsi Mungu alivyo, lakini Mungu anaendelea na kutukamilisha ili siku moja tufanane na Mwana wake Bwana Yesu Kristo.  “Wapenzi, sasa tu watoto wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua ya kwamba, Yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo.  Kila mmoja mwenye matumaini haya katika Yeye hujitakasa, kama vile Yeye alivyo mtakatifu” (1 Yohana 3:2-3).

 

2.  Kanisa ni kundi la Mungu (Matendo 20:28).

 

Mtume Paulo alisema katika mstari huu, “Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake.  Lichungeni kanisa la Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.”  Kuna mambo mawili ambayo Paulo anasema hapa.

 

(i) Anasema kwamba kanisa ni kundi la Mungu.  Hii inamaanisha kwamba sisi ni watu wa Mungu, tunamtegemea Mungu kwa kila kitu.  Kundi la kondoo haliwezi kwenda lenyewe kujitafutia chakula na maji, ni lazima liongozwe na mchungaji.  Ikiwa mchungaji hataliongoza kundi la kondoo kwa malisho mema na kwenye maji matulivu basi kondoo watakufa kwa sababu ya njaa.  Kondoo wanamtegemea mchungaji kabisa kwa kila kitu maishani mwao.  Vivyo hivyo watu wa Mungu wanamtegemea Mungu katika maisha yao ya kiroho.  Tumezaliwa mara ya pili kwa sababu Mungu ametuwezesha.  Pia kazi ya Mungu haishi baada ya kutufanya tuzaliwe mara ya pili.  Baada ya kuzaliwa mara ya pili, anatulinda katika maisha yetu ya kiroho.  Tunapookolewa, Roho Mtakatifu huja kukaa ndani yetu.  Ni Roho Mtakatifu ambaye anatupatia nguvu kila siku ili tuweze kuishi maisha yetu ya ukristo.  Ni Roho Mtakatifu ambaye anatufundisha neno la Mungu tunapolisoma kila siku.  Bila kazi ya Roho Mtakatifu hatuwezi kulielewa neno la Mungu tunapolisoma.  Roho Mtakatifu anatuwezesha kuelewa neno la Mungu.  Ni Roho Mtakatifu anayetupatia hamu ya kuishi maisha ya kumcha Mungu kila siku: “Kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kutimiza kusudi lake jema” (Wafilipi 2:13).  Hivi ndivyo Mungu analishughulikia kundi lake kila siku: anawalisha na anafanya kazi ndani yao ili wawe tayari kuingia mbinguni.

 

(ii) Anasema kwamba Kristo alinunua kanisa kwa damu yake mwenyewe.  Hii inamaanisha kwamba washirika wa kanisa ni mali ya Mungu na ni wafanyikazi wake.  Tunapozaliwa humu duniani, tunazaliwa tukiwa wenye dhambi.  Tunazaliwa katika ufalme wa giza na tukiwa watumwa wa dhambi.  Lakini Mungu ametukomboa kupitia kwa damu ya Yesu Kristo.  Ametutoa katika utumwa wa dhambi na kutufanya kuwa watu wake: “Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa, nanyi mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki” (Warumi 6:17-18).  Kwa hivyo sisi ambao tumeokoka ni mali ya Mungu na kwa hivyo tunapaswa kuishi maisha ya kumletea Mungu heshima na utukufu: “Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu, akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu?  Ninyi si mali yenu wenyewe, kwa maana mmenunuliwa kwa gharama.  Kwa hivyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu” (1 Wakorintho 6:19-20).

 

3.  Kanisa ndiye bibi arusi wa Kristo (Waefeso 5:25-27).

 

Katika kifungu hiki Paulo anaongea na waume na anasema, “Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda kanisa akajitoa kwa ajili yake kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika neno lake, apate kujiletea kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote bali takatifu lisilo na hatia.”  Kifungu hiki kinatueleza mambo mawili.

 

(i) Bwana Yesu Kristo anafanya kazi katika kila kanisa akiwaosha dhambi watu wake ili wawe watakatifu na wakamilifu.  Hii ndiyo kazi kubwa ya Bwana Yesu Kristo katika kanisa, hili ndilo jambo anafurahia sana kufanya.  Jambo kuu ambalo anafurahia sana ni kwamba kanisa liwe takatifu na kamilifu: “Haya ndiyo mapenzi ya Mungu ninyi mwe watakatifu” (1 Wathesalonike 4:3).

 

(ii) Siku moja Yesu Kristo atajiletea kanisa tukufu.  Siku ile Kristo atakaporudi, kanisa litakuwa, “Tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote bali takatifu lisilo na hatia.”  Hili ndilo lengo Bwana Yesu alilo nalo na hakika atafaulu katika jambo hili.

 

4.  Kanisa ni mwili wa Yesu Kristo (Waefeso 5:29-33).

 

Paulo anaandika, “Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo alivyolitunza kanisa lake.  Sisi tu viungo vya mwili wake.”  Sisi watu wa Mungu tumeunganishwa na Kristo na sisi ni mwili wake: “Sasa nyinyi ni mwili wa Kristo na kila mmoja ni kiungo” (1 Wakorintho 12:27).  Hivi ndivyo inafanyika wakati tunaokolewa.  Mungu hutuunganisha na Kristo na tunakuwa washirika wa mwili wa Kristo.  Bwana Yesu huendelea kutulisha na kutushughulikia jinsi mtu anaulisha na kuushughulikia mwili wake mwenyewe.

 

5.  Kanisa ni jengo la Mungu (1 Wakorintho 3:9).

 

Kanisa ni jengo ambalo Mungu anaendelea kulijenga hapa duniani.  Kila mtumishi wa Mungu ako na kazi ya kufanya katika kulijenga jengo hili.  Paulo anasema, “Kwa neema Mungu aliyonipa, niliweka msingi kama mjenzi stadi na mtu mwingine anajenga juu ya huo msingi” (1 Wakorintho 3:10).  Hii ndiyo sababu hatupaswi kulinganisha kazi ambayo mchungaji fulani anafanya na kazi ambayo mchungaji mwingine anafanya mahali pengine.  Tunapaswa kukumbuka kwamba sisi sote tunafanya kazi tofauti tofauti katika kulijenga kanisa hili la Mungu.  Ukichunguza mjengo wowote unapojengwa, hutasema “Mtu ambaye anatengeneza milango ni wa maana sana kuliko mtu ambaye anaweka mawe kwa ukuta.”  Haya mambo mawili ni tofauti na hayawezi kulinganishwa.  Kanisa la Korintho lilikuwa linalinganisha wahubiri ili kuamua ni nani anayefundisha vizuri ili wamfuate.  Paulo aliwaambia, “Sisi ni watenda kazi pamoja na Mungu, ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu” (1 Wakorintho 3:9).  Siku ile Bwana Yesu atakaporudi, Yeye ataipima kazi yetu kwa jinsi Yeye alivyo (1 Wakorintho 3:12-15).

 

6.  Kanisa ni hekalu la Mungu na Roho Mtakatifu anaishi ndani yake (1 Wakorintho 3:16-17).

 

Katika Agano la Kale, Mungu aliwaamuru watu wa Israeli kujenga hekalu mahali ambapo taifa lote la Waisraeli lingeenda kuabudu.  Hekalu hili lilikuwa makao ya Mungu.  Mungu alisema, “Katika hekalu hili na katika Yerusalemu niliochagua kutoka kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele” (2 Mambo ya Nyakati 33:7).  Watu wa Israeli hata hivyo walianguka dhambini mara kwa mara kila wakati na Mungu akaliondoa lile hekalu miongoni mwao.  Hii haimaanishi kwamba hakuna hekalu la Mungu hapa duniani.  Mahali ambapo jengo la hekalu la Yerusalemu lilikuwa limenjengwa, wakati huu pamejengwa mskiti, lakini kila mahali kwingine humu duniani kumejaa mahekalu kwa sababu kunao makanisa mengi.  Kama vile hekalu la Yerusalemu lilikuwa na jina la Mungu, na kama vile lilikuwa ndilo makao ya Mungu, kila kanisa liko na chapa ya jina la Mungu na ndilo makao ya Mungu: “Ninyi ni hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu” (1 Wakorintho 3:16).

 

Mistari hii kutoka Agano Jipya inatuonyesha kwamba kanisa ni watu wa Mungu, na inatufundisha hii inamaanisha nini.

 

II. Kanisa ni ya Mungu aliye hai.

 

Paulo anasema katika 1 Timotheo 3:15, “Kama nikikawia utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli.”  Kuna mambo mawili ambayo Paulo anafundisha hapa kuhusu kanisa.

 

1.  Kanisa

 

Neno “kanisa” linamaanisha watu wa Mungu ambao wameitwa kutoka kwa ulimwengu kwa sababu maalum.  Nyakati za Agano Jipya, watu wa mji kama wa Korintho au wa Efeso walichagua watu ambao walikwa wafanyi-biashara, ili waache biashara zao na kuendesha shughuli za mji.  Wale ambao walichaguliwa hawakuendelea na biashara zao bali walijitolea kabisa kushughulikia mji.  Waliitwa kusanyiko ambao waliacha kazi zao za kawaida ili wahudumie mji.  Hivi ndivyo neno “kanisa” linamaanisha.  Linamaanisha kwamba kuna wakati ambapo washirika wa kanisa walikuwa watu wanaoshughulika na mambo ya dunia kabisa.  Walikuwa duniani na pia walikuwa wa dunia, na mambo ambayo walikuwa wanajali nayo yalikuwa tu mambo ya ulimwengu, yaani mambo ya pesa, mali na heshima kutoka kwa watu.  Haya ndiyo mambo waliyokuwa wakishughulika nayo kila wakati.  Bwana Mungu basi aliwaokoa watu hawa na akawaita katika ufalme wake.  Watu hawa waliendelea kufanya kazi ile waliokuwa wakifanya lakini hawakuwa wa ulimwengu huu.  Waliishi ulimwenguni na waliendelea kufanya biashara zao, na hata kufanya kazi katika afisi za serikali na kufanya mambo mengine mengi, lakini hawakuwa wa ulimwengu huu.  Heshima na mamlaka ya watu wa ulimwengu hayakuwa mambo ya muhimu sana maishani mwao kwani hawakuwa wanatumaini vitu vya ulimwengu huu, badala yake wao sasa walikuwa wafanyakazi wa Mungu.  Walimtumikia Mungu katika sehemu zao za kazi, walimtumikia Mungu kwa kumsifu na kumheshimu.  Kwa hivyo watu hawa hawakusema uongo katika sehemu zao za kazi, kuchukua ama kupeana hongo, ama kufuata anasa za dunia kila wakati.  Waliishi maisha yao kwa kumtukuza Mungu.  Hivi ndivyo neno “kanisa” linamaanisha.  Linamaanisha kusanyiko la watu ambao wameitwa kutoka kwa maisha ya dunia na kuingia katika ufalme wa Mungu na kuishi maisha ya kumcha Mungu.

