Header

“Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, hamtatumia tena mithali hii katika Israeli. Kwa kuwa kila roho ni mali Yangu, kama vile ilivyo roho ya baba, vivyo hivyo roho ya mtoto ni mali Yangu. Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa” (Ezekieli 18:3-4).

Wayahudi siku za Ezekieli walikataa kuajibika kwa ajili ya dhambi ambazo walikuwa wametenda. Walisema, “Baba wamekula zabibu zenye chachu, nayo meno ya watoto yametiwa ganzi” (Ezekieli 18:2). Kwa kusema hivi walimaanisha kwamba, “tunaadhibiwa kwa sababu ya dhambi za baba zetu. Ni baba zetu ambao walianguka katika dhambi na sasa Mungu anatuadhibu sisi, ilhali sisi wenyewe hatujafanya dhambi yoyote.” Hivi ndivyo walikuwa wakisema. Lakini katika Ezekieli 18:4, Mungu anawaambia kwamba, “Nafsi itendayo dhambi ndiyo itakayokufa.” Mungu alikuwa akimaanisha kwamba, “Mtu ambaye anatenda dhambi ndiye atahukumiwa; ikiwa mtu anahukumiwa, basi ni kwa sababu ya dhambi zake.” Hivi ndivyo Mungu alikuwa akisema na watu wa Israeli.

Tunasoma mambo matatu kutokana na mstari huu.

1. Kila mwanadamu ni kiumbe cha Mungu: “Kwa kuwa kila roho ni Yangu, kama vile roho ya baba, vivyo hivyo roho ya mtoto ni mali yangu.”

Biblia ni wazi kwamba sisi wanadamu hatujapatikana hapa ulimwenguni kwa bahati au kwa sababu jambo fulani lilitendeka ndipo tukawa hapa. Hatujatoka kwa kiumbe fulani ambacho kimekuwa kikibadili maumbile kwa miaka fulani. Katika Mwanzo sura za 1 na 2, Biblia inatueleza kwamba tumeumbwa na Mungu na tumeumbwa katika mfano wa Mungu mwenyewe: “Kwa hivyo Mungu alimwumba mtu kwa mfano wake mwenyewe, kwa mfano wa Mungu aliwaumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba” (Mwanzo 1:26-27). Neno aliwaumba au alimwumba limerudiwa kusisitiza kwamba, mwanamume na mwanamke, wote wawili wameumbwa na Mungu.

Baba na mwanawe wa kiume, mama na mwanawe wa kike, mzee na kijana, mzungu na mwafrika, tajiri na maskini, aliyesoma sana na yule ambaye hajasoma; wote ni viumbe vya Mungu na kwa asili wote ni sawa machoni pa Mungu. Mungu huwa hana ubaguzi miongoni mwa viumbe vyake na hapendelei wengine na kuwachukiwa wengine kiasili. Wewe na mimi, ni viumbe vya Mungu ambavyo vimeumbwa naye kwa mikono Yake na kwa nguvu Zake kutoka kwa udongo ule ule. Wanadamu wote ni mali vya Mungu aliye hai. Sisi ni viumbe vyake na Mungu anaweza kufanya nasi jinsi anavyotaka.

2. Kila mwanadamu ana jukumu la kutekeleza mbele za Mungu: “Kwa kuwa kila roho ni Yangu, kama vile roho ya baba, vivyo hivyo ya mtoto ni mali yangu.”

Tumeona kwamba tumeumbwa na Mungu na kwa mfano Wake, alituumba. Swali ambalo kila mmoja wetu anafaa kujiuliza ni, “Kwa nini Mungu aliniumba?” Hili ni swali ambalo kila mmoja wetu anafaa kujiuliza: “Kwa nini niko hapa? Je, kwa nini Mungu alichukua wakati akaniumba? Je, jukumu langu kama kiumbe cha Mungu ni gani?”

Biblia inatupatia jibu kwa swali hili. “Ye yote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Ye yote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile apewazo na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una Yeye milele na milele. Amen” (1 Petro 4:11). Mungu alituumba ili tuweze kumletea utukufu katika kila jambo. Alituumba kwa ajili ya utukufu Wake. Alituumba ili kwa kila jambo, Yeye pekee atukuzwe na si mwanadamu au kiumbe kingine chochote.

Je, hii inamaanisha nini kwako? Inamaanisha kwamba Mungu anakutarajia uishi maisha yako kwa ajili Yake. Katika kila jambo ambalo unalifanya, Mungu ndiye anachukua nafasi ya kwanza. Swali lingine ni, je, mwanadamu anaweza kutimiza haya kwa njia gani? Njia ambayo tunafaa kutumia ili tutimize haya ni, kupitia kwa “Yesu Kristo.” Bwana Yesu Kristo mwenyewe alizungumza kuhusu kutekeleza mapenzi ya Mungu. Mapenzi ya Mungu hutekelezwa kwa Yeye kutukuzwa kupitia kwa Kristo Yesu. Wakati Moja Yesu aliulizwa na Wayahudi; “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu? Yesu akawajibu, Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini Yeye aliyetumwa Naye” (Yohana 6:28-29).

Kile Yesu Kristo alimaanisha ni kwamba, ikiwa mtu yeyote anataka kumfurahisha Mungu au kutii Mungu, lazima awe na imani ndani ya Kristo Yesu. Hili ndilo jukumu ambalo kila mmoja wetu analo mbele za Mungu. Ni jukumu letu kumwamini Mwana wa Mungu ambaye Mungu mwenyewe alimtuma aje hapa ulimwenguni afe msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Hii inamaanisha kwamba, mwanamume yeyote au mwanamke yeyote ambaye hamwamini Kristo Yesu, hawezi akamfurahisha Mungu au kumtii Mungu hata afanye nini. Mungu hukubali tu yale majukumu ambayo tumetekeleza kwake kupitia kwa Kristo Yesu pekee.

Je, unayo imani ndani ya Mwana wa Mungu? Je, umeamini katika kifo cha Kristo Yesu msalabani kwamba ndiyo njia ya pekee ya kupata msamaha wa dhambi zako? Ikiwa hujafanya hivi, basi wewe hujamtii Mungu na kwa kufanya hivi, wewe hutekelezi majukumu yako kwa Mungu jinsi Mungu anavyotaka uyatekeleze. Mwisho wako wewe ni jahanum na hakuna mtu yeyote ambaye atakuokoa. Hii ndiyo fursa yako, usiangalie nyuma, wewe mwamini tu Kristo Yesu na utakuwa umetekeleza majukumu yako kwa Mungu. Utafanyika mwana wa Mungu na mbinguni patakuwa nyumbani kwako milele. “Wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu” (Yohana 1:12).

3. Kila mwanadamu anao waajibu mbele za Mungu kwa sababu ya dhambi zake: “Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa.

Huu ni ukweli ambao kila mtu anafaa kufahamu vyema kabisa: sisi tunao waajibu mbele za Mungu kwa sababu sisi sote ni watenda dhambi. Hii ndiyo sababu wale wote ambao hawatatubu dhambi zao watatupwa jahanum. Hili ndilo fundisho langu la mwisho katika kijitabu hiki kwa sababu ninataka ufahamu hali yako kamili machoni pa Mungu na pia ni kwa sababu sitaki udanganywe. Ikiwa hujaokoka, Mungu atakutupa jahanum na hakuna mtu ambaye atalaumiwa kwa ajili ya dhambi isipokuwa wewe wenyewe.

Sisi sote tumezaliwa tukiwa watenda dhambi na waasi dhidi ya Mungu (Zaburi 58:3). Mungu katika neno Lake amesema kwamba, “Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa” (Ezekieli 18:4). Kila mmoja wetu anao waajibu mbele za Mungu kwa ajili ya dhambi zake. Kwa sababu hii, wale wote ambao wanakataa kutubu, watapatana na kifo cha pili ambacho ni kutupwa kwa moto wa jahanum.

Ninajua kwamba kuna wengi nchini mwetu na ulimwenguni kote ambao wanapenda sana kutoa vijisababu vingi kwa ajili ya dhambi zao. Wanapenda sana kuwalaumu watu wengine kwa zile dhambi ambazo wanafanya. Wanasahau kwamba kila mmoja wetu analo jukumu mbele za Mungu na kwamba kama hatutatimiza majukumu yetu, tutahukumiwa jahanum. Kwa mfano, mtu anaiba pesa halafu anasema kwamba alifanya hivyo kwa sababu ana shida fulani fulani katika maisha yake. Mwingine anasema uongo, halafu anasema ni kwa sababu bosi wake kazini alimwambia aseme hivyo. Mwanamume au mwanamke anafanya uasherati halafu anasema kwamba mume au mke wangu si mwaminifu kwangu au ni mwili wangu ambao umeniongoza kwa hayo. Mtu mwingine ambaye hataki kuokoka, atakueleza kwamba, kwa jamii yetu yote hakuna mtu ambaye ameokoka. Kila wakati ni vijisababu na masingizio; “katika jamii yetu sisi ni walevi, waganga, wachawi, makahaba. Baba yangu anafanya hivi au alikuwa hivi na ndiyo sababu niko hivi.” Mungu hatasikiliza haya, ustasimama mbele za Mungu na swali ambalo Mungu takuuliza halitakuwa, “Je, ni nani aliyekufunza kufanya dhambi; je, ulijifunzia wapi dhambi?” Swali la Mungu kwako litakuwa, “Je, ulimwamini Yule ambaye nilimtuma (yaani Kristo)?” (Yohana 6:29).

Wewe ambaye hajaokoka, usidanganywe. Biblia inasema, kaburi inakungoja kukutana nawe (Isaya 14:9). Unahitaji kufanya jambo kwa haraka sana. Sahau yaliyopita na usiwajali watu watasema nini. Njoo kwa Kristo Yesu jinsi ulivyo. Kristo Yesu anakualika uje Kwake leo; “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28). Kristo pia anakuhakikishia kwamba atakulaki na hatakukataa: “Ye yote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe” (Yohana 6:37).

Je, kwa nini ungoje ilhali upanga wa Mungu utakutana nao peke yako? Kimbilia maisha yako sasa, njoo kwa Kristo ili akuokoe.

Kwa wale wote wameokoka, sifa kwa Mungu kupitia kwa Kristo Yesu kwa sababu dhambi zetu haziko juu yetu tena. Zimeondolewa kutoka kwetu na Kristo Yesu. Mungu ametusamehe na sasa sisi ni watoto wake na warithi wa Ufalme Wake. Tusikubali mafundisho ambayo yanatueleza kwamba tutapoteza wokovu wetu ambao tulinunuliwa na Kristo Yesu. Sasa sisi tuko katika Ufalme wa Mungu na tutakuwa humo milele na milele. “Haya ndiyo mapenzi yake Yeye aliyenituma, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho” (Yohana 6:39).