Header

“Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa, kila siku. Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’ Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. Zaidi ya hayo kati yetu na ninyi huko, kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu ye yote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’ Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso. Abrahamu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Mose na Manabii, wawasikilize hao.’ Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Abrahamu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’ Abrahamu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Mose na manabii, hawataweza kushawishiwa hata kama atafufuka mtu kutoka kwa wafu’” (Luka 16:19-31).

Katika kifungu hiki tunasoma mfano wa tajiri na Lazaro. Ni hapa tu pekee ambapo tunasoma ni nini wale ambao hawajaokoka wanahisi baada ya kufa, hakuna kifungu kingine katika Biblia ambacho kinatufundisha ni nini watu hawa wanahisi baada ya kuacha dunia hii. Ni hapa peke yake tunalisoma jambo hili, na kwa sababu hii, ni lazima tuangazie kifungu hiki kwa hekima sana.

1. Kwanza, tunajifunza kwamba jinsi mtu anaonekana hapa ulimwenguni haimaanishi hivyo ndivyo anaonekana mbele ya Mungu.

Katika kifungu hiki Yesu Kristo anatuambia kuhusu watu wawili, mmoja alikuwa tajiri sana, na mwingine maskini kabisa. Mmoja “aliishi kwa anasa” na mwingine alikuwa anaombaomba kwa sababu alikuwa maskini. Lakini kwa hawa wawili, yule maskini alikuwa na neema kutoka kwa Mungu, na yule tajiri hakuwa na neema yake Mungu. Maskini aliishi maisha yake kwa kumwamini Mungu katika kila kitu, alitembea katika nyayo za Abrahamu ambaye alikuwa mtu wa imani. Tajiri naye hakuwaza mambo ya kuokoka, na kwa hivyo alikuwa amekufa katika makosa na dhambi.

Haya yote yanatufundisha kwamba hatuwezi kuhesabu thamani ya mtu kulingana na utajiri yake. Yanatufundisha kwamba mtu anaweza kuwa tajiri sana lakini hii haimaanishi kwamba yeye kweli ni mtu wa thamani mbele za Mungu. Biblia inatufundisha kwamba watu wa Mungu ni wale ambao hawana thamani hapa ulimwenguni: “Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi waliozaliwa katika jamaa zenye vyeo” (1 Wakorintho 1:26). Pia Mungu anasema, “Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake au mwenye nguvu asijisifu katika nguvu zake au tajiri asijisifu katika utajiri wake, lakini yeye ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii: kwamba ananifahamu na kunijua mimi” (Yeremia 9:23-24). Mtu anaweza kuwa tajiri, lakini hii haimaanishi kwamba hakika Mungu amembariki, na mtu anaweza kuwa maskini kabisa, lakini hii haimaanishi kwamba Mungu amemlaani. Wale ambao Mungu anawaokoa mara mingi hawana vitu vingi vya dunia. Lazima sisi tuwaze kuhusu watu kama vile Mungu anavyowazia. Hatufai kuwathamini wale ambao ni tajiri, bali wale ambao wamepata neema kutoka kwa Mungu.

2. Pili, tujifunze kwamba tajiri na maskini wote siku moja watakufa.

Tunasoma katika kifungu hiki, “Wakati ukafika yule maskini akafa, yule tajiri naye akafa na akazikwa” (mstari 22). Biblia inatufundisha wazi kwamba wale ambao ni matajari sana na wako na vitu vingi vya dunia hii siku moja watakufa, na wale ambao ni maskini kabisa na hawana chochote cha dunia hii pia watakufa: “Wote huenda mahali panapofanana” (Mhubiri 3:20). Sisi sote tunajua kwamba siku moja tutakufa lakini wengi hawataki kuwaza juu ya kifo. Kuna wengi ambao wanaishi maisha yao hapa ulimwenguni kana kwamba wataishi hapa milele! Wao hawataki kuwaza juu ya kifo na hawataki kukubali kwamba siku moja watakufa. Wanataka kuwaza tu juu ya maisha, si kifo. Lakini yule ambaye ameokoka anapaswa kuwaza juu ya kifo. Mtu akiwa maskini sana na hana vitu vingi vya dunia anapaswa kukumbuka kwamba siku moja sisi sote tutaacha dunia hii. Katika kifungu hiki maskini alikufa na hakuwa maskini tena, na tajiri alikufa na hakuwa na utajiri wake tena.

3. Tatu, tujifunze kwamba nafsi ya yule ambaye ameokoka inachungwa sana na Mungu wakati wa kifo.

Yesu Kristo alisema, “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu” (mstari 22). Hapa wale ambao wameokoka wanapata faraja nyingi. Mstari huu unatufundisha kwamba wale ambao wameokoka, Yesu Kristo mwenyewe atawachunga ile dakika wanakufa. Ni yeye mwenyewe atawapeleka kwake, na wao watakuwa pamoja na wengine ambao wameokoka hadi ile siku miili yao itafufuliwa. Sisi hatujui mengi kuhusu wale ambao wamekufa lakini kitu kimoja tunajua, wao wako pamoja na Kristo (Wafilipi 1:23).

4. Nne, tunajifunza hapa kwamba kuna hukumu ya milele jahanum.

Yesu Kristo anatuambia wazi kwamba huyu tajiri alienda jahanum na huko aliteseka sana na maumivu makuu kwenye moto. Tunasoma kwamba alimwomba Abrahamu, “Nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu” (mstari 24). Lakini yeye aliambiwa na Abrahamu, “Kati yetu na ninyi huko, kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu ye yote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu” (mstari 26). Haya ni mafundisho ya Yesu Kristo mwenyewe, si mawazo ya mwanadamu. Ni lazima sisi sote tukumbuke kwamba kuna mahali ambapo panaitwa jahanum, na wale ambao hawajaokoka wataenda huko milele. Shetani anawadanganya wengi kwamba hakuna mahali kama hapo, vile alimdanganya Hawa, “Hakika hamtakufa.” Sisi tusidanganywe naye. Kuna jahanum kwa wale ambao hawajaokoka, kama tu vile kuna mbinguni kwa wale ambao wameokoka. Biblia inasema kumhusu Mungu, “Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu” (2 Wathesalonike 1:8). Yule ambaye anataka kuepuka jahanum lazima amkimbilie Yesu Kristo kwa kutubu dhambi zake na kwa imani. Mtu akienda jahanum mwishowe, si kwa sababu Mungu alikataa kumwokoa, bali kwa sababu alikataa kuja kwake Yesu.

5. Tano, tujifunze kwamba wale ambao hawajaokoka wanafahamu thamani ya nafsi yao baada ya kufa.

Tunasoma kwamba wakati huyu tajiri alikuwa duniani hakujali mambo ya nafsi yake, alijali tu mambo ya dunia hii, kama chakula na nguo na nyumba. Lakini baada ya kufa, alifahamu kwamba nafsi ya mtu ni ya thamani sana kuliko mambo ya dunia. Kwa hivyo alimwomba Abrahamu, “Nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso” (mstari 27-28). Baada ya kufa alifahamu kwamba wale ambao hawajaokoka kweli watapata mateso mengi jahanum na mateso haya yatakuwa ya milele. Kwa hivyo alitaka kuwaonya ndugu zake watano. Kuna wengi kama mtu huyu ulimwenguni leo. Wao wanapenda sana vitu vya dunia na wanavifuata. Wanaishi maisha ya dhambi sana, wanadanganya wengine na wanafanya mambo mengi mabaya mabaya kupata vitu vya dunia. Wanajua kwamba siku moja Yesu Kristo atawahukumu watu wote wa ulimwengu, lakini hawafahamu sana thamani ya nafsi. Lakini siku moja wataingia jahanum na wataelewa vizuri thamani ya nafsi zao, na siku ile watalia. Siku ile watatamani kutubu na kumwamini Yesu Kristo, lakini hawataweza, saa ya kuokoka itakuwa imekwisha.

6. Sita, tunajifunza kwamba hata kama watu wataona miujiza mikubwa mikubwa hapa ulimwenguni, bado hawataokoka.

Tajiri huyu alitaka mtu atumwe kwake kuwaonya mandugu zake watano kuhusu mateso ya wale ambao hawajaokoka. Alisema, “Mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.” Lakini Abrahamu alimjibu, “Kama wasipowasikiliza Musa na manabii, hawataweza kushawishiwa hata kama atafufuka mtu kutoka kwa wafu” (mstari 31). Kuna funzo kubwa sana hapa kwetu ambalo ni tunahitaji tu neno la Mungu lihubiriwe tukitaka watu waokoke. Mtu akifufuka na kutoka kaburi, watu bado hawatamwamini Yesu Kristo na kuokoka. Wale ambao hawajaokoka wamebaki katika dhambi zao kwa sababu wanapenda dhambi zao na wanapenda vitu vya dunia, si kwa sababu hawajaona miujiza mingi. Wao wanaweza kuona miujiza mingi sana, lakini hawataokoka. Pia, wale ambao wamekufa, wakirudi hapa ulimwenguni, hakuna mamo zaidi ya neno la Mungu ambayo wanaweza kutuambia. Watasema tu kwamba njia ya kuokoka ni kutubu na kumwamini Yesu Kristo peke yake, na mtu akikataa kufanya hivi basi ataenda jahanum milele. Na haya yote sisi tayari tunajua kutoka kwa Biblia!