 

2.  Ni kanisa la Mungu aliye hai.

 

Hii inamaanisha kwamba kiongozi na mwenye kanisa ni Mungu.  Washirika wa kanisa wana mwenyewe, wao ni mali ya Mungu.  Wanapaswa kuishi maisha ya kumtii Mungu na kumheshimu na kumtukuza Mungu.

 

Hii inamaanisha kwamba Mungu aliye hai anaishi ndani ya watu wake wanapokusanyika.  Mungu anaishi ndani ya kila mshirika na pia anaishi ndani ya kusanyiko lote la watu wake.  Ni Yeye ambaye analipatia kanisa lake kutambulikana na kuwa na umoja.  Hii ndiyo sababu makanisa mengi yamejumlisha watu kutoka mataifa tofauti tofauti na kabila tofauti tofauti, kwa sababu Mungu aliye hai amewaleta katika kanisa lake na amewapatanisha pamoja kuwa watu wake.

 

Hii inamaanisha kwamba Mungu anafanya kazi katika kila mmoja wa watu wake akimkamilisha na kumtayarisha kuingia mbinguni.  Ni Mungu aliye hai ambaye anawapa washirika wake vipawa.  Mungu anawapa vipawa hivi bila malipo ili mtu avitumie kwa kufaidi kanisa lote: “Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa roho kwa faida ya wote” (1 Wakorintho 12:7).  Vipawa hivi vinapeanwa ili watu wa Mungu waendelee kukamilika na kubadilika ili wafanane na Bwana Yesu Kristo.

 

Hii inamaanisha kwamba siku moja Mungu aliye hai atawachukua watu wake na kuishi nao milele.  Bwana Yesu atakaporudi, kila kusanyiko litakuwa kamilifu na bila kasoro na Bwana Yesu atalichukua kuwa nalo milele.

 

III. Kanisa ndilo nguzo la msingi wa kweli.

 

Hivi ndivyo Paulo anaendelea kusema kuhusu kanisa katika 1 Timotheo 3:15.  Neno “kweli” linamaanisha neno la Mungu: “Neno lako ndilo kweli” (Yohana 17:17).  Paulo anaposema kwamba kanisa ndilo nguzo la kweli, anamaanisha mambo matatu.

 

1.  Anamaanisha kwamba kanisa linahubiri na linafundisha ukweli.

 

Nguzo hushikilia nyumba na vivyo hivyo kanisa linashikilia ukweli mbele ya kila mtu.  Kazi ya kanisa ni kuhubiri na kufundisha neno la Mungu kwa wale ambao hawajaokoka ili wasikie Kristo kwamba yeye ndiye njia moja tu ya wokovu ili waje kwake kwa imani na awaokoe kupitia kifo chake msalabani.  Kanisa pia linafundisha na linahubiri neno la Mungu kwa wale wameokoka kwa sababu Mungu anatumia neno lake kutuosha dhambi zetu na kutufanya kuwa watakatifu, wasafi na wakamilifu (Waefeso 5:25-26).  Nyakati zingine tunasikia kanisa ambalo lina matatizo mengi.  Tunasikia mingawanyiko na vita kati ya viongozi kanisani.  Nyakati zingine hata tunaona katika televisheni ama tunasoma magazetini matatizo ya kanisa.

 

Ikiwa kanisa liko na matatizo mengi sana kama haya kwa muda mrefu na hayaishi, basi kuna uwezekano kwamba neno la Mungu haifundishwi katika kanisa hilo.  Mchungaji anaweza kusimama kanisani kila wiki na kuhubiri lakini awe hafundishi neno la Mungu, bali anahubiri maoni yake mwenyewe.  Yeye hasomi kifungu kutoka kwa Bibilia na kukifafanua.  Ikiwa neno la Mungu litahubiriwa kwa uaminifu basi watu watakua katika kweli na kuelewa neno la Mungu na wataanza kuishi maisha ya kutii neno la Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.  Makanisa yatakuwa na shida nyingi, lakini ikiwa kanisa litakuwa na shida fulani kila wakati basi inamaanisha hakuna kuelewa ama kutii neno la Mungu katika kanisa hilo.

 

 

2.  Hii inamaanisha kwamba kanisa litaheshimu neno la Mungu kwa kuishi maisha ya kutii.

 

Haitoshi tu kuwa na wahubiri wazuri katika madhabahu.  Haitoshi tu kuwa na watu kila siku wakisikiliza neno na kuandika kila kitu wanachofundishwa.  Haitoshi tu watu kuelewa ni nini Biblia inafundisha.  Mambo haya pekee hayataleta heshima kwa Mungu.  Ni wakati tu watu watakapoishi maisha yao kuambatana na neno la Mungu ndipo neno la Mungu litaheshimiwa.  Ni wakati tu watu wanapoishi maisha yao kwa kutii neno la Mungu ndipo wanamletea Mungu utukufu na sifa.  Mtume Paulo aliandika, “Wafundisheni watumwa kuwatii mabwana zao katika kila jambo, wakijitahidi kuwapendeza wala wasijibizane nao, wala wasiwaibie, bali watumwa waonyeshe kuwa wanaweza kuaminika kabisa, ili kwamba kwa kila namna wayafanye mafundisho ya Mungu Mwokozi wetu kuwa ya kupendeza” (Tito 2:9-10).  Bwana Yesu alisema, “Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:16).

 

3.  Hii inamaanisha kwamba kanisa linatetea kweli.

 

Neno la Mungu limeshambuliwa na maadui kwa miaka mingi na litaendelea kushambuliwa.  Watu wa dunia wanalichukia neno la Mungu kwa sababu wanamchukia Mungu.  Neno la Mungu linawadhihirishia kwamba wao ni wenye dhambi na kwa hivyo wanalichukia na wanajaribu kuliangamiza, lakini kanisa ni nguzo na msingi wa kweli.  Kama vile nguzo hushikilia nyumba ili isianguke chini, vivyo hivyo kanisa linashikilia Biblia na kulilinda kutokana na kushambuliwa.  Neno la Mungu linashambuliwa kwa njia tofauti tofauti.

 

(i) Kuna watu humu duniani ambao wanakataa kwamba Biblia ni neno la Mungu.  Baadhi ya watu hawa ni wale ambao wanafuata dini zingine, lakini pia kunao ambao wanadai kuwa wakristo, lakini wanasema kwamba Biblia iliandikwa na wanadamu na kwa hivyo ni kazi ya mwanadamu wala si neno la Mungu.  Hii ndiyo sababu wachungaji na makasisi wengine wanaruhusu dhambi kutendeka kama kufanya ndoa za jinsia moja, yaani mwanaume kumwoa mwanaume.  Biblia inasema wazi kwamba hii ni dhambi lakini wachungaji na makasisi hawa wanasema kwamba Biblia si neno la Mungu na kwamba Mungu hatahukumu mambo kama hayo.  Kanisa ni lazima itetee neno la Mungu dhidi ya watu hao.

 

(ii) Kuna watu wengine ambao wanakataa kwamba Biblia pekee ni neno la Mungu.  Wanadai kwamba wao wako na ufunuo mpya kutoka kwa Mungu na wanadai kwamba kile ambacho wamepokea ni neno la Mungu.  Katika makanisa mengi hapa nchini mwetu utasikia mtu akisema hivi, “Mungu aliongea na mimi na akaniambia jambo fulani,” halafu anaanza kufundisha jambo hilo kwa watu wengine.  Kile watu hawa wanasema ni kwamba si Biblia pekee ambalo ni neno la Mungu, bali wanadai kwamba Mungu anaendelea kuzungumza na watu leo.  Hayo ni mafundisho ya uongo.  Maneno ya mwisho katika Biblia ni haya: “Namwonya kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza chochote Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.” (Ufunuo 22:18).

 

(iii) Kuna watu wengine pia wanadai kwamba Mungu hakupeana neno lake kwa watu wake wote. Wanadai kwamba ni wao tu wenyewe wanaweza kueleza wengine ni nini neno la Mungu linamaanisha.  Kuna wachungaji siku hizi wanawaambia washirika wao, “Biblia ni ngumu sana kwako kulielewa, hupaswi kulisoma, nitakueleza kila Jumapili.”  Pia haya ni mafundisho ya uongo.  Mungu alipopeana neno lake, alilipeana kwa watu wake wote, siyo watu fulani tu.  Hii inamaanisha kwamba sisi sote tuko na wajibu wa kusoma na kuelewa Biblia.  Ni kweli kuna mambo katika Biblia ambayo ni magumu kuelewa lakini kuna mambo mengi tunaweza kuyaelewa.

 

(iv) Kuna watu wengine wanaosema kwamba Biblia haishughulikii mila.  Wanasema, “Tunajua kwamba Biblia inafundisha mambo fulani kuhusu ndoa na jinsi maisha ya ndoa yalivyo, kuhusu kifo na mazishi.  Lakini mila zetu zinaeleza mambo tofauti sana na hatuwezi tukaacha mila zetu.  Ni lazima tufuate mila zetu.”  Pia haya ni mafikira mabaya.  Ikiwa Biblia inatueleza wazi kuhusu jambo fulani ni lazima tufuate Biblia bila kujali ni nini mila zetu zinasema.

 

Haya ndiyo mafunzo ya uongo ambayo tunapata ulimwenguni leo, na kanisa kama nguzo na msingi wa kweli ni lazima litetee maandiko dhidi ya mafundisho ya uongo.

 

 

 

Funzo la Pili, Matendo 2:37-47, Washirika wa Kanisa.

 

Katika kifungu hiki tunasoma tukio la siku ya Pentekote.  Tunasoma kwamba watu wengi walikusanyika mahali mitume walikuwa, na Petro akawahubiria.  Baadaye tunaambiwa watu waliosikiliza mahubiri ya Petro yaliwachoma mioyo kwa sababu ya dhambi zao.  Watu hawa walitubu dhambi zao na wakabatizwa na wakawa washirika wa kanisa la Yerusalemu.  Katika kifungu hiki, tunasoma jinsi kanisa la kwanza ulimwenguni lilianza.  Pia kifungu hiki kinaendelea kutueleza ni nini watu walifanya baada ya kuwa washirika wa kanisa.  Biblia inafundisha wazi kwamba ni mapenzi ya Mungu kwamba kila mmoja wa watu wake awe mshirika wa kanisa.  Si vizuri mtu ambaye ameokoka kurada-randa kutoka kanisa moja hadi nyingine kila wakati.  Mapenzi ya Mungu ni kwamba tuwe washirika wa kanisa na tumtumikie katika kanisa hilo.  Hii ndiyo sababu wakati watu waliokoka siku ya Pentekote walianza kushiriki katika kanisa.  Katika kifungu hiki  tunasoma mambo fulani kuhusu washirika wa kanisa.

 

1.  Washirika wa kanisa ni lazima wawe watu ambao wameokoka.

 

Tunasoma katika kifungu hiki kwamba Petro alihubiria umati wa watu huko Yerusalemu jinsi walivyofanya dhambi kwa kumwua Mwana wa Mungu: “Ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimwua kwa kumgongemea msalabani” (Matendo 2:23).  “Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, 'Ndugu zetu tufanye nini?’” (Matendo 2:37).  Walisikia mahubiri kuhusu dhambi na walidhirishiwa dhambi zao na Roho Mtakatifu.  Walimwuliza Petro wafanye nini, na akawaambia watubu.  Hii inamaanisha ni lazima waache dhambi zao na kumgeukia Kristo pekee kwa msamaha wa dhambi zao.  Hivi ndivyo watu 3,000 walifanya siku hiyo huko Yerusalemu.  Walitubu dhambi zao zote na walimgeukia Kristo kwa imani na walipewa wokovu na msamaha wa dhambi na Mungu .

 

Hapa kuna funzo muhimu sana kwetu sisi kwamba, mtu ambaye hajaokoka hawezi kuwa mshirika wa kanisa.  Mtu ambaye hajaokoka anaweza kuja kanisani kila wiki lakini hiyo haimaanishi kuwa yeye ni mshirika wa kanisa, hata kama atasema kwamba yeye ni mshirika.  Kama vile tumeona katika funzo la kwanza kwamba kanisa ni watu wa Mungu, hekalu la Mungu na pia ni mwili wa Kristo.  Je, basi inawezekanaje mtu ambaye hajaokoka kuwa mshirika wa kanisa?  Mtu ambaye hajaokoka si mali ya Mungu bali ya shetani.  Mtu ambaye hajaokoka hayuko ndani ya nuru bali ako gizani.  “Kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu?  Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza?  Kuna mapatano gani kati ya Kristo na Belieri?  Yeye aaminiye ana sehemu gani na asiyeamini?” (2 Wakorintho 6:14-15).

 

Biblia inatueleza wazi kwamba ikiwa mtu anataka kuwa mshirika wa kanisa ni lazima awe ameokoka na ni lazima aonyeshe wazi kwamba jinsi anavyoishi maisha yake ameokoka.  Petro aliwaambia watu wa Yerusalemu siku ya Pentekote, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka” na hivi ndivyo walifanya kwa sababu tunasoma, “Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika kuumega mkate na katika kusali” (Matendo 2:42).  Hili ndilo lilikuwa hakikisho kwamba watu hawa walikuwa wameokoka: kwamba walijitolea kuishi maisha ya kumcha Mungu.

 

2.  Washirika wa kanisa lazima wabatizwe.

 

Wakati watu wa Yerusalemu walipomwuliza Petro, “Ndugu zetu tufanye nini?”  Petro aliwajibu na kusema, “Tubuni mkabatizwe kila mmoja abatizwe kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate msamaha wa dhambi zenu.”  Ilikuwa ni lazima wale wote ambao walikuwa wanataka kuwa washirika wa kanisa hili mpya la Yerusalemu kwanza kutubu dhambi zao na kubatizwa.  Hii ndiyo amri Petro alitoa kwa sababu ndiyo amri pia Kristo mwenyewe alitoa.  Kristo alisema, “Endeni ulimwenguni kote mkawafanye mataifa kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu” (Mathayo 28:19).  Tunaona amri hii wazi katika mafundisho ya Bwana Yesu Kristo.  Watu wa kwanza kukubali injili ya Yesu walifanywa kuwa wanafunzi halafu wakabatizwa.

 

Ubatizo ni jambo ambalo linaleta kuchanganyikiwa kwingi sana humu nchini mwetu, na watu wengi hawalielewi.  Kwa hivyo ni vizuri sana kwetu kuelewa mambo haya.

 

Ubatizo si:

 

Ubatizo siyo kupata wokovu.  Si kweli kwamba ikiwa mtu ambaye hajaokoka akibatizwa atapata wokovu.  Ubatizo hauokoi mtu.  Pia ubatizo hauoshi dhambi zetu.  Hili ni jambo ambalo watu wengi humu nchini wamechanganyikiwa sana nalo kwa sababu wanawaza kwamba ikiwa mtu anataka kuoshwa dhambi zake basi ni lazima abatizwe ili haya maji ya ubatizo yamwoshe dhambi zake.  Biblia inatufundisha wazi kwamba siyo maji ya ubatizo ambayo yanaosha dhambi zetu bali ni damu ya Bwana Yesu: “Damu ya Yesu, Mwana wake yatusafisha dhambi yote” (1 Yohana 1:7).  Hakuna mahali popote Biblia inatufundisha kwamba ubatizo unaosha dhambi zetu, lakini Biblia inafundisha wazi kwamba damu ya Yesu inatuosha kutoka kwa dhambi zetu.

 

Kwa hivyo Biblia inafundisha wazi kwamba ubatizo hauoshi dhambi zetu na pia ubatizo hautupatii wokovu.

 

Je, ubatizo ni nini?

 

Biblia inatufundisha kwamba ubatizo unaonyesha mambo mawili.

 

1. Kwanza, ubatizo unaonyesha kwamba mtu amekufa na Kristo na pia amefufuka katika maisha mapya na Kristo.  Mtu anapookoka hivi ndivyo mambo hufanyika ndani yake.  Mtu yule wa kale hufa, na Mungu anaumba mtu mwingine.  Hivi ndivyo Biblia inasema, “Hamjui kwamba ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?  Kwa hivyo tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti, ili kama vile Kristo alivyofufuka kutoka kwa wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo sisi nasi pia tupate kuenenda katika upya wa uzima” (Warumi 6:2-4).  Kumbuka ni nini Paulo anasema katika kifungu hiki, anasema kwamba tulizikwa pamoja na Kristo na pia tulifufuliwa katika maisha mapya pamoja na Kristo.  Hivi ndivyo inafanyika wakati mtu anapookoka.  Tunazaliwa mara ya pili kwa Roho Mtakatifu.  Mtu wa kale huwa anakufa na mtu mpya anaanza kuishi.

 

Hivi ndivyo ubatizo unaonyesha: Unaonyesha kwamba sisi tumefanywa wapya kupitia kwa imani ndani ya Kristo.

 

2. Ubatizo ni ishara kwamba dhambi zetu zimeoshwa na damu ya Yesu Kristo na kwamba tumesamehewa dhambi zetu zote.  Petro aliwaambia watu wa Yerusalemu siku ya Pentekote, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kusamehewa dhambi zenu” (Matendo 2:38).  Aliwaamuru watu wabatizwe kwa sababu walipotubu dhambi zao walimwamini Yesu Kristo ili wasamehewe dhambi zao.  Biblia inafundisha wazi kwamba ni lazima mtu atubu dhambi zake na kumwamini Bwana Yesu Kristo ili aokoke (Marko 1:15, Matendo 20:21).  Ubatizo basi ni ushuhuda kwa watu wote kwamba mtu anayebatizwa ametubu dhambi zake na amemwamini Yesu Kristo na kwamba amesamehewa dhambi zake zote.

 

Ni muhimu sana kujua hapa kwamba ubatizo ni ushuhuda ambao unaonyesha jambo lililofanyika ndani ya mtu.  Ni ushuhuda kwamba mtu ameokoka, amekufa na Bwana Yesu na amefufuka katika maisha mapya na Bwana Yesu, na kwamba dhambi zake zimeoshwa na kusamehewa kabisa.  Haya mambo yote hufanyika wakati mtu ameokoka wala si wakati mtu amebatizwa.  Ubatizo ni ushuhuda kwamba Mungu amemwokoa mtu.

 

3.  Washirika wa kanisa wanadumu katika mafundisho ya neno la Mungu.

 

Biblia inasema, “Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume” (Matendo 2:42).  Hili ndilo lilikuwa jambo la kwanza kwa wale wote waliokoka siku ya Pentekote.  Walidumu katika mafundisho ya mitume.  Mitume walikuwa watu ambao Bwana Yesu aliwachagua kwenda kuhubiri neno lake.  Hii inamaanisha, wakristo hawa wa kwanza walidumu katika neno la Mungu kila wakati.  Hili ni dhihirisho ya kwamba mtu ameokoka, kwamba anatamani neno la Mungu na anadumu ndani yake.  Mtu ambaye ameokoka hapendi tu kwenda kanisa mahali ambapo mchungaji hafundishi neno la Mungu bali mawazo yake.  Mafundisho ya aina hiyo haimletei furaha mtu ambaye ameokoka.  Mtu ambaye ameokoka huwa hataki kusikia mahubiri kuhusu mawazo ya mwanadamu bali anataka kulishwa neno la Mungu na anataka kuishi maisha yake hapa ulimwenguni akiongozwa na neno la Mungu.

 

4.  Washirika wa kanisa wanadumu katika ushirika.

 

Biblia inasema, “Walidumu katika ushirika.”  Kanisa ni jamii, si kusanyiko tu la watu ambao wanakutana tu siku ya Jumapili.  Ni kusanyiko la watu ambao wanashiriki pamoja katika kila jambo, yaani kila mmoja anamjali mwingine, wanaomba pamoja na wanatumia vipawa ambavyo Mungu amewapa kuwatumikia wenzao.  Mtu ambaye ni mshirika wa kanisa huwa anaenda kanisa kila Jumapili ili akutane na washirika wenzake ili awahimize na awatumukie.  Mshirika wa kanisa hazururi kutoka kanisa moja hadi lingine bali huwa anashiriki katika kanisa moja tu na anamtumikia Mungu akiwa katika kanisa hilo.  Anaweza kuwa na ushirika na wakristo wengine, lakini anadumu katika kanisa moja.

