Header

Kusudi la kitabu hiki ni kueleze ni nini Biblia inafunza kuhusu mwanadamu na dhambi.  Tutasoma kitabu cha Mwanzo sura ya 1 hadi ya 5.  Katika sura hizi tunapata yale ambayo tunafaa kujua kuhusu mwanadamu na dhambi.  Tafadhali kitumie kijitabu hiki kwa kukusaidia kusoma sura hizi za Mwanzo.  Hakikisha kwamba wakati unasoma mafunzo haya uko na Biblia yako karibu nawe.  Kila funzo litatoka kwa mojawapo wa hizi sura tano.  Hakikisha kwamba unasoma mistari katika sura hizi kwa uangalifu sana kabla ya kusoma kijitabu hiki.  Pia kuna mistari kutoka katika vitabu vingine vya Biblia ambayo tumenukuu kuhakikisha kwamba tunaushaidi kwa yale tunasema.  Hakikisha kwamba unasoma mistari hii pia kwa uangalifu kabla ya kuendelea na mafunzo katika kijitabu hiki.

 

Funzo la Kwanza: Tafadhali soma Mwanzo 1:26-31.

 

Katika Mistari hii tunajifunza mambo mawili.

 

1.  Mungu ndiye aliyemwumba mwanadamu.

2.  Mungu alimwumba mwanadamu katika mfano wake.

 

Katika funzo hili tunatazama mambo haya mawili.

 

I.  Mungu ndiye aliyemwumba mwanadamu.

 

Wakati wana wetu wanaenda shuleni, wanafunzwa kwamba mwanadamu hakuumbwa na Mungu, bali alitoka kwa aina fulani wa mnyama ambaye alikuwa akibadilika badilika kila wakati hadi alipokuwa mwanadamu.  Jambo hili si la ukweli.  Ni jambo la uongo kwamba mwanadamu alitoka kwa mnyama na baadaye akawa mwanadamu.  Sisi sote tuliumbwa na Mungu.  Ukweli huu kwamba mwanadamu aliumbwa na Mungu unamaanisha mambo mawili muhimu sana.

 

1.  Kwanza, jambo hili linamaanisha kwamba kila mwanadamu ni kiumbe muhimu sana.  Adamu alikuwa kiumbe muhimu sana cha Mungu; kwa hivyo sisi ambao ni watoto wa Adamu ni watu muhimu sana pia.  Jambo hili linaonekana wazi wakati tunaposoma kitabu cha Mwanzo sura ya 1 na ya 2.

 

(i) Kwanza kabisa tunaona kwamba Mungu aliumba mahali ambapo mwanadamu angeishi  ndipo baadaye akamwumba mwanadamu.  Mungu hakuumba kwanza mwanadamu ndipo baadaye akaumba mahali pa mwanadamu kuishi.  Kwanza Mungu aliumba kila kitu vyema ndipo baadaye akamwumba mwanadamu kuonyesha kwamba mwanadamu ni kiumbe muhimu sana.  Bustani ya Edeni ndiyo ilikuwa mahali pa mwanadamu kuishi na mimea ambayo ilikuwa huko ndiyo ilikuwa chakula chake.  Kwa mfano, jamii moja huko mashambani ambayo inatarajia kuwa na mgeni, kwa muda mrefu inamtayarishia mahali ambapo atalala wakati atakuja.  Ikiwa watatumia bidii sana kwa kumtayarishia mahali pa kukaa, basi inaonyesha kwamba huyo mgeni ni mtu muhimu sana kwao.  Mungu naye  alimtayarishia mwanadamu mahali pa kuishi ndipo akamwumba.

(ii) KatikaMwanzo 1:26 Biblia inasema kwamba, “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu.”  Kwa ufupi ni kwamba Mungu katika utatu walijadiliana kabla wamfanye mwanadamu.  Wakati wa kuumba vitu vingine Biblia haisemi kwamba kulikuwa na majadiliano ya aina hii.

 

(iii) Mwanadamu aliumbwa katika mfano wa Mungu.  Hili ni jambo muhimu sana na katika funzo hili tutaliangazia zaidi.

 

(iv) Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, “Akampulizia puani pumzi ya uhai” (Mwanzo 2:7).  Mungu hakufanya jambo hili kwa kiumbe chochote kile, ni mwanadamu peke yake ambaye Mungu alipulizia uhai.

 

(v) Mwanadamu iliumbwa awe ili kiongozi juu ya kila kitu hapa ulimwenguni (Mwanzo 1:26).

 

Huu ni ushahidi ambao unaonyesha kwamba mwanadamu ni kiumbe muhimu sana.  Mara mingi, wakati Biblia inatumia neno “Mwandamu” humaanisha mwanamume na mwanamke (mstari wa 27).

 

Biblia inatufundisha  kwamba mwanadamu ni kiumbe muhimu sana.  Lakini baada ya kuanguka dhambini, akili yake yote iliharibiwa na anawaza kwamba kuna wanadamu fulani muhimu kuliko wengine.  Tunaheshimu watu kulingana na mali yao, masomo yao, vyeo vyao, mavazi ambayo wanavaa na makao ambayo wanaishi.  Mtu akivaa vizuri na awe anaendesha gari zuri sana, basi mara moja tunaanza kumheshimu.  Lakini tunapokutana mfanyakazi wa nyumba na awe anatoka katika jamii ambayo ni maskini na awe pia hana masomo, mara moja tunaanza kumdharau.  Hatuwezi kuwaza kwamba machoni pa Mungu huyu mfanyakazi wa nyumba na yule tajiri wote ni sawa machoni pa Mungu kwa sababu wote wameumbwa kwa mfano wa Mungu.  Hatuwazi kwamba askari wa mlango na  mfanyakazi wa nyumba wanafaa kuheshimiwa kama watu wengine kwa sababu ni Mungu ambaye amewaumba wote.

 

Haya ni madhara ya dhambi ndani mwetu.  Tunafaa kila wakati kujikumbusha kwamba sisi sote tumeumbwa na Mungu na ni viumbe muhimu sana.  Machoni pa Mungu hakuna mtu bora zaidi kuliko mwingine.  Kutoheshimu mtu ni jambo ambalo linamchukiza Mungu sana kwa sababu tunamdharau mtu ambaye aliumbwa kwa mfano wa Mungu.

 

Jambo hili kwamba wanadamu ni muhimu kwa sababu waliumbwa na Munga linajumlisha pia watoto ambao bado wako tumboni.  Biblia inasema kwamba mtoto huyu ni kiumbe ambacho kiko na uhai.  Si kweli kwamba maisha inaanaza wakati mtoto anazaliwa, bali inaanza tumboni.  Kuua mtoto ambaye hajazaliwa ni kuua mwanadamu ambaye ameumbwa na Mungu kwa mfano wake mwenyewe; na hii ni dhambi ya uuaji.

 

Jambo hili pia linajumlisha wanawake.  Mwanaume anaweza kuwaza kwamba mkewe siyo kitu cha maana kwani yeye akiwa mwanaume na kichwa cha nyumba yake, yeye ni wa muhimu sana.  Lakini Biblia inasema kwamba, “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe” (1 Petro 3:7).  Ni lazima tuwe waangalifu sana hapa kwa kile ambacho Biblia inasema.  Biblia inawaamuru waume wawe na hekima kwa wake wao na kuwapa heshima.  Sababu ni kwamba mume na mkewe ni warithi wa neema na uzima.  Hapa Biblia inamaanisha kwamba mke ni mtu muhimu sana kama vile tu mume alivyo muhimu machoni pa Mungu.  Mtu akiwa anawaachia wanawe wawili urithi, hii inamaanisha kwamba wanawe wote ni sawa ndiyo maana wanarithi mali yake wote wawili.  Mume na mkewe wote wawili ni warithi wa neema na uhai; kumaanisha kwamba machoni pa Mungu wote wako sawa.  Mume asipo mheshimu mkewe, anamchukiza Mungu na maombi yake hayatasikika.

 

2.  Kwa sababu Mungu ndiye aliyetuumba, tuko na jukumu mbele ya Mungu jinsi tunavyoishi maisha yetu hapa ulimwenguni.   Wakati wazazi wanamzaa mtoto, mtoto huyu ako na jukumu la kuwaeleza jinsi anavyoishi maisha yake hapa ulimwenguni.  Hawezi kufanya kile ambacho anataka, lazima afanye kile ambacho kinawapendeza wazazi wake.  Kwa hivyo mtoto hawezi kuwaambia wazazi kwamba hataki kuenda shuleni.  Ikiwa wazazi wa mtoto huyu watamwambia kwamba anafaa kuenda shuleni fulani, anafaa kutii.  Mtoto asipoenda shuleni wazazi wake wako na ruhusa ya kumwaadhibu kwa sababu amekataa kuwatii.  Kwa njia hiyo hiyo tumeumbwa na Mungu na tuko na jukumu la kufanya jinsi anavyotaka tufanye hapa ulimwenguni.  Hatuwezi kumwambia kwamba, “Hatutaki sheria zako na tumeamua kutozifuata.”  Mungu ametuumba na kwa hivyo ni jukumu letu kuishi jinsi anavyotaka hapa ulimwenguni.  Baada ya kufa, tutasimama mbele yake na kuhukumiwa kulingana na jinsi tumeishi maisha yetu hapa.  Wakati Bwana Yesu atakaporudi hapa ulimwenguni, tutasimama mbele yake na yale yote tumefanya wakati huu yatafunuliwa (Ufunuo 20:11-15).

