Header

Mambo yaliyo ndani ya kijitabu hiki.

 

Biblia inatufundisha kwamba wokovu ni kazi ya Mungu Baba, Mungu Mwana, na Mungu Roho Mtakatifu (1 Petro 1:1-2).  Kijitabu hiki kiko na sehemu tatu.

 

Sehemu ya Kwanza, Kazi ya Mungu Baba katika wokovu wetu.

 

1.  Mungu Baba alipanga wokovu wetu:

 

(i) Alituchagua.

(ii) Alitupeana kwa Mungu Mwana.

(iii) Alimtuma Bwana Yesu Kristo aje kutuokoa.

 

2.  Mungu Baba anatuita kwake

 

Sehemu ya Pili, Kazi ya Yesu Kristo katika wokovu wetu.

 

1. Maisha ya Yesu Kristo ndiyo haki yetu.

 

2. Kifo cha Yesu Kristo kilimshinda na kumfunga shetani.

 

3. Kifo cha Yesu Kristo kilitupatanisha na Mungu.

 

(i) Kristo alikufa ili alipe fidia ya dhambi zetu.

(ii) Kristo alikufa ili atusafishe kutoka kwa uchafu wa dhambi zetu.

(iii) Kristo alikufa ili atukomboe kutoka kwa utumwa wa dhambi.

(iv) Kristo alikufa ili aondoe ghadhabu ya Mungu iliyokuwa juu yetu.

 

4. Kufufuka kwa Yesu Kristo kunatuhakikishia msamaha wa dhambi zetu.

 

5. Yesu Kristo aliporundi mbinguni inamaanisha alimtuma Roho Mtakatifu na pia Kristo ndiye wakati huu kuhani wetu mkuu.

 

Sehemu ya Tatu, Kazi ya Roho Mtakatifu katika wokovu wetu.

 

1. Roho Mtakatifu hutufanya kuzaliwa mara ya pili.

 

2. Roho Mtakatifu hutuleta kwa Yesu Kristo kwa kutupatia toba na imani.

 

3. Roho Mtakatifu anatutakasa na anatukamilisha

 

Utangulizi, Tafadhali soma 1 Petro 1:2.

 

Katika mstari huu Petro anasema kwamba wale wameokoka, “Mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba kulingana na alivyotangulia kuwajua, kwa ya utakaso wa Roho, katika utii na  kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo.”  Tukisoma mstari huu kwa makini tunaona kwamba unaeleza mambo mawili muhimu sana.

 

1. Petro katika mstari huu anaongea kuhusu wokovu.  Petro anaongea kuhusu watu ambao wameokoka na jinsi walivyookoka.

 

2. Katika mstari huu, Petro anaongea kuhusu Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu.  Angalia tena katika mstari huu na utaona kwamba kila mmoja ametajwa: “Mungu Baba alivyotangulia kuwajua kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo.”

 

Hii inamaanisha kwamba wokovu wetu ni kazi ya Mungu wa Utatu.  Inamaanisha kwamba wote Watatu walishiriki katika wokovu wetu.  Hili ni jambo ambalo linawashangaza wengi.  Mara nyingi tunafikiria Bwana Yesu Kristo kuwa mwokozi wetu, lakini hatufikirii wokovu wetu kuwa kazi ya Mungu Baba na pia hatufikirii wokovu wetu kuwa kazi ya Roho Mtakatifu.  Kwa wakristo wengi Mungu Baba ako mbinguni na hashughuliki sana na mambo ya wokovu wetu, naye Roho Mtakatifu alikuja kutupatia vipawa na kuwawezesha watu wawe na ibada za kufurahisha sana katika kanisa zao.  Lakini hawajui kwamba kazi ya Roho Mtakatifu kubwa ni wokovu.

 

Tunaposoma Biblia tunapata kwamba kila Mmoja wa hawa Watatu alikuwa na jukumu fulani katika wokovu wetu.  Yaani tunapata kwamba kuna mambo fulani Mungu Baba alifanya katika wokovu wetu, kuna mambo fulani Mungu Mwana alifanya katika wokovu wetu na kuna mambo fulani Mungu Roho Mtakatifu alifanya katika wokovu wetu.  Wote Watatu walihusika katika wokovu wetu na kila Mmoja alifanya mambo fulani.  Hii inatuonyesha kwamba wokovu wetu ulipangwa kwa utaratibu sana.  Wokovu wetu ni jambo ambalo Mungu wa Utatu alihusika, yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu walipanga kwa utaratibu sana kabla ulimwengu kuumbwa.  Katika kijitabu hiki tutaangalia kazi ya kila Mmoja katika wokovu wetu.  Kwa ufupi tunaweza kusema:

 

1. Mungu Baba alipanga wokovu wetu.

2. Mungu Mwana alitimiza mpango wa Mungu Baba wa kuwaokoa watu wake.

3. Mungu Roho Mtakatifu anatupatia wokovu huo.

 

Kwa hivyo kijitabu hiki kimegawanywa katika sehemu tatu.  Tutaangalia kwanza kazi ya Mungu Baba, halafu kazi ya Mungu Mwana na halafu kazi ya Mungu Roho Mtakatifu katika wokovu wetu.

 

Sehemu Ya Kwanza, Kazi ya Mungu Baba Katika Wokovu Wetu.

 

Funzo la Kwanza, Yohana 6:37-40, Mungu Baba

alipanga wokovu wetu.

 

Katika kifungu hiki (yaani Yohana 6:37-40), Bwana Yesu anasema kwamba alikuja kufanya mapenzi ya Mungu Baba na mapenzi ya Baba ni kwamba Yeye awaokoe watu wake.  Yesu anasema, “Nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake Yeye aliyenituma.  Haya ndiyo mapenzi yake aliyenituma, kwamba nisimpoteze hata mmoja wa wale aliyonipa, bali niwafufue siku ya mwisho.”  Tunapoangalia mafundisho ya Biblia tunapata kwamba kuna mambo matatu ambayo Mungu Baba alifanya wakati alipanga wokovu wetu.

 

1.  Mungu Baba aliwachagua wale watakaookolewa.

 

Hili ni jambo ambalo watu wengi hupata ugumu mwingi sana kukubali.  Huwa tunapenda sana kufikiria kwamba sisi wenyewe tunajiongoza kwa wokovu na kwamba ni sisi wenyewe tunachagua kuokolewa.  Lakini Biblia haifundishi jambo hili hata kidogo.  Biblia inatufundisha kwamba ni Mungu mwenyewe ambaye anaongoza kila kitu.  Huu ni ukweli wazi kabisa hata wewe ukiufikiria.  Mungu ndiye mwenye mamlaka yote na mwenye nguvu zote.  Sisi ni wanadamu tu.  Basi ni nani ataamua kwamba ni nani ataingia mbinguni: je, ni mwanadamu ama ni Mungu?  Jibu ni wazi,  kwamba ni Mungu anayeamua kila kitu na ni Yeye anaongoza kila kitu, hata kuamua ni nani atakayeokoka.  Paulo anawaandikia Waefeso, “Kwa maana alituchagua katika Yeye kabla ya kuumba ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake” (Waefeso 1:4).  Jambo ambalo Paulo anaeleza hapa ni wazi, kwamba, Mungu alituchagua kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu na akapanga wokovu wetu hata kabla hajaumba ulimwengu ili tuokolewe kupitia kwa Yesu Kristo, ili tuwe watakatifu na watu wasio na hatia kupitia imani ndani ya Yesu Kristo.  Wakati Paulo aliwaandikia Wathesalonike, alisema, “Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana,kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe, kwa kutakaswa na Roho, na kuiamini kweli” (2 Wathesalonike 2:13).

 

Biblia inasema wazi kwamba, “Wokovu watoka kwa Bwana” (Yona 2:9), akimaanisha kwamba ni Mungu anayeupanga na ni Mungu anaukamilisha.

 

2.  Mungu Baba alimpatia Mungu Mwana wale wote aliowachagua.

 

Wakati Bwana Yesu alikuwa huku duniani aliongea kuhusu wale Mungu Baba alimpa.  Alisema:

 

“Wale wote anipao Baba watakuja kwangu; na  ye yote ajaye kwangu, sitamfukuza nje kamwe.  Kwa kuwa nimekushuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenituma.  Haya ndiyo mapenzi yake aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho” (Yohana 6:37-39).

Bwana Yesu Kristo aliongea katika kifungu hiki kuwahusu wale Mungu Baba alimpatia.  Hawa ni wale Mungu Baba aliwachagua ili wapate wokovu.  Yesu Kristo anasema mambo mawili kuhusu wale ambao Mungu aliwachagua.

 

(i) Anasema kwamba wale wote ambao Mungu Baba alimpatia watakuja kwake ili waokolewe.  Siyo kweli kwamba kuna baadhi ya wale ambao wamechaguliwa kwa wokovu watakataa kuja kwake Kristo, na kwa sababu hiyo watahukumiwa jahanum.  Yesu mwenyewe anasema wale wote ambao Mungu Baba aliwachagua kwa hakika watakuja kwake Yesu kwa wokovu.  Jambo hili linapatikana katika kitabu cha Yohana 6:44, “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma.”  Yesu anasema hapa kwamba hakuna mtu yeyote anaweza kuja kwake kwa wokovu.  Hii ni kwa sababu sisi sote ni watumwa wa dhambi na kwa uwezo wetu hatuwezi kamwe kuja kwa Mungu atuokoe.  Njia moja tu tunaweza kuja kwa Yesu ili tupate wokovu ni ikiwa Mungu Baba atatuvuta.  Kabla mtu aje kwa Yesu Kristo ni lazima Mungu Baba afanye kazi moyoni mwake.  Bila hii kazi ya Mungu ndani ya roho ya mtu kwanza kufanyika, hakuna mtu anaweza kuja kwake Yesu ili apate wokovu.

 

(ii) Yesu Kristo anasema kwamba sababu yake kuu kuja hapa ulimwenguni ilikuwa kuwaokoa watu wale Mungu Baba alimpatia.  Yesu Kristo anasema, “nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenituma.  Haya ndiyo mapenzi yake Yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho.”

 

Tunaona hapa wazi kwamba Mungu Baba kwanza aliwachagua wale alikuwa awaokoe na akawapeana hao kwa Mungu Mwana ili awaokoe.  Pia tunaona katika mistari hii kwamba Yesu Kristo alikuja kuwaokoa wale ambao Mungu Baba alimpatia.  Yesu Kristo alikuja kuhakikisha kwamba hakuna hata mmoja wa hao walioteuliwa na Mungu atapotea bali wote waokolewe.

 

3.  Mungu Baba mwenyewe alimtuma Yesu Kristo duniani ili awaokoe watu wake kutoka kwa dhambi zao.

 

Katika kifungu hiki tunaona wazi Bwana Yesu akisema ni Mungu Baba aliyemtuma: “Mimi sikushuka kutoka mbinguni ili nifanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.  Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja.”  Bwana Yesu Kristo alikuja duniani kwa sababu Mungu Baba alimtuma kuja kufanya kazi fulani.  Kazi hiyo ilikuwa kuwaokoa wote wale ambao Mungu Baba aliwachagua kuokolewa kabla ya ulimwengu kuumbwa.  Yesu alikuja ili aishi maisha matakatifu na ya kumtii Mungu Baba kwa niaba ya wateule na pia afe msalabani kwa sababu yao.  Hii ndiyo sababu Yesu Kristo alisema, “Mimi ndimi mchungaji mwema; Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. Kama vile Baba anavyonijua Mimi, nami ninavyomjua Baba, Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.” (Yohana 10:14-15).

 

Funzo la Pili, 1 Petro 2:9-10, Mungu Baba hutuita kwake.

 

Katika mistari hii, Petro anasema, “Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu la Mungu, mlioitwa kutoka gizani mkaingia katika nuru yake ya ajabu.  Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu.  Mwanzo mlikuwa hamkupata rehema, lakini sasa mmepata rehema.”  Kuna mambo matatu ambayo Petro anaongea katika mistari hii.

 

1.  Hali yetu kabla ya kuokolewa.

 

Petro anaeleza namna watu wanakuwa kabla ya kuokolewa.  Anaeleza jambo hili kwa njia tatu.

 

(i) Wale hawajaokoka wako gizani.

(ii) Wale hawajaokoka siyo watu wa Mungu.

(iii) Wale hawajaokoka hawajapewa rehema.

 

Tukichunguza kwa makini mambo haya matatu tunaona kwamba watu wale hawajaokoka wako katika hali baya sana.  Wao hawana Kristo ambaye ndiye nuru ya ulimwengu, wao siyo watoto wapendwa wa Mungu Baba na hawajapata rehema kutoka kwa Mungu.  Hii inamaanisha kwamba watu hawa bado hawajasamehewa dhambi zao.  Watu hawa wako ndani ya dhambi na wako njiani wakielekea jahanum.  Hii ndiyo ilikuwa hali ya kila mtu ambaye ameokolewa sasa, na pia ndiyo hali ya kila mtu ambaye hajaokoka.

 

2.  Wale wameokoka wameitwa kutoka kwa hali hii.

 

Petro anasema, “Lakini ninyi ni taifa teule ukuhani wa kifalme, taifa takatifu la Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake Yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru Yake ya ajabu.”  Fikiria mfano huu, mama ambaye ako kwa nyumba na anataka mtoto wake ambaye anacheza nje aje ndani.  Mama huyu anachungulia kwa dirisha halafu anamwita mtoto wake, “Kuja hapa!”  Hivi ndivyo neno “kuitwa” linamaanisha.  Biblia inatuambia kwamba Roho Mtakatifu anatuita kutoka kwa ufalme wa giza ili tuingie ufalme wa Mungu.

 

Kuna mambo manne kuhusu “kuitwa” ambayo tunafaa kutilia maanani.

 

(i) Ni kazi ya Mungu mwenyewe kuwaita wenye dhambi, si kazi ya mwanadamu kamwe. Petro hasemi, “Unaweza kutoka kwa hiyo giza na utafute njia yako mwenyewe uingie kwa nuru.”  Petro anasema, “Tuliitwa kutoka gizani.”  Ni Mungu mwenyewe anafanya kazi hii ya kutuita kutoka kwa dhambi na giza.  Kama Mungu hangetuita tutoke gizani, tungeendelea kuishi dhambini.  Ni lazima Mungu atuite kwanza kabla mtu hajaokoka.

 

Hii kazi ya kuwaita wenye dhambi kutoka gizani ni ya Roho Mtakatifu na inamaanisha ni Roho Mtakatifu anayeamua ni nani atamwita, ni wakati gani atamwita, na ni kwa namna gani atamwita.  Mhubiri hawezi akamwambia Roho Mtakatifu ni nani atamwita. Mhubiri hawezi kumwamrisha Roho Mtakatifu kufanya jambo lolote.  Kile mhubiri anaweza kufanya ni kutengeza mahubiri mazuri ya neno la Mungu na kuyafafanua kwa uaminifu na kuyahubiri kwa uwazi na kwa njia ya kueleweka.  Hakuna jambo lingine mhubiri anaweza kufanya kwa kuwaokoa watu wa Mungu.  Ni kazi ya Roho Mtakatifu kuchukua neno lile lililohubiriwa na kulitumia kuwaita watu kutoka gizani waingie katika nuru yake ya ajabu.

 

(ii) Mungu anamtumia Roho Mtakatifu kuwaita wenye dhambi waje kwake.  Hii inaonekana wazi katika kitabu cha Matendo ya Mitume 13:1-3, wakati Roho Mtakatifu alizungumza na kanisa la Antiokia na kuwaambia wamtengee Barnaba na Sauli kwa kazi ile aliyowaitia.  Kutoka hapo Roho Mtakatifu aliwapeleka wajumbe hawa wawili wa injili katika sehemu ya Wagalatia na akawatumia sana kugeuza nafsi za wengi ili waingie kwa ufalme wa Mungu.  Kazi ya kuwaita wenye dhambi kutubu dhambi zao ni kazi ya Mungu na anaifanya kazi hii kupitia kwa Roho Mtakatifu.

 

(iii) Mungu anatumia neno lake wakati anamwita mwenye dhambi kutoka gizani.  Ukweli huu unafundishwa wazi kila pahali, hasa hasa kitabu cha Matendo ya Mitume.  Siku ya Pentekote wakati watu wengi walikusanyika, Petro hakufundisha mambo yake mwenyewe, alifunza maandiko na akanukuu kutoka kwa Biblia ili aonyeshe kweli kwamba alikuwa anahubiri neno la Mungu.  Wakati Stefano aliitwa ajitetee, hakusema maneno yake mwenyewe bali alihubiri neno la Mungu mbele ya viongozi wa Wayahudi (Matendo ya Mitume 7).  Katika safari yake ya kwanza, Paulo alialikwa kuhubiri katika sinagogi na alihubiri neno la Mungu (Matendo ya Mitume 13:16-47).  Matokeo ya safari ya mtume Paulo yalikuwa, “Neno la Bwana linaenea katika nchi ile yote” (Matendo ya Mitume 13:49).  Kumbuka Biblia haisemi, “Mawazo ya Paulo yalienea katika nchi yote,” bali, “Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote.”

 

Neno la Mungu ndilo jambo la muhimu popote mtu anapookoka.  Watu wengine wanaitwa na Roho Mtakatifu wakiwa wanasoma Biblia ama kitabu kingine ambacho kinafafanua neno la Mungu.  Wakiwa tu nyumbani wakisoma Biblia ama kijitabu kinachofafanua Biblia, Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani ya mioyo yao na wanaelewa ni nini wanasoma.  Wengine Roho Mtakatifu anawaita wakiwa wanasikiliza mahubiri ya neno la Mungu.  Wakiwa wanaketi kanisani na kusikiliza mhubiri, Roho Mtakatifu anafanya kazi mioyoni mwao na wanakuja kwa Kristo na kupata wokovu.

 

(iv) Mwito wa Mungu kupitia kwa Roho Mtakatifu ni wa nguvu sana, unamtoa mwenye dhambi kutoka kwa ufalme wa giza na kumpeleka katika ufalme wa Mungu.  Mara nyingi wakati mama anamwita mtoto aje mahali anapotakikana, mtoto huwa mara nyingi haji.  Labda anacheza na watoto wenzake na hataki kuja mahali mama yake ako, kwa hivyo anajifanya hasikii, ama anapuuza mwito wa mama yake.  Lakini mwito wa Roho Mtakatifu siyo kama kuitwa na mama yako.  Roho Mtakatifu anapomwita mtu huwa anafanya kazi ndani ya moyo wake ili amwezeshe mtu huyo kuja.  Hakuna mtu anaweza kupuuza mwito wa Roho Mtakatifu.

 

3.  Tumeitwa tuingie ndani ya ufalme wa Mungu.

 

Petro anatumia maneno kadhaa kueleza kuhusu watu wa Mungu: “Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu la Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake Yeye aliyewaita mtoka gizani mkaingie katika nuru Yake ya ajabu.....sasa ninyi ni taifa la Mungu....sasa mmepata rehema.”  Maneno haya yote yanaeleza faida tuliyo nayo na ambayo tunaifurahia sana sisi watu wa Mungu wale tumeokoka.

 

(i) Sisi ni uzao mteule.  Mungu alituchagua sisi kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama ndani ya Yesu Kristo.  Wokovu wetu ulipangwa kabla ya ulimwengu kuumbwa.

 

(ii) Sisi ni ukuhani wa kifalme.  Katika Agano la Kale, kabila moja ndiyo ilichaguliwa kuwa ya makuhani.  Hii inamaanisha kabila hiyo ndiyo ilikuwa na wajibu wa kuwaakilisha watu mbele za Mungu.  Kabila hiyo ndiyo ilikuwa inafanya kazi ya kuchoma sadaka za dhabihu zilizoletwa hekaluni.  Lakini katika Agano Jipya hatuna makuhani.  Kuna makanisa mengine siku hizi wanadai kuwa na makuhani, hiyo ni kinyume na Agano Jipya.  Katika Agano Jipya kila mkristo ni kuhani.  Hii inamaanisha kwamba wakristo wote ni sawa machoni pa Mungu, na wote wanaweza kuenda mbele zake.

 

(iii) Sisi ni taifa takatifu, watu wa milki za Mungu.  Katika mstari huu neno “takatifu” inamaanisha watu ambao wameteuliwa kwa kazi muhimu sana ya Mungu.  Tunaona kwamba siyo watu wachache tu ambao ni “muhimu” na “wa kiroho sana” machoni pa Mungu ambao Mungu amewateua kwa kazi hii muhimu.  Wale wote ambao wameokoka ni watakatifu mbele za Mungu na ni watu wa milki ya Mungu.  Wao wote waliitwa kutoka kwa giza na kuingia katika nuru ya Mungu ya ajabu ili watukuze sifa za Mungu aliyewaokoa.  Kwa hivyo, yeyote ambaye ameokoka anapaswa kumtukuza Mungu sana mahali popote Mungu amemweka.  Ikiwa anafanya kazi katika afisi ya serikali basi anapaswa kuhakikisha kwamba tabia yake na jinsi anafanya kazi inamletea Mungu utukufu.  Hili ni jukumu ambalo limepewa kila mtu ambaye ameokoka.  Yesu alisema, “Ninyi ni nuru ya ulimwengu.....Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, wapate kuona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:14-16).

 

 

 

 

 

 

 

Sehemu Ya Pili, Kazi ya Bwana Yesu Kristo katika wokovu wetu.

 

Katika sehemu hii ya pili, tutaangalia ni nini Bwana Yesu Kristo alifanya ili atuokoe.  Tutaangalia kazi ya Yesu Kristo katika mambo manne.

