Header

Maombi ya Solomoni

Mafundisho haya yametoka kwa 1 Wafalme 3:3-15. Tafadhali hakikisha kwamba umesome kifungu hiki kabla ya kusoma mafundisho haya.

Utangulizi

Tunaposoma kifungu hiki, tunaona mambo mawili wazi kumhusu Solomoni. Kwanza, ni wazi kwamba maombi yake yamejengwa juu ya uhusiano wa upendo. Biblia inatuambia kwamba Bwana alimpenda Solomoni (2 Samweli 12:24), na kwamba Solomoni naye alimpenda Bwana (1 Wafalme 3:3). Uhusiano huu wa upendo ulikuwa msingi wa maisha ya Solomoni ya maombi. Pili, ni wazi kwamba Solomoni alikuwa mtu wa maombi. Tunasoma katika kifungu hiki kwamba wakati Mungu alijitambulisha kwa Solomoni, Solomoni alijua Yeye ni nani. Solomoni hakuwa kama Yakobo ambaye alikutana na Mungu bila kujua Yeye ni nani (Mwanzo 28:16), na yeye hakuwa kama Samweli wakati Samweli alisikia sauti ya Mungu bila kujua ni sauti ya nani (1 Samweli sura 3). Solomoni alijua kwamba ni Mungu ambaye alijitambulisha kwake kwa sababu yeye alikuwa na tabia ya maombi.

Kuna mambo matatu ambayo tunapaswa kujifunza kuhusu maombi ya Solomoni.

1. Solomoni aliomba kama vile Daudi alivyoomba

Katika toleo la pili la jarida hili, tunajifunza maombi ya Daudi katika 2 Samweli 17:18-29, na katika maombi haya tuliona mambo matatu. Haya mambo matatu pia yanapatikana katika maombi haya ya Solomoni.

(i) Solomoni alimtukuza Mungu katika maombi yake. Tunasoma kwamba Mungu alimwambia Solomoni, “Omba lo lote utakalo nikupe” (1 Wafalme 3:5). Tungewaza kwamba Solomoni angeomba mambo mengi ya dunia. Lakini yeye hakufanya hivyo. Badala yake, tunasoma katika mstari 6 kwamba yeye alianza maombi yake kwa kumtukuza Mungu na kuongea kuhusu rehema na neema ya Mungu na uaminifu wa Mungu kwa agano lake.

(ii) Solomoni aliomba kwa unyenyekevu. Alisema, “Mimi ni mtoto mdogo tu wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu” (1 Wafalme 3:7). Solomoni hakuwa na majivuno, ingawa yeye alikuwa mfalme wa nchi kuu, yeye alikuwa mnyenyekevu.

(iii) Solomoni aliomba kulingana na mapenzi ya Mungu. Yeye alijua kwamba yeye alifanywa mfalme ili awaongoze watu wa Mungu (mstari 8), na kwa hivyo aliomba, “Mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya” (mstari 9). Yeye hakumwomba Mungu vitu vya dunia, bali alimwomba Mungu hekima kuwaongoza watu wa Mungu kwa sababu hili lilikuwa lengo la Mungu wakati alimfanya Solomoni mfalme.

2. Mungu anapenda kujibu maombi ambayo ni ya heshima.

Tunasoma kwamba Mungu alimjibu Solomoni, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba ufahamu katika kutoa haki, nitafanya lile ulioomba” (1 Wafalme 3:11-12). Mungu alipendezwa na maombi ya Solomoni kwa sababu yeye aliomba kulingana na mapenzi ya Mungu. Mungu alitaka Solomoni awe mtu wa hekima ili aweze kuwaongoza watu Wake na hili ndilo jambo Solomoni aliomba. Kwa sababu Mungu alipendezwa na maombi ya Solomoni, alimpatia zaidi ya yale ambayo yeye aliomba. Mungu alimwambia, “Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba, yaani utajiri na heshima, ili kwamba maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme” (1 Wafalme 3:13).

3. Tunapaswa kulinda majibu ya maombi yetu.

Mungu alimwambia Solomoni, “Nawe kama ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu kama baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu” (1 Wafalme 3:14). Mungu alimwonyesha Solomoni neema Yake na akampa Solomoni hekima na alimwongoza katika kazi yake ya ufalme. Pia Mungu alimwahidi Solomoni vitu vingi vya dunia na maisha marefu, hata ingawa Solomoni hakumwomba Mungu mambo haya. Lakini Solomoni aliamrishwa kwamba anapaswa kumtii Mungu na kuzitii sheria zake zote kama vile Daudi babake alivyozitii.

Haya ni mafundisho makuu kwetu. Kila kitu ambacho tunapata, tunapata kutoka kwa neema na rehema ya Mungu, lakini Mungu anatarajia tulinde vizuri yale ambayo Yeye anatupatia. Zaidi ya haya, Mungu anatarajia kwamba tutatembea naye maishani mwetu mwote ili tuweze kutumia vipawa vyetu vizuri. Solomoni alipewa kipawa cha hekima ili awaongoze watu wa Mungu, na Solomoni angeweza kufanya kazi hii kama yeye mwenyewe anatembea na Mungu na kuzitii sheria zake. Solomoni angeanguka dhambini na kuondoka kwa Mungu basi yeye hangeweza kutumia vipawa vyake na kuwaongoza watu wa Mungu.

Mungu anajibu maombi yetu kutoka kwa neema Yake, lakini Yeye anatarajia kwamba tutatumia vipawa vyetu kwa njia ya hekima na kwa uaminifu katika Ufalme Wake.

**********

Jinsi mkristo anafaa kukabiliana na majaribu kulingana na Biblia.

Maisha ya ukristo ni maisha ambayo yamejawa na shida nyingi na matatizo. Mungu hajawahi kusema kwamba hatutawahi kuwa na maisha bila shida au matatizo hapa ulimwenguni. Kwa hivyo wale wote ambao wameokoka wanafaa kujifunza jinsi ya kukabiliana na shida hizi na matatizo kulingana na Biblia. Kuna mambo matatu ambayo yatatusaidia kukabiliana na shida hizi na matatizo haya.

1. Kumbuka kwamba majaribu yako yameruhusiwa na Mungu mwenyewe katika maisha yako.

Katika kitabu cha Ruthu, wakati Naomi alipowapoteza mume wake na watoto wake wawili alisema, “Bwana amenitendea mambo machungu, Mwenyezi Mungu ameniletea msiba” (Ruthu 1:21). Hakuna majaribu ambayo yatakuja kwetu ikiwa Mungu hatayaruhusu. Wakati Ayubu alipoteza jamii yake yote pamoja na mali yake yote hakusema, “Bwana alinipa na shetani amenyakua.” Badala yake alisema, “Bwana alinipa naye Bwana ameviondoa, jina la Bwana litukuzwe” (Ayubu 1:21). Haijalishi majaribu yanakuja kwa njia gani kwetu, Mungu ndiye huwa anayaruhusu katika maisha ya watu wake.

2. Kumbuka kwamba majaribu yako yameruhusiwa na Mungu katika maisha yako kwa ajili ya faidi yako.

Daudi aliandika hivi, “Ilikuwa vyema mimi kupata shida ili nipate kujifunza amri zako” (Zaburi 119:71). Hivi ndivyo watu wa Mungu wote wanafaa kuwaza juu ya majaribu ambayo yanakuja katika maisha yao. Wanafaa kukumbuka kwamba majaribu yao yameruhusiwa na Mungu katika maisha yao kwa sababu Mungu anataka kuwafaidi wao wenyewe. Biblia imejawa na mifano mingi ambayo inaonyesha jinsi watu wa Mungu wamefaidika kutokana na majaribu ambayo Mungu ameruhusu katika maisha yao.