 

II. Mungu alimwumba mwanadamu kwa mfano wake.

 

Biblia inasema kwamba, “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba” (Mwanzo 1:27).  Hii inamaanisha kwamba mwanadamu kwa njia fulani ako kama Mungu.  Jambo hili halimaanishi kwamba mwanadamu ni Mungu au mwanadamu ni kama Mungu kwa kila njia, bali linamaanisha kwamba kwa njia fulani tuko kama Mungu.

 

1.  Kwanza, inamaanisha kwamba sisi tuko na akili na uwezo wa kufanya mambo fulani.  Tunajua kutokana na Biblia kwamba Mungu ni mwenye uwezo wote na maarifa yote.  Ameumba ulimwengu wote kwa njia ambayo inapendeza sana.  Kwa njia hiyo hiyo wanadamu ni watu ambao wako na akili na uwezo wa kufanya mambo fulani.  Kama Mungu, tuko na uwezo wa kuwaza mambo na kuyafanya.

 

2.  Pili, inamaanisha kwamba sisi ni watu ambao tuko na ushirikiano.  Mungu anaishi milele kwa Utatu akiwa Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu na katika Utatu wanashirikiana kama Mungu Mmoja.  Kwa njia hiyo hiyo tumeumbwa kuishi katika ushirika na wengine siyo tuishi peke yetu.  Hii ndiyo sababu jamii inafaa kuhakikisha kwamba wanaishi pamoja.  Siyo jambo jema mume kuishi peke yake mjini na mkewe ako mashambani na watoto.  Pia siyo jambo jema mume kumaliza wakati wake mwingi na marafiki wake na kurudi nyumbani usiku.  Kwa njia hiyo hiyo mtu ambaye ameokoka anafaa kuwa mshirika wa kanisa na ajitolee kutumia vipawa vyake katika kanisa hilo.  Siyo jambo jema kwa mkristo kuhudhuria kanisa hili leo na lingine kesho.  Tumeumbwa na Mungu tuishi kama jamii moja ambayo imejitolea kutumikiana.

 

3.  Tatu, inamaanisha kwamba tumeumbwa tukiwa viumbe vya kiroho.  Tunasoma katika Mwanzo 2:7 kwamba Mungu alipulizia mwanadamu puani uhai ili mwanadamu awe na uhai.  Mstari huu unatueleza kwamba mwanadamu aliumbwa akiwa na mwili pamoja na nafsi.  Tazama jinsi Biblia inavyofafanua kuumbwa kwa mwanadamu; “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai” (Mwanzo 2:7).  Mungu alianza na kuumba mwili wa mwanadamu kutoka kwa mavumbi ndipo akampa mwanadamu nafsi.  Kumbuka kwamba ni mwanadamu peke yake ambaye alipewa nafsi na Mungu.  Kila mnyama ako na mwili lakini ni mwanadamu peke yake ambaye Mungu alimpa nafsi.  Hii inamaanisha kwamba ni mwanadamu peke yake ambaye anaweza kuwa katika ushirika na Mungu.  Wakati mwanadamu alipopewa nafsi, mara moja alianza kuwa na ushirika na Mungu.  Hii ndiyo sababu Biblia inasema kwamba “Mtu akawa nafsi hai” (Mwano 2:7).  Wakati Mungu alimwumba mwanadamu kutoka kwa mavumbi, moyo wake ulianza kufanya kazi na damu yake ilikuwa ikitembea mwilini mwake.  Lakini mwanadamu hakuwa na maisha ya kiroho, alikuwa kama mnyama.  Lakini Mungu alimpa nafsi na mara moja akawa hai kiroho na mara moja akaanza ushirika na Mungu.

 

Kuelewa jambo hili ni muhimu sana kwetu leo.  Mwanadamu hatawahi kuwa na furaha hadi atakapokuwa na ushirika mwema na Mungu.  Hivi ndivyo tumeumbwa.  Wakati Adamu na Hawa walipoanguka dhambini, ushirika wao na Mungu ulikatwa mara moja na mwanadamu amekuwa akitafuta jinsi anaweza kujitosheleza hapa ulimwenguni.  Watu wengi huwaza kwamba wanaweza kupata furaha katika mali ya ulimwengu huu na kwa sababu hii wanaishi wakitafuta mali ya ulimwengu.  Lakini ukweli ni kwamba hatutawahi kutosheka hadi tutakaporudi katika ushirika mwema na Mungu.  Hii ndiyo sababu kuokoka ni kupata uhai (Yohana 10:10).

 

4.  Nne, inamaanisha kwamba tumeumbwa tukiwa viumbe vyenye kufahamu mabaya na mazuri.  Hii inamaanisha kwamba tunauwezo wa kuelewa mabaya na mazuri.  Tunajua kwamba mambo fulani ni mabaya na mengine ni mazuri.  Mwanadamu ndiyo kiumbe cha peke ambacho Mungu amepea ufahamu wa mambo mzuri na mabaya.  Simba anapomuua mwanadamu hatajihisi kwamba ako na hatia kwa yale ambayo amefanya.  Lakini mwandamu anapomuua mwingine mara moja atajua kwamba amefanya jambo baya sana hata kama machoni pa watu hatalikubali.  Hata kama hakuna mtu atakayewahi kujua kuhusu dhambi yake, ndani moyoni mwake anajua kwamba amefanya jambo baya la kumuua mwingine.  Tumezaliwa na akili ya kujua baya na zuri kwa sababu tumeumbwa katika mfano wa Mungu mwenyewe.

 

 

Funzo la Pili: Tafadhali soma kitabu cha Mwanzo 2:15-25.

 

Katika kifungu hiki tunasoma kwamba, wakati Mungu alipomwumba mwanadamu, alimpatia maagizo fulani ambayo yalikuwa yamwongoze katika maisha yake.

 

Tunaambiwa katika mstari wa 15 kwamba Mungu alimweka Adamu katika bustani la Edeni na akampatia maagizo fulani kuhusu jinsi alifaa kuishi katika ulimwengu huu.  Kuna maagizo manne muhimu ambayo alipewa.

 

1.  Adamu alitakikana afanye kazi.  Tunaambiwa kwamba, “Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza” (mstari wa 15).  Huu ndiyo ulikuwa mpango wa Mungu kwa Adamu na mpango huu haujabadilika.  Hatufai kuwa wavivu hapa duniani, bali tunafaa kufanya kazi kwa bidii.  Kazi haikutokana na dhambi na kazi siyo kitu kibaya au kiovu.  Hili ni jambo ambalo Mungu alimwamuru mwanadamu afanye kabla ya dhambi kuja duniani.  Hii ndiyo sababu Biblia inasisitiza kwamba tunafaa tufanye kazi.  Kukataa kufanya kazi ili tuwategemee wengine ni dhambi machoni pa Mungu.  Fikiria juu ya maneno haya ya Biblia:

 

“Ndugu, twawaangazia katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu.  Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu yeyote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu kwa kwenu awaye yote.  Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielezo kwenu, mtufuate.  Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwa kwenu tuliwaangazia neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula” (2 Wathesalonike 3:6-10).

 

“Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini” (1 Timotheo 5:8).

 

Mistari hii kutoka Agano jipya inatufafanulia wazi kwamba tukikataa kufanya kazi tunatenda dhambi.  Pia inasema wazi kwamba tusipowajali watu wa jamii zetu, na tuendelee kuwategemea wengine kwa kuwaombaomba, basi tunakana imani yetu ya kikristo na kuwa wa wabaya kuliko wale wasioamini.  Labda utasema kwamba, “Ninafanya kila niwezalo lakini sijapata kazi au kazi ambayo niko nayo mshara wake haunitoshelezi pamoja na jamii yangu.  Basi nitafanya nini?”  Kuna mambo matatu unafaa kufanya.

 

(i) Unafaa kuomba Mungu akubariki na kazi.  Ikiwa Mungu mwenyewe ametuambia tufanye kazi basi Yeye mwenyewe atatupa kazi ya kufanya.  Ikiwa tuko tayari kufanya kazi, basi Mungu atatupa kazi hiyo.

 

(ii) Wewe ambaye unatafuta kazi hufai kuanza kuchagua kazi.  Kuna watu ambao wamepewa kazi na Mungu lakini wako na majivuno sana na wanakataa kufanya kazi hiyo.  Kuna watu pia ambao hawana bidii kazini, wanapenda tu kuishi maisha bila ugumu wowote.  Watu hawa wanafaa kukumbuka kwamba wanafaa kufanya kazi na kukosa kufanya kazi ni dhambi.

 

(iii) Mtu hafai kuwa na hali ya maisha ambayo hawezi.  Ni hali ya maisha kwamba sisi sote hatuko sawa; wengine hawana uwezo sana na wengine wako na uwezo kuliko wengine.  Ikiwa mtu anafanya kazi ya ufundi au yeye ni mfanyakazi wa nyumba, anafaa kuelewa kwamba hivyo ndivyo maisha yalivyo: kuna wale ambao kwa neema ya Mungu ni matajiri na pia wengine wengi kwa neema na mapenzi ya Mungu hawajiwezi sana au ni maskini.  Wote wanafaa kujua kwamba kwa hali hizi zote bado Mungu anawapenda kama viumbe vyake.  Kwa hivyo mtu wa aina hii anafaa kuwa na hekima sana kuhusu ni wapi anaishi, watoto wangapi atakuwa nao, na ni wapi atapeleka watoto wake kusoma.  Biblia inatuambia kwamba tunafaa kutosheka na kile ambacho tuko nacho (Waebrania 13:5).

