Header

Kuhusu kijitabu hiki.

 

Katika kijitabu hiki tutajifunza kuhusu Mungu.  Jambo muhimu ambalo sisi wanadamu tunafaa kufanya ni kujua Mungu ni nani.  Kwa haya tumebarikiwa sana kwa sababu Mungu ametufunulia ukweli kumhusu katika neno lake ambalo ni Biblia.  Katika somo hili badala ya kusoma Biblia yote, tutasoma na kuangazia kitabu kimoja ambacho ni kitabu cha Kutoka.  Kitabu cha Kutoka kiliandikwa ili Waisraeli wamjue Mungu wao ni nani; nasi kila kitu tunataka kujua kumhusu Mungu kiko hapa.  Katika somo hili tutasoma sura ya 1-20 ya kitabu cha Kutoka na tuone ni nini kila kifungu kinafunza kuhusu Mungu.  Kuna mafunzo kumi katika somo hili, na katika kila funzo tutasoma kifungu fulani kutoka kitabu cha Kutoka.  Kabla hujaanza kila funzo, hakikisha kwamba umesoma kifungu ambacho funzo limetolewa.

 

Mafundisho kuhusu Mungu ni mafundisho ambayo ni muhimu sana.  Kwa hivyo ni jambo muhimu kwamba tunasoma mafundisho haya kwa makini sana.  Kuna watu wengi ambao wanasoma Biblia ili wajifunze kuhusu Mungu lakini hawafaidiki na lolote kwa sababu hawasomi kwa njia inayofaa.  Ninawasihi kwamba kabla ya kila funzo hakikisheni kwamba mnakuwa na wakati wa maombi kwanza, mkiomba Mungu atayarishe mioyo yenu mweze kutii Biblia.  Watu wengi ulimwenguni wanamjua Mungu kwa njia tofauti tofauti.  Mara mingi kufahamu kwao ni kutokana na mawazo yao na mafunzo ya uongo ambayo wamepokea, bali siyo neno la Mungu.  Labda jambo hili ni la ukweli kukuhusu wewe.  Labda wewe unafikiria kwamba unaelewa Mungu ni nani na jinsi alivyo, lakini ukweli ni kwamba hujawahi kusoma Biblia ili uelewa kwa ukweli jinsi Mungu anavyozungumza kujihusu.

 

Kumbuka kwamba mafunzo ambayo umepata kumhusu Mungu yanaweza kuwa ni ya uongo kabisa.  Kuna uwezekano kwamba wakati unapoanza kusoma mafunzo haya unajua machache kabisa kuhusu Mungu ni nani.  Kuna watu ambao wakisoma neno la Mungu na kufahamu Mungu ni nani, wanalikataa kuliamini.  Hii ni kwa sababu tayari wamefunzwa mambo ambayo ni ya uongo na hawako tayari kuyaacha.  Pia ni kwa sababu Biblia haikubaliani na mawazo yao kumhusu Mungu.  Mara mingi utamsikia mtu akisema, “Siwezi kukubaliana na jambo hilo, kwa sababu si jambo la ukweli.”  Mara mingi wanasema hivi kwa sababu wamesoma jambo kutoka kwa Biblia ambalo liko kinyume na mawazo yao kumhusu Mungu; na kwa hivyo wanakataa neno la Mungu.  Tabia ya aina hii ni kiburi na kukataa neno la Mungu; hii ni dhambi hatari sana.  Kwa hivyo kabla hujaanza mafunzo yoyote umwombe Mungu akupe moyo ambao ni mnyenyekevu na uko tayari kukubali neno la Mungu.  Uombe akupe moyo ambao uko tayari kukataa mawazo yote ambayo yako kinyume na neno lako.

 

 

Funzo la Kwanza: Tafadhali soma kitabu cha Kutoka 1:1-2:22

 

Kifungu hiki ndicho utangulizi wa kitabu cha Kutoka.  Kinatukumbusha kwamba kitabu cha Kutoka kimeandikwa kuendelesha kitabu cha Mwanzo, hata kama matokeo yake ni ya miaka 400 baada ya matokeo katika kitabu cha Mwanzo.  Unaweza kusoma sura za mwisho za kitabu cha Mwanzo ili uweze kuelewa vyema kitabu cha Kutoka.  Wakati wa Yusufu, Waisraeli walienda Misri kwa sababu katika nchi ya Kanani kulikuwa na kiangazi.  Kule Misri waliishi maisha ya starehe kwa sababu Yusufu alikuwa na cheo kikuu katika serikali ya Misri.  Katika kifungu hiki (Kutoka 1:1-2:22), tunaambiwa jinsi Waisraeli waliishi Misri (1:1-5).  Baadaye tunaambiwa baada ya muda fulani, Yusufu na wale wote ambao walitoka Kanani walikufa, lakini baraka za Mungu zilibaki juu ya Waisraeli na waliendelea kuongezeka kwa idadi kubwa sana.

 

Baada ya miaka 400, kulitokea mfalme mwingine wa Misri ambaye hakumjua Yusufu.  Wakati huu Waisraeli walikuwa wengi sana na mfalme huyu aliogopa kwamba vita ikitokea pengine Waisraeli wataungana na maadui wao.  Kwa sababu hii mfalme huyu aliamua kuwafanyisha kazi ngumu sana ili awaangamize.  “Lakini kadiri walivyoteswa ndivyo Waisraeli walivyoongezeka na kuenea nchini” (1:12).  Kwa hivyo mfalme alipanga mpango wa kuwamaliza wote, aliwaambia wale ambao wanawasaidia wamama wakati wanapokuwa wakizaa kwamba mwanamke Mwisraeli akizaa mtoto kijana wachukue mtoto huyu na wamtupe katika mtoni.

 

Kifungu hiki kinaendelea kutueleza jinsi Musa alivyozaliwa, na kwa mpango wa Mungu alifanyika mwana wa binti ya Farao.  Musa akiwa miaka 40 aliua mtu na akatoroka Misri.  Alienda akaishi katika nchi ya Midiani na akamwoa Zipora, mmoja wa mabinti wa kuhani wa Midiani.  Ilionekana kwamba wakati huu Musa hakuwa na mpango wa kurudi Misri kwani alikuwa ametosheka na kusihi kule Midiani.

 

Ni jambo la kushangaza kwamba katika kifungu hiki chote hakuna mahali jina la Mungu limetajwa.  Mara ya kwanza tunaona jina la Mungu ni katika sura ya 2:23.  Lakini jambo hili halimaanishi kwamba hakuna mafundisho ya kujifunza kuhusu Mungu katika kifungu hiki.  Kuna funzo moja ambalo ni muhimu sana tunafaa kujifunza kuhusu Mungu: Mungu ndiye anaongoza maisha ya watu wake kwa kila hali.  Tunajua jambo hili kwa sababu Mungu alikuwa amemwongelesha Ibrahimu na akamwambia, “Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watatesewa kwa miaka 400 hata na taifa lile, watakaowatumikia nitawahukumu badaye watatoka na mali mengi” (Mwanzo 15:13-14).

 

Mungu alimwambia Ibrahimu mambo yote kuhusu yale ambayo yangewatendekea Waisraeli kule Misri na jinsi Mungu angewaokoa.  Je, Mungu alijuaje mambo haya yote?  Jibu ni kwamba Mungu anajua kila kitu kwa sababu ni Yeye ambaye anapanga kila kitu.  Kuishi na mateso ya Waisraeli kule Misri hayakuwa mambo ambayo yalitendeka tu bila Mungu kujua.  Mambo haya yote yalipangwa na Mungu.  Mungu anaongoza maisha ya watu wake kwa kila hali.

 

Funzo la Pili: Tafadhali soma kitabu cha Kutoka 2:23-25

 

Katika kifungu hiki tunapata jina la Mungu mara ya kwanza katika kitabu hiki.  Katika mistari hii mitatu tunasoma mambo muhimu kumhusu Mungu.

 

1. Kwanza, Mungu anasikia maombi ya watu wake.  Tunaambiwa katika mstari wa 23 kwamba watu waliomba kwa muda mrefu.  Labda kwao walifikiria kwamba Mungu hakuwa anasikia maombi kwa sababu waliomba kwa muda mrefu.  Tunaambiwa kwamba “Kilio cha Waisraeli kimenifikia; nimeona jinsi Wamisri wanavyowatesa.”  Mungu alisikia maombi yao hata kama kwao ilionekana kwamba Mungu alikuwa hasikii kilio chao.  Tunafaa kukumbuka kwamba Mungu anasikia maombi yetu na anayajibu kwa wakati wake ufaao.  Mungu hafanyi kazi kulingana na matakwa yetu, ako na mpango wake na wakati wake wa kutimiza kila jambo.  Tunafaa kuomba kwa Mungu kwa sababu hii ni amri yake kwetu, lakini hatuwezi kumlazimisha Mungu ajibu maombi yetu kwa wakati fulani na kwa njia fulani.  Tumeambiwa tuombe na pia tumeambiwa tuvumilie kwa maombi (Luka 18:1-8).  Lakini hakuna mahali popote ambapo Biblia inasema kwamba tunaweza kumfanya Mungu ajibu maombi yetu kulingana na jinsi tunavyotaka.

 

2. Pili, Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake.  Tunaambiwa, “Akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu, Isaka na Yakobo.”  Kwa miaka mingi iliyopita, Mungu alitengeneza agano na Ibrahimu na akamwambia, “Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako” (Mwanzo 17:7).

 

Hapa Mungu alitengeneza uhusiano kati yake na Ibrahimu.  Aliahidi kwamba Yeye atakuwa Mungu wa Ibrahimu na Mungu wazawa wa Ibrahimu.  Alikuwa ameahidi kwamba atalaani yeyote ambaye angelaani Ibrahimu (Mwanzo 12:3).  Hizi ni ahadi ambazo Mungu aliahidi Ibrahimu.  Baada ya miaka mingi baadaye Waisraeli walimlilia Mungu, na Mungu alikumbuka agano lake na ndiyo sababu alikuja na akawaokoa Waisraeli.  Aliwaadhibu Wamisri kwa sababu waliwatesa watu wake.

 

3. Tatu, Mungu anajali sana maisha ya watu wake.  Katika kifungu hiki tunasoma, “Nimeona mateso ya watu wangu walioko nchini Misri na nimesikia kilio chao.”  Aliona kwamba watu wake walikuwa watumwa wa Wamisri na aliwajali.  Mungu hakuwapuuza bali aliona yote ambayo ilikuwa inawatendekea.  Jambo hili ni himizo kubwa sana kwa watu wote wa Mungu.  Shida zetu si kitu zikilinganishwa na mateso ambayo Waisraeli walipitia.  Mara mingi kama Waisraeli tunamwomba Mungu na mara mingi huonekana kama Mungu hasikii maombi yetu.  Mara mingi tunawaza kwamba Mungu ako mbali nasi na hajali maisha yetu.  Tupate himizo kutoka kwa kifungu hiki.  Hata tusipoona jibu la maombi yetu kwa haraka, tunaweza kuwa na hakikisho kwamba Mungu ametusikia na kwamba Yeye ni mwaminifu kwa ahadi zake ambazo ametuahidi.  Biblia inasema, “Mwekeeni matatizo yenu yote maana yeye anawatunzeni” (1 Petro 5:7).

 

Funzo la Tatu: Tafadhali soma kitabu cha Kutoka 3:1-12

 

Katika kifungu hiki tunasoma kuhusu Musa, ambaye alikuwa na miaka 80, alikuwa siku moja akichunga kondoo katika jangwa.  Wakati huo Mungu alimtokea na akamwongelesha.  Hiki ni kifungu ambacho kimejawa na mafunzo ya utajiri mwingi kuhusu Mungu na jinsi alivyo.

 

1. Kwanza, Mungu anajitambulisha kwa watu wake.  Tunaona katika kifungu hiki kwamba Mungu aliongea na Musa.  Jambo hili ndiyo msingi wa kitabu hiki cha Kutoka.  Mistari kama, “Mungu alisema” na “Mungu amesema” imerudiwa mara 80 katika kitabu hiki.  Mara kwa mara, katika kitabu hiki, Mungu anajitambulisha kwa watu wake.  Anajitambulisha kwa Musa, halafu kwa wazee Waisraeli, halafu kwa Farao na kwa taifa zima la Uisraeli.  Mungu wetu ni Mungu ambaye anajitambulisha kwa watu wake.  Hili ni jambo muhimu sana kwa sababu kama Mungu hangejitambulisha kwetu, hatungejua Yeye ni nani.  Sisi ni wanadamu na hatujui kila kitu na pia sisi ni wenye dhambi.  Hii inamaanisha kwamba kama tutamjua Mungu, basi Mungu lazima ajitambulishe kwetu.  Mungu asipozungumza hatuwahi kumjua.  Hii ndiyo sababu Biblia ni kitabu cha maana sana: ni Mungu anajitambulisha kwetu.  Hatuwezi kubahatisha njia za Mungu au jinsi alivyo, mambo haya yote tunaweza kuyapata katika Biblia pekee.  Kuna watu leo ambao husema kwamba wanajua mapenzi ya Mungu na njia za Mungu bila kusoma Biblia.  Wanasema kwamba wanajua Mungu ni nani na ni nini atafanya katika maisha yao na mambo mengine.  Watu kama hao ni waongo na hakuna chochote wanaelewa.  Wanapuuza Biblia ambayo Mungu ametumia kujitambulisha kwetu na wanaanza kutumia mawazo yao ya uongo ambayo haielewi chochote kumhusu Mungu.  Watu hawa wanamwasi Mungu; wao ni waasi.  Mungu anajitambulisha kwetu kupitia kwa neno lake, kwa hivyo tusianze kujidanganya kuhusu Mungu ni nani na ni nini anafanya.  Badala ya upumbavu huu, tujitolee kusoma na kujifunza Biblia ambayo ni mahali pa pekee Mungu anazungumza nasi.

 

2. Pili, Mungu ni Mtakatifu.  Mungu alimwambia Musa, “Vua viatu vyako kwa sababu mahali unaposimama ni mahali patakatifu.”  Neno “patakatifu” ni moja wapo wa maneno muhimu sana katika Biblia.  Katika kifungu hiki neno hili linamaanisha kwamba, “Mungu ni Mtakatifu, bila uchafu wowote au dhambi yoyote.”  Hii ndiyo sababu Musa alihitajika kuwa mwangalifu wakati alikuwa akija mbele ya Mungu.  Kama mwanadamu wote, Musa alikuwa mwenye dhambi na kwa hivyo hangeweza kuenda mbele ya Mungu bila kujua ni nini alikuwa akifanya.  Biblia inatukumbusha mara kwa mara kwamba Mungu ni mtakatifu na ni mkamilifu.  Mungu anawaambia watu wake, “Jiwekeni wakfu na kuwa watakatifu kwa maana mimi ni Mtakatifu” (Walawi 11:44). Watu wa Mungu ni lazima wawe watakatifu kwa sababu Baba yao wa mbinguni ni mtakatifu.

 

3. Tatu, Mungu ni Mungu wa wokovu.  Katika mstari wa 7 Mungu anamwambia Musa, “Nimeona mateso ya watu wangu walioko nchini Misri na nimekisikia kilio chao kinachosababishwa na mateso ya wanyapara wao.  Najua mateso yao, na hivyo, nimeshuka ili niwaokoe mikononi mwa Wamisri.  Nitawatoa humo nchini na kuwapeleka katika nchi nzuri na kubwa; nchi inayotiririka maziwa na asali.”  Kukombolewa kwa Waisraeli kutoka Misri ni mfano wa wokovu wetu; kwani tunapotazama kukombolewa huku tunaelewa kuhusu wokovu wetu kutoka kwa dhambi.  Kuna mambo matano ya kuangazia kuhusu wokovu.

 

(i) Ni Mungu mwenyewe ambaye aliokoa Waisraeli kutoka Misri.  Ingawa alimwita Musa na kumtuma kwa Farao, kazi yenyewe ya kuwaokoa Waisraeli ilikuwa kazi ya Mungu mwenyewe.  Mungu anasema, “Nashuka ili niwaokoe mikononi mwa Wamisri.”  Kwa njia hiyo hiyo kazi ya wokovu wetu ni kazi ya Mungu mwenyewe; ni Mungu ambaye alipanga wokovu wetu na ni Mungu ambaye alikamilisha kazi hii kwa kumtuma Mwanawe katika ulimwengu huu ili awe mwokozi wetu.  Hatuokolewi kwa matendo yetu mazuri; tunaokolewa na Mungu: “Wokovu hutoka kwa Bwana” (Yona 2:9).

 

(ii) Mungu aliwaokoa Waisraeli kutoka kwa mateso na utumwa.  Huu ni mfano wa dhambi.  Mara mingi watu huwaza kwamba maisha bila wokovu ni maisha ya furaha na kwamba wakati mtu anapookolewa hatapata tena furaha yake.  Lakini watu wanafikiria hivi kwa sababu dhambi imewadanganya.  Hii ni sababu Paulo anasema, “Maana dhambi ilichukua fursa iliyopatiwa na amri hiyo, ikanidanganya na kuniua” (Warumi 7:11).  Dhambi ni kitu kidanaganyifu.  Dhambi inatuongoza kuwaza kwamba maisha katika ulimwengu huu ni mazuri, ilhali ni maisha ya mateso na utumwa.  Wakati tunaokoka tunaondolewa katika maisha ya utumwa wa dhambi.

 

(iii) Mungu aliahidi kuwatoa Waisraeli katika nchi ya utumwa na kuwapeleka “nchi mzuri ambayo inatiririka na maziwa na asali.”  Hivi ndivyo Mungu alivyopanga wokovu wao.  Hakuwatoa katika utumwa na kuwaacha huru jangwani ili wajishughulikie.  Hakuwaambia, “Mliniuliza niwatoe katika utumwa.  Nimefanya hivyo, basi nendeni na mfanya jinsi mnavyotaka katika ulimwengu.” Aliwatoa katika nchi ya Misri na kuwapeleka katika nchi mzuri.  Hivi ndivyo wokovu wetu ulivyo.  Mungu hatutoi katika utumwa wa dhambi na kutuacha tufanye jinsi tunavyotaka.  Anatuokoa kutoka kwa dhambi na kutufanya tuwe wanawe.  Anamtuma Roho Matakatifu ambaye anakuja na kuishi ndani mwetu akitukamilisha kuwa kama Kristo mwenyewe; na badaye anatupeleka mbinguni tuishi naye milele.

 

(iv) Wakati aliwaokoa Waisraeli kutoka Misri alimtumia Musa.  Kama tutakavyoona badaye katika masomo haya, Mungu ni mwenye nguvu na anaweza kufanya lolote apendalo.  Siyo tu kwamba alihitaji kumtumia Musa na kwamba bila Musa hangeweza kufanya lolote.  Lakini kukombolewa kwa Waisraeli ni mfano kwetu tujifunze kuhusu wokovu wetu.  Mungu alimtuma Musa kwa Wamisri na kupitia Musa Mungu aliwaokoa Waisraeli.  Ni Musa ambaye aliwaongoza kutoka Misri. Waisraeli wote ambao walitaka kuwa huru walihitaji tu kumfuata Musa.  Kama hawangemfuata Musa hawangeokolewa.  Tunapotazama jambo hili kwa makini tutaona kwamba Musa ni mfano wa Kristo Yesu.  Kama vile Mungu alivyomtuma Musa kwa Waisraeli wakiwa Misri, ndivyo pia alivyomtuma Kristo Yesu kwa watu wake kote ulimwenguni.  Kama tu vile Musa alikumbana na Farao na akamshinda na kuwaongoza Waisraeli kutoka Misri, ndivyo pia Bwana Yesu Kristo alivyokumbana na shetani ambaye aliwaongoza watu wa Mungu katika utumwa wa dhambi na kwa ushindi Yesu aliwaokoa.  Kama tu vile Musa alivyowaongoza Waisraeli katika jangwa hadi nchi ya ahadi, Bwana Yesu Kristo anatuongoza maishani mwetu mwote hapa ulimwenguni na siku moja atatuongoza kuingia mbinguni.

 

(v) Mungu aliokoa tu wale ambao walikuwa watu wake.  Mungu aliwatoa wana wa Ibrahimu kutoka Misri.  Hatusomi mahali popote katika Biblia kwamba aliwaokoa watu wengine.  Inawezekana kwamba katika nchi ya Misri kulikuwa na watu wengine ambao walikuwa watumwa.  Lakini watu hawa hawakuwa katika mpango wa Mungu wa kuokolewa.  Hili ni jambo ambalo tunafaa kuelewa vizuri.  Kwa nini kuna watu ambao wataenda mbinguni na wengine hapana?  Jibu ambalo Biblia inapeana ni kwamba wale ambao wataenda mbinguni ni wateule wa Mungu.  Wanaenda mbinguni kwa sababu waliteuliwa na Mungu kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu kwamba wataokoka (Waefeso 1:3-4; 2 Wathesalonike 2:13).  Wakati Bwana Yesu alikuwa hapa ulimwenguni kulikuwa na watu wengi ambao hawakumwamini.  Yesu aliwaambia, “Lakini nyinyi hamsadiki kwa sababu nyinyi si kondoo wangu” (Yohana 10:26).  Kama tu vile kulikuwa na kikundi cha watu kule Misri ambacho kilikuwa kikundi cha Mungu, pia kuna watu katika ulimwengu huu ambao ni kondoo wa Mungu.  Hawa tu ndiyo wale ambao watasikia sauti ya Yesu na kuja kwake: “Kondoo wangu wanaisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata” (Yohana 10:27).

