Utangulizi
Kijitabu hiki kinahusu maisha ya ukristo. Lengo la kijitabu hiki ni kueleza ni nini Biblia inafundisha kuhusu maisha ya ukristo na jinsi tunapaswa kuishi. Kuna mambo mawili ambayo tunapaswa kujua kuhusu maisha ya ukristo.
1. Kwanza, Biblia inaeleza wazi kwamba ijapokuwa watu wengi husema kwamba wameokoka, ni wale tu ambao wanaishi maisha ya ukristo kila siku ndiyo wameokoka na hao ndiyo wataingia mbinguni. Hivi ndivyo Biblia inasema kuhusu jambo hili.
“Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu” (1 Yohana 3:9).
“Wapenzi na tupendane, kwa kuwa upendo watoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu naye anamjua Mungu” (1 Yohana 4:7).
“Kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Huku ndiko kuushinda kuushindako ulimwengu, yaani, hiyo imani yetu” (1 Yohana 5:4).
“Tunajua ya kuwa yeye aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, bali aliyezaliwa na Mungu hujilinda wala yule mwovu hawezi kumdhuru” (1 Yohana 5:18).
Mistari hii inaonyesha wazi kwamba ikiwa mtu ameokoka, basi mtu huyo ataishi maisha ya ukristo na hilo litakuwa dhihirisho kwamba yeye ameokoka.
2. Pili, Biblia inafundisha kwamba maisha ya ukristo ni yale ambayo tunajifunza zaidi na zaidi kumhusu Yesu Kristo. Na jinsi tunavyoendelea kujifunza kumhusu Kristo, ndivyo tunavyoendelea kuwa kama Yeye. Biblia inasema, “Nasi sote, tukiwa na nyuso zisizotiwa utaji tunaakisi utukufu wa Bwana, kama kwenye kioo. Nasi tunabadilishwa ili tufanane naye, toka utukufu hadi utukufu zaidi, utokao kwa Bwana, ambaye ndiye Roho” (2 Wakorintho 3:18).
Katika kifungu hiki, Paulo anasema tunapowaza kuhusu utukufu wa Bwana Yesu Kristo zaidi na zaidi, tunaendelea kubadilika na kuwa kama Yeye. Maisha ya ukristo yanaweza kueleweka kwa ufupi kama: “Kuishi maisha ya kusoma Bwana Yesu Kristo zaidi na zaidi na kumfikiria Yeye zaidi na zaidi, na kuwa kama Yeye zaidi na zaidi hadi wakati ule tutakamilika.” Lengo kuu la maisha ya ukristo ni kukamilika kabisa kama Kristo. Hili ndilo lengo letu sisi, na ndilo tunapaswa kutamani.
Funzo la Kwanza, Wagalatia 5:16-
Kifungu hiki ni mojawapo ya vifungu muhimu sana katika Biblia kuhusu maisha ya ukristo. Kuna watu wengi humu nchini mwetu ambao wameokoka kwa neema ya Mungu na wanataka kuishi maisha ya kumpendeza Mungu, lakini hawajui jinsi wanaweza kuishi maisha ya ukristo. Katika kifungu hiki tunayo mafundisho ambayo yatatusaidia kuhusu jambo hili.
1. Tunahitaji kuelewa kwamba kuna vita vinavyoendelea ndani mwetu wakati tunaokoka.
Paulo anaandika katika kifungu hiki, “Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, nayo Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka” (mstari 17). Mstari huu unatueleza kwamba kila mtu ambaye ameokoka, ndani yake ako na dhambi ambazo zimebaki, na pia ako na Roho Mtakatifu akiishi ndani yake. Kabla ya kuokoka mtu huyu alikuwa mtumwa wa dhambi na dhambi ilitawala maisha yake yote. Kila kitu ambacho alifanya kilikuwa dhambi kwa sababu yeye aliongozwa na kutawaliwa na dhambi.
Lakini
mtu anapookoka huwa haongozwi na kutawaliwa na dhambi kwa sababu yeye
sasa ni mtu wa Mungu. Biblia inasema, “Lakini Mungu ashukuriwe
kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii
kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa, nanyi mkiisha kuwekwa huru
mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki” (Warumi 6:17-
Kwa mfano, kuna kiongozi ambaye ni mkatili na ambaye anatawala watu kwa mabavu akitumia jeshi lake. Kiongozi huyu ako na wafanyakazi wake kila mahali na watu wote wanaishi kwa uoga kwa sababu ni lazima wamtii la sivyo watauawa. Siku moja utawala wake unapinduliwa na kiongozi mpya anachukua uongozi. Huyu kiongozi mkatili angali ako na wafuasi wake kila mahali nchini na wataendelea kuwashawishi watu wawe waasi dhidi ya kiongozi huyu mpya na wamtii kiongozi wao wa zamani. Wanaendelea kuwashawishi watu kwamba, ikiwa watamkataa kiongozi huyu mpya na kumfuata yule wa zamani watapata faida kubwa sana kama kazi mzuri na pesa mingi. Hali hii inaleta wasiwasi mwingi katika nchi kwa sababu watu wako na kiongozi mpya lakini yule alikuwa anaowaongoza zamani angali anawasihi wamfuate.
Hivi ndivyo ilivyo kwa mtu ambaye ameokoka. Dhambi haitawali maisha ya mkristo lakini dhambi ambayo imebaki ndani yake inaendelea kumshawishi ili aishi maisha ya dhambi. Hivi ndivyo vita vilivyo ndani ya kila mtu na ni vita ambavyo vinaendelea katika maisha ya wakristo wote hapa duniani. Vita hivi vitaisha tu wakati mkristo anaondoka hapa duniani.
2. Tunapaswa kuenenda kwa Roho Mtakatifu katika maisha yetu ya ukristo.
Paulo anasema katika kifungu hiki, “Kwa hivyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtatimiza kamwe tamaa za mwili.....Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria....basi tuenende kwa Roho” (mistari 16, 18, 25). Maneno haya, kuenenda kwa Roho, kuongozwa na Roho, na kuenenda katika Roho, yote yanamaanisha kitu kimoja. Yanamaanisha kuishi maisha ambayo yanaongozwa na Roho Mtakatifu ambaye anaishi ndani yetu. Roho Mtakatifu huanza kuishi ndani ya mtu wakati mtu huyo anaokoka na anamwongoza ili aweze kuishi maisha matakatifu. Hivi ndivyo Mungu amewaahidi watu wake, “Nami nitaweka Roho yangu ndani yenu na kuwafanya ninyi mfuate amri zangu na kuwafanya kuwa waangalifu kuzishika sheria zangu” (Ezekieli 36:27).
Je,
ni namna gani Roho Mtakatifu anamwongoza mkristo kuishi maisha
matakatifu? Jibu la swali hili linapatikana katika kitabu cha
Wafilipi 2:12-
(i) Roho Mtakatifu ndiye anampa mtu hamu ya kuishi maisha matakatifu: “Kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu.” Kabla hatujaokoka tulikuwa watumwa wa dhambi na kwa hivyo tamaa zetu zilikuwa ni tamaa za dhambi. Mtu ambaye hajaokoka, nia yake kuu ni kutafuta anasa na mali za dunia hii. Yeye hatamani Mungu kamwe, bali anatamani dhambi kila wakati. Lakini mtu ambaye ameokoka anatamani mambo ya Mungu, Yeye hashughuliki na mambo ya anasa na mali za dunia hii bali anatamani kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu.
(ii) Roho Mtakatifu ndiye anampa mtu ambaye ameokoa nguvu za kuishi maisha matakatifu: “Kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.” Mtu ambaye hajaokoka hana nguvu ya kuishi maisha ya kumpendeza Mungu kwa sababu yeye ni mtumwa wa dhambi. Nyakati fulani anaweza kutamani kuziacha dhambi zake halafu aanze kuishi maisha mazuri kwa sababu dhambi zinasumbua dhamira yake. Anaweza kuacha dhambi fulani na kuanza kuishi maisha mazuri kwa muda, lakini baadaye atarudi tena katika dhambi zake kwa sababu yeye ni mtumwa wa dhambi.
Lakini mtu ambaye ameokoka amepewa nguvu na Roho Mtakatifu ili aweze kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Mtu ambaye ameokoka si mtumwa wa dhambi tena, bali amewekwa huru ili amtumikie Mungu na amepewa hamu ya kutamani mambo ya Mungu. Chochote ambacho anahitaji ili aishi maisha matakatifu hapa ulimwengu, Roho Mtakatifu amempatia: “Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima uchaji wa Mungu” (2 Petro 1:3).
Ni muhimu sana kujua kwamba katika mistari hii Mungu ametupatia jukumu la kuishi maisha matakatifu. Amri za Mungu kutoka vifungu hivi ni wazi kabisa: kwamba ni jukumu letu kuishi tukiongozwa na Roho Mtakatifu kuutimiza wokovu wetu kwa kuogopa na kutetemeka. Roho Mtakatifu hatubebi na kutupeleka mbinguni kama vile mama anambeba mtoto mdogo, bali Yeye anatarajia sisi tutatembea katika njia ya utakatifu, yaani tutatii neno la Mungu na tutapigana na dhambi. Mungu anatupatia nguvu za kuishi maisha matakatifu na pia anatupatia tamaa ya kuishi maisha matakatifu, sasa ni jukumu letu kuishi maisha matakatifu.
3. Tukiishi maisha ya kuongozwa na Roho Mtakatifu tunazaa tunda la Roho Mtakatifu.
Katika
kifungu hiki Mtume Paulo anaongea kuhusu matendo ya mtu ambaye
hajaokoka na pia anafundisha kuhusu tunda la Roho Mtakatifu (mistari 19-
(i) Paulo anaongea kuhusu “tunda” la Roho. Tunda la Roho linaweza kulinganishwa na tunda la chungwa, yaani ni tunda moja lakini limegawanywa sehemu tisa. Ni muhimu sana kujua jambo hili kwa sababu kuna watu ambao hawajaokoka lakini wako na baadhi ya sehemu za tunda hili. Lakini tunapaswa kujua ni wale tu ambao wameokoka ndiyo wako na hizi sehemu tisa za tunda la Roho Mtakatifu zote. Kuna watu ambao hawajaokoka na wako na upendo, amani na uvumilivu lakini hawana hizi sehemu tisa za tunda la Roho Mtakatifu.
Pia kwa wale ambao wameokoka, tunda la Roho kwao huwa linakua na kuiva kila wakati. Mtu ambaye ameokoka ataendelea kuwa na upendo zaidi, kuwa na furaha zaidi, kuwa na amani na uvumilivu zaidi anapoendelea katika maisha yake ya ukristo. Mtu ambaye hajaokoka anaweza kuwa na upendo, uvumilivu na rehema lakini hataendelea kukua zaidi katika upendo, uvumilivu ama rehema anapoendelea na maisha yake kwa sababu Roho wa Mungu hafanyi kazi ndani yake.
(ii) Tunda la Roho linahusu sana tabia ya mtu kuliko matendo yake. Wakati Roho Mtakatifu anakuja kuishi ndani ya mtu, anaanza kumgeuza mtu tabia yake ili aendelee na kufanana na Yesu Kristo. Mtu huyu anakuwa mtu wa upendo zaidi, mtu wa furaha zaidi, mtu wa uvumilivu na amani zaidi na pia anakuwa mtu mwenye huruma zaidi. Tabia yake inabadilika kabisa hadi mambo haya yanayohusu tunda la Roho Mtakatifu yataonekana ndani yake kila wakati. Mtu ambaye hajaokoka anajijali yeye mwenyewe lakini anaweza kuonyesha huruma nyakati zingine. Anaweza kuona mwanamke akiomba pesa mtaani akiwa na mtoto wake na anaweza kumhurumia na kumsaidia na pesa, lakini hii haimaanishi kwamba tabia yake imebadilika sasa. Yeye bado ni mtu anayejijali ijapokuwa ametenda kitendo cha huruma.
Ni
jambo muhimu kufahamu kwamba siku ya hukumu wale ambao hawajaokoka
wataongea kuhusu kazi zao, lakini Bwana Yesu ataangalia tabia zao.
Katika kitabu cha Mathayo 7:22-
Angalia kwa makini ni nini inatendeka hapa. Watu hawa watasimama mbele ya Yesu siku ya hukumu na kuongea kuhusu matendo yao makubwa waliofanya. Wataeleza jinsi walitoa mapepo na vile walifanya miujiza mingi. Lakini Bwana Yesu atasema, “Sikuwajua kamwe.” Hapa Yesu anawaambia kwamba, “Ninajua kwamba mnadai kuwa mlifanya kazi kubwa sana ya ufalme wa Mungu, lakini ninaangalia sana tabia yenu zaidi kuliko kazi yenu, na ninapoangalia tabia yenu, Mimi sijioni ndani yenu, Sioni tabia ambayo inaambatana na tabia yangu kamwe, yaani tabia inayompendeza Mungu, kwa hivyo, ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!”
Hili ni jambo muhimu sana kwetu sisi sote, hasahasa wale ambao ni wachungaji na wahubiri. Mara mingi tunafikiria kwamba Mungu anashughulika tu na kazi ya ufalme ambayo tunafanya na kwamba tabia yetu haijalishi sana. Mara mingi tunafikiria kwamba tukifanya kazi ya Mungu kwa bidii sana na kuwa waaminifu sana katika kufanya kazi hiyo, basi Mungu anapendezwa sana nasi na hatajali tabia zetu. Lakini hii si kweli. Kazi ya Roho Mtakatifu ndani ya kila mtu ambaye ameokoka ni kumgeuza mtu ili afanane na Yesu Kristo, yaani kumgeuza tabia yake kabisa. Ni kweli Mungu anapenda kazi tunayofanya katika ufalme wake lakini anajali zaidi tabia ya mtu. Mungu anafurahia sana tunapoendelea kugeuzwa zaidi na zaidi ili tufanane na Kristo Yesu, ili tubadilike kabisa tabia yetu na tuweze kufanya matendo mazuri ya kumtukuza.
Somo la Pili, Waefeso 4:1-
Ukristo Katika Kanisa.
Katika,
kitabu cha Waefeso sura ya 4 hadi ya 6, Paulo anapeana mwongozo wa
jinsi tunapaswa kuishi maisha ya ukristo. Anasema, “Ninawasihi
mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa” (mstari 1), halafu
anaeleza mafundisho fulani jinsi jambo hili linapaswa kufanywa.
Katika mistari 1-
1. Tunapaswa kudumisha umoja na amani katika kanisa.
Paulo
anaandika, “Iweni wanyenyekevu kabisa na wapole, mkiwa wavumilivu,
mkichukuliana kwa upendo. Jitahidini kudumisha umoja wa Roho
katika kifungo cha amani” (mistari wa 2-
Kwanza,
Paulo anaeleza kwamba ni lazima tuwe wanyenyekevu kabisa. Mtu
ambaye ana kiburi na anapuuza watu kila wakati atasababisha shida na
mgawanyiko katika kanisa kwa sababu anafikiria kuwa yeye ndiye mtu
muhimu sana katika kanisa lote. Tunapaswa kufikiria wenzetu kuwa
bora zaidi kuliko sisi na tunapaswa kujali mapenzi ya wengine kwanza
kabla ya kuangalia mambo yetu wenyewe (Wafilipi 2:3-
Pili, tunapaswa kuwa wapole. Mtu ambaye ni mpole hatilii mkazo sana mambo yafanyike kulingana na maoni yake, halazimishi watu kufanya kile yeye mwenyewe anataka bali yeye ni mpole, na ako tayari kuwapa nafasi wengine.
Tatu, tunapaswa kuvumiliana na kila mmoja wetu katika upendo. Hii inamaanisha kwamba ni lazima tuwavumilie na tuwajali wengine. Kanisa liko na watu tofauti tofauti, na wengine wao siyo rahisi kuishi nao. Lakini tunapaswa kuwavumilia wote. Ikiwa tutafanya hivi, basi tutadumisha umoja na amani katika kanisa.
2. Tunapaswa kutumia vipawa ambavyo Mungu ametupatia kuwahudumia wengine.
Paulo anasema, “Lakini kila mmoja wenu amepewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Kristo” (mstari 7). Kwa kusema hivi Mtume Paulo anasema kwamba Bwana Yesu amewapa watu wake vipawa. Kuna mambo manne muhimu sana kuhusu vipawa katika kifungu hiki.
(i) Mungu anawapa watu vipawa hivi kwa neema yake. Hii ndiyo sababu Paulo anasema, “Kila mmoja amepewa neema.” Sababu kuu ya Mungu kumpa mtu neema si kwamba mtu huyu amefanya jambo lolote ambalo linamwezesha kupewa kipawa hicho, ama kwa sababu anastahili kupewa. Vipawa hivi Mungu anawapa watu wake kwa neema yake, na hii inamaanisha kwamba Mungu anawapa bila malipo. Mtu anaweza kuwa amepewa vipawa vingi na Bwana lakini hiyo haimaanishi kuwa yeye ni mtakatifu sana na ni mtu muhimu sana kuliko wengine mbele za Mungu. Mungu anawapa watoto wake wote vipawa bila kuwalipisha.
(ii) Kuna aina nyingi za vipawa. Paulo anasema kwamba vipawa hivi vinapeanwa, “Kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Kristo.” Watu wa Mungu wote wamepewa vipawa tofauti tofauti, na vipawa hivi havifanani: “Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa” (Warumi 12:6). Ni jambo la kusikitisha wakati mtu anatamani kipawa cha mkristo mwenzake badala ya kutumia kile chake ambacho Mungu amempa.
(iii) Kila mshirika wa kanisa amepewa kipawa na Mungu. Paulo anasema, “Kila mmoja wetu amepewa neema,” kumbuka hasemi, “Kuna watu fulani ndani yetu ambao wamepewa neema.” Washirika wa kanisa hawapaswi kuwaza kwamba ni mchungaji pekee ambaye Mungu amempa vipawa na kwa hivyo wao hawana lolote la kufanya. Ni lazima tukumbuke kwamba kila mtu amepewa vipawa na Mungu.
(iv) Kila mshirika wa kanisa ako na jukumu la kutumia vipawa vyake katika kanisa. Katika kifungu hiki Paulo anasema kwamba wachungaji na walimu wanapaswa, “Kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma” (mstari wa 12). Kila mshirika wa kanisa ako na kazi ya huduma ambayo Mungu amempa. Wachungaji na walimu wanapaswa kuwatayarisha washirika wa kanisa zao kwa kazi hizi za huduma. Hii inamaanisha kwamba ikiwa wachungaji hawatayarishi na kuwahimiza washirika wa kanisa zao kutumia vipawa vyao basi wachungaji hao wanafanya makosa. Pia ikiwa washirika wa kanisa hawatumii vipawa vyao ambavyo Mungu amewapa bali wanavificha, basi wao pia wanafanya makosa.
3. Tunapaswa kuendelea kukua katika imani yetu ya ukristo.
Paulo
anatuambia kwamba sababu kuu ya Kristo kuwapa watu vipawa katika kanisa
lake ni waweze kuufikia “Umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana
wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo”
(mstari wa 13). Tunapookoka huwa tunazaliwa mara ya pili.
Hii inamaanisha kwamba tunakuwa wachanga sana katika mambo ya
ukristo tunapookoka. Hatuwezi kuwa wachanga kila wakati, ni
lazima tukue. Mungu hafurahii kamwe wakati watoto wake hawakui
katika imani (1 Wakorintho 3:1-
Njia mzuri ya kuhakikisha kwamba unakua katika ukristo ni kuhudhuria kanisa ambapo neno la Mungu linafundishwa kwa uaminifu na kwa kweli. Usihudhurie kanisa tu kwa sababu umefurahia nyimbo fulani ambazo zinakupendeza, bali hudhuria kanisa ambalo neno la Mungu linafundishwa kwa ukweli. Pia hakikisha kwamba wewe mwenyewe unasoma na kuelewa Biblia kila siku. Usipuuze neno la Mungu, ni chakula cha moyo wako na kitakuwezesha kukua.
Somo la Tatu, Waefeso 4:17-
Ukristo Ulimwenguni.
Katika kifungu hiki cha Biblia, Paulo anatupatia mafundisho kuhusu vile tunapaswa kuishi tukiwa wakristo hapa ulimwenguni, yaani mahali tunafanya kazi, miongoni mwa majirani wetu na marafiki wetu. Kumbuka hili ni jambo muhimu sana. Paulo anasema, “Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana ” (mstari 17). Kuishi maisha ya ukristo katika ulimwengu huu wa dhambi ni jambo muhimu sana. Katika kifungu hiki Paulo anatueleza mambo matatu.
1. Tunapaswa kukumbuka sisi ni watu wa aina gani.
Katika kifungu hiki Paulo anasema tusiwe kama wale ambao hawajaokoka: “Msiishi tena kama watu wa mataifa waishivyo” (4:17). Katika mstari huu “watu wa mataifa” inamaanisha wale ambao hawajaokoka. Paulo hapa anatukumbusha jinsi wale ambao hawajaokoka walivyo: kwanza, wao wanapuuza njia za Mungu, “Akili zao zimetiwa giza” (mstari 18). Pili, watu hawa “wametengwa mbali na Mungu” (mstari 18). Tatu, “Wamejitia katika kila mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu” (mstari 19).
Wale ambao wameokoka wamefundishwa Yesu Kristo. Hawakufundishwa mambo machache fulani kumhusu Kristo bali wamefundishwa Kristo ni nani na ni nini amewafanyia na pia ni nini anatarajia kutoka kwao. Sisi wakristo hatupaswi kuishi kama watu wa dunia kwa sababu sisi si wa dunia hii. Tumekombolewa kutoka kwa dunia na tumeunganishwa na Kristo. Kwa hivyo tunapaswa kutii Kristo na kuwa na uhusiano wa karibu sana naye katika kila jambo.
2. Tunapaswa kuishi maisha mapya (4:22-
Paulo anasema katika kifungu hiki kwamba wakati Mungu anatuokoa, tunafundishwa, “Kuuvua utu wetu wa kale, ulioharibiwa na tamaa za udanganyifu, tufanywe upya roho ya nia zetu, tuvikwe utu upya, ulioumbwa sawa sawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.” Wakati tuliokolewa, tulitolewa kutoka ufalme wa giza na tukaingizwa katika ufalme wa Yesu Kristo (Wakolosai 1:13).
Kwa
hivyo kuokoka ni kama kuhamia katika nchi nyingine. Fikiria
kuhusu mtu ambaye alizaliwa na kulelewa katika kijiji fulani katika
nchi ya Brazil halafu anahamia Marekani. Mtu huyu hawezi
kuendelea kuishi jinsi alikuwa anaishi akiwa Brazil kwa sababu yeye
sasa ako katika nchi nyingine. Nguo ambazo anavaa, nyumba ambamo
anaishi, chakula ambacho anakula na lugha ambayo anazungumza, haya yote
ni mambo mapya. Mtu huyu ameacha maisha aliyokuwa anaishi na
kuanza maisha mengine mapya. Kila wakati anapoendelea kuishi
katika hii nchi mpya, anaendelea na kubadilika. Yeye haendelei na
kufikiria jinsi alivyokuwa akifikiria mbeleni, bali sasa yeye ameanza
kuwaza tofauti kabisa kwa sababu ako katika nchi mpya. Hivi
ndivyo inavyokuwa wakati tunaokoka. Tunavua utu wa kale halafu
tunavaa utu upya, yaani maisha matakatifu. Kila wakati
tunavyofanya hivi, akili zetu zinaendelea kufanywa upya, na pole pole
tunaendelea kufanana na Kristo wala si kuwa kama watu wa
ulimwengu. Hii ndiyo sababu Paulo anasema, “Kwa maana zamani
ninyi mlikuwa giza, lakini sasa nyinyi ni nuru katika Bwana.
Enendeni kama watoto wa nuru (kwa kuwa tunda la nuru hupatikana
katika wema wote, haki na kweli), nanyi tafuteni yale yanayompendeza
Bwana. Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni”
(Waefeso 5:8-
3. Tumepewa mifano wazi kwamba inamaanisha nini kuishi maisha ya ukristo hapa duniani (Waefeso 4:25-
Katika kifungu hiki Paulo anaeleza mambo fulani kwa wale ambao sasa wameokoka ili waweze kujua kwamba maisha wanayoishi sasa ni tofauti na vile walikuwa wanaishi kabla ya kuokoka. Paulo anaeleza mambo yafuatayo:
(i)
Hatupaswi kuambiana uongo kwa sababu sisi sote ni mwili mmoja (4:25):
Pia tunapaswa kuhakikisha kwamba maneno mabaya yasitoke vinywani mwetu
bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine (4:29).
Mazungumzo yetu hayapaswi kuwa machafu na ya aibu (5:4).
Tunapaswa kuhakikisha katika kila jambo mazungumzo yetu ni ya kumsifu
na kumshukuru Mungu kila wakati (5:19-
(ii)
Hatupaswi kuruhusu hasira kukaa ndani ya mioyo yetu kwa sababu hii
inampatia ibilisi nafasi ya kuangamiza ushirika wetu na wenzetu (4:26-
(iii) Hatupaswi kuiba, bali tunapaswa kufanya kazi kwa bidii sana ili tuwagawie wahitaji (4:28).
(iv) Tusiwashughulikie wengine kwa uchungu, ghadhabu, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu, bali tunapaswa kuwa wafadhili na wenye kuhurumiana sisi kwa sisi tukisameheana kwa upendo, kama vile Mungu alivyo (4:28).
(v) Uasherati na uchafu wa aina yoyote hupaswi kuwa miongoni mwa watu wa Mungu (5:3;18).
(vi)Tunapaswa kunyenyekea sisi kwa sisi kwa heshima na kwa ajili ya Kristo (5:21).
Soma la Nne, Waefeso 5:22-
Katika kifungu hiki Paulo anaandika kuhusu jinsi tunapswa kuishi maisha ya ukristo nyumbani mwetu. Watu wengi ambao wameokoka, hawajali sana maisha yao ya ukrito katika jamii yao kama vile wanajali maisha ya kanisa lao ama maisha yao duniani. Jambo hili sana sana linaonekana kwa wachungaji ambao wanatumia muda kidogo sana na jamii zao nyumbani. Haya ni makosa sana. Jamii ni kitu muhimu sana na hii ndiyo sababau Paulo aliandika mistari mingi sana katika kifungu hiki. Pia tunapaswa kujua kwamba mahali ambapo mtu anapata vigumu sana kuwa kama Kristo ni wakati ako na jamii yake. Hii ndiyo sababu kifungu hiki ni muhimu sana.
1. Mafundisho kwa wake (5:22-
Paulo anawaambia wanawake wawatii waume wao “Kama kumtii Bwana.” Hii inamaanisha kwamba wake wanapaswa kuwatii waume wao jinsi wanamtii Bwana Yesu Kristo. Watu ambao wameokoka wanamtii na wanapenda Yesu Kristo kwa furaha, si kwa sababu wamelazimishwa, na hivyo ndivyo wake wanapaswa kuwatii waume wao. Kumbuka hakuna mahali Paulo anasema, “Ninyi wake mwatii waume wenu ikiwa wanawaheshimu.” Mwanamke anapaswa kumtii mume wake kwa sababu Mungu mwenyewe amesema hivyo, si kwa sababu mume wake anafaa heshima ama hafai.
Paulo
anawaeleza wanawake ni kwa nini wanapaswa kuwatii waume wao. Kuna
sababu mbili. Kwanza mume ndiye kichwa cha mkewe (mstari 23).
Hivi ndivyo Mungu alipanga jamii iwe katika bustani la
Edeni, Adamu alikuwa kichwa cha mke wake, na mpangilio huu uko
hata leo. Sababu ya pili kwa nini mke anapaswa kumweshimu mume
wake ni kwa sababu ya uhusiano kati ya mume na mke unafanana na
uhusiano kati ya Kristo na kanisa (mistari 23-
2. Mafundisho kwa waume (5:25-
Katika kifungu hiki Paulo anawaeleza waume jambo moja: kwamba ni lazima wawapende wake wao (mistari 25;28). Paulo anaendelea kusema kwamba jinsi Yesu alilipenda kanisa ndiyo mfano wa vile waume wanapaswa kuwapenda wake wao. Tukiangalia upendo wa Kristo kwa kanisa lake, tunaona mambo manne wazi ambayo mume anahitajika kufanya.
(i) Yesu Kristo alipenda kanisa kwa upendo wa kujitolea: “Alijitoa kwa ajili yake.” Kristo alikufa ili aweze kuliokoa kanisa. Vile vile, mume anapaswa kuwa tayari kujitolea kuacha starehe zake na mahitaji yake kwa sababu ya mke wake. Ikiwa mke wake anamhitaji nyumbani ili amsaidie basi anapaswa kuacha marafiki wake ambao wanatazama michezo ya mpira pamoja na kuwa na bibi yake nyumbani. Mume anapaswa kujitolea kwa sababu ya mke wake.
(ii) Yesu Kristo alilipenda kanisa kwa upendo maalum. Yesu Kristo anawapenda watu wote duniani na anawajali (Mathayo 5:44-
(iii) Yesu Kristo aliipenda kanisa kwa upendo wa neema. Sisi watu wake tulikuwa wachafu na waasi dhidi ya Kristo Yesu wakati alitufia na wakati alituokoa. Sisi hatukustahili upendo wake. Vivyo hivyo mume anapaswa kumpenda mke wake kila wakati hata wakati yule mume anaona mke wake hastahili upendo wake. Mume hawezi kusema, “Huyu mke wangu sasa ni mzee, yeye siyo mchanga na mrembo na hata hawezi akapata watoto kwa hivyo nitaoa mke wa pili.”
(iv) Upendo wa Kristo kwa kanisa lake ulikuwa na kusudi fulani: “Kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake” (mstari 26). Yesu Kristo haonyeshi upendo wake kwetu kwa kututimizia mahitaji yetu ya mwili pekee, bali kwa kututayarisha ili tuweze kuingia mbinguni. Vivyo hivyo kazi ya mume si kushughulika na chakula na makao ya mke wake pekee, bali anapaswa kumshughulikia mke wake mambo ya kiroho. Anapaswa kumsaidia kupigana na dhambi, anapaswa kusoma na kujifunza Biblia pamoja na mke wake, na anapaswa kuomba naye ili aweze kukua katika imani yake na amtumikie na kumheshimu Mungu.
3. Mafundisho kwa watoto (6:1-
Mafundisho ya Paulo kwa watoto ni kwamba wanapaswa kuwatii wazazi wao “Katika Bwana.” Hii inamaanisha kwamba wanapaswa kutii wazazi wao katika mambo ambayo yanampendeza Mungu. Ikiwa wazazi watawaeleza watoto wao kusema uongo basi hawawezi kutii jambo hilo kwa sababu ni kinyume na neno la Mungu. Paulo pia anasema kwamba hii ni amri yenye ahadi: watoto watapata baraka na wataishi siku nyingi duniani. Watoto ambao watatii wazazi wao na wanafuata ushauri wa wazazi, wataepuka mambo mengi mabaya na watakuwa na maisha mazuri ya furaha na yenye afya. Hii inaonekana vizuri zaidi ikiwa watoto wataokoka. Maisha yao katika jamii yao yatakuwa ya furaha sana kwa sababu jamii yote watamheshimu Mungu katika kila jambo na watakuwa na umoja.
4. Mafundisho kwa akina baba (6:4).
Inashangaza kwamba Paulo hawaelezi mafundisho haya wazazi bali anawaeleza akina baba hasa hasa. Hii ni kwa sababu baba ndiye kiongozi wa nyumba, na labda kwa sababu akina baba mara mingi wanapuuza kazi ya kuwalea watoto. Kuna mafundisho mawili hapa kuhusu akina baba. Kwanza, hawapaswi kuwachokoza watoto wao. Hii inamaanisha kwamba hawapaswi kufanya maisha ya watoto wao kuwa magumu. Baba anaweza kuyafanya maisha ya watoto wake kuwa magumu wakati anakuwa mkali sana. Ikiwa anatarajia wao kufanya kazi kwa bidii sana shuleni na wawe wanaongoza kila wakati, hiyo inaweza kufanya maisha yao kuwa magumu. Baba pia anaweza kufanya maisha ya watoto kuwa magumu ikiwa atawapeleka kusoma katika shule ambazo hawatakuwa wakija nyumbani kila siku, yaani boarding school, mahali ambapo hawafurahi na hawapati mafundisho ya Biblia kila siku. Pia baba anaweza kufanya maisha ya watoto wake kuwa magumu kwa kuwalazimishia mambo ya ukristo kama kukariri mistari ya Biblia kila siku.
Pili, baba ni lazima awalee watoto wake kwa nidhamu na mafundisho ya Kristo. Hii inamaanisha anafaa awafundishe watoto wake neno la Mungu kila siku, na pia anafaa kuomba nao na kuwaombea ili wapate kuokoka na kuishi maisha matakatifu. Hili ni jukumu la Baba na ni lazima alitekeleze. Baba anafaa kujua kwamba maisha ya kiroho ya watoto wake ni muhimu zaidi ya vile wanafanya katika masomo yao shuleni.
5. Mafundisho kwa watumwa (6:5-
Maneno haya yalikuwa mwanzo yameandikiwa watumwa, lakini yanahusu kila mmoja ambaye ameajiriwa, iwe ni katika afisi ya serikali ama kazi ya kuwa msaidizi katika nyumba. Paulo ako na funzo moja hapa: kwamba wafanyakazi wote wawatii mabwana wao na kuwatumikia kwa mioyo yao yote. Wanapaswa kuwatii mabwana wao kama tu wanavyomtii Kristo na kuwa waaminifu na waangalifu katika kazi zao. Hii ni kwa sababu ni mapenzi ya Mungu wao wafanye hivi (mstari 6), na wakifanya hivi Bwana atawapa thawabu.
6. Mafundisho kwa mabwana ( 6:8-
Paulo anasema hapa kwamba “Nanyi mabwana watendeeni watumwa wenu kwa jinsi iyo hiyo.” Watumwa wanapaswa kuwatumikia mabwana zao kama vile wanamtumikia Kristo, nao mabwana wanapaswa kuwatendea wafanyakazi wao jinsi Kristo angewatendea. Hawapaswi kuwatisha watumishi wao kwa sababu Bwana Yesu Kristo ako mbinguni na anaangalia kila kitu. Ni jambo ambalo linafanyika sana hapa nchini mwetu kwamba wafanyakazi wanalipwa vibaya na wanatumiwa vibaya na mabwana wao. Haya yote ni kinyume na mapenzi ya Mungu, na mabwana wote ambao wanafanya mambo haya siku moja wote watahukumiwa na Mungu.
Somo la Tano, Waefeso 6:10-
Katika kifungu hiki Paulo anaendelea kufundisha jinsi tunafaa kuishi maisha ya ukristo kila siku. Ametufundisha jinsi tunapaswa kuishi maisha ya ukristo katika kanisa, ulimwenguni na katika jamii. Sasa anaanza kutufundisha vile tunapaswa kupigana vita na majeshi ya pepo wabaya. Kuna mambo matatu muhimu ambayo Paulo anafundisha hapa.
1. Tunapaswa kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake (mstari 10).
Maisha ya mkristo ni maisha ya vita. Mtu anapookolewa, anakuwa askari katika jeshi la Mungu na anakumbana na adui kila wakati uso kwa uso. Tunahitajika kupigana vita kila wakati wala si kuwa wanyonge na kukaa bila kufanya chochote kwa maadui wetu. Adui mkubwa wa mkristo ambaye ni shetani huwa anatumia aina mbili ya silaha kupigana nasi.
(i) Ulimwengu. Hii inamaanisha kwamba watu wale walikuwa marafiki sana wanabadilika na kuwa maadui wako. Watu wa dunia wako katika mamlaka na uongozi wa shetani na watafanya kila jambo ili waweze kumletea mkristo majaribu ili wamrudishe tena katika maisha ya dunia. Mtu akiokoka marafiki wake wanaweza kumchekelea na kumdharau na kumshawishi aache maisha ya wokovu na waungane naye tena kwa mambo ya ulimwengu kama kunywa pombe pamoja baa.
(ii) Dhambi ambayo imebaki ndani mwake. Hili ni jambo ambalo tulizungumzia katika somo la kwanza katika kijitabu hiki. Dhambi ambayo iko ndani yetu itampiga mkristo vita ili kujaribu aishi maisha ya dhambi wala si kumfuata na kumtii Kristo.
Bwana Yesu Kristo alifundisha kwamba hawa wakilishi wawili wa shetani, yaani ulimwengu na dhambi iliyo ndani ya mkristo wana nguvu sana. Katika mfano wa mpanzi na mbegu, Yesu aliongea kuhusu mtu ambaye anasikia neno lake na kulikubali kwa haraka na kwa furaha, na kuonekana kabisa kama ameokoka. Lakini “Inapotokea dhiki au mateso kwa ajili ya hilo neno, yeye huchukizwa” (Mathayo 13:21). Sisi sote tunajua hii ni kweli. Mtu anakuja kanisani na anasikia mahubiri kutoka kwa Biblia halafu anasema kwamba ameokoka. Lakini punde tu marafiki wake kazini wanagundua jambo hili, wanamchekelea na wanamdharau. Anapata kwamba wao si marafiki wake tena na wamemtenga kabisa na kwa sababu hii yeye anaacha wokovu na anarudi tena katika mambo ya dunia. Hii inaonyesha kwamba yeye hakuwa ameokoka kutoka mwanzo, na hii inatuonyesha kwamba ulimwengu ni adui ambaye ana nguvu sana.
Yesu Kristo pia alieleza jinsi dhambi iliyobaki ndani mwetu ilivyo na nguvu. Alisema, “Masumbufu ya dunia na ushawishi wa mali” u wafanya wengi kurudi katika dunia. Pia hili ni jambo ambalo tunajua linafanyika. Mtu ambaye alikuwa akipata pesa nyingi kupitia njia ya hongo anasema kwamba ameokoka. Sasa anaelewa kwamba hapaswi kuchukua ama kupeana hongo na yeye anajua hii inamaanisha kwamba pesa zake zitapunguka, na kwa hivyo anarudi tena katika maisha ya dunia na kuanza kuchukua hongo tena.
Tunapaswa kuwa hodari katika Bwana kwa sababu ya hawa maadui. Nguvu zetu hazitoki kwetu wenyewe kwa sababu sisi ni wadhaifu lakini zinatoka kwa Mungu mwenyewe. Yeye ni mwenyu nguvu na anatuwezesha kusimama. Tunahitaji kuomba na kuwaombea wengine ili waweze kusimama katika Bwana na wapigane vita bila kukata tamaa.
2. Tunapaswa kukumbuka kwamba vita vyetu si vya damu na nyama bali ni dhidi ya falme, mamlaka na wakuu wa giza (mstari 12).
Shetani anaitwa, “Mtawala wa falme za anga” (Waefeso 2:2) na “Mungu wa dunia hii” (2 Wakorintho 4:4). Hii haimaanishi kwamba shetani ni mwenye nguvu kama Mungu ama shetani anaweza kukataa mapenzi ya Mungu. Mungu mwenyewe ndiye mtawala na mwenye anga yote na chochote kinatendeka duniani kinatendeka kwa mapenzi yake na kwa ruhusa yake. Mungu katika hekima yake amemruhusu shetani kuwa na mamlaka juu ya wale ambao hawajaokoka humu duniani na kuwatumia. Hii ndiyo sababu Biblia inasema, “Mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Kristo, aliye sura ya Mungu” (2 Wakorintho 4:4).
Hii
inamaanisha kwamba vita vyetu si vita dhidi ya watu wa ulimwengu huu.
Hatupigani vita na majirani wetu na marafiki wetu wale
hawajaokoka. Ni lazima tujue kwamba wao ni watumwa hata ikiwa
hawajui. Wakati wanatusumbua kwa sababu ya imani yetu ya ukristo,
ni kwa sababu shetani anawatumia. Kwa hivyo hatupaswi kuwapiga
vita majirani wetu bali tunapaswa kuwaombea wale wanatuchukia na
wale wanatutatiza (Mathayo 5:44-
3. Tunapaswa kuvaa silaha zote za Mungu (mistari 13-
Vita vyetu kama vile tumeona si vya kupigana na watu bali ni vya kupigana na pepo wabaya. Hii inamaanisha kwamba ni lazima tuvae silaha zote za Mungu za kiroho ili tuweze kupigana vita hivi. Kumbuka katika mstari wa 12 Paulo anatueleza ni nani tunayepigana naye, halafu katika mstari wa 13 anasema, “Kwa hivyo,” akimaanisha kwa sababu mnapigana na adui wa aina hii, mnahitaji kuvaa silaha za Mungu. Katika kifungu hiki Paulo anaeleza kuhusu silaha hizi.
(i) Neno la Mungu. Hili limesemwa mara tatu katika kifungu hiki: “Kweli kiunoni” (mstari 14), “Injili ya amani” (mstari 15), na “Neno la Mungu” (mstari 17). Neno la Mungu ndilo silaha muhimu sana ambalo tuko nalo kwa sababu linatulinda dhidi ya shetani, linatuhimiza wakati ulimwengu unatushusha moyo na linatuwezesha kushinda maadui wetu na kuwaleta waungane nasi wakati tunahubiri injili. Ikiwa tutashinda vita vyetu dhidi ya shetani, ni lazima tusome na tuelewe neno la Mungu kila siku na tulijue kabisa.
(ii) Darii ya haki. Shetani anaitwa “Mshtaki wa ndugu zetu, anayewashtaki mbele za Mungu usiku na mchana” (Ufunuo 12:10). Shetani kila wakati anataka kuwashusha moyo wakristo na kuwafanya wasiwe na nguvu katika maisha yao ya ukristo. Jambo hili anafanya kwa kutukumbusha maovu yetu mbele za Mungu. Lakini wakati tuliokoka, tulipewa haki ya Yesu Kristo na kwa hivyo tukawa wenye haki machoni pa Mungu. Hii ndiyo sababu tumepewa darii ya haki ili tutumie katika vita hivi dhidi ya shetani.
(iii) Ngao ya imani. Imani inamaanisha kukubali na kuamini vile Mungu amesema katika neno lake. Imani inalinda na kuzuia mishale yenye moto ya shetani kwa sababu neno la Mungu limejawa na ahadi nyingi kwa watu wake. Tukiamini ahadi hizi za Mungu na kuzitumainia katika maisha yetu, basi tutalindwa dhidi ya hii mishale ya shetani.
(iv)
Chepeo ya wokovu. Katika kitabu cha 1 Thesalonike 5:8, Paulo
anasema tuvae, “tumaini letu la wokovu kama chepeo.” Tumaini letu
la mbinguni ni silaha muhimu sana kwa sababu linatukumbusha kuhusu
uzima wa milele. Tukikumbuka kwamba tutakuwa na Bwana Yesu milele
mbinguni, basi mafikira hayo yatatuwezesha kupambana na majaribu ya
maisha: “Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha
na utukufu utakaodhihirishwa kwetu” (Warumi 8:18). Hatutashushwa
moyo wakati wa, “Dhiki au mateso kwa ajili ya hilo neno” (Mathayo
13:21) bali tutavumilia. Pia tukiendelea kuwaza kuhusu makao yetu
ya milele kule mbinguni, basi tutaishi maisha matakatifu hapa
ulimwenguni: “Lakini twajua kwamba, Yeye atakapodhihirishwa, tutafanana
naye , kwa maana tutamwona kama alivyo. Kila mmoja mwenye
matumaini haya katika Yeye hujitakasa kama vile Yeye alivyo mtakatifu”
(1 Yohana 3:2-
(v) Maombi (18-
Kwanza, anatuambia kwamba tunapaswa kuwa watu wa maombi: “Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi.” Ni lazima tuwe na wakati wa maombi kila siku, na pia tunapaswa kuwa watu wa kuomba kila wakati. Fikiria kuhusu rafiki yako ambaye amekupigia simu yako ya rununu na simu hiyo haikatiki na unaendelea kuongea naye kila wakati. Kila wakati ukiwa na hitaji unamwita na anakuja kukusaidia. Hivi ndivyo tunapaswa kuwa kila wakati kuhusu maombi.
Pili, Paulo anawaambia Waefeso wamwombee yeye katika huduma wake wa kueneza injili (mistari 19-
Vitabu ambavyo vinaweza kukusaidia katika maisha yako ya ukristo.
Vile tumeona, ni vyema zaidi kwa wale ambao wameokoka kuishi maisha matakatifu katika ulimwengu huu. Watumishi wa Mungu wengi wameandika vitabu vizuri sana ambavyo vinaweza kumsaidia kila mkristo kujifunza jinsi anafaa kuishi maisha matakatifu ambayo ni maisha ya kumtukuza Mungu. Ikiwa unaweza kupata vitabu hivi, ninakusihi uvisome na ujifunze kwa uangalifu sana.
1. Utakatifu (mwandishi J.C. Ryle).
2. Kutembea na Mungu (mwandishi J.C. Ryle).
Vyote hivi vinapatikana katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili.