Header

Ujumbe Kutoka kwa Mchapishaji

Karibuni kwa toleo la kwanza la jarida hili la Ujumbe wa Biblia. Ni lengo letu, Mungu akipenda, kuchapisha jarida hili baada kila miezi mitatu. Pia ni lengo letu, Mungu akipenda, kuchapisha jarida hili katika lugha ya Kiingereza. Tunamwomba Mungu kwamba unaposoma jarida hili, Yeye atakubariki na kwamba atalitumia jarida hili kukufundisha neno lake na kukuongoza katika njia zake.

Tumeliita jarida hili Ujumbe wa Biblia kwa sababu huu ni ujumbe muhimu sana ambao sisi wanadamu tumepewa. Biblia ni neno la Mungu, kila neno katika Biblia limeandikwa na Mungu mwenyewe. Hii ndiyo sababu tunahitaji kuisoma na kufahamu ni nini Biblia inatufundisha leo.

Ujumbe wa Biblia unaweza kujumlishwa katika maneno manne.

1. Biblia inatufundisha kumhusu Mungu. Inatuambia kwamba Mungu ni mtakatifu na mwenye haki na msafi. Inatuambia kwamba Yeye huchukia dhambi na ni lazima ahukumu dhambi kwa sababu Yeye ni Mungu. Pia Biblia inatufundisha kwamba Mungu ni mwenye neema, mkarimu na mwenye rehema. Inatufundisha kwamba Mungu hujali viumbe vyake, na kwamba ametayarisha njia kwa wenye dhambi kuokoka kutoka kwa dhambi zao.

2. Biblia inatufundisha kuhusu mwanadamu. Inatufundisha kwamba mwanadamu aliumbwa na Mungu akiwa amekamilika na bila dhambi, lakini yeye ameanguka dhambini na yeye sasa ni mwenye hatia na mchafu mbele za Mungu. Biblia inatufundisha kwamba hakuna chochote ambacho mwanadamu anaweza kufanya kujiokoa; yeye hana uwezo wa kufanya yale ambayo yatampendeza Mungu. Inatufundisha kwamba ikiwa Mungu hatamwokoa mtu, yule mtu hana uwezo wa kujiokoa.

3. Biblia inatufundisha kuhusu Kristo na kuhusu njia ya wokovu. Inatufundisha kwamba Bwana Yesu Kristo, ambaye ni Mungu kamili na mwanadamu kamili, alikuja hapa ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi kupitia kwa kifo chake na ufufuo wake. Inatufundisha kwamba kuna njia moja tu ya kuokoka kutoka kwa dhambi zetu na hii ni kutubu dhambi zetu na kumwamini Yesu Kristo pekee.

4. Biblia inatufundisha kuhusu maisha ya ukristo. Inatufundisha kwamba wale ambao wameokoka, Roho Mtakatifu anaishi ndani mwao, na kwamba Mungu anawaamuru wao waishi maisha ya utakatifu na ya kumtumikia ili wamtukuze.

Haya ni mambo ambayo utapata katika jarida hili. Tunaomba kwamba Mungu atakubariki unapolisoma na kujifunza.

“Karibuni, kila kitu ni tayari sasa” (Luka 14:17).

Wakati Bwana Yesu Kristo alizungumza maneno haya, alikuwa anawaeleza Wayahudi wa siku zake. Lakini hata hivyo, maneno haya ni ya maana sana kwetu leo. Mfano huu unazungmza kuhusu karamu. Biblia inatueleza kwamba kuna karamu kuu ambayo itafanyika wakati Bwana Yesu Kristo atarudi: karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo (Ufunuo 19:9). Hii ndiyo sababu tunafaa kuelewa maneno haya. Kama tu jinsi watu katika mfano huu walikuwa wamealikwa kwa karamu, vivyo hivyo, hata sisi tumealikwa kwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo.

Maneno haya ya Bwana Yesu Kristo; “Karibuni kila kitu ni tayari,” ni ya muhimu sana kwetu leo. Siku ya Pentekote, Roho Mtakatifu alikuja na alianza kuujenga ufalme wa Kristo hapa ulimwenguni. Mungu ameweka kila kitu tayari ili watenda dhambi waweze kuja Kwake na wapate wokovu. Leo anakualika wewe uje kwake na upate kuokoka. Ninakusihi, usianze kutoa vijisababu, bali kuja kwa Kristo Yesu leo kwa sababu anakualika uje. Bwana Yesu Kristo anasema wazi kwamba, “kila kitu ni tayari sasa.” Ni Mungu ambaye ameweka kila kitu kuwa tayari na ni Mungu ambaye anakualika uje Kwake. Hili ndilo jambo ambalo ninataka kukufundisha katika mahubiri haya.

1. Kwa kawaida, Mungu huweka kila kitu kiwe tayari.

Ni kawaida ya Mungu kupanga na kutayarisha kila kitu kwa makini sana. Wakati wageni wanakuja, huwa hawampati akikimbia hapa na pale ili aweze kutayarisha mambo kwa haraka. Wageni wanapokuja kwa Mungu, wanapata kwamba kila kitu kiko tayari.

Hivi ndivyo mambo yalivyo wakati tunasoma kuhusu kuumbwa kwa mbingu na ulimwengu. Kabla Mungu hajaumba mimea, alitayarisha kwanza mahali ambapo mimea ingemea. Pia Mungu alitayarisha mahali ambapo wanyama wangeishi na chakula ambacho wangekula, ndipo akawaumba. Mwisho Mungu alitayarisha mahali ambapo mwanadamu anageishi kwa amani, ndipo akamwumba mwanadamu. Wakati alipomaliza kazi yake ya uumbaji, kila kitu kilikuwa kizuri. Wanyama hawakukosa chakula, Adamu hakukosa chakula au maji au hewa. Kila kitu kilikuwa kimetayarishwa vyema kwanza.

Tunapata pia jambo hili wakati wa gharika. Kabla ya Mungu kuleta gharika katika ulimwengu huu, kwanza alimwambia Nuhu ajenge safina. Wanyama waliingia ndani ya safina na wakatoshea vizuri. Halafu Mungu akamwambia Nuhu, “Ingia katika safina wewe na jamaa yako yote” (Mwanzo 7:1). Kila kitu kilikuwa kimetayrishwa vyema kwa Nuhu na jamaa yake ili waweze kuokolewa kutokana na gharika na pia kwa ajili ya mwanzo mpya wa maisha duniani.

Kwa njia hiyo hiyo, tunasoma kwamba ulikuwa mpango wa Mungu kwamba Waisraeli waishi katika nchi ya Misri (Mwanzo 15:13). Mungu alipanga kwamba Yusufu angetangulia huku na awe mtu mkuu katika nchi hiyo. Halafu Mungu alileta njaa katika nchi ya Kanaani. Halafu Yakobo na watoto wake waliweze kuelekea nchi ya Misri na wakaishi huko kwa amani. Ni Mungu ambaye alipanga waende huko na waishi huko.

Waisreali hawakuingia Kanaani hadi wakati kila kitu kilikuwa kimetayarishwa kabisa na Mungu. Mungu alikuwa amemwambia Abrahamu kwamba, “dhambi ya Waamori bado haijafika kipimo kilichojaa” (Mwanzo 15:16). Hii inamaanisha kwamba Mungu hakuwa tayari kuwahukumu wale ambao walikuwa katika nchi ya Kanaani hadi wakati Yoshua aliwaongoza Waisreali kuingia humo. Kwa neema Yake, Mungu alikuwa mvumilivu na Waamori hadi wakati wa hukumu wao ulipofika. Wakati ulipofika, Mungu alienda mbele za Waisraeli na aliwapigania na kuwapa makao ambayo hawakuwa wameyajenga na chakula ambacho walikuwa hawajafanyia kazi. Waliingia katika nchi ambayo ilikuwa inatiririka maziwa na asali.

Tunaona ukweli huu katika mpango wa Mungu wa wokovu. Mungu alipanga wokovu wetu kabla ya kuumba mbingu na dunia. Kabla ya kuumba mbingu na dunia, alichagua ni nani ataokoka na ataokoka kwa njia gani. Alipanga haya yote kabla hajaumba chochote. Aliwapenda watu Wake kabla ya kuumba chochote.

