Header

Katika kijitabu hiki tunajifunza ni nini Biblia inafundisha kumhusu Roho Mtakatifu.  Humu nchini mwetu kuna kuchanganyikiwa kwingi kumhusu Roho Mtakatifu na kazi yake.  Kuna watu wengi wanaongea sana juu ya Roho Mtakatifu na wanasema mambo mengi sana kumhusu, lakini wakati unachunguza maneno yao unapata kwamba wanaongea tu maoni yao wenyewe; hawahubiri vile Biblia inasema.  Hili ni jambo hatari sana.  Tunahitaji kuelewa kwa uangalifu kabisa vile Biblia inafundisha kumhusu Roho Mtakatifu na kazi yake la sivyo hatutaelewa ukristo ni nini.

 

Mafundisho ya Kristo kumhusu Roho Mtakatifu.

 

Masaa machache kabla Yesu kufa msalabani Kalivari, alikutana na wanafunzi wake katika chumba cha juu.  Walikuwa wamemaliza kula, ndipo Yesu Kristo akaanza kuwafundisha.  Mafundisho haya yanapatikana katika kitabu cha Yohana sura ya 13 hadi sura ya 16.  Wakati wa mafunzo haya Bwana Yesu Kristo aliwafundisha wanafunzi wake kumhusu Roho Mtakatifu na kazi yake.  Kuna vifungu vinne katika injili ya Yohana ambapo Yesu Kristo alifundisha kumhusu Roho Mtakatifu.  Katika kijitabu hiki tutaangalia vifungu hivi vinne tuone vile Yesu alifunza kumhusu Roho Mtakatifu.  Hivi ndivyo vifungu tutakavyoviangalia: Yohana 14:15-18; Yohana 14:25-26; Yohana 15:26-27; Yohana 16:8-16.

 

Kwa sababu tunaangazia vifungu hivi vinne kwa wakati huu, unaposoma kijitabu hiki utapata kwamba kuna mambo mengi ambayo hayajazungumziwa ya Roho Mtakatifu.  Kwa mfano kijitabu hiki kimezungumzia machache kuhusu vipaji za Roho Mtakatifu.  Mambo hayo yatazungumziwa katika somo lingine baadaye.

 

Unaposoma kijitabu hiki kumbuka unasoma mafundisho ya Bwana Yesu Kristo.  Kuna uwezekano kwamba kuna mambo ambayo hukubaliani nayo.  Kumbuka kuna watu wengi ambao wamepewa mafundisho kumhusu Roho Mtakatifu ambayo siyo ya ukweli.  Yaani wamefundishwa mafunzo ya mwanadamu badala ya mafundisho ya neno la Mungu.  Labda wewe uko katika hali hiyo.  Umepata mafunzo kutoka kwa watu fulani na unayashikilia kwa nguvu sana ijapokuwa hayatoki kwa Biblia.  Labda umeshikilia kwa nguvu sana mafundisho juu ya maoni ya watu badala ya mafundisho ya neno la Mungu ambalo liko hai.  Katika kijitabu hiki hatutaangalia maoni ya watu kumhusu Roho Mtakatifu bali tutazingatia mafundisho ya Yesu mwenyewe.  Unaposoma mafundisho haya ya Yesu na uone kwamba maoni yako ni kinyume na jinsi Yesu anafundisha, huna budi bali kuacha kushikilia maoni yako na kutii mafundisho ya Yesu Kristo.

 

 

Funzo la Kwanza, Tafadhali soma Yohana 14:15-18.

 

Kuna mambo mawili muhimu hapa ambayo tunapaswa kujifunza kutoka kwa kifungu hiki.

 

1.  Roho Mtakatifu ni Mungu kamili.

 

Biblia inafundisha wazi kwamba wakati tunaongea kumhusu Roho Mtakatifu tunaongea kumhusu Mungu mwenyewe.  Biblia inafundisha kwamba tunampenda, tunamwabudu na tunamtumikia Mungu Mmoja ambaye anaishi milele katika utatu: Mungu Baba, Mungu Mwana, Mungu Roho Mtakatifu.  Kila Mmoja ni Mungu kamili.  Hii inamaanisha kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu kamili.  Ukweli huu wote unapatikana katika mafundisho ya Yesu Kristo katika kifungu hiki.  Katika kifungu hiki Yesu anaongea na wanafunzi wake akiwa karibu kurudi mbinguni.  Yesu alikuwa anajua kwamba wanafunzi wake watafadhaika kwa sababu ya jambo hili na kwa hivyo aliwapatia mafundisho haya ili awahimize na kuwafariji.  Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba anarudi kwa Baba lakini hii haimaanishi kwamba atawaacha.  Katika kifungu hiki Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba hatawaacha kama watoto yatima bali atamtuma Roho Mtakatifu kuwa nao.  Tukiangalia mafundisho haya ya Yesu Kristo kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu tunapata kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu.

 

(i) Kwanza, Yesu anasema, “Baba atawapa msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.”  Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba anaenda, lakini “Msaidizi mwingine” anakuja na kwamba msaidizi huyo atakuwa na wanafunzi hawa milele (msitari 16).  Ni wazi hapa kwamba msaidizi anayekuja ataendelea na kazi ile Yesu Kristo mwenyewe alikuwa akifanya na kazi hiyo ni ya milele.  Atakuwa na wanafunzi hawa milele.  Tunaona hapa kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu.  Ni namna gani Roho Mtakatifu anaweza kufanya kazi milele isipokuwa awe Mungu Mwenyewe?

 

(ii) Pili, Yesu Kristo anasema Roho Mtakatifu ni mwakilishi wake.  Katika msitari wa 18 anasema, “Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.”  Yesu Kristo hasemi “Kuna kitu fulani kitakuja kwenu,” bali anasema, “Naja kwenu.”  Kwa hivyo wakati Roho Mtakatifu alikuja kwa wale wameamini ilikuwa kama Yesu Kristo mwenyewe alikuja.  Hii haimaanishi kwamba Roho Mtakatifu ni Yesu mwenyewe, bali inamaanisha kwamba Roho Mtakatifu ako kiwango sawa na Yesu Kristo: Roho Mtakatifu ni Mungu kamili.  Kama hangekuwa Mungu kamili hangeweza kuiendeleza kazi ile Yesu Kristo alikuwa anafanya.  Roho Mtakatifu hangekuwa Mungu, basi wanafunzi wa Yesu Kristo wangeachwa yatima.

 

Hiki si kifungu pekee kwa Biblia ambacho tunaambiwa kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu.  Katika kitabu cha Zaburi 139:7 Daudi anasema wazi kwamba Roho ni Mungu.  Daudi anasema katika maombi yake, “Niende wapi ni jiepushe na Roho wako?  Niende wapi ni ukimbie uso wako?”  Roho wa Mungu ni uwepo wa Mungu kwa sababu Roho ni Mungu.

 

Katika Agano Jipya pia tunafundishwa kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu.  Wakati Anania alidanganya kanisa, Petro alimwambia, “Anania, kwa nini shetani amekujaa moyoni mwako kumwambia uongo Roho Mtakatifu.  Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu” (Matendo ya Mitume 5:3-4).  Wakati Yesu Kristo alikuwa akieleza jinsi wale wameokoka watakuwa wakibatizwa, alisema tuwabatize kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu (Mathayo 28:19).  Haya ni mambo wazi kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu, kama vile Baba ni Mungu na Mwana ni Mungu.

 

Huu ndiyo ukweli mkuu wa kwanza tunapata katika kifungu hiki, kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe.  Ukweli huu unatuongoza katika mambo mengi muhimu kwetu wakristo.

 

(i) Kwanza, ni lazima tuwe waangalifu sana vile tunafikiria kumhusu Roho Mtakatifu.  Wakristo wengi hawafikirii sana kumhusu Roho Mtakatifu na wakati wanamfikiria, wanafikiria tu mambo ya vipaji na ibada za kuwafurahisha.  Hawaelewi kuwa yeye ni Mungu na kwamba wanapaswa kuwa waangalifu wakati wanawaza juu yake.

 

(ii) Pili, ni lazima tuhakikishe kwamba tumeelewa kabisa kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu.  Katika kifungu hiki cha Yohana tunapata mafunzo mengi sana kumhusu Roho Mtakatifu na kazi yake.  Katika kifungu hiki hakuna mahali popote Bwana Yesu anazungumzia kuhusu vipaji kama kuongea kwa ndimi au miujiza ya uponyaji au ibada za kufurahisha.  Bwana Yesu anasema kwamba Roho Mtakatifu atakuwa mfariji wa wanafunzi wake.  Ni kweli kwamba katika nchi yetu leo siyo wengi ambao wamesoma Biblia kwa uangalifu ili wajue Biblia inasema nini kumhusu Roho Mtakatifu.  Watu wengi wako na maoni yao tofauti tofauti kumhusu Roho Mtakatifu na vile anafanya kazi yake, lakini hawasomi Biblia kuhakikisha kwamba kile wanasema ni ukweli.  Hii ni makosa kubwa sana.  Roho Mtakatifu ni Mungu.  Ikiwa hatutasoma Biblia na kuona vile inafundisha kumhusu Roho Mtakatifu basi hatutawahi kumwelewa Mungu wetu.

 

(iii) Tatu, tanapaswa kuwa waangalifu jinsi tunavyoongea kumhusu Roho Mtakatifu.  Biblia inatuonya juu ya kuongea bila kuwa waangalifu na pia inatuamru kuwa waangalifu wakati tunaongea kumhusu Mungu.  Kwa hivyo ni muhimu sana kufikiria kwa makini sana kabla hatujaongea mambo ya Roho Mtakatifu.  Ikiwa hatujui ni nini Biblia inasema kumhusu Roho Mtakatifu ni vizuri tusiongee mambo mengi kumhusu hadi kwanza tusome Biblia na kujifunza inasema nini kumhusu Roho Mtakatifu.  Kumbuka Roho Mtakatifu ni Mungu na tunapoongea kumhusu Mungu na kazi yake ni lazima tuwe waangalifu sana ili tusiongee maneno yasiyo na heshima na ya kupuuza.  Tukiongea mambo ya Mungu bila kujali tunalosema, tutakuwa tunamkosea heshima Mungu.

 

(iv) Nne, tunapaswa kukumbuka kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu na ni mwenye mamlaka.  Hii inamaanisha kwamba yeye ndiye anaongoza kila kitu duniani.  Siyo mwanadamu anaongoza mambo ulimwenguni bali ni Mungu pekee.  Wakati mwingine wanadamu hufikiria kwamba wanaweza kumwambia Roho Mtakatifu afanye mambo ambayo wanataka yafanyike. Wanafikiria kwamba Roho Mtakatifu ako na nguvu sana na wanaweza kumwongoza.  Wanajua kwamba Roho Mtakatifu hufanya miujiza na kwa hivyo wanafikiria wanaweza kumwambia jinsi atafanya miujiza.  Mafikira haya hayaambatani na Biblia na ni dhambi kuwaza hivyo.  Roho Mtakatifu si mfanyakazi wetu bali sisi ni wafanyakazi wake.  Roho Mtakatifu hayuko chini ya uongozi wetu bali sisi tuko chini ya uongozi wake.  Roho Mtakatifu hayuko hapa duniani kutii amri zetu bali ni sisi tunapaswa kutii amri zake.  Roho Mtakatifu ni Mungu na ako na mamlaka juu ya kila kitu.

 

Mfalme Nebukadreza alisema haya kuhusu Mungu: “Na watu wote wanaokaa duniani wamehesabiwa kuwa si kitu, naye hufanya kama atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa duniani; wala hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, 'unafanya nini wewe'?” (Danieli 4:35).  Maneno haya yanahusu Roho Mtakatifu.  Roho Mtakatifu ni Mungu na anafanya kazi kulingana na mipango yake mwenyewe, yeye si mfanyakazi wa wanadamu bali wanadamu wote ni wafanyakazi wake.  Hatuna uwezo wa kumwamrisha bali yeye ndiye anatuamrisha.

 

Uwezo wa Roho Mtakatifu unaonekana wazi katika wokovu.  Yesu aliongea haya wakati alisema, “Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho” (Yohana 3:8).  Kazi ya wokovu ni kazi yake Mungu wala si kazi ya mwanadamu.  Ni Mungu mwenyewe huamua ni nani ataokoka, si mwanadamu.  Mtoto hawezi kuamua azaliwe, hawezi akasema akiwa tumboni mwa mama kwamba, “Wakati umefika ili nizaliwe, sasa nitatoka tumboni humu.”  Mtoto anazaliwa wakati Mungu anaamua azaliwe.  Watoto wengine huzaliwa mapema zaidi ya wakati uliotarajiwa na wengine huzaliwa baada ya kuzidisha muda uliotarajiwa.  Si mtoto anaamua wakati anazaliwa bali ni Mungu mwenyewe.  Vile vile hakuna mtu anaweza akaamua kuzaliwa mara ya pili.  Mwanadamu amekufa kwa sababu ya makosa na dhambi (Waefeso 2:1), na mtu ambaye amekufa hafanyi uamuzi.  Ni Mungu mwenyewe huamua ni nani anazaliwa mara ya pili na ni wakati gani.  Roho Mtakatifu ni Mungu na ako na mamlaka na uwezo katika wokovu wa wanadamu.  Yeye hufanya kazi yake kulingana na mpango wa Mungu wa Utatu wala si kulingana na mipango ya wanadamu.

 

2.  Roho Mtakatifu anaishi.

 

Kuishi inamaanisha kufikiria, kuhisi na kupanga mambo.  Roho Mtakatifu anaishi.  Tunajua haya kulingana na jinsi Yesu aliongea katika kifungu hiki.  Yesu anamwita Roho Mtakatifu msaidizi.  Msaidizi ni mtu ambaye anasaidia wakati wa mahitaji.  Hii inamaanisha msaidizi ni lazima awe na uhai.  Hawezi kuwa kitu kama mawe au mti.  Pia Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Siwaachi ninyi yatima; naja kwenu.”   Hii pia inatuonyesha kwamba Roho Mtakatifu anaishi: Yeye ndiye uwepo wa Kristo katika watu wake.  Tena katika kitabu cha Matendo ya Mitume tunasoma, “Roho Mtakatifu akasema, 'Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia'” (Matendo ya Mitume 13:2).  Haya yote yanatuonyesha kwamba Roho Mtakatifu anaishi: ndiye msaidizi, na ako kwa niaba ya Kristo Yesu katika watu wa Mungu, na huongea.  Mafundisho haya yanatueleza wazi mambo muhimu sana maishani mwetu ambayo tunapaswa kuzingatia.

 

(i) Ni lazima tuwe waangalifu sana wakati tunaongea kumhusu Roho Mtakatifu.  Wakristo wengi siku hizi wanafikiria kwamba Roho Mtakatifu ni nguvu fulani.  Hii ni makosa sana.  Roho Mtakatifu anaishi na pia yeye ni Mungu.

 

(ii) Tunapaswa kuwa waangalifu jinsi tunafikiria kumhusu Roho Mtakatifu.  Watu wengi bado hawajui kwamba Roho Mtakatifu anaishi na ako na maoni yake na hisia zake kuhusu mambo tofauti tofauti.  Kwa mfano, makanisa mengi wanadai kwamba wako na Roho Mtakatifu wakati wanafanya ibada, lakini hawajawahi kujiuliza swali hili, Je, Roho Mtakatifu anawafikiria vipi wakati wanambudu Mungu.  Je, Roho Mtakatifu anafurahia wakati watu wanaomba maombi marefu na kwa sauti ya juu sana wakijirudiarudia?.  Je, Roho Mtakatifu anafurahia wakati watu kanisani wanaimba wakirudiarudia wimbo moja kwa masaa mengi?  Je, Roho Mtakatifu anafurahia wakati watu wanalazimishwa kutoa pesa kanisani na mchungaji?  Haya ni maswali muhimu sana na ni lazima tujiulize tukiwa katika kanisa la Mungu.

 

(iii) Tunapaswa kukumbuka kwamba Roho Mtakatifu anaishi na kwamba anaangalia vile tunaishi maisha yetu.  Yeye ni Mungu na ako kila mahali.  Ni ukweli wa kuhuzunisha kwamba watu wengi wanafikiria ukristo ni kufanya mambo fulani kanisani au mahali kuna watu wengi.  Ni ukweli wa kuhuzunisha kwamba watu wengi ukristo wao ni wa kujionyesha tu, yaani wako makini sana kuonyesha kwamba wao ni watu wazuri na wa kuheshimika sana na kwamba tabia yao mbele ya watu inastahili.  Lakini wakati watu hawa wako peke yao wenyewe au wako na marafiki wao wa karibu hawajali kuwa wakristo, bali wanakuwa kama watu wa dunia.  Watu hawa wanasahau kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu na anaangalia chochote tutendacho.  Hakuna chochote kimefichwa machoni pa Mungu.  Hatuwezi tukaficha dhambi zetu na mafikira zetu machoni pa Mungu.  Mungu hutuona jinsi tunavyoonekana kwa wengine.

 

 

Funzo la Pili, Tafadhali soma Yohana 14:15-18.

 

Mistari hii imejawa na mafundisho muhimu sana kumhusu Roho Mtakatifu na kwa hivyo katika somo hili la pili tutaangazia mistari hii tena.  Haya ndiyo mafunzo tunayopata kutoka kifungu hiki.

 

1.  Roho Mtakatifu ni Msaidizi wetu.

 

Yesu alisema, “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa msaidizi mwingine” (msitari 16).  Kuna mambo matatu muhimu sana ambayo Roho Mtakatifu anafanya akiwa msaidizi wetu.

 

(i) Roho Mtakatifu anatupatia usaidizi na faraja.  Neno “Msaidizi” pia inaweza kuelezwa kama “Mfariji,” na neno hili inamaanisha mtu ambaye anasimama nasi na kutusaidia wakati wa mahitaji. Roho Mtakatifu alitumwa na Yesu Kristo aje kuwasaidia na kuwafariji wakristo hapa duniani. Baadaye katika kifungu hiki Yesu anasema, “Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia” (Yohana 15:19).  Maisha ya wakristo huku duniani siyo rahisi.  Tunachukiwa na dunia hii kwa sababu sisi ni watu wa Yesu Kristo na kila wakati tunakumbwa na majaribu ya kutaka kurudi dhambini na kumwacha Kristo.  Dunia kila wakati inaendelea kutujaribu kwa anasa na mali za ulimwengu ili tuifuate.  Kuna wengi sana ambao hawashughuliki kupigana vita na dhambi, bali wameamua kuendelea kufurahia anasa na dhambi za dunia hii.  Lakini wale ambao ni waaminifu kwa Bwana Yesu Kristo wameamua kupiga dhambi vita na kwa hivyo wako na hitaji kubwa sana.  Vita dhidi ya dhambi na dunia ni vita vigumu na wakristo hawawezi kushinda kwa nguvu zao wenyewe.  Tunahitaji msaada kutoka mbinguni, hii ndiyo sababu Roho Mtakatifu alitumwa kwetu.  Roho Mtakatifu anaishi dani mwetu na anatusaidia kuishi maisha ya ukristo hapa duniani ambapo dhambi imejaa.

 

(ii) Roho Mtakatifu anatuongoza kwa kutumia neno la Mungu.  Msaidizi ni mtu ambaye anaongoza na pia anapeana mawaidha kwa watu.  Vivyo hivyo Roho Mtakatifu ako humu duniani ili atuongoze.  Tunakumbwa na mambo mengi duniani na wakati mwingi hatujui ni nini tunapaswa kufanya.  Mara mingi hatujui tuishi namna gani ili kumletea Mungu utukufu na heshima.  Roho Mtakatifu hutumia neno la Mungu kutuongoza.  Ni muhimu sana kuelewa kwamba katika kazi yake yote Roho Mtakatifu hutumia neno la Mungu.  Yeye hafanyi chochote kando na Biblia na pia hawezi kuongoza mtu yeyote kinyume na neno la Mungu.  Kwa hivyo kijana akisema kwamba, “Roho Mtakatifu aliniambia nimwoe huyu msichana hata kama yeye hajaokoka,” basi tutakuwa na uhakika kwamba huo ni uongo kabisa kwa sababu Biblia inasema wazi kwamba mtu ameokoka asimwoe mtu hajaokoka.  Kwa hivyo Roho Mtakatifu hawezi kumwongoza kinyume na maandiko ya Mungu.  Hii ndiyo sababu muhimu sana kujua neno la Mungu.  Roho Mtakatifu hafanyi kazi yake bila neno la Mungu bali anatumia neno la Mungu katika kila jambo afanyalo.

 

(iii) Roho Mtakatifu hutupatia faraja kupitia neno la Mungu.  Biblia inaposema mfariji, haimaanishi mfariji wetu wakati tumepatwa na msiba kama kufiwa na mmoja wa jamii yetu.  Bali Biblia inasema kazi ya Roho Mtakatifu ni kuwapa watu wa Mungu uhakikisho kwamba wameokolewa kwa hakika na kwamba wako na maisha ya milele mbinguni baada ya maisha hapa duniani.  Kazi ya uhakikisho ni kazi muhimu sana ya Roho Mtakatifu.  Ni kweli kwamba Yesu Kristo ametuokoa na ametusamehe dhambi zetu zote na tumehesabiwa haki machoni pa Mungu kwa sababu ya imani dani ya Yesu.  Lakini upande mwingine tuko na dhambi ndani mwetu.  Hii inamaanisha kwamba mtu ambaye ameokoka anaweza shushwa moyo kwa haraka, kwa sababu anaona dhambi zake na anazichukia na pia anajua hazimpendezi Mungu, na anashangaa kama Mungu kweli anampenda na kama Mungu kweli atamkubali kuingia mbinguni.  Kwa sababu ya mafikira haya mkristo anaweza kuishi maisha yasiyo ya furaha kwa sababu anafikiria Mungu hampendi kwa sababu ya dhambi zake.  Hii ndiyo sababu moja kuu Yesu Kristo alimtuma Roho Mtakatifu.  Paulo anasema, “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Warumi 8:16). Hii ndiyo kazi ya Roho Mtakatifu akiwa msaidizi wetu, anatuhakikishia kwamba sisi ni watoto wa Mungu.

 

2.  Ulimwengu hauwezi kumpokea Roho Mtakatifu.

 

Yesu anasema katika msitari wa 17, “Ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui.”  Ulimwengu (yaani wale ambao hawajaokoka) hawawezi kumpokea Roho Mtakatifu.  Neno “kumpokea” inamaanisha kumtambua.  Yesu anasema hapa kwamba ulimwengu hauwezi kutambua kwamba Roho Mtakatifu ako na anaendelea na kazi yake hapa duniani.  Roho Mtakatifu hufanya mambo mengi muhimu sana humu duniani, anathibitishia wenye dhambi dhambi zao na anawaleta kwa Kristo ili watubu na kumwamini.  Roho Mtakatifu pia humleta mwenye dhambi katika ufalme wa Mungu na anamfanya kuwa mtu wa jamii ya Mungu, halafu anaanza kazi ya kumbadilisha mtu kutoka ndani.  Tunasikia habari mingi za watu ambao walikuwa wenye dhambi wakuu na ambao waliishi maisha mabaya sana ya dhambi lakini walitubu dhambi zao na maisha yao yakabadilika na wakawa watumishi wakuu wa Mungu.  Hii yote ni kazi ya Roho Mtakatifu, lakini ulimwengu hauwezi kupokea mambo haya.  Walimwengu wako tayari kukubali kwamba maisha ya mtu imebadilika kabisa lakini hawako tayari kukubali kwamba hii ni kazi ya Roho Mtakatifu.  Wanafikiria kwamba mtu mwenyewe amejaribu sana kwa nguvu zake na ndiyo sababu maisha yake imebadilika.