Mandugu wa Yosefu walimtupa katika shimo na baadaye walimwuza katika utumwa. Lakini haya yote Mungu aliyakusudia kwa uzuri. Yosefu alifanyika mtu mkuu sana kando na Farao katika nchi ya Misri na Mungu alimtumia kuwaokoa watu wake kutoka kwa njaa. Hii ndiyo sababu wakati Yosefu alikuwa amefika mwisho wa maisha yake aliwaambia ndugu zake kwamba, “Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema ili litimie hili linalofanyika sasa kuokoa maisha ya watu wengi” (Mwanzo 50:20). Mfalme Manase alishikwa na akapelekwa katika nchi ya Babeli na maadui wake. Lakini haya yote yalikusudiwa na Mungu kwa uzuri wa Manase. Huko Babeli alijinyenyekeza na akautafuta uso wa Bwana na aliokolewa. Baadaye alirudi Yerusalemu na akaanza kumwabudu Mungu badala ya miungu. Paulo alipofushwa alipokuwa njiani akielekea Damesiki, lakini Mungu alitumia upofu huu kumwonyesha nuru ya neema yake katika wokovu.

3. Kumbuka kwamba majaribu yako yatakufundisha mafundisho ya maana ya kiroho.

Nabii Mika aliwaambia watu wa Israeli kwamba, “tii hiyo fimbo na Yeye aliyeiamuru” (Mika 6:9). Kwa kusema hivi alimaanisha kwamba majaribu ambayo watu wa Isreali walikutana nayo yalikusudiwa kuwafundisha mambo ya maana sana ya kiroho.

Kwanza, majaribu yetu yanatufundisha dhambi ni nini. Tunaweza kusikia mafundisho kwamba dhambi ni mbaya sana lakini wakati tunapoona matunda mabaya ya dhambi katika maisha yetu ndipo tunafahamu vyema uovu na ubaya wa dhambi. Mtu anaweza kusoma kitabu fulani kuhusu ugonjwa fulani lakini hawezi kufahamu kabisa ugonjwa huo hadi yeye mwenyewe apate ugonjwa huo. Kwa njia hiyo hiyo hatuwezi kufahamu kabisa uovu wa dhambi hadi tunapoona matunda mabaya ya dhambi katika maisha yetu.

Pili, majaribu yetu yanatufundisha kuhusu sisi wenyewe. Huwa hatufahamu kabisa mioyo yetu wakati mambo ni mazuri kwetu. Ni wakati tunapitia katika majaribu ndipo tunafahamu kabisa kile ambacho kiko katika mioyo yetu. Ni wakati wa majaribu ndipo tunaona kile ambacho kimejificha katika mioyo yetu. Ni wakati wa majaribu ndipo tunaona kiburi na uchoyo na upendo wa ulimwengu ambao umejificha ndani mwetu.

Faida ambazo majaribu yetu hutuletea

Kama tu jinsi tumeona katika mafundisho haya, majaribu yetu huwa yanaruhusiwa na Mungu kwa ajili ya faida yetu ya milele. Je, majaribu haya yanatuletea faida gani?

Kwanza, majaribu ndiyo njia ya kutakasa mioyo yetu. Wakati mambo ni mazuri kwetu, mioyo yetu inaweza kuanza kupenda vitu vya ulimwengu na kutafuta vitu hivi. Lakini wakati tunakumbana na majaribu, huwa tunamkimbilia Mungu kwa haraka sana na kumlilia Yeye pekee.

Pili, majaribu ndiyo njia ambayo Mungu anatumia kuondoa dhambi katika maisha yetu. Majaribu ni kama dawa ambayo ni bora sana. Huwa watu hawataki kumeza dawa kwa sababu dawa huwa inaonja vibaya lakini hata kama ni hivyo, dawa huwa ndiyo ya kuponya. Majaribu yanaweza kuonekana kuwa makali sana lakini hii ndiyo njia Mungu anatumia kutuleta Kwake.

Tatu, majaribu ndiyo njia ambayo Mungu hutumia kutugeuza hadi tuwe kama Kristo mwenyewe. Bwana Yesu Kristo alikuwa “mtu wa huzuni nyingi ajuaye mateso” (Isaya 53:3). Ni kwa njia hii Bwana Yesu Kristo aliweza kumtumikia Mungu na akatimiza mapenzi ya Mungu Baba. Majaribu hayo ndiyo yalikuwa njia ya kupata wokovu. Majaribu yetu hayawezi kutuletea wokovu lakini yanaweza kutuleta karibu sana na Kristo na kutufanya tuwe kama Yeye mwenyewe na tumtumikie kwa upendo.

Nne, majaribu ndiyo njia ambayo upendo wa ulimwengu na vitu vyake unaondolewa katika mioyo yetu. Mungu anapoondoa starehe zetu za ulimwengu, huwa tunafanywa tuwaze kuhusu mbinguni nyumbani mwetu mwa milele. Tunapokuwa wagonjwa, tunakumbushwa kwamba hatutakuwa hapa ulimwenguni milele na kwamba tunafaa kuandaa mioyo yetu kwa ajili ya mbinguni ambamo ndimo nyumbani mwetu.

Tano, majaribu yetu yanatuletea furaha kwa sababu yanatuleta karibu sana na Mungu. Biblia inasema kwamba, “Heri mtu yule ambaye Mungu humrudi, kwa hiyo usidharau marudi yake Mungu Mwenye nguvu” (Ayubu 5:17). Majaribu yetu hudhihirisha kwamba sisi ni watoto wa Mungu kwa sababu Mungu huwa anawaadhibu tu watoto Wake. Hii ndiyo njia ambayo Mungu anatumia kutufundisha njia Zake na wakati tunapofuata njia zake, huwa tunapata furaha kamili.

Bidii ya kufanya kazi ya Mungu

Hakikisha kwamba umesoma Hagai 1:12-15 kabla ya kukisoma kifungu hiki.

Watu wa Yuda walikuwa uamishoni Babeli kwa muda wa miaka 70 kwa sababu ya dhambi zao dhidi ya Mungu. Baada ya miaka 70 kumalizika wao walirudi Yerusalemu. Hekalu ambalo Solomoni alijenga lilikuwa limeangamizwa kabisa na watu wa Babeli wakati waliwavaamia watu wa Yuda. Kwa hivyo baada ya kurudi Yerusalemu wao walianza kazi ya kujenga hekalu hili. Punde tu baada ya kuanza kujenga hekalu hili, maadui wa Mungu waliinuka dhidi yao na kusababisha kazi ya kujenga hekalu hili kusimama kwa miaka 16. Katika huu muda wa miaka 16 watu walijijengea manyumba yao mazuri sana na wakapuuza kazi ya Kujenga hekalu la Mungu (Hagai 1:1-11). Kwa hivyo Mungu alimwita nabii Hagai kuwakumbusha watu hawa na kuwahimiza kuanza kazi ya kuijenga hekalu ambalo lilikuwa nusu kumalizika. Katika kifungu hiki tunasoma jinsi kazi ya kujenga hekalu ilianza tena, baada ya Hagai kuwahubiria watu wa Yuda.

1. Jinsi Mungu aliwawezesha watu wake kujitolea kwa kazi ya kujenga hekalu.

Hii kazi ya kujenga hekalu hili la Agano la Kale ni kama kazi ya kuujenga ufalme wa Mungu humu duniani leo. Hii ni kazi ambayo watu wa Mungu wanapaswa kufanya kwa mioyo yao yote. Katika kifungu hiki tunasoma mambo mawili ambayo Mungu alifanya ili kuwawezesha watu wake kuanza kufanya kazi ya kujenga hekalu tena.