 

 

 

Funzo la Nne: Tafadhali soma kitabu cha Kutoka 3:11-22

 

Katika kifungu hiki tunasoma kuhusu mazungumzo kati ya Musa na Mungu.

 

1. Kwanza, Mungu anaelewa udhaifu wa wanadamu.  Wakati Mungu alimwamuru Musa arudi Misri akaongoze Waisraeli kutoka huko, Musa alijibu, “Mimi ni nani hata nimwendee Farao na kuwatoa Waisraeli nchini Misri?”  Hili lilikuwa swali la kawaida kwani Musa alikuwa ameacha kuwa mwana wa binti ya Farao.  Alikuwa katika jangwa la Midiani kwa miaka 40 na wakati huu haikuwa rahisi kwamba kuna mtu yeyote ambaye alimkumbuka.  Kulingana na Farao Musa alikuwa mchungaji wa mifugo tu jangwani.  Na labda pia hangewahi kupata nafasi ya kuzungumza na Farao.  Mungu alielewa shida ya Musa na aliahidi kumsaidia.  Sisi wakristo mara mingi tunajipata katika hali kama hii ambayo hatuwezi kufanya kile tunataka kufanya.  Tunafaa kukumbuka kwamba Mungu anaelewa udhaifu wetu na atatusaidia.

 

2. Pili, Mungu ni Mungu wa milele na amekuwepo siku zote na ataendelea kuwepo.

 

Katika mazungumzo haya, Musa anamwuliza Mungu jina lake.  Mungu akamjibu, “Mimi Ndimi Niliye.”  Neno, “Ndimi” ni tafsiri ya Kiebrania Yehovah.  Jina hili linamaanisha kwamba Mungu amekuwepo siku zote kabla ya kila kitu au mtu yeyote; Yeye amekuwepo.  Pia inamaanisha kwamba ataendelea kuwepo hata kama hakuna chochote kitakuwepo mbeleni; kila kitu kiko mikononi mwa Mungu na ni Yeye anafanya mambo yatendeke.  Jina hili pia linamaanisha kwamba Mungu hategemei kitu chochote au mtu yeyote ndipo akuwepo.  Wanadamu wote wanamtegemea Mungu ndiyo waweze kuishi.  Kama Mungu hangekuwepo, hata sisi hatungekuwepo.  Hii ndiyo sababu Paulo anasema, “Kwa maana, ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu” (Matendo ya Mitume 17:28).

 

3. Tatu, kila jambo linalotendeka ni kwa sababu Mungu ameliamuru litendeke.  Katika mistari ya 18-22 Mungu alimweleza Musa mambo matano ambayo yalikuwa yatendeke.

 

(i) Alimwambia kwamba wazee wa Waisraeli watasikia maneno yake (mstari wa 18).

(ii) Alimwambia Musa kwamba yeye na wazee wa Waisraeli watakubaliwa kumwona Farao (mstari wa 18).

(iii) Alimwambia Musa kwamba Farao hatawaachilia waende hadi atakapoona nguvu za ajabu za Mungu (mstari wa 19).

(iv) Alimwambia Musa kwamba mapigo mengi yatatokea kabla ya Farao kuwaruhusu Waisraeli waende (mstari wa 20).

(v) Alimwambia Musa kwamba Wamisri watakuwa wazuri kwa Waisraeli na watakapoondoka Misri hawataondoka mikono mitupu (mstari wa 21-22).

 

Sababu ya Mungu kusema haya yote ni Yeye ambaye alipanga mambo haya yote.  Sababu kwa nini Mungu anajua ya mbeleni ni kwa sababu ni Yeye ambaye anapanga ya mbeleni.  Ni yeye ambaye alipanga kwamba wazee wa Waisraeli watamsikiza Musa.  Ni Yeye ambaye alipanga kwamba Farao angewaruhusu Musa na wazee wa Waisraeli wamwone na waongee naye hata kama yeye alikuwa mfalme.  Ni Mungu ambaye alipanga kwamba Farao angekataa kuwaachilia Waisraeli waende.  Mambo haya yote yanaonyesha kwamba Mungu ndiye anapanga kila jambo na kulidhibiti hapa ulimwenguni na mbinguni.

 

4. Nne, Mungu ni mwenye hekima kwa kila mpango wake.  Vile tumeona, Mungu ndiye anapanga kila jambo na kulidhibiti.  Chochote anataka kitendeke kitatendeka.  Mungu angeweza kuwaachilia Waisraeli kutoka Misri mara moja.  Angeweza kuuguza moyo wa Farao na awaachilie Waisraeli waende au angewaangamiza Wamisri pamoja na Farao ili Waisraeli waende.  Mungu alimwambia Farao, “Ningelikwisha kukuangamiza tayari wewe na watu wako kwa maradhi mabaya, nanyi mngalikuwa mmekwisha angamia” (Kutoka 9:15).  Tunajua kwamba baadaye katika historia ya Uisraeli kwamba Mungu alifanya kazi katika moyo wa mfalme fulani na aliwaachilia watu wake.  Hili lilitendeka wakati Waisraeli walikuwa katika utumwa kule Babeli kwa sababu ya dhambi zao. Baada ya miaka 70, Biblia inasema kwamba, Mungu alimfanya mfalme Koreshi awaachilie watu wake (Ezra 1:1).

 

Kwa hivyo pia Mungu angeweza kumfanya Farao awaachilie Waisraeli bila kutumia Musa au Haruni au Wazee wa Waisraeli au pia Mungu angeweza kuwaangamiza Misri pamoja na Farao.  Lakini tunapata kwamba Mungu hakufanya hivyo.  Jambo la kushangaza ni kwamba aliufanya moyo wa Farao kuwa mgumu sana ili asiweze kumsikia Musa.  Musa aliambiwa, “Utakapofika Misri, hakikisha kwamba umetenda mbele ya Farao miujiza yote niliyokupa uwezo ufanye.  Lakini mimi nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hatawaachilia Waisraeli waondoke” (Kutoka 4:21).  Hivi ndivyo Mungu alivyofanya; baadaye tunaambiwa kwamba, “Mwenyezi Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi naye hakuwasikiliza kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwambia Musa; Lakini mwenyezi Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, naye hakuwaachilia Waisraeli waondoke” (Kutoka 9:12, 10:20).

 

Swali ni kwa nini Mungu akafanya hivi?  Kwa nini Mungu anaufanya moyo wa mtu kuwa mgumu ili asiweze kutii neno lake?  Kuna vifungu viwili katika kitabu hiki cha Kutoka ambapo tumepewa jibu la swali hili.