 

Yesu mwenyewe anatueleza sababu gani ulimwengu hauwezi kumkubali Roho Mtakatifu.  Ni kwa sababu haumwoni wala haumtambui.  Walimwengu hawawezi kumwona Roho Mtakatifu kwa sababu yeye hana mwili na huishi katika mioyo ya wanaomwamini Yesu Kristo.  Pia hawamtambui kwa sababu hawajaokoka, ni yule tu ambaye ameokoka anaweza kumjua Mungu.  Mtu ambaye hajaokoka anaweza kujua mambo ya Mungu lakini hawezi kumjua Mungu mwenyewe.  Paulo anasema, “Mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni” (1 Wakorintho 2:14).

3.  Roho Mtakatifu alikuwa anafanya kazi katika Agano la Kale na pia wakati wa Yesu Kristo.

 

Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake hivi, “Ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu  haumwoni wala kumtambua; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu.”  Angalia kwa makini jinsi Bwana Yesu anaongea kuhusu uwepo wa Roho Mtakatifu.  Hasemi, “Roho Mtakatifu atakuwa nanyi,” bali anasema, “anakaa kwenu.”  Hii inamaanisha kwamba wakati Yesu Kristo alikuwa hapa ulimwenguni Roho Mtakatifu pia alikuwa humu akifanya kazi.  Tunajua hii ni kweli kwa sababu katika vitabu vya injili tunaambiwa Roho Mtakatifu alikuwa anafanya kazi katika huduma wa Kristo.  Ni Roho Mtakatifu ambaye alimwongoza Yesu Kristo nyikani ili ajaribiwe na Ibilisi (Mathayo 4:1), na ni kwa “Nguvu za Roho Mtakatifu” Yesu alirudi Galilaya baada ya kujaribiwa (Luka 4:14).  Siku nyingine Yesu alisema, “Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia,” yaani Yesu akimaanisha ni Roho Mtakatifu alimpa nguvu za kuondoa mapepo.  Kwa hivyo ni lazima tuelewe kwamba kazi ya Roho Mtakatifu humu duniani haikuanza siku ya Pentekote.  Si kweli kwamba Roho Mtakatifu alikuwa mbinguni hadi siku ya Pentekote ndipo alishuka kuja duniani mara ya kwanza siku hiyo.  Tunajua Roho Mtakatifu alikuwepo wakati wa Agano la Kale kwa sababu ndiye aliwaongoza manabii wa Agano la Kale kuandika neno la Mungu: “Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu” (2 Petro 1:21).  Wakati wa Agano la Kale na wakati wa Yesu Kristo, Roho Mtakatifu alikuwa humu duniani na alikuwa anakaa na watu wa Mungu.

 

4.  Roho Mtakatifu sasa anaishi ndani mwa watu wote wa Mungu.

 

Yesu anaendelea kusema katika kitabu cha Yohana 14:17, “Anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.”  Hii inahusu siku ya Pentekote.  Siku ya Pentekote Roho Mtakatifu alianza kazi yake hapa duniani kwa njia maalum.  Mbeleni Roho Mtakatifu alikuwa na watu wa Mungu lakini siku ya Pentekote alikuja kukaa ndani ya watu wote wa Mungu.  Hivi ndivyo Yesu alisema, “Mtu akinipenda atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” (Yohana 14:23).

 

Kuna mafundisho fulani nchini mwetu kwamba kuna watu ambao wanajazwa na Roho Mtakatifu na wengine hawajazwi.  Kuna makanisa mengi ambayo yanafundisha kwamba mtu anaweza kuzaliwa mara ya pili na akose kuwa na Roho Mtakatifu na kwa hivyo ni lazima abatizwe na Roho Mtakatifu.  Hivi ndivyo makanisa fulani wanafundisha siku hizi, lakini mafunzo haya siyo ya kweli.  Roho Mtakatifu sasa anaishi ndani mwa kila mtu ambaye amezaliwa mara ya pili.  Siyo kweli kwamba ni wakristo fulani tu wamejazwa na Roho Mtakatifu.  Biblia inasema, “Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake” (Warumi 8:9).  Kila mtu ambaye amezaliwa mara ya pili Roho Mtakatifu anaishi ndani mwake, Roho Mtakatifu ako ndani mwa kila mtu wa Mungu.  Mungu mwenyewe alisema, “Nitawamwagia watu wote Roho yangu” (Matendo ya Mitume 2:17)).  Hii inamaanisha wale wote ambao wameokoka Roho Mtakatifu anaishi ndani mwao, wala si watu fulani tu kati ya wale wameokoka.

 

5.  Roho Mtakatifu ni mwakilishi wa Kristo hapa ulimwenguni.

 

Katika kitabu cha Yohana 14:18 Yesu anasema, “Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.”  Wakati huu Yesu alipokuwa anafundisha katika chumba cha juu, haja yake kuu ilikuwa kuwafariji wanafunzi wake na kuwahimiza.  Baada ya masaa machache wanafunzi wake wangemwona ameshikwa na kuteswa sana na pia kusulubiwa.  Yesu hakutaka wanafunzi wake wapoteze imani yao ndani yake.  Kwa hivyo akawaambia, “Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu.”  Yesu hapa anaongea kuhusu kuja kwake Roho Mtakatifu.  Hii inamaanisha kwamba Roho Mtakatifu anafanana na Yesu kwa kila hali.  Roho Mtakatifu ni Mungu kama vile Yesu Kristo ni Mungu.  Pia hii inamaanisha kuwa Roho Mtakatifu ataendelea kuwatumikia wanafunzi wa Yesu Kristo kama vile Yesu Kristo alivyowatumikia mwenyewe.  Kuna kuchanganyikiwa kwingi sana katika mafunzo haya kwa wakristo siku hizi.  Wakristo wengi hawaoni muungano kati ya kazi ya Yesu Kristo na kazi ya Roho Mtakatifu.  Kulingana na mafikira yao, Yesu Kristo alikuja duniani kama mwokozi na akafa msalabani kwa ajili yetu, naye Roho Mtakatifu alikuja kufanya jambo lingine tofauti kabisa.  Kulingana na maoni ya wakristo wengi siku hizi, Roho Mtakatifu na kazi yake haina uhusiano na Yesu Kristo na kazi yake, na kazi yake Roho Mtakatifu leo haina uhusiano kamwe na kazi ile Yesu Kristo alifanya.  Kwa wakristo wengi, kazi ya Yesu Kristo na kazi ya Roho Mtakatifu ni mambo mawili tofauti na hayana uhusiano kabisa.  Hivi ndivyo wakristo wengi huwaza siku hizi.