 

I. Maisha ya Yesu Kristo.

II. Kifo cha Yesu Kristo.

III. Kufufuka kwa Yesu Kristo.

IV. Kuenda mbinguni kwa Yesu Kristo.

 

I.  Maisha ya Yesu Kristo.

 

Biblia inatuambia kwamba Yesu alizaliwa na bikira na kwamba aliishi hapa ulimwenguni kwa miaka kama 30.  Mambo mengi ya maisha ya Yesu Kristo yameandikwa katika vitabu vya injili, yaani Mathayo, Marko, Luka na Yohana.  Kile ambacho tunapaswa kuelewa wazi ni kwamba maisha ambayo Yesu aliishi hapa ulimwenguni yalikuwa muhimu sana kwa wokovu wetu.  Watu wengi wanafikiria kwamba Yesu Kristo alikufa juu ya msalaba kwa kuwaokoa watu wake.  Hiyo ni kweli.  Lakini tunapaswa kuelewa kwamba Bwana Yesu hangeishi kwanza maisha yake hapa duniani hatungeweza kuokolewa.  Kifo chake msalabani ni mojawapo ya kazi alifanya ili atuokoe.  Yesu Kristo anatuokoa kwa maisha yake ambayo aliishi hapa ulimwenguni, kwa kifo chake, kwa kufufuka kwake, kwa kurudi kwake mbinguni na kwa kurudi kwake ulimwenguni mara ya pili.  Mambo haya yote ni kwa ajili ya wokovu wetu.

 

Funzo la tatu, Warumi 5:19, Kristo ni haki yetu.

 

Katika kifungu hiki Paulo anasema kwamba dhambi ya Adamu iliwaingia wanadamu wote na Yesu Kristo kwa kutii sheria ya Mungu inawafanya watu wake kuwa wenye haki.  Tutazingatia jambo hili kwa undani zaidi.

 

1.  Kile Mungu anataka.

 

Mungu anasema kwetu, “Mwe watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu” (Mambo ya Walawi 11:44), na Bwana Yesu anasema, “Kwa hivyo iweni wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Mathayo 5:48).  Kuwa mtakatifu inamaanisha kuishi maisha ambayo hayana dhambi kabisa, yaani maisha safi.  Inamaanisha kutii sheria ya Mungu yote kila dakika katika maisha yetu yote kutoka siku ya kuzaliwa hadi siku ya kufa.  Biblia inaeleza wazi kwamba ikiwa mtu si mtakatifu basi hawezi akaingia mbinguni.  Hili ni jambo ambalo watu wengi wamechanganyikiwa sana.  Watu wengi wanafikiria kwamba kuingia mbinguni ni kama kuingia shule ya upili baada ya kufanya mtihani wa shule ya msingi.  Sisi sote tunajua kwamba mwanafunzi anahitajika kuwa na alama nzuri sana za mtihani wake ili aingie shule iliyo nzuri ya upili.  Lakini si lazima mwanafunzi apate asili mia moja katika kila somo ili afaulu mtihani huo.  Wale ambao wanasahihisha mtihani huo huwa wanachukua kila karatasi ya mwanafunzi na kuangalia kama amejaribu kwa bidii sana kujibu maswali vizuri.  Wakiridhika kwamba amejaribu sana kujibu kila swali, basi watampa alama zinazomwezesha kuingia shule ya upili na ataingia.

 

Hivi ndivyo wengi wanafikiria kuhusu kuingia mbinguni.  Wanafikiria kwamba ikiwa watajaribu sana kutii sheria ya Mungu, basi Mungu ataona bidii yao na kuwaruhusu kuingia mbinguni.  Watu hawa wanajiwazia, “Si lazima tuwe wakamilifu, kwa sababu hakuna mtu hata mmoja mkamilifu.  Kwa hivyo Mungu hatuambii, 'Mwe wakamilifu kabisa bila dhambi.'”  Watu hawa wanaendelea kujiwazia kwamba Mungu anasema, “Jaribuni sana kuishi maisha mazuri, ya kidini na ya kupendeza na mtaingia mbinguni.”  Hivi ndivyo watu wengi wanafikiria wataingia mbinguni.

 

Lakini mafikira haya siyo ya kweli.  Yesu hakusema, “Jaribu sana uwezavyo,” bali alisema “Mwe wakamilifu.”  Yesu hakusema, “Hakikisha wewe si mbaya sana kama watu wengine,” bali alisema, “Iweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Mathayo 5:48).  Yaani Yesu anasema kwamba hatupaswi kujilinganisha na watu wengine, bali tujilinganishe na Mungu mwenyewe.  Hatupaswi kulinganisha maisha yetu na ya watu wengine ili kuangalia kama tuko wazuri kuwaliko, bali tunapaswa kuwa, “Wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”  Mtu anaweza kuwa wa dini sana na anaishi maisha mazuri kuliko marafiki wake na watu wa jamii yake wote na washirika wa kanisa lake lote.  Lakini hilo halitampeleka mbinguni.  Haitoshi kuwa bora kuliko wengine, bali anapaswa kuwa mkamilifu na mtakatifu kama Mungu mwenyewe ikiwa ataingia mbinguni.  Ikiwa mtu hatakuwa mkamilifu jinsi Mungu ako, basi atatumwa jahanum milele kwa sababu Mungu hatamruhusu mtu yeyote ambaye siyo mkamilifu na ambaye ako na dhambi, kuingia mbinguni.  Katika kitabu cha Zaburi, tunasoma mistari hii:

 

“Wewe si Mungu unayefurahia uovu, kwako mtu muovu hataishi.  Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako, unawachukia wote watendao mabaya.  Unawaangamiza wasemao uongo, wamwaga damu na wadanganyifu Bwana huwachukia” (Zaburi 5:4-6).

 

“Bwana ni nani awezaye kukaa katika hekalu lako?  Nani awezaye kuishi juu ya mlima wako mtakatifu?  Ni yule aendaye pasipo mawaa, anayetenda yaliyo haki, asemaye kweli toka moyoni mwake na hana masingizio ulimini mwake, asiye mtenda jirani yake vibaya na asiyemsingiziya mwenzake” (Zaburi 15:1-3).

 

Angalia kwa makini sana kile Biblia inasema hapa.  Biblia haisemi kwamba ni wale ambao wamejaribu sana na wamefanya vyema sana ndiyo watakaoingia mbinguni.  Biblia inasema kuhusu Mungu kwamba, “Unawachukia wote watendao mabaya.”  Biblia inasema, ni mtu, “anayetenda yaliyo haki” ndiye ataingia mbinguni.  Yeyote atendaye hata dhambi kidogo hawezi kuingia mbinguni.  Biblia inatuambia kwa Mungu ni mtakatifu sana, hata hawezi akaangalia dhambi (Habakuki 1:13).

2.  Shida ya dhambi.

 

Tunaweza kuona wazi kwamba kuna shida kubwa hapa.  Ikiwa tunapaswa kuwa wakamilifu na wasafi kabisa bila dhambi, je, tutawezaje kuingia mbinguni?  Tunajua kwamba hata tukijaribu namna gani kutimiza sheria ya Mungu, tunashindwa mara zaidi ya milioni kila siku.  Tunajua kwamba hakuna hata mtu mmoja hapa duniani ambaye ni mkamilifu.  Hata mtu yule anadai kuwa mtumishi mkuu wa Mungu na anadai ni mtakatifu bado hajakamilika.  Biblia inasema, “Hakuna mwenye haki hata mmoja” (Warumi 3:10).  Basi, ni vipi tutakuwa na tumaini la kuingia mbinguni?

 

3.  Haki ya Yesu Kristo.

 

Jibu ni kwamba Yesu ndiye haki yetu.  Haki ile itatuwezesha kuingia mbinguni haitoki ndani mwetu bali inatoka kwa Mungu.  Biblia inasema, “Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria; ambayo torati na manabii wanaishuhudia.  Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote waaminio” (Warumi 3:21-22).

 

Mfano huu utatusaidia kuelewa vile Biblia inaeleza hapa.  Fikiria ile siku ulizaliwa, Mungu alichukua kitabu na aliandika jina lako katika jalada la kitabu hicho.  Basi kuanzia wakati huo, kila dhambi ambayo umefanya Mungu ameiandika katika kitabu hicho.  Wakati ulipokuwa na miaka kama 20 au 30, kitabu hicho kilikuwa na rekodi ya mamilioni ya dhambi kwa sababu tunafanya dhambi kila wakati, hata wakati hatujui.

 

Sasa fikiria siku ile Yesu alizaliwa huko Bethlehemu, Mungu alifanya vivyo hivyo: yaani alichukua kitabu na akaandika jina la Yesu Kristo katika jalada lake.  Baada ya miaka 30, Yesu alisulubiwa na akafa.  Je, ni nini kimeandikwa ndani ya kitabu cha Yesu?  Jibu ni kwamba hakuna dhambi yoyote imeandikwa hapo, kwa sababu hakufanya dhambi: “Yeye mwenyewe alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo, lakini Yeye hakutenda dhambi” (Waebrania 4:15).  Yesu aliishi maisha makamilifu na ya utiifu machoni pa Mungu, kwa hivyo katika kitabu chake kinasema, “Mtu huyu ametii sheria ya Mungu kabisa na alikuwa mkamilifu, Yeye ni mwenye haki kabisa.”  Haya ndiyo yameandikwa katika kitabu cha Yesu Kristo.

 

Sasa wakati tunaokolewa, kunakuwa na mabadiliko makubwa sana.  Mungu huchukua ile rekodi yetu ya dhambi na uasi na anaiweka katika kile kitabu cha Yesu Kristo.  Pia Mungu anatoa ile rekodi kamilifu na ya utiifu ya Yesu Kristo na anaiweka katika kitabu chetu.  Kwa hivyo Kristo anachukua dhambi zetu na uasi wetu na anahukumiwa.  Lakini sisi tunapewa hiyo haki yake.  Angalia kwa makini maneno ya Paulo kwa Warumi: “Kwa kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki” (Warumi 5:19).  “Mtu mmoja” katika mstari huu ni Yesu Kristo mwenyewe.  Ni kupitia kutii kwa Yesu Kristo kwamba wengi watahesabiwa haki.  Si kupitia kwa matendo yao mazuri watu wanahesabiwa haki, bali wanahesabiwa haki kupitia utiifu wa Yesu Kristo.

Akiwaandikia Wakorintho Paulo alisema, “Yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu katika Yeye” (2 Wakorintho 5:21).  Angalia tena kwa makini mstari huu.  Yesu hakuwa na dhambi kwa sababu alikuwa mkamilifu, lakini Mungu alimwekelea rekodi yetu ya dhambi kwake asiyejua dhambi ili amfanye kuwa dhambi kwa ajili yetu.  Mungu alichukua haki ya Yesu Kristo na kutupatia ili tupate kuwa haki ya Mungu katika Kristo.

 

Sasa wakati Mungu Baba anatuangalia, haoni ile rekodi ya dhambi na kutotii kwetu, kwa sababu hiyo imetolewa kutoka kwetu na kupewa Yesu.  Kile sasa Mungu Baba anaona ni ile rekodi kamilifu ya Yesu Kristo ambayo alitii sheria ya Mungu yote na ambayo imewekwa kwa rekodi yetu.  Yesu Kristo ndiye haki yetu (1 Wakorintho 1:30).  Bila maisha makamilifu ya Kristo hapa ulimwenguni hatuwezi kuingia mbinguni, tunaweza kuingia mbinguni tu kwa sababu Yesu Kristo alitii sheria ya Mungu kwa ukamilifu na akatupatia utiifu wake.

 

 

 

II.  Kifo cha Yesu Kristo.

 

Bwana Yesu Kristo aliishi hapa ulimwenguni kama miaka 30 halafu akafa msalabani Kalivari.  Je, kwa nini?  Jibu ni kwamba Mungu alikuwa amemtuma kuja kuwaokoa watu wake kutoka kwa dhambi zao na ilikuwa lazima afe ili awaokoe.  Bila Yesu Kristo kufa msalabani hakungekuwa na wakovu wa watu wake.  Kifo cha Yesu Kristo msalabani Kalivari kilitimiza mambo mawili.

 

1. Kupitia kifo chake msalabani, Bwana Yesu Kristo alimshinda shetani na akamfunga ili hasiendelee kudanganya mataifa.

 

2. Kupitia kifo chake msalabani, Bwana Yesu Kristo alikamilisha wokovu wa watu wake.

 

Funzo la nne, Mathayo 12:29, Yesu Kristo alimshinda shetani na akamfunga kupitia kwa kifo chake msalabani.

 

Kama vile tumeona katika somo letu hapo nyuma, Mungu Baba aliwachagua watu wengi ili awaokoe, na akamtuma Yesu Kristo aje ulimwenguni kuwaokoa.  Tunapaswa kujua kwamba jambo la kwanza Yesu Kristo alikuwa afanye ni kumshinda na kumfunga shetani.  Hii ni kwa sababu shetani alikuwa anawaweka katika utumwa mataifa yote.  Kwa hivyo Yesu Kristo alikuwa kwanza amshinde shetani na kumtoa mamlakani.  Hili ndilo funzo la mstari huu wa Mathayo 12:29.  Katika mstari huu Yesu Kristo anasema, “Mtu awezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu?  Akiisha mfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali zake.”

 

Mfano huu unaeleza nyumba ambayo iko na vitu vingi vya thamani sana na nyumba hii inalindwa na mtu mwenye nguvu sana.  Lakini siku moja mtu mwenye nguvu kuliko huyu mlinzi anakuja na anapigana vita na huyu mlinzi, na mlinzi anashindwa nguvu na anafungwa.  Basi mwenye kumshinda huyu mlinzi nguvu anaingia ndani ya nyumba hii na kuanza kuchukua vitu.  Kuna mambo matatu tunayaona katika mfano huu wa mstari 29.

 

1.  Mtu mwenye nguvu analinda nyumba.

 

Biblia inatuambia kwamba kabla Yesu Kristo kuja hapa duniani Mungu aliruhusu shetani kuwa na mamlaka juu ya mataifa yote ya ulimwengu.  Mungu alichagua taifa la Uisraeli kuwa watu wake, lakini hakuongea na mataifa mengine, bali alimruhusu shetani kuwapofusha katika ufalme wa giza.  Hii ndiyo sababu Paulo alisema, “Zamani aliwaachia watu waishi walivyotaka” (Matendo ya Mitume 14:16). Kwa hivyo katika mfano huu, nyumba iliyokuwa na vitu vya thamani sana ni mataifa ya ulimwengu na mlinzi wa nyumba hiyo aliye na nguvu ni shetani.

 

 

2.  Mtu mwenye nguvu anakuja na kumshinda mlinzi wa nyumba na anamfunga.

 

Biblia inatueleza kwamba Bwana Yesu Kristo, kupitia kwa kifo chake msalabani Kalivari alimshinda shetani na akamfunga.

 

“Basi kwa kuwa watoto wana nyama na damu, Yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani, shetani, na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti” (Waebrania 2:14-15).

 

Hii ndiyo sababu kitabu cha Ufunuo kinasema,

 

“Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa ameshika ufunguo wa lile shimo lisilo na mwisho na mnyororo mkubwa mkononi mwake.  Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ndiye Ibilisi na shetani, naye akamfunga miaka 1,000. Akamtupa katika lile shimo lisilo na mwisho, akamfunga humo na kulitilia lakiri, ili kumzuia asiendelee kudanganya mataifa” (Ufunuo 20:1-3).

 

Kifungu hiki kinaeleza kifo cha Yesu Kristo msalabani.  Kifungu hiki kinatueleza kwamba kupitia kwa kifo cha Yesu msalabani, Yesu alimshinda shetani na akamfunga, ili, “Asipate kuwadanganya mataifa tena.”  Kifungu hiki hakisemi kwamba shetani hafanyi chochote wakati huu.  Tunajua kwamba shetani hutujaribu na kutaka kutuondoa kwa Mungu ili turudi dhambini.  Lakini kifungu hiki cha Ufunuo kinasema kwamba shetani alifungwa ili asipate kuwadanganya mataifa tena.  Hii inamaanisha kwamba Yesu Kristo amemfunga shetani ili asiendelee kuwaweka watu wa dunia gizani.

 

3.  Mtu mwenye nguvu sana anaingia nyumbani na kuchukua vyombo vya thamani.

 

Msalabani Kalivari, Bwana Yesu Kristo alimshinda shetani na kumfunga, na baada ya kufufuka,  Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.  Kwa sababu hii, enendeni ulimwenguni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi” (Mathayo 28:18-19).  Bwana Yesu Kristo ako na mamlaka yote mbinguni na duniani.  Kuna wakati shetani aliruhusiwa kuyaweka mataifa ya ulimwengu gizani, lakini sasa ameshindwa na amefungwa.  Hii ndiyo sababu Yesu Kristo anawatuma wanafunzi wake ulimwenguni, ili waeneze ufalme wake.  Hatupaswi kusema nchi kama Somalia hawawezi kuokoka kamwe.  Wakati utakapofika, Roho Mtakatifu atafanya kazi ndani ya roho za watu wa taifa lile na atawaleta ndani ya ufalme wa Mungu.

 

Hii ndiyo sababu ya kwanza kwa nini Yesu Kristo alikufa.  Alikufa ili amshinde shetani na amfunge asipate kuwadanganya mataifa tena.  Kazi ya kuwatoa watu wa dunia kutoka kwa giza inaendelea kwa sababu shetani hana mamlaka kuwakatalia ikiwa Yesu anataka kuwaokoa.

Funzo la tano, 1 Petro 3:18, Kifo cha Yesu Kristo kiliwapatanisha watu wa Mungu na Mungu mwenyewe.

 

Katika mstari huu wa 1 Petro 3:18, Petro anasema, “Kristo naye aliteswa mara moja tu, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki, ili atulete ninyi kwa Mungu.”  Katika maneno haya, Petro anatuambia kwamba kusudi la kifo cha Yesu lilikuwa kutuleta kwa Mungu.  Yaani kuna kutengana baina ya Mungu na mwanadamu.  Hawa wawili hawana ushirika na hawako pamoja.  Ni kifo cha Yesu pekee kinaweza kuwaleta pamoja.  Tukisoma Biblia tunaona kwamba, msalabani Kalivari, Yesu Kristo alifanya mambo fulani ili alete upatanisho hili.

 

1.  Yesu Kristo alikufa ili alipe fidia ya dhambi zetu.

 

Sheria ya Mungu ni kama tu sheria ya Kenya.  Wakati mtu anavunja sheria huwa anahitajika kulipa faini.  Mtu huyu hupelekwa kotini na anasomewa mashitaka na akipatikana na hatia basi analipa faini ama atumikie kifungo gerezani.  Ni lazima alipe fidia kwa sababu ya makosa aliyofanya.  Vivyo hivyo sheria ya Mungu inasema kwamba ikiwa mtu ameivunja ni lazima alipe fidia.  Fidia ya dhambi ni mauti: “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti” (Warumi 6:23).  Biblia inapoongea kuhusu mauti au kifo katika mstari huu, haimaanishi kifo cha mwili bali inamaanisha kutenganishwa na Mungu milele.  Bwana Yesu Kristo akiwa msalabani Kalivari alilipa fidia ya watu wake.  Aliposulubiwa msalabani, dhambi za watu wake ziliwekwa juu yake na akazilipia fidia ili aondoe hatia ya watu wake: “Alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake, Na kwa majeraha yake sisi tumepona.  Sisi sote, kama kondoo, tumepotea; kila mmoja wetu umegeukia njia yake mwenyewe; na Bwana aliweka juu yake maovu yetu sisi sote” (Isaya 53:5-6).

 

Hii ndiyo sababu Bwana Yesu Kristo akiwa msalabani alitengana na Mungu Baba na akalia, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” (Mathayo 27:46).  Bwana Yesu Kristo akiwa msalabani Kalivari alilipa fidia ya dhambi za watu wake.

 

2.  Yesu Kristo alikufa ili atusafishe kutoka kwa dhambi zetu.

 

Dhambi zetu hutuletea hatia mbele ya Mungu, na pia zinatufanya kuwa wachafu machoni pa Mungu.  Dhambi ni kitu kichafu na tunapoanguka dhambini, tunakuwa kama mtoto anayecheza matopeni wakati wa mvua, yaani tunakuwa wachafu.  Biblia inatueleza kuna kitu kimoja tu ambacho kinaweza kutusafisha kutoka kwa dhambi zetu, na kitu hicho ni damu ya Yesu Kristo: “Damu yake Yesu, Mwana Wake, yatusafisha dhambi yote” (1 Yohana 1:7).  Kuoshwa kutoka kwa uchafu wa dhambi haipatikani kwa maji ya kubatizwa ama kwa damu ya wanyama.  Mtu yeyote anayetaka kuoshwa dhambi zake ni lazima amwombe Yesu Kristo pekee kwa kuoshwa dhambi na ataoshwa kutoka kwa dhambi zake.

 

3.  Yesu Kristo alikufa ili atukomboe kutoka kwa utumwa wa dhambi.

 

Biblia inasema kwamba tunazaliwa humu ulimwenguni tukiwa watumwa wa dhambi.  Hili ni jambo ambalo wale hawajaokoka wanaliona kuwa gumu sana kuamini.  Watu wengi duniani hufikiria kwamba wako huru kufanya watakavyo na wanashangaa sana wakati wanaambiwa, “Wewe ni mtumwa.”  Lakini huu ni kweli.  Paulo akiwaandikia wakristo wa Roma anasema, “Lakini Mungu na ashukuriwe, kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa.  Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki” (Warumi 6:17; 20).  Mafunzo ya Biblia ni wazi kwamba mtu ambaye hajaokoka ni mtumwa wa dhambi.  Mtu anaweza kuwa hajui jambo hili na pia anaweza kukataa kuyakubali mafundisho haya anapoyasikia, lakini ni mafunzo ya kweli kwa sababu yanapatikana katika neno la Mungu.

 

Wakati Bwana Yesu alikufa msalabani Kalivari, alimwaga damu yake ambayo ndiyo fidia ya kuwatoa watu wake kwa utumwa wa dhambi: “Katika Yeye tunao ukombozi kwa njia ya damu Yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema Yake” (Waefeso 1:7).  Hii ndiyo sababu Yesu Kristo alisema, “Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi” (Mathayo 20:28).  Fidia ni bei ya malipo ambayo hulipwa ili mtumwa aachiliwe, na damu ya Yesu Kristo ndiyo fidia iliyolipwa ili watu wake waachiliwe kutoka kwa utumwa wa dhambi.  Wanatolewa kutoka kwa utumwa wa dhambi kwa malipo ya damu ya Yesu.  Hii ndiyo sababu Paulo anasema, “Ninyi si mali yenu wenyewe; kwa maana mmenunuliwa kwa gharama.  Kwa hivyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu” (1 Wakorintho 6:19-20).  Tunapookolewa huwa tunakuwa mali ya Kristo kwa sababu yeye ndiye ametununua kutoka kwa utumwa na kutufanya kuwa watu wake.  Kwa hivyo hatuwezi kuishi maisha yetu vile tunapenda, bali tunapaswa kuishi tukitii amri za Bwana Yesu.

 

4.  Kristo alikufa ili aondoe ghadhabu ya Mungu juu ya watu wake.

 

Mungu ni msafi na hapendi dhambi kamwe.  Dhambi humfanya Mungu apatwe na hasira takatifu na ya haki.  Tunaona jambo hili la hasira yenye utakatifu ndani ya Yesu Kristo wakati aliwapata wafanya biashara hekaluni (Yohana 2:12-16), na pia jinsi Yesu Kristo alivyoongea kuhusu viongozi wa dini wakati wake (Mathayo 23).  Mungu anakasirishwa na wenye dhambi kila siku: “Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Mungu aghadhibikaye kila siku.  Bwana huwajaribu mwenye haki; lakini waovu na wale wanaopenda jeuri nafsi yake huwachukia.  Juu ya waovu atawanyeshea makaa ya moto mkali na kiberiti kinachowaka, upepo wenye joto kali ndiyo fungu lao” (Zaburi 7:11; 11:5-6).

 

Wakati Bwana Yesu Kristo alikufa msalabani Kalivari, alichukua dhambi za watu wake juu yake na akaichukua ghadhabu ya Mungu mwilini mwake kwa sababu ya watu wake.  Ghadhabu ya Mungu ilimwagwa juu yake wakati alikuwa msalabani.  Huu ndiyo upatanisho na Biblia inasema, “Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake” (Warumi 3:25).

 

Hii basi ndiyo sababu kuu kwa nini Yesu Kristo alikufa, kwa sababu ya dhambi za watu wake.  Alikufa ili alipe fidia ya dhambi zao, alikufa ili awaoshe watu wake dhambi zao, alikufa ili awakomboe watu wake kutoka kwa utumwa wa dhambi na alikufa ili aondoe ghadhabu ya Mungu juu ya watu wake.

 

 

 

III.  Kufufuka kwa Yesu Kristo.

 

Funzo La Sita, 1 Wakorintho 15:17-19, Kufufuka kwa Yesu kwa sababu ya wokovu wa watu wake.

 

Katika kifungu hiki, mtume Paulo anaandika kuhusu kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo.  Paulo anasema, “Tena kama Kristo hajafufuka, imani yenu ni batili, nanyi bado mko katika dhambi zenu.  Hivyo basi wote waliolala katika Kristo wamepotea.”

 

1.  Ikiwa Kristo hakufufuka kutoka kwa wafu basi hakuna msamaha wa dhambi kwa watu wake.

 

Watu wengi wanashangaa sana wanaposoma mstari 17 ambapo Paulo anasema, “Tena kama Kristo hajafufuka, imani yenu ni batili, nanyi bado mko katika dhambi zenu.”  Mara nyingi tunafikiria kwa sababu ya kifo cha Bwana Yesu msalabani Kalivari tumesamehewa dhambi zetu na kwamba kufufuka kwa Bwana Yesu hakuna uhusiano na msamaha wa dhambi zetu.  Lakini hivi si kweli.  Paulo anasema, “Kama Kristo hajafufuka,....bado mko katika dhambi zenu.”  Yaani Paulo anasema, ikiwa Yesu Kristo hakufufuka kutoka kwa wafu, basi hatuna msamaha wa dhambi na hatuna wokovu.  Ni kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo wokovu wetu umehakikishwa.

 

2.  Kristo ndiye kuhani mkuu wa watu wake.

 

Ni kwa nini kama Yesu Kristo hakufufuka kutoka kwa wafu, hatungesamehewa dhambi zetu?  Ili tuweze kuelewa vizuri jambo hili tunapaswa kufikiria kuhusu siku ya upatanisho katika Agano la Kale (Mambo ya Walawi 16) na (Waebrania 9:11-28).  Utapata usaidizi sana kama utasoma vifungu hivi viwili kabla hujaendelea.

 

Wakati wa siku ya upatanisho (Mambo ya Walawi 16), kuhani mkuu alikuwa anaenda mbele za Mungu akiwa na damu ya mnyama ili awaombee msamaha watu wa Mungu.  Kuhani huyu alikuwa anaenda mbele za Mungu siku moja tu kwa mwaka na kulikuwa na masharti mengi ambayo alikuwa atimize kabla ya kwenda mbele za Mungu.  Kulikuwa na nguo fulani kuhani mkuu alikuwa anavaa na mnyama aliyechinjwa alikuwa bila kasoro yoyote.  Kuhani huyu akifanya makosa kidogo tu juu ya jambo hili na aje mbele za Mungu, Mungu angemwua.  Ikiwa damu ile ameleta mbele za Mungu ilikuwa imetoka kwa mnyama aliye na kasoro, ama nguo zake alizozivaa zilikuwa na kasoro, basi hatatoka mbele za Mungu akiwa hai.  Kwa hivyo, ikiwa kuhani ametoka mbele za Mungu akiwa hai baada ya kutoa dhabihu kwa niaba ya watu wake, basi watu hawa walijua kwamba Mungu ameikubali sadaka yao na kwamba dhambi zao zimesamehewa.  Ikiwa kuhani hatatoka akiwa hai, ilimaanisha kwamba sadaka yao haikukubaliwa na Mungu na kwa hivyo bado wako katika dhambi zao.

Katika kitabu cha Waebrania 9:11-28, tunaambiwa kwamba Bwana Yesu Kristo, akiwa kuhani mkuu, pia aliingia katika patakatifu pa Mungu na sadaka ya damu yake.  Pahali Yesu aliingia hapakuwa pametengenezwa na mwanadamu kama lile hema lililokuwa jangwani, na ile damu aliingia nayo haikuwa ya mnyama.  Mwandishi wa Waebrania anasema,

 

“Kristo alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikujengwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu.  Hakuingia kwa njia ya damu ya mbuzi na ndama, lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata  ukombozi wa milele” (Waebrania 9:11-12).

 

Kwa hivyo Bwana Yesu Kristo alifanya vile tu kuhani alikuwa anafanya katika Agano la Kale, aliingia katika patakatifu pa Mungu akiwa na sadaka ya damu.  Tofauti iliyopo hapa baina ya Yesu Kristo na makuhani wa Agano la Kale ni kwamba Yesu aliingia patakatifu pa Mungu penyewe na akatoa sadaka ya damu yake mwenyewe.

 

3.  Kufufuka kwa Yesu Kristo ni hakikisho tosha kwetu kwamba dhambi zetu zimesamehewa.

 

Kama jinsi tulivyoona katika Agano la Kale, kwamba kuhani akirudi kutoka kwa Patakatifu pa Patakatifu akiwa hai, ilikuwa dhihirisho kwamba Mungu ameikubali sadaka aliyoitoa na kwamba dhambi za watu wa Mungu zimesamehewa.  Ikiwa hakutoka akiwa hai basi ilikuwa wazi kwamba sadaka ambayo kuhani ametoa haikukubalika na Mungu na kwamba watu hao bado wako katika dhambi zao.  Vivyo hivyo, ukweli kwamba Kristo alifufuka ni wazi kwamba sadaka aliyoitoa kwa Mungu kwa niaba yetu ilikubalika: “Tena kama Kristo hajafufuka, imani yenu ni batili; bado mko katika dhambi zenu” (1 Wakorintho 15:17).

 

Kwa hivyo kufufuka kwa Yesu Kristo ni muhimu sana katika wokovu wetu.

 

 

IV. Kupaa kwa Yesu juu Mbinguni.

 

Funzo la saba, Matendo ya Mitume 1:9-11, Kupaa kwa Yesu juu Mbinguni.

 

Katika kifungu hiki, tunasoma kuhusu kupaa juu mbinguni kwa Yesu Kristo.  Bwana Yesu Kristo, baada ya kufufuka, alifundisha kuhusu ufalme wa mbinguni, halafu akachukuliwa kwenda juu mbinguni.  Je, ni kwa nini Yesu Kristo alipaa juu mbinguni?  Agano Jipya linatupatia sababu mbili:

 

1. Bwana Yesu Kristo alipaa juu mbinguni ili amtume Roho Mtakatifu.

 

Bwana Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake, “Yafaa mimi niondoke, kwa kuwa nisupoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; lakini nikienda nitamtuma kwenu” (Yohana 16:7).  Msaidizi katika mstari huu ni Roho Mtakatifu.  Bwana Yesu Kristo aliwaambia mitume wake kwamba asiporudi juu mbinguni Roho Mtakatifu hatakuja.  Sababu kubwa ya kufanya hivi ni kwamba wokovu wetu ulipangwa kwa utaratibu sana huko mbinguni kabla ya kuumbwa kwa dunia.  Si kwamba Roho Mtakatifu atakataa kuja Yesu asiporudi bali ni kwa sababu kila kitu kilikuwa kimepangwa taratibu tangu mwanzo.  Mungu Baba aliwachagua wale wataookoka kabla ya dunia kuumbwa (Waefeso 1:4), halafu akawapeana kwa Mwana.  Kwa hivyo Mwana alikuja ulimwenguni ili awakomboe.  Mungu Mwana naye alimtuma Roho Mtakatifu ili aendeleze kazi ya wokovu.  Kazi hii ni kuwadhibitishia watu dhambi zao na kuwaita wale ambao Mungu amewachagua na Mwana amewafia waingie ufalme wake.

 

2.  Bwana Yesu Kristo alipaa juu mbinguni kuanzisha kazi yake ya kuhani mkuu.

 

Kazi ya Bwana Yesu Kristo haikuisha wakati alipaa mbinguni.  Sisi ambao tumeokoka tuko, “Ndani ya Kristo,” yaani, sisi ni watu wake na tumeunganishwa na yeye.  Kwa hivyo Yesu Kristo anaendelea na kazi yake ya wokovu akiwa kuhani mkuu.  Kazi ya Yesu akiwa kuhani mkuu inahusu mambo mawili:

 

(i) Yesu anatuombea.  Hili ni jambo la kutufariji sana kujua kwamba kila siku Bwana Yesu Kristo anawaombea watu wake wote.  Yesu hutuombea kila siku kwa maisha yetu ya kiroho ili tukue katika maisha yetu ya ukristo na pia tukue katika utakatifu na tuwe kama Yeye kila siku.  Yesu anajali maisha ya utakatifu sana ya watu wake, zaidi ya mambo mengine.  Yesu Kristo anajali sana watu wake wawe watakatifu, wakamilifu na wasafi kila siku na kwa hivyo anawaombea.

 

(ii) Yesu hufanya maombi yetu na huduma wetu kukubalika mbele za Mungu.  Maisha ya mkristo ni kwa imani na si kwa matendo mazuri.  Hatuwezi tukasema kwamba Mungu atakubali maombi yetu na huduma wetu kwa sababu tumejitahidi sana.  Ni kwa imani tu maombi yetu yanakubaliwa na Mungu kwa sababu Yesu Kristo ambaye ni kuhani wetu mkuu huyafanya yakubalike.

Sehemu Ya Tatu, Kazi ya Roho Mtakatifu katika wakovu wetu.

 

Katika masomo haya tayari tumeona kazi ya Mungu Baba na kazi ya Mungu Mwana.  Sasa tutaangalia kazi ya Roho Mtakatifu katika wokovu wetu.  Ni jambo la kushangaza kwa wakristo wengine kwamba Roho Mtakatifu anahusika katika wokovu wetu.  Watu wengi huwaza kwamba Roho Mtakatifu anahusika kidogo sana ama hahusiki kamwe katika wokovu wetu.  Wanawaza kwamba Roho Mtakatifu alikuja kuwapa watu vipawa na kuwawezesha kuhubiri mahubiri kwa njia ya kupendeza na kufurahisha.  Lakini hii si kweli.  Tunaposoma Agano Jipya, ni wazi kwamba Roho Mtakatifu alikuja kwa sababu ya jambo moja: na hii ni wokovu wa watu wa Mungu.  Kazi yake yote, kwa mfano, kuwapa watu wa Mungu vipawa, yote yako na kusudi moja: kuwaletea watu wa Mungu wokovu wa milele.  Hivi basi ndivyo Roho Mtakatifu hufanya kazi yake katika wokovu wetu.

 

Kuna mambo matatu ambayo Roho Mtakatifu hufanya ili atulete kwa Yesu Kristo tuokolewe.   Katika mafunzo matatu yanayofuata tutasoma kila moja ya mambo haya.

 

1. Roho Mtakatifu hutufanya tuzaliwe mara ya pili (funzo la nane).

 

2. Roho Mtakatifu hutuleta kwa Kristo (funzo la tisa).

 

3.Roho Mtakatifu hutusafisha na kutukamilisha (funzo la kumi).

 

 

Funzo la nane, Yohana 3:1-8, Roho Mtakatifu hutufanya tuzaliwe mara ya pili.

 

Katika kifungu hiki cha injili ya Yohana Bwana Yesu Kristo anatupatia mafundisho kuhusu kuzaliwa mara ya pili.

 

Kuna mambo manne muhimu sana Yesu Kristo anatufundisha hapa.

 

1.  Mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuingia mbinguni.

 

Yesu alimwambia Nikodemo, “Amin, amin, nakuambia, mtu hawezi kuuona ufalme wa Mungu asipozaliwa mara ya pili” (Yohana 3:3).  Kuna watu wengi humu nchini mwetu leo wanaosema kwamba wao ni wakristo lakini hawajaokoka ama kuzaliwa mara ya pili.  Watasema jambo kama hili, “Mimi nilizaliwa katika jamii ya wakristo na nilibatizwa nikiwa mtoto.  Mimi huenda kanisani kila Jumapili.  Mimi bado sijaokoka ama kuzaliwa mara ya pili lakini mimi ni mkristo.  Ninaishi maisha mazuri na ninamwamini Mungu, kwa hivyo ninajua nitaingia mbinguni nitakapokufa.”  Hili ni jambo ambalo watu wengi hapa nchini mwetu wanaamini.  Lakini hili silo jambo la kweli.  Mtu hafanyiki mkristo kwa sababu amezaliwa katika jamii ya wakristo na kubatizwa akiwa mtoto.  Mtu anakuwa mkristo wakati anazaliwa mara ya pili.  Hadi ile siku atazaliwa mara ya pili, yeye si mkristo na hataingia mbinguni ikiwa hajazaliwa mara ya pili.  Ni wale tu wamezaliwa mara ya pili watakaoingia mbinguni.

 

2.  Ni lazima tuzaliwe mara ya pili kwa sababu tuko katika mwili.

 

Yesu alisema, “Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho.  Kizaliwacho kwa mwili ni mwili” (Yohana 3:6).  Mungu alipomwumba Adamu, aliumba kwanza mwili wa Adamu kutoka kwa, “mavumbi ya ardhi” (Mwanzo 2:7).  Hii inamaanisha Adamu alikuwa na mahitaji ya kiroho na pia alikuwa na mahitaji ya vitu vya dunia.  Adamu alipewa mwili na roho, na maisha yake yalijumlisha mwili na roho.  Adamu hangeweza kuishi humu duniani bila kushughulikia mahitaji ya mwili wake.  Hakuna mtu anaweza kutumia muda wake wote kwa maombi na kusoma Biblia bila kula chakula.  Vivyo hivyo, Adamu hangeshughulikia tu mahitaji ya kimwili bila kujali mahitaji ya kiroho.  Yesu alisema, “Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu” (Mathayo 4:4).  Adamu aliumbwa akiwa na roho na mwili na alihitajika kuishi maisha ya kiroho na pia kujali mahitaji ya mwili.

 

Wakati Adamu alianguka dhambini, mojawapo ya matokeo ya dhambi yake ni kwamba aliacha kujali mambo ya kiroho na kujali tu mambo ya mwili.  Hivi ndivyo dhambi inamfanya mtu.  Dhambi inamfanya mtu kujali tu mambo ya mwili na kupuuza mambo ya kiroho.  Hivi ndivyo tunavyozaliwa hapa duniani.  Tunashughulika tu na mambo ya maisha ya hapa duniani, yaani chakula, nguo na nyumba na kadhalika.  Watu wa dunia wamejawa na mambo haya yote mioyoni mwao.  Haja yao kubwa duniani ni kutafuta mali kwa wingi na kuendelea kuongezea mali zao humu duniani.  Wanataka elimu ile mzuri ili wapate kazi mzuri inayowaletea pesa nyingi ili wawe na vitu vya dunia kama nyumba mzuri, gari mzuri na mavazi mazuri.  Hivi ndivyo watu wa dunia hii walivyo, wamezaliwa na mwili na wanajali tu mambo ya mwili, yaani mambo ya hapa duniani.  Watu hawa wamekufa kwa mambo ya Mungu.  Ufalme wa Mungu na utakatifu wake hayana maana kwao.

 

Hivi ndivyo tulivyo tunapozaliwa na ndivyo tunavyoendelea, yaani tukiwa hai tu kwa vitu vya ulimwengu na tukiwa tumekufa kwa mambo ya Mungu.  Hii ndiyo sababu tunapaswa kuzaliwa mara ya pili.  Bila kuzaliwa mara ya pili, tutaendelea kujali tu mambo ya vitu vya dunia na tutashughulika tu na mambo ya ulimwengu huu kwa sababu tumekufa kwa mambo ya Mungu: “Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili.”  Tunapozaliwa mara ya pili, tunakuwa hai kiroho.  Tunakuwa hai katika mambo ya Mungu na mambo ya Mungu yanakuwa ndiyo ya muhimu sana katika maisha yetu.  Paulo alisema, “Wale wanaoishi kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho” (Warumi 8:5).

 

Tunaona wazi hapa ni kwa nini tuzaliwe mara ya pili.  Ikiwa hatufikirii mambo ya kiroho basi hatufai kuingia mbinguni wala kuuona ufalme wa Mungu.  Hii ndiyo sababu Yesu alisema, “Amin, amin, nakuambia, mtu hawezi kuuona ufalme wa Mungu asipozaliwa mara ya pili” (Yohana 3:3).  Ikiwa maisha yetu yote yatashughulika tu na mambo ya dunia hii basi hatuko tayari kwa ufalme wa Mungu kwa sababu ufalme wa Mungu siyo kuhusu mambo ya ulimwengu huu:  “Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu” (Warumi 14:17).  Ni lazima tuzaliwe mara ya pili ili tuwe hai kwa mambo ya Mungu na tuanze kujali mambo ya Mungu kwanza kila wakati.  Yesu alisema, “Utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake; na hayo yote mtazongezwa” (Mathayo 6:33).

 

3.  Ni Roho Mtakatifu peke yake anayemfanya mtu kuzaliwa mara ya pili.

 

Yesu alisema, “Upepo huvuma po pote upendako.  Mvumo wake unausikia lakini huwezi ukafahamu utokako wala uendako.  Ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa na Roho” (Yohana 3:8).  Yesu anatumia mfano wa upepo kutuonyesha kwamba kuzaliwa mara ya pili ni kazi ambayo mwanadamu hawezi kufanya.  Hakuna mtu anaweza kuamuru upepo kupitia mahali fulani.  Hakuna lolote mwanadamu anaweza kufanya ili audhibiti upepo.  “Ndiyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa na Roho.”  Ni Roho Mtakatifu anaamua ni nani atazaliwa mara ya pili, na ni wakati gani, na kwa namna gani.  Hakuna mtu anaweza kuamrisha kazi ya Roho Mtakatifu.  Mtu anapozaliwa mara ya pili kwa Roho Mtakatifu, mambo matatu hufanyika kwake.

 

(i) Anaanza kuelewa kwamba yeye ni mwenye dhambi mbele za Mungu.  Anaanza kuelewa kwamba amevunja sheria ya Mungu na kwamba yeye ako na hatia mbele za Mungu.  Anaelewa kwamba maisha yake yote na tabia yake yote ni makosa mbele za Mungu na Mungu anachukizwa na tabia yake na maisha yake yote.  Ikiwa mtu atazaliwa mara ya pili, ni lazima Roho Mtakatifu amwonyeshe ya kwamba yeye ni mwenye dhambi mbele ya Mungu.

 

(ii) Anaanza kuona kwamba hali yake haina tumaini na haimsaidii kamwe.  Anaanza kuelewa kwamba yeye ni mwenye dhambi anayeelekea jahanum na kwamba hakuna chochote anaweza kufanya.  Anajua kwamba hawezi kujiokoa na kwamba hakuna lolote anaweza kufanya kwa uwezo wake ili ajitoe katika hali hii ngumu.  Anajua kwamba kazi yake ya kidini na matendo yake mazuri hayawezi kumpendeza Mungu.

 

(iii) Anaanza kuelewa kwamba ni Yesu Kristo pekee anaweza kumwokoa.  Anaposoma neno la Mungu na kusikiliza mahubiri kutoka kwa neno la Mungu, anaelewa kwamba Yesu Kristo ndiye mwokozi ambaye Mungu alimtuma na ni yeye tu anaweza kumtendea mema.  Anajua kwamba hawezi kufanya chochote ili ajiokoe na kwamba ikiwa ataokolewa ni lazima aje kwa Yesu kumwomba wokovu.

 

Kutokana na mambo haya tunaona wazi kwamba huwa inachukua muda kabla mtu aokoke.  Wakati huu, Mungu huwa anafanya kazi moyoni mwa mtu huyo.  Roho Mtakatifu humwezesha mtu huyo kuelewa neno la Mungu kwa muda fulani kabla aokoke.

 

4.  Mtu ambaye amezaliwa mara ya pili anakuwa kiumbe kipya.

 

Bwana Yesu Kristo anatumia lugha ya kuzaa anapoongea kuhusu wokovu.  Inakubalika kwamba maisha ya mtu huanza anapozaliwa, yaani mtu huanza kuishi anapozaliwa.  Vivyo hivyo, mtu ambaye amezaliwa mara ya pili, huanza maisha mapya.  Yeye ni mtu mpya, yaani kiumbe kipya.  Hii ndiyo sababu Paulo anasema, “Mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita tazama, yamekuwa mapya” (2 Wakorintho 5:17).  Mtu ambaye amezaliwa mara ya pili, Roho Mtakatifu anaishi ndani mwake.

 

Roho Mtakatifu alikuja siku ya Pentekote kuwafanya watu wa Mungu kuwa wakamilifu na kufanana na Yesu ili wawe tayari kwa Bwana wao wakati atakaporudi kumchukua bibi arusi.  Mtu anapozaliwa mara ya pili, Roho Mtakatifu huja kukaa ndani yake na kuanza kazi ndani ya huyo mtu ya kumkamilisha.  Kila mtu ambaye amezaliwa mara ya pili ana Roho Mtakatifu akiishi ndani mwake na huyu Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani yake ili afanye mapenzi ya Mungu (Wafilipi 2:13).  Hii inamaanisha kwamba Roho Mtakatifu anayafanya mafikira yetu kuwa mapya ili tusiendelee kufikiria kama tulivyokuwa mbeleni.  Roho Mtakatifu anazigeuza hamu zetu ili tusitamani mambo ya dunia kama ilivyokuwa mbeleni.  Baada ya kugeuzwa mawazo yetu na hamu zetu, pia matendo yetu yanabadilika na tunaacha kuishi jinsi tulivyokuwa tunaishi, na kuanza kuishi maisha ya watu wa Mungu.

 

 

Funzo La Tisa, 1 Wathesalonike 1:2-10,

Roho Mtakatifu hutuleta kwa Kristo.

 

Paulo, Barnaba na Timotheo waliingia mji wa Wathesalonike kuhubiri injili kwa watu wa mji huo.  Watu wa mji huo hawakuwa wameisikia habari njema na walikuwa wanaabudu sanamu.  Lakini wakati hawa watatu walihubiri injili katika huo mji, Roho Mtakatifu alianza kufanya kazi katika roho za watu wa Thesalonike.  Matokeo ya kazi ya Roho Mtakatifu katika mioyo ya watu hawa ni kwamba waliokoka.  Hii ndiyo sababu Paulo anasema katika kifungu hiki, “Ndugu zetu mpendwao na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua, kwa maana ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia aliudhihirishwa katika nguvu, katika Roho Mtakatifu, tena ukiwa na udhibitisho kamili ” (1 Wathesalonike 1:4-6).

 

Bwana Yesu Kristo hututuma kuhubiri injili, lakini tunahitaji nguvu na usaidizi wa Roho Mtakatifu ikiwa mahubiri yetu yataleta wokovu kwa wale watakaotusikiliza.  Ni kazi ya Roho Mtakatifu kumleta mtu kwa Kristo, mhubiri hawezi.  Ni Roho Mtakatifu ambaye anamfanya mtu kuzaliwa mara ya pili, na ni yeye anayemleta mtu huyo kwa Kristo.

 

Punde tu mtu anapozaliwa mara ya pili, huanza kusikiliza injili ya Yesu.  Hadithi ya Lazaro katika kitabu cha Yohana 11 ni mfano mzuri wa kueleza jambo hili.  Lazaro alikuwa amekufa na kuzikwa ndani ya kaburi.  Bwana Yesu Kristo alisimama karibu na hiyo kaburi na akamwita Lazaro aje.  Lazaro hangeweza kutii maneno ya Yesu Kristo hadi alipopewa uhai.  Ikiwa hangefanywa hai kwanza Lazaro hangeweza kuja kwa sababu wafu hawawezi kusikia chochote na kutii amri yoyote.  Vivyo hivyo sisi sote tumekufa katika dhambi na makosa.  Ikiwa tutatii sauti ya Mungu anapotuita tuje kwake, ni lazima kwanza atufanye hai.  Hatuwezi kuja kwa Mungu kabla hatujafanywa kuwa hai kwanza.  Ni Roho Mtakatifu ambaye hutufanya kuzaliwa mara ya pili, yaani ni yeye anatufanya tuwe hai kiroho.  Tukiwa hai kiroho, basi tunaweza kuisikia sauti ya Mungu na kuitii na kuja kwake.

 

Hii haimaanishi baada ya kufanywa hai kazi ya Mungu imeisha na mtu anaweza kujiongoza na kufanya chochote anachotaka.  Wokovu, kama tulivyoona, ni kazi ya Mungu kutoka mwanzo hadi mwisho.  Hata baada ya kufanywa hai, Mungu bado anaendelea na kazi yake ya kutuokoa.  Kuna mambo mawili ambayo Roho Mtakatifu hufanya wakati anatuleta kwake Kristo.

 

1.  Roho Mtakatifu hutupatia toba.

 

Kutubu inamaanisha kugeuka kutoka kwa dhambi na kuendelea kugeuka kila wakati kutoka dhambini.  “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia.  Tubuni, na kuiamini Habari Njema” (Marko 1:15).  Biblia inatueleza kwamba toba ni kazi ya Mungu anayofanya mioyoni mwetu.  Biblia inasema hivi kuhusu Kristo, “Mungu alimtukuza akamweka mkono wake wa kuume kuwa kiongozi na Mwokozi, ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi” (Matendo ya Mitume 5:31).  Baadaye katika kitabu hiki cha Matendo ya Mitume tunasoma, “Mungu amewapa hata watu Mataifa toba liletalo uzima wa milele” (Matendo ya Mitume 11:18).

 

Mistari hii inatuonyesha kwamba toba ni kitu ambacho Mungu anatupatia, ikiwa hatatupatia, kwa uwezo wetu hatuwezi kutubu.  Tumezaliwa katika dhambi na tunapenda dhambi zetu sana, hatuko tayari kizichukia dhambi zetu na kuziacha.  Ni wakati tu Mungu anapofanya kazi mioyoni mwetu ndipo tunaona dhambi kuwa jambo baya na kitu cha kuangamiza.  Pasipo kazi ya Mungu mioyoni mwetu tutaendelea kupenda dhambi na kuishi maisha ya dhambi.  Kuna kifungu katika Biblia ambacho kinaeleza jambo hili wazi.  Kinasema,

 

“Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi; bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu.  Inampasa kuwaonya kwa upole wale wapingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtengo wa Shetani ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake” (2 Timotheo 2:24-26).

 

Angalia kwa makini ni nini kifungu hiki kinasema.  Kinasema, “Kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu,” kumaanisha kwamba toba ni kazi ya Mungu, Mungu ndiye hupeana toba kwa watu.  Pia kifungu hiki kinaendelea kusema kwamba, “Na kujua kweli, wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi.”  Hii inamaanisha wakati mtu hajaokoka, yeye huwa anaishi maisha ya dhambi na huwa hafahamu ni nini anafanya.  Yeye hana ufahamu ndani mwake wa kujua kwamba maisha anayoishi hayampendezi Mungu na kwamba anaelekea jahanum milele.  Mungu ndiye humleta mtu huyu katika kufahamu ukweli na kuona hali ile ako ndani yake na kutoka kwa hali hiyo.  Hii ni kutubu.

 

Fikiria kuhusu mtu anaketi gizani kwa sababu nyumba anayoishi haina taa.  Mtu huyu anazungusha mkono ili atafute ni nini kiko karibu na naye.  Anapozungusha mkono anapata kitu kama kamba.  Mtu huyu anachukua kamba hiyo na anaanza kucheza nayo.  Baada ya muda kidogo mtu mwingine anaingia ndani ya hiyo nyumba akiwa na taa na yule mtu aliyekuwa anacheza na kamba anagundua si kamba bali ni nyoka ya sumu mbaya sana.  Mtu huyu anatupa huyo nyoka haraka chini halafu anaanza kumwua kwa sababu nyoka ni mbaya sana na sumu yake inaweza kuua mtu.

 

Hivyo ndivyo alivyo mtu ambaye bado hajaokoka.  Yeye ako gizani na anacheza na dhambi.  Mtu huyu hajui hatari ya dhambi kwa sababu ako gizani na hana taa.  Mungu akimletea nuru yake katika akili yake na moyo wake ndipo ataona anacheza na kitu hatari sana, na ataacha mara moja na kuanza kukiua.  Hii ni kutubu.  Toba inamaanisha kuziacha dhambi zetu na kuanza kuziua.  Tunaweza kufanya hivi wakati Roho Mtakatifu anatupatia nuru na ufahamu na uwezo wa kuzichukia dhambi zetu na kuanza kuziua.  Hadi Roho Mtakatifu atakapoileta nuru tutaendelea kucheza na dhambi hadi itupeleke katika hukumu ya milele.

 

2.  Roho Mtakatifu hutupatia imani.

 

Kama vile toba ni zawadi kutoka kwa Mungu, pia imani ni zawadi kutoka kwa Mungu.  Biblia inasema, “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; wala hii si kwa matendo yenu mema.  Hii ni zawadi ya Mungu” (Waefeso 2:8).  Kuwa na imani ndani ya Kristo inamaanisha kumtumainia yeye pekee kabisa kwa wokovu wetu.  Inamaanisha kumwambia Kristo kwamba, “Mimi sina tumaini lolote na usaidizi wowote wa maisha ya milele.  Mimi sina tumaini lolote la kuingia mbinguni pasipo kupitia kwako.  Ikiwa hutaniokoa, basi nitaangamia milele.”  Hii imani inaweza tu kutoka kwa Roho Mtakatifu.  Hiki si kitu ambacho tunaweza kujifanyia sisi wenyewe.  Ikiwa Roho Mtakatifu hatampatia mtu imani basi mtu huyo ataendelea kujiamini yeye mwenyewe na kazi zake.

 

Hivi ndivyo tulivyo sisi wanadamu.  Tunajisifu sana na tunafikiria kuwa, kwa kazi zetu nzuri za kidini tutamfurahisha Mungu na ataturuhusu tuingie mbinguni.  Watu wengi nchini mwetu hufikiria kwamba wakijaribu sana kwa bidii kumpendeza Mungu kwa kazi zao nzuri na pia kazi zao za kidini, basi Mungu atawakubali na kuwaruhusu waingie mbinguni.  Lakini Biblia inasema kwamba ni Kristo pekee ambaye anaweza kutuokoa na kwamba ni lazima tumtumainie yeye pekee.

 

Habari ya mtume Paulo (Wafilipi 3:1-11) ni mfano mkuu kwa jambo hili.  Kabla hajaokoka, Paulo alitumainia katika kazi zake nzuri na za kidini pia; “Mtu yeyote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumania mwili, mimi ni zaidi.  Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwisreali wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya sheria, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, nilikuwa nalitesa kanisa, kuhusu haki ipatikanayo kwa sheria, mimi nilikuwa sina hatia” (Wafilipi 3:4-6).  Paulo alikuwa na uhakika kwamba ataingia mbinguni akikufa na tumaini lake lilikuwa juu ya kazi yake ya kidini.

 

Lakini alielewa haya yote hayawezi kumwokoa; “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo” (Wafilipi 3:7).  Paulo alielewa kwamba kazi zake njema na za kidini haziwezi kumwokoa, na ikiwa anataka kuokoka ni lazima aende kwake Kristo.  Hii ndiyo sababu Paulo anaandika, “Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi ya kumjua Kristo Yesu Bwana wangu; ambaye kwa ajili Yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; nami nionekane mbele zake nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani” (Wafilipi 3:8-9).

 

Hii ndiyo imani iletayo wokovu ambao Roho Mtakatifu huwapa wote anaowaleta kwake Kristo.  Yaani mtu ambaye anaokoka anagundua kwamba matendo yake mazuri hayatamletea faida yoyote na kwa hivyo anaondoa imani yake hapo, na kumgeukia Kristo na kuweka imani yake kwake pekee kwa wokovu.

 

Haya ndiyo mambo mawili ambayo Roho Mtakatifu hufanya wakati anamleta mtu kwa Yesu Kristo: anampatia mtu huyo toba ili ageuke kutoka kwa dhambi na pia anampatia mtu huyo imani ili amgeukie Kristo na kumtumainia yeye pekee kwa wokovu wake.  Mtu akifanya mambo haya basi ameokolewa kutoka kwa dhambi zake zote milele.

 

 

 

 

Funzo la kumi, Waefeso 5:25-27, Roho Mtakatifu huwatakasa na kuwakamilisha watu wa Mungu.

 

Katika kifungu hiki cha Biblia Paulo anaongea kuhusu jinsi waume wanapaswa kuwapenda wake wao na anawaambia kwamba mfano mkuu wa jambo hili ni Kristo.  Bwana Yesu analipenda kanisa lake na anaonyesha upendo huo kwa jinsi alivyojitoa yeye mwenyewe kwa kanisa na kwa kulitakasa na kulikamilisha kanisa ili liwe kamili siku ile atakaporudi kulichukua.  Hii ndiyo sababu Bwana Yesu alimtuma Roho Mtakatifu wakati alienda mbinguni.  Kuna mambo mawili ambayo tunapaswa kujifunza kuhusu jambo hili.

 

1. Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani ya wote ambao wameokoka akiwatakasa.

 

Mtume Petro anaandika kuhusu, “Kutakaswa kwa Roho Mtakatifu” (1 Petro 1:2).  Kazi ya kutakasa ni kazi ambayo Roho Mtakatifu anafanya ndani mwetu akitufanya tuwe kama Yesu Kristo.  Kazi hii inahusu mambo mawili.

 

(i) Roho Mtakaifu anaondoa dhambi iliyomo ndani mwetu.  Kuna mafunzo fulani siku hizi humu nchini mwetu ambayo yanasema kwamba punde tu mtu anapookoka dhambi inamondokea kabisa.  Kuna watu ambao wanasema kuokoka inamaanisha kuwa mkamilifu na kuwa bila dhambi. Wanasema kwamba ikiwa mtu anayesema ameokoka na apatikane akifanya dhambi, basi hiyo inamaanisha kwamba amepoteza wokovu wake.  Hii ni fundisho linafunzwa sana hapa nchini mwetu siku hizi na si la ukweli.  Hakuna mahali popote Biblia inatuambia kwamba mtu anakuwa mtakatifu na mkamilifu mara tu anapookoka, bali ni wazi kwamba tunaposoma barua za Agano Jipya tunapata kwamba wakristo wako na dhambi ndani mwao hata baada ya kuokoka, kusamehewa na kukubalika katika jamii ya Mungu.

 

Kwa mfano, tunaposoma 1 Wakorintho, tanapata kwamba watu hawa walikuwa wameokoka kwa sababu Paulo anasema, “Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa kuwa watakatifu” (1 Wakorintho 1:2).  Lakini katika kanisa hili kulikuwa na mgawanyiko wa washirika (1 Wakorintho 1:10-12); pia katika kanisa hili mlikuwa na mshirika aliyekuwa akilala na mke wa babaye (1 Wakorintho 5:1); katika kanisa hili mlikuwa na mshirika aliyekuwa akimpeleka mshirika mwenzake kotini (1 Wakorintho 6:1-11); katika kanisa hili mlikuwa washirika ambao walikuwa wanafanya ukahaba (1 Wakorintho 6:12-20) na pia katika kanisa hili kulikuwa na washirika waliokuja katika Meza ya Bwana wakiwa wamelewa (1 Wakorintho 11:21).

 

Sisi wenyewe tunajua kutokana na maisha yetu kwamba tunapokoka, hatui bila dhambi na wakamilifu.  Tunaweza kuzificha dhambi zetu ili watu wasizione, lakini ni wazi kwamba tunakuwa na dhambi ndani yetu hata baada ya kuokoka.  Hii ndiyo sababu Paulo anasema, “Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, nayo Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili.  Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka.” (Wagalatia 5:17).

 

Kazi ya Roho Mtakatifu kwetu sisi wale tumeokoka ni kuitoa dhambi inayobaki ndani mwetu.  Roho Mtakatifu hutumia neno la Mungu kufanya kazi hii.  Anafanya kazi ndani ya mioyo yetu na akilini mwetu ili aiondoe tamaa ya dhambi na kutupatia hamu ya Mungu: “Kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Wafilipi 2:13).  Hii haimaanishi kwamba hatufanyi juhudi yoyote kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.  Kazi ya kutakaswa ni ya kushirikiana: Roho Mtakatifu anazaa matunda ndani yetu na sisi, “Tuyaua matendo ya mwili” (Warumi 8:13).  Hii ni kazi inayoendelea katika maisha yote ya mtu hapa ulimwenguni.  Hii ndiyo sababu Mungu ametupatia silaha, ili tupingane dhidi ya dhambi na kuishinda kabisa.

 

(ii) Roho Mtakatifu anatubadilisha ili tufanane na Bwana Yesu Kristo mwenyewe.  Mambo mawili yanafanyika wakati kazi hii ya kutakaswa inapoendelea ndani ya mtu, kwamba dhambi inaendelea kutolewa ndani mwetu na pia hali yetu yote na tabia yetu yote inaendelea kubadilishwa ili tuendelee kufanana na Kristo mwenyewe.  Yesu Kristo si mfano tu kwetu bali pia ni kielelezo.  Siku moja tutakuwa kama yeye, yaani tutakuwa wakamilifu.  Wakati huo tutakuwa na upendo na huruma, wenye neema na wenye kuwajali wengine jinsi Kristo alivyo.  Hii ndiyo kazi Roho Mtakatifu anafanya ndani yetu, akitubadilisha sisi tufanane na Yesu mwenyewe.

 

Kazi ya kutakaswa ni ya muda mrefu na ni kazi ngumu sana kwetu.  Si jambo linafanyika kwa haraka.  Tunazaliwa tukiwa wenye dhambi na tuliishi maisha ya dhambi hadi siku ile tuliokoka.  Ndani mioyoni mwetu tunazo tabia na hamu mbaya ambazo zinaondolewa pole pole.  Hii kazi ya kutakaswa inaendelea maishani mwetu yote hadi siku ile tutasimama mbele ya Bwana Yesu Kristo atakaporudi.

 

2. Roho Mtakatifu siku moja atatukamilisha.

 

Wakati kuna vita, matokeo ya mwisho huwa hayajulikani.  Mataifa mawili yanapingana kwa miaka mingi, na hakuna mmoja anajua ni nani ataibuka kuwa mshindi.  Vita vya wale wameokoka dhidi ya dhambi si hivyo.  Wale tumeokoka tunajua kwamba ni vita vya muda mrefu na pia ni vita vikali sana na wakati mwingine tunaweza kushangaa kama tutashinda vita hivi.  Shetani ni adui ambaye ana nguvu na pia dhambi iliyo ndani mwetu inaonekana kuwa na nguvu.  Lakini Biblia imetuhakikishia kwamba ikiwa tumeokoka kweli tutashinda.  Hili ni jambo ambalo Mungu anatuhakikishia.  Biblia inasema kwamba Yesu Kristo atajiletea, “Kanisa tukufu, lisilo na doa wala kunyanzi au waa lo lote,  bali takatifu lisilo na hatia” (Waefeso 5:27).  Hii ni ahadi ya Kristo kwetu.  Yesu Kristo alitupenda na alituokoa.  Yesu Kristo ametupatia Roho Mtakatifu ambaye anafanya kazi ndani yetu ili atufanye kuwa wakamili kila siku hadi Yeye mwenyewe atakaporudi kutuchukua.

Kumbuka Roho Mtakatifu ni Mungu na mipango yake haiwezi kushindwa.  Shetani ako na nguvu lakini hawezi kushinda Mungu Roho Mtakatifu.  Dhambi zetu zinatushika kwa nguvu sana lakini haziwezi kumshinda Mungu Roho Mtakatifu.  Mungu ameamua kutufanya tuwe kamili na atatukamilisha.  Hakuna mtu anaweza kuzuia Mungu kufanya kazi yake.  Hii ni faraja kubwa na himizo kubwa kwa wale wote wameokoka.