 

2.  Adamu alifaa kufanya kazi siku sita na siku ya saba alifaa kupumzika.  Tunaambiwa katika mstari wa 3 kwamba, “Mungu akaibariki siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoumba na kuifanya.”  Baadaye katika Agano la Kale, Mungu alisema kwamba mwanadamu anafaa kupumzika kutoka kwa kazi yake siku moja kwa kila juma kwa sababu hivi ndivyo Mungu alivyofanya wakati alipoumba mbingu na dunia.  Alibariki siku ya saba na kuitakasa.  Siku ya Bwana (ambayo katika Agano Jipya ni Jumapili) ni siku ya kupumzika na kumwabudu Mungu.  Si siku ambayo tunafaa kutumia kwa kazi zetu.

 

Jambo hili kuhusu siku ya Bwana ni jambo ambalo wakristo wengi hawalifahamu vyema.  Kuna kuchanganyikiwa kwingi kuhusu siku hii.  Tutatazama jambo hili kwa kujiuliza maswali haya.

 

(i) Je, siku ya Bwana ni muhimu leo?  Je, Bwana Yesu hakuondoa siku hii?  Haya ni mawazo ambayo ni ya kawaida leo.  Tunajua kwamba kuna mambo fulani fulani katika Sheria ya Musa ambayo Yesu aliondoa wakati alipoleta Agano Jipya.  Kwa mfano, zile sadaka zote ambazo zilikuwa zikitolewa kwa ajili ya dhambi za watu ziliondolewa kwa sababu Yeye ndiye Mwanakondoo wa Mungu aliyejitoa kwa ajili ya dhambi za watu wake (Waebrania 9:26-28).  Tunajua pia kwamba Bwana Yesu aliondoa sheria kuhusu chakula ambazo zilikuwa zinapatikana katika Sheria ya Musa (Marko 7:1-19).  Mambo haya yote yanafunzwa wazi katika Agano Jipya.  Lakini Agano Jipya halifunzi mahali popote kwamba Siku ya Bwana iliondolewa.  Bali inatuonyesha wazi kwamba wakristo katika Agano Jipya waliendelea na kuifuata.

 

(ii) Je, kifungu katika kitabu cha Marko 2:23-27 Hakionyeshi kwamba Yesu aliondoa siku hii?  Hiki ni kifungu ambacho kimewachanganyisha watu wengi kwa kuwa wengi wanawaza kwamba Yesu aliondoa siku hii.  Lakini unaposoma kifungu hiki kwa makini utaona kwamba Yesu hakuondoa siku hii.  Yesu anamalizia katika kifungu hiki kwa kusema, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya Sabato” (Marko 2:27).  Kwa hivyo ikiwa Yesu aliondoa siku hii hangesema maneno haya.  Angesema maneno kama haya, “Sabato ilikuwa siku ya Agano la Kale.”  Lakini hakusema jambo hili, alisema kwamba Sabato ilikuwa siku ambayo Mungu mwenyewe alitengeneza kwa ajili ya mwanadamu.  Kwa hivyo kama hili ndilo kusudi la Mungu, kwa nini Kristo aiondoe?.

 

(iii) Je, Sabato ni ya Jumamosi au Jumapili?  Hili ni swali ambalo linawasumbua watu wengi.  Kuna watu leo ambao wanasisitiza kwamba Sabato ni ya Jumamosi na kama hatutazingatia siku hii ya Jumamosi, basi tunatenda dhambi.  Katika Agano la Kale Sabato ilikuwa siku ya Jumamosi, hadi siku ya leo wale ambao ni Wayahudi wanaendelea kushikilia siku hii ya Jumamosi.  Ni wazi katika Agano Jipya kwamba Wakristo walikuja pamoja kuabudu si siku ya mwisho ya juma bali ile ya kwanza na wakaita Siku ya Bwana (Matendo ya Mitume 20:9; 1 Wakorintho 16:2).  Kwa hivyo tangu wakati huo hadi sasa, wakristo wameendelea kufuata mfano wa kanisa la kwanza kukutana siku ya kwanza ya juma; yaani Jumapili.

 

(iv) Je, ni nini wakristo wanafaa kufanya siku ya Sabato?  Katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:12-15 tunapewa maagizo kuhusu siku ya Sabato.  Kuna mambo mawili muhimu ambayo tunafaa kufanya siku ya Sabato.  Kwanza kabisa tunafaa kupumzika kutoka kwa kazi zetu za kila siku (Kumbukumbu la Torati 5:13-14).  Tunafaa kuhakikisha kwamba sisi wenyewe na wafanyakazi wetu na wanyama ambao wanatufanyia kazi wanapumzika siku hii.  Pili tunafaa kukumbuka kwamba Mungu ametuokoa kutoka kwa dhambi na akatuleta katika ufalme wake, kama vile Waisraeli walivyostahili kukumbuka siku hii wakati walipokombolewa kutoka kwa utumwa nchini Misri (Kumbukumbu la Torati 5:15).  Hii ndiyo sababu tunakutana pamoja kila Jumapili na kumwabudu Mungu. Ni njia ya kukumbuka wokovu wetu kwa kumsifu Mungu.

 

3.  Adamu alikuwa achunge viumbe vya Mungu.  Tunasoma katika mstari wa 15, Adamu aliamrishwa afanye kazi katika bustani la Edeni “Ailime na kuitunza.”  Mungu alimpatia mamlaka juu ya viumbe vyake vyote.  Amri hii bado iko nasi siku ya leo.  Ulimwengu ambao tunaishi ni wa Mungu na ni lazima tuutunze.  Hatuwezi kuharibu mazingira kwa minajili ya kujifaidisha.  Tunafaa kuhakikisha kwamba hatuharibu mazingira yetu; kwa mfano kwa wale ambao wanafanya kazi ya kukata miti kwa sababu ya kuuza makaa, wanafaa kila wakati wanapokata mti wapande mti mingine; kwa sababu mazingira haya ni kwa manufaa yetu.  Kama tutakata miti yote bila kupanda mingine, basi tutajikuta katika jangwa na jambo hili litafanya tusiweze kupanda hata chakula.

 

4.  Adamu alikuwa aoe.  Katika mstari wa 18, tunasoma kwamba Mungu alisema, “Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye,” na Mungu alimletea Adamu mke.  Wakati Bwana Yesu aliulizwa swali kuhusu ndoa na taraka, hiki ndicho kifungu alinukuu katika mafundisho yake (Mathayo 19:4-6).  Kwa ufupi Bwana Yesu anatuambia kwamba mfano mwema wa ndoa ni ule wa Adamu na Hawa.  Kama tunataka kuelewa kuhusu ndoa njema mfano mwema ni huu, lazima tutazame Adamu na Hawa bali siyo watu wengine katika Biblia.  Hili silo jambo la kushangaza hata kidogo.  Ndoa ya Adamu na Hawa ilitendeka wakati walikuwa hawajaanguka dhambini.  Kwa hivyo lazima iwe ndoa ambayo ilikuwa imekamilika, kwa sababu ilitendeka wakati walikuwa hawajaanguka dhambini.  Tunapotazama ndoa ya Adamu na Hawa, tunapata mafunzo muhimu sana kuhusu ndoa.

 

(i) Hatuoni kusisitizwa kwa sherehe wakati watu wanaingia katika ndoa.  Tunaambiwa kwamba Mungu alimwumba Hawa akiwa mke wa Adamu na akamleta kwa Adamu na wakaoana.  Machoni pa Mungu maisha ya watu wawili ambao wameoana ni muhimu sana kuliko sherehe.  Sherehe ni ya siku moja tu, na maisha ya watu wawili ambao wameoana ni ya muda mrefu hadi mmoja wao atakapokufa.  Ni jambo la kushangaza kwamba siku ya leo tunasisitiza mambo ambayo haina umuhimu kabisa.  Watu wawili ambao wanataka kuoana wanamaliza wakati mwingi na pesa mingi wakipanga mambo ya arusi yao; lakini hawafikirii sana kuhusu maisha ambayo wataishi wakati watakapooana na jinsi watakumbana na majaribu katika ndoa yao.

 

(ii) Kusudi kubwa la ndoa ni urafiki.  Adamu alikuwa peke yake, na Mungu akaona kwamba hafai kuwa hivi kwa hivyo akamletea rafiki.  Tena katika haya tunaona jinsi tumepotea sana siku hizi.  Siyo jambo la kushangaza kwamba leo katika ndoa tunapata hakuna urafiki kati ya mke na mume.  Mara mingi tunaona kwamba mume ataenda katika mji kufanya kazi na mke wake atabaki nyumbani akichunga ng'ombe na watoto,  na kufanya kazi katika shamba.  Au kama watu hawa wawili wanaishi katika nyumba moja utapata kwamba mume hamwoni mke kama rafiki wa karibu.  Badala yake utapata kwamba mume ako na marafiki ambao anakutana nao  baada ya kazi na kuketi nao kwa muda mrefu sana.    Anaporudi nyumbani anaitisha tu chakula lakini hana wakati wa kuongea na mke wake.  Pia mke anaweza kumwacha mumewe na aende kukaa na wanawake wenzake kwa muda mrefu.

Hivi sivyo Mungu alivyotaka tuishi kwa ndoa, na ndoa ya aina hii haiwezi kuwa na baraka za Mungu.  Mungu anahitaji mke kuwa rafiki wa mume wa dhati.

 

(iii) Ndoa ni kati ya mume na mke.  Katika mataifa mengi ulimwenguni kuna watu ambao wamefanya ndoa kati mume na mume na mke na mke.  Wengine wanachukua wanyama  na kuwafanya wake au waume wao.  Watu hawa wanafanya jambo ambalo halitakikani machoni pa Mungu na ni dhambi kubwa sana (Mambo ya Walawi 18:22-24) na Mungu atahukumu watu hawa.

 

(iv) Ndoa ni kati ya mume mmoja na mke mmoja.  Ni baada ya dhambi ndipo watu walianza kuwa na wake zaidi ya mmoja.  Siyo mapenzi ya Mungu kwamba mume awe na zaidi ya mke mmoja.  Mungu alimpa Adamu mke mmoja kwa sababu hayo ndiyo mapenzi yake.  Leo mtu anapooa wake wengi anaanza kutoa vijisababu vingi kama, Daudi na Suleimani walikuwa na wake wengi na kwa hivyo inakubalika hata yeye awe na wake wengi.  Ni ukweli kwamba Daudi na Suleimani walikuwa na wake wengi, lakini siyo ndoa zao ambazo Mungu ameweka kama mfano kwetu, bali ni ndoa ya Adamu na Hawa ambayo Kristo anasema kwamba hiyo ndiyo mfano wa ndoa ambayo anafurahia.

 

(v) Ndoa ni jambo la maisha.  Mungu anasema kwamba wawili watakuwa mwili mmoja.  Hii inamaanisha kwamba ndoa siyo jambo la kujaribu kati ya mwanamke na mwanaume, kama jinsi wengi wanavyofanya hapa nchini kwa kusema “kuja tuishi.”  Katika uhusiano kama huu hakuna kujitolea kwa sababu hakuna mtu amehapa kwa mwingine.  Ikiwa kwamba baada ya miaka fulani mmoja ataamua kutoka katika uhusiano huo, basi atafanya hivyo bila kutatizwa.  Lakini kulingana na Biblia ndoa haikai hivi.  Ndoa ni jambo la maisha na kila mmoja anajitolea ili waweze kuishi pamoja.  Uhusiano huu unaisha wakati mmoja anakufa.

 

(vi) Ndoa ni kati ya watu wawili pekee.  Mume anaamrishwa kuacha babake na mamake na ajiunge na mkewe.  Hii inamaanisha kwamba wazazi wa watu hawa wawili hawafai kuingilia ndoa hii.  Katika jamii fulani, wanasema kwamba mke ni wa jamii nzima.  Na katika jamii zingine ni kawaida mama mkwe kuingilia nyumba ya watoto wake.  Kufanya jambo hili ni kuenda kinyume na Biblia.  Wawili ambao wako katika ndoa ni lazima wawaheshimu wazazi wao na pia wanaweza kupata ushauri kutoka kwao, lakini wazazi hawana ruhusa ya kuingilia ndoa ya watoto wao.

 

(vii) Adamu hakulipa chochote ndipo aoe Hawa.  Mungu aliona kwamba Adamu alikuwa peke yake na alihitaji mke; ndipo akamuletea Hawa awe mke wake.  Mungu hakutarajia malipo yoyote kutoka kwa Adamu.  Kuna wazazi wengi leo ambao wanatarajia kulipwa ndipo mabinti zao waweze kuoleka.  Wazazi hawa wanafaa kujua kwamba jambo hili halikubaliki machoni pa Mungu; kwa sababu linamzuia kijana kuoa wakati ufaao kwa sababu hana mali ambayo inaitishwa.  Huyu kijana katika miaka yake ya ujana, ako na hisia mingi za kufanya mapenzi na Biblia inasema kwamba mtu akiwa na hisia za aina hii, lazima aoe.  Asipooa huenda anguke katika dhambi (1 Wakorintho 7:9).  Mtu anapoitisha malipo ya binti yake, anazuia kile ambacho Mungu aliamrisha kifanywe.

 

(viii) Kuna mamlaka katika ndoa ambayo Mungu alipanga.  Mungu alimwumba mume kwanza na baadaye akamwumba mwanamke akiwa msaidizi wa mume.  Hii haimaanishi kwamba mke ni mdogo kwa mume na kwa hivyo anafaa kudharauliwa au kufanywa jinsi  mwanaume anavyotaka.  Lakini jambo hili linamaanisha kwamba mume ndiyo kichwa cha nyumba na mke anafaa kumtii mume wake.  Biblia inasema, “Lakini ninataka mjue kwamba kichwa cha kila mwanadamu ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume   lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume maana mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanamume” (1 Wakorintho 11:3,7-8).  Hii ndiyo sababu wake wameamrishwa na Mungu kutii waume wao (Waefeso 5:22).  Tunaondoka kwa haya wakati mume anaanza kutumia mamlaka yake vibaya kwa njia ambayo anafanya mambo kama yeye ni muhimu sana kuliko mkewe machoni pa Mungu, na pia wakati mke anakataa kutii mumewe.  Mambo haya ni kinyume na mapenzi ya Mungu.  Mume hafai kumdharau mkewe na pia mke hafai kukataa kumtii mumewe.

 

Hizi ndizo amri ambazo mwanadamu alipewa zimwongoze hapa ulimwenguni.  Anafaa kufanya kazi, kuizingatia siku ya Sabato, anafaa kulinda mazingira ambayo anaishi ndani na anafaa kuoa, lakini kuna wakati mwingine ambapo anawapa watu fulani kipawa ya kukaa bila kuoa.  Hawa ni watu ambao wanakaa bila kuoa “kwa ajili ya ufalme wa mbinguni (Mathayo 19:12).

 

 

 

Funzo la Tatu: Tafadhali soma Mwanzo 3:1-6

 

Katika kifungu hiki tunasoma jinsi Adamu na Hawa walivyoanguka dhambini.  Haya ni mafunzo muhimu sana.

 

I.  Jinsi Hawa alianguka dhambini.

 

1.  Kwanza, tunajifunza kwamba Hawa alianguka katika dhambi kwa sababu alisikiliza uongo wa shetani.  Mwanzoni mwa sura tunaambiwa kuhusu nyoka ambaye “Alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu.”  Ni wazi kwamba ni shetani ambaye alikuwa akimtumia nyoka huyu.  Siyo nyoka aliyemjaribu Hawa, bali ni shetani.  Ni Shetani aliyeongea na Hawa akimwuliza maswali.  Mara mingi wakati mtu hamtujui anapokuja na kuanza kuongea nasi, si rahisi kuendelea tu katika mazungumzo.  Lakini anapoanza kuuliza maswali, mara mingi tunajipata tukiendelea katika mazungumzo naye.  Kwa hivyo shetani alikuwa mwerevu, kwani alitumia maswali kumwongelesha Hawa.  Mwishowe alimwambia Hawa uongo wa wazi: “Hakika hamtakufa” (mstari wa 4).  Tunaanguka dhambini wakati tunapomsikiliza shetani.

 

2.  Pili tunajifunza kwamba Hawa alianguka katika dhambi kwa sababu hakuelewa vyema neno la Mungu.  Wakati nyoka alipomwuliza swali alimjibu, “Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa” (mstari wa 2-3).  Tukitazama amri yenyewe ambayo Mungu alipeana katika Mwanzo 2:17, tunaona kwamba Mungu hakusema kwamba hawafai kuugusa mti ule.  Alisema kwamba hawafai kula tunda kutoka kwa mti ule.  Hawa hakuelewa vyema neno la Mungu.  Kwa njia hiyo hiyo leo kuna wakristo ambao hawaelewi vyema neno la Mungu.  Mara mingi utamsikia mkristo akisema jambo kama hili, “Je, katika Biblia si kuna mahali inasema hivi?”  Mkristo huyu haelewi kabisa ni nini Biblia inasema; bali ni fahamu kidogo ambayo ako nayo.  Jambo hili haliwezi kutusaidia katika vita vyetu dhidi ya dhambi.  Wakati Bwana Yesu alijaribiwa katika jangwa alinukuu maandiko vyema na jambo hili ndilo lilimwezesha kumshinda shetani.

 

3.  Tatu, tunajifunza kwamba Hawa alianguka dhambini kwa sababu alikosa kumwamini Mungu, kwa kudhani kwamba kuna baraka ambazo Mungu alikuwa amezuia.  Shetani alimwambia kwamba, “Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu , mkijua mema na mabaya” (Mstari wa 5).  Kwa ufupi shetani anamwambia kwamba, Mungu hataki ajue lolote bali aendelee katika hali ya kutofahamu.  “Kuna cheo cha juu ambacho unaweza kuwa nacho, lakini Mungu anakusudi usipate cheo hicho.  Ukila tunda hili utaweza kupata baraka ambazo Mungu anakufungia usipate.”  Hivi ndivyo wengi wetu wanvyoanguka katika dhambi.  Shetani hutudanganya kwamba kuna baraka nyingi za mali ambazo zinatungojea lakini Mungu ndiye anayetuzuia kupata baraka hizi.  Hii ndiyo sababu watu wengi wako tayari kuwadanganya wengine; watu hawa wanahakika kwamba kuna furaha nyingi katika vitu vya ulimwengu huu, lakini Mungu kupitia kwa sheria yake ambayo ametupatia, hataki tupate baraka hizi.

 

4.  Nne, tunajifunza kwamba Hawa alianguka dhambini kwa sababu ya tamaa za mwili. Tunasoma katika mstari wa 6 kwamba, “Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala.”  Kuna mambo matatu ambayo yalimfanya Hawa kutamani lile tunda: tunda lilipendeza macho yake, tunda lilifaa kuwa chakula na lilikuwa la kutamanika kwa maarifa.  Mambo haya yote yalikuwa yanahusu tu mwili na maisha ya hapa ulimwenguni bali siyo mambo ya kiroho na uhusiano wake na Mungu.  Hii ndiyo njia ya kawaida jinsi shetani anavyotuongoza katika dhambi.  Anatuonyesha furaha na anasa za ulimwengu huu ambazo tutapata kutoka kwa mambo fulani, lakini huwa hatuonyeshi madhara ya mambo haya juu ya maisha yetu ya kiroho.

 

5.  Tano, tunajifunza kwamba kabla ya Hawa kuanguka katika dhambi alipitia katika hali fulani fulani.  Biblia inasema kwamba, “Mwanamke alipoona ya kuwa mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake na akala” (mstari wa 6).  Unapotazama mstari huu utaona kwamba kuna kuendelea katika hali moja hadi nyingine.  Kuanguka katika dhambi huanza kwa njia ndogo sana halafu inakuwa kitu kikubwa.

 

(i) Kitu cha kwanza ambacho kilitendeka ni kwamba Hawa aliona kwamba mti ulikuwa mzuri kwa chakula na wa kutamanika kwa macho.  Sisitizo hapa ni kwa macho: aliona kwamba mti ulikuwa mzuri na wa kutamanika kwa macho.  Mara mingi dhambi huanza kwa kutazama.  Mtu anaenda kwa nyumba ya rafiki wake na kuona simu ambayo rafiki wake amenunua.  Anaichukua na kuitazama kwa makini sana.  Bila yeye kujua, moyoni mwake  anamepata miba ya dhamUsraeli.  Baadaye wakati Akani alikiri dhambi yake, alisema, “Nilipoona katika nyara joho nzuri ya Babeli, na shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu, uzani wake shekeli hamsini, basi nalivitamani nikavitwaa” (Yoshua 7:21).  Kwa njia hiyo hiyo wakati mfalme Daudi alipoanguka dhambini na Bathsheba, alianza wakati, “aliona mwanamke anaoga” (2 Samweli 11:2).  Watu hawa wawili walianguka dhambini kwa sababu hawakuchunga macho yao.  Yesu alisema, “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru.  Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza.  Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!” (Mathayo 6:22-23).  Kile Yesu anamaanisha ni kwamba macho ni kama mwangaza ambao mwanadamu anatumia katika giza.  Akitumia mwangaza huo kutazama mambo mabaya, basi moyo wake utajawa na dhambi.  Lakini akitumia mwangaza huo kutazama mambo mazuri basi moyo wake utajawa na mambo mazuri.  Tunaweza tu kutazama mambo mabaya au mazuri na macho yetu.

 

(ii) Jambo lingine ambalo lilimtendekea Hawa ni kwamba alitamani tunda: “Nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa.”  Hii ndiyo hatua ambayo inafuata wakati tumetazama kitu: tunakitamani.  Akani alikiri kwamba, “Nilipoona katika nyara joho nzuri ya Babeli, na shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu, uzani wake shekeli hamsini, basi nalivitamani” (Yoshua 7:21).  Kwanza aliona vitu hivi na baadaye akawa na tamaa moyoni mwake ya vitu hivi.  Jambo hili pia lilifanyika kwa Daudi wakati alipomwona Bathsheba akioga na akaanguka katika dhambi naye.  Hii ndiyo sababu tunafaa kuwa chonjo na macho yetu.  Ayubu anasema, “Nilifanya agano na macho yangu; basi nawezaje kumwangalia msichana? (Ayubu 31:1).

 

(iii) Jambo lingine ambalo lilitendeka ni kwamba Hawa alichukua tunda na akala.  Yakobo anazungumzia kile ambacho kilitendeka kwa wakati huu: “Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.  Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti” (Yakobo 1:14-15).  Hawa alidangaywa kwa sababu ya tamaa yake, tamaa ilijaa ndani mwake na akachukua lile tunda na akala.

 

Hivi ndivyo kila mmoja wetu anavyodanganywa na kuongozwa katika dhambi.  Njia hizi tatu huwa zinarudiwa mara kwa mara kila siku katika maisha yetu.

 

II.  Jinsi Adamu alianguka dhambini.

 

Ni wazi kwamba tunaposoma Biblia Adamu alikuwa na mkewe Hawa wakati alijaribiwa na shetani na kuanguka dhambani: Hawa alimpa mumewe, ambaye alikuwa naye, tunda naye akala.  Adamu alikuwa na mkewe wakati alianguka dhambini.

 

1.  Kwanza, Adamu alikosa kufanya kazi yake ya kuongoza nyumba yake.

 

(i) Kama kiongozi wa nyumba, Adamu angehakikisha kwamba mkewe anajua neno la Mungu kwa uhakika.  Kama vile tumeona, mojawapo ya sababu Hawa alianguka dhambini ni kwamba hakujua neno la Mungu kwa uhakika.  Ni jukumu la kila mume kufunza mkewe neno la Mungu na kuhakikisha kwamba analijua waziwazi.

 

(ii) Adamu angemrekebisha mkewe wakati alikosa kunukuu neno la Mungu sahihi.  Angejua mkewe alikosa kunukuu neno la Mungu sahihi wakati alimjibu shetani lakini alikosa kumrekebisha.

 

(iii) Adamu angemzuia mkewe kula tunda.  Alijua kwamba ni kinyume na mapenzi ya Mungu kwa mkewe kula tuna lile na hakumkataza kula.

 

2. Pili, Adamu alikuwa mdhaifu kwa sababu alikubali kuongozwa katika dhambi.  Tunaambiwa kwamba mkewe alimpa tunda na akala.  Hatusomi pahali popote kwamba alijaribu kukataa.  Hili ni jambo ambalo hutendeka mara mingi maishani, kwamba mwenye dhambi mmoja huongoza mwenye dhambi mwingine katika dhambi.

 

 

 

Funzo la Nne:Tafadhali soma mwanzo 3:7-19

 

Katika kifungu hiki tunaona matokeo ya dhambi ya mwanadamu.  Katika mistari 1-6 tunaelezwa vile mambo yaliendelea, na katika msitari wa 7 tunaelezwa matokeo yake, yaani kuanzia mstari huu tutaelezwa ni nini ilifanyika kwa sababu ya mambo yale yalitendeka mistari 1-6.  Punde tu mwanadamu alipoanguka dhambini mambo fulani yalitendeka.

 

1.  Kwanza wakati Adamu na Hawa walifanya dhambi walipatwa na hatia (mstari wa 7). Tukisoma msitari wa 7, “Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajua kuwa wa uchi, wakashona majani ya miti, wakajifanyia nguo.”  Punde tu walipofanya dhambi, walijua kwamba wamefanya kitu kibaya sana.  Walijihisi vibaya na wakajijua kuwa wako uchi. Hawakuendelea kuishi maisha ya starehe bila shida kama hapo mbeleni.  Hii yote huletwa na hatia.  Kuwa na hatia inamaanisha kwamba umevunja sheria ya Mungu.  Sisi sote tuko na dhamira na wakati tunavunja sheria ya Mungu, dhamira yetu huwa inatuzungumzia kwa sababu ndiyo sauti ya Mungu ndani ya moyo wa kila mwanadamu.  Dhamira huwa inatufanya tusijisikie huru wakati tunafanya dhambi.  Dhamira huwa inatueleza kwamba  kuna kitu kibaya kimefanyika na kinahitaji kurekebishwa.  Kama Adamu na Hawa, kila wakati tukifanya dhambi huwa tunajaribu kujirekebisha kwa njia zetu wenyewe.lakini tunashindwa.  Adamu na Hawa walijitengenezea nguo za majani kuficha uchi wao lakini hawakufaulu ndipo wakakimbia na kujificha nyuma ya mti.  Hii ndiyo ilikuwa tokeo la kwanza baada ya kufanya dhambi, yaani walikuwa na hatia.

 

2.  Pili, ushirika kati ya Mungu na Adamu na Hawa ulivunjika, kwa sababu walikufa kiroho (mistari ya 8-11).  Tunasoma msitari wa 8, “Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani.”  Kabla Adamu na Hawa kuanguka dhambini, walikuwa hai kiroho.  Mungu alikuwa amempulizia uhai kupitia kwa mapua yake na Adamu alikuwa kiumbe hai, yaani alikuwa na ushirika na Mungu.  Lakini wakati walikosa kutii neno la Mungu ushirika huo ulivunjika na Adamu na Hawa wakapatwa na aibu kubwa mbele ya Mungu, kwa sababu ya yale waliyafanya.  Walijificha kati ya miti ili wahepuke kukutana na Mungu.  Hii ndiyo sababu Mungu alikuwa amemwambia Adamu katika kitabu cha Mwanzo 2:17 kuhusu tunda ya mti ule: “Walakini matunda ya mti wa ujuzi na wema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”  Adamu na Hawa hawakufa kimwili punde tu walitenda dhambi lakini walikufa kiroho. Yaani ushirika wao na Mungu ulikatika mara moja.

 

3.  Tatu, Adamu na Hawa walianza kulalamikia wengine kwa sababu ya dhambi yao.(mistari 12-13).

Wakati Mungu alimwuliza Adamu kuhusu dhambi aliyoifanya, kwa haraka alisema, “Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo nikala” (mstari 12).  Na pia wakati Mungu alimwuliza Hawa kuhusu dhambi yake naye alijibu, “Nyoka alinidanganya, nikala” (mstari 13).  Hii ni mojawapo ya matokeo mabaya yaletwayo na dhambi kwa mwanadamu.  Dhambi humfanya mwanadamu akatae majukumu ya matendo yake.  Baadaye katika kijitabu hiki tutaona vile dhambi humfanya mtu asiweze kutubu hadi Mungu mwenyewe aubadilishe moyo wake.  Jambo ambalo tunaliona hapa siyo kwamba Adamu na Hawa walikataa kutubu dhambi zao, ukweli ni kwamba hawakuwa na uwezo wa kutubu dhambi zao. Hii ni kwa sababu wao wenyewe walichagua kuwa watumwa wa dhambi na kwa hivyo kwa uwezo wao hawawezi kutubu.

 

4.  Nne, dhambi ya Adamu na Hawa ilileta laana kutoka kwa Mungu (mistari 14-19).

Mungu alitamka laana nne hapa.

 

(i) Nyoka alilaaniwa kwa kutumiwa na shetani kuwadanganya Adamu na Hawa (msitari 14).  Hii ni kumbusho muhimu sana kwetu kwamba wale wanatumiwa na shetani hata ikiwa hawajui ni nini wanafanya, watahukumiwa na Mungu.  Laana ya nyoka ni kwamba atakuwa akienda kwa tumbo na atakula mavumbi.

 

(ii) Shetani mwenyewe alilaaniwa (msitari 15).  Aliambiwa kwamba kutakuwa na uadui kati yake na watu wa Mungu na kwamba mwishowe yeye atashindwa: “Naye Mungu wa amani atamseta shetani chini ya miguu yenu upesi” (Warumi 16:20).

 

(iii) Mwanamke alilaaniwa (msitari 16).  Anaambiwa kwamba kwa uchungu atakuwa anazaa.  Pia anaambiwa kwamba tamaa yake itakuwa kwa mume wake naye atamtawala.

 

(iv) Mwishowe ardhi ililaaniwa kwa ajili ya Adamu (mistari 17-18).  Ardhi haitatoa mazao kama vile mwanadamu anatarajia, bali itazaa michongoma na miiba na pia ni kwa uchungu na jasho mwanadamu atakula chakula.  Pia Adamu aliambiwa kwamba, kwa sababu ya dhambi mauti imeingia duniani na imeingia kwa kila kiumbe chote.  Sasa Adamu hataishi milele katika hali hii ya dhambi bali atakufa.

 

Haya ndiyo matokeo ya dhambi ya Adamu na Hawa.

 

 

Funzo la Tano: Tafadhali soma Mwanzo 3:20-24

 

Katika kifungu hiki tunasoma jinsi Mungu alivyofanya kuhusu dhambi za mwandamu.  Baada ya kutoa laana, Mungu alifanya mambo fulani juu ya Adamu na Hawa.  Kuna mambo mawili ambayo alifanya.

 

1.  Mungu alikuwa na huruma na neema juu ya Adamu na Hawa.  Jambo hili linaonekana kwa mambo matatu.

 

(i) Tunaambiwa katika mstari wa 20 kwamba Hawa alikuwa awe mama wa wanadamu wote.  Inaonekana kwamba Mungu alikuwa na Agano na Adamu na Hawa kwamba kizazi cha wanadamu hakingeangamia chote katika dhambi na baadaye kuhukumiwa.  Bali alikuwa na mpango ambao mamilioni wa wazao wa Hawa wangekombolewa kutoka kwa nguvu za dhambi.  Hii ndiyo sababu Adamu alimwita mama wa mataifa.

 

(ii) Mungu aliwatengenezea nguo Adamu na Hawa kwa sababu walikuwa sasa wanahatia na aibu (mstari wa 21).  Hili ni tendo la neema na huruma kutoka kwa Mungu.  Adamu na Hawa walikuwa wametenda dhambi dhidi yake kwa kumwasi na baadaye kutoka katika ushirika naye.  Baada ya kutenda dhambi walikuwa na aibu kubwa sana kwa hivyo Mungu aliwasaidia kwa kuwatengenezea nguo ya kufunika uchi wao.  Jambo hili linatuongoza kwa kazi kuu ya Mungu kupitia kwa Mwanawe ambaye alikufa msalabani kwa niaba ya watenda dhambi na kufunika dhambi zao ili hatia na aibu yao iondolewe.

 

(iii) Mungu alihakikisha kwamba hawaali tunda lile kutoka kwa mti wa uhai.  Hatuelewi kabisa kuhusu mti huu.  Katika mstari huu inaonekana kwamba kama Adamu na Hawa wangekula tunda lile, hawangekufa kifo cha mwili bali wangeishi milele katika hali ya dhambi.  Kwa hivyo Mungu katika neema na huruma wake, alihakikisha kwamba hawafanyi jambo hili kwa sababu wangeishi katika hali yakutokuwa na tumaini.

 

2.  Mungu alijitenga na Adamu na Hawa.

 

Kama jinsi tumeona, Mungu ni Mungu wa neema.  Lakini pia ni Mtakatifu na hawezi kuishi katika uwepo wa dhambi.  Kwa hivyo aliwafukuza Adamu na Hawa kutoka katika bustani ya Edeni na katika uwepo wake.  Hii ni kwa sababu Adamu na Hawa walikuwa na dhambi.  Kufukuzwa kwa Adamu na Hawa kutoka bustani ya Edeni, inatuonyesha ubaya wa dhambi.  Biblia inatufunza kwamba kwa sababu ya ile dhambi Adamu, alifanyika mwenye dhambi.  Hii haimaanishi tu kwamba Adamu alitenda tu dhambi, bali inamaanisha kwamba moyo wa Adamu ulianza kupenda dhambi sana.  Adamu alifanyika mtumwa wa dhambi na moyo wake ulitamani dhambi kila wakati.  Kuanzia wakati huo alianza kuwa mwenye dhambi kwa asili, na kwa kawaida akawa mwenye dhambi.

 

Mara mingi sisi huzungumza hivi kuhusu watu fulani: ikiwa kuna mtu kwa kijiji ambaye kila wakati huwa anafanya mambo mabaya, tunasema, “Mtu huyu ni mtu mbaya sana, yeye siyo mtu mzuri hata kidogo.”  Kama jinsi tutakavyoona baadaye, jambo la kushangaza ni kwamba maneno haya yanafaa kusemwa kwa kila mtu, bali siyo kwa watu fulani pekee.  Adamu alifanyika “mtu mbaya sana.”  Tunaweza kutazama jambo hili kwa makini tujue linamaanisha nini.

 

(i). Linamaanisha kwamba mawazo ya Adamu yaliongozwa na dhambi.  Kabla ya kuanguka katika dhambi, mawazo yake yalielekezwa kwa Mungu pekee na mambo kumhusu Mungu.  Mawazo yake yalijawa na mawazo kumhusu Mungu na mawazo haya yalimletea furaha.  Lakini baada ya kuanguka katika dhambi mawazo yake yalielekezwa katika dhambi.  Hakuwaza tena kumhusu Mungu, bali alitaka kuwaza tu juu ya dhambi na furaha ambayo matendo ya dhambi yangemletea.

 

(ii). Linamaanisha kwamba hisia zake ziliongozwa na dhambi.  Kabla ya kuanguka katika dhambi Adamu alimpenda Mungu na mambo kumhusu Mungu.  Moyo wake ulijawa na pendo kumhusu Mungu na pia alipenda ushirika na Mungu na kutaka kufanya mapenzi yake kila wakati.  Lakini baada ya kuanguka dhambini, hisia zake zote zilibadilika.  Adamu alipenda dhambi na kila wakati kupenda kufanya dhambi.  Alipenda dhambi na moyo wake wote.  Mambo ya Mungu yalikuwa majaribu kwake, kwani hakuyapenda kamwe.

 

(iii). Linamaanisha kwamba chaguo lake liliongozwa na dhambi. Mahubiri ya siku hizi tunasikia sana kwamba mtu anaweza kuchagua aokoke au la.  Mara mingi utamsikia mhubiri akisema kwamba wakati Mungu alimwumba mwanadamu, alimwumba akiwa anawezo wa kuchagua mambo fulani bila kushawishiwa na mtu yeyote au jambo lolote.  Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna katika Biblia mahali ambapo unapata jambo kama hili.  Hakuna popote katika sura ya 1 na ya 2 ya kitabu cha Mwanzo ambapo Biblia inasema kwamba Adamu aliumbwa na uwezo wa chagua bila kushawishiwa na chochote.  Kusema ukweli Adamu hakuumbwa akiwa na uwezo wa kuchagua bila kushawishiwa.  Wakati Mungu alipoumba mwanadamu alipa madaraja au vyeo, na madaraja haya yalikuwa: akili kwanza, halafu hisia, halafu chaguo na baadaye matendo.  Akili yake na moyo wake yote mawili yangeongoza chaguo lake , na chaguo lake lingemwongoza kufanya matendo fulani.  Kwa hivyo mpangilio wa mwanadamu ni akili, moyo, chaguo na matendo.  Chaguo lake halikuwa huru kufanya yale yeye mwenyewe alitaka bila kushawishiwa na akili na moyo.  Chaguo kila wakati lilikuwa liongozwe na akili na moyo na lingeweza tu kufanya yale ambayo akila na moyo yalitaka lifanye.  Hii ndiyo sababu tunasema kwamba chaguo la mwanadamu halitawahi kuwa huru.

 

Kwa njia fulani mwanadamu aliumbwa akiwa kama jeshi ambalo limepangwa vizuri.  Katika jeshi ambalo limepangwa vizuri, mkuu wa jeshi ndiye aliye na cheo cha juu zaidi na ni yeye ambaye anapokea habari jinsi mambo yalivyo katika vita na ni yeye ambaye anayesema kile ambacho kinafaa kufanywa.  Yale ambayo anasema yanajulikana na mwanajeshi ambaye anafanya kile mkuu wa jeshi amesema kupitia kwa wakubwa tofauti tofauti kulingana na ngazi za vyeo vyao.  Mwanajeshi hufunzwa kutii amri bila kuuliza swali lolote.  Haya ndiyo masomo ya juu sana kwa mwanajeshi.  Kwa hivyo njia rahisi ya adui yeyote ni kumteka nyara mkuu wa jeshi ambaye anatoa amri.  Baada ya adui kufanya hivi, basi hana haja na mwanajeshi wa kawaida; kwani mwanajeshi wa kawaida atafuata tu yale ataambiwa.

 

Hivi ndivyo shetani amefanya.  Ameteka nyara akili na moyo wa mwandamu ili chochote anacho amua ni dhambi.  Kwa hivyo chaguo la mwanadamu yote linaongozwa na dhambi kwa sababu akili yake na hisia zake yote yanaongozwa na dhambi.  Hii ndiyo sababu Yesu alisema, “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba” (Yohana 6:44).  Angazia kwa makini maneno ya Yesu hapa.  Hasemi kwamba, “Hakuna yeyote ambaye anataka kuja kwangu,” balia anasema, “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu.”  Mwanadamu hana nguvu za kujileta kwa Mungu: akili yake na moyo wake, yote yanaongozwa na dhambi na kwa hivyo chaguo lake ni kufuata dhambi, siyo Mungu.

 

(iv). Linamaanisha kwamba matendo yake yote yaliongozwa na dhambi.  Kabla ya kuanguka dhambini matendo ya Adamu yalikuwa yamekamilika machoni pa Mungu.  Baada ya kuanguka dhambini, matendo yake yalianza kuwa ya dhambi, kwani akili yake na hisia zake yote yalikuwa ni dhambi tupu.  Hii ndiyo sababu Mungu hangemkubali kula kwa mti wa uhai.  Adamu alifanyika mwenye dhambi machoni pa Mungu na akawa na moyo wa dhambi.  Mawazo yake, hisia zake, chaguo lake na matendo yake yote yalikuwa yamejawa na dhambi.  Hangeweza kula kwa mti wa uhai ili aendelea kuishi katika hali hiyo.  Mungu kwa huruma wake hangekubali Adamu aishi katika hali hiyo mbaya sana.

 

Haya ndiyo matokeo ya dhambi ya Adamu na Hawa.

 

 

 

 

Funzo la Sita: Tafadhali soma Mwanzo 4:1-16

 

Katika kifungu hiki tunasoma kuhusu matokeo ya dhambi ya Adamu na Hawa kwa wajukuu wao.  Katika somo la Nne tuliona matokeo ya dhambi Adamu aliyoifanya.  Katika sura hii tunaangazia madhara ambayo dhambi ya Adamu iliwaletea watoto wake.  Sura hii inatufundisha kwamba matokeo ya dhambi ya Adamu hayakumdhuru tu yeye pekee bali pia watoto wake.  Hii ni kwa sababu Adamu ndiye alikuwa mwakilishi wa jamii yote ya wanadamu.  Kile Adamu alifanya basi kinajumlisha wanadamu wote.  Kwa mfano raisi wa nchi anapokopa mkopo wa pesa kutoka banki ya dunia.  Wakati raisi anazungumza ili apewe mkopo huo, huwa hazungumzi kwa niaba yake mwenyewe bali kwa niaba ya nchi yote kwa sababu yeye ndiye mwakilishi.  Hata atakapoacha kuwa raisi, ni lazima nchi iendelee kuulipa mkopo huo kwa benki ya dunia.  Adamu ndiye alikuwa mwakilishi wa wanadamu duniani na mambo yote aliyoifanya, wanadamu wote walihusika hadi siku ya leo.  Katika kitabu cha Mwanzo 4 na 5 tunaona mambo mawili yenye uzito sana kwa wajukuu wa  Adamu kwa sababu ya dhambi yake.

 

1. Wajukuu wa Adamu waliridhi dhambi yake.

2. Wanadamu wote wamegawanyika katika vikundi viwili.

 

I.  Wajukuu wa Adamu wote waliridhi asili yake ya dhambi.

 

Hili ni jambo ambalo linaonekana wazi katika sura hii kwa sababu tunaona Kaini akimwua ndugu yake Habili.  Biblia inafundisha mambo matatu muhimu hapa

 

1.  Sisi sote wanadamu tumeridhi asili ya dhambi ya Adamu.  Tunapenda dhambi sana na tunafanya mambo ya dhambi kila wakati, hatupendi Mungu kamwe.  Biblia inafundisha jambo hili katika mistari ifuatayo:

 

“Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; Tangu tumboni wamepotea wakisema uongo”(Zaburi 58:3).  Hapa nchini mwetu watu wengi wanaamini kwamba watoto ni malaika wadogo ambao wanazaliwa bila dhambi hadi wakati ule watafunzwa kufanya dhambi.  Lakini Biblia haifundishi hivyo, bali inasema wazi kwamba tuko wenye dhambi tangu tumboni.

 

“Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia.  Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machumbuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwa-zongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta” (Isaya 1:5-6).

 

“Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, na una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?” (Yeremia 17:9).

 

“Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano; hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi” (Mathayo 15:19).

 

Ukweli huu unaonekana wazi kwa tabia ya Kaini.  Kaini na ndungu yake walimletea Mungu sadaka.  Mungu alipendezwa na Habili na sadaka yake, lakini hakupendezwa na Kaini na sadaka yake.  Kwa sababu hii Kaini alikasirika na kumwua Habili ndungu yake.  Kumbuka kwamba hapa dhambi ya Kaini siyo kama dhambi ya Hawa katika sura ya tatu.  Shetani alikuja mwenyewe na kumdanganya Hawa kwa maneno ya ujanja na ushawishi mbaya.  Lakini tunaona kuhusu Kaini kwamba dhambi tayari iko moyoni mwake, alizaliwa akiwa na moyo wa dhambi, ambao unapenda kufanya dhambi, na moyo ambao haupendi Mungu.  Alizaliwa akiwa katika hali ya kupenda dhambi sana na kuchukia Mungu sana.  Ilikuwa jambo la kawaida kwa Kaini kumwinukia ndungu yake na kumwua.

 

2.  Wajukuu wa Adamu wameridhi matokeo ya dhambi ya Adamu.  Katika funzo letu la mwisho tuliona punde tu Adamu alipofanya dhambi kuna matokeo mabaya yalimfanyikia, yaani: dhambi ilidhuru mafikira yake na matendo yake.  Kwa sababu tumeridhi hali ya dhambi ya Adamu, madhara yaliyoletwa na dhambi ya Adamu yametupata.  Mafikira yetu yamejawa na dhambi na tunawaza kuhusu dhambi kila wakati hadi tunapookolewa na Kristo Yesu.  Dhambi inatawala hisia zetu.  Tunapenda dhambi na tunaongozwa na hisia za dhambi kila wakati hadi siku ile Kristo Yesu anatuokoa.  Mipango yetu yote ya maisha imechafuliwa na dhambi.  Mafikira yetu na mipango yetu yote inafuata njia za dhambi badala ya njia za haki.  Kwa hivyo kama Adamu tunafanya matendo ya dhambi kila wakati.  Mtume Paulo anaeleza hali ya mwanadamu hivi:

 

Hakuna mwenye haki hata mmoja; Hakuna afahamuye, Hakuna amtafutaye Mungu.

Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.

Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila.

Sumu ya fira i chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.

Miguu yao ina mbio kumwaga damu. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao

Wala njia ya amani hawakuijua  Kumcha Mungu hakupo machoni pao” (Warumi 3:10-18).

 

Kifungu hiki kinaonyesha wazi vile dhambi ya Adamu ilitudhuru sisi wanadamu wote.  Sisi tunazaliwa na dhambi na tunapenda dhambi sana.  Kwa uwezo wetu hatuwezi kutafuta wokovu wa Kristo Yesu.  Hakuna mtu yeyote kwa uwezo wake anaweza kuja kwa Kristo Yesu amwokoe kwa sababu uwezo wetu umefungwa na dhambi kabisa.  Uwezo wa mtu unaongozwa na akili yake na roho yake, na hizi mbili, yaani akili na roho ya mwanadamu zimejawa na dhambi na zinapenda dhambi.  Akili na roho ya mwanadamu haiwezi kumwelekeza kwa wokovu kwa sababu inapenda dhambi.

 

3.  Sisi sote tuko na hatia kwa sababu ya dhambi ya Adamu.  Kitabu cha Warumi 5:12 Paulo anaandika kuhusu dhambi ya Adamu na anasema “Kwa hivyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hiyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.”  Paulo anasema kwamba sisi zote tuko na hatia ya dhambi ya Adamu kwa sababu sisi sote ni wajukuu wake.  Hii inamaanisha zaidi na kuwa wenye dhambi waasi machoni pa Mungu, pia tulishiriki katika uasi wa kwanza ambao Adamu alitenda.  Hii inaweza onekana kuwa jambo la ajabu lakini ukiangalia kwa umakini unaona ukweli huu ni wazi.  Ikiwa Adamu alikuwa mwakilishi wetu basi ni lazima ile hatia alipata tulipata pamoja naye, pia ikiwa dhambi ya Adamu ilitufanya tuwe wenye dhambi basi ni lazima tulishiriki naye kuifanya dhambi hiyo.  Kwa hivyo dhambi ya Adamu ni dhambi yetu.  Tuko na hatia mbele za Mungu jinsi alikuwa Adamu.

 

Kuna Mambo mawili muhimu sana kukumbuka kuhusu matokeo ya dhambi ya Adamu.

 

Kabla tumalize funzo hili tunapaswa kukumbuka mambo mawili yanayohusu dhambi ya Adamu.

 

1.  Ni muhimu sana tuelewa kwamba uzao wote wa Adamu umeridhi asili ya dhambi ya Adamu, hii inamaanisha kila mtu, Siyo watu fulani fulani.  Tunapaswa kukumbuka haya sana hasa hasa wakati tunasoma sura ya 4 ya kitabu cha Mwanzo kwa sababu ni rahisi kufikiria kwamba Kaini alikuwa mwenye dhambi na Habili alikuwa mwenye haki na kwa hivyo dhambi ya Adamu haikumpata Habili.  Biblia inasema kwamba Bwana alipendezwa na Habili na sadaka yake (Mwanzo 4:4).  Hii haimaanishi kwamba Habili alikuwa mwema na kwamba dhambi ya Adamu haikumpata.  Habili alikuwa mwenye dhambi kama Kaini.  Tunajua huu ni ukweli kwa sababu baadaye Biblia inatueleza ni kwa nini Mungu alipendezwa na sadaka ya Habili.  Biblia inasema “Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini ; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake” (Waebrania 11:4).  Kuna njia mbili tu za kumwendea Mungu, yaani kumwendea kwa imani, ama kumwendea na matendo yetu mazuri.  Wale ambao ni wenye haki na siyo wenye dhambi humwendea Mungu kwa matendo yao mazuri.  Hivi ndivyo Yesu mwenyewe alifanya, na ni yeye tu ako na uwezo wa kufanya hivi.  Lakini wenye dhambi hawawezi kumwendea Mungu kwa matendo yao mazuri, wanaweza tu kuja kwa Mungu kwa imani pekee.  Habili alikuja kwa Mungu kwa imani na Mungu akamshuhudia kuwa mwenye haki, hangeweza kumjia Mungu kwa matendo yake mazuri kwa sababu alikuwa ameridhi dhambi ya Adamu na kwa hivyo alikuwa mwenye dhambi kama tu ndungu yake Kaini.

 

2.  Pili, ni muhimu sana kukumbuka kwamba hata kama sisi ni wenye dhambi, hatuko wabaya jinsi tungekuwa.  Ni kweli kwamba dhambi imeshawishi mawazo na moyo na uwezo na matendo ya mwanadamu, lakini hii haimaanishi kwamba mwanadamu amepotelea dhambini kabisa.  Hii ni kwa sababu ya neema ya Mungu ambayo inafanya kazi katika wanadamu wote.  Ijapokuwa sisi sote ni wenye dhambi, tunaweza kufanya mambo mazuri ya upendo, huruma na kazi ya kujitolea.  Kuna watu wengi duniani humu ambao wanatumia muda wao mwingi kila wakati maishani mwao wakitumikia wengine, siyo kwa sababu wao ni wazuri na wenye haki bali ni kwa sababu ya neema ya Mungu kwa watu wote nawawezesha kufanya haya.  Hii ndiyo sababu Yesu alisema “Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe?,Au akiomba samaki, atampa nyoka?  Basi ikiwa nyinyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?” (Mathayo 7:9-11).

 

Funzo la Saba: Tafadhali soma Mwanzo 4:17-5:32

 

Kifungu hiki kimejawa na majina ya watu na tunaweza kujiuliza je, ni nini tunajifunza kutokana na majina haya.  Lakini kifungu hiki kiko na mafunzo muhimu sana ambayo ni: kwa sababu ya matokeo ya dhambi  ya Adamu, wajukuu wake wamegawanyika katika vikundi viwili.  Jambo hili lilifanyika kwa sababu ya yale ambayo Mungu alimwambia shetani katika kitabu cha Mwanzo 3:15, “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake.”  Katika mstari huu, Mungu anatangaza mpango wake wa wokovu ambao alipanga kabla ya kuumba ulimwengu.  Lazima tukumbuke kwamba kuanguka kwa Adamu halikuwa jambo ambalo Mungu hakutarajia.  Biblia inasema kwamba Mungu anajua mwanzo hadi mwisho kwa hivyo alijua kwamba Adamu na Hawa wangeanguka kati dhambi.  Biblia inatuambia kwamba kabla ya kuumba ulimwengu, Mungu alipanga jinsi ya kuwaokoa watu wake (Waefeso 1:4).  Mungu alijichagulia idadi ya watu fulani kutoka kwa idadi ya watu wote ulimwenguni na kuamua kwamba watu hao ndiyo wataokolewa.  Hatuokolewi kwa sababu tumeamua kuokolewa, ni kwa sababu Mungu aliamua kwamba tuokolewe: kwa hivyo ni chaguo la Mungu siyo la mwanadamu.

 

Baada ya Mungu kuamua hivyo, Mungu alipanga kwamba katika nyakati zote ulimwenguni, kutakuwako makundi mawili ya watu ambao wataishi pamoja yaani wale ambao ni wateule wake na wale ambao ni siyo wateule wake.  Jambo hili linaonekana katika sura za Mwanzo 4 na 5.  Tumeona kwamba Habili wakati alileta sadaka yake mbele ya mungu, alikuja kwa imani kwa sababu yeye alikuwa mteule wa Mungu; “Si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake” (1 Yohana 3:12).  Pia tunaona jambo hili katika orodha ya majina ambayo yako katika kifungu ambacho tunajifunza.

 

1.  Kizazi cha Kaini.

 

(i). Ni watu ambao wanapenda ulimwengu.  Kaini alijenga mji na akaupatia jina ambalo lilikuwa la mwanawe Henoko (Mwanzo 4:17).  Hii ni thibitisho kwamba kwa kizazi hiki, ulimwengu ndiyo ulikuwa makao yao kwa sababu walikuwa wanapenda starehe ya hapa  ulimwenguni.

 

(ii). Kizazi hiki cha Kaini dhambi zao zilizaana kwa haraka sana.  Tunasoma kumhusu Lameki ambaye alikuwa na wanawake wawili (Mwanzo 4:24) na alimwua mtu (Mwanzo 4:23).

 

(iii). Kizazi hiki kilikuwa na kiburi sana kuhusu dhambi zao.  Lameki hakuona kwamba amefanya jambo baya kumwua mtu.  Badala yake tunamwona akijisifu kwa kumwua mtu, “Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba” (Mwanzo 4:24).

 

 

2.  Kizazi cha Sethi.

 

(i). Hawakuona ulimwengu kuwa makao yao.  Hii ndiyo sababu hatuambiwi kuhusu ni wapi waliishi au ni kazi za aina gani walikuwa wakifanya.  Ni orodha tu ya majina.  Ni jambo la kawaida kwamba watu ambao wametajwa kwenye orodha hii walikuwa na miji walimokaa na kufanya kazi.  Lakini haya yote ambayo ni mambo ya ulimwengu huu hatuelezwi chochote kuyahusu.

 

(ii). Pili, watu ambao wako kwa orodha hii “wanaliita jina la BWANA”(Mwanzo 4:26). Wanakuja kwa Mungu kwa imani na wanampenda na wakamwabudu.  Maisha yao yote wanaishi wakimtukuza Mungu.

 

(iii). Tatu, watu ambao wako kwa orodha hii walitembea na Mungu.  Tunaambiwa kwamba Henoko alienda pamoja na Mungu (Mwanzo 5:24), alikuwa na ushirika wa karibu sana na Mungu.  Hii ni orodha ya wana wa Mungu na tunaona mfano huu mkubwa sana kwamba mmoja wao alitembea na Mungu kwa karibu sana.

 

(iv). Nne, watu katika orodha hii waliishi maisha yao wakitumainia wokovu wa milele kupitia majiribu ya ulimwengu huu.  Hii inaonekana wazi wakati mmoja wa wajukuu wao alipozaliwa, yaani Nuhu, walisema, “Huyu ndiye atayetufariji kwa kazi yetu na kwa taabu ya mikono yetu katika nchi aliyoilaani BWANA”(Mwanzo 5:29).  Dhamira zao zilikuwa zinawakumbusha vile Adamu alivyoanguka dhambini na matokeo yake kwa wanadamu, kwa hivyo walingoja kwa imani na tumaini siku ile watakombolewa kutoka kwa laana ya Mungu duniani.

 

(v). Mwisho, watu katika orodha hii walijua neema ya Mungu.  Tunaambiwa “Nuhu akapata neema machoni pa BWANA”.(Mwanzo 6:8).  Watu hawa walizaliwa wakiwa wenye dhambi lakini kwa neema ya Mungu waliletwa katika ufalme wa Mungu na wakafanywa watoto wapendwa na walitembea na Mungu siku zote.  Watu hawa hawakuwa wa ulimwengu huu bali walitumainia siku ile watakuwa huru na dunia yote kurudishwa katika hali isiyokuwa na laana.

 

Mambo haya matano ndiyo alama za wakristo.  Hata siku ya leo wakristo wote wako na hizi alama: yaani wao siyo wa ulimwengu huu, wanamwita Bwana kila wakati awaokoe na awaongoze, wanatembea na Mungu, wanatumainia siku ile watakombolewa milele kutoka kwa ulimwengu huu wa dhambi na wanajua neema ya Mungu katika wokovu wao na katika maisha yao ya kila siku