 

Ni muhimu sana kujua Roho Mtakatifu ni Mungu kama vile Yesu Kristo ni Mungu na Roho Mtakatifu alikuja kuendeleza ile kazi Yesu Kristo alianzisha.  Hakuna tofauti hata kidogo kati ya  kazi ile Yesu Kristo alifanya wakati alikuwa humu duniani na kazi ambayo Roho Mtakatifu anafanya sasa.  Kumbuka kazi ya wokovu bado haijakamilika.  Bwana Yesu Kristo kupitia kifo chake msalabani alihakikisha wokovu wetu, lakini Roho Mtakatifu alikuja kuendeleza kazi hii hadi mwisho.  Sisi wanadamu tumekufa kwa sababu ya makosa na dhambi na hatuwezi kutii neno la Mungu hadi Roho Mtakatifu kwanza afanye kazi ndani mwetu.  Hatuwezi kwa nguvu zetu kuja kwa Kristo na kutubu na kumwamini hadi Roho Mtakatifu atufanye tuzaliwe mara ya pili.  Kwa hivyo Roho Mtakatifu alikuja kumwakilisha Kristo na kuendeleza kazi aliyoianzisha.

 

 

Funzo la Tatu, Tafadhali soma Yohana 14:25-26.

 

Hiki ni kifungu cha pili kati ya vifungu vinne ambavyo Bwana Yesu Kristo anafundisha kumhusu Roho Mtakatifu na kazi yake.

 

1.  Roho Mtakatifu alitumwa ili awafundishe mitume mambo yote ambayo Yesu aliwafundisha.

 

Yesu anasema, “Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu.  Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yohana 14:25-26).  Wakati tunaposoma vitabu vya injili ni wazi kwamba Bwana Yesu Kristo aliwafunza wanafunzi wake mambo mengi sana na kwa wakati mwingi hawakumwelewa.  Aliwafunza mambo mengi kuhusu maisha yake, kifo chake na kufufuka kwake lakini hawakuelewa.  Aliwafunza mambo mengi kuhusu ufalme wa Mungu lakini wanafunzi wake hawakumwelewa.  Hii ni kwa sababu mtu hawezi akaelewa mambo ya Mungu hadi Roho Mtakatifu amfundishe: “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni” (1 Wakorintho 2:14).

 

Angalia kwa makini ni nini Bwana Yesu Kristo anazungumza hapa.  Bwana Yesu Kristo hasemi Roho Mtakatifu atawafundisha watu mambo ambayo hayako kwa Biblia.  Bwana Yesu Kristo hasemi hapa kwamba Roho Mtakatifu atawafundisha watu fulani mambo fulani ambayo si kila mkristo atapata.  Bwana Yesu Kristo anasema Roho Mtakatifu atawaeleza watu wa Mungu neno la Mungu.  Hii ndiyo sababu Yesu Kristo anasema, “Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu.”  Yesu aliongea na wanafunzi wake mambo mengi lakini hawakuyaelewa mengi ya mafunzo yake.  Na sasa anawaambia, “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote.”  Kuna mambo mawili muhimu tunafundishwa  hapa.

 

(i) Tunaweza tu kuelewa neno la Mungu wakati Roho Mtakatifu anatufundisha.  Mtu hawezi kuelewa neno la Mungu kwa kutumia akili ya kiasili, kwa sababu yanatambulikana kwa jinsi ya kiroho.  Kuna watu wengi ambao wamesoma sana mambo ya huku duniani, lakini hawawezi kuelewa Biblia kwa sababu ni ukweli wa kiroho na unatambulikana kwa jinsi ya kiroho.  Hii inatuonyesha hatupaswi kutilia mkazo sana kwa masomo ya mwanadamu.  Wengi hufikiria ikiwa mtu amesoma hadi chuo kikuu na amepata shahada basi anaweza kuelewa Biblia kwa sababu amesoma, lakini si kweli.  Mtu anaweza kuwa na shahada nyingi kutoka chuo kikuu, lakini haimaanishi mtu huyu ataelewa Biblia.  Kumbuka hata wale wamesoma masomo ya shule za msingi tu wanaweza kuelewa Biblia kwa sababu ni Roho Mtakatifu anayewafundisha.

 

(ii) Watu wa Mungu wote wanapaswa kusoma Biblia.  Kuna maoni ya ajabu hapa nchini kwetu eti si wakristo wote wanaweza kuelewa Biblia.  Wengi wanafikiria ni mchungaji ama kasisi ama askofu pekee anaweza kuelewa Biblia, na kwamba mtu wa kawaida hawezi kuelewa hata akijaribu kusoma Biblia.  Hili si jambo la kweli hata kama wengi hapa nchini mwetu wanaliamini.  Hakuna mahali popote kwa Biblia tumeambiwa ni mchungaji ama kasisi ama askofu peke yake anaweza kuelewa Biblia.  Hakuna mahali popote Biblia inasema mtu wa kawaida akisoma Biblia hawezi  kuelewa, bali tunaambiwa Roho Mtakatifu atamfunza yeyote anayesoma Biblia na anataka kuielewa.  Si lazima tuwe na shahada ndiyo tuweze kusoma na kuelewa Biblia.  Yeyote anayesoma Biblia kwa uangalifu na kwa maombi na unyeyekevu, Roho Mtakatifu atamfunza Biblia.

 

2.  Roho Mtakatifu alikuja kuwakumbusha wanafunzi wa Yesu mafundisho yale Yesu aliwafundisha.

 

Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba Msaidizi, “atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yohana 14:26).  Tunaweza kushangaa ni kwa nini wanafunzi wa Yesu walikuwa wakumbushwe kila kitu Yesu aliwafunza.  Jibu ni kwamba baada ya Yesu kurudi mbinguni kwa Baba, wanafunzi hawa walikuwa na kazi mbili muhimu sana za kufanya:

 

(i) Wanafunzi hawa walikuwa na kazi ya kufundisha kanisa la kwanza.  Baada ya Bwana Yesu kurudi kwa Baba, Roho Mtakatifu alikuja na idadi ya wafuasi wa Yesu ikaongezeka kwa haraka sana.  Siku ya Pentekote peke yake watu 3,000 waliokoka na wakawa wafuasi wa Yesu, na wiki zilizofuata maelfu ya wengi walimwamini Yesu Kristo.  Biblia ni wazi kwamba wakati watu wanaokoka ni lazima waendelee kufundishwa kuhusu imani ya kikristo ndipo waweze kukua katika ukristo.  Mtu akiokoka anakuwa kama mti ambao umepandwa katika mahali penye upepo mwingi na unahitaji kuweka mizizi kwa haraka ndani ya udongo ili usipigwe na dhoruba ya upepo.  Hii ndiyo sababu katika kanisa la kwanza mitume wote walishughulika na mambo ya kufundisha neno la Mungu (Matendo ya Mitume 6:4).  Msingi wa ukristo ni mafundisho na kazi ya Bwana Yesu Kristo.  Wakati tunafundisha imani ya ukristo huwa tunafundisha Yesu Kristo ni nani, na ni nini alifanya, na ni nini alifunza.  Kwa hivyo wanafunzi wa Yesu walikuwa wakumbushwe yote Yesu Kristo aliwafunza wakati alikuwa nao.  Walikuwa wanapaswa kukumbuka yote Yesu Kristo aliwafunza kwa miaka mitatu wakati alikuwa nao.  Roho Mtakatifu alikuja ili afanye kazi hii ya kuwakumbusha.

 

(ii) Wanafunzi wa Yesu Kristo walihusika kuandika neno la Mungu.  Miaka mingi baada ya kufa na kufufuka na kupaa mbinguni kwa Yesu Kristo, wanafunzi wake waliandika mambo mengi kuhusu maisha yake hapa duniani.  Vitabu vingi kama hiki cha injili ya Yohana kiliandikwa zaidi ya miaka hamsini baada ya Yesu kurudi mbinguni.  Je, Yohana (ambaye alikuwa amezeeka sana wakati aliandika injili hii) angekumbukaje mafunzo ya Yesu Kristo?  Je,Yohana alikumbuka namna gani mafundisho ya Yesu Kristo wakati walikuwa chumba cha juu kabla Yesu kusulubiwa?  Jibu ni kwamba Roho Mtakatifu alimkumbusha.  Hii ilikuwa kazi muhimu sana ya Roho Mtakatifu wakati wa kanisa la kwanza: Roho Mtakatifu aliwaongoza wanafunzi wa Yesu kuandika Agano Jipya, kama vile aliwaongoza manabii kuandika Agano la Kale (2 Petro 1:19-21).