(i) Mungu alizungumza na watu wake. Kitabu cha Hagai kina mahubiri manne ambayo Hagai aliwahubiria watu wa Yuda akiwahimiza waanze kazi ya ufalme wa Mungu. Hagai alikuwa "Mjumbe wa Bwana" (mstari 13), na kwa hivyo maneno aliyoyasema yalikuwa maneno ya Bwana. Hii ndiyo sababu kifungu hiki kinasema, "Watu wakatii sauti ya Bwana Mungu wao pamoja na ujumbe wa nabii Hagai" (mstari 12). Ujumbe wa Hagai ulikuwa ujumbe wa Mungu, Mungu ndiye alikuwa akiongea na watu wake.

Wakati watumishi wa Mungu wanahubiri neno la Mungu kwa uaminifu na kwa njia inayostahili watu wa Mungu watahimizwa na kwa hivyo wao wataanza kufanya kazi ya Bwana kwa mioyo yao yote. Mahubiri ya neno la Mungu ndiyo njia Mungu anatumia kuwafundisha watu wake, kuwahimiza na kuwaamsha ili wafanya kazi yake wakati wanazembea kiroho. Wakati tunaposoma ama kusikia kazi kuu ya Mungu ikiendelea, huwa inaendelea kwa sababu neno lake limehubiriwa. Neno la Mungu ndicho chombo ambacho Mungu anatumia kufanya kazi yake hapa ulimwenguni.

(ii) Mungu aliichochea mioyo ya watu wake. Tunaambiwa katika mstari wa 14, "Kwa hivyo Bwana akachochea roho za Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na roho ya kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadiki, pamoja na roho ya mabaki yote ya watu." Hivi ndivyo inafanyika wakati neno la Mungu linahubiriwa: watu wa Mungu huchochewa roho zao ili wafanye kazi ya ufalme. Watu wa Mungu hapa walikuwa wamepoteza maono yao kuhusu ufalme wa Mungu lakini kupitia mahubiri ya neno la Mungu, Mungu aliwaamsha kutoka kwa hiyo hali na akawahimiza kufanya kazi yake tena.

Kazi ya kuujenga ufalme wa Mungu ni kazi ya Mungu mwenyewe, ni Mungu mwenyewe ambaye anaanzisha kazi hii na ni Mungu mwenyewe ambaye anawapatia watu wake vyombo vya kazi yake, anawahimiza na anawawezesha kufanya kazi yake. Bila kazi ya Mungu mioyoni mwetu kupitia kwa neno lake hatutakuwa na himizo ya kufanya kazi ya ufalme wake.

2. Ni nini watu walifanya baada ya kusikia neno la Mungu.

Hagai alipowaendea watu wa Mungu na neno la Mungu, watu wa Mungu walifanya mambo matatu.

(i) "Watu wakaitii sauti ya Bwana Mungu wao" (mstari 12). Kitu cha kwanza ambacho mtu anafanya anapolisikia neno la Mungu, ni kuitii. Hakuna faida yoyote kwa mtu kulisikia neno la Mungu kila wakati ama kila wiki ikiwa mtu huyo halitii neno hilo ambalo analisikia. Kulisikia tu neno la Mungu hakumletei mtu faida yoyote. Kutii amri za Mungu ndilo dhihirisho la wazi kwamba mtu ameokoka.

(ii) "Watu walimwogopa Bwana " (12). Neno "Ogopa" hapa linamaanisha kwamba watu hawa walimheshimu Mungu kwa kutii neno lake. Haya ndiyo matokeo mazuri zaidi ya neno la Mungu. Tunapaswa kumheshimu Mungu zaidi ya kila kitu na tunapaswa pia kumwabudu na kumtii. Kumwogopa Mungu kunamaanisha kujitoa kufanya kazi yake kwa mioyo yetu yote.

(iii) Watu "Wakaanza kufanya kazi katika nyumba ya Bwana Mwenyezi" (mstari 14). Kwa miaka 16 hakuna kazi yoyote ilikuwa inaendelea katika hekalu. Hekalu hili lilikuwa nusu kumalizika na kazi ya kulijenga ilikuwa imepuuzwa. Lakini wakati watu walianza kutii neno la Mungu, walirudia kazi ya Bwana. Hii ni ishara ya watu wa Mungu: Wao wanatumikia ufalme wa Mungu. Kusikia neno la Mungu hakutoshi, kusema kwamba unaamini neno la Mungu pia haitoshi na pia kusema kwamba unatii neno la Mungu haitoshi. Haitoshi kusema kwamba siku moja tutatumika katika kazi ya ufalme wa Mungu. Haya yote ni maneno tu. Ishara ya kweli ya mtu ambaye ameamini neno la Mungu ni kutumika katika kuujenga ufalme wa Mungu. Hii inamaanisha kwamba mtu anajitolea kwa moyo wake wote kutumia vipawa ambavyo Mungu amempatia kwa kazi ya kuujenga ufalme wa Mungu. Hivi ndivyo watu wa Mungu walifanya wakati wa Hagai.

**********

Mambo sita ambayo tajiri aliona mara ya kwanza

wakati aliingia jahanum

“Yule tajiri naye akafa na akazikwa. Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu’” (Luka 16:22-24).

Katika kifungu hiki Yesu Kristo anatuambia ni nini ilitendekea huyu tajiri wakati alifika jahanum. Wakati huyu tajiri alikuwa ulimwenguni, yeye hakumwomba Mungu msamaha wa dhambi zake na hakutafuta wokovu. Yeye alitosheka bila Mungu, aliishi maisha yake yote bila Mungu na kwa hivyo alikufa bila Mungu na kuenda jahanum na kukaa huko milele bila Mungu.

Sasa katika kifungu hiki, Kristo anatuambia kwamba wakati huyu tajiri aliingia jahanum kuna vitu fulani ambavyo yeye aliona kwa mara ya kwanza. Katika sehemu hii tutaangalia hivi vitu ambavyo huyu tajiri aliona mara ya kwanza wakati aliingia jahanum.

Jambo la kwanza ambalo huyu tajiri aliona kwa mara ya kwanza ni umaskini.

Wakati yeye alikuwa ulimwenguni alivaa mavazi mazuri sana na alikula chakula kizuri sana kila siku. Yeye hakuwa na mahitaji yoyote ya vitu vya dunia. Lakini wakati alifika jahanum, yeye hakuwa na hata tone la maji na alihitaji kuliomba kwa Abrahamu. Kuna wengi ulimwenguni ambao husahau kwamba mtu anaweza kuwa na vitu vingi vya ulimwengu, lakini hawezi kuenda na hata kitu kimoja wakati anakufa. Biblia inasema, “Hatukuja humu duniani na kitu cho chote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu” (1 Timotheo 6:7).

Je, ni kwa nini huyu tajiri hakupata hata maji kule jahanum? Ni kwa sababu kila kitu ambacho tunapata hapa ulimwenguni tunakipata kupitia kwa neema ya Mungu. Yesu Kristo alisema kwamba “Mungu huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki” (Mathayo 5:45). Tunapata jua na mvua hapa duniani kwa sababu Mungu mwenyewe anatupatia vitu hivi kutoka kwa neema Yake. Tunapata jua na mvua na chakula na maji si kwa sababu ni mambo ya kawaida, bali ni kwa sababu ni Mungu mwenyewe ambaye anatupatia vitu hivi kutoka kwa neema yake. Hapa ulimwenguni, hata waovu wanaweza kujua neema ya Mungu. Lakini huko jahanum hakuna neema ya Mungu. Wale ambao wanaenda jahanum wamekataa neema ya Mungu hapa ulimwenguni, na kwa hivyo watakaa bila neema ya Mungu huko milele. Hii ndiyo sababu huyu tajiri hakuwa na maji, ni kwa sababu huko jahanum hakuna neema ya Mungu.

