Header

Utangulizi

 

Kijitabu hiki kinahusu baraka ambazo Mungu anatupatia wakati anatuokoa.  Wokovu ni zawadi kubwa sana kutoka kwa Mungu na inawaletea watu wa Mungu baraka nyingi sana za kufurahia.  Jambo la muhimu sana ambalo kila mkristo anapaswa kufanya ni kusoma kwa makini sana Biblia ili ahakikishe kwamba amezielewa baraka hizi ambazo Mungu amempa.  Ni jambo la kuhuzunisha kwamba kuna watu wengi ambao wameokolewa lakini hawajawahi kufikiria kuhusu baraka ambazo Mungu amewapa tangu awaokoe.  Kwa hivyo hili ni jambo muhimu sana.  Watu wa Mungu wanapaswa kutumia muda mwingi kusoma Biblia ili wachunguze kwa makini na kuelewa wazi baraka ambazo Mungu ametupatia wakati alituokoa.  Kuna sababu tatu kwa nini tusome na kuelewa Biblia.

 

1.  Ikiwa hatutasoma na kuelewa baraka ambazo Mungu ametupatia wakati ametuokoa, basi tutakuwa katika hatari ya kumtukana.  Mungu.  Fikiria kwamba umefanya kazi kwa bidii sana kwa miaka miwili ili upate pesa ambazo unatarajia kununulia rafiki yako simu nzuri sana.  Baada ya kununua hiyo simu unampelekea rafiki yako nyumbani kwake na unampatia kama zawadi.  Hebu fikiria ukimpatia hiyo simu halafu anaiangalia tu kwa muda kidogo tu halafu anaiweka chini na kuanza kuongea kuhusu mambo mengine.  Ukweli ni kwamba hutafurahia, kwa sababu zawadi hii ilikugharimu sana na rafiki yako haonekani kushukuru.  Ameiangalia simu uliyomletea kwa muda kidogo tu na hakuonekana kufurahia kamwe.  Tunahitaji kuchunguza kwa makini sana zawadi kubwa ya wokovu ambayo Mungu ametupatia, la sivyo tutakuwa katika hatari ya kumtukana Mungu.

 

2.  Ikiwa tutaelewa baraka ambazo Mungu ametupatia katika wokovu basi tutaishi maisha ya kumpendeza.  Kuna mambo matatu ambayo Mungu anataka kutoka kwa watoto wake wote: Anataka tumpende, anataka tumtii na pia anataka tumtumikie.  Hii ndiyo kumwabudu Mungu kwa ukweli na hii ndiyo anatarajia kutoka kwa kila  mmoja wetu.  Sasa ikiwa tutaelewa baraka ambazo Mungu ametupatia, basi tutaweza kuyafanya mambo ambayo Mungu anatarajia kutoka kwetu.  Yesu alisema, yule ambaye amesamehewa mingi, atapatapenda sana (Luka 7:47).  Kile Yesu anamaanisha hapa ni kwamba wale ambao wanaelewa kwamba wamesamehewa sana watampenda Bwana sana, lakini wale  ambao hawajaelewa kwamba wamesamehewa sana, hawatampenda sana.

 

3.  Kuna kuchanganyikiwa kwingi sana humu nchini mwetu kuhusu baraka tunazozipata kutokana na wokovu.  Kuna wahubiri wengi siku hizi wanaongea sana kuhusu mambo ya humu duniani sana lakini wanaongea mambo machache sana kuhusu mambo ya mbinguni.  Watu wanaambiwa kwamba ikiwa watakuja kwa Kristo ili awaokoe watapata baraka nyingi za mali na watakuwa wenye afya jema.  Kwa sababu ya hii kuchanganyikiwa tunahitaji kuchunguza kwa makini ni nini Biblia inafundisha kuhusu baraka za wokovu.

 

Katika kijitabu hiki tutaona baraka saba kubwa za wokovu wetu:

 

1.Tumehesabiwa haki.

2.Tumekombolewa kutoka kwa ufalme wa giza na kupelekwa katika ufalme wa nuru.

3.Tumepatanishwa na Mungu na watu wake.

4.Tumefanywa wana katika jamii ya Mungu.

5.Tumehakikishiwa wokovu wetu na Roho Mtakatifu.

6.Tunaendelea kugeuzwa ili tufanane na Yesu.

7.Siku moja tutatukuzwa.

 

Funzo la kwanza, Warumi 3:20-31, Tumehesabiwa haki

kwa neema ya Mungu.

 

Katika funzo hili, tutaangazia kuhusu kuhesabiwa haki kwa kuuliza maswali manne na kuyajibu.

 

1.  Je, kuhesabiwa haki inamaanisha nini?

 

Kuhesabiwa haki ni kazi ya neema ya Mungu ambapo anatusamehe bure dhambi zetu zote, na anatupatia haki ya Kristo ili tuhesabiwe haki machoni mbele yake.  Tunahesabiwa haki kwa imani pekee katika kazi ya Yesu Kristo pekee na si kwa matendo yetu.  Paulo anasema katika kifungu hiki, “Kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu” (Warumi 3:23-24).  Kuna mambo matatu hapa ambayo tunapaswa kujifunza kwa makini sana.

 

(i) Kuhesabiwa haki ni kazi ya Mungu mwenyewe, siyo kitu ambacho mwanadamu anaweza kufanya.  “Wokovu watoka kwa Bwana; Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?” (Yona 2:9; Marko 2:7).  Hii ni kwa sababu tunapofanya dhambi huwa tunamkosea Mungu mwenyewe, ijapokuwa wengine pia wanapata madhara kwa sababu ya dhambi zetu.  Wakati Yosefu alijaribiwa na bibi wa Potifa, alisema, “Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?” (Mwanzo 39:9).  Yosefu alijua kwamba angelala na bibi wa Potifa angekuwa anafanya dhambi kubwa sana dhidi ya mwajiri wake na pia alijua kwamba angekuwa anakosa dhidi ya mwenyezi Mungu.  Biblia inasema, “Dhambi ni uasi” (1 Yohana 3:4).  Hii inamaanisha kwamba wakati tunafanya dhambi huwa tunavunja sheria ya Mungu: kumaanisha kwamba ni Mungu tunayemkosea.  Kwa hivyo kuhesabia haki mwenye dhambi ni kazi ya Mungu peke yake.  Ni yeye tunayemkosea tunapofanya dhambi na ni yeye tu anaweza kumpa mwenye dhambi msamaha.  Hakuna mwanadamu yeyote ambaye amepewa mamlaka ya kumsamehe mwenye dhambi, ni Mungu pekee anaweza kupeana msamaha wa dhambi.

 

(ii) Pili, kuhesabiwa haki ni kazi ya neema ya Mungu.  Hii inamaanisha kwamba Mungu anatuhesabia haki wakati tunastahili kuadhibiwa.  Biblia inatueleza kwamba Mungu anatupatia baraka hii ya kuhesabiwa haki wakati tunastahili kupata ghadhabu ya hukumu yake.  Biblia inasema, “Yeye ambaye huwahesabia waovu haki” (Warumi 4:5).  Sisi ni wenye dhambi wakuu machoni pa Mungu na tunastahili ghadhabu na hukumu ya Mungu.  Ikiwa Mungu angewatuma watu wote jahanum, hakuna hata mmoja angeweza kulalamika.  Hakuna mmoja angesema kwamba Mungu hana haki ya kufanya hivyo.  Tunajua kweli kwamba sisi ni wenye dhambi na kwamba tunastahili hukumu ya Mungu.  Lakini Mungu ni Mungu wa neema.  Mungu amejawa na huruma nyingi na anatuhurumia sisi wenye dhambi. Badala ya kuwahukumu watu wake na kuwatuma jahanum, anawahesabia kuwa wenye haki na anawaokoa.  Kuhesabiwa haki ni kazi ya neema ya Mungu.

 

(iii) Tatu, kuhesabiwa haki ni kazi ya neema ya Mungu kupitia kazi ya Yesu Kristo.  Paulo anasema katika kifungu hiki, “Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake.  Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake” (Warumi 3:25).  Fikiria kuhusu mtu humu nchini mwetu ambaye ni jambazi mbaya sana.  tunasoma habari zake kila wakati jinsi anavyoua watu na vile anawaimbia watu wengi mali yao.  Wakati moja polisi wanamshika jambazi huyo na wanampeleka kotini.  Akiwa kotini mwamuzi anasikiliza ushahidi na anasema, “Ni wazi kabisa kwamba kutokana na ushahidi huu kwamba wewe ni jambazi mbaya sana, na pia ni wazi kwamba umefanya haya makosa yote.  Lakini sitakupeleka jela wala kukutoza faini.  Wewe enda  nyumbani na ujaribu kuishi vizuri.”  Mwamuzi akifanya hivi, atakuwa amefanya kwa sababu haki haikutendeka.  Hii ni kwa sababu mtu huyo alifanya makosa makubwa sana ambayo hajayalipia.  Hii itakuwa ukosefu wa haki na tutakasirika.

 

Haki ambayo Mungu anawahesabia watu wake siyo kama hiyo.  Wakati Mungu anatuhesabia kuwa bila hatia siyo kweli kwamba huwa hafanyi haki.  Sababu kuu ya Mungu kuwahesabia watu wake haki ni kwa sababu dhambi zao zimelipiwa na Bwana Yesu Kristo.  Hii ndiyo sababu Biblia inasema, “Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu” (Warumi 3:26).  Ni kwa sababu ya Kazi ya Yesu Kristo Mungu anaweza kuamua watu wake kuwa bila hatia na kwa hivyo Mungu angali mwenye haki.  Hebu fikiria kuhusu mfano wa jambazi tumeusoma hapa juu.  Fikiria mwamuzi akimwambia jambazi huyu, “Ninakutoza faini ya shilingi milioni kumi kwa sababu ya hatia yako,” halafu mtu fulani anakuja na anamlipia jambazi huyu hiyo faini ya milioni kumi.  Mwamuzi ako na haki ya kumwambia huyu jambazi, “Faini yako imelipwa, uko huru kwenda.”  Kwa kumwachilia jambazi huyu, mwamuzi hatakuwa amekosa kufanya haki, kwa sababu anatimiza sheria.  Vivyo hivyo wakati Mungu anawahesabia watu wake haki siyo kweli kwamba anakosa kufanya haki, kwa sababu anatimiza sheria yake.  Anawaachilia huru wale ambao dhambi zao zimelipiwa na Yesu Kristo.

 

2.  Je, Mungu huwa anafanya nini wakati anatuhesabia haki?

 

Biblia inatueleza kwamba kuna mambo matatu ambayo Mungu hufanya wakati anamhesabia mwenye dhambi kuwa haki:

 

(i) Anatusamehe dhambi zetu zote, dhambi za wakati uliopita, wakati ulioko sasa na dhambi za wakati ujao.

 

Paulo anasema katika kifungu hiki, “Kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa” (Warumi 3:25).  Kifungu hiki kinatueleza kwamba kuhesabiwa haki kunahusu adhabu ya dhambi zetu na msamaha wa dhambi zetu.  Dhambi zetu zinahitaji kuadhibiwa kwa sababu wakati tunafanya dhambi tunavunja sheria ya Mungu.  Mtu yeyote akivunja sheria ya nchi hupelekwa kotini na kuhukumiwa kwa sababu ya makosa hayo.  Vivyo hivyo mtu yeyote anayevunja sheria ya Mungu anastahili adhabu.  Lakini Mungu ni wa neema na alimtuma Mwanawe aje kuadhibiwa kwa niaba ya watu wake.  Wakati Bwana Yesu alikufa msalabani, alizichukua dhambi za watu wake na akazilipia.  Na sasa Mungu amewasamehe watu wake dhambi zao zote, dhambi ambazo walifanya zamani, dhambi ambazo wanazofanya wakati huu na dhambi watakazofanya.

 

Msamaha wa dhambi ni zawadi kubwa sana kutoka kwa Mungu.  Biblia inasema kwamba wakati Mungu anatusamehe dhambi zetu, huwa anazitupa katika vilindi vya bahari (Mika 7:18-19).  Hii inamaanisha kwamba Mungu huwa hakumbuki dhambi zetu kamwe na hatatuhukumu inavyostaili, “Yeye hatuadhibu kulingana na dhambi zetu wala hatulipizi sawasawa na maovu yetu.  Kama vile mbingu zilivyo juu sana juu ya dunia, ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha, kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo Mungu ameziweka dhambi zetu mbali na sisi” (Zaburi 103:10-12).

 

Wakristo wengi huogopa kwamba wakati watasimama mbele ya Yesu Kristo siku ya hukumu dhambi zao zote zitafunuliwa kwa kila mtu.  Hii si kweli.  Mungu ametusamehe dhambi zetu zote na hatazileta tena kwetu.  Mungu hatuadhibu jinsi dhambi zetu zinapaswa kuadhibiwa, bali anatushughulikia akiwa Baba yetu.

 

(ii) Mungu hutupatia utiifu mkamilifu wa Bwana Yesu Kristo.

 

Wakati Mungu anatuhesabia haki, huwa hatusamehi tu dhambizetu zote, bali huwa anaweka katika rekodi yetu ule utiifu mkamilifu wa Bwana Yesu Kristo.  Katika kijitabu nambari  sita (kijitabu ulichosoma kabla ya hiki, kurasa 10-11) nilitumia mfano fulani kueleza jambo hili.  Nitautumia mfano huo tena hapa kueleza jambo hili.

 

Fikiria ile siku ulizaliwa, Mungu alichukua kitabu na aliandika jina lako katika jalada la kitabu hicho.  Basi kuanzia wakati huo, kila dhambi ambayo umefanya Mungu anaiandika katika kitabu hicho.  Wakati ulipokuwa miaka kama 20 au 30 kitabu hicho kitakuwa na rekodi ya mamilioni ya dhambi kwa sababu tunafanya dhambi kila wakati, hata wakati hatujui.  Sasa fikiria siku ile Yesu alizaliwa huko Bethlehemu, Mungu alifanya vivyo hivyo: yaani alichukua kitabu na akaandika jina la Yesu Kristo katika jalada lake.  Baada ya miaka 30, Yesu alisulubiwa na akafa.  Je, ni nini kimeandikwa ndani ya kitabu cha Yesu?  Jibu ni kwamba hakuna dhambi yoyote imeandikwa hapo, kwa sababu hakufanya dhambi: “Yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi” (Waebrania 4:15).  Yesu aliishi maisha makamilifu na ya utiifu machoni pa Mungu, kwa hivyo katika kitabu chake kinasema, “Mtu huyu ametii sheria ya Mungu kabisa na alikuwa mkamilifu, Yeye ni mwenye haki kabisa.”  Haya ndiyo yameandikwa katika kitabu cha Yesu Kristo.

 

Sasa wakati tunaokolewa, kunakuwa na mabadiliko makubwa sana.  Mungu huchukua ile rekodi yetu ya dhambi na uasi na anaiweka katika kile kitabu cha Yesu Kristo.  Pia Mungu anatoa ile rekodi kamilifu na ya utiifu ya Yesu Kristo na anaiweka katika kitabu chetu.  Kwa hivyo Kristo anachukua dhambi zetu na uasi wetu na anahukumiwa, lakini sisi tunapewa hiyo haki yake.  Angalia kwa makini maneno ya Paulo kwa Warumi: “Kwa kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki” (Warumi 5:19).  “Mtu mmoja” katika msitari huu ni Yesu Kristo mwenyewe.  Ni kupitia kutii kwa Yesu Kristo kwamba wengi watahesabiwa haki.  Si kupitia kwa matendo yao mazuri watu wanahesabiwa haki, bali wanahesabiwa haki kupitia utiifu wa Yesu Kristo

 

Akiwaandikia Wakorintho Paulo alisema, “Mungu alimfanya Yeye asiyejua dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu katika Yeye” (2 Wakorintho 5:21).  Angalia tena kwa makini msitari huu.  Yesu hakuwa na dhambi kwa sababu alikuwa mkamilifu, lakini Mungu alimwekelea rekodi yetu ya dhambi kwake asiyejua dhambi ili amfanye kuwa dhambi kwa ajili yetu.  Mungu alichukua haki ya Yesu Kristo na kutupatia ili tupate kuwa haki ya Mungu katika Kristo.  Sasa wakati Mungu Baba anatuangalia, haoni ile rekodi ya dhambi na kutotii kwetu, kwa sababu hiyo imetolewa kutoka kwetu na kupewa Yesu.  Kile sasa Mungu Baba anaona ni ile rekodi kamilifu ya Yesu Kristo ambayo alitii sheria ya Mungu yote na ambayo imewekwa kwa rekodi yetu.  Yesu Kristo ndiye haki yetu (1 Wakorintho 1:30).  Bila maisha makamilifu ya Kristo hapa ulimwenguni hatuwezi kuingia mbinguni, tunaweza kuingia mbinguni tu kwa sababu Yesu Kristo alitii sheria ya Mungu kwa ukamilifu na akatupatia utiifu wake.

 

(iii) Mungu anatangaza uamuzi kwamba yule ambaye amemwamini Yesu Kristo ni mwenye haki milele katika sheria yake.

 

Hivi ndivyo inafanyika wakati Mungu anawahesabia watu wake haki.  Yule ambaye ni mwenye dhambi na rekodi yake inaonyesha ako na dhambi, anapelekwa kwa koti ya Mungu.  Hapo Bwana Yesu Kristo anachukua rekodi yake ambayo ni ya dhambi na anatumpatia ile rekodi yake ya utiifu.  Hapo basi, Mungu ambaye ndiye mwamuzi anachunguza rekodi yake.  Mungu anafungua kitabu ambacho jina lake limeandikwa na kuasoma kile kimeandikwa ndani:, “Mtu huyu ametii sheri ya Mungu kabisa na alikuwa mkamilifu, yeye ni mwenye haki kabisa.”  Kwa hivyo Mungu anasema, “Wewe umetii umetii sheria yangu kamilifu.  Sina mashitaka dhidi yako.”

 

Kumbuka huu ni uamuzi wa kotini, kumaanisha kwamba haya ni maneno yanaelezwa mtu akisimama mbele ya sheria.  Fikiria kuhusu mtu katika kijijini mwenu ambaye tabia yake ni mbaya sana, ni mtu mchoyo na anapuuza watu sana na pia ni mang'aa sana.  Siku moja mtu huyu anapelekwa kotini kwa sababu polisi wanafikiria yeye ni mwizi.  Mwamuzi anachunguza ushahidi na anasema mtu huyu hana hatia kamwe, inaonekana ni mtu mwingine ambaye alifanya wizi huo lakini siyo huyu polisi wamemleta hapa kotini.  Kwa hivyo mwamuzi anamwambia mshitakiwa, “Huko huru kwenda, huna hatia yoyote.”  Angalia kwa makini vile mwamuzi anasema.  Mwamuzi hasemi kwamba, “Wewe ni mtu mzuri, mtu msafi ama mtu anayemcha Mungu.”  Koti haina haja na kujua tabia ya mtu huyu, kama ni mzuri ama mbaya, lakini iko na haja moja tu kumhusu, kama ako na hatia ya wizi au la.  Anaweza kuwa ni mtu anapuuza watu huko kijijini lakini ikiwa hana hatia ni lazima mwamuzi asema mtu huyu hana hatia.  Huu uamuzi unaambatana na sheria, wala si tabia ya mtu.  Vivyo hivyo kuhesabiwa haki kunaambatana na sheria ya Mungu, si kwa sababu ya tabia.  Wakati Mungu anatuhesabia kuwa wenye haki, anasema kwamba mbele ya sheria yake hatuna hatia, sisi ni wenye haki.  Mungu hasemi kwamba sisi ni watu wazuri na watu wakupendeza ama watu waheshimiwa.

 

3.  Je, Mungu anatuhesabia haki namna gani?

 

Jibu la swali hili muhimu limepeanwa wazi katika Biblia.  Paulo anasema, “Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si matendo ya sheria” (Warumi 3:28), na tena, “Mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa njia ya imani katika Yesu Kristo” (Wagalatia 2:6).  Kuhesabiwa haki kama vile tumeona ni zawadi kubwa sana ya ajabu kutoka kwa Mungu.  Mungu ndiye anaondoa dhambi zetu na anatusamehe.  Halafu anatupatia utiifu kamili wa Yesu Kristo na anatutangaza kuwa wenye haki kuambatana na sheria  yake.  Je, baraka hizi za ajabu zinatufikia kwa njia gani?  Je, tumepewa baraka hizi kwa sababu tumejaribu kwa bidii zetu kuishi maisha mazuri na ya kidini?  Je, Mungu anatupatia baraka hizi za ajabu kwa sababu tumejaribu sana kutii Amri Kumi zake?  Jibu kutoka kwa Biblia ni wazi: hatuhesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa imani.

 

Imani inamaanisha kutumainia.  Tunahesabiwa haki wakati tunamtumainia Bwana Yesu Kristo pekee atuokoe kutoka kwa dhambi zetu na kutupeleka mbinguni.  Ikiwa tutajitumainia sisi wenyewe na kazi zetu nzuri basi hatutapata msamaha wa dhambi zetu.  Ni wakati tu tunaweka tumaini letu la kusamehewa dhambi na tumaini la kuingia mbinguni kwa Yesu Kristo pekee ndipo tunaokolewa.

 

Ushuhuda wa Paulo katika kitabu cha Wafilipi 3:4-11 ndiyo mfano mzuri sana kwa jambo hili.  Paulo alikuwa akizitegemea kazi zake nzuri akifikiria kwamba zitampeleka mbinguni.  Paulo alikuwa ameridhika kwamba kwa sababu yeye alizaliwa Myahudi, alitahiriwa, na aliishi maisha mema basi ataingia mbinguni bila shaka yoyote.  Wakati mwanga wa injili ulimwangazia aliona wazi kwamba mambo haya yote hayawezi kumwokoa.  Na kwa hivyo akayahesabu kuwa takataka na akaja kwa Yesu kwa imani, akimtumainia yeye pekee kwa wokovu.  Wakati Paulo alifanya hivi, alipata haki, “Ipatikanayo kwa imani katika Kristo- ile itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani” (Wafilipi 3:9).

 

4.  Mambo haya yote yanaamanisha nini maishani?

 

Labda tangu uanze kusoma funzo hili hadi ukurasa huu umekuwa ukijiuluza, “Je, si hii yote ni mafundisho ya juu sana ya Biblia, yana maana gani maishani mwangu?”  Katika sehemu hii sasa tutaangazia ni nini mafundisho haya yanamaanisha maishani mwetu.  Tutaelewa vizuri sana tukiyaangalia mafundisho haya katika maisha ya watu watatu: yaani mtu ambaye hajaokoka, mtu ambaye ameokoka na ako hapa duniani, na mtu ambaye ameokoka na ako mbinguni.

 

(i) Mtu ambaye hajaokoka.  Biblia anaeleza kwamba mtu ambaye hajaokoka ako na shida mbili kubwa sana kuhusu uhusiano wake na Mungu.  Kwanza, yeye ako na hatia mbele ya Mungu kwa sababu amevunja sheria ya Mungu, na pili hali yake ya maisha ni ya dhambi, kumaanisha kwamba maisha yake yote ni ya dhambi tupu.  Fikiria kuhusu chokora ambaye anavuta gamu na anawaibia watu vitu vyao.  Sisi sote tutasema huyu chokora si mtu mzuri bali ni mtu mbaya sana.  Fikiria kuhusu huyu chokora kwamba amemwibia mtu fulani pesa nyingi na sasa anajificha polisi wasimshike.  Chokora huyu ako na shida mbili: kwanza tabia yake si nzuri bali ni mbaya, na bali na hayo, yeye ako na hatia kwa sababu amevunja sheria ya nchi kwa kuiba pesa na sasa polisi wanamtafuta.  Hivi ndivyo alivyo mtu ambaye hajaokoka, ako na moyo mbaya na ako na rekodi mbaya.

 

(ii) Mtu ambaye ako duniani na ameokoka.  Biblia inatueleza kwamba mtu ambaye ameokoka humu duniani ako tofauti sana na yule ambaye hajaokoka kwa njia mbili.  Kwanza, mtu ambaye ameokoka hana hatia mbele za Mungu.  Dhambi zake zote zimeondolewa na amepewa haki ya Yesu Kristo.  Yeye sasa ni mtu ambaye amehesabiwa haki.  Huo uamuzi ni wa milele, na hakuna siku hata moja mtu ambaye ameokoka atakuwa na hatia mbele ya Mungu, kwa sababu Mungu ameamua mtu huyo ni mwenye haki milele.  Kwa hivyo mtu ambaye ameokoka hayuko kiwango moja na mtu ambaye hajaokoka kwa sababu yule ameokoka hana hatia mbele za Mungu. Mungu hamwambii mtu ameokoka, “Uko na hatia ya dhambi ambazo umefanya.”  Dhambi za mtu ambaye ameokoka zimewekwa juu ya Yesu Kristo na kusamehewa.

 

Pili, mtu ambaye ameokoka ako tofauti na mtu ambaye hajaokoka kwa sababu yule ameokoka anaendelea kubadilishwa ili afanane na Yesu Kristo.  Mtu ambaye hajaokoka, kama vile tumeona ako na maisha ya dhambi.  Tabia yake yote ni ya dhambi.  Mtu yule ameokoka, wakati moja alikuwa kama mtu huyu ambaye hajaokoka lakini Mungu alimwokoa.  Hii inamaanisha kwamba Mungu aliugeuza moyo wake.  Wakati alikuwa hajaokoka alipenda na kutenda dhambi, lakini sasa anaichukia dhambi na anaitoroka.  Maoni yake kuhusu dhambi yamebadilika.  Yeye hapendezwi na dhambi kamwe, anaichukia dhambi sana kwa sababu ameokoka na moyo wake umegeuzwa.

 

Pia, Mungu wakati huu anaendelea na kufanya kazi ndani ya mtu ambaye ameokoka akimgeuza ili afanane na Kristo.  Mtu ambaye ameokoka bado hajakamilika kwa sababu kuna kazi nyingi itafanyika ili mtu huyo awe mkamilifu na bila dhambi, na kazi hii haifanyiki siku moja.  Hivi ndivyo mtu anaokolewa: yaani mtu huyu hatia yake ya dhambi imeondolewa.  Mtu huyu hapendezwi na dhambi na maisha ya dhambi kwa sababu moyo wake umebadilishwa.  Tabia yake inabadilika polepole na anaendelea kufanana na Yesu.

 

(iii) Mtu ambaye ameokoka na ako mbinguni.  Kuna mambo mawili kuhusu mtu ambaye ameokoka na ako mbinguni.  Kwanza, yeye hana hatia mbele za Mungu.  Dhambi zake zote zimesamehewa na yeye ni mwenye haki kupitia imani ndani ya Yesu Kristo.  Pili, yeye amekamilika kabisa kama Yesu Kristo.  Hana dhambi yoyote inayobakia ndani mwake.  Mungu amefanya kazi ndani mwake na amemkamilisha.

 

Hii inamaanisha kwamba mtu ambaye ameokoka bado hajakuwa mkamilifu.  Hili ni jambo ambalo linawachanganya watu wengi sana hapa nchini mwetu.  Watu wengi wanatarajia mtu ambaye ameokoka kuwa mkamilifu katika kila jambo.  Lakini tukumbuke mtu ambaye ameokoka bado si mkamilifu.  Huwa inachukua muda mrefu sana kwa mtu ambaye ameokoka tabia zake zote za dhambi kuondolewa ndani mwake.  Hii ndiyo sababu wakati mchungaji anashughulika na mambo ya washirika wake anapaswa kuwa mvumilivu sana.  Kazi ya mchungaji ni kuwasaidia washirika wake kukua katika mfano wa Yesu Kristo.  Washirika wa kanisa hawatakuwa wakamilifu baada ya siku chache ama wiki chache, mshirika anaweza kuwa aliishi maisha mabaya sana kabla aokoke na hizo tabia zote ziko ndani mwake.  Huyo ndiye mtu ambaye mchungaji ameitwa amtumikie na anapaswa kumwombea na kumhimiza apigane na dhambi zake.

 

Hivi ndivyo Biblia inafundisha kuhusu kuhesabiwa haki.

 

 

Funzo la pili, Wakolosai 1:13-14, Alitukomboa kutoka katika ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana.

 

Katika kifungu hiki Biblia inasema, “Kwa maana alituokoa kutoka katika ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana Wake mpendwa, ambaye katika Yeye tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi.”  Kuna mafunzo matatu ambayo tunafundishwa hapa.

 

1.  Tunafundishwa kwamba wokovu ni kazi ya Mungu.

 

Paulo anasema katika kifungu hiki, “Ametuokoa.”  Hili ni jambo ambalo Biblia inatufundisha kila wakati, kwamba ni Mungu mwenyewe ambaye anapanga wokovu wetu na ni Mungu mwenyewe ambaye anatuokoa, “Wokovu watoka kwa Bwana” (Yona 2:9).  Biblia inaeleza wazi kwamba Mungu ndiye mwenye uwezo katika wokovu wetu.  Ni Mungu pekee ambaye anaamua ni nani ataokoka, wakati gani atamwokoa na kwa namna gani.  Hii si chaguo la mwanadamu bali ni chaguo la Mungu mwenyewe: “Haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutengemea huruma ya Mungu” (Warumi 9:16).

 

2.  Pili, tunajifunza kwamba Mungu akituokoa huwa anatutoa kutoka kwa ufalme wa giza.

 

Biblia inafundisha kwamba kuna falme mbili hapa duniani, ufalme wa Mungu na ufalme wa giza.  Biblia inatueleza kwamba sisi sote tunazaliwa katika ufalme wa giza kwa sababu tunazaliwa tukiwa wenye dhambi.  Tunazaliwa na mioyo ambayo ni ya dhambi na inapenda kufanya dhambi.  Hii ndiyo hali yetu tunapozaliwa, yaani tukiwa watoto wa giza.  Lakini Mungu anapotuokoa, hututoa kutoka kwa huu ufalme wa giza.

 

Katika msitari wa 14 Paulo anasema, “Ambaye katika yeye tunao ukombozi – msamaha wa dhambi.”  Haya ni maelezo ya jambo ambalo Mungu hufanya wakati anatutoa kwa ufalme wa giza.  Mungu anatukomboa na anatusamehe.  Wale wote ambao hawajaokoka wako na shida mbili kubwa sana: wao ni watumwa wa dhambi na pia wako na hatia mbele ya Mungu kwa sababu ya dhambi zao.  Wao ni watumwa wa dhambi kwa sababu dhambi imewanasa na kuwashika mateka na kuwafunga.  Hii ndiyo sababu watu humu duniani wanaishi maisha ya dhambi.  Ni kwa sababu dhambi ndiyo bwana wao na dhambi ndiyo inawaongoza jinsi wanavyoishi katika maisha yao.  Wao wako na hatia ya dhambi kwa sababu wamevunja sheria ya Mungu na wanahitajika kuilipia faini.  Wakati Mungu anatuokoa huwa anashughulika na haya.  Mungu anatukomboa kutoka kwa utumwa.  Kukomboa inamaanisha kumwondoa mtumwa kutoka kwa hali ya utumwa.  Bwana Yesu Kristo kupitia kifo chake msalabani aliwakomboa watu wake kutoka kwa utumwa wao.  Zaidi ya hayo Mungu alituondolea hatia kwa kutusamehe dhambi zetu.  Wakati Yesu Kristo alikufa msalabani, alikufa ili alipe faini ya dhambi zetu ili tupate msamaha wa dhambi zetu.  Hivi ndivyo Mungu anatutoa kwa ufalme wa giza, anatukomboa kutoka kwa utumwa wa dhambi halafu anatoa hatia yetu.

 

Hii inamaanisha kwamba wakati mtu ameokolewa anakuwa hayuko tena chini ya mamlaka ya dhambi.  Paulo analishughulikia jambo hili kwa undani sana katika sura ya 6 katika kitabu cha Warumi.  Anasema, “Dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema; lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa, Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.  Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki.  Lakini sasa kwa kuwa mmewekwa huru mbali na dhambi na mmekuwa watumwa wa Mungu, faida mnayopata ni utukufu, ambao mwisho wake ni uzima wa milele” (Warumi 6:14;17-18;20;22).

 

Hii haimaanishi kwamba mtu ambaye ameokoa hafanyi dhambi.  Inamaanisha kwamba sasa sisi si watumwa wa dhambi na hatuko chini ya mamlaka ya dhambi tena.  Mtu ambaye hajaokoka ni mtumwa wa dhambi na ako chini ya mamlaka ya dhambi siku zote.  Hakuna jambo lingine mwenye dhambi anaweza kufanya bali tu kutenda dhambi kila wakati.  Hakuna chochote mwenye dhambi anaweza kufanya ili ampendeze Mungu.  Hata matendo ambayo anaweza kusema ni mazuri yanatoka kwa moyo ambao ni wa dhambi.  Lakini mtu ambaye ameokoka hayuko katika hali hiyo.  Anaweza kuifanya dhambi lakini yeye si mtumwa wa dhambi.  Mtu ambaye ameokoka ako na uwezo wa kupigana na dhambi na kuiua.  Mtu ambaye ameokoka anaendelea kuondolewa kwa mamlaka ya dhambi na kubadilishwa ili afanane na Yesu Kristo.  Dhambi siyo bwana wake na haiwezi kumwongoza.  Nguvu ya dhambi ambazo ziko ndani mwake zinaendelea kuouteza nguvu kwa sababu Roho Mtakatifu anaishi ndani ya mtu ambaye ameokoka na Roho Mtakatifu anamwongoza mtu huyo kutii sheria ya Mungu (Ezekieli 36:27).

 

3.  Tatu, tunajifunza kwamba wakati Mungu antuokoka hutuleta katika ufalme wa Yesu Kristo.

 

Paulo anasema katika kifungu hiki kwamba, “Na kutuingiza katika ufalme wa Mwana Wake mpendwa.”  Wokovu wetu ni kazi kubwa ya Mungu kwa sababu mabadiliko makubwa hutokea katika maisha yetu.  Fikiria kuhusu mtu ambaye amehamia Amerika na anaanza maisha mapya huko.  Maisha yake yote huwa yanabadilika.  Vivyo hivyo wakati tunakuwa watoto wa Mungu hali yetu ya maisha hubadilika, yaani:

 

(i) Tunakuwa raia wa ufalme wa Mungu.  Kabla ya kuokolewa tulikuwa raia wa ufalme wa giza. Tulichukia nuru ya Mungu na tulikuwa tunaogopa kuja karibu na nuru ya Mungu ili dhambi zetu zisijulikane.  Kwa hivyo tuliishi maisha ya dhambi na kuyaficha mambo haya.  Sasa sisi ni watoto wa nuru.  Sasa hatuishi maisha ya aina mbili, yaani kujifanya mbele ya watu kwamba tumeokoka na kuendelea na maisha ya dhambi wakati tuko peke yetu.  Mtu yeyote anayeishi maisha kama haya hajaokoka.  Sisi sasa si watoto wa giza kwa sababu tumetolewa kutoka kwa ufalme wa giza na kuingizwa kwa ufalme wa nuru.

 

(ii) Maisha yetu yanabadilika kwa sababu tunakuwa watu wa ufalme wa Mungu.  Mtu ambaye amehamia Ulaya ama Marikani hawezi kuendelea kuishi jinsi alivyokuwa anaishi nchini mwake kwa sababu maisha ya nchi ambayo ameenda ni tofauti, hata hali ya anga ni tofauti sana.  Ni lazima aishi kulingana na mazingira ya nchi ambayo ameenda.  Vivyo hivyo mtu ambaye ameokoka amekuwa mshirika wa ufalme wa Mungu.  Ni mtu ambaye ameingia kwa ufalme ambao maisha yake ni tofauti.  Katika ufalme huu hatutumikii dhambi bali tunatumikia Yesu Kristo.  Katika ufalme huu hatuishi ili tufurahie anasa za dunia hii bali tunatumika katika ufalme wa Mungu.

Funzo la tatu, 1 Petro 3:18, tumepatanishwa na

Mungu na watu wake.

 

Katika msitari huu Petro anaandika, “Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki, ili awalete sisi kwa Mungu”.  Baraka kubwa tunayo sisi wakristo ni kwamba tumepatanishwa na Mungu.  Kuna mambo matatu muhimu sana kuhusu jambo hili ambayo tunapaswa kuyaelewa.

 

1.  Mtu ambaye hajaokoka huwa ametenganishwa na Mungu kabisa.

 

Biblia inatueleza wazi kwamba wale ambao hawajaokoka ndani ya Yesu Kristo ni maadui wa Mungu.  Siyo kweli kwamba wao ni watoto wa Mungu na kwamba Mungu anapendezwa nao, bali ukweli ni kwamba wale wote hawajaokoka wanamchukia Mungu na  wanaichukia sheria yake na kwa hivyo hao ni maadui wa Mungu.  Wanaweza kuonekana machoni pa watu wakiwa watu wazuri sana na wenye tabia za kupendeza kwa sababu wanaenda kanisani kila wiki.  Lakini ikiwa hawajaokoka kupitia kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo msalabani basi wote wametenganishwa na Mungu na hao ni maadui wa Mungu.

 

Biblia inatueleza kwamba Mungu ni mwenye huruma na mwenye neema sana na kwamba yeye huwapa mvua, jua na chakula maadui wake (Mathayo 5:44).  Lakini hii haimaanishi kwamba watu hawa ni wazuri machoni pa Mungu ama wanampendeza, bali inamaanisha  kwamba Mungu ni mwenye huruma na neema hata kuwashughulikia maadui wake.  Lakini kumbuka mwisho wa haya yote Mungu atawahukumu maadui wake milele: “Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti.  Hii ndiyo mauti ya pili” (Ufunuo 21:8).

 

2.  Mtu ambaye ameokoka amepatanishwa na Mungu.

 

Mtu anapookoka, hupokea baraka nyingi kutoka kwa Mungu.  Yeye hupokea msamaha wa dhambi na pia Mungu anamleta kwenye ufalme wake.  Baraka hizi haziishii hapo, bali baraka lile kubwa sana tunapata kutoka kwa Mungu ni kuwa tumepatanishwa na Mungu mwenyewe.  Hii ndiyo sababu kubwa kwa nini Kristo alikuja hapa ulimwenguni: “Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupatia sisi huduma ya upatanisho” (2 Wakorintho 5:19); “Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki, ili atulete sisi kwa Mungu” (1 Petro 3:18).

 

Tunapopatanishwa na Mungu huwa inamaanisha kwamba Mungu ako upande wetu wala hayuko kinyume na sisi.  Inamaanisha kwamba sisi tuko na ushirika na yeye.  Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Siwaiti ninyi watumishi tena kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu” (Yohana 15:15).  Hivi ndivyo inamaanisha kupatanishwa na Mungu.  Inamaanisha kwamba Mungu ni rafiki wetu.

 

Urafiki baina yetu na Mungu siyo kama urafiki tulionao na watu wengine hapa duniani.  Angalia tena jinsi Biblia anasema katika 1 Petro 3:18.  Biblia inasema, “Kristo aliteswa mara moja tu, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki, ili atulete sisi kwa Mungu.”  Kuna mambo mawili kuhusu urafiki wetu na Mungu katika kifungu hiki.

 

(i) Kwanza, kifungu hiki kinatueleza kwamba Mungu kamwe hatatusaliti.  Petro anasema, “Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki ili atulete sisi kwa Mungu”.  Hii inamaanisha kwamba vizuizi vyote kati ya Mungu na mwanadamu vimeondolewa: kwa sababu Kristo alikufa kwa ajiri ya dhambi zetu.  Tunajua kwamba urafiki wa humu duniani na watu wa dunia hauwezi kutengemewa.  Mtu anaweza kumwambia mwenzake, “Mimi ndiye rafiki yako mzuri,” lakini haya yote yanaweza kuwa  maneno tu.  Ndani mwa moyo wake mtu huyu anaweza kuwa na kisasi dhidi ya mwenzake, na wakati fulani unaokuja mtu huyu anaweza kumsaliti mwezake.  Humu duniani hatuwezi kuwaamini kabisa marafiki wetu.  Lakini Yesu Kristo kupitia kifo chake ametoa vizuizi vyote kati ya Mungu na watu wake, na kwa hivyo urafiki wa Mungu na watu wake ni wa kudumu.  Mungu mwenyewe ndani ya moyo wake hana chochote dhidi yetu.  Yesu anaposema, “Nimewaita ninyi rafiki” kwa kweli anamaanisha hivyo kabisa.  Kila wakati Yesu Kristo atakuwa upande wetu.  Yesu akiwa kuhani mkuu anatushughulikia mbele za Mungu na pia anatuombea.  Yesu ako na mahitaji yetu yote katika mawazo yake na kilajambo analofanya ni kwa manufaa yetu.

 

(ii) Pili, kifungu hiki kinatueleza kwamba urafiki wetu na Mungu ni urafiki wa milele.  Sisi sote tunajua kwamba mara mingi urafiki baina ya wanadamu unaweza kuwa dhaifu sana.  Wanafunzi wawili shuleni wanaweza kuwa marafiki sana, lakini kutokee jambo fulani na liharibu huo urafiki kiasi kwamba hata hawatazungumza tena.  Ama jamii mbili ambazo ziko na umoja sana, halafu jambo fulani linaweza kutokea na kukasirisha jamii moja na kwa hivyo wanakata ushirika wao wote na kuacha kuzungumziana.  Lakini Biblia inasema, “Kristo naye aliteswa mara moja tu” kumaanisha kwamba kifo cha Yesu Kristo kilifanyika mara moja tu lakini matokokeo yake ni ya milele.  Hii inamaanisha kwamba wakati Yesu Kristo alikufa msalabani, alikufa kwa ajili ya dhambi zetu zote na wakati tunapata msamaha wa dhambi, msamaha huo ni wa milele.  Hakuna siku Bwana Yesu Kristo ataacha kuwa rafiki wetu; Hakuna siku hata moja Yesu Kristo atakasirika na sisi na kukata uhusiano wetu na yeye.  Alikufa kwa sababu ya dhambi zetu, dhambi za zamani, za wakati huu na zile tutakazozifanya.

 

3.  Mtu ambaye ameokoka amepatanishwa na watu wa Mungu.

 

Biblia inatufundisha kwamba wakati Bwana Yesu anatupatanisha na Mungu, pia wakati huo huo Bwana Yesu anatupatanisha na watu wa Mungu.  Biblia inatufundisha kwamba mtu ambaye ni mwenye dhambi huwa ni adui wa Mungu, na pia ni adui wa watu wa Mungu.  Inawezekana kwamba mtu huyu ijapokuwa hajaokoka anaenda kanisani kila Jumapili na anaonekana kuwa mtu mwema na rafiki sana wa kanisa.  Lakini ukweli ni kwamba mtu huyo siyo mshirika wa kanisa, yeye ni mtu wa dunia na maisha yake yako kwa ufalme wa giza.  Wakati mtu huyu atakaokoka ndipo ataingia katika ufalme wa Mungu na ndipo atakuwa mtoto wa Mungu.  Wakati huo ndipo ataunganishwa na jamii ya Mungu.  Hii ndiyo sababu Biblia inasema, “Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume au mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu” (Wagalatia 3:28).  Kabla mtu aokoke huwa anajali sana uraia wake na kabila lake.  Anashughulika sana na kabila lake.  Lakini mtu anapookoka, mambo ya ukabila hayajalishi kwake.  Anashughulika sana na watu wa Mungu bila kujali uraia na ukabila wake.

 

 

 

 

Funzo la nne, Warumi 8:12-16, tumefanywa kuwa wana katika jamii ya Mungu.

 

Katika kifungu hiki Biblia inatueleza kwamba wakati mtu anapookoka hufanywa mwana katika jamii ya Mungu na mtu huyo anakuwa mtoto wa Mungu.  Kuna mafundisho matatu muhimu sana katika kifungu hiki.

 

1.  Kwanza, tunaambiwa kwamba wale ambao wanaongozwa na Roho Mtakatifu ni wana wa Mungu.

 

Paulo anasema katika kifungu hiki, “Wote wanaongozwa na Roho wa Mungu hao ndio watoto wa Mungu” (msitari 14).  Kifungu hiki kinatufundisha kwamba kuna watu aina mbili humu duniani: wale wanaishi kuufuata mwili (msitari 13), na wale wanaoongozwa na Roho wa Mungu (msitari 14).

 

(i).Wale wanaishi kuufuata mwili.  Biblia inafundisha kwamba tunapozaliwa humu duniani,tunazaliwa tukiwa wenye dhambi.  Biblia inatueleza kwamba tunazaliwa tukiufuata mwili (yaani tukiwa na dhambi ndani yetu) na ni kwa sababu hii tunatamani na tunapenda dhambi.  Tunazaliwa tukiwa maadui wa Mungu na tukiwa tunachukia sheria ya Mungu.  Hii ndiyo hali yetu tunapozaliwa, na tunabaki katika hali hii hadi Mungu anapotuokoa.  Ikiwa Mungu hatuokoi tunabaki katika hali hii na kufa tukiwa katika hali hii.  Mtu ambaye hajaokoka basi huishi katika hali ya dhambi.  Hii inamaanisha kwamba mtu huyu anaishi ili apendeze tamaa zake za dhambi.  Ukimwangalia mtu huyu kwa kawaida anaweza kuonekana mtu wa dini sana na hata anaweza kuwa anajiita mkristo.  Anaweza kuwa anakuja kanisa kila Jumapili na kujulikana na watu kuwa mtu mzuri sana, lakini ikiwa hajaokoka yeye ni mwenye dhambi na anaishi maisha ya kupendeza tamaa za dhambi kila wakati.  Ukiyachunguza maisha yake utapata kwamba nia yake kuu si kumpendeza Mungu.  Utapata kwamba mtu huyu nia yake kuu ni anasa na mali za dunia hii, na anazitafuta kwa moyo wake wote.  Hata utapata kwamba matendo yake ya dini siyo ya kumpendeza Mungu, bali matendo yake ya kidini ni ya kujipendeza mbele za watu ili aheshimiwe, na kwa haya yote anatumainia kwamba Mungu atampa baraka.  Huyu ndiye mtu ambaye anaishi kuufuata mwili.

 

(ii).Mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu.  Biblia inatuambia kwamba mtu ambaye  ameokoka, Roho Mtakatifu huja na kuishi ndani yake.  Hii ndiyo sababu katika kifungu hiki Paulo anasema, “Mtu yeyote ambaye hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo” (Warumi 8:9).  Roho Mtakatifu huja kuishi kwa kila mtu ambaye ameokoka na anamwongoza mtu huyo katika maisha ya utakatifu.  Mungu anasema hivi kwa kila mtu ambaye ameokoka, “Nitaweka Roho yangu ndani yenu na kuwafanya ninyi mfuate amri zangu na kuwafanya kuwa waangalifu kuzishika sheria zangu” (Ezekieli 36:27).  Roho wa Mungu ni Roho Mtakatifu na kazi yake ni kuwafanya watu wa Mungu kuwa watakatifu.  Roho Mtakatifu hufanya kazi ndani ya kila mtu ambaye ameokoka, akimpa kila mtu ambaye ameokoka hamu ya kuchukia dhambi na hamu ya kumpenda na kumtumikia Mungu.

 

Mtu ambaye ameokoka ataendelea kuwa na mabadiliko makubwa mwaka baada ya mwaka.  Maisha yake yanabadilika na haongozwi na dhambi kama zamani.  Hii haimaanishi kwamba yeye hafanyi dhambi ama amekamilifu.  Lakini hii inamaanisha kwamba polepole mtu huyu anabadilika kufanana na Kristo.  Hii ndiyo sababu Biblia inasema, “Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, Yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa, kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu” (Warumi 8:11).  Wale wote wanaongozwa na Roho wa Mungu ni wana wa Mungu.

 

2.  Pili, tunaambiwa kwamba wale ambao ni wana wa Mungu wao si watumwa wa uoga.

 

Biblia inasema katika kifungu hiki, “Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu” (msitari 15). Wale ambao hawajaokoka huishi maisha ya kuogopa.  Kuna mambo matatu ambayo wale hawajaokoka huogopa.

 

(i).Wanaogopa Mungu.  Mtu ambaye hajaokoka anajua kwamba Mungu ni mwenye uwezo na mwenye nguvu na kwamba anathibiti kila kitu.  Pia anajua kwamba dhambi zake ni hatia mbele za Mungu na Mungu anazichukia.  Hii ndiyo sababu mtu ambaye hajaokoka huishi akimwogopa Mungu.  Anajua kwamba hukumu ya Mungu iko juu yake na kwamba Mungu anaweza kuangamiza maisha yake yote siku moja.  Anaweza kuwa ni tajiri mwenye mali nyingi na pesa mingi, lakini anajua kwamba Mungu ndiye mwenye uwezo na anaweza kuchukua mali yote aliyo nayo na pesa zake zote na hata achukue uhai wake.  Hii ndiyo sababu wengi wanajaribu kutenda mambo mazuri iliwapate baraka za Mungu.  Wataenda kanisani kila Jumapili na kutoa sadaka kubwa wakitarajia Mungu atapendezwa na kujitolea kwao na hatawaangamiza.  Kwa sababu hawana uhakika kama Mungu anapendezwa nao wanaishi kwa uoga sana.

 

(ii).Wanamwogopa shetani.  Watu wengi wanajua kwamba shetani ni adui ambaye ana nguvu sana na anaweza kuangamiza maisha ya mtu.  Wanajua kwamba shetani anaweza kuwashambulia na hawatakuwa na chochote cha kufanya, na kwa hivyo wanaishi kwa uoga sana.  Hii ndiyo sababu watu wengi watajaribu kumpendeza Mungu, wakitarajia kwamba atawalinda dhidi ya shetani.  Hii pia ndiyo sababu wengi wao wanaenda kwa waganga na kuwapatia pesa nyingi kwa sababu wanaamini mganga anaweza kumzuia shetani hili asiwangamize.

 

(iii).Wanaongopa kifo.  Kwa wale hawajaokoka kifo kwao ni kitu cha kutisha sana kwa sababu ni kama mlango ambao hawajui unakoelekeza watu.  Watu wengi wanajua kwamba wamefanya dhambi machoni pa Mungu na kwamba Mungu atawahukumu jahanum milele.  Hii ndiyo sababu wanaongopa kifo.  Wakati wanapopatwa na magonjwa wanajaribu sana wawezavyo ili wazuie kifo.  Watu hawa watatumia mamilioni ya pesa kwa mahospitali wakitumainia kuendelea kuishi humu duniani.  Mtu huyu akisikia tu kama kuna laana fulani juu yake, anajaribu sana, tena kwa haraka kwenda kwa mganga na ampatie pesa nyingi sana ili atoe hiyo laana.  Wakati mmoja wa jamii yake amefariki mtu huyu atahakikisha kwamba kila aina ya mila zimefanywa na kutimizwa wakati wa kuzika marehemu ili mapepo ya yule aliyekufa yasiwazsumbue.  Kifo ni kitu ambacho wale hawajaokoka wanaongopa sana.

 

Kwa hivyo mtu ambaye hajaokoka ni mtumwa wa uoga.  Maisha yake yote yanatawaliwa na uoga.  Lakini mtu ambaye ameokoka, ametolewa kwa uoga huu.  Bwana Yesu alikuja, “Kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu, tupate kumtumikia yeye pasipo hofu” (Luka 1:74).  Yule ambaye ameokoka hamwongopi Mungu kwa sababu Mungu ni Baba yake.  Yeye sasa ni mtoto wa Mungu na Mungu anampenda na anamlinda.  Wakati Biblia inatuambia, “Enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni” (1 Petro 1:17), inamaanisha tumheshimu Mungu wetu na tumpenda na tusimwongope kama wale wasioamini.

 

Kwa kawaida mtoto anawagopa wale hawajui lakini si baba yake, vivyo hivyo mtu ambaye ameokoka amwongopi Mungu kwa sababu Mungu ni baba yake.  Mtu ambaye ameokoka hamwogopi shetani kwa sababu anajua Mungu ndiye mwenye uwezo wote na ndiye anatawala kila kitu. Na pia anajua kwamba Mungu analitumia kila jambo kwa faida wa yule ameokoka.  Kwa hivyo wakati shida na shaka zinakuja maishani mwake, yeye hataanza kumwogopa shetani, bali anajua Mungu anatumia mambo yote kwa kumletea faida;.  Pia anajua kwamba majaribu anayoyapatia, Mungu anayatumia kuhakikisha imani yake (1 Petro 1:7), na ili apate kuwa kamilifu (Yakobo 1:2-4).  Pia mtu ambaye ameokoka haogopi kifo kwa sababu anajua kwamba atakuwa na Bwana Yesu milele akikufa.  Mtu ambaye ameokoka akipewa kuchagua kati ya kuishi huku duniani na kufa, yeye atasema, “Lakini sijui nichague lipi?  Mimi sijui!  Ninavutwa kati ya mambo mawili:  Ninatamani kuondoka nikae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi; Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili” (Wafilipi 1:22-24).

 

Kwa hivyo mtu ambaye ameokoka na amefanywa mwana katika jamii ya Mungu yeye si mtumwa wa uoga.  Mtu huyu hatarudi kwa yale mambo aliyoyaamini kabla hajaokoka.  Yeye ameondolewa kwa uoga huu na anaendelea kusherekea uhuru ambao Kristo amempatia.

 

3.  Tatu, tunaambiwa kwamba wakati tunaokoka huwa tunaingia katika uhusiano wa ndani sana na Mungu.

 

Paulo anasema katika kifungu hiki, “Mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, 'Abba,' yaani Baba.  Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu” (Warumi 8:15-16).  Neno “Abba” lilikuwa neno ambalo mtoto alikuwa anatumia wakati anazungumza na baba yake ambaye wako na uhusiano wa karibu sana.  Neno “Abba” linamaanisha kwamba kuna uhusiano wa karibu sana baina ya baba na mtoto.  Mtu ambaye ameokoka amefanywa kuwa mwana wa Mungu na kwa hivyo anaingia katika uhusiano wa karibu sana na Mungu mwenyewe.  Roho wa Mungu aliye ndani yetu anatuwezesha kuingia katika uhusiano huu.  Uhusiano kati ya Mungu na mtu ambaye ameokoka unaonekana kwa njia tatu katika maisha yake ya kila siku.

 

(i) Mtoto wa Mungu atakuwa na ushirika na Mungu kila siku.  Hivi ndivyo mambo yalivyo katika kila jamii kila mahali.  Mtoto anapenda kuwa na wazazi wake, na anapenda kuwaeleza jinsi anavyofanya shule, michezo anayocheza shuleni na mambo mengine.  litaonekana jambo la ajabu mtoto akikosa kuongea na wazazi wake.  Watoto hupenda kuongea na wazazi wao kila siku na kuwa pamoja nao.  Vivyo hivyo mtu ambaye ni mtoto wa Mungu anapenda sana kuwa katika ushirika na Mungu.  Mtu huyu atasoma neno la Mungu kila wakati kwa sababu Baba yake wa mbinguni anazungumza naye kupitia kwa neno lake.  Atakuwa na muda wa maombi kila siku kwa sababu hivyo ndivyo anaongea na Mungu na anamshukuru Mungu kwa sababu ya baraka zake za ajabu.  Mtu huyu atakuwa na ushirika na watu wa Mungu kwa sababu akishirikiana nao anashirikiana na Mungu mwenyewe.

 

(ii) Mtoto wa Mungu kila wakati atakuwa na hamu ya kumpendeza Mungu kwa kumwabudu, kumtii na kumtumikia.  Watoto wote wako na hamu ya kuwapendeza wazazi wao.  Wanataka wazazi wapendezwe na maisha yao na waongee mambo mazuri kuwahusu.  Mtoto hufuraia sana wakati mzazi anamwambia kwamba, “Umefanya vizuri sana, nimependezwa nawe.”  Hili ni jambo ambalo mtoto hufurahia sana kusikia kutoka kwa wazazi wake.  Vivyo hivyo mtoto wa Mungu hupenda sana kumfurahisha baba yake wa mbinguni.  Atasoma Biblia kila wakati ili ajue ni nini Mungu anapenda halafu anafanya hivyo.  Anajua kwamba Mungu anataka yeye aishi maisha ya kumwabudu na kumtii na kwa hivyo atafanya hayo yote kwa nguvu zake zote ili Mungu apendezwe naye.

 

(iii) Mtoto wa Mungu kila siku atakua ili awe jinsi Mungu alivyo.  Kwa kawaida watoto wanafurahia kuwa jinsi wazazi wao walivyo na wanapenda wawe kama wazazi wao.  Hivi ndivyo watoto wanawapenda wazazi wao, yaani wanafuata desturi zao kila siku maishani mwao.  Vivyo hivyo mtoto wa Mungu anafurahia sana kuwa na tabia kama ya Baba yake wa mbinguni.  Yesu alisema, “Iweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Mathayo 5:48), na hivi ndivyo mtoto wa Mungu atafanya.  Atakuwa mtu mwenye huruma, mkarimu, mwenye upendo kwa wengine na kuwajali wengine jinsi Baba yake Mungu alivyo.  Mtoto wa Mungu atachukia dhambi na ataishi maisha matakatifu kama tu Baba yake wa mbinguni.  Hivi ndivyo mtu huyu anaonyesha kuwa na uhusiano wa ndani sana na Mungu.

 

 

 

Funzo la tano, Warumi 8:16-27, tumepewa

hakikisho na Roho Mtakatifu.

 

Kifungu tunachokisoma katika funzo hili ni mojawapo ya vifungu muhimu sana katika Biblia.  Paulo katika kifungu hiki anaongea kuhusu kufanywa wana wa Mungu, na jinsi Roho Mtakatifu anavyofanya kazi ndani ya watoto wa Mungu.  Kuna mafunzo matatu muhimu sana hapa.

 

1.  Roho Mtakatifu anatupatia hakikisho.

 

Paulo anasema, “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu” (msitari 16).

 

Kile Paulo anamaanisha ni kwamba Roho Mtakatifu anatuhakikishia kwamba sisi ni watoto wa Mungu.  Tunaweza kujiuliza swali, “Je, ni kwa nini Roho Mtakatifu afanye hivi?  Je, ni kwa nini Roho Mtakatifu aje na kuishi ndani yangu na kunipa hakikisho kwamba mimi ni mtoto wa Mungu?”  Jibu ni kwamba, kama vile tumeona katika funzo la kwanza, sisi ni watakatifu na pia sisi ni wenye dhambi.  Yaani sisi ni watoto wapendwa wa Mungu.  Mungu ametuokoa kwa damu ya Yesu Kristo na ametuhesabia haki.  Mungu ametusamehe dhambi zetu zote na akaamua kwamba sisi hatuna hatia bali sisi ni wenye haki.  Lakini dhambi bado himo ndani mwetu.  Ni kweli Mungu ametuokoa na ametusamehe lakini bado tuko na tabia ya dhambi ndani mwetu na mara mingi tunaanguka dhambini kila siku.  Hii ndiyo sababu Mungu ametupatia Roho Mtakatifu, ili atupatie hakikisho hata wakati tunaanguka dhambini ili tukumbuke tungali watoto wake.  Kuna mambo mawili muhimu sana ambayo tunapaswa kuelewa kuhusu hakikisho.

 

(i) Ikiwa Roho Mtakatifu hangeishi ndani yetu na kutupatia hakikisho, basi ukristo wetu ungekuwa katika hali mbaya.  Ni jambo la kuhuzunisha lakini hivi ndivyo wakristo wengi walivyo nyakati hizi, yaani wameokoka kweli lakini hawaelewi ukristo ni nini na unahusu nini na hawaelewi hakikisho linapatikana wapi.  Kwa sababu hii utapata wengi ambao wameokoka wakitafuta hakikisho katika kazi zao mzuri.  Wanafikiria kwamba bora tu unaishi maisha mazuri na unamwamini Mungu basi ukifa utaingia mbinguni.  Hii inamaanisha hakikisho lao liko katika kazi zao.  Kuna wengine ambao wameokoka kweli lakini wanasumbuka akilini mwao sana kwa sababu wanaona kwamba dhambi ingali ndani mwao na wanashindwa kupingana nayo.  Kwa sababu hii wanakuwa nashaka kama kweli wameokoka.

 

(ii) Ikiwa hakikisho la mtu halitoki kwa Roho Mtakatifu, basi mtu huyo hajaokoka.  Kuna watu nchini mwetu leo ambao watakuambia kwamba wao wameokoka na wanaenda mbinguni.  Ukiongea nao unaelewa kwamba hakikisho lao liko kwa kazi zao wanazozifanya.  Watasema, “Niliamua kumchukua Yesu, na mimi ninaenda kanisani kila Jumapili.  Ninajaribu sana niwezavyo kuishi maisha mazuri na ninajua kwamba Mungu anapoziangalia bidii zangu, anapendezwa nami na ataniruhusu kuingia mbinguni.”  Hakikisho la mtu huyu liko kwa yeye mwenyewe na kazi anazozifanya.  Roho Mtakatifu hajampa hakikisho lolote, ni yeye tu amejipatia hakikisho hilo. Mtu kama huyu anapaswa kujichunguza sana kama ameokoka.

 

Tunahitaji kuelewa kwamba hakikisho letu halitoki kwetu bali hutoka kwa Mungu.  Ni Roho Mtakatifu ambaye anatupatia hakikisho hili.

 

2.  Roho Mtakatifu anatuhakikishia kwamba sisi tu watoto wa Mungu.

 

Angalia kwa makini vile Paulo anasema katika kitabu cha Warumi 8:16.  Paulo hasemi, “Roho Mtakatifu mwenyewe hushuhudia na roho zetu kwamba tumeokoka.”  Bali anasema, “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu kwamba sisi tu watoto wa Mungu.”  Kile Biblia inasema hapa ni kwamba Mungu anapotuokoa, tunakuwa watoto wake.  Hii inamaanisha kwamba tuko na ulinzi wa milele kutoka kwake.  Ikiwa mtoto amemkasirisha baba yake kwa kutenda jambo mbaya, baba yake anaweza kumwadhibu mtoto huyo.  Baba hawezi kumkataa mtoto wake na kusema, “Wewe si mwanangu tena.”  Hata ikiwa makosa mtoto aliyoyafanya yalikuwa makubwa sana, na hata kama adhabu mtoto aliyopewa na babake ilikuwa kubwa sana, mtoto huyu anazidi kuwa wa babake.  Hakuna mabadiliko yanatokea katika jamii yake.  Vivyo hivyo tunapookoka, tunakuwa watoto wa Mungu.  Tukianguka kwa dhambi baada ya kuokoka, Mungu atatuadhibu.  Kuadhibiwa haimaanishi kwamba Mungu ametuacha na kusema, “Wewe si mtoto wangu tena.”  Mungu hawezi kufanya jambo hilo.  Ukweli ni kwamba, kwa sababu anatuadhibu tukikosa inamaanisha kweli sisi ni watoto wake: “Bwana huwaadhibisha wale awapendao na humwadhibu kila mmoja anayemkubali kuwa mtoto wake.  Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu.  Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadhibishwa na mzazi wake?  Kama hakuna kuadhibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto haramu wala si watoto halali” (Waebrania 12:6-8).

 

Kwa hivyo kazi ya Roho Mtakatifu ndani yetu ni kutuhakikishia kwamba sisi tu watoto wa Mungu.  Ni kutuakikishia kwamba sisi ni watoto wa milele wa Mungu na kwamba wokovu wetu ni wa milele na hatuwezi kuupoteza kamwe.  Hii ndiyo kazi Roho Mtakatifu anafanya ndani yetu.

 

3.  Roho Mtakatifu hutuhakikishia kwamba sisi ni warithi wa Mungu.

 

Katika kitabu cha Warumi 8:17-27, Paulo anasema kwamba wale wameokoka wamefanywa wana wa jamii ya Mungu na sasa ni warithi wa Mungu.  Mrithi ni mtu ambaye ataachiwa au kupewa kitu fulani.  Mara mingi utasikia mtu akisema, “Huyu ni mwanangu na mrithi wangu,” akimaanisha siku moja mtu huyo ndiye atapata mali yake yote.  Katika kifungu hiki cha Warumi Paulo anasema, “Ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo” (Warumi 8:17).  Je, Paulo anamaanisha nini anaposema hivi?  Urithi wa watoto wa Mungu ni gani?

 

Bwana Yesu Kristo alifundisha kwamba sisi watoto wa Mungu tutarithi vitu viwili.  Alisema, “Amin amin nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, wakati mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti cha utukufu cha enzi, ninyi mliomfuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.  Kila mmoja aliyeacha nyumba au ndugu zake wa kiume au wa kike au baba au mama au watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo na utaurithi uzima wa milele.”(Mathayo 19:28-29).  Hivi ndivyo vitu viwili ambavyo watoto wa Mungu watarithi.

 

(i) Tutaurithi uzima wa milele.  Yesu alisema, “Kila mtu aliyeacha nyumba au ndugu zake wa kiume au wa kike au baba au mama au watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo, na ataurithi uzima wa milele.”  Wakati Yesu anaposema kuhusu ufalme wa milele, anamaanisha wokovu wa milele.  Anamaanisha kwamba tutakamilishwa ili tusiwe na dhambi kamwe ndani yetu na tena tutaishi naye milele.  Haya ndiyo maisha Yesu anamaanisha, yaani kuwa wakamilifu na kuwa na ushirika wa milele na Mungu.

 

(ii) Tutarithi mbingu na nchi mpya.  Mathayo 19:28 Yesu anasema, “Wakati wa kufanywa upya vitu vyote.”  Je, hii inamaanisha nini?  Biblia inasema katika Zaburi 37:10-11, “Bado kitambo kidogo, waovu hawataonekana, ingawa utawatafuta, hawataonekana.  Bali wanyenyekevu watarithi nchi na watafurahia amani tele.” pia Bwana Yesu alisema, “Ni heri walio wapole, maana hao watarithi nchi” (Mathayo 5:5).  Vifungu hivi viwili vyote zinatueleza kwamba wakati Yesu Kristo atakaporudi mara ya pili, mambo mawili yatafanyika.  Wale hawajaokoka watahukumiwa na kutumwa jahanum, na wale wameokoka watarithi nchi.  Paulo anasema katika Warumi 8:20-22, “Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitikisha katika tumaini.  Ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka katika utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.  Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa uchungu kama utungu wa wakati wa mwanamke kuzaa hata sasa.”

 

Kile Biblia inatufundisha hapa ni kwamba wakati Adamu na Hawa walianguka dhambini wakiwa katika bustani la Edeni, Mungu alilaani nchi.  Hii ndiyo sababu tuko na miiba na mibaruti na kiangazi na mafuriko, mitetemeko ya ardhi na majanga mengine mengi.  Hii nchi imelaaniwa na Mungu.  Lakini Biblia inatueleza kwamba Kristo atakaporudi, hii laana itaondolewa: “Ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka katika utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu” (Warumi 8:21).  Nchi itarudishwa katika hali yake ya zamani iliyokuwamo kabla Adamu na Hawa kutenda dhambi, na wote ambao wameokoka watarithi nchi, ndipo patakuwa makao yao milele.

 

Huu ndio ulikuwa mpango wa Mungu alipowaumba Adamu na Hawa.  Aliwaweka katika bustani ya Edeni ili wailime na kuitunza  (Mwanzo 2:15).  Kwa hivyo wakati Bwana Yesu Kristo atakaporudi, mpango wa mwanzo wa Mungu kwa mwanadamu utafufuliwa.  Wale wameokoka ndani ya Yesu Kristo watawekwa katika nchi ili wafanye kazi na kuitunza.  Hii itakuwa ni nchi mpya kwa sababu laana ya dhambi itaondolewa na nchi itakuwa kamilifu tena, na zaidi Mungu mwenyewe atakuwa nasi: “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita---Nami nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, 'Tazama, makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao.  Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.  Atafuta kila chozi, kutoka katika macho yao.  Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita” (Ufunuo 21:1, 3-4).  Huu ndio urithi wetu sisi watoto wa Mungu.

 

 

 

Funzo la sita, Waefeso 5:25-27, tunaendelea

kugeuzwa ili tufanane na Kristo.

 

Katika kifungu hiki Paulo anaandika, “Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo alivyolipenda kanisa akajitoa kwa ajili yake.”  Halafu anaendelea mistari wa 26-27 kuonyesha ni kazi gani Kristo anayolifanyia kanisa ili liwe tayari wakati atakaporudi.  Kuna mambo matatu muhimu sana ambayo Paulo anafundisha hapa.

 

1.  Yesu Kristo anaendelea na kufanya kazi ya kutakasa kanisa lake.

 

Mtume Paulo anasema kwamba Yesu Kristo, “Akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika neno lake.”  Hii inamaanisha kwamba kuna kazi inaendelea hapa duniani leo ambapo Bwana Yesu Kristo anawatakasa watu wake kutoka kwa dhambi zao.  Yesu anaendelea na kufanya kazi kwa watu wake, wale amewaokoa kwa damu yake.  Anaendelea na kufanya kazi ndani yao, akiwaosha dhambi zao.

 

Ili tuelewe jambo hili vizuri, tunahitaji kuelewa hali ya mtu ambaye hajaokoka.  Mtu ambaye hajaokoka ako na shida mbili kubwa:

 

(i) Ako na hatia ya kuvunja sheria ya Mungu.

(ii) Yeye ni mwenye dhambi.

 

Mfano huu utasaidia kuelewa jambo hili.  Fikiria kuhusu chokora akiwa mtaani.  Mtoto huyu alizaliwa mtaani na maisha yake yote ameishi mtaani.  Katika maisha yake yote amekuwa na tabia mbaya sana za dhambi, kama kuvuta bangi, kuvuta gamu na kutisha watu na kuwaibia pesa na mambo mengine mengi mabaya.  Haya yote ni mambo ambayo yamemwingia moyoni mwake kwa miaka mingi.  Siku moja mtoto huyu anamwona mwanamke akitembea akiwa na kibeti mkononi mwake, halafu huyo kijana wa mtaa anamnyang'anya huyu mama kibeti chake na kukimbia nacho na kutoa pesa zilizoko ndani zote.  Mama huyu anaenda kwa kituo cha polisi na kuripoti mambo haya.  Hii inamaanisha kwamba kijana huyu ni mtu mwenye tabia mbaya sana na tena amevunja sheria ya nchi.  Polisi watakapompata watampeleka kotini na atapatikana na makosa na kufungwa jela.

 

Wale ambao hawajaokoka, wako katika hali hii.  Kama huyu kijana wa mtaa, wamevunja sheria ya Mungu na pia wamejawa na tabia mbaya sana.  Hawa wameishi maisha ya dhambi kwa miaka mingi.  Mioyo yao ni mioyo ya dhambi na maisha yao yote ni ya dhambi tupu.

 

Mungu anapomwokoa mtu, kuna shida mbili anashughulikia kwa sababu mtu amevunja sheria na pia hali yake ya hasili ni ya dhambi.  Mambo haya mawili ni lazima yashughulikiwe ikiwa mtu ataokolewa.  Jambo la kwanza Mungu anafanya ni kushughulika na hatia ya huyu mtu.  Kama vile tumeona katika funzo la kwanza, Mungu huwa anachukua rekodi ya mwenye dhambi na kuiweka kwa rekodi ya Yesu Kristo, halafu anachukua rekodi ya Yesu Kristo ya utiifu kamili na kuiweka kwa rekodi ya yule mtu anayeokolewa.  Mungu akisha fanya hivi, anaamua kwamba huyu mtu ni mwenye haki: yaani kulingana na sheria yake mtu huyu hana hatia.  Hadi hapo Mungu anakuwa amemaliza kushughulikia shida ya kwanza, mtu huyu sasa hana hatia ya kuvunja sheria ya Mungu, dhambi zake zote, za wakati uliopita, wakati wa sasa na hata wakati ujao zimewekwa kwa Kristo Yesu .  Mtu huyu sasa ni mwenye haki milele kupitia kwa imani ndani ya Yesu Kristo.

 

Kufika hapo shida imetatuliwa nusu.  Mtu huyu tabia yake ni ya dhambi.  ako na moyo  unaopenda dhambi na ako na tabia nyingi sana za dhambi ambazo alikuwa akifanya kwa miaka mingi.  Mungu anashughulikia jambo hili wa kumpa mtu moyo mpya.  Hivi ndivyo tunamaanisha tunaposema kwamba mtu amezaliwa mara ya pili.  Moyo wake wa dhambi umeondolewa na kupewa moyo mpya, ambao unachukia dhambi na unapenda utakatifu.  Kumbuka hii haimaanishi kwamba mtu huyu sasa hana dhambi.  Tabia yake ya dhambi bado imo ndani mwake na inafaa kushughulikiwa.  Huu moyo mpya unampatia mtu hamu mpya ya mambo ya Mungu lakini haumfanyi kuwa mkamilifu papohapo.  Ni lazima mtu huyu aoshwe tabia zake za dhambi alizo nazo.

 

Hili ni jambo ambalo watu wengi wanafanya wamekosea humu nchini.  Waanamini kwamba mtu ambaye ameokoka ni mkamilifu na mtakatifu na hana dhambi kamwe.  Tunajua kwamba hii si kweli, kwa sababu tunaweza kuficha dhambi sana na kujionyesha kuwa watu watakatifu sana mbele ya wenzetu lakini ndani mioyoni mwetu tunajua ukweli huu kwamba tunafanya dhambi.  Tunajua kwamba mtu ambaye ameokoka anaweza kuwa na dhambi kama, kuwa mchoyo, mwongo,mlevi, mwizi.  Mtu ambaye ameokoka ni mtu amehesabiwa haki na anaendelea na kuoshwa dhambi ambazo ziko ndani mwake.  Huyu ni mtu ambaye Roho Mtakatifu anaishi ndani yake na pia dhambi iko ndani yake.  Hawa wote wawili wako ndani yake.

 

Hii ndiyo sababu Paulo  alisema, “Kwa hivyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.  Kwa maana mwili hutamani yaliyo kinyume na Roho, nayo Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili.  Roho na mwili hupingana kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka” (Wagalatia 5:16-17).  Kifungu hiki kiliandikiwa watu ambao wameokoka.  Angalia kwa makini ni nini Paulo anasema hapa.  Anaanza kwa kusema enendeni kwa Roho wala hamtazitimiza tamaa za mwili.  Hii inamaanisha tuko na tamaa za dhambi ndani mwetu na hatupaswi kuzitimiza kamwe, bali tunapaswa kuenenda katika Roho.  Katika msitari wa 17 Paulo anasema hawa wawili wako ndani yetu, yaani tamaa za dhambi na Roho Mtakatifu.  Hawa wawili wako ndani yetu na wanapigana.  Kwa hivyo dhambi iko ndani mwetu na pia Mungu Roho Mtakatifu ako ndani yetu akiondoa  dhambi.

 

Jambo hili tunaliona wazi katika maisha ya mtume Paulo.  Alikuwa mtu ambaye alitesa kanisa kwa sababu alikuwa anamchukia Kristo.  Paulo alikuwa na moyo wa dhambi na alivunja sheria ya Mungu na alikuwa na hatia mbele za Mungu.  Hatia yake ya dhambi iliondolewa kwa sababu Yesu Kristo alilipa faini ya dhambi zake.  Paulo alipewa moyo mpya na akaanza kumpenda Mungu na kupenda kumtumikia Mungu kwa moyo wake wote.  Paulo alikuwa na dhambi dani mwake ambazo  zilihitajika kuondolewa polepole.

Hivi ndivyo Kristo anafanya wakati anatuokoa.  Kwanza Kristo analipa faini ya dhambi zetu na anatupatia haki ili tuwe bila hatia, halafu anaanza kazi ya kutufundisha jinsi tunapaswa kuishi na kuondoa njia za dhambi ndani yetu.

 

Mungu anaendelea na kazi yake ndani yetu akituosha ili tamaa za mwili zilizo ndani yetu ziendelee kutoka.  Kazi hii ni ya maisha yetu yote.  Hii siyo kazi inamalizika haraka.  Hii ni kazi inaendelea kila wakati na tunayo sehemu yetu ya kushiriki katika kazi hii.  Ni Kristo mwenyewe anayetuosha, lakini tunaambiwa tutimize wokovu wetu kwa kuogopa na kutetemeka (Wafilipi 2:12); tunaambiwa “Ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na kutamani, ambayo ndiyo ibada ya sanamu” (Wakolosai 3:5).

 

Hili ndilo jambo la kwanza Paulo anafundisha kutoka Waefeso 5:26.  Anafundisha kwamba Kristo anaendelea na kazi ya kutuosha na kututakasa.

 

2.  Kristo anatuosha kwa neno lake.

 

Paulo anaendelea kusema katika Waefeso 5:26, “Kusudi alifanye takatifu, alitakase kwa kuliosha kwa maji katika neno lake.”  Watu mara mingi huchanganyikiwa sana wanaposoma msitari huu kwa kufikiria kwamba Paulo anaongea kuhusu ubatizo kwa sababu ametaja maji, lakini hii si kweli.  Paulo anatumia maji  kama mfano.  Kama vile maji yanatumika kuosha miili yetu na nguo zetu, vivyo hivyo neno la Mungu linatuosha sisi.  Njia ile Mungu anatumia kutoa dhambi ambazo ziko ndani yetu ni neno lake.  Neno la Mungu ni kama zabuni ambayo Mungu anatumia kutuosha, kututakasa na kutukamilisha.  Hii ndiyo sababu Bwana Yesu Kristo aliomba kwa Baba, “Uwatakase kwa ile kweli, Neno lako ndilo kweli” (Yohana 17:17).  Mungu hutumia neno lake kutuosha na kutukamilisha.  Hii inamaanisha mambo mawili yanayohusu maisha yetu.

 

(i) Kwanza, tunapaswa kuhakikisha kwamba tunasoma na kuelewa neno la Mungu kila siku.  Biblia inasema, “Haya ndiyo mapenzi ya Mungu ninyi mwe watakatifu” (1 Wathesalonike 4:3).  Yaani ni mapenzi ya Mungu Baba kwamba dhambi zilizo ndani mwetu zitolewe na tutakaswe ili tuwe kama yeye.  Haya ndiyo mapenzi ya Mungu.  Na njia ambayo Mungu anatatumia kufanya mambo haya ni kupitia kwa neno lake, kwa sababu anatumia neno lake kutuosha.  Kwa hivyo ni wajibu wa kila mkristo kusoma na kuelewa Biblia kila siku.  Hili si jambo ambalo linafanywa na mchungaji peke yake bali ni jambo ambalo kila mtu ambaye ameokoka lazima afanye.

 

(ii) Tunapaswa kuenda kanisa ambalo linafundisha neno la Mungu kwa uaminifu.  Kuna  maelfu ya makanisa ambapo neno la Mungu linahubiriwa humu nchini mwetu kila wiki.  Lakini tukichunguza kwa makini tunapata kwamba si neno la Mungu linahubiriwa, yaani mahubiri hayo hayatoki kwa Biblia.  Ni wajibu wetu kuhudhuria kanisa ambapo mchungaji anasoma kifungu kutoka kwa Biblia halafu anafafanua ni nini kifungu kinaeleza.  Ikiwa mchungaji hatafanya hivi mahubiri hayo hayatatufaidi kamwe.  Yanaweza kutufurahisha kwa muda kidogo lakini hayatatuzaidia kuoshwa kutoka kwa dhambi zetu.  Ni lazima tuhakikishe kwamba tunasikiliza mafundisho ya Biblia ambayo ni ya ukweli.

3.  Siku moja Kristo atatuwasilisha kwake mwenyewe kama bibi arusi aliye kamilika.

 

Paulo anasema katika Waefeso 5:27, “Apate kujiletea kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu lisilo na hatia.”  Bwana Yesu Kristo hako kazini ndani ya watu wake, akihakikisha kwamba wao wamekamilika, wamekuwa wasafi na watakatifu.  Hii ndiyo kazi Bwana Yesu anafanya na ataikamilisha: “Nina hakika kwamba, yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu” (Wafilipi 1:6).  Hii inamaanisha kwamba Kristo Yesu atahakikisha kwamba wakati atarudi tutakuwa tumekamilika.

 

Mtu ambaye ameokoka kwa kweli ako na hii faraja kutoka kwa Mungu.  Anaweza kuwa na dhambi nyingi ambazo zimejaa ndani mwake na wakati mwingine anaweza kujihisi kama ameshindwa na hizo dhambi.  Lakini akiwa ameokoka kweli basi Kristo anamhakikishia kwamba siku ile atarudi atakuwa amekamilika kwa kila hali.  Atakuwa mtakatifu, msafi na mkamilifu kama Kristo mwenyewe.  Hii ni hakikisho la Kristo.  Tumaini la mbinguni ni tumaini la kweli, limehakikishwa.  Kwa sababu tumepewa hakikisho hili la mbinguni, basi tuhakikishe tunapiga vita dhambi na kuiua na kuufuata utakatifu na kuwa kama Kristo kabisa.  “Wapenzi, sasa tu watoto wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua ya kwamba, Yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo.  Kila mmoja mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama vile Yeye alivyo mtakatifu” (1 Yohana 3:2-3).

 

 

 

 

Funzo la saba, 1 Wakorintho 15:42-44,

Siku moja tutatukuzwa.

 

Katika kifungu hiki Paulo anaandika kuhusu kufufuliwa kwa wafu.  Anawaambia watu wa Korintho ni nini kitafanyika kwa wale wote wameokoka wakati Kristo atakaporudi.  Paulo anawaambia kwamba watapokea miili mipya, yaani miili isioharibika.  Hivi ndivyo Yesu Kristo alifundisha kuhusu siku ile atakaporudi: “Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake-wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe” (Yohana 5:29).  Bwana Yesu Kristo anasema hapa kwamba wakati atakaporudi, wale wote waliokufa watafufuliwa na kupewa miili isioharibika.  Wale wameokoka watafufuliwa wapate uzima wa milele na wale hawajaokoka watafufuliwa wahukumiwe milele.

 

Katika funzo hili, tutaangalia hii baraka kubwa ambayo Mungu anawapa wote ambao wameokoka, yaani anawatukuza.  Katika kifungu hiki, Paulo anasema mambo manne hapa kuhusu nini kitafanyika mkristo akitukuzwa.

 

1.  Tutapewa miili isioharibika, kufa ama kuzeeka.

 

Paulo anasema, “Ule mwili wa kuharibika uliopandwa utafufuliwa usioharibika.” (1Wakorintho 15:42).  Mwili tunao wakati huu ni mwili wa kuharibika.  Hii inamaanisha kwamba mwili wetu unazeeka, mikono na miguu yetu inaisha nguvu, macho na masikio yetu yanakosa nguvu, meno ianaanza kutoka.  Hivi ndivyo miili yetu inakuwa tunapozeeka.  Na mwishowe huu mwili unakufa, kwa sababu ni mwili wa kuharibika.  Lakini mwili ambao Yesu Kristo atatupatia wakati atakaporudi ni mwili usioharibika, kuzeeka ama kufa.  Tutaishi na Mungu milele na miili yetu itakuwa na nguvu na afya kila wakati.  Mikono na miguu yetu itabaki kuwa na nguvu, macho na masikio yetu yatakuwa kamilifu kwa sababu mwili huu mpya utakuwa na afya na hautakufa.  Hili ndilo jambo la kwanza Paulo anaeleza kuhusu mwili wa ufufuo.

 

2.  Tutapewa miili mipya ambayo haina dhambi.

 

Paulo anasema, “Unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu.” (1 Wakorintho 15:43).  Mwili tunao wakati huu ni mwili wa aibu kwa Mungu kwa sababu umechafuliwa na dhambi.  Mungu alipowauba Adamu na Hawa, walikuwa wakamilifu.  Miili yao ilikuwa kamilifu bila dhambi yoyote.  Hii ndiyo sababu Mungu alipomwuba Adamu ilikuwa vizuri sana (Mwanzo 1:31).  Lakini Adamu na Hawa wakaanguka dhambini, na dhambi ikiwaingia mioyoni mwao.  Hawakuwa tena wakamilifu bali walikuwa sasa wenye dhambi.  Na dhambi iliwaletea laana ya Mungu.  Mungu alisema kwamba mwili hutaishi milele lakini utakufa.

 

Sisi sote tumerithi mwili ambao umeharibiwa na dhambi.  Hii ndiyo sababu Paulo anauita, “Mwili huu wa mauti” (Warumi 7:24).  Mwili tulio nao wakati huu uko na dhambi na umechafuliwa na dhambi.  Lakini Bwana Yesu Kristo atakaporudi, mwili huu utafufuliwa kwa utukufu.  Hii inamaanisha kwamba mwili huo mpya hutachafuliwa na dhambi.  Utakuwa mwili wa utukufu na mwili usiyo na dhambi.

 

3.  Tutapewa miili mipya ambayo tutamtumikia Mungu kabisa na kwa ukamilifu.

 

Paulo anasema mwili, “Unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu.” (1 Wakorintho 15:43).  Mwili ambao tuko nao wakati huu ni mwili dhaifu kwa sababu ya dhambi iliyo ndani mwake na pia kwa sababu unazeeka na unakufa.  Hii inamaanisha kwamba huduma wetu kwa Mungu hutakuwa wa nguvu bali dhaifu.  Kuna mambo tungependa kufanya katika huduma wa Mungu lakini dhambi inatupinga.  Hii ndiyo sababu Paulo anasema, “Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote likaalo ndani yangu, yaani, katika asili yangu ya dhambi.  Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda.  Sitendi lile jema nitakalo kutenda bali lile baya nisililitaka kutenda ndilo nitendalo.  Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.  Hivyo naiona sheria ikitenda kazi.  Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo” (Warumi 7:18-21).

 

Huduma wetu kwa Mungu pia ni dhaifu kwa sababu miili yetu ni dhaifu na inakufa.  Hatuna nguvu za mwili na hata za akili zile tunapaswa kuwa nazo ili tumtumikie ipasavyo.  Lakini miili ya ufufuo itafufuliwa ikiwa na nguvu.  Itakuwa miili ambayo haina dhambi na si ya kuzeeka wala kufa.  Itakuwa miili imekamilika kabisa kwa kumwabudu na kumtumikia Bwana.  Milele yote tutamtumikia Bwana huduma ya heshima na inayofaa jina lake.  Tutamtumikia Bwana kwa mioyo yetu yote jinsi inavyotakikana.

 

4.  Tutapewa miili mipya ya kiroho.

 

Paulo anasema, “Unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho.” (1 Wakorintho 15:44).  Biblia inaposema kwamba tutakuwa na miili ya kiroho, haimaanishi kwa huo mwili mpya utakuwa kama mzuka.  Kuna watu wengi wanaofikiria kwamba miili ya ufufuko haitakuwa inaonekana, itakuwa miili ya roho fulani ambayo hata inaweza kupitia kwa ukuta.  Hivi sivyo Biblia inafundisha.  Mwili mpya tutakaopewa utakuwa mwili unaoonekana, kama vile mwili wa Yesu baada ya kufufuka ulikuwa unaonekana.  Yesu aliwaambia wanafunzi wake baada ya kufufuka, “Tazameni mikono yangu na miguu yangu, mwone kuwa ni mimi hasa.  Niguseni mwone, kwa maana mzuka hauna nyama na mifupa, kama mnionavyo kuwa nayo.” (Luka 24:39).  Kwa hivyo mwili wa ufufuko utakuwa mwili unaoonekana, wala si kama mzuka.

 

Paulo anaposema, “Unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa kiroho,” kile anamaanisha ni kwamba mwili tulio nao wakati huu unashughulika sana na mambo ya dunia.  Mtu ambaye hajaokoka hutumia wakati wake wote akikimbizana na vitu vya dunia.  Mtu huyu anajali tu  kuhusu chakula kizuri na nyumba mzuri, nguo mzuri na gari mzuri.  Haya mambo ya dunia ndiyo sana anatamania.  Hata mtu akiokoka angali huwa anatamani vitu vya dunia hii.  Mambo kama chakula na mavazi tunatumia muda mwingi sana kuyashughulikia.  Lakini mwili wa ufufuo hutakuwa hivyo.  Huko mbinguni mambo makuu kwetu yatakuwa mambo ya kiroho.  Tutakuwa na ushirika mtakatifu na mkamilifu wa milele na Mungu na ni ushirika huu ambao tutaushughulikia kila wakati: “Kwa maana ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu” (Warumi 14:17).