 

Tunapaswa kuelewa basi ni muhimu kufunza neno la Mungu na si vizuri kuhubiri na kufunza maoni na mafikira yetu.  Ni ukweli wa kuhuzunisha kwamba humu nchini wako wengi wachungaji na wahubiri ambao hawaelezi ukweli ambao unapatikana katika neno la Mungu kwa makanisa yao.  Mara mingi tunamwona mhubiri ama mchungaji akisoma mistari michache kutoka kwa Biblia halafu anatumia muda mrefu sana akieleza maoni na mawazo yake na pia kueleza hadithi zisizofaidisha kanisa.  Haya ni makosa makubwa kwa sababu mchungaji huyu amefunza mambo machache sana kutoka kwa Biblia.  Roho Mtakatifu alikuja ili awafundishe wanafunzi wa Yesu yale yote Yesu aliongea.  Maneno yale Yesu aliongea ni ya muhimu sana.  Wanafunzi wa Yesu hawakuyaelewa yote na Roho Mtakatifu alikuja kuwawezesha kuyaelewa.  Pia neno ambalo limeandikwa katika Biblia ni la umuhimu sana.  Ni jukumu la kila mhubiri kujifunza Biblia kwa makini ili aweze kujua kwa uhakika vile kifungu fulani kinasema.  Ndipo anaweza kukihubiri kile kifungu na kuwaeleza wanaosikiliza vile kinahusu maisha yao.  Haya ndiyo mahubiri Mungu anaamuru.

 

 

Funzo la Nne, Tafadhali soma Yohana 15:26-27.

 

Katika kifungu hiki Yesu anasema, “Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, yeye atanishuhudia.  Nanyi pia mnanishuhudia. Kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami.”

 

Kuna mafundisho manne muhimu sana tunafundishwa hapa.

 

1.  Roho Mtakatifu alitumwa siku ya Pentekote na Bwana Yesu Kristo.

 

Katika kifungu hiki Yesu anasema, “Ajapo huyo Msaidizi nitakayewapelekea.”  Wakati Yesu alirudi kwa Baba baada ya kufufuka, alimtuma Roho Mtakatifu aje duniani.  Hii ndiyo sababu wakati Petro alieleza mambo ambayo yalikuwa yametendeka siku ya Pentekote alisema, “Basi yeye, akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu, na kupokea kwa Baba ile ahadi ya Roho Mtakatifu, amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisikia” (Matendo ya Mitume 3:32-33).  Kuna mambo muhimu tunapaswa kujua kuhusu kuja kwa Roho Mtakatifu.

 

(i) Inaonyesha kwamba wokovu wetu ulipangwa kwa uangalifu sana na Mungu wetu.  Mungu Baba mwenyewe alipanga ni nani atakayeokolewa na akamtuma Mwanawe Yesu Kristo ili afe msalabani ili awaokoe wale Mungu aliwachagua.  Baada ya Yesu Kristo kumaliza kazi yake msalabani, na kurudi mbinguni alimtuma Roho Mtakatifu.  Kazi ya kuwaokoa wenye dhambi ilipangwa kwa utaratibu sana kutoka mwanzo hadi mwisho.

 

(ii) Inaonyesha kwamba Roho Mtakatifu alikuja kuendeleza na kumaliza kazi ile Yesu Kristo alianzisha.  Hili ni jambo ambalo watu wengi hawalielewi sawasawa.  Wakristo wengi wanafikiria kwamba matendo ya Yesu Kristo hayana husiano kamwe na matendo ya Roho Mtakatifu.  Wengi hawaelewi kwamba Roho Mtakatifu alikuja kuendeleza kazi ile ile tu ya Yesu Kristo.

 

(iii) Inatuonyesha kwamba Roho Mtakatifu hayuko chini ya uongozi wa mwanadamu.  Haya ni makosa makubwa ambayo wengi hufanya.  Kuna wengi wanafikiria wanaweza kuwawekea mikono watu na kuwapatia Roho Mtakatifu.  Mara mingi tunasikia kwa mikutano watu wakiitwa mbele ili “wampokee Roho Mtakatifu.”  Halafu mchungaji ama mhubiri anawawekelea mikono watu hawa na kuwaambia kwamba sasa wamepokea Roho Mtakatifu.  Kile mchungaji ama mhubiri huyu anaonyesha ni kwamba Roho Mtakatifu ako chini ya uongozi wake na anaweza kumpatia mtu yeyote.  Hii, tafadhali, sivyo Biblia inafundisha.  Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe na alikuja kukamilisha ile kazi Yesu Kristo alianzisha.

 

 

 

2.  Roho Mtakatifu alitumwa kutoka kwa Mungu Baba.

 

Yesu anasema, “Huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba.”  Ni wazi katika msitari huu kwamba Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu wanafanya kazi pamoja katika mpango huu mkubwa wa wokovu.  Si kweli kwamba Roho Mtakatifu na Bwana Yesu Kristo wanafanya kazi hii ya wokovu wakiwa kando na Mungu Baba.  Mungu Baba alihusika katika kila hatua ya mpango wa wokovu.  Roho Mtakatifu alikuja kutoka kwa Baba na alitumwa duniani na Mwana.  Mpango wa wokovu ni mpango wa Mungu wa Utatu.

 

3.  Roho Mtakatifu alikuja kumshuhudia Bwana Yesu Kristo.

 

Neno “kushuhudia” linamaanisha kueleza jambo ambalo limetokea.  Mtu akiwa kotini hushuhudia nini aliona na nini alisikia: yaani anaeleza jambo lililotokea ambalo yeye mwenyewe aliliona na kulisikia.  Roho Mtakatifu alikuja kushuhudia kwamba Bwana Yesu Kristo alikuja duniani kuwaokoa watu wake kutoka kwa dhambi zao.  Kuna njia mbili ambazo Roho Mtakatifu hushuhudia kuhusu Bwana Yesu Kristo.

 

(i) Roho Mtakatifu aliwashuhudia wanafunzi wa Yesu kuhusu kazi ya wokovu ya Yesu Kristo. Petro alisema, “Mungu wa Baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti.  Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe mkuu na mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi.  Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio” (Matendo ya Mitume 5:30-32).  Ni Roho Mtakatifu ambaye aliwapa wanafunzi wa Yesu kuelewa vizuri maana ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo.  Ni Roho Mtakatifu ambaye aliwaeleza wanafunzi wa Yesu kuhusu mpango wa wokovu na jinsi ulikuwa unafanyika.  Hii ndiyo sababu Yesu alisema, “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake” (Yohana 16:13).

 

(ii) Roho Mtakatifu aliwapa wanafunzi wa Yesu uwezo na himizo ya kumshuhudia Kristo.  Yesu anasema hapa, “Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayempeleka kutoka kwa Baba, yeye atanishuhudia.  Nanyi pia mnanishuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami.”  Toka siku ya Pentekote na kuendelea, wanafunzi wa Yesu walihubiri Kristo kila mahali, hata wakati walitishwa na kuamrishwa wasihubiri.  Hii ni kwa sababu walipewa uwezo kutoka juu wakati Roho Mtakatifu alikuja.  Ni Roho Mtakatifu aliwaongoza katika Yerusalemu, na katika Uyahudi na Samaria na hata mwisho wa nchi (Matendo ya Mitume 1:8).

 

 

 

Funzo la Tano, Tafadhali soma Yohana 16:8-11.

 

Katika kifungu hiki, Bwana Yesu anaongea kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu ulimwenguni.

 

1. Roho Mtakatifu alikuja kuuhakikishia ulimwengu kwa habari ya dhambi.

 

Yesu anasema, “Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.  Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi.”  Katika mistari hii Yesu anaongea kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu ambaye atawahakikishia watu wa ulimwengu habari ya dhambi zao.  Watu wale hawajaokoka huishi maisha ya dhambi na watahukumiwa kwa dhambi zao.  Inashangaza kuona kwamba kuna dhambi moja hapa ambayo Roho Mtakatifu anawahakikishia wale watahukumiwa: kwamba hawamwamini Bwana Yesu Kristo.  Biblia inaeleza wazi kwamba dhambi za wale hawajaokoka ndizo zitawapeleka jahanamu.  Biblia inaendelea kueleza kwamba dhambi ya kutomwamini Yesu Kristo ni dhambi kubwa kuliko dhambi yoyote.  Hii ni kwa sababu Roho Mtakatifu mwenyewe (ambaye ni Mungu) ameshuhudia kwamba Yesu Kristo ndiye mwokozi aliyetumwa kutoka kwa Mungu na mitume wa Yesu Kristo pia wameshuhudia hivi.  Ni muhimu sana kujua kwamba sababu kuu ya wale hawajaokoka kupelekwa motoni wa milele ni kwamba hawakumwamini Bwana Yesu Kristo.  Hii ndiyo sababu kuu ya kuondolewa kutoka kwa Mungu na kutupwa jahanamu milele.  Si kwa sababu waliishi maisha ya dhambi tu humu duniani, bali ni kwa sababu hawakumwamini Mwana wa Mungu.

 

Labda mfano huu utatusaidia kuelewa zaidi jambo hili.  Fikiria kuhusu mtu asiyejua kuogelea na ameanguka ndani ya mto wa kina kirefu na anaendelea kuzama majini.  Mvuvi anakuja kwa haraka na mashua yake kumsaidia, anampa mkono na anamwambia, “Shika mkono wangu nami nitakuokoa,” na kwa sababu zisizoeleweka mtu huyu anakataa kutii.  Anakataa kabisa kuushika mkono wa mvuvi huyu na kwa hivyo anaangamia.  Baadaye wazee wa kijiji wanaita mkutano ili wachunguze ni nini ilisababisha kifo cha mtu huyu, na wanaanza kwa kuuliza swali hili, “Ni kwa nini mtu huyu alikufa?”  Ni kweli kwamba watapata majibu tofauti na maoni tofauti ya swali hili: wengi watasema alikuwa mtu asiyejali na ndiyo sababu alitembea karibu na mto na akaanguka dani.  Wengine watasema hakujua kuogelea ndiyo sababu alikufa, na pia wengine watasema mambo mengine mengi.  Haya yote ni majibu ya ukweli lakini sababu kuu ya kifo cha mtu huyu ni kwamba hakushika mkono wa mvuvi aliyekuja kumtoa akizama majini.  Vivyo hivyo wale wanaokufa ndani ya dhambi zao na kuenda jahanamu milele wanaangamia kwa sababu kadhaa: Kwa sababu walizaliwa wakiwa wenye dhambi na wenye makosa na pia kwa sababu wameishi maisha ya dhambi na kadhalika.  Lakini sababu kuu ya watu hawa kuangamia jahanamu milele ni kwamba walikataa kuja kwa Yesu Kristo ili awaokoe.

 

 

 

2.  Roho Mtakatifu alikuja kuuhakikishia ulimwengu kwa habari ya haki.

 

Yesu anasema kwamba Roho Mtakatifu atauhakikishia ulimwengu, “Kwa habari ya haki kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba wala hamnioni tena.”  Ili tuelewe jambo hili vizuri ni lazima kwanza tuhakikishe tumelewa neno “haki.”  Biblia inafundisha mambo mawili kuhusu “haki.”

 

(i) Kwanza Biblia inasema kwamba haki inamaanisha kutii sheria ya Mungu yote bila kukosea hata kidogo.  Mtu ambaye maishani mwake yote amefuata sheria ya Mungu bila kukosea hata siku moja ndiye anayeitwa mwenye haki.  Hivi ndivyo neno hili linamaanisha.

 

(ii) Pili Biblia inafundisha kwamba njia moja tu mtu anaweza kuwa mwenye haki ni kupitia kwa imani ndani ya Yesu Kristo.  Paulo anasema, “Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio” (Warumi 3:21-22).  Kwa urahisi Biblia inasema kwamba sisi wanadamu hatuwezi tukafuata sheria ya Mungu na kuitii kabisa.  Lakini Bwana Yesu Kristo alitii sheria ya Mungu kwa ukamilifu wote na ametupatia huo utiifu wake.  Tumehesabiwa haki machoni pa Mungu kwa sababu Bwana Yesu Kristo hutupatia haki yake.

 

Kwa hivyo Yesu anasema hapa kwamba Roho Mtakatifu alikuja kuuhakikishia ulimwengu kwa habari ya haki kwa sababu anaenda zake kwa Baba baada ya kuishi maisha matakatifu humu duniani.  Sababu kuu ya wale ambao hawajaokoka kukosa haki ni kwamba hawajakuja kwa Kristo kuiomba.  Wangekuja kwake Kristo, angewapa haki yake.  Ukweli kwamba Kristo amekwenda kwa Baba inaonyesha kwamba aliishi maisha ya haki humu dunia, kwa sababu kama hangeishi maisha ya haki,  basi hangeenda kwa Baba, bali angetupwa mbali na uwepo wa Mungu milele.  Kwa hivyo Roho Mtakatifu atauhakikishia ulimwengu kwa habari ya kukosa haki.

 

3.  Roho Mtakatifu alikuja ili auhakikishie ulimwengu kwa habari ya hukumu.

 

Yesu anasema kwamba Roho Mtakatifu atauhakikishia ulimwengu kwa habari ya hukumu “kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa.”  Biblia inaeleza wazi kwamba siku moja Yesu anarudi kuwahukumu waliokufa na walio hai.  Pia Biblia inasema kwamba hukumu ya Mungu ni jambo linaloendelea, siyo jambo litakalofanyika tu siku ile Yesu atarudi mara ya pili, hata sasa hukumu ya Mungu inaendelea.  Lakini tunapowatazama watu wa dunia vile wanaishi ni wazi kwamba hawaelewi Mungu anahukumu dhambi.  Wangeamini kweli Mungu ni mtakatifu na anahukumu dhambi, hawangeishi jinsi wanavyoishi.

 

Watu wengi duniani hufikiria kwamba maneno ambayo Biblia inaongea kuhusu Mungu akiadhibu dhambi siyo ya maana sana.  Wanafikiria kwamba Mungu ni kama mzazi ambaye anatisha mtoto wake kwamba akifanya jambo fulani atampiga.  Mtoto huyu anaweza kufanya jambo alilokatazwa na mzazi akose kuchukua hatua yoyote kwa sababu alikuwa tu anamtisha.  Watu wengi hufikiria Mungu ako namna hiyo, yaani anatisha tu bila kuchukua hatua yoyote ya kuhukumu wenye dhambi na kuwapeleka jahanamu.

 

Kuna jambo moja ambalo linatuhakikishia kwamba ni kweli Mungu ni mtakatifu na kwamba huhukumu dhambi na wenye kufanya uovu: Ukweli huu unaonekana kwa sababu tayari Mungu amekwisha kumhukumu yule mkuu wa ulimwengu.  Msalabani kalivari Bwana Yesu Kristo alimshida shetani na akamhukumu.  Ukweli kwamba tayari Mungu amekwisha kumhukumu mkuu wa ulimwengu ni wazi kwamba yeye ni mtakatifu na ni kweli kwamba atahukumu wote walioishi maisha ya dhambi.  Hii ndiyo sababu Yesu Kristo anasema kwamba Roho Mtakatifu atauhakikishia ulimwengu kwa habari ya hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu tayari amekwisha kuhukumiwa.  Yesu Kristo anasema kwamba Roho Mtakatifu atawahakikishia watu habari ya dhambi zao na atawahukumu.

 

 

Funzo la Sita, Tafadhali soma Yohana 16:12-16.

 

Haya ndiyo maneno ya mwisho ya Bwana Yesu Kristo kumhusu Roho Mtakatifu.  Mambo ambayo Yesu anafundisha hapa alikwisha fundisha hapo mbeleni lakini kwa sababu ni mambo ya umuhimu mkubwa, hapa anayarudia tena.  Haya ni mambo muhimu sana kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu, na ndiyo sababu Yesu anayafundisha tena ili ayatilie mkazo.

 

1.  Roho Mtakatifu alitumwa kuja kuwafundisha wanafunzi wa Yesu Kristo neno la Mungu.

 

Yesu alisema,”Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.”  Bwana Yesu Kristo aliwafundisha wanafunzi wake mambo mengi sana ambayo hawakuelewa wakati huo.  Ni kweli kwamba wanafunzi wa Yesu hawakuelewa mambo mengi kuhusu ufalme wa Mungu hata baada ya kuwafundisha kwa muda mrefu na kwa njia wazi.  Na pia hata baada ya kufufuka kwake tunasoma kwamba walimwuliza, “Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?” (Matendo ya Mitume 1:6).  Walikuwa wangali wakifikiria kwamba Yesu alikuja kuanzisha ufalme katika nchi ya Israeli na kuweka ikuru yake Yerusalemu.

 

Katika kifungu hiki basi Bwana Yesu Kristo anawaeleza wanafunzi wake kwamba wakati Roho Mtakatifu atakapokuja atawaeleza wazi zaidi yale mafundisho Yesu mwenyewe aliwafunza.  Ni lazima tukumbuke kwamba Roho Mtakatifu hakuja ili awape watu ufunuo mpya, bali alikuja kuwaongoza katika ukweli ambao walikuwa tayari wamepewa na Yesu.  Yesu Kristo alikuwa amewapa wanafunzi wake mafunzo mengi ambayo yalikuwa kwa akili zao ijapokuwa hawakuwa wameyaelewa kabisa.  Wakati Roho Mtakatifu alikuja aliwapa kuelewa vizuri mafunzo yale Yesu Kristo aliwafundisha.  Hapa tunafunzwa mambo mawili.

 

(i) Neno la Mungu linatosha kwa kila hitaji.  Roho Mtakatifu hakuleta ufunuo mpya zaidi ya yale wanafunzi wa Yesu Kristo walikuwa wamepokea kutoka kwa Yesu mwenyewe.  Si kweli kwamba Roho Mtakatifu aliwafundisha wanafunzi wa Yesu Kristo ukweli na mafundisho mengine ambayo hawakuwa wamesikia mbeleni, hata mafundisho yanayopatikana katika maandiko ya mtume Paulo Yesu aliwafundisha wanafunzi wake.  Roho Mtakatifu alichukua mafundisho ya Yesu ambayo ni kama mbegu na aliinyunyizia maji ili ichipuke ndani ya mioyo na akili zao ili wayaone mafundisho ya Yesu kwa wazi kabisa na kuyafafanua zaidi katika maandiko yao.  Tunaposoma maandiko yaliyoandikwa na watu kama Petro, Paulo, Yakobo na Yohana, tunasoma tu mambo ambayo Yesu Kristo alifundisha.  Mitume waliyaelewa mafudisho haya na wakayaweka vizuri kwa maandiko ili watu wasome.  Hii inamaanisha Roho Mtakatifu hakuja kuwapa watu wa Mungu ufunuo mpya.  Kuna watu wengine humu nchini mwetu ambao wanasema kwamba Roho Mtakatifu anawafunulia mambo fulani ambayo hayapatikani kwa Biblia.  Ajabu ni kwamba mambo haya wanadai kufunuliwa ni kinyume na Biblia.  Hii ndiyo sababu moja wakristo hapa nchini mwetu hawana haja ya kusoma Biblia kwa makini, kwa sababu wanaamini kwamba Biblia haitoshi na kwamba Roho Mtakatifu atawapatia mafundisho mapya kila siku.  Haya ni makosa makubwa sana.  Roho Mtakatifu alitumwa ili afundishe yale Yesu Kristo alikuwa amekwisha kuwafundisha mitume wake.  Roho Mtakatifu anaweza tu kutupatia kuelewa zaidi ya kile tu kimeandikwa kwa Biblia.  Ikiwa hatusomi Biblia basi hatuwezi kupata kutoka kwa Roho Mtakatifu uwezo wa kuelewa zaidi neno la Mungu na tutabaki kuwa wakristo wachanga.

 

(ii) Biblia inaweza kueleweka na kila mtu wa Mungu kwa sababu ni Roho Mtakatifu anawapa watu wa Mungu kuelewa neno lake.  Kuna mamilioni humu nchini ambao wanaamini kwamba ni lazima mtu awe mchungaji, yaani “Mtu wa Mungu,” kabla aelewe Biblia.  Wanaamini kwamba ikiwa mtu wa kawaida ambaye si mchungaji, ama “Mtu wa Mungu” akijaribu kuisoma Biblia hataelewa.  Watu hawa wanaamini kwamba ni watu fulani mashuhuri ambao wanaweza kuielewa Biblia.  Hii si kweli kabisa.  Roho Mtakatifu ametumwa kwa kila mtu wa Mungu na siyo watu fulani peke yao, na kazi yake inaendelea ndani ya kila mkristo bali si wakristo fulani.  Ikiwa mtu anataka kujua ni nini iko ndani ya Biblia na Biblia inasema nini na anataka kuelewa, kile anapaswa kufanya ni kusoma Biblia kwa makini na kwa maombi, akimwuliza Roho Mtakatifu amwezeshe kuelewa.  Anapofikiria na kutafakari mambo ambayo amesoma, atapata kwamba polepole ataendelea kuelewa zaidi Biblia na kujua jinsi ya kuishi katika nuru ya neno la Mungu.

 

2.  Roho Mtakatifu alikuja kumtukuza Kristo.

 

Yesu anasema katika kifungu hiki, “Yeye atanitukuza mimi.”  Njia ile Roho Mtakatifu anatumia kumtukuza Yesu ni kwamba anatufundisha tabia na mafundisho yake Bwana Yesu Kristo.  Hii ndiyo Yesu anamaanisha wakati anasema katika kifungu hiki, “Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.”  Bwana Yesu Kristo ni Mungu kamili.  Hii ndiyo sababu anasema, “Na yote aliyo nayo Baba ni yangu.”  Yesu ako na tabia yote aliyo nayo Mungu Baba.  Kwa hivyo Roho Mtakatifu humletea utukufu Yesu Kristo kwa kuwaeleza watu wa Mungu Yesu ni nani.  Tunapomtazama sana Bwana Yesu Kristo na kuelewa yeye ni nani, basi tunaona utukufu wake tunapofahamu zaidi yeye ni nani.

 

Mambo ambayo tunaelezwa hapa sisi wakristo leo ni kwamba tunamletea Mungu utukufu kwa kumhubiri Yesu kwa ulimwengu uliopotea.  Wakristo wengi siku hizi wanasema nia yao kuu ni kumletea utukufu Mungu.  Lakini ni vipi wanafanya jambo hili?  Jibu ni kwamba maisha ambayo tunaishi na meneno ambayo tunasema yanafaa kuonyesha ulimwengu Mungu ni nani.  Ni lazima tuzungumze kumhusu tukieleza watu vile alivyo na jinsi anafanya kazi.  Ni lazima tufuate mfano wa Kristo ili watu wakituangalia waone Yesu ni nani maishani mwetu kila siku.  Hivi ndivyo tunapaswa kumletea utukufu Mungu katika dunia hii iliyopotea.