 

Kuwa mshirika wa kanisa ni jambo la kutiliwa maanani sana.  Si kweli kwamba ikiwa unaenda kanisa fulani kila Juma pili wewe ni mshirika wa kanisa hilo.  Kuna mpangilio ambapo mtu anakuwa mshirika wa kanisa.  Hii ni kwa sababu washirika wa kanisa fulani ni lazima wadumu katika kanisa hilo.  Kabla mtu hajakuwa mshirika wa kanisa, ni lazima aongee na wachungaji wa kanisa na washirika wa kanisa.  Ni lazima mtu huyo ajue kwamba atadumu katika kanisa hilo na hataliacha.

 

5.  Washirika wa kanisa wanautegemea msalaba wa Bwana Yesu Kristo.

 

Tunasoma, “Wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika na katika kumega mkate.”  Mambo haya yanahusu meza ya Bwana na tunaelezwa kwamba meza ya Bwana ilikuwa jambo muhimu sana katika kanisa la Yerusalemu.  Sababu kuu ya kuwa na meza ya Bwana ni kukumbuka kifo cha Bwana Yesu Kristo.  Bwana Yesu alisema, “Huu ndio mwili wangu ambao ni kwa ajili yenu.  Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu,” na, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu.  Fanyeni hivi kila mnywapo kwa ukumbusho wangu” (1 Wakorintho 11:23-25).

 

Kwa hivyo wakati Biblia inasema kwamba kanisa la kwanza walidumu katika kumega mkate, inamaanisha kwamba walikuwa wanawaza kila wakati katika akili zao kuhusu mambo ya kifo cha Bwana Yesu msalabani.  Siyo vigumu kujua ni kwa nini walikuwa wakifanya jambo hili.  Ni rahisi sana kwa kanisa kukosa mwelekeo wao na kuanza kushughulika na mambo mengine.  Makanisa mengi hapa nchini mwetu siku hizi wanatilia mkazo sana kuhusu mambo ya wachungaji na maaskofu na mavazi ya waimbaji, mijengo, mambo ya arusi na mambo ya mazishi na pesa.  Mambo haya na mengine mengi yanaonekana kuwa ya muhimu sana na yanachukua nafasi kubwa sana katika kanisa.  Ni jambo la kuhuzunisha sana kwamba mara mingi hatusikii mahubiri ya Yesu Kristo na kusulibiwa kwake.  Mahubiri mengi yanahusu jinsi mtu anaweza kufaulu katika biashara yake, katika ndoa yake na kuhusu kazi kuu ya mchungaji.  Kanisa la kwanza lilikuwa na lengo moja kabisa ambalo lilikuwa ni Kristo pekee.  Kristo ndiye msingi, kichwa na ndiye moyo wa kanisa.

 

6.  Washirika wa Kanisa wanaombeana.

 

Tunasoma katika kifungu hiki kwamba walikuwa wakidumu katika kusali.  Maombi ni jukumu ambalo limepewa kila mkristo.  Kila mkristo anapaswa kumwombea mshirika mwenzake katika kanisa.  Maombi ni muhimu kwa sababu maisha ya mkristo na maisha ya kanisa yote iko mikononi mwa Mungu.  Ni Mungu ambaye anatuokoa na anatulinda na anatuwezesha kukua na kumtumikia.  Kwa hivyo ni muhimu sana kwetu kuenda mbele ya Mungu kwa maombi tukiwaombea washirika wa kanisa ili wasianguke bali wakue katika imani yao na wamheshimu Mungu maishani mwao.

 

 

 

 

Funzo La Tatu, 1 Timotheo 3:1-13, Afisi za Kanisa.

 

Katika kifungu hiki mtume Paulo anatupatia mwongozo kuhusu afisi za kanisa.  Ni vizuri kujua kwamba kanisa liko na afisi mbili tu za wasimamizi, yaani maaskofu na mashemasi.  Agano Jipya halizungumzi mambo kama mchungaji mkubwa na mchungaji msaidizi, ama mchungaji wa vijana.  Agano Jipya linasema kwamba kanisa liwe na wachungaji na mashemasi, na katika kifungu hiki tunaona jinsi wanafaa kuwa.

 

I.  Mchungaji, askofu na mzee wa kanisa.

 

Kuna kuchanganyikiwa kwingi sana hapa nchini mwetu kuhusu afisi hizi tatu.  Katika makanisa mengi tunaona kwamba haya mambo matatu yanamaanisha vitu tofauti tofauti.  Tunaona kwamba kanisa liko na Askofu ambaye ndiye mkuu wa mkoa ama kiongozi wa dhehebu yote, pia tunaona kwamba kunao wazee ambao ndio kamati ya kuendeleza mambo ya kanisa na mwisho kuna mchungaji ambaye kazi yake ni kuhubiri, kuunganisha ndoa na kufanya mambo mengine.  Swali ambalo tunapaswa kujiuliza ni, je, mpangilio huu unaambatana na Biblia?  Tukiangalia Biblia tunapata kwamba huu mpangilio haumo.  Kuna vifungu viwili ambavyo vinatueleza jinsi kanisa la Agani Jipya lilifanya mambo.

 

1. Kifungu hiki ni muhimu sana (Matendo 20:17-38).  Kuna mistari miwili ambayo ni muhimu sana hapa.  Kwanza katika mstari wa 17 tunaambiwa, “Paulo akiwa Mileto, akatuma ujumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kanisa waje wakutane naye.”  Kwa hivyo wazee wa kanisa la Efeso walienda kukutana na Paulo Mileto.  Kumbuka mstari 18 unaongea kuhusu “wao” yaani wazee kwa jumla ambao walienda kukutana na Paulo.  Katika msitari wa 28 tunasoma mashauri ya Paulo kwa wazee hawa wa kanisa akiwaambia, “Jilindeni nafsi zenu na lilindeni lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake.  Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.”

 

Kuna maneno matatu hapa ambayo ni muhimu sana kwetu.  Kwanza kukumbuka kwamba Paulo anaongea na wazee wa kanisa la Efeso.  Pili kumbuka kwamba anawaambia kuwa Mungu amewafanya kuwa “waangalizi”.  Neno hili waangalizi pia linatafsiriwa katika Agano Jipya kuwa “Askofu” (angalia 1 Timotheo 3:2, Tito 1:7).  Pia Paulo anawaambia hawa wazee, ambao Mungu aliwafanya kuwa maaskofu, kwamba wanafaa “kulinda” kanisa la Mungu.  Neno “mlinzi” pia linamaanisha “mchungaji”.

 

2. Kifungu kingine ambacho ni muhimu sana katika jambo hili ni 1 Petro 5:1-2.  Hapa Petro anaandika, “Kwa wazee waliomo miongoni mwetu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shaidi wa mateso ya Kristo na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa, lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi.”  Pia hapa tunaona haya maneno matatu tena, yaani wazee, wachungaji na maaskofu na maneno haya yote yanahusu kundi moja la watu.  Petro anawaambia wachungaji wa makanisa kwamba wanapaswa kulinda ama kuchunga kundi la Mungu ambalo wao ndiyo waangalizi.

Kwa hivyo kutokana na mafundisho haya tunaona kwamba kuna kundi la wanaume katika kila kanisa ambalo Mungu amewapa kipawa cha kutumika kama wazee.  Watu hawa wanateuliwa na kanisa kuwa wazee.  Wao wakiwa wazee wa kanisa wako na majukumu mawili: kulinda na kuwa waangalizi wa kundi la watu wa Mungu.  Hizi ndizo njia mbili ambazo mzee wa kanisa anapaswa kufanya kazi yake.  Anawalisha watu wa Mungu kwa neno la Mungu na anawatumikia akiwa askofu kwa kuwaongoza katika mambo ya kanisa.  Kanisa ni lazima liwe na mwongozo mzuri wa Biblia na mchungaji anapaswa kuongoza kanisa katika jambo hili.  Katika Agano Jipya, mchungaji ni mzee wa kanisa na ni askofu ya lile kansia.  Mpangilio tunaouona leo makanisani kwamba kuna mchungaji na pia kuna askofu aliye na mamlaka kuliko mchungaji, haupatikani mahali popote katika Agano Jipya.

 

II. Kazi ya wazee wa kanisa na mashemasi.

 

Katika kitabu cha matendo ya mitume 6:1-6 tunasoma kwamba kanisa la Yerusalemu lilikuwa na afisi mbili.  Mitume walikuwa wanafanya kazi ya kufundisha neno na kuomba, na kundi lingine la wanaume saba lilichanguliwa ili lifanye kazi ya kugawa chakula kwa wajane.  Kwa hivyo kanisa la Yerusalemu ni mfano wa jinsi kanisa la leo linapaswa kuwa.  Ijapokuwa wazee wa kanisa siyo mitume, kanisa la Yerusalemu ndiyo mfano ambao tunapaswa kuufuata leo.  Kazi kuu ya  wachungaji ni kufundisha neno la Mungu na kuomba.  Hii inamaanisha kwamba kazi yao kuu ni kuwaombea washirika wa kanisa na kazi zinazofanyika kanisani.  Kazi yao pia ni kuhubiri na kufundisha neno la Mungu.  Siyo vyema kwa mchungaji kushughulika na mambo ya aina ingine ya kanisa.  Mambo ya pesa za kanisa na mambo ya kushughulikia mijengo siyo kazi ya mchungaji.  Kazi ya mchungaji kuu ni kuhubiri na kuomba na kufundisha neno la Mungu.

 

Wanaume saba waliochaguliwa na kanisa la Yerusalemu ndiyo mfano wa mashemasi wa kanisa leo.  Hawa walishughulika na mambo mengine ya kanisa na kuhakikisha kwamba chakula kimegawanywa kwa wajane inavyostahili.  Kwa hivyo mashemasi wanapaswa kushughulikia mambo ya pesa za kanisa, mambo ya mijengo na shughuli zingine zote za kanisa.  Biblia inafundisha kwamba mashemasi wanapaswa kuwa watu ambao wamekomaa katika ukristo wao.  Wanaume saba waliochaguliwa na kanisa la Yerusalemu walikuwa “Wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima.”  Walikuwa watu ambao wameokoka.  Pia hii haimaanishi kwamba shemasi anapaswa tu kushughulika na mahitaji ya kanisa pekee.  Katika kitabu cha Matendo ya Mitume tunaona wawili wa mashemasi walikuwa wahubiri wakuu wa neno la Mungu, yaani Filipo na Stefano.  Kila kanisa linapaswa kuomba kwamba mashemasi wao wawe wahubiri wakuu.

 

III. Mchungaji anapaswa kuwa namna gani.

 

Katika kitabu cha 1 Timotheo 3:1-7 Biblia inatueleza jinsi mchungaji anafaa awe.

 

1.  Anafaa kutamani kazi hiyo.  Paulo anasema, “Mtu akitamani kazi ya uaskofu, atamani kazi nzuri” (msitari wa 1).  Biblia inasema wazi kwamba mtu anapaswa kuingia kwa kazi hii akiwa ameitamani.  Petro anasema kwamba kazi ya mzee wa kanisa ni kutumika, “Si kwa kulazimishwa bali kwa hiari” (1 Petro 5:2).  Inawezekana kuna mtu ndani ya kanisa anayeonekana kuwa tayari kabisa kufanya kazi hii ya uaskofu lakini kwa sababu zake mwenyewe hataki kufanya kazi hii.  Haitakuwa mzuri kwa kanisa kumlazimisha mtu huyu kufanya kazi hii.  Inawezekana mchungaji kuwa na mtoto wake kijana ambaye alikuwa akitarajia kwamba atakuwa mchungaji na kwa hivyo anaanza kulazimisha kijana kufanya kazi hii ya uaskofu.  Hivyo si vizuri.  Ni lazima mtu atamani hii kazi ya uaskofu.

 

2.  Askofu anapaswa kusimamia nyumba yake vizuri.  Hili ndilo jambo la kwanza kabisa Paulo anaeleza hapa.  Haanzi kwa kueleza kuhusu uwezo wa kufundisha ama wa kuongoza bali jambo la kwanza ni maisha ya mtu huyu nyumbani kwake.  Paulo anasema mambo mawili kuhusu jambo hili hapa.

 

(i) Ni lazima awe mume wa mke mmoja (msitari wa 2).  Mume aliye na mke zaidi ya mmoja anaweza kubatizwa na kuwa mshirika wa kanisa lakini hawezi kuchaguliwa katika afisi yoyote ya kanisa kuwa mchungaji au shemasi.  Ni wale tu wako na mke mmoja ambao wanafaa kuwa wachungaji ama mashemasi.  Kumbuka pia hapa Paulo hasemi kwamba mchungaji ni lazima awe ameoa.  Inawezekana sana kwa mtu ambaye hajaoa kuwa mchungaji wa kanisa.

 

(ii) Ni lazima aweze kusimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia (msitari wa 4).  Hii inamaanisha kwamba mchungaji ni lazima aonyeshe kwamba ana mamlaka kwa watoto wake na kwamba watoto wake wanamtii.  Mara mingi tunawaona watu ambao ni wadhaifu sana kwa kutawala nyumbani zao, kwamba hata watoto wao hawana heshima bali wanaishi maisha ya dhambi na anaonekana kuwa hawezi kuwaongoza kamwe.  Mtu kama huyo, Paulo anasema hafai kuwa mchungaji wa kanisa. Sababu ya Paulo kusema hivi iko katika msitari wa 5, “Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?”  Mojawapo ya mambo mchungaji anafanya katika kanisa ni kuongoza kanisa.  Anapaswa kuhakikisha kwamba kuna mpangilio katika kila jambo kanisani na ikiwa kuna mshirika ambaye anaishi maisha ya dhambi mchungaji anapaswa kulishughulikia jambo hilo.  Ikiwa mtu ameonyesha kuwa dhaifu katika nyumba yake basi hataweza kuwashughulikia wale washirika wanaotenda dhambi ipasavyo.

 

3.  Mchungaji anafaa kuwa mtu asiye na lawama.  Paulo anasema mchungaji anapaswa kuwa, “Mtu asiye na lawama, mkarimu, mwenye kiasi, asiwe mlevi wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha” (Msitari 2-3).  Haya mambo yote yanahusu hali ya mchungaji kwamba anapaswa kuwa mtu mwenye kiasi, mpole, asiye mgomvi.  Kuhusu pesa anafaa asiwe mpenda pesa ama mtu wa tamaa.  Mtu ambaye kila wakati anafikiria kuhusu pesa, anatamani pesa na kushughulika na njia za kupata pesa, na mahubiri yake pia anahubiri kuhusu pesa, hafai kamwe kuwa mchungaji wa kanisa.

 

4.  Mchungaji anafaa kuwa anajua kufundisha.  Hivi ndivyo Paulo anasema katika msitari wa 2, na hii ndiyo kazi kuu ya mchungaji.  Kuna mambo matatu kuhusu jambo hili ambayo tunapaswa kuelewa.

 

(i) Mchungaji ni lazima ajue Biblia na mafundisho ya Biblia vizuri.  Kwa sababu kazi yake ni kufundisha Biblia, hawezi kuwa mtu ambaye anajua tu Biblia hapa na pale na hajui mafundisho ambayo maandiko yanafundisha.  Si lazima awe amehudhuria chuo cha Biblia lakini ni lazima ahakikishe kwamba anasoma Biblia kila siku na anasoma vitabu vinavyoeleza mafundisho ya Biblia.  Bila kujua Biblia vizuri mchungaji hawezi akafanya kazi yake vizuri.

 

(ii) Mchungaji anafaa ajue kufundisha Biblia, lakini hii haimaanishi ni wachungaji wote wanaweza kuhubiri katika madhabahu.  Kuna wachungaji ambao wako na kipawa cha kuhubiria umati mkubwa na pia kuna wengine ambao wana kipawa cha kuwatembelea washirika na kuwahimiza na kuwafunza neno la Mungu wakiwa nyumbani mwao.  Si hekima kwa kanisa kusisitiza kwamba ni lazima mtu awe anaweza kuhubiri katika madhabahu ili ateuliwe kuwa mchungaji.  Ikiwa mtu anawatembelea washirika nyumbani mwao na kila nyumba anafundisha neno la Mungu na kuwahimiza watu kumfuata Bwana Yesu basi mtu huyo anafanya kazi ya mchungaji.

 

(iii) Wazee wa kanisa wote ni wachungaji.  Hii haimaanishi kwamba wote wanahusika na kazi ya uchungaji kila siku kanisani.  Kwa mfano, kanisa linaweza kuwa na wachungaji wanne.  Watatu wanaweza kuwa wanafanya kazi sehemu zingine na mmoja ndiye anayeajiriwa na kanisa na ndiye ako kanisani kila siku.  Hawa wote ni wachungaji na wao wote wako kiwango moja, lakini yule mmoja ambaye ameajiriwa na kanisa ameteuliwa kwa kazi ya kuhubiri na kufundisha kanisa neno la Mungu kila wakati.  Kanisa la Agano Jipya lilifuata mtindo huu kwa sababu Paulo anasema, “Wazee wa kanisa wanaoongoza shughuli za kanisa vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha” (1 Timotheo 5:17).

 

5.  Mchungaji ni lazima awe amekomaa kwa ukristo.  Mchungaji hafai kuwa mtu ambaye amaeokoka juzijuzi.  Paulo anasema katika msitari wa 6 kwamba, “Asiwe mtu ameokoka karibuni asije akajivuna na kuanguka kwenye hukumu ile ile ya shetani.”  Kuwa katika cheo cha mchungaji katika kanisa ni kazi ngumu sana na yeyote anayetamani kazi hii ni lazima awe mwangalifu sana.  Ni rahisi sana kwa mchungaji kuwa na kiburi kwa sababu amewekwa katika cheo cha uongozi wa kanisa, mara mingi jambo hili linafanyika kwa wale ambao hawajakomaa katika maisha ya ukristo na ni vijana.  Kiburi ni mojawapo ya dhambi mbaya zaidi katika Biblia na hapa Paulo anasema kwamba ni dhambi hii ya kiburi ambayo ilimfanya shetani kuanguka.  Ni lazima mchungaji ajichunguze sana ili asije akaanguka katika dhambi hii ya kiburi, kupuuza watu na kuwa mdanganyifu.  Ni lazima ajichunguze sana ili asije akaanza kuona kwamba yeye ni mtu muhimu sana kuliko watu wengine, yaani kuwaza kwamba yeye ni mtu wa kiroho sana na amebarikiwa sana kuliko watu wengine.  Akifanya hivi, hiyo ndiyo itakuwa mwanzo wa kuanguka kwake, “Kiburi hutangulia maangamizi, roho ya majivuno kabla ya uanguko” (Mithali 16:18), na “Kiburi cha mtu humshusha” (Mithali 29:23).

 

6.  Mchungaji anapaswa kuwa na ushuhuda mzuri hapa duniani.  Paulo anasema, “Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi” (msitari 7).  Sisi sote tunajua kwamba watu wanawazia kanisa kulingana na tabia ya wachungaji wake.  Ikiwa mchungaji wa kanisa ako na tabia ya kuwa na tamaa ama mambo ambayo hayaambatani na neno la Mungu, basi watu watasema kwamba kanisa hilo ni ya watu wa tamaa.  Kwa hivyo ni jambo muhimu sana mchungaji kuwa na ushuhuda mzuri akiwa humu duniani.  Wakati watu wanaanza kusema kwamba tabia ya mchungaji fulani ni mbaya basi mchungaji huyo hafai kamwe kuwa katika afisi ya wazee wa kanisa bali anapaswa kujiuzuru.

 

IV.  Jinsi mashemasi wanapaswa kuwa.

 

Baada ya kumaliza kushughulikia jinsi wazee wa kanisa wanafaa kuwa, Paulo anaenelea kueleza kuhusu cheo cha mashemasi kanisani.  Tazama jinsi sentensi hii inaanza, “Vivyo hivyo.” Kumaanisha kwamba mambo mengi ambayo mtu anafaa kuwa nayo ili awe mchungaji ni hayo hayo tu ambayo mtu anafaa kuwa nayo ili awe shemasi.  Tutaangazia mambo haya kila moja baada ya lingine.

 

1.  Tabia ya shemasi.  Paulo anasema, “Mashemasi, Vivyo hivyo nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali” (msitari 8).  Shemasi anapaswa kuwa mtu ambaye anaheshimika, kumaanisha kwamba anafaa kuwa mtu ambaye anaheshimika.  Pia shemasi anapaswa asiwe mtu wa kuongea ongea maneno ovyo ovyo kwamba anamwambia mtu jambo fulani halafu anamwambia mwingine jambo lingine.  Pia kama tu ilivyo na mzee wa kanisa, shemasi hapaswi kuwa mlevi na mtu ambaye anatamani pesa.

 

2.  Jinsi shemasi anawashughulikia washirika wa kanisa.  Katika msitari wa 9 Paulo anaeleza kuwa shemasi anafaa, “Kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamira safi.”  Je, hii inamaanisha nini?  Neno siri ya imani inamaana fulani katika maandiko haya ya Paulo na inaelezwa wazi sana katika kitabu cha Waefeso 3:6, “Siri hii ni kwamba, kwa njia ya Injili, watu wa mataifa ni warithi pamoja na Israeli, viungo vya mwili mmoja na washiriki pamoja wa ahadi katika Kristo Yesu.”  Siri hii ni kwamba katika Agano Jipya hakuna mpaka kati ya Wayunani na Wayahudi, bali wote wako sawa machoni pa Mungu.  Tunapaswa kujiuliza swali hili, “Je, ni kwa nini shemasi anaambiwa ni lazima aishikilie siri hii ya imani kwa dhamira safi?”  Jibu ni kwa sababu shemasi atakuwa akishughulika na mahitaji ya kanisa lote na mara mingi anaweza kujaribiwa kupendelea upande mmoja.  Jambo hili la kupendelea upande mmoja ndilo lilikuwa shida katika kanisa la Yerusalemu wakati shemasi walichaguliwa mara ya kwanza, Wayahudi wa Kiyunani walikuwa wanasahauliwa wakati wa kupeana chakula kwa wajane (Matendo 6:1-6).  Shemasi anapaswa kuwa si mtu wa mapendeleo kwa sababu akipendelea atasababisha mgawanyiko ndani ya kanisa.  Wakati kanisa linachunguza mtu ili kuona kama anafaa kuwa shemasi ni lazima wahakikishe kwamba hatakuwa anapendelea jamii yake na marafiki wake wakati anashughulika na mahitaji ya kanisa.

 

3.  Shemasi anafaa awe mtu ambaye amekomaa kwa ukristo.  Katika msitari wa 10 Paulo anasema, “Ni lazima wapimwe kwanza, kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.”  Paulo hapa anawahimiza wakristo wahakikishe kwamba kuna muda wa kupima mtu kabla ya kumchagua kuwa shemasi.  Hili si jambo gumu kufanya.  Shemasi anashungulika na mambo ya pesa, mijengo na kazi ya kanisa ya kila siku.  Ikiwa kanisa inaona kwamba mtu fulani anaweza kufanya kazi hii ya shemasi anaweza kupatiwa muda wa siku fulani na aangaliwe jinsi anavyoshughulikia kazi hizi.  Ikiwa atafaulu katika kufanya na kuongoza kazi na kuwa mwaminifu basi anaweza kuchaguliwa kuwa shemasi.

 

4.  Jamii ya shemasi.  Katika msitari wa 11-12 Paulo anasema, “Vivyo hivyo wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio zungumza maneno ya kuwadhuru wengine, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.  Shemasi anafaa awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vema.”  Kwa sababu shemasi ni mtu ambaye ana jukumu kanisani basi bibi yake anafaa kuwa mtu ambaye anastahili heshima na ambaye ako na tabia mzuri.  Pia shemasi hafai kuwa mtu ambaye ako na mke zaidi ya mmoja na anafaa kuonyesha kuwa anaweza kuongoza nyumba yake vyema.

 

5.  Matokeo ya kazi ya uaminifu ya shemasi.  Katika msitari wa 13 Paulo anasema, “Wale ambao wamehudumu vema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu.”  Shemasi waaminifu hujipatia msimamo mzuri.  Kwa haya yote Paulo anamaanisha kwamba mashemasi watakuwa na jina zuri katika kanisa na hata katika jamii.  Shemasi waaminifu watakuwa na imani ya nguvu sana.  Hii inamaanisha kwamba ikiwa watatumikia kanisa kwa njia inayofaa basi watawashuhudia watu wengi kwa ushuhuda wao.

 

V.  Jinsi ya kuwachagua wazee wa kanisa na mashemasi.

 

Ni vizuri sana kwa kanisa kufuata njia inayoonyeshwa katika Biblia wakati wanachagua wazee wa kanisa na mashemasi, kwa sababu afisi hizi mbili zote ni muhimu sana katika maisha ya kanisa.

 

1. Jinsi ya kuwachagua wachungaji wa kanisa.

 

Katika kitabu cha Matendo ya Mitume 14:23 tunasoma, “Nao baada ya kuwawekea wazee katika kila kanisa, kwa kufunga na kuomba ambaye wamemwamini wakawakabidhi kwa Bwana waliyemwamini.”  Jambo hili lilitokea karibu mwisho wa safari ya kwanza ya mtume Paulo.  Paulo na Barnaba walitembelea miji mingi katika sehemu inayojulikana siku hizi kuwa Uturuki wakihubiri injili na watu wakaokoka.  Walipokuwa wakirudi waliwatembelea wakristo hawa na wakawafanya kuwa kanisa.  Mistari hii inatuonyesha mambo mawili ambayo yanapaswa kutuongoza kuhusu jinsi tunapaswa kuwachagua wachungaji katika kila kanisa.

 

(i) Wachungaji wanapaswa kuchaguliwa kwa njia ya washirika kupiga kura.  Katika kifungu hiki tunalo neno “Kuwawekea.”  Ni kweli hatuwezi kabisa kujua maana ya neno hili lakini ni wazi kwamba neno hili lina maana ya washirika kupiga kura kwa kumchagua kiongozi.  Inaonekana wazi kwamba si Paulo na Barnaba waliwachagua wachungaji halafu wakawapeana kwa makanisa bali washirika wa kanisa walishiriki katika hiyo kazi ya kuwachagua viongozi.  Kutokana na jambo hili tunaweza kusema kwamba hakuna mchungaji anapaswa kuchaguliwa kuwa kiongozi wa kanisa pasipo kanisa lote kumchagua.

 

(ii) Wachungaji wanapaswa kuchaguliwa kwa kuongozwa na wakristo ambao wamekomaa.  Katika mstari huu tunaona kwamba Paulo na Barnaba walishiriki katika jambo hili la kuwachagua wachungaji wa kanisa.  Ni rahisi kufikiria jinsi walifanya jambo hili.  Paulo na Barnaba walikutana na washirika wa kila kanisa na wakaongea na wanaume kuhusu jambo hili.  Halafu waliwatambua wale ambao wanaweza kufanya kazi ya wachungaji, na kuwapendekea kwa kanisa.  Basi washirika wakapiga kura ya kukubali ama kupinga jinsi walivyohisi.  Hii ni njia mzuri ambayo kanisa linafaa kufuata leo.

 

Njia mzuri ya kuchagua mchungaji ni kwamba wale ambao tayari ni wachungaji kwanza inafaa wazungumze na yule anatamani kufanya kazi hii ya uchungaji.  Katika hali hii ya kuongea wazee wa kanisa watachunguza na kuona ikiwa mtu huyu anafaa kweli kuwa mchungaji wa kanisa na kama anatimiza yote yanayohitajika kulingana na Biblia.  Ikiwa wametosheka kwamba anaweza kufanya kazi hii basi wanawaeleza washirika wa kanisa ili wapige kura ya kumkubali au kumkataa.  Ikiwa baada ya wazee wa kanisa kuongea na yule anatamani kufanya kazi ya uchungaji na waone ya kuwa hastahili basi wanafaa kumweleza ni kwa nini wanaona hafai.  Basi mtu huyo hatachaguliwa kuwa mchungaji.

 

2.  Jinsi ya kuwachagua mashemasi.

 

Katika kitabu cha Matendo ya mitume 6:1-6 tunasoma jinsi kanisa la Yerusalemu liliwachagua wanaume kufanya kazi ya kugawia wajane chakula.  Kifungu hiki kinatuonyesha njia mbili ambazo tunapaswa kufuata wakati tunawachagua mashemasi.

 

(i) Mitume waliwahimiza washirika wa kanisa wachague miongoni mwao wanaume wafanye kazi katika afisi hii.  Hii inamaanisha kwamba washirika wa kanisa walihusika katika hali hii ya kuchagua mashemasi.  Walielezwa na mitume jinsi wanapaswa kuchunguza wanaume ili waone kama wanaweza kufanya kazi hii na kwa hivyo washirika wa kanisa ndiyo walifanya jambo hili.  Pia ni jambo zuri sana kwa kanisa kufikiria ni nani anaweza kufanya kazi hii ya ushemasi.

 

(ii) Wale wanaume waliochaguliwa kwanza walikabidhiwa wachungaji (msitari wa 6).  Hii inamaanisha kwamba kanisa halikuchagua tu mashemasi halafu wakaanza kufanya hii kazi bali waliwaleta kwanza kwa wachungaji wa kanisa.  Vivyo hivyo njia mzuri ya kuwachagua mashemasi ni kwa kuwaeleza wachungaji wa kanisa ni nani anayeonekana kuwa anaweza kufanya kazi hiyo vizuri.  Wachungaji basi wanaweza kuchunguza wale ambao wametajwa.  Ikiwa wametosheka kwamba wale ambao wametajwa kuwa wanaweza kufanya kazi hii, basi wanaita mkutano wa kanisa na wanawachagua.  Kwa njia hii wote, yaani wachungaji na washirika wa kanisa wanashiriki katika jambo hili.

 

 

 

 

Funzo La Nne, 1 Wathesalonike 1:4-10, Mfano wa Kanisa.

 

Paulo, Silvano na Timotheo walitembelea mji wa Thesalonike wakati wa safari ya pili ya mtume Paulo (Matendo ya Mitume 17:1-9) na wakiwa katika mji huu wakapanda kanisa.  Baadaye waliliandikia barua kanisa hili wakiwahimiza wavumilie, hata ikiwa washirika wa kanisa hili walikuwa katika shida mingi sana kwa sababu ya kuwa wakristo (1 Wathesalonike 1:6).  Paulo anasema kwamba kanisa hili ndilo lilikuwa mfano wa makanisa yote.  Alisema, “Hivyo ninyi mkawa kielelezo kwa waamini wote katika Makedonia na Akaya” (1 Wathesalonike 1:7).  Kanisa hili ni mfano mzuri, siyo tu kwa watu wa Thesalonike bali hata kwetu leo.  Ikiwa tunataka kujua ni kanisa la aina gani ambalo Kristo anapendezwa nalo basi tutazame kanisa la Thesalonike.  Katika mistari wa 4-10 Paulo anasema mambo tisa ambayo yalifanya kanisa hili kuwa mfano mzuri.  Tunahitaji kujifunza mambo haya kwa uangalifu sana.

 

1.  Mungu aliwapenda.

 

Jambo la kwanza ambalo Paulo anaongea kuhusu kanisa hili ni kwamba Mungu alilipenda.  Anasema katika msitari wa 4, “Ndugu zetu mpendwao na Mungu.”  Hili ni jambo ambalo tunapaswa kukumbuka kwa uangalifu.  Sababu kuu ya watu hawa kuwa kanisa ni kwamba Mungu aliwachagua kabla hajaumba ulimwengu.  Washirika wa kanisa si ati wanajaribu kufanya jambo fulani ili waufikie upendo wa Mungu kwa kazi zao mzuri, bali ukweli ni kwamba wanafanya kazi mzuri kwa sababu Mungu anawapenda.  Ni upendo wa Mungu ambao unawafanya kuishi maisha matakatifu na kumtumikia Mungu.  Mtume Paulo anasema hivi kuhusu jambo hili, “Kwa sababu upendo wa Kristo unatutia nguvu” (2 Wakorintho 5:14).

 

Washirika wa kanisa hupitia majaribu mengi sana na mara mingi hujaribiwa kukata tamaa.  Lakini tunahitaji kukumbuka kwamba hata kama tu wadhaifu na tungali tuko na dhambi ndani mwetu, Bwana Yesu Kristo anatupenda sana.  Ni kwa sababu ya upendo huu alikuja hapa ulimwenguni na akafa kwa ajili yetu: “Mungu ana hudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu” (Warumi 5:8).  Upendo wa Yesu Kristo uko juu yetu kila wakati, hata wakati tunapitia katika majaribu makali, Mungu hatawahi kutuacha.

 

Mchungaji wa kanisa pia anapaswa kukumbuka kwamba Mungu anawapenda washirika wa kanisa.  Ni jambo la kuhuzunisha kwamba mara mingi humu nchini mwetu tunasikia na kuona wachungaji wakitumia washirika wao vibaya.  Mara mingi mchungaji anawalazimisha washirika wake kutoa pesa na mara mingi pia anawatisha kwamba hatawaunganisha katika ndoa ama kuwazika wakifa ikiwa hawatafanya mambo fulani.  Inafaa mchungaji kama huyo kujua kwamba anatatiza watu ambao Mungu anawapenda sana, watu ambao Kristo aliwafia msalabani.  Ikiwa mchungaji anawatatiza watu wa Mungu na kuwatumia vibaya basi ni lazima Mungu atamhukumu mchungaji huyo.

 

 

 

2.  Mungu aliwachagua wapate wokovu.

 

Paulo anaandika, “Kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua, kwa maana ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu, katika Roho Mtakatifu, tena akiwa na uthibitisho kamili” (1 Wathesalonike 1:4).  Kile Paulo anasema hapa ni kwamba washirika wa kanisa la Thesalonike walichaguliwa na Mungu ili wapate wokovu: “Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe” (2 Wathesalonike 2:13).  Biblia inatufundisha wazi kwamba Mungu alichagua kutoka mwanzo kabla hajaumba ulimwengu wote wale ambao atawaokoa (Waefeso 1:4).  Paulo anasema hapa kwamba washirika wa kanisa la Thesalonike walikubali neno la Mungu kwa sababu walikuwa wamechaguliwa ili waokoke.  Wale wote ambao walichaguliwa kupata wokovu watayakubali mahubiri ya Biblia na wataokoka.  Hili ni jambo la kuwahimiza wahubiri wote sana.  Ni lazima kila wakati tuwe waangalifu sana kuhubiri na kufundisha Biblia.  Si wajibu wetu kuhakikisha kwamba mtu ameokoka.  Wokovu ni kazi ya Mungu na Mungu mwenyewe atahakikisha kwamba wote wale ambao aliwachagua kupata wokovu wameokoka.

 

3.  Ni wafuasi wa Bwana.

 

Paulo anasema, “Ninyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana.”  Kuwa mfuasi inamaanisha kufanya jinsi mtu mwingine anavyofanya na kuishi kama yeye na pia kuwa na tabia kama yake.  Barua hii iliandikwa na mtume Paulo, Silvano na Timotheo na ni hawa watatu ambao wakristo wa Thesalonike walikuwa wafuasi wao, lakini hawakufuata mifano ya watu wengine bali walikuwa wafuasi wa Mungu.  Ni vizuri kwetu kufuata tabia ya wakristo wenzetu ikiwa wanamfuata Bwana Yesu Kristo.  Kuna mambo mawili ambayo tunajifundisha hapa.

 

(i) Wakristo wachanga kila wakati watafuata tabia ya wakristo walio komaa.  Hivi ndivyo Mungu amepanga mambo katika ufalme wake.  Wale ambao ni wachanga katika imani yao kila wakati watawaangalia wale ambao wamekuwa wakristo kwa muda mrefu na kufuata mienendo yao katika mambo kama, jinsi wanavyoomba, jinsi ya kusoma na kujifunza Biblia, jinsi ya kuishi maisha ya ukristo hapa duniani na mambo mengine mengi.  Hili ni jambo la kweli hasa hasa kwa wachungaji. Wachungaji wanapaswa kuweka mfano mzuri ili wakristo waweze kuufuata, hii ndiyo sababu Petro anasema kwamba wachungaji wanapaswa kulinda kundi la Mungu kwa mfano mzuri (1 Petro 5:3).  Hii inamaanisha kwamba wale ambao waliokolewa miaka mingi iliyopita wanafaa kuwa waangalifu sana jinsi wanavyoishi maisha yao.  Wanapaswa kujua kwamba wakristo wachanga wanatazama maisha yao na kwamba wanapaswa kuwa mfano mzuri wa kufuatwa.

 

(ii) Wakristo wote wanafaa kuwa wafuasi wa Mungu.  Bwana Yesu alisema, “Wapendeni adui zenu waombeeni wanaowatesa ninyi, ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:44-45).  Ni kweli kwamba Mungu si kama sisi wanadamu na kwamba kwa njia mingi sana hatuwezi kuwa kama Mungu.  Lakini ni lazima tujue kwamba Mungu ni mwenye huruma, ni mwenye rehema na neema na tunapaswa kuwa wafuasi wake.  Ni kweli pia kwamba Mungu anachukia dhambi kwa chuki takatifu na kwamba hatakubali dhambi kamwe.  Pia sisi tunahitaji kuwa wafuasi wa Mungu katika jambo hili.  Ni lazima tuchukie kile Mungu anachukia na ni lazima tupende kile Mungu anapenda.  Tunapaswa kuwa kama Mungu na kuepuka tabia yoyote ambayo itatufanya tusimpendeze.

 

4.  Walivumilia mateso.

 

Paulo anaandika, “Ingawa mlipata mateso mengi, mlilipokea lile Neno kwa furaha katika Roho Mtakatifu” (Msitari wa 6).  Tunajua kutoka kwa kifungu hiki kwamba kuna siku ambazo watu hawa wa Thesalonike walikuwa wakiabudu sanamu, na inaonekana kwamba walipookoka, wenzao katika mji huo walianza kuwatesa.  Hili ni jambo ambalo hufanyika mara kwa mara.  Ikiwa mtu alizaliwa katika jamii ambayo inafuata dini fulani halafu aokoke, wale watu ambao wanafuata ile dini aliotoka wanamgeuka na kuanza kumletea mateso.  Hivi ndivyo ilifanyika katika mji huu wa Thesalonike.  Wakristo huko waliteswa na watu wa jamii zao ama marafiki wao.  Fikiria kuhusu mwanamke ambaye jamii yake yote wanaabudu sanamu halafu awe yeye pekee ndiye ameokoka katika jamii yake, bwana yake na wazazi wake bado hawajaokoka.  Kwa watu hawa itakuwa ni aibu kubwa kwa mwanamke huyu kwenda kanisani badala ya kwenda kuabudu sanamu hekaluni mwao na hata bwana yake anaweza kumpiga.

 

Wakristo huko Thesalonike walipata mateso lakini hawakuacha imani yao katika Bwana.  Badala yake wakristo hawa walivumilia.  Hii ni dhihirisho kwamba imani yao ilikuwa ya kweli na kwamba walikuwa kweli wameokoka.  Mtume Petro alisema kwamba wakati mwingine tunapata mateso ili imani yetu ionekane kuwa ni ya kweli (1 Petro 1:7).  Bwana Yesu alizungumza kuhusu watu ambao waliipokea neno kwa furaha sana lakini wakati mateso yalikuja kwa sababu ya hilo neno wakakata tamaa (Mathayo 13:20-21).  Watu wale wanakata tamaa siyo wakristo wa kweli, na imani yao siyo ya kweli.  Mtu ambaye anavumilia ndiye mkristo wa kweli.  Bwana Yesu Kristo alisema kwamba, “Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ndiye atakayeokoka” (Mathayo 24:13).

 

5.  Walikuwa kielelezo kwa kanisa lote.

 

Paulo anaandika, “Hivi ninyi mkawa kielelezo kwa waamini wote katika Makedonia na Akaya” (mstari wa 7).  Wakati barua hii iliandikwa, injili ilikuwa imefika bara la Uropa mara ya kwanza na kulikuwa na wakristo wachanga.  Walihitaji kufuata mwongozo mzuri wa maisha ya ukristo katika maisha yao.  Wathesalonike wenyewe walikuwa wachanga lakini walikuwa kielelezo kwa wengine kufuata.  Wakristo waliokuwa sehemu za Makedonia na Akaya walihitaji kielelezo wafuate, kwa hivyo hawa wakristo wa Thesalonike ndio walikuwa hicho kielelezo.  Hili ni jambo ambalo linafurahisha Mungu sana kwamba wakristo wachanga wanakuwa wafuasi wa Bwana Yesu na kielelezo kwa wakristo wote.  Si jambo la furaha machoni pa Mungu wakati tunabaki kuwa watoto wachanga kwa muda mrefu bila kukua.  Mungu ndiye Baba wetu, na kila baba anapenda kuona watoto wake wakikua na wakikomaa.

 

6.  Walihubiri neno la Mungu.

 

Paulo anaandika, “Kwa maana kutoka kwenu Neno la Mungu limesikika” (Msitari wa 8).  Kanisa la Thesalonike lilitilia maanani sana neno la Mungu.  Walilikubali wakati walihubiriwa (1 Wathesalonike 2:13), walilikubali kwa mioyo yao yote, na walilihubiri kwa wengine.  Watu hawa hawakusema, “Sisi ni kanisa changa na hatujui mambo mengi, hata bado hatujafundishwa vya kutosha, na kwa hivyo hatuwezi kuhubiri.”  Kazi ya kufundisha neno la Mungu ni kazi ambayo kila mkristo inafaa afanye.  Ni kweli kwamba Mungu amewainua wachungaji makanisani ambao kazi yao ni kuwafundisha watu neno la Mungu, lakini hii haimaanishi wakristo wengine hawafai kufundisha.

 

Biblia inasema wazi kwamba Mungu amewapa vipawa watoto wake ili wavitumie katika huduma wa kanisa na ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba tunatumia vipawa vyetu kwa kazi ya Mungu kanisani (Mathayo 25:14-30, 1 Wakorintho 12:7, Waefeso 4:7-13).  Si vizuri kuona watu wachache tu wakifanya kazi kanisani na wale wengine hawafanyi chochote.  Hii sivyo kanisa inapaswa kuwa, kwa sababu kila mshirika wa kanisa anapaswa kutafuta ni kipawa gani Mungu amempatia ili akitumie katika kazi ya kanisa.  Ikiwa mtu ni mshirika wa kanisa na hafanyi chochote kanisani mwake basi inaonyesha kuna kasoro fulani naye.  Wakristo wa Thesalonike walitumia vipawa vyao kuhakikisha kwamba neno la Mungu limejulikana.

 

Ni lazima tufundishe neno la Mungu kwa uangalifu na kwa ukweli wote.  Kuna watu wengi humu nchini mwetu ambao wanafikiria kwamba wao wako na kipawa cha kufundisha neno la Mungu lakini hawajui Biblia, kwa hivyo wakati wanapofundisha huwa wanafunza kwa njia isiyo ya kweli.  Hili ni jambo hatari sana.  Kila mmoja wetu anafaa asome Biblia kwa uangalifu ili aelewe ndipo aweze kuwafundisha wengine.  Pia ni wajibu wetu kuwafundisha Biblia wale ambao hawajaokoka na kuwasihi watubu dhambi zao na kumwamini Bwana Yesu Kristo.

 

7.  Walimgeukia Mungu na kuacha sanamu.

 

Paulo anasema, “Mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu” (1 Wathesalonike 1:9).  Ni wazi hapa kwamba kabla injili haijaingia katika mji wa Thesalonike, watu wa mji huo walikuwa wanaabudu sanamu.  Paulo anaposema, “Mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu,” anamaanisha mambo mawili:

 

(i) Waliacha maisha yao ya zamani na wakaanza kuishi maisha mapya.  Kabla ya kuokoka walikuwa wanaenda hekaluni, mahali sanamu wanaabudiwa, na kuungana na kundi la kuabudu sanamu.  Lakini baada ya kuokoka, waliacha kwenda katika hekalu hizo za kuabudu sanamu bali walishiriki na wakristo wenzao katika kanisa.  Jinsi walivyoishi maisha yao baada ya kuokoka ilikuwa tofauti kabisa, kwa sababu wao walikuwa watu wapya na walikuwa wamezaliwa mara ya pili.

 

Mungu anatarajia hivi kutoka kwa kila mtu ambaye ameokoka.  Mtu ambaye ameokoka ni mtu amezaliwa mara ya pili, kumaanisha kwamba yeye ni kiumbe kipya: “Amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya” (2 Wakorintho 5:17).  Mungu anamwamuru mtu ambaye amezaliwa mara ya pili kuacha maisha yake ya kale ya dhambi na kuanza maisha mapya, maisha ambayo yanayoambatana na mapenzi ya Mungu na ambayo yanampendeza, “Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu.  Mfanywe upya roho ya nia yenu, mkajivike utu upya, ulioumbwa sawa sawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu” (Waefeso 4:22-24).  Haya ndiyo maagizo ya Mungu kwetu, kwamba tuuvue ule utu wa kale ambao ni mchafu na tuuvae utu upya ambao ni wa haki na utakatifu.  Hii inamaanisha kwamba ni lazima tuache kabisa mafikira yote tuliyokuwa nayo kuhusu Mungu na mwanadanu, kuhusu dhambi na wakovu tuliyokuwa nayo kabla hatujaokoka na tuanze kufundishwa upya kutoka kwa Biblia.  Shida moja kubwa nchini mwetu leo ni kwamba watu hawataki kuacha imani potofu waliyokuwa nayo mababu zao zamani.  Watu wengi wako na imani tofauti kuhusu Mungu na mwanadamu, dhambi na wokovu ambazo hazitoki katika Biblia bali zinatoka katika mila zao.  Wanapokutana na jambo katika Biblia ambalo ni kinyume na mila zao, wanapuuza Biblia na wanaendelea kushikilia mila zao.

 

Tunahitaji kusoma Biblia na kuelewa na kuamini lililo dani yake.  Hatuwezi kuweka imani yetu kwa watu ama kwa mila kwa sababu hiyo si kumheshimu Mungu.  Neno la Mungu ni lazima litawale katika mioyo yetu.

 

(ii) Waliendelea kumgeukia Mungu kutoka kwa sanamu na kuishi maisha ya ukristo.  Hii ndiyo sababu “walipata mateso mengi” (mstari 6).  Hii inamaanisha walikumbwa na majaribu mengi hata ya kuwashawishi warudi katika kuabudu sanamu.  Hili ni jambo ambalo linafanyika kwa kila mtu ambaye ameokoka.  Watu wa jamii yake watapenda yeye afuate mila wakati wa mambo kama ndoa na mazishi.  Wanahitajika kufuata mila kuhusu mambo ya kuwalea watoto na kuhusu maisha ya jamii zao.  Sababu kuu ya kanisa la Thesalonike kuwa kielelezo ni kwamba walikataa kufanya yale ambayo walitarajiwa kufanya kulingana na mila zao badala yake wakafanya yale Biblia inaamuru. Hii ndiyo sababu walipata mateso sana.

 

Watu wa dunia hii watawatesa wale wanaokataa kushiriki nao katika mambo ya dhambi na wanaoendelea kuwa na msimamo mkali kuhusu dhambi.  Ikiwa mtu ambaye ameokoka amekubali kufanya yale ambayo mila inakubali, hata kama anajua kwamba hiyo ni dhambi, basi ulimwengu hautakuwa na shida yoyote naye.  Dunia haijali mtu kuwa mkristo, mradi tu hana msimamo mkali wa kumfuata Mungu na kukataa dhambi.  Ni wakati tu tunatilia mkazo wa kufuata Biblia katika mambo kama mazishi, ndoa na mambo mengine ya jamii kama ya kulea watoto, tunapata mateso makubwa kutoka kwa wazee wa jamii.  Mara mingi wakristo hawapingi mila, kama wakati wazee wa kijiji wanaeleza watu jinsi wanapaswa kufanya wakati wa arusi ama wakati wa mazishi.  Wakristo wengi hufuata mila hizi hata kama wanajua kwamba jambo hilo ni dhambi.  Lakini kanisa la Thesalonike hawakufanya hivyo.  Wakati mambo ya mila yalitokea na wakaona kwamba ni kinyume na Biblia, walikataa kuyafuata hata kama ilimaanisha kupata mateso.

 

Hivi ndivyo Mungu anatarajia kutoka kwetu.  Mungu anatarajia kwamba tutoke katika imani zote ambazo haziko kwa Biblia, na pia anatarajia tugeuke kutoka kwa mila zote ambazo haziambatani na Biblia.

 

8.  Walimtumikia Mungu wa kweli aliye hai.

 

Paulo anaendelea kusema, “Ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli.”  Washirika wa kanisa hili walitumia vipawa vyao kwa kazi ya kumtumikia na kumtukuza Mungu.  Biblia inatufundisha mambo matatu muhimu sana hapa kuhusu vipawa.

 

(i) Kwanza Biblia inatueleza kwamba Mungu amewapatia vipawa kila mmoja wa watoto wake (Waefeso 4:7-11).  Si kweli kwamba kuna watu wa Mungu ambao wako na vipawa na pia kuna wengine ambao hawana.  Watu wa Mungu wote wako na vipawa kutoka kwa Mungu.

 

(ii) Pili, Biblia inafundisha kwamba kila mkristo anapaswa kutumia kipawa chake.  Ni dhambi kubwa sana ikiwa hutumii kipawa chako (Mathayo 25:14-30).  Ni kazi ya mchungaji kuwahimiza washirika kutumia vipawa vyao na ni jukumu la kila mshirika kuhakikisha kwamba anatumia kipawa Mungu alichompatia na anakitumia kwa utukufu wa Mungu.

 

(iii) Tatu, Biblia inatueleza kwamba vipawa ambavyo tuko navyo ni vya kutumika kwa faida ya kanisa lote (1 Wakorintho12:7).  Sababu kuu kwa nini Mungu anampa kipawa mtu si ili mtu huyo aanze kujisifu ama kuonyesha wengine jinsi alivyo wa kiroho sana, bali ni kwa sababu ya kuwafanyia wengine mema kwa kutumia kipawa hicho.

 

9.  Walingoja kwa bidii sana kurudi kwa Bwana Yesu Kristo.

 

Paulo anaendelea kusema hivi kuhusu kanisa hili, “Na ili kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, yaani Yesu, Yeye aliyetuokoa kutoka katika ghadhabu inayokuja.”  Kanisa la Thesalonike halikuwa linajali mambo ya ulimwengu huu.  Hili ni jambo ambalo tunapata hapa nchini mwetu siku hizi.  Watu ambao wanadai kuwa wameokoka wanaonekana kutokuwa na shughuli yoyote kuhusu mambo ya mbinguni.  Kwao kile wanashughulika nacho sana ni mambo ya hapa duniani.  Wanafurahia sana maisha ya hapa duniani na pia wanafuata anasa za dunia hii kila wakati.  Hawasomi Biblia na hawaongozwi na Biblia katika maisha yao.  Lakini kanisa hili la Thesalonike hawakuwa hivyo.  Walijua kwamba duniani siyo nyumbani kwao na kwamba walitarajia mji wenye misingi ya kudumu ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu (Waebrania 11:10).  Walijua kwamba ulimwengu huu unapita na haifai kamwe kufuata mali na anasa za ulimwengu.  Kwa hivyo walitazamia kurudi kwa Bwana Yesu Kristo.  Matarajio yao kuhusu kurudi kwa Bwana Yesu Kristo yaliwawezesha kuishi maisha matakatifu.  Biblia inasema, “Kila mmoja mwenye matumaini haya katika Yeye hujitakasa, kama vile Yeye alivyo mtakatifu” (1 Yohana 3:3).  Tumaini la mbinguni ni tumaini la kweli na tumaini hili linatuongaza jinsi tunavyoishi maisha yetu hapa duniani.