 

(i) Kutoka 9:16 Mungu anamwambia Farao, “Lakini nimekusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uwezo wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote.”  Katika mstari huu tunapata sababu mbili kwa nini Mungu aliufanya moyo wa Farao kuwa mgumu wakati Musa alipokuwa akizungumza naye.

 

Kwanza, Mungu alitaka kumwonyesha  Farao nguvu zake.  “Lakini nimekusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uwezo wangu.”  Farao alikuwa mfalme wa Misri, nchi ambayo wakati huo ilikuwa nchi yenye mamlaka zaidi kuliko nchi yoyote.  Ilikuwa nchi ambayo ilikuwa na utajiri mwingi.  Kwa mfalme wa nchi kama hii alijiwazia kwamba yeye ndiye mtu mwenye mamlaka sana kuliko mtu yeyote hapa ulimwenguni na kwamba hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kubishana naye.  Farao alikuwa mtu wa aina hii kwa sababu alikuwa amewafanya watumwa Waisraeli na pia alijaribu kuwaangamiza.  Ukombozi wa Waisraeli ulipangwa ili kumwonyesha Farao kwamba Mungu ndiye mwenye nguvu zote kuliko kiumbe chochote.  Miaka mingi baadaye jambo hili lilimtendekea mfalme wa Babeli ambaye alikuwa na kiburi sana kwa sababu ya mamlaka ambayo alikuwa nayo.  Mungu alimfanya ale nyasi pamoja na wanyama (Dan. sura ya 4).

 

Pili, “Tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote.”  Mungu alitaka Farao ajue kwamba yeye ni mwenye nguvu zote ulimwenguni kote.  Ikiwa Mungu angemfanya Farao awaachilie Waisraeli bila mambo makubwa, basi jambo hili halingekuwa kubwa sana.  Lakini Mungu kwa mapenzi yake alitaka jambo hili liwe kubwa ili mataifa ya ulimwengu yamjue Yeye ni nani.  Miaka 40 baadaye, wakati Yoshua aliwaongoza Waisraeli kuingia Kanani, walipatana na mama ambaye aliitwa Rahabu katika mji wa Yeriko ambaye aliwaeleza kwamba, “Tumesikia jinsi Mwenyezi Mungu alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu mlipotoka nchi ya Misri” (Yoshua 2:10).

 

Kwa hivyo tunajifunza katika kitabu cha Kutoka 9:16 sababu mbili kwa nini Mungu aliufanya moyo wa Farao kuwa mgumu: alitaka Farao na mataifa ya ulimwenguni kujua kwamba Yeye ni mwenye nguvu.

 

(ii) Katika kitabu cha Kutoka 10:1-2 Mungu alimwambia Musa, “Ingia wewe kwa Farao, kwa kuwa mimi nimeufanya moyo wake mzito, nipate kuzionyeshe ishara zangu hizi kati yao; nawe upate kusema masikioni mwa mwanao, na masikioni mwa mjukuu wako, ni mambo gani niliyotenda juu ya Misri na ishara zangu nilizozifanya kati yao; ili mpate kujua kuwa mimi ndimi Bwana.”  Katika kifungu hiki tunapata sababu mbili kwa nini Mungu aliufanya moyo wa Farao kuwa mgumu.

 

Kwanza, ilifanyika hivi ili Waisraeli wawaambie watoto wao na wajukuu wao jinsi Mungu alivyowapigania nchini Misri.  Wamisri walikuwa watenda dhambi wakuu machoni pa Mungu, na hii ndiyo sababu Mungu aliwaadhibu vibaya sana.  Siku moja Mungu alipita katika nchi ya Misri na akaangamiza kila uzao wa kwanza wa Wamisri, watoto na wanyama.  Sababu ya kufanya hivi inapeanwa katika Biblia, “Usiku huo, nitapita katika nchi ya Misri na kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Misri, watu na wanyama.  Nitaadhibu miungu yote ya Misri.  Mimi ndimi Mwenyezi Mungu” (Kutoka 12:12).  Mungu alitaka Waisraeli wajifunze funzo hili ili wasianguke katika dhambi.  Ikiwa Waisraeli wangeona jinsi Mungu anavyohukumu watu wangezingatia jambo hili na kujiweka vyema ili wasije wakaanguka katika dhambi.   Hii ndiyo sababu Mungu aliufanya moyo wa Farao kuwa mgumu ili pigo la kufa kwa mtoto wa kwanza na mnyama wa kwanza lingetendeka.

 

Pili, aliufanya moyo wa Farao kuwa mgumu ili Waisraeli wajue kwamba Yeye ni Bwana. Kama jinsi tutakavyoona baadaye katika mafunzo haya, Waisraeli walikuwa pia wakiabudu masanamu.  Walikuwa wamepoteza ufahamu wao kumhusu Mungu na walianza kuabudu masanamu.  Mungu alipanga kuwakomboa kutoka kwa utumwa na kuwafanya watu wake.  Kwa hivyo lilikuwa jambo muhimu sana kumjua Mungu kwamba Yeye si kama yale masanamu walikuwa wakiabudu; bali Yeye ni Mungu mwenye nguvu zote na mamlaka. Kwa sababu walihitajika kuishi wakiwa watu wa Mungu, walihitaji kumjua Mungu vyema. Kwa hivyo Mungu alitumia miujiza hii kuonyesha yeye ni nani.

 

Sisi pia tunaweza kusahau jinsi Mungu wetu alivyo mkuu sana.  Tunahitaji kujikumbusha kuhusu kazi zake za ajabu na kazi yake kuu ya wokovu.  Hadi tutakapomwelewa Mungu vyema, ndipo tutaweza kumpenda na kumtumikia kwa njia inayofaa.

Funzo la Tano: Tafadhali soma kitabu cha Kutoka 4

 

Katika sura hii tunasoma mambo muhimu kumhusu Mungu.

 

1. Kwanza, Mungu ako na mamlaka yote juu ya kila kitu ulimwenguni.  Katika mistari ya 1-9 tunasoma kuhusu miujiza tatu.  Katika muujiza wa kwanza, Musa alitupa fimbo yake chini na ikageuka nyoka.  Wakati alishika fimbo yake kutoka chini iligeuka tena ikawa fimbo.  Katika muujiza wa pili, mkono wa Musa ulikuwa na ukoma na baadaye ukapona.  Mwisho, Mungu alimwambia Musa kwamba kama Waisraeli hawatamsikia, alikuwa achukue maji kutoka mto na ayamwage chini na yatageuka kuwa damu.  Miujiza hii mitatu ilikuwa iwaonyeshe Waisraeli kwamba Mungu ako na mamlaka juu ya kila kitu hapa ulimwenguni; na anadhibiti kila kitu kwa utukufu wake.  Kuna sababu mbili kwa nini Waisraeli walihitaji kufunzwa mambo haya.