Jambo la pili ambalo huyu tajiri aliona kwa mara ya kwanza ni mateso.

Tunasoma kwamba kule kuzimu yeye aliteseka. Hapa ulimwenguni yeye hakupata mateso hata kidogo kwa sababu yeye alikuwa tajiri. Lakini huko jahanum aliteseka sana hadi alilia. Je, ni kwa nini jahanum ni mahali pa mateso? Je, ni kwa nini watu ambao wanaenda jahanum wanapata mateso mengi? Jibu ni kwamba jahanum imetengenezwa na Mungu kuwa mahali pa hukumu.

Biblia inatufundisha kwamba Mungu ni Mungu Mtakatifu na ni Mungu wa haki. Yule ambaye anaishi maisha yake katika dhambi na anavunja sheria ya Mungu atahukumiwa. Yule ambaye ni mwasi dhidi ya Mungu hataepuka hukumu ya Mungu. Yule tajiri wakati alikuwa hapa ulimwenguni aliwaza kwamba ameepuka hukumu ya Mungu kwa sababu ingawa yeye aliishi maisha yake dhidi ya neno la Mungu, alikuwa na maisha mazuri hapa. Lakini hakuna yeyote ambaye anaweza kuepuka hukumu ya Mungu. Mungu anaona kila kitu ambacho tunafanya na anahukumu kila dhambi.

Kuna njia moja tu ya kuepuka hukumu ya Mungu na hii ni kupitia kwa imani ndani ya Yesu Kristo. Wakati Yesu Kristo alikufa juu ya msalaba, alilipa deni la dhambi za watu wake. Kwa hivyo kuna njia moja tu ya kuepuka hukumu ya Mungu na hii ni kuomba Kristo atuondolee dhambi zetu. Kama deni la dhambi zetu limelipwa na Kristo, basi sisi tunaweza kusamehewa dhambi zetu na kuingia mbinguni.

Jambo la tatu ambalo tajiri aliona kwa mara ya kwanza ni ufalme wa Mungu.

Yesu Kristo alisema, “Mtu hawezi kuuona ufalme wa Mungu asipozaliwa mara ya pili” (Yohana 3:3). Ufalme wa Mungu uko hapa ulimwenguni miongoni mwa watu wa Mungu. Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake, “Ufalme wa Mungu umo ndani yenu” (Luka 17:21). Lakini wale ambao hawajaokoka, hawawezi kuuona ufalme wa Mungu kwa sababu wao wamepofushwa na shetani.

Wao ni kama vile Sauli alivyokuwa kabla ya kuokoka. Sauli alitesa na kujaribu kuangamiza watu wa Mungu kwa sababu yeye hakujua kwamba hawa watu wa Mungu ni ufalme wa Mungu. Lakini wakati Sauli alikuwa barabarani akielekea Damesiki, alikutana na Yesu Kristo ambaye alifungua macho yake, na Sauli aliona kwamba kweli yeye anawatesa watu wa Mungu. Ufalme wa Mungu ulikuwa hapa lakini yeye hakuuona kwa sababu yeye hakuwa amezaliwa mara ya pili. Lakini baada ya kuzaliwa mara ya pili, yeye aliona ufalme wa Mungu na alianza kumtumikia Mungu katika ufalme huu.

Kuna watu wa aina mbili pekee ambao wanaona ufalme wa Mungu: wale ambao wameokoka, na wale ambao wako jahanum. Na wakati hawa wawili wanaona ufalme wa Mungu, wote wawili wako sawa kwa sababu wote wawili wanataka kuingia humo. Yule ambaye ako hapa ulimwenguni, wakati Mungu Roho Mtakatifu anafungua macho yake na kumwezesha kuona ufalme wa Mungu, basi yeye hatatosheka hadi apate kuingia humo. Yeye atakuwa kama yule mwenye biashara ambaye alisikia kuhusu lulu ya bei kali sana na kuenda kila mahali kuitafuta hadi alipoipata. Na baada ya kuipata aliuza mali yake yote ili aweze kununua ile lulu (Mathayo 13:45-46).

Pia, yule ambaye ameingia jahanum, wakati anaona ufalme wa Mungu, basi anafahamu ni nini amekosa kupata na yeye pia anaanza kuwa na tamaa ya kuingia humo. Pia, kama huyu tajiri, anaanza kuwa na tamaa kwamba jamii zake waingie ufalme wa Mungu. Yule ambaye bado ako duniani, ako na nafasi ya kuingia ufalme wa Mungu, lakini yule ambaye ameenda jahanum, yeye hana nafasi kamwe ya kuingia humo.

Msomaji, ikiwa wewe hujaokoka, basi hii ni kwa sababu wewe bado hujaona ufalme wa Mungu. Wewe umepofushwa na shetani na unawaza kwamba maisha hapa ulimwenguni yanaweza kukutosheleza. Lakini siku moja bila shaka utauona ufalme wa Mungu na siku hiyo utakuwa na tamaa kubwa sana ya kuingia ufalme huu. Pengine utauona ufalme huu wakati bado uko hapa ulimwenguni, au pengine utauona wakati utakuwa jahanum. Jambo ambalo unahitaji kufanya ni kumwomba Mungu afungue macho yako ili uweze kuona ufalme wa Mungu wakati wewe uko hapa ulimwenguni. Wakati utakapoona ufalme wake, wewe pia utakuwa tayari kuacha yote ili uweze kuingia humo.

Jambo la nne ambalo huyu tajiri aliona kwa mara ya kwanza ni jahanum.

Watu wa ulimwengu mara kwa mara wanakumbushwa kuhusu jahanum, lakini wao wanakataa kuamini yale ambayo wamefundishwa, au baada ya muda, wao wanasahau mafundisho hayo. Kwa mfano, mtu anaenda kwa matanga na analazimika kuwaza juu ya kifo kwa sababu rafiki yake au mtu wa jamii yake amekufa. Pia katika matanga anasikia mafundisho kutoka kwa neno la Mungu kuhusu kifo na maisha baada ya kifo. Na kwa masaa machache yeye anaweza kuwaza sana juu ya mambo haya na kuwaza juu ya Mungu na juu ya dhambi zake. Lakini baada ya siku chache utampata yeye amerudi kwa kazi yake ya kawaida na amesahau yote ambayo alisikia.

Au, mtu anaweza kupata ugonjwa mbaya sana na akumbushwe kuhusu kifo na maisha baada ya kifo. Wakati huo wa ugonjwa yeye ako tayari kusikia mahubiri ya neno la Mungu na hata kuwauliza wachungaji wamwombee, hata kama kwa kawaida yeye hahudhurii kanisa. Lakini baada ya muda, kwa rehema ya Mungu yeye anapona na kurudi kwa maisha yake ya kawaida. Baada ya wiki chache utaona kwamba amerudi kwa maisha yake ya kawaida na amesahau kabisa kuhusu kifo na maisha baada ya kifo.

Lakini wakati yule ambaye hajaokoka anakufa, yeye ataenda jahanum na kwa mara ya kwanza maishani mwake ataona ukweli wa jahanum. Ataona kwamba jahanum ni mahali pa mateso na pa hukumu. Ataona kweli hapa ni mahali pabaya sana. Hii ndiyo sababu huyu tajiri alitaka Lazaro arudi ulimwenguni kuwaonya mandugu zake watano.

Msomaji, wewe unajua kwamba kuna mahali ambapo panaitwa jahanum, na unajua kwamba wale wote ambao ni wenye dhambi na hawajaokoka wataenda huko. Wewe mwenyewe unajua vizuri sana kwamba Mungu ni Mtakatifu na hataruhusu yeyote ambaye hajasamehewa dhambi zake aingie mbinguni. Ikiwa wewe hujaokoka, leo unaweza kusahau mafundisho kuhusu jahanum na kuendelea na maisha yako ya dhambi. Lakini ukikaa bila kuokoka, siku moja utajipata kule jahanum. Halafu hutaweza kupuuza mafundisho kuhusu jahanum.

Leo Yesu Kristo anakualika uje kwake ili upate wokovu kutoka dhambi zako. Usipuuze mwaliko wake. Kuja kwake leo na utaokoka. Halafu hutaenda jahanum, bali utaingia ufalme wa Mungu.

Jambo la tano ambalo tajiri aliona kwa mara ya kwanza ni thamani ya wokovu.

Pengine wakati alikuwa hapa ulimwenguni alijua wale ambao wameokoka, na aliwadharau na kuwapuuza. Pengine yeye alijua kwamba yule maskini ambaye aliketi karibu na nyumba yake alikuwa ameokoka na alimdharau. Lakini wakati alifika jahanum aliona kwamba kuna kitu kimoja tu cha thamani hapa ulimwenguni na hiki ni wokovu. Hii ndiyo sababu alimwomba Abrahamu amtume Lazaro kwake ili mandugu zake watano wapate nafasi ya kuokoka.

Ikiwa wewe hujaokoka, hii ni kwa sababu wewe hujaona thamani ya wokovu. Pengine unawajua wengine ambao wameokoka na unawacheka na kuwadharau na kuwapuuza. Lakini ukiendelea hivi katika maisha yako, siku moja bila shaka utaona thamani ya wokovu na utakuwa na tamaa sana ya kuokoka, lakini utakuwa umechelewa. Usingoje hadi siku hiyo. Kuja kwake Kristo leo na mwombe akuokoe.

Jambo la sita huyu tajiri aliona kwa mara ya kwanza wakati aliingia jahanum ni jinsi dhambi zake zilivyokuwa mbaya sana mbele za Mungu.

Pengine wakati yeye alikuwa hapa ulimwenguni alikuwa mtu wa dini na mtu ambaye anajaribu kuishi maisha mema. Hatusomi katika kifungu hiki kwamba yeye alikuwa mlevi au mzinzi au mtu mbaya sana. Pengine yeye aliwaza kwamba yeye hana dhambi kubwa sana, na kwamba ile siku atakufa, Mungu atamruhusu tu aingie mbinguni kwa sababu yeye alijaribu kuishi maisha mema na alikuwa mtu wa dini. Lakini wakati aliingia jahanum alifahamu kwamba yule ambaye hajaokoka ni mwenye dhambi mkuu mbele za Mungu. Hata yule ambaye anajiwazia kwamba yeye si mtu mbaya sana ni mwenye dhambi mkuu mbele za Mungu na anastahili kuenda jahanum.

Haya ni mambo sita ambayo huyu tajiri aliona kwa mara ya kwanza wakati aliingia jahanum.

******

Mume ambaye anayemcha Mungu

Biblia ina maagizo ya jinsi tunafaa kuishi katika nyumba zetu kama mume na mke. Kuna maagizo kwa mke na maagizo kwa mume. Tutajifunza Waefeso 5:25-33 ili tuone ni nini Biblia inafundisha kuhusu jinsi waume wanafaa kuishi katika nyumba zao.

“Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda kanisa akajitoa kwa ajili yake kusudi alifanye takatifu, akalitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake, apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lo lote, bali takatifu lisilo na hatia. Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza kanisa Lake. Sisi tu viungo vya mwili Wake. Kwa sababu hii Mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe na hawa wawili watakuwa mwili mmoja” (Waefeso 5:25-33).

1. Waume wanaamrisha kuwapenda wake wao: “Ninyi waume, wapendani wake zenu.”

Kuwapenda wake wetu si jambo ambalo ni la kuchagua kufanya au la. Mungu ameamrisha tupende wake wetu. Tunafaa tujitolea kabisa ili tuwapenda wake wetu kwa mioyo yenye furaha kwa sababu Mungu hupenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu (2 Wakorintho 9:7). Ikiwa hatutawapenda wake wetu kwa furaha na kwa kujitolea, tutakuwa tunakosa kumtii Mungu na maombi yetu yatazuiliwa (1 Peter 3:7).

2. Waume wanafaa kuwapenda wake wao “kama Kristo alivyolipenda Kanisa.”

Je, Kristo alilipenda kanisa lake vipi?

(i) Kristo alilipenda kanisa lake kwa kujitolea.

Yeye Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi za watu wake; “akajitoa kwa ajili yake kusudi alifanye takatifu.” Kristo alipokufa msalabani Kalivari kwa ajili ya kanisa Lake alifanya hivyo kwa kujitolea na bila kulazimishwa. Biblia inasema, “Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri” (2 Wakorintho 8:9). Waume wanafaa kujitolea kabisa kuwapenda wake wao bila kulazimishwa. Tunafaa kuacha starehe zetu kwa ajili ya wake wetu.

(ii) Kristo alilipenda kanisa kiroho.

Baada ya Kristo kuwaokoa watu wake, Yeye huanza kazi ya utakaso katika maisha yao akilitakasa kanisa lake “kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake.” Kupitia kwa Biblia, Kristo hutuongoza katika kweli yote, lengo lake likiwa kutufanya tuwe kama Yeye mwenyewe. Yeye huwa anatushughulikia kiroho. Kwa nguvu za Roho Mtakatifu Yeye hutusaidia kusoma, kuelewa na kuishi kulingana na neno Lake. Kwa nguvu za Roho Mtakatifu Yeye hutusaidia kuomba jinsi inatupasa tuombe (Warumi 8:26).

Waume wanafaa kujishughulisha sana na mahitaji ya kiroho ya wake wao. Tunafaa kuwa na mazingira mema katika manyumba yetu ambapo wake wetu wataweza kufurahia baraka za kiroho. Kwa kufanya hivi tunafaa:

- Kusoma Biblia pamoja na wake wetu kila siku.

- Tunafaa kuwafundisha wake wetu Biblia.

- Tunafaa kuomba nao na pia kuwaombea wake wetu

- Tunafaa kuandamana nao katika ushirika wa wakristo na tunafaa kuwahimiza kuhudhuria ushirika wa madada.

Pia hakikisha kwamba humwachi mke wako nyumbani siku ya Juma Pili wakati unaenda kanisani ikiwa hakuna sababu kuu ya kufanya hivyo. Kumbuka hili; usimlazimishe mke wako kufanya mambo haya, bali mhimize kuyafanya wewe ukiwa kielelezo na mfano kwake.

(iii) Kristo anao upendo wa maalum kwa kanisa lake; “Kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake kusudi alifanye takatifu.....apate kujiletea kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lo lote, bali takatifu lisilo na hatia” Kristo alipokuja kutoka mbinguni, alikuja ili afe kwa ajili ya dhambi za kanisa lake na si kwa ajili ya dhambi za kila mtu. Yeye alikuja na kusudi moja ambalo ni kufa kwa ajili ya watu ambao Mungu Baba aliwachagua waokolewe kupitia Kwake: “Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi Yangu, bali mapenzi yake Yeye aliyenituma. Haya ndiyo mapenzi yake Yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho” (Yohana 6:38-39).

Kristo Yesu alikuja kuwaokoa wateule wa mwenyezi Mungu. Waume mnalo jukumu la kuwapenda wake wenu. Mke wako ndiye anafaa kuwa jambo la kwanza katika maisha yako kando na watu wa jamii yako, wazazi wako na marafiki wako. Chochote unachofanya na uamuzi wowote unaofanya katika maisha yako, hakikisha kwamba mke wako ndiye anayekuja wa kwanza.

(iv) Kristo Yesu ndiye anayetunza na kushughulikia mahitaji ya kimwili ya kanisa lake.

Mume anapaswa kumpenda mke wake kama vile anavyoupenda mwili wake. Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza Kanisa Lake.

3. Je, ni kwa nini mume anafaa kumpenda mke wake? “Hawa wawili watakuwa mwili mmoja.”

Hii ni kwa sababu mke na mume wote ni mwili mmoja na kwa sababu hii, “vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama mwili yao mwenyewe. Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri.”

Kalivari!

Msomaji, labda unajua kwamba Kalivari ni mahali palikuwa karibu na mji wa Yerusalemu, ni mahali ambapo Bwana Yesu Kristo Mwana wa Mungu alisulibiwa. Zaidi ya hili hatujui jambo lingine kuhusu mahali hapa Kalivari. Sura hii inaitwa Kalivari kwa sababu inafundisha kuhusu mateso na kifo cha Yesu Kristo.

Mateso na kifo cha Yesu Kristo ni mambo ambayo watu wengi wanayapuuza sana. Watu wengi hawaoni utukufu na faida yoyote katika kusulibiwa msalabani kwa Yesu Kristo.

Ni makosa sana kuwaza namna hivi. Ni jambo zuri kila wakati kuwaza na kuendelea kukumbuka kifo cha Yesu Kristo, jinsi alisalitiwa kwa maadui wake na jinsi alihukumiwa kwa njia isiyo ya haki. Pia tunapaswa kukumbuka jinsi alitemewa mate, alivyodharahuliwa na kupigwa na hata jinsi alivyovishwa taji ya miiba kichwani mwake. Tunafaa kukumbuka jinsi Bwana Yesu alipelekwa kama kondoo wa kuchinjwa bila kunung'unika na bila kukataa. Tunafaa kukumbuka jinsi Bwana Yesu alipigiliwa misumari katika mikono na miguu yake na kusulibiwa msalabani akiwa katikati ya wezi wawili, vile maadui wake walimdunga mkuki mbavuni mwake, na jinsi walimchekelea akiteseka na vile walimwacha pale msalabani akiwa uchi na akitokwa na damu hadi kufa. Ni vizuri sana kuyakumbuka mambo haya yote. Tukumbuke kwamba vitabu vya injili vyote vinne, yaani Mathayo, Marko, Luka na Yohana, vinaeleza wazi kuhusu msalaba wa Yesu Kristo na kifo chake. Hii inaonyesha kwamba kifo cha Bwana Yesu Kristo Kalivari ni jambo ambalo si la kupuuzwa.

1. Kwanza, watu wengi wanasahau kwamba mateso ya Bwana Yesu Kalivari yalikuwa yamepangwa na Mungu Baba. Mateso ya Yesu hayakuja kwake kwa bahati mbaya au bila Yeye kujua, bali yalikuwa yote yamepangwa, kukubalika na kuamuliwa kabla ya dunia kuumbwa. Msalaba wa Yesu Kristo ulikuwa katika mpango wa Mungu wa kuwaokoa wenye dhambi kabla ya dunia kuumbwa. Maumivu yote ya Yesu Kristo na kila tone la damu yake ambalo alimwaga ilikuwa imekusudiwa tangu mwanzo.

2. Pili, watu wengi wanasahau kwamba mateso ya Yesu Kalivari yalikuwa yanafaa kwa wokovu wa wanadamu. Yesu ndiye alikuwa azibebe dhambi za watu wake mwilini mwake na ni kupitia kwa kupigwa kwake watu wake walikuwa wapate kuponywa. Mateso haya yalikuwa baadhi ya malipo ya deni yetu kwa Mungu na hii ilikuwa inajumlisha dhabihu ya wokovu wa watu wa Mungu milele. Ikiwa Yesu hangekubali msalaba na kuteseka kwa niaba yetu, mwenye haki kwa wasio na haki, hatungekuwa na tumaini lolote na kungekuwa na kizuizi kikubwa sana kati yetu na Mungu ambacho hakuna mwanadamu angeweza kukivuka. Bila msalaba wa Yesu hakungekuwa na msamaha wa dhambi.

3. Tatu, watu wengi wanasahau kwamba Bwana Yesu aliyavumilia mateso yake kwa kujitolea na kwa mapenzi yake mwenyewe. Yesu hakulazimishwa na yeyote kupata mateso haya, bali Yeye ndiye alichagua kutoa uhai wake na kwa hivyo alienda Kalivari bila kulazimishwa ili aimalize kazi yake ambayo alikuja duniani kufanya. Bwana Yesu alikuwa na uwezo wa kuita kundi kubwa la malaika kutoka mbinguni ili wawatawanye Pilato na Herode na kulipeperusha jeshi la Warumi kama makapi yapeperushwavyo na upepo, lakini Yeye alichagua kuteseka kwa sababu ya kuwaokoa wenye dhambi. Bwana Yesu alikuwa ameamua kuwa chemichemi ya kuosha dhambi za wanadamu kupitia damu yake mwenyewe.

Msomaji, unaposoma mambo haya yote unaona kwamba kusulibiwa kwa Bwana Yesu msalabani ni jambo la hekima na la nguvu sana, ni jambo la amani, tumaini na furaha na pia ni jambo la faraja sana. Yeyote anayewaza kuhusu kusulibiwa kwa Yesu anapata kwamba kuna mengi ya kutosheleza na ya kujifunza.

Je, nikitaka kujua upana wa upendo wa Mungu kwa wenye dhambi, ni wapi ninatazama? Ninatazama msalaba wa Yesu. Msalaba wa Yesu ndilo hakikisho la upendo wa kweli wa Mungu Baba. Katika msalaba wa Yesu Kristo tunaona kwamba Mungu aliupenda ulimwengu huu mwovu na akamtoa Mwana wake wa pekee, alimtoa ateseke na kufa ili yeyote amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele.

Je, ninawezaje kuelewa jinsi dhambi ni jambo la kuchukiza sana machoni pa Mungu? Je, tuangalie katika historia ya gharika na kuona jinsi Mungu aliuangamiza ulimwengu? Je tutaenda kando ya bahari ya chumvi na kutazama ni nini dhambi iliwaletea watu wa Sodoma na Gomora? Ama je, nitatazama jinsi Wayahudi waliangaika jangwani na vile dhambi iliwatawanya wote duniani kote? La sivyo, tunaweza kujua jinsi dhambi ilivyo mbaya tukitazama ni nini kilifanyika Kalivari. Tunapotazama Kalivari tunaona jinsi dhambi ilivyo mbaya na inavyochukiza, kwamba hakuna kitu chochote kile kinaweza kuisafisha isipokuwa damu ya Mwana wa pekee wa Mungu. Hii inatuonyesha wazi jinsi dhambi ilivyotutenganisha na Mungu mwumba wetu na kwamba hata malaika wote mbinguni hawangeweza kutuletea amani kati yetu na Mungu.

Je, nikitaka kujua ukamilifu wa wokovu ambao Mungu anawapa watu wake, ni wapi nitatazama ili niweze kuuona wazi? Je, nitasoma jinsi Biblia inaeleza kuhusu huruma wa Mungu kwa ujumla, ama kutosheka na ukweli kwamba Mungu ni Mungu wa upendo? La sivyo, nitatazama kusulibiwa kwa Bwana Yesu Kalivari. Hakuna thibitisho lingine kuliko Kalivari. Hakuna faraja nyingine ya kutuliza moyo ambao unasumbuka kwa sababu ya dhambi kuliko kumtazama Bwana Yesu akifa msalabani. Ni msalabani pa Mwokozi ambapo dhambi za watu wa Mungu zililifidiwa. Laana iliyokuja kwa sababu ya kutotii sheria ya Mungu, iliwekwa juu ya Yesu Kristo na akateseka kwa niaba yetu na kutimiza mahitaji yote ya sheria ya Mungu. Sasa dhambi zote za watu wa Mungu zimefidiwa kabisa milele.

Je, kuna sababu ya kuufuata utakatifu? Je, nifanye nini kuhusu jambo hili? Je, nisome na kukariri ni nini Biblia inafundisha kuhusu Amri Kumi ama nisome ni nini Biblia inafundisha kuhusu neema ya Mungu? La sivyo, ninapaswa kutazama Kalivari na kutazama kusulibiwa kwa Bwana Yesu msalabani. Unapotazama msalabani Kalivari utaona upendo mwingi wa Yesu Kristo ambao utakuwezesha kuishi maisha ya kumtumikia Bwana Yesu pekee. Utaona kwamba ulinunuliwa kwa bei ya juu sana, na unapaswa kumtukuza Yesu Kristo kwa mwili wako na kwa nafsi yako.

Je, ni namna gani mtu anaweza kuwa ameridhika na mchangamfu hata wakati wa masumbuko ya ulimwengu? Jibu ni kwamba ni vyema zaidi kutazama Kalivari ambapo Yesu alisulibiwa. Mungu ambaye alimtoa Mwana wake wa pekee afe kwa ajili ya watu wake atayatimiza mahitaji yako yote na hatakosa kuwapa watu wake chochote anaona ni kizuri kwao. Yeye aliwafanyia watu wake mambo makuu, pia atawafanyia mambo madogo madogo.

Je, nitakuwa na hakikisho gani kwamba nitaingia mbinguni? Je, niridhike kwa kusema niko na tumaini la kutosha kwamba Mungu hatanitupa nje? Je, ninapaswa kutumaini ndani ya vipawa ambavyo Mungu amenipa ama nifarijike tu katika juhudi zangu za imani na maombi? Je, nitauamini moyo wangu na kusema kwamba kamwe hautakuwa moyo wa kudanganya? La sivyo. Nitatazama Kalivari na msalaba wa Yesu Kristo. Msalaba wa Yesu Kristo Kalivari ndilo hakikisho kwamba kweli nitaingia mbinguni. Yesu Kristo ambaye alipitia mateso mengi sana ili akomboe maisha yangu hatakubali kabisa maisha yangu yaangamie.

Msomaji, kuna watu mamilioni ambao hawaoni chochote cha faida katika msalaba wa Yesu Kristo. Hii inatuonyesha upofu wa wale ambao hawajaokoka, wao wamepofushwa hadi hawaoni faida ya msalaba wa Yesu Kristo. Hii ndiyo sababu mamilioni ambao wanahudhuria kanisa kila wiki wanasikia neno la Mungu lakini hawalipokei. Mioyo yao ni kama jiwe, mawazo yao yako gizani na wao wamekufa katika dhambi. Msomaji, ikiwa wewe hujawaza sana juu ya msalaba wa Yesu Kristo, ninakusihi, uwaze juu yake sana. Jiulize, “Je, ni kwa nini Mwana wa Mungu alikuwa tayari kufa kwa njia hii?” Jiulize, “Je, ni kwa nini wale ambao wameokoka wanapenda sana msalaba wa Yesu Kristo?” Kumbuka kwamba msalaba wa Yesu Kristo ndiyo njia ya pekee kwa wenye dhambi kuokoka.

******

Ushuhuda wa Beatrice Achieng

Beatrace Achieng aliokoka mwaka huu (2011) na alibatizwa mwezi wa Julai. Huu ndiyo ushuhuda wake.

Mimi nilizaliwa mwaka wa 1991. Jina langu naitwa Beatrice Achieng. Tangu utotoni mwangu nilikuwa ninapenda sana kuenda kanisa. Nilikuwa na udhaifu mwingi sana wa kubadilisha makanisa na kwa sababu ya hii nilibatizwa bila kujua.maana ya ubatizo.

Lakini nilipoingia kanisa la Injili Bible Church nilifunzwa Biblia na nikaelewa ni nini mafundisho ya Biblia.

Siku moja mchungaji alikuwa anafundisha jinsi Mungu alimwokoa Abrahamu. Mchungaji alikuwa anafundisha kutoka kitabu cha mwanzo 12:1-10, jinsi Abarahamu alikuwa akiambudu miungu. Kupitia mafundisho hayo, nilielewa kwamba dhambi zangu pia zinaweza kusamehewa na Mungu. Baada ya ibada nilienda nyumbani na nikapiga magoti nanikaomba Mungu anisamehe dhambi zangu. Niliamini kwamba Bwana Yesu Krisro alikufa msalabani kwa sababu ya dhambi zangu na baada ya siku tatu akafufuka kutoka kwa wafu na sasa ako mbingu pamoja na Mungu Baba. Ninaamini kwamba tangu siku ile nilimwomba, Yeye alinisamehe dhambi zangu, na ninajua kwamba ikiwa dunia itaisha leo, mimi nitaenda mbinguni kwa sababu ninaamini kabisa kwamba nimeokolewa na damu ya Yesu Kristo. Ninamshukuru Bwana kwa kuniokoa na pia ninawashukuru wachungaji wa Injili Bible Church na walimu kwa kuniletea habari njema kupitia mahubiri na mafundisho ya neno la Mungu.

*****

Wafilipi 1:12-26, Mateso, Maisha na Kifo.

Katika kifungu hiki mtume Paulo anafundisha mambo matatu ambayo yanawakumba wakristo maishani mwao. Kifungu hiki kinafunza jinsi mkristo anapaswa kukumbana na mambo haya. Katika injili ya Mathayo 5:11-12, Bwana Yesu alisema, "Ni heri ninyi watu watakapowashutumu na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia kwa maana dhawabu yenu ni kuu." Hivi ndivyo mtume Paulo alifanya wakati alikuwa gerezani, alitii neno la Mungu kwa kufurahi na alishangilia kama tu vile Bwana Yesu alisema. Katika kifungu hiki anaeleza mambo mawili kuhusu ni kwa nini yeye alifurahi.

1. Paulo alifurahi kwa sababu Injili ya Yesu Kristo ilikuwa inaenezwa.

Hivi ndivyo tunasoma katika msitari wa 12, "Nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia kueneza Injili." Hapa tunaona kwamba Paulo halalamiki kwa sababu ya mateso ambayo alipata akiwa gerezani. Yeye anawaza kuhusu mbinguni na mawazo yake yote yanahusu ufalme wa Mungu na jinsi Injili itaendelea kuenezwa. Kwa hivyo yeye anafurahia sana wakati anaendelea na hii kazi ya kuhubiri Injili ya Bwana hata wakati amefungwa gerezani. Tunapaswa kila wakati kukumbuka kwamba mateso, shida na majaribu ambayo tunapata sisi wakristo yameruhusiwa na Mungu, kwa kusudi la kutuleta karibu sana na Yesu Kristo ili nasi pia tuwalete wengine kwa yesu Kristo na kuwahimiza wamtumainie Yeye pekee. Unaweza kusema kwamba shida ambazo zimekupata ni nyingi sana na kwamba hujui ni vipi zitakuleta karibu na Bwana Yesu au ni namna gani kupitia kwa hizo shida utawaleta wengine kwa Kristo. Lakini unapaswa kukumbuka kwamba Mungu hataruhusu majaribu ama mateso ambayo huwezi kuyavumilia (1 Wakolintho 10:13). Mungu wetu ni mwema kila wakati katika kila jambo ambalo anafanya, na ikiwa ameruhusu mateso yaje kwa mtu wake, atampa huyo mtu njia ya kutokea ili aweze kustahimili. Paulo alikuwa na mpango wa kwenda Roma lakini Mungu akampeleka Roma kwa njia maalum; yaani alifungwa jela huko Rumi na akiwa gerezani alipata fursa mzuri sana ya kuwahubiria walinzi (mstari 13). Mtume Paulo aliwahubiria walinzi wakiwa katika hali zao za kazi na baada ya kutoka kazini pia wao waliwahubiria wengine.

Mahubiri ya Paulo akiwa kifungoni yaliwatia moyo wandugu wengine wengi, na wao pia wakaanza kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi bila uoga (mstari wa 14). Kazi ya kuhubiri neno la Mungu ni kazi ambayo siyo ya kufanywa na mtu mmoja. Hii ni kazi ambayo haifai kusimama hata kama mtu fulani amekosekana, wengine wanapaswa kuindeleza. Paulo alifurahi sana kwa sababu ya kuenea kwa Injili ya Bwana Yesu, hata hakujali kuhusu watu ambao walikuwa wanahubiri kwa nia zingine. Paulo hasemi kwamba wale wanafundisha neno la Mungu wakiwa na nia fulani wasiendelee, bali yeye anasema kwamba anafurahia bora tu Kristo anahubiriwa. Katika mstari wa 18 anasema, "Lakini inadhuru nini? Jambo la muhimu ni kwamba kwa kila njia, ikiwa ni kwa nia mbaya au njema Kristo anahubiriwa. Nami kwa ajili ya jambo hilo ninafurahi."

Tunapaswa kufarahi wakati neno la Mungu linahubiriwa. Hatufai kamwe kukasirika ama kuwapinga wale wanahubiri Kristo bali tunapaswa kuwasaidia. Ni kweli kabisa kuna wale ambao watahubiri vizuri sana kuhusu Yesu Kristo, lakini katika mambo fulani tukose kukumbaliana, lakini ikiwa wanahubiri Injili ya Yesu Kristo hatufai kuwa kinyume nao. Katika Injili ya Marko 9:38-40, Yohana alimwambia Bwana Yesu, "Tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa Jina Lako nasi tukamkataza kwa sababu yeye si mmoja wetu." Lakini Bwana Yesu aliwaambia wasimkataze. Hatujui mtu huyo alikuwa akikemea pepo wachafu kwa nia gani lakini tunajua chochote alikuwa akifanya, alifanya kwa Jina la Yesu

2. Paulo anafurahi kwa sababu yale yaliyompata yatageuka kuwa wokovu wake.

Katika mstari wa 19-20 Paulo anasema hivi, "Kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Yesu Kristo, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu. Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yoyote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wowote, Kristo atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa." Paulo anasema hapa kwamba dhamira yake ni safi kabisa kwamba yeye hakuzuia kuenea kwa Injili ya Yesu Kristo hata wakati alikuwa amefungwa jela

3. Mawazo ya Paulo kuhusu uzima na kifo (1:21-26).

Katika kifungu hiki Paulo anafundisha mambo mawili; yaani uzima na kifo.

(i) Uzima. Paulo anasema hapa kwamba maisha hapa duniani ni ya maana ikiwa mtu anatumika kueneza Injili ya BwanaYesu. Katika mstari wa 21 Paulo anasema, "Kwangu mimi kuishi ni Kristo na kufa ni faida." Halafu katika mstari wa 22 anaeleza hii inamaanisha nini, kwamba "Kama nitaendelea kuishi katika mwili, hii ni kwa ajili ya matunda ya kazi." Pia katika mstari wa 24 anasema, "Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili." Kwa hivyo tunaona hapa kwamba Paulo anayaona maisha yake hapa duniani kuwa ya maana ikiwa atatumika katika kazi ya Mungu. Katika mstari wa 25 na 26, Paulo anasema ana matumaini kwamba mapenzi ya Bwana ni kwamba yeye ataendelea kuwa nao: "Ninajua kwamba nitaendelea kuwapo na kuwa pamoja nanyi nyote, ili mpate kukua na kuwa na furaha katika imani." Mipango ya Paulo siyo tu kuishi na kufurahia maisha hapa duniani, lengo lake kuu katika maisha yake lilikuwa ni kueneza Injili, na hiyo kazi ikiisha yeye hakuona faida yoyote ya kuendelea kuishi duniani.

Hivi sivyo watu wa ulimwengu huu wanafikiria. Wao wanawaza sana kuhusu mali zao na afya yao. Wengine wanaishi kutimiza starehe zao na kueneza sifa zao, wakitumaini kujitengenezea jina ili wakati watakufa, wakumbukwe. Kila mtu anafaa ajiulize yeye anaishi akimtumikia nani. Tunafaa kukumbuka kwamba, kuwa na maisha ya furaha ya kweli ni kuwa tu ndani ya Kristo Yesu. Haya ndiyo yanafaa kuwa mawazo ya kila mkristo. Ikiwa wewe unasema kwamba umeokoka, na katika mawazo yako huwazi chochote jinsi unamtumikia Kristo basi haufikirii inavyostahili.

(ii) Kifo. Paulo anasema anatamani kufa. Alitamani sana kuondoka duniani ili awe pamoja na Kristo. Katika mstari wa 21 anasema,"Kwangu mimi, kuishi ni Kristo na kufa ni faida." Je, ni kwa nini Paulo anasema kwamba kufa ni faida? Kifo kilikuwa faida kwa Paulo kwa sababu kingemweka huru kutoka kwa dhambi za ulimwengu huu na majaribu yake. Pia kifo kingemwepusha na maadui wake na pia maadui wa Bwana. Kwa Paulo kifo kilikuwa mlango wa kuingia mbinguni, mahali ambapo ni patakatifu na ambamo atafurahia milele. Hii ndiyo sababu katika mstari wa 23 anasema, "Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi." Mafikira ya Paulo kuhusu mbinguni yalikuwa wazi kabisa. Yeye alitarajia kwa furaha sana siku hiyo kufika ili aweze kuingia mbinguni. Hili lilikuwa jambo kuu sana katika mafundisho yake. Aliwakumbusha watu wa Thesalonike kuhusu mambo ya mbinguni (1 Wathesalonike 1:10, 2 Wathesalonike 2:1-5). Paulo aliona mbinguni kuwa makao yake ya milele na kwa hivyo alikuwa anangoja siku hiyo. Haya ndiyo yanafaa kuwa mawazo ya kila mkristo.

Habari kutoka Injili Bible Church, Kawangware

Tunafuraha kutagaza kwamba kutakuwa na mkutana wa masoma ya neno la Mungu kuanzia tarehe 25 hadi 27 mwezi wa Kumi 2011. Masoma haya ni ya kila mkristo ambaye angependa kuhudhuria. Wakati huo tutajifunza kuhusu: mafundisho muhimu sana kutoka kitabu cha Warumi, kurudi kwa Bwana Yesu duniani na jinsi ya kuabudu katika kanisa. Kila mtu amealikwa kuungana nasi wakati huo. Mafundisho haya yatakuwa yakianzia saa nne ya asubuhi, na kumalizika saa tisa ya mchana kila siku.

Pia mwezi wa kumi na moja kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 2 mwenzi wa kumi na mbili kutakuwa na mkutano wa vijana katika kanisa la Injili Bible Church, Kawangware. Tutakuwa tukifundisha mafunzo haya: Mafundisho muhimu kutoka kitabu cha Kutoka, Ufalme wa Mungu na jinsi ya kuishi maisha ya ukristo. Kila mtu amealikwa kuhudhuria mafundisho haya.