“Karibuni, kila kitu ni tayari sasa.” Mungu hajapanga tu wokovu wetu, bali pia ametayarisha kila kitu kwa wokovu wetu. Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili ya watu Wake msalabani Kalivari. Alimwaga damu Yake ili tuweze kuoshwa kutoka kwa dhambi zetu. Tumepewa neno la Mungu, na Roho Mtakatifu ametumwa kuja kutufundisha neno hili. Ujumbe wa injili ni kwamba, Mungu ametuahidi wokovu mkuu na kwamba pia Mungu ametutayarishia wokovu mkuu. Ikiwa hujaokoka, kuna himizo kubwa sana kwako ili uje kwa Kristo Yesu. Mungu hakuambii kwamba uache dhambi zako ndipo uje Kwake. Mungu ameshaa kufanyia yote. Kile unahitaji kufanya ni kuja Kwake kwa imani na ukubali zawadi yake bila malipo ambayo ni wokovu.

Kwa sababu Mungu ametayarisha kila kitu, inaonyesha kwamba yeyote ambaye atakuja Kwake atapokelewa. Kwa mfano, rafiki wako anakualika katika nyumba yake, lakini unapofika huko, unapata kwamba rafiki wako hakuwa tayari kukupokea. Unapofika huko unapata kwamba analala na hajajitayarisha kwa kuja kwako. Unapopata mambo yakiwa hivi, utajua kwa kweli kwamba, hakuwa makini wakati alikuwa anakualika. Alikuwa anataani tu.

Lakini Mungu anaposema, “Karibu,” Yeye huwa anamaanisha jambo hili, kwa sababu amesha tayarisha kila kitu kwa ajili ya wokovu wako na sasa anakutarajia uje Kwake. Ametayarisha wokovu kwa ajili ya nafsi yako na nafasi ya kumpumzika milele mbinguni. Kwa hivyo mwaliko Wake kwako ni wa kweli.

Hili ndilo jambo la kwanza tunajifunza, kwamba Mungu amepanga kila kitu kwa makini sana kabla ya kuumba chochote.

2. Kwa sababu kila kitu kiko tayari, watoto wa Mungu wanafaa kuja kwa Mungu mara kwa mara.

Ikiwa wewe umeokoka, ninataka uzingatie jambo hili. Unajua kwamba wakati Bwana Yesu Kristo anawaalika watu Wake waje kwake, huwa kila kitu kiko tayari.

Katika Yohana 21:1-14, tunasoma kuhusu wanafunzi wa Yesu ambao walikuwa wamefanya kazi usiku wote wakijaribu kuwashika samaki. Asubuhi na mapema walimwona Bwana Yesu akiwa kando ya bahari na aliwaita kwa kusema, “Njoni mpate kifungua kinywa” (Yohana 21:12). Wakati walopifika mahali Yesu alikuwa, “wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake na mikate” (Yohana 21:9). Waliona kwamba kila kitu kilikuwa tayari. Bwana Yesu Kristo aliwaalika na alihakikisha kwamba kila kitu kilikuwa tayari kwanza.

Katika Biblia, Bwana Yesu Kristo anatualika tuje kwa Mungu kwa maombi (Luka 18:1). Anatupatia mwaliko huu kwa sababu kila kitu kiko tayari kwa ajili yetu. Je, uko katika hali ya umaskini wa kiroho? Kuja kwake katika maombi na umwombe akusaidie katika hali yako ya kiroho. Je, unahitaji nguvu katika maisha yako ya kiroho? Mungu anasema, “Nguvu zako zitakuwa sawa na siku zako” (Kumbukumbu la Torati 33:25). Je, unahitaji faraja na kuhimizwa? Kumbuka kwamba Mungu, ni Mungu wa faraja na kwamba ukija kwake kwa maombi, atakufariji na atakuhimiza. Kila kitu kiko tayari. Kwa hivyo kuja kwa kiti cha rehema cha Mungu kwa maombi.

Kumbuka kwamba kwa sababu Kristo Yesu alikufa msalabani, mlango wa kufika kwa Mungu umefunguliwa. Kristo alipokufa msalabani, pazia la hekalu lilipasuka vipande viwili. Yeyote ambaye anaamini na kuokolewa, anaweza kuja mbele za Mungu na kumwambia mahitaji yake yote. Huhitaji kuja na chochote wakati unakuja mbele za Mungu katika maombi; njoo jinsi ulivyo kwa Kristo.

Ukweli kwamba Mungu ameweka kila kitu tayari kwa ajili yetu unafaa kutuhimiza katika maisha yetu ya kila siku. Wakati tunapoamka asubuhi, huwa hatujui kabisa ni nini tutakumbana nayo. Lakini tunafaa kukumbuka kwamba Mungu ametayarisha kila kitu kwa ajili ya kila siku. Ikiwa tutakuwa na moyo wa kumpenda na kumtumikia Mungu kila mahali tupo, basi tunafaa kuwa na uhakika kwamba Mungu ametayarisha kila kitu ili tuweze kumtumikia sawasawa. Ikiwa utamwomba Mungu akupatie fursa la kumshuhudia Kristo au kumhimiza mtu katika neno Lake, utapata kwamba fursa hiyo imeshatayarishwa na Mungu. Kila kitu kiko tayari kwa watu wa Mungu.

3. Kwa sababu kila kitu kiko tayari, wale ambao hawajaokoka wanafaa kuja kwa Mungu leo ili waweze kuokolewa.

Je, wewe ni mtu ambaye hajaokoka na unataka kuokoka? Je, uko na tamaa ya vitu hivyo ambavyo vitatosheleza nafsi yako na kukupatia tumaini la mbinguni? Basi sikiza maneno haya ya Bwana Yesu Kristo: “Karibuni, kila kitu ni tayari sasa.” Kila kitu ambacho unahitaji ili upate kuokoka, kimewekwa tayari kupitia kwa Kristo Yesu na kazi Yake. Kila kitu ambacho unahitaji: uzima wa milele, msamaha wa dhambi zako, kuoshwa kutoka na dhambi zako, vazi la haki, furaha ya milele mbele za Mungu, haya yote yanapatikana katika Kristo Yesu pekee na yako tayari kwa ajili yako.

Huwezi kusema kwamba, “siwezi kuja kwa sababu sina hili wale lile.” Mungu anakualika kwa karamu ambayo ametayarisha. Mungu haulizi wewe utayarishe karamu, wala hakuulizi utayarishe lolote kwa ajili ya karamu hii. Yeye mwenyewe ametayarisha kila kitu ambacho unahitaji ili uweze kuokoka. Kile unahitaji kufanya ni kuja Kwake. Litakuwa jambo la kumdharau Mungu ikiwa wewe utakuja Kwake na matendo yako mazuri. Ikiwa mtu amekualikwa kwake kwa ajili ya chakula, litakuwa jambo la madharau wewe kuenda na chakula chako. Ni kama kumwambia mtu huyu kwamba chakula chake si cha maana. Mungu anakueleza kwamba kila kitu kiko tayari na unafaa uje jinsi ulivyo na atakuokoa.

4. Kwa sababu kila kitu kiko tayari, huna sababu ya kukaa mbali na Kristo.

Katika mfano huu, mtumishi alitumwa aende awaelezee kwamba kila kitu kiko tayari. Wakati aliwaambia, kila mmoja wao alianza kutoa vijisababu vya kukosa kuja kwa karamu. Lakini vijisababu vyao vyote vilikuwa vya upumbavu kwa sababu kila kitu kilikuwa tayari kwao. Hawa wageni hawangeweza kusema kwamba, “nilitaka kuja lakini chakula hakikuwa tayari.” Mwenye nyumba alikasirika kwa sababu alikuwa ametayarisha kila kitu lakini wao walikata kuja.

Kuna wengi ambao walikataa kuja kwa karamu kwa sababu walijali sana mali yao ya ulimwengu. Mmoja wao alisema, “Nimenunua shamba, lazima niende kuliona” (Luka 14:18); mwingine alisema, “Ndipo nimenunua jozi tano za ng'ombe wa kulimia, nami ninakwenda kuwajaribu” (Luka 14:19). Kwa sababu walipenda sana vitu vya ulimwengu huu, walikataa kwenda kwa karamu. Kuna wengi ambao wanatoa vijisababu hivi kwa sababu wanapenda sana vitu vya ulimwengu huu. Wanajua kwamba ikiwa watakuja kwa Kristo Yesu, ni lazima waache upendo wa vitu vya ulimwengu huu na hili hawako tayari kufanya. Kwa sababu watu wengi wanapenda ulimwengu huu na vitu vyake vyote, huwa wanakataa kuja kwa Kristo Yesu. Mara kwa mara ni wale tu ambao hawana vitu hivi, ndiyo huja kwa Kristo kwa idadi kubwa. Wengine mali hii ya ulimwengu huwa ni kizuizi kwao kuja katika ufalme wa Mungu.

Pia kuna yule ambaye alikataa kuja kwa karamu kwa sababu alikuwa amemwoa mke. Hii inatuonyesha kwamba kuna wengi ambao wanazuiliwa na uoga wa watu wa jamii zao na marafiki wao kuja kwa Kristo. Mwanamke anataka kuokoka lakini kwa sababu anamwogopa mumewe, anatoa vijisababu. Kuna vijana wengi ambao wanaogopa kuchekelewa na marafiki wao wa ulimwengu, kwa hivyo wanamkataa Kristo kwa kutoa vijisababu. Mtoto wa shule anakataa kuokoka kwa sababu anajua atachekelewa na wenzake. Kwa hivyo anabaki akiwa hajaokoka.

Mfano huu unafundisha kwamba wale ambao wanabaki wakiwa hawajaokoka, hawatakuwa na vijisababu vya kutoa siku ya hukumu. Mungu ametayarisha kila kitu na anakualika uje Kwake. Huna sababu ya kubaki katika dhambi zako.

Yesu Kristo ndiye Mchungaji wa watu Wake

Haya ni mafundisho kutoka katika Zaburi 23. Tafadhali soma Zaburi hii kabla ya kusoma mafundisho haya.

Zaburi 23 inafahamika sana na wale ambao wameokoka na wale ambao hawajaokoka. Wengi huikariri kama ishara ya kuonyesha kwamba wanamwamini Mungu. Tujifunze Zaburi hii ili tuone ni mafundisho gani yanapatikana ndani.

1. Bwana Yesu Kristo ndiye Mchungaji wa watu Wake.

Zaburi inaanza hivi, “Bwana ndiye mchungaji wangu” (mstari wa 1). Yesu mwenyewe alisema, “Mimi ndimi Mchungaji Mwema. Mchungaji Mwema hutoa uhai Wake kwa ajili ya kondoo” (Yohana 10:11). Je, kondoo ni kina nani na je, mchungaji alifanya nini ili aweze kuhakikishia kondoo wake uzima? Jibu ni, Aliyatoa maisha Yake kwa ajili yao. Alikufa ili kondoo wake waweze kupata uzima wa milele.

Wakristo wote wakati mmoja walikuwa watenda dhambi wakuu ambao walifuata njia na tamaa zao wenyewe. Kama kondoo, kila mmoja alienda njia yake (Isaya 53:6). Sisi sote tulikuwa tumepotelea katika dhambi zetu na mwisho wetu ulikuwa jahanum. Lakini kama mchungaji mwema wa kondoo wake anavyoenda kila mahali akiwatafuta kondoo wake ambao wamepotea, ndivyo Kristo Mwana wa Mungu alivyofanya kwetu. Alitoka mbinguni na akaja hapa na kufa kifo cha aibu sana msalabani ili awaokoe watu Wake kutoka kwa dhambi zao na kuwapatanisha na Mungu Mtakatifu. Yesu Kristo mwenyewe alisema, “Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yohana 15:13). Katika Luka 15, Yesu Kristo alizungumza mfano kuhusu kondoo aliyepotea na jinsi mchungaji alivyoenda kila mahali akimtafuta kondoo wake. Baada ya kutuokoa kutoka kwa dhambi zetu, kama mchungaji ambaye anampata kondoo wake, Kristo huwa hatuachi peke yetu, bali Yeye huwa nasi maishani mwetu mwote. Kondoo ni watenda dhambi na Mchungaji ni Kristo Yesu.

Hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kutufanyia jinsi Kristo alivyotufanyia sisi watu Wake. Wale wote ambao hawamwamini Kristo, ni mbuzi ambao watatawanywa kutoka kwa kondoo na Bwana Yesu Kristo wakati atakaporudi na mwishowe atawatupa jahanum (Mathayo 25:45-46). Wewe ambaye hajaokoka, ninakusihi uje Kwake leo. Kwa sababu Yeye ni mchungaji, anakutafuta na yuko tayari kukuokoa kutoka kwa dhambi zako. Njoo Kwake leo na usingoje.

2. Kwa sababu Bwana Yesu Kristo ni Bwana wa watu wake, Yeye anawapatia watu Wake mahitaji yao yote.

Zaburi inasema, “Sitapungukiwa na kitu” (Mstari wa 2). Bwana Yesu Kristo ametupatia kila kitu ambacho tunahitaji. Zaidi ya yote ametupatia wokovu kupitia kwa kifo chake msalabani. Watu wa Mungu hawatawahi kukosa lolote ambalo wanahitaji, kwa sababu hawatawahi kupungukiwa “na kitu.” Bwana Yesu Kristo huwapatia kondoo Wake mambo yafuatayo.

(i) Amewasamehe dhambi zao na kuwaletea amani na Mungu. “Katika majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza” (mistari wa 2-3). Biblia inatueleza wazi kwamba Bwana Yesu Kristo anazo nguvu za kusamehe dhambi za watu Wake (Marko 1:1-12). Kizuizi kikubwa kati ya mwanadamu na Mungu ni dhambi. Wanadamu wote wamezaliwa wakiwa watenda dhambi na waasi dhidi ya Mungu. Kwa sababu ya dhambi zetu, milele tulikuwa tumetenganishwa na Mungu. Tunazaliwa bila tumaini na bila Mungu na mwisho wetu huwa ni jahanum kwa sababu ya dhambi zetu. Kristo Yesu alitoka mbinguni kuleta amani kati ya Mungu na mwanadamu. Ili amani hii iwepo, Kristo alikufa kifo cha aibu msalabani. Aliteswa na kudharauliwa kwa ajili ya dhambi zetu: “Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu” (Warumi 5:8). Yesu Kristo alijua kwamba alikuwa afe kwa ajili ya dhambi zetu. Alisema, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwa Kwangu” (Yohana 14:6). Kwa sababu Kristo Yesu alikufa msalabani, sisi ambao tumemwamini tunafanywa wenye haki kwa imani na tuna amani na Mungu kupitia Kwake (Warumi 5:1).

Sasa kwa sababu Kristo Yesu alikufa na akafufuka, wale wote ambao wameokoka milele wana amani na Mungu.

(ii) Bwana Yesu Kristo anawaongoza na anawalinda watu Wake maishani mwao mwote kwa ajili ya utukufu Wake. “Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina Lake. Naam, nijapopita katikati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami” (mistari 3b-4).

Je, Bwana Yesu Kristo huwaongoza watu Wake kwa njia gani? Jibu ni, kwa njia za haki. Je, ni kwa nini anawaongoza katika njia hizi? Jibu ni, ili waweze kulitukuza Jina Lake. Bwana Yesu Kristo huwa pamoja na watu Wake kila mahali. Huwa anawalinda, huwa anawapatia mahitaji yao ya kiroho na ya kimwili, huwa anawalinda kutokana na maadui wao na huwa anawafundisha neno Lake. Moyo wa Mungu huwa kwa watoto wake wakati wote. Mahitaji ya watu wake huwa ni shughuli Yake. Hii ndiyo sababu Mungu huwahimiza watu wake kwamba, “utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake na haya yote mtaongezewa” (Mathayo 6:33).

Mungu ametupatia neno Lake (Biblia) ili tuweze kufahamu njia zake na tuzishikilie ahadi Zake. Mungu hutuongoza kwa kutumia neno Lake: “Kila andiko, lililovuviwa na Mungu lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kuwaongoza na kuwafundisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila kazi njema” (2 Timotheo 3:16-17).

(iii) Bwana Yesu Kristo anawapatia watu Wake ushindi dhidi ya maadui wao. “Waandaa meza mbele yangu machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, kikombe changu kinafurika” (mstari 5).

Huu ni ushindi wa watu wa Mungu dhidi ya maadui wao. Sisi ambao tumeokoka tunao maadui wenye nguvu. Ulimwengu na anasa zake ni adui wetu mkubwa; miili ambayo tuko nayo inatujaribu mara kwa mara, hata shetani mwenyewe huwa hapumziki kwa sababu anapanga kutuangamiza. Je, tunawezaje kushinda vita hivi bila Kristo Yesu? Shukurani kwa Kristo kwa sababu katika mambo haya yote, tunashinda, naam na zaidi ya kushinda kwa Yeye aliyetupenda (Warumi 8:37). Hakuna yeyote ambaye anaweza kuwashinda watu wa Mungu kwa sababu Kristo Yesu mwenyewe ambaye ndiye Simba wa kabila la Yuda ni ngao yao. Utukufu kwa Mungu kwa sababu ushindi ni wetu kupitia kwa Kristo Yesu.

(iv) Bwana Yesu Kristo huwapatia watu wake kupumzika milele. “Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu, nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele” (mstari wa 6).

Yesu Kristo ametuokoa, hutuongoza na hutulinda. Yesu Kristo anarudi kutupeleka nyumbani mahali ambapo tutaishi naye milele. Kila mkristo anayo nafasi mbinguni pamoja na Bwana Yesu (Yohana 14:1-4). Watoto wa Mungu wote siku moja wataletwa katika pumzisho na Kristo Yesu. Pumzisho hili ni la watu wa Mungu pekee (Mathayo 25:34). Wale ambao hawajaokoka hawatafurahia pumziko hili bali watatupwa katika moto wa jahanum milele.

Watoto wa Mungu watapumzishwa kutokana na uwepo wa dhambi, kutokana na anasa za ulimwengu huu na kutokana na tamaa za mwili. Watapewa miili mipya ambayo haitakuwa imenajisiwa na dhambi. Njoo kwa Kristo leo na utakuwa na tumaini la kumpumzika na Kristo milele.

******

Kutoamini ni jambo la kushangaza sana.

“Akashangazwa sana kwa jinsi wasivyokuwa na imani” (Marko 6:6).

Mstari huu unatukumbusha kwamba Bwana Yesu alikuwa mwanadamu kamili. Yeye alikuwa mwanadamu kamili na pia alikuwa Mungu kamili. Hii ndiyo sababu alishangaa. Akiwa Mungu, alijua kila kitu na hakuna chochote kingemshangaza. Lakini akiwa mwanadamu alikuwa tu kama sisi na kuna mambo ambayo yangemshangaza. Hii ndiyo sababu wakati alienda katika mji alikozaliwa na kupata kwamba watu hawamwamini alishangaa.

Katika mahubiri haya ninataka kuongea kuhusu kutoamini. Hii ni kwa sababu kutoamini ni jambo la kushangaza sana, na Yesu Kristo alishangaa alipowaona watu wakikosa kuamini. Kuna watu wengi humu ulimwenguni leo ambao hawaamini, na kwa hivyo katika mahubiri haya ninataka kuzungumza kuhusu mambo mawili:

1. Kwanza, ninataka kueleza kuhusu kutoamini ni nini.

2. Pili, ninataka kueleza kwa nini kutoamini ni jambo la kushangaza.

1. Je, kutoamini ni nini?

Kutoamini ni wakati mtu anakataa kuamini kile Mungu amesema. Ni wakati mtu anakataa kutii onyo kutoka kwa Mungu ama kukubali ahadi ambazo Mungu amesema. Ni wakati mtu anakataa kukubali ushauri ambao Mungu anampatia ama tisho ambalo Mungu amesema ama ujumbe ambao Mungu amemtumia. Kwa ufupi kutoamini ni wakati mtu anakataa kutii mambo ambayo yameandikwa katika Biblia, ambayo ni neno la Mungu. Ni wakati mtu anakataa kuamini kwamba Biblia ndilo neno la Mungu na kwamba kila neno ambalo liko ndani yake ni kweli. Kutoamini ni wakati mtu anawaza kwamba Biblia siyo muhimu ama kitu cha maana kwake. Ni wakati mtu anawaza kwamba Biblia haina chochote cha umuhimu kwake. Hii ndiyo kutoamini.

Kukosa kuamini ndiyo dhambi ya zamani sana katika Biblia. Kutoamini kulianza wakati Adamu na Hawa walikula tunda ambalo walikatazwa na Mungu katika bustani la Edeni na kwa hivyo wakaleta dhambi duniani. Mungu alikuwa amawaeleza kwamba siku ile watakula matunda ya mti aliowakataza watakufa, lakini wao hawakuwamini Mungu. Wao hawakuwaza kwamba Mungu atawahukumu kwa kweli ikiwa hawatatii maneno yake. Kutoamini kulisababisha kifo cha mamilioni ya watu wakati wa Noa kupitia gharika. Noa alikuwa mhubiri wa haki na kwa miaka 120 alikuwa anawaeleza watu kila wakati kwamba kulikuwa na gharika inayokuja na kwamba walihitajika kuwa ndani ya safina wakati huo, lakini watu wa dunia walikataa kuamini mambo hayo yote. Kutoamini kulifanya miji ya Sodoma na Gomora kuangamizwa. Wakati Loti alizungumza na wakwe zake na kuwaeleza kwamba miji itateketezwa walifikiria anawatania na kwa hivyo walikataa kuamini maneno yake (Mwanzo 19:14). Kwa sababu ya kutoamini, wana wa Israeli walizunguka jangwani kwa muda wa miaka 40. Biblia inasema, “Hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutoamini kwao” (Waebrania 3:19). Kwa sababu ya kutoamini taifa la Waisraeli liliangamizwa miaka 50 baada ya Kristo kurudi mbinguni. Wao walikataa kumwamini Yeye na kumkubali Yeye kuwa mwokozi aliyetumwa kutoka kwa Mungu. Badala yake, walimuua kwa kumsulibisha msalabani. Ni kwa sababu ya kutoamini kwa Wayahudi ambako kulifanya Yerusalemu iliangamizwa.

Kutoamini ndiyo sababu kuu ambayo watu wengi ambao wanajiita wakristo hawajaokoka. Sababu kuu kwa nini mamilioni ya watu hawajaokoka na hawaendi mbinguni ni kutoamini. “Asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; yeyote asiyeamini atahukumiwa; yeye asiyemwamini Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yake; Msiponiamini kwamba mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu” (Yohana 3:16; Marko 16:16, Yohana 8:24). Msomaji, popote upo, kumbuka ukweli huu: siyo dhambi inamtuma mtu jahanum bali ni kutoamini. “Kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa; damu yake Yesu, Mwana Wake yatusafisha dhambi yote; Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu zitakuwa nyeupe kama theluji, ingawa ni nyekundu sana kama damu, zitakuwa nyeupe kama sufu” (Mathayo 12:31; 1 Yohana 1:7; Isaya 1:18). Mungu ako tayari kuwakubali wote wanaokuja kwake na kumwamini, lakini wengi wamekataa kumwamini, na kwa hivyo wao wanakataa huruma wa Mungu. Ninaamini kwamba baada ya kumsaliti Bwana Yesu, Yuda Isakariote angetubu na kumwamini Yesu angepata wokovu. Sababu kuu ya watu kukaa ndani ya dhambi zao na mwishowe kuenda jahanum milele inapatikana katika maneno haya ya Yesu Kristo, “Mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima” (Yohana 5:40).

Kutoamini ni ugonjwa wa kiroho ambao unawapata watu wengi leo. Tukitazama kila mahali duniani tunapata kwamba kuna watu wengi sana ambao hawaamini Biblia. Ugonjwa huu wa kiroho uko katika kila nyumba na kila jamii na inaonekana kwamba hakuna njia ya kuuondoa. Huu ni ugonjwa ambao unapatikana kwa matajiri na kwa wale ambao ni maskini. Ni ugonjwa ambao unapatikana katika kila mji, kila kijiji na vijiji. Kila mahali utaenda duniani kote utapata kwamba kuna mtu ambaye hamwamini Yesu Kristo. Kuna watu ambao wanaamini kwamba kwa sababu wao wameelimika sana hawana haja ya kuiamini Biblia: Wao wanaamini kwamba Biblia ni ya watu ambao ni wa kiwango cha chini.

Kuna watu wengine ambao kutoamini kwao kuko katika akili zao. Wao wanakataa kabisa kukubali kwamba Biblia ni neno la Mungu kwa sababu hawawezi kuielewa ama kuieleza. Wao hawaelewi kabisa jinsi Yona angekuwa katika tumbo la samaki kwa siku tatu, ama kuelewa jinsi Bwana Yesu angewaponya wangonjwa na kuwarudishia wafu uhai. Kwao Biblia inaonekana kuwa kitabu ambacho kimejawa na hadithi za kushangaza sana na ambazo siyo za kweli.

Kuna wengi ambao kutoamini kwao kuko katika mioyo yao. Wao wanajua kwamba Biblia ni neno la Mungu, lakini wao wanapenda dhambi zao sana na wameamua kwamba hawataziacha. Wao wanajua kweli kwamba Biblia haikubaliani na desturi za maisha yao kwa hivyo wanakataa kukubali Biblia na mafundisho yake.

Kuna wengine ambao kutoamini kwao kuko katika tamaa yao. Wao wanajua Biblia ni neno la Mungu lakini wao ni wazembe sana kuisoma, kuielewa na kuitii. Wao wanadai kwamba maisha ya ukristo ni magumu sana kufuatwa. Mawazo kuhusu kupigana na dhambi na ulimwengu na kufuata utakatifu ni jambo gumu sana kwao na hawako tayari kulifanya. Kwa hivyo wao wanaendelea na maisha ya kutoamini.

Tusishagae kuwaona watu wasioamini humu duniani. Tusishangae kuwaona jirani wetu ama wenzetu katika sehemu zetu za kazi wakikosa kuiamini Biblia na kuamua kuishi maisha ya dhambi. Hili si jambo geni. Mtume Petro aliandika, “Lazima mfahamu ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbaya” (2 Petro 3:3). Kumbuka kwamba mara mingi mtu anaweza kuonekana kwa nje akiwa hajali kabisa Biblia inasema nini, lakini ndani moyoni mwake inawezakuwa dhamira yake inamsumbua sana kuhusu neno la Mungu.

II. Je, ni kwa nini kutoamini kunashangaza?

Kuna sababu kadhaa kwa nini kutoamini kunashnagaza sana.

1. Kutoamini kunashangaza kwa sababu kunapatikana tu humu duniani na hakuna mahali pengine. Malaika walio mbinguni na wale walianguka na ambao wako jahanum, watakatifu walio mbinguni ambao wanangoja kufufuka na wenye dhambi ambao wameangamia jahanum wakingoja hukumu ya mwisho, wao wote wako na jambo moja sawa: kwamba wanaamini! Katika mfano wa Lazaro na tajiri (Luka 16:19-31), wakati tajiri alienda jahanum, alitaka mandugu zake watano ambao walikuwa duniani na hawakuwa wameamini, waone wafu wakifufuka ili waweze kuamini. Biblia inasema kwamba hata mapepo wanaamini Mungu yupo na wanatetemeka (Yakobo 2:19). Bwana Yesu alipokuwa humu duniani mapepo walisema, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu?” (Mathayo 8:29). Ni hapa tu ulimwenguni ambapo kuna watu ambao hawaamini.

2. Kutoamini kunashangaza kwa sababu ni jambo la majivuno. Mtu ambaye ulimwengu unamtabua kuwa mwerevu, ukweli ni kwamba anajua mambo machache sana. Daktari ambaye anasemekana kuwa mwerevu anajua mambo machache sana kuhusu jinsi mwili wa mwanadamu unafanya kazi. Yeye anajua tu mambo machache hapa na pale lakini yeye hajui hata mwili wake mwenyewe jinsi unafanya kazi! Lakini hata hivyo mamilioni ya watu hapa duniani hawaamini Biblia. Hakuna mtu anajua dunia iliumbwa namna gani, lakini wanakataa kuamini mafundisho ya Biblia kuhusu kuumbwa kwa ardhi na mbingu. Wao kabisa hawajui dhambi ni nini ama jinsi dhambi inaweza kuondolewa, na pia hawaamini Yesu Kristo na kifo chake. Kutoamini ni jambo la kiburi sana.

3. Kutoamini ni jambo la kushangaza kwa sababu ni jambo ambalo silo la haki. Ukiongea na mtu ambaye haamini Biblia, atataja vitu kama safina ya Noa, jinsi wana wa Israeli walivuka bahari, Balamu na punda wake na pia Yona akiwa ndani ya samaki. Mtu huyu atasema, “Mambo haya hayawezekani, na kwa hivyo mimi si amini Biblia.” Lakini mtu huyu amechagua kupuuza yale mambo ambayo yanaonyesha bila shaka yoyote kwamba Biblia ni neno la Mungu. Watu hawa wanachagua kupuuza Bwana Yesu Kristo na kazi yake, pia wanachagua kupuuza miujiza ya Yesu Kristo ambayo inaonyesha wazi Biblia ndiyo neno la Mungu. Watu hawa wanakataa kukubali nguvu za neno la Mungu ambazo zinabadilisha dunia kabisa. Wao wanapuuza kwamba ukristo umekuwa hapa duniani kwa muda wa zaidi ya miaka elfu mbili hata baada ya kupigwa vita kwa muda mrefu. Watu hawa wanapuuza kwamba ukristo ulileta mabadiliko makubwa sana duniani. Haya ni mambo wazi kabisa lakini wale ambao wanakataa kuamini wanayapuuza.

4. Kutoamini ni jambo la kushangaza kwa sababu halimletei mtu faraja ya milele. Watu wengi wako na marafiki wao ambao walikufa wakiwa bado hawajaokoka, na wanajua wazi kwamba ikiwa mtu anakufa akiwa hajamwamini Kristo hatapata faraja. Wao wameona marafiki wao, ama watu wa jamaa zao wakifa bila kuwa na furaha, tumaini ama faraja ya milele. Lakini hata hivyo, hata baada ya kuelewa kwamba kutoamini hakumletei mtu furaha ama faraja yoyote, wao wanaendelea tu kutoamini hata wakati wanakufa. Wao hawamtafuti Mungu hata baada ya kuona marafiki wao na watu wa jamaa zao wakifa bila imani, wao wanaendelea tu katika kutoamini kwao na wanakufa wakiwa katika hali hiyo.

Msomaji, kutoamini ni dhambi kubwa ambayo inaumiza sana. Ni dhambi kubwa sana dhidi ya Mungu wakati tunakataa kuamini neno lake. Yeyote anakataa kuliamini neno la Mungu ataenda jahanum milele. Unapaswa kuuchunga moyo wako dhidi ya dhambi ya kutoamini.

Yesu Kristo ndiye anafaa kuwa kielelezo

cha viongozi wa makanisa

Kila raia, kulingana na umri wake, elimu yake ama dini yake, ana jukumu la kuchangia katika mjadala wa siasa katika nchi yetu. Viongozi wa makanisa wanapaswa kuwa waangalifu sana jinsi wanavyochangia katika mijadala hiyo, kwa sababu wanapochangia, wanamwakilisha vizuri au vibaya kiongozi wa kanisa ambaye ni Yesu Kristo, na ambaye hata wakati alikuwa hapa ulimwenguni aliheshimu serikali ya Warumi ambayo ilikuwa katili sana. Kiongozi wa serikali ya Rumi alimhukumia Yesu Kristo hukumu isiyokuwa ya haki, ili asulibiwe msalabani. Biblia inasema, “Pilato akitaka kuuridhisha ule umati wa watu, akawafungulia Baraba, naye baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulibiwe” (Marko 15:15), lakini hatuoni mahali popote ambapo Yesu Kristo aliongea matamshi ya chuki ama ya kulaani kitendo hicho. Yesu Kristo alikuwa amejawa na mambo ya mbinguni kwamba hata matendo mabaya ambayo alifanyiwa aliyaona kuwa mpango wa Mungu na kwa hivyo kwa neema na unyenyekevu alimweleza Pilato, ambaye alikuwa kiongozi wa serikali ya Rumi na ambaye alifikiria mamlaka yote ya kuamua kile Yesu atafanyiwa yako mikononi mwake kwamba, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu” (Yohana 19:11).

Hii ndiyo inafaa kuwa desturi ya wale wote wanaodai kwamba ni wafuasi wa Yesu Kristo na wanahubiri injili ya wokovu. Viongozi wa makanisa wanafaa kuona serikali jinsi Bwana Yesu alivyoiona serikali ya Rumi. Viongozi wa makanisa hawapaswi kamwe kusema mambo ambayo yataleta chuki na uasi dhidi ya serikali na viongozi wa serikali, na ikiwa watafanya hivyo basi hawatakuwa tofauti na wanasiasa ambao wanalaumiwa kila wakati. Bwana Yesu alisema mambo haya kuonyesha kwamba kazi yake humu duniani haikuwa ya kukomboa taifa la Wayahudi kutoka kwa utumwa wa Warumi bali alikuwa na lengo lingine la juu sana ambalo lilikuwa ni kushughulikia dhambi na madhara yake kwa watu wake kupitia kifo chake msalabani. Yesu alijua kwamba dhambi ndiyo inafanya watu kuwa waasi dhidi ya Mungu na hata dhidi ya serikali za hapa duniani. Hivi ndivyo Bwana Yesu alimwambia Pilato, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu, ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu wafuasi wangu wangenipigania” (Yohana 18:36). Kwa hivyo wafanyi kazi wa Yesu Kristo pia hawapaswi kupigana na serikali ama wafanyi kazi wa serikali.

Kwa hivyo viongozi wa makanisa wanafaa kujua kazi yao ni gani kwa kutazama mfano wa Yesu Kristo. Wao wanafaa kurekebisha madhara ambayo yamefanywa na watu wa nchi yetu kwa kuhubiri toba na msamaa wa dhambi katika Jina la Yesu Kristo (Luka 24:47). Ikiwa viongozi wa makina hawataki kufanya hivi basi inawapasa kuacha huduma na kutafuta kazi nyingine. Ikiwa kiongozi yeyote ana maoni mengine kinyume na haya ambayo nimeeleza hapa anafaa ajue kwamba maoni yake hayatabadilisha kanuni ya neno la Mungu kama linavyodhihirishwa katika Biblia ili tuweze kutii na kufanya.

Waraka wa Paulo kwa Wafilipi

Jinsi kanisa la Filipi lilianza.

Kanisa la Filipi lilianza wakati Paulo, Sila na Timotheo walihubiri injili (Matendo 16:11-14). Hawa watatu, yaani Paulo, Sila na Timotheo walianza safari ya kwenda kuhubiri injili ya Yesu Kristo hadi Filipi mji mkuu wa Makedonia. Walipokuwa katika mji huu, na siku ya sabato ikafika walienda nje ya lango la mji kando ya mto wakitafuta mahali pa kufanyia maombi (mstari 13). Inaoneka kuwa wengi ambao walikuwa wanahudhuria maombi haya kando ya mto walikuwa wanawake. Miongoni mwa wale walioudhuria maombi ni mwanamke aliyeitwa Lidia ambaye alitoka mji wa Thiatira. Wakati Paulo, Sila na Timotheo walihubiri neno la Mungu, Bwana aliufungua moyo wa Lidia na akaamini neno la Mungu na akaokoka, na akabatizwe na wengine wa nyumba yake (mistari 14-15). Baada ya kubatizwa aliwakaribisha nyumbani mwake hawa wahubiri. Walikaa kwake kwa muda wote ambao walikuwa katika mji wa Filipi.

Katika mji huu kulikuwa na mtumwa wa kike ambaye alikuwa akiwafuata Paulo na wenzake kila wakati akipiga kelele na kusema “Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu” (mstari 17). Haya makelele ya huyu mtumwa wa kike yaliudhi Paulo sana na kwa hivyo Paulo alimwamuru yule pepo amtoke huyo mschana, na akamtoka saa ile ile. Jambo hili liliwaletea matata sana Paulo na wenzake kwani walitupwa gerezani. Wakiwa gerezani walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu hadi kukatokea tetemeko kubwa la ardhi likatingisha msingi wa gereza, milango ya gereza ikafunguka na minyororo iliyowafunga wafungwa wote ikafunguka. Tukio hili lilimfanya yule askari wa gereza na jamii yake kumwamini Yesu Kristo baada ya kuhubiriwa neno la Mungu, na wakabatizwa (Matendo 16:31-32).

Kwa hivyo kanisa la Filipi lilianza na jamii mbili, yaani jamii ya Lidia na jamii ya askari wa gereza. Washirika wa kanisa hili hawakumsahau Paulo hata baada ya kuondoka kutoka mji wa Filipi. Waliendelea kuwa na ushirika naye katika injili ya Yesu Kristo (Wapili 1:5). Walishughulikia mahitaji ya Paulo hata kwa kumtumia msaada (Wafilipi 4:16).

Lengo kuu la Paulo la kuliandikia kanisa la Wafilipi.

Tunaweza kuona wazi baadhi ya sababu ambazo zilimfanya Paulo aliandikie kanisa la Wafilipi barua hii.

1. Aliwaandikia ili aeleze upendo wake kwa kanisa lote (1:5,7).

2. Aliandika barua hii ili awaonyesha wakristo jinsi wanapaswa kuwa na furaha katika maisha yao ya ukristo (4:4).

3. Aliwaandikia ili afundishe kanisa umuhimu wa kuwa na umoja.

Ufafanuzi wa Wafipi 1:1-2

Barua hii imeandikiwa watakatifu wote katika Kristo walioko Filipi. Mkristo ni mtu mtakatifu. Hivi ndivyo kila mtu ambaye amemwamini Yesu Kristo anatabulikana. Mtu mtakatifu si mtu ambaye ni msafi zaidi kuliko wakristo wengine. Biblia inawaita wote ambao wamemwamini Yesu Kristo watakatifu; ni watakatifu hapa duniani na pia watakuwa watakatifu mbinguni. Hivi ndivyo wakristo wanaitwa katika barua nyingi. Kwa mfano, Warumi 1:7 hivi ndivyo Paulo anawaandikia wakristo: “Kwa wote walio Rumi wapendwao na Mungu na kuitwa watakatifu.” 1Wakorintho 1:1, Paulo anasema, “Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Kristo Yesu walioitwa kuwa watakatifu.” Waefeso 1:1, Paulo anasema, “Kwa watakatifu walioko Efeso waaminifu katika Kristo Yesu.”

Kuwa mtakatifu imaanisha kutenganishwa na ulimwengu. Katika kitabu cha Walawi 11:44 Mungu aliwaambia Watu wake wawe watakatifu kwa sababu Yeye ni mtakatifu ili waweze kumtumikia Yeye pekee. Hii inamaanisha kwamba maisha yao hapa ulimwenguni ni tofauti kabisa na ya watu wa ulimengu huu ambao hawajaokoka. Kuwa mtakatifu kunamaanisha kuwa safi. Tena katika kitabu cha Walawi 11:44 Mungu anawaambia watu wake wasijitie unajisi. Hii inamaanisha mkristo hapaswi kamwe kuishi katika maisha ya dhambi, badala yake anafaa kuishi maisha ya kumcha Mungu kwa sababu Mungu amemchagua ili amtumikie Yeye.

Yesu Kristo ndiye Bwana wa wakristo wote.

Paulo anaandika barua hii kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu. Hapa Paulo anatuonyesha uhusiano wetu wa ndani sana na Yesu Kristo. Hii inatuonyesha kwamba mkristo ni mali ya Bwana Yesu, baraka za Mungu zote ambazo mkristo anapata zinapitia ndani ya Yesu.

Katika msitari wa 2 Paulo anasema, “Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.” Katika mstari huu tunaona kwamba wokovu wetu ni zawadi kuu kutoka kwa Mungu na kwa hivyo wale wote ambao wameokoka wako na amani na Mungu. Pia tunaona hapa kwamba wokovu wetu unatoka kwa Mungu Baba kupitia kwa Yesu Kristo. Ni wakati mwenye dhambi anakuja kwa Yesu Kristo na kukiri dhambi zake na kumwamini Yeye pekee ndipo anapata wokovu.

Mkristo ni mtumishi wa Bwana Yesu Kristo. Paulo anaanza hii barua yake kwa kujiita yeye na Timotheo watumishi wa Kristo Yesu. Mtu anapookoka anakuwa mtumishi wa Yesu Kristo. Tukumbuke kwamba wale ambao hawajaokoka ni watumishi wa dhambi na dhambi ndiyo bwana wao.

Jukumu la kanisa katika ulimwengu.

Kanisa ambalo Paulo aliliandikia barua hii lilikuwa katika mji wa Filipi. Paulo pia aliandikia makanisa mengine mengi waliokuwa katika sehemu tofauti tofauti za dunia, kama Korintho, Efeso na wengine. Hii inaonyesha kwamba kanisa linamtumikia Kristo hapa ulimwenguni. Kwa hivyo maisha ya mkristo ni maisha ya kumtukuza Mungu, yeye ni mtumishi na mwakilishi wa Kristo hapa duniani. Kwa hivyo wakristo wanapaswa kukumbuka kila wakati kwamba wao wako hapa ulimwenguni lakini wao siyo wa ulimwengu huu. Wanafaa kukumbuka kwamba Bwana Yesu amewaweka duniani ili wamtumikie na wamtukuze kila wakati.

Kitabu cha Hagai

Historia ya Kitabu hiki.

Biblia inatuambia kwamba wakati Mungu aliwaokoa watu wa Israeli kutoka nchi ya Misri, Yeye aliwapeleka katika nchi ya Kanaani, ambayo ilikuwa Nchi ya Ahadi, na kuwawapa nchi hiyo. Lakini hawa watu wa Israeli hawakuwa waaminifu kwa Mungu, bali walianguka katika dhambi ya kuabudu masanamu. Hivyo, walimdharau Mungu ambaye aliwaokoa kutoka kwa utumwa katika nchi ya Misri.

Kwa sababu ya dhambi zao, Mungu aliwahukumu hawa watu wa Israeli. Kwanza, nchi yao iligawanyika ikiwa nchi mbili: nchi ya Israeli na nchi ya Yuda. Halafu, wakati Mungu aliona kwamba hawa watu waliendelea kutenda dhambi, Mungu aliwaondoa kutoka nchi yao. Nchi moja, ambayo iliitwa Asiria, ilikuja na kuwaondoa watu wa nchi ya Israeli, na baadaye, watu wa nchi ya Babeli waliongozwa na Mungu kwa mji wa Yerusalemu. Wao waliangamiza mji huu wote, na pia hekalu ambalo lilikuwa ndani yake na kuwaondoa watu wote wa mji huu. Kwa miaka 70 watu wa Yuda waliishi katika nchi ya Babeli kama wageni. Baada ya miaka 70, mfalme Koreshi aliwaaruhusa watu wa Yuda warudi kwao.

Wakati hawa watu wa Yuda walirudi katika mji wa Yersualemu, hekalu lao lilikuwa limeangamizwa kabisa. Lakini mtu mmoja, Zerubabbeli aliwaongoza waanze kutengeneza hili hekalu. Lakini wakati huo, kulikuwa na watu wa nchi zingine ambao waliishi katika mji wa Yerusalemu. Wao walizuia watu wa Yuda wakati wao walianza kazi ya kutengeneza hekalu na kwa hivyo kazi ya kutengeneza hekalu ilisimamishwa kwa miaka 16 (angalia Ezra sura ya 4). Wakati wa hii miaka 16, watu wa Yuda walisahau jambo la kutengeneza hekalu, na badala yake, walijijengea manyumba mazuri mazuri na kufuata vitu vya dunia.

Wakati huu, Mungu aliwatumia watu wa Yuda nabii Hagai kuwahimiza wasisahau kazi ya kujenga hekalu na badala yake kuishi maisha mazuri. Hagai aliwaambia watu kwamba hata kama watatafuta furaha katika vitu vya dunia, hawataipata kwa sababu wao hawajamaliza kazi ya kujenga hekalu.

Ni nini inapatikana katika kitabu cha Hagai

Kitabu cha Hagai kiko na mahubiri manne ambayo Hagai aliyahubiri katika miezi minne.

Katika mahubiri ya kwanza (Hagai 1:2-11), Mungu anawaambia watu wa Israeli kwamba wao wamesahau hekalu yake, na badala yake, wamejijengea manyumba mazuri mazuri. Hagai aliwaambia kwamba wamesahau kazi ya Mungu na badala yake wanakimbilia fedha za dunia. Hii ndiyo sababu hawakuvuna kulingana na ile walipanda; na pia ingawa walikuwa na vitu vingi vya dunia, hawakupata furaha na kutosheka kutoka kwa vitu hivi.

Mahubiri ya pili ya Hagai (Hagai 2:1-9) yalihubiriwa kwa Zerubbabeli na wale watu wa Israeli ambao walikuwa waaminifu kwa Mungu na ambao walijali hekalu yake. Katika ujumbe huu, Mungu anawahimiza hawa wawe wenye nguvu. Wao walihitaji ujumbe huu kwa sababu wakati waliona lile hekalu ambalo walijenga, waliona kwamba halikuwa zuri kama lile la Solomoni ambalo liliangamizwa na maadui wa Mungu.

Ujumbe wa tatu ya Hagai (Hagai 2:10-19) ulihubiriwa ile siku watu wa Yuda walimaliza kujenga hekalu. Hapa, Hagai anawaambia watu wa Yuda kwamba wanapaswa kuchunga sana tabia ya maisha yao. Anawaambia kwamba ikiwa wao hawatapenda Mungu kwa mioyo yao yote, sadaka zao ambazo watazileta kwa Mungu zitachafua hekalu.

Ujumbe wa nne wa Hagai (Hagai 2:20-23) pia ulihubiriwa ile siku watu wa Yuda walimaliza kujenga hekalu na ulikuwa kwa Zerubbabeli ambaye alikuwa kiongozi wa watu wa Wayahudi. Hagai hapa anasema kwamba Mungu bado ako na mpango wa kuwatumia Wayahudi kumleta Mwokozi wa watu wote duniani.

Ni nini Kitabu cha Hagai kinatufundisha.

Kitabu cha Hagai kinahusu watu wa Israeli wakijenga hekalu, hakihusu watu wa Mungu wakijenga kanisa leo. Mhubiri akihubiri kutoka kitabu hiki kwa kuomba pesa kwa mjengo, hakitumii kitabu hiki vizuri. Kitabu hiki kiliandikwa kutufundisha mambo mawili.

1. Kwanza, kitabu hiki kiliandikwa kuwakumbusha watu wa Mungu kwamba wao wanapaswa kutafuta kwanza Ufalme wa Mungu na si vitu vya dunia. Hekalu la Agano la Kale si mjengo wa kanisa leo, bali ni mafno wa Ufalme wa Mungu, na kama vile watu wa Israeli walisahau kulijenga hekalu, sisi pia tunaweza kusahau mambo ya Ufalme wa Mungu.

2. Pili, kitabu hiki kiliandikwa kutukumbusha kwamba Mungu ni mwenye rehema kwa watu wake kila wakati. Watu wa Yuda walianguka dhambini na waliondolewa kutoka kwa nchi yao. Halafu, hata wakati walirudi, walisahau kazi ya kujenga hekalu kwa miaka mingi. Lakini hata baada ya haya yote Mungu aliwarehemia kwa kuwatumia Hagai kuwahubiria na kuwahimiza.

Jinsi Biblia inavyofafanua mtu ambaye

amebarikiwa na Mungu.

“Kwa hiyo kila mtu mtauwa na akuombe” (Zaburi 32:6).

Katika Zaburi ya 32, Daudi anatueleza kuhusu mtu ambaye amebarikiwa na Mungu. Ulimwengu utatuambia kwamba mtu ambaye ni mrembo na atabasamu, mtu ambaye anaheshimiwa na watu wengi na mtu ambaye ana mali nyingi, ndiyo mtu ambaye amebarikiwa na Mungu. Hivi ndivyo ulimwengu unavyofahamu kubarikiwa na Mungu; urembo, heshima na utajiri. Daudi hasemi, “amebarikiwa yule ambaye ni mrembo na anatabasamu, yule ambaye anaheshimiwa na wengine na yule ambaye ana mali nyingi.” Badala yake Daudi anasema, amebarikiwa yule ambaye, “amesamehewa makosa yake, ambaye dhambi zake zimefunikwa” (Zaburi 32:1). Daudi anasema kwamba mtu ambaye dhambi zake zimesamehewa na Mungu ndiye mtu ambaye amepokea baraka nyingi kutoka kwa Mungu. Wala si mtu ambaye ana mali nyingi au anatabasamu au ni mrembo.

Wakati Agano la Kale linasema kwamba mtu amesamehewa dhambi zake, linamaanisha kwamba dhambi zake zimeondolewa na hazipo tena. Mungu huwa ameziondoa kabisa. Hii ndiyo sababu Yeremia anasema, “Katika siku hizo, wakati huo, asema Bwana, uchunguzi utafanyika kwa ajili ya kosa la Israeli, lakini halitakuwepo” (Yeremia 50:20). Baraka ambazo tunapokea wakati tunasamehewa dhambi zetu ndiyo baraka kuu zaidi mtu yeyote anaweza kupokea. Ninataka kukufundisha mambo matano kuhusu msamaha wa dhambi.

1. Kusamehewa dhambi ni kitendo cha neema kutoka kwa Mungu.

Hatusamehewi kwa sababu tunastahili kusamehewa, tunasamehewa kwa sababu Mungu ni mwenye neema. Mungu anasema, “Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako, kwa ajili yangu mwenyewe, wala sizikumbuki dhambi zako tena” (Isaya 43:25). Huwa Mungu hatusamehe kwa sababu ya matendo mazuri ambayo tumefanya, bali kwa ajili yake, yaani kwa neema yake. Hii ndiyo sababu Paulo anasema kwamba, “Nilipata rehema” (1 Timotheo 1:13). Paulo alikuwa mkufuru, mtesaji na mwenye jeuri. Lakini alipata rehema. Wakati Mungu anamsamehe mtenda dhambi, huwa hamsamehe tu dhambi zake zote, bali pia huwa anamleta mtu huyu katika Ufalme wake na kumpatia urithi.

2. Mungu anapomsamehe mtu, anahakikisha kwamba fidia ya dhambi za mtu huyu inalipwa.

Kwa sababu Mungu ni mwenye haki, lazima ahukumu dhambi. Yeye huwa hapuuzi dhambi, ni lazima aihukumu dhambi hiyo. Wakati Adamu alipokula tunda katika bustani la Edeni, alihukumiwa. Mtu ambaye anatenda dhambi, lazima alipe fidia ya dhambi zake. Mungu anapomsamehe mtu, anahakikisha kwamba fidia ya mtu huyu imelipiwa. Yeye mwenyewe huwa anahakikisha kwamba fidia ya dhambi zetu imelipwa wakati tunakuja Kwake kusamehewa.

3. Msamaha wa dhambi unapatikana kupitia kwa damu ya Kristo Yesu.

Sababu kuu kwa nini Mungu hutusamehe dhambi zetu ni, kwa sababu Mungu ni Mungu wa neema; Mungu hutusamehe kupitia kwa damu ya Kristo Yesu. Biblia inasema kwamba, “Pasipo kumwaga damu, hakuna msamaha wa dhambi” (Waebrania 9:22). Kwa sababu Mungu ni Mungu wa haki, ni lazima dhambi zetu zilipiwe. Bila dhambi zetu kulipiwa, hakuna msamaha wa dhambi kwetu. Ni lazima tuzilipie dhambi zetu au Kristo azilipie. Huwa tunapokea msamaha wa dhambi kwa sababu Kristo Yesu alizilipia dhambi zetu.

4. Tunaweza kupokea msamaha wa dhambi zetu kwa njia moja tu na hiyo ni kutubu.

Katika mafundisho ya Kristo Yesu, toba na msamaha wa dhambi ni mambo mawili ambayo hayawezi kutenganishwa. “Toba na msamaha wa dhambi utatangazwa kupitia Jina Lake” (Luka 24:47). Mungu hatawahi kutusamehe ikiwa hatutatubu na kuondoka kwa dhambi. Mtu ambaye anatubu anaonyesha kwamba kweli amefahamu hatari ya dhambi na jinsi Mungu anavyoichukia sana. Pia atafahamu kwamba msamaha wa dhambi ni jambo la thamani sana kutoka kwa Mungu (Luka 7:38-47).

5. Mungu anapotusamehe dhambi zetu, huwa hazikumbuki tena (Yeremia 31:34).

Mungu huwa haweki rekodi ya dhambi zetu baada ya kutusamehe. Biblia inasema kwamba, “Utazikanyaga dhambi zetu chini ya nyayo zako na kutupa maovu yetu yote katika vilindi vya bahari” (Mika 7:19). Dhambi zetu zinapoondolewa machoni pa Mungu huwa hazionekani tena. Hii ndiyo sababu tunahitaji kumtafuta Mungu kwa uangalifu sana ili atusamehe dhambi zetu. Hii ni baraka kuu sana kutoka kwa Mungu kwetu.

Je, tunajifunza nini kutokana na mafundisho haya?

1. Ni jambo la hatari sana kuishi bila msamaha wa dhambi zako.

Hutawahi kuwa na furaha ya kweli katika maisha yako ikiwa dhambi zako bado ziko juu yako. Kumbuka pia kwamba laana za Mungu zote ziko juu ya mtu ambaye hajaokoka. Biblia inaongezea kwa kusema kwamba, Mungu atalaani baraka za mtu huyu (Malaki 2:2). Hakuna mtu yeyote anaweza kuwa na furaha hapa duniani wakati bado hajaokoka kwa sababu anajua kwamba siku ya hukumu inakuja na atasimama mbele za Kristo Yesu.

2. Ni jambo la baraka sana kuwa na msamaha wa dhambi zako.

Mtu ambaye dhambi zake zimesamehewa huwa haogopi hata wakati shetani anamshitaki kwa sababu anajua kwamba dhambi zake zote zimesamehewa (Warumi 8:33). Pia mtu ambaye amesamehewa ataenda kwa Mungu kwa ujasiri katika maombi. Mtu ambaye hajasamehewa huwa dhambi zake zinamlemea kiwango kwamba hawezi akaomba jinsi anapaswa kuomba. Lakini yule ambaye amesamehewa huwa anamtazama Mungu kwa ujasiri.

Daudi alitenda dhambi kubwa sana dhidi ya Mungu. Lakini hata hivyo alikuwa mtu ambaye alikuwa amebarikiwa sana kwa sabau alikuwa mtu ambaye alikuwa amesamehewa dhambi zake; “ndipo uliponisamehe hatia ya dhambi yangu” (Zaburi 32:5). Daudi alijua kwamba Mungu ni “mwenye kusamehe, mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo” (Nehemia 9:17). Kwa sababu hii aliwahimiza wengi wamtafute Mungu: “Kwa hiyo kila mtu mtauwa na akuombe” (Zaburi 32:6).