 

Kwanza, kwa miaka 400 Waisraeli walikuwa wakiishi nchini Misri, mahali ambapo watu wa huko walikuwa wakiabudu sanamu.  Ni jambo la kawaida kwamba tukiishi miongoni mwa watu ambao wanaabudu sanamu, wakati mwingine tunaanza kufanya jinsi wanavyofanya bila kuwaza sana juu ya mambo haya.  Wamisri, kama wale wote ambao wanaabudu sanamu, walifikiria kwamba kuna miungu mingi na kila mungu alikuwa na sehemu yake ambayo anadhibiti.  Kwa mfano walidhani kwamba kulikuwa na mungu ambaye alikuwa anadhibiti ukulima, mwingine kuvua samaki na mambo mengine.  Mawazo ya aina hii ni ya uongo. Kuna Mungu mmoja na adhibiti kila kitu mikononi mwake.  Waisraeli walihitaji kujua jambo hili ikiwa walikuwa watembee na Mungu kwa uaminifu.

 

Pili, Waisraeli walikuwa watoke Misri na waende wamalize miaka 40 katika jangwa wakati ambapo walihitaji kumtegemea Mungu kabisa kwa kila kitu.  Ikiwa walikuwa watembee na Mungu kwa uaminifu walihitaji kumjua Mungu ni nani na kwamba anadhibiti kila kitu mikononi mwake na alikuwa na uwezo wa kutosheleza mahitaji yao.

 

2. Pili, Mungu ndiye anayedhibiti kila uwezo wa mwanadamu, mambo magumu yote anayopitia na magonjwa yake yote.  Tunasoma katika kifungu hiki kwamba wakati Musa alijibishana na Mungu akisema kwamba yeye alikua anagugumia kwa kuongea kwake, Mungu alimjibu, “Ni, nani aliyeumba kinywa cha mtu?  Ni nani amfanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi?  Aone au awe kipofu?  Je, si mimi mwenyezi Mungu?” (Mstari wa 11).  Kuna mafunzo hapa ambayo watu wengi wanapata ugumu kukubali.  Watu wengi huamini kwamba ikiwa mtu ako na afya njema na anaweza kuona na kuongea, basi mtu huyu amebarikiwa sana na Mungu.  Lakini mwingine akiwa na afya mbaya, awe hawezi kuona au kusikia, ni shetani ambaye amemletea matatizo haya yote.  Wanasema kwamba Mungu anataka kila mtu awe na afya mzuri na lazima awe na uwezo wa kuona na kusikia, lakini shetani anafanya mapenzi ya Mungu yasitimike hata kidogo au ni kwa sababu mtu hana imani ya kutosha.  Lakini mstari huu unatuonyesha kwamba ni Mungu ambaye anafanya haya yawe jinsi yalivyo.  Mungu alimwambia Musa, “Ni, nani aliyeumba kinywa cha mtu?  Ni, nani amfanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi?  Aone au awe kipofu?  Je, si mimi mwenyezi Mungu?”

 

Hili jambo ambalo tunapata mara mingi kuwa si jambo rahisi kuelewa na kuamini.  Je, ni kwa nini Mungu amfanye mtu kuwa kipofu au bubu au kiziwi?  Jibu ambalo tuko nalo ni kwamba Mungu anafanya kila kitu kwa utukufu wake; na kwa njia ambayo hatuwezi kuelewa, mtu ambaye ni kipofu au kiziwi au bubu humletea Mungu utukufu katika hali yake.  Wakati Yesu alikuwa hapa ulimwenguni watu walikuwa wakiamini kwamba, ikiwa mtu ni kipofu au kiziwi au bubu au kiwete, ilikuwa ni kwa sababu yeye au wazazi wake walikuwa wametenda dhambi.  Hii ndiyo sababu wakati tunasoma kitabu cha Yohana 9:1-2, “Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa.  Basi, wanafunzi wakamwuliza, 'Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: mtu huyu, ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?'”  Watu wengi wanaamini hivi leo.  Ikiwa mtu ni kiwete au kiziwi au kipofu au bubu ni kwa sababu ya mambo mabaya ambayo ametenda au wazazi wake.  Wanaamini kwamba Mungu hataki mtu huyu awe katika hali ambayo ako, na kwamba mtu akiwa na imani kubwa Mungu atamponya.  Haya si mafunzo ambayo yanapatikana katika Biblia.  Wakati wanafunzi walimwuliza Yesu swali hili, Yesu aliwajibu, “Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake” (Yohana 9:3).

 

Hii ndiyo mafunzo ya Biblia.  Ni Mungu ambaye anamfanya mtu kuwa kipofu, kiziwi, bubu na kiwete na anafanya hivyo ili kazi yake katika mtu huyu iweze kuonekana.  Inawezekana kwamba mtu ambaye ni bubu ataweza kustahimili majaribu kwa uvumilivu.  Hatuelewi kila jambo kwa hivyo hatuwezi kuelewa ni jinsi gani Mungu anavyofanya kazi katika maisha ya mtu huyu.  Hivi ndivyo Biblia inavyofunza na tunafaa kutii kila funzo katika neno la Mungu.

 

3. Tatu, Mungu akimtuma mtu kufanya kazi fulani anamhitaji afanye kazi hiyo bila kusitasita.  Tunapata katika kifungu hiki kwamba Musa hakuwa tayari kufanya kazi ambayo Mungu alikuwa amempatia.  Musa alitoa sababu ya kwanza kwamba, yeye anaguguia kwa kuongea.  Mungu alimjibu “Ni nani aliyeumba kinywa cha mtu?” (mistari ya 10-11).  Musa baadaye alimwuliza Mungu amtume mtu mwingine (mstari 13).  Lakini Mungu alikuwa ameamua kwamba ni Musa ambaye alikuwa amechagua kufanya kazi hiyo.  Mungu hangeweza kubadilisha mipango yake kwa sababu Musa alikuwa anakataa.  Mungu alikasirika lakini kwa sababu ya neema yake alimwambia Musa kwamba Haruni, ndugu yake, alikuwa aende naye.  Tunapoendelea kusoma kitabu cha Kutoka tunaona kwamba ni Musa ambaye aliyeongea na Farao, na ni yeye ambaye aliwaongoza Waisraeli kutoka Misri.  Hivi ndivyo Mungu anavyofanya kazi yake; anampa mtu vipaji fulani na anamhitaji avitumie kwa ajali ya kazi yake.  Kwa hivyo hawezi kumwacha mtu atoroke kazi ile ambayo amempa.  Mfano mkubwa wa haya ni Yona ambaye aliambiwa aende Ninawi akahubiri huko (Yona 1:1).  Yona hakutaka kufanya kazi hii na alijaribu kutoroka; Mungu alimtuma samaki mkubwa ambaye alimmeza na akamtema baadaye.  Halafu alienda na akafanya kazi ambayo Mungu alikuwa amemwambia afanye (Yona 3:1).

 

Kama Musa na Yona, Mungu amewapatia wakristo wote vipaji na anawahitaji kuvitumia kwa kazi yake.  Kama mtu ako na kipaji cha kufunza watoto katika kanisa, basi ni jukumu lake kuhakikisha kwamba kazi hiyo inafanyika.  Mtu huyu hawezi kusema, “Ninajua kwamba ni jukumu langu kuwafunza watoto kanisani lakini niko na kazi mingi; wacha mtu mwingine afanye kazi hiyo.”  Mungu hatafurahia tabia hii hata kadogo.

 

4. Nne, watu wa Mungu ni wa Mungu peke yake.  Farao aliwafanya watumwa watu wa Mungu na kuwaza kwamba watu hao ni wake.  Musa aliambiwa apeleke ujumbe huu kwa Farao: “Israeli ni mzaliwa wangu wa kwanza wa kiume!”(mstari wa 22).  Wale ambao Mungu ameita katika ufalme wake ni wake; ni watu wake na mali yake.  Hii ndiyo sababu Paulo anasema, “Ninyi si mali yenu penyewe; maana mlinunuliwa wa thamani.  Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu” (1 Wakorintho 6:19-20).  Kwa sababu sisi ni mali ya Mungu, hatuna uhuru wa kufanya yale ambayo tunataka.  Bwana Yesu Kristo ni mwokozi wetu,  Yeye anatuletea msamaha wa dhambi zetu kwa kutuosha kwa damu yake.  Yeye anatuhitaji tumtii kabisa.  Watoto wa Mungu hawana budi kutii kila neno ambalo linapatikana katika Biblia.  Mtu hawezi kusema, “Ninajua kwamba Biblia inaniamuru kufanya hivi, lakini mke au bwana au mchungaji au mwajiri wangu anataka nifanye kinyume na siwezi kukataa kumtii.”  Mke au bwana au mchungaji au mwajiri hana mamlaka juu ya mtu yeyote; mtu huyu ni wa Mungu na neno la Mungu ni lazima walitii.

 

5. Tano, Mungu atawahukumu sana wale wote ambao wanakataa kutii neno lake wakati wamelipokea waziwazi.  Maneno ambayo Musa alikuwa ampelekea Farao yalikuwa haya:  “Nami nakuambia: Mwache mwanangu aondoke, ili anitumikie! Kama ukikataa kumwachia aondoke, tazama nitamwua mzaliwa wako wa kwanza wa kiume” (mstari wa 23).  Katika kitabu cha Kutoka 12:29 tunasoma maneno haya, “Mnamo usiku wa manane, Mwenyezi Mungu aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Misri.  Wote walikufa, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa wanyama nao walikufa.”  Sababu kwa nini mzaliwa wa kwanza wa Farao aliuliwa, ni kwa sababu Farao alikataa kuwaachilia watoto wa Mungu hata baada ya kuamrishwa waziwazi.  Kusikia neno la Mungu ni baraka kubwa sana; lakini pia ni muhimu kujua kwamba baraka hii iko na jukumu ambalo tunafaa kutii kile ambacho tumesikia.  Kuna wengi leo nchini mwetu ambao wanaweza kusoma na wako na Biblia. Hii ni baraka kubwa sana kutoka kwa Mungu.  Lakini tunafaa kukumbuka kwamba kuna jukumu kubwa sana ambalo tumepewa kufanya kwa sababu tumepewa baraka nyingi. Yesu alisema, “Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana.  Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo.  Aliyepewa vingi zaidi atadaiwa vingi zaidi” (Luka 12:47-48). Kuna watu wengi ulimwenguni kote ambao hawajui mapenzi ya Mungu kwa sababu hawana Biblia na hawajawahi kusoma Biblia.  Jambo hili sila ukweli kwetu hapa, kwani sisi tunajua mapenzi ya Mungu kupitia kwa neno lake (Biblia).  Kwa hivyo tusipuuze baraka hizi kwa sababu Mungu atatuhukumu kwa kufanya hivyo.

 

 

Funzo la Sita: Tafadhali soma kitabu cha Kutoka 5:1-6:8

 

Katika kifungu hiki tunasoma mambo matatu ya ukweli kumhusu Mungu.

 

1. Kwanza, Mungu ni wa huruma na ni mwenye neema hata kwa wale ambao hawamjui.  Wakati Musa na Haruni walienda kwa Farao, Farao aliwaambia, “Ni nani huyu Mwenyezi Mungu, hata nikimsikiliza na kuwaacha Waisraeli na waondoke?  Mimi simtambui huyu Mwenyezi Mungu, wala sitawaruhusu Waisraeli waondoke” (mstari wa 2).  Katika agano la Kale Mungu alijitokeza kwa Waisraeli pekee.  Wakati mambo haya katika kitabu cha Kutoka yalitendeka hakuna kitabu chochote cha Biblia kilikuwa kimeandikwa.  Kwa hivyo kuna uwezekano kwamba Farao alikuwa anazungumza ukweli wakati alisema kwamba hakumjua Mungu hata ingawa yeye alikuwa mfalme wa taifa ambalo lilikuwa kuu ulimwenguni.  Kutokana na haya kuna mafundisho mawili ambayo tunafaa kujifunza.

 

Kwanza, tunajifunza kwamba, kwa sababu mtu au taifa liko na mali nyingi haimaanishi kwamba linamjua Mungu.  Ni kawaida nchini mwetu watu kusema kwamba, “Mtu huyu amebarikiwa, ako na kazi mzuri, nyumba mzuri na gari kubwa.  Kweli Mungu amembariki na amefurahishwa naye.”  Biblia inafunza kwamba mtu ambaye hamjui Mungu kabisa kama Farao anaweza kuwa tajiri na mwenye afya njema.  Siyo kwa sababu Mungu amependezwa naye, ni kwa sababu Mungu ni mwenye neema.  Yesu alisema, “Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu” (Mathayo 5:45).  Katika kitabu cha Zaburi 73:3-5;12, tunasoma maneno haya: “Maana niliwaonea wivu wenye kiburi, nilipoona wakosefu wakifanikiwa.  Maana hawa hawapatwi na mateso; miili yao ina afya na wana nguvu.  Taabu za binadamu haziwapati hao; hawapati mateso kama watu wengine.  Hivi ndivyo watu walivyo; wana kila kitu na wanapata mali zaidi.”  Kwa hivyo tusiwaze kwamba wale ambao wako na mali na afya wamependwa na Mungu sana.

 

Pili, tunajifunza kwamba Mungu ni mwenye neema.  Hata kama Farao hakumjua au kumheshimu, Mungu alikuwa akilinda na kulisha Farao na watu wote wa Misri na alifanya nchi yao yote iwe na utajiri mwingi.  Biblia inatuambia kwamba Mungu ni mzuri kwa maadui wake kwa sababu wakati tulikuwa bado wenye dhambi Kristo alikufa kwa ajili yetu (Warumi 5:8).

 

2. Pili, Mungu atasababisha watu wake wapitie hali ngumu sana ili imani yao ijaribiwe na ikue.  Tunasoma katika kifungu hiki kwamba wakati Musa na Haruni walienda kuongea na Farao, Farao hakuwaachilia watu; badala yake alifanya kazi yao ikawa ngumu sana.  Alitoa amri kwamba Waisraeli wasipewe majani bali wao wenyewe wakajitafutie majani na waendelee kutengeneza idadi sawa ya matofali ambayo walikuwa wakitengeneza.  Jinsi tumeona katika mafunzo haya kwamba Mungu ni mwenye nguvu zote na amedhibiti kila kitu mikononi mwake.  Je, ni kwa nini hakumwacha Farao akawaachilie Waisraeli mara moja?  Moja wapo wa sababu kama tulivyoona, ni kwamba alitaka kuonyesha utukufu wake kwa Farao na watu wake wa Waisraeli  Lakini pia kuna sababu nyingine kwa nini alifanya hivi.  Alitaka kuwajaribu na kuimarisha imani ya Waisraeli kwa sababu kulikuwa na majaribu mengi mbele yao jangwani na katika nchi ya Kanani  Walihitaji kuwa na imani dhabiti ndani ya Mungu na majaribu haya yalikuwa kwa ajili ya kusudi hilo.  Hivi ndivyo Mungu anavyofanya na watu wake kila wakati.  Anajua kwamba tunahitaji imani dhabiti ndani yake ikiwa tutaishi maisha ya ukristo hapa ulimwenguni bila kukata tamaa.  Kwa ajili hii mara mingi ataleta majaribu ili imani yetu iwe dhabiti ndani mwake (Yakobo 1:2-4).

 

3. Tatu, tunajifunza kwamba Mungu ni Mungu wa Agano.  Anamwambia Musa, “Tena nilifanya Agano nao kwamba nitawapa nchi ya Kanani ambako waliishi kama wageni” (Kutoka 6:4).  Hili ni jambo la maana ambalo tunafaa kujifunza kutoka kwa Mungu katika Biblia; kwamba Yeye ni Mungu ambaye ako na Agano na watu wake.  Ukweli ni kwamba Mungu hafanyi lolote kando na Agano lake.  Je, Agano ni nini?  Agano ni uhusiano kati ya watu wawili ambao wamejitolea kuwa pamoja.  Katika kitabu cha Hosea Mungu anazungumza kuhusu uhusiano wake na Uisraeli kama ndoa; kwa sababu ndoa ni mfano mzuri wa Agano.  Katika ndoa mwanamke na mwanamume wote wawili wanahapa kuwa waaminifu, kupendana na kujuliana hali kila wakati.  Hivi ndivyo Mungu anaishi nasi kama wanadamu.  Katika kifungu hiki anamwambia Musa kwamba ako na Agano na Ibrahimu, Isaka na Yakobo.  Agano hili linapatikana katika kitabu cha Mwanzo sura 17:1-9.  Katika kifungu hiki Mungu anamwambia Ibrahimu, “Nitalidhibitisha Agano langu nawe, wazawa mwako na vizazi vyao vyote milele; tena nitakuwa Mungu wako na Mungu wa wazawa wako milele” (Mwanzo 17:7).  Hapa Mungu aliingia katika Agano na Ibrahimu na anaahidi kuwa Mungu wa Ibrahimu, akimaanisha kwamba kutosheleza mahitaji ya Ibrahimu na wazawa wake na kuwalinda milele.  Kwa kufanya hayo alimwambia Ibrahimu, “Fuata mwongozo wangu na kuishi bila lawama” (Mwanzo 17:1).  Wakati alikomboa Waisraeli kutoka Misri, alifanya hivyo ili wawe watu wake wa Agano.  Hii ndiyo sababu anasema, “Kwa hiyo, waambie Waisraeli hivi, 'Mimi ni Mwenyezi Mungu! Mimi nitawatoa katika nira mlizowekwa na Wamisri.  Nitawaokoeni utumwani mwenu.  Nitaunyosha mkono wangu wenye nguvu na kuwaadhibu vikali Wamisri na kuwakomboa nyinyi.  Nitawafanyeni kuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.  Nyinyi mtatambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu niliyewatoa katika nira za Wamisri'” (Kutoka 6:6-7).

 

Ni muhimu kwa wakristo wote kuelewa kwamba tuko katika agano na Mungu.  Wakati anatuokoa tunaanza kuwa na uhusiano naye.  Wokovu wetu siyo Mungu anatuokoa kutoka kwa utumwa wa dhambi halafu baadaye anatuacha.  Wakati Mungu anatuokoa anatufungua kutoka kwa minyororo ya dhambi na nguvu za dhambi halafu anatuleta katika jamii yake na kutufanya kuwa watu wake.  Tunakuwa wanawe na anatuonyesha jinsi ya kuishi maisha yetu hapa ulimwenguni.  Hakuna wokovu mahali hakuna uhusiano na Mungu.  Hatuwezi kusema kwamba Kristo ametuokoa kutoka kwa dhambi zetu na sasa tunaweza kuishi jinsi tunavyotaka bila kuzingatia neno lake.  Ametuokoa kwa utukufu wake ili tuweze kuwa kama Yeye mwenyewe.

 

 

Funzo la Saba: Tafadhali soma Kutoka sura ya 7 hadi 10.

 

Katika sura hizi tunamwona Musa mbele ya Farao mara kumi.  Pia katika sura hizi tunasoma kuhusu mapigo tisa ambayo Mungu alituma Misri.  Kabla ya kuendelea na mafundisho haya, hakikisha kwamba unaandika mapigo haya chini ili uweze kufaidika wakati unaposoma.

 

1. Kwanza, wakati Mungu anawaokoa watu wake Yeye hushinda maadui wake kabisa.  Katika sura za kwanza katika kitabu hiki tunasoma kuhusu Farao akiwa mfalme mwenye nguvu na mamlaka kuliko mtu yeyote katika ulimwengu.  Lakini hadithi inapoendelea tunamwona Farao akiwa hana nguvu machoni pa Mungu.  Vile tumeona ukombozi wa Waisraeli ulipangwa ili tuweze kujifunza kuhusu wokovu wetu.  Jinsi tu Waisraeli walivyokuwa watumwa nchini Misri, jinsi hiyo hiyo sisi ni watumwa wa dhambi; jinsi tu Mungu alimtuma Musa kuwaongoza Waisraeli kutoka Misri, hivyo hivyo Mungu alimtuma Kristo Yesu ili atuokoe kutoka kwa utumwa wa dhambi; jinsi tu Musa alivyowaongoza Waisraeli katika jangwa hadi nchi ya Kanani, hivyo hivyo Bwana Yesu anatuongoza katika matatizo na majaribu yetu hapa ulimwenguni hadi mbinguni.  Katika sura hizi tunaona kwamba ili Waisraeli watoke Misri, Musa alihitaji kukabiliana na Farao na Farao alikuwa ashindwe kabisa.  Waisraeli hawakutoroka Misri katikati mwa usiku wakati hakuna mtu yeyote alikuwa akiwaona, walitoka wakishangilia baada ya makabiliano na Farao na kushindwa kwa Farao kabisa ili asiweze kufanya lolote kuwasimamisha kuenda.

 

Katika makabiliano ya Farao na Musa tuko na mfano wa Bwana Yesu Kristo akikabiliana na shetani na ushindi wake dhidi yake na kuwaondoa watu wake kutoka utumwa wa dhambi.  Tukitazama maisha ya Musa tunaona mfano wa Kristo Yesu.

 

(i) Kwanza, tunaona kwamba Farao alijaribu kumwua Musa wakati alizaliwa.  Farao alitoa amri kwamba watoto wote wa kiume Waisraeli watupwe katika mto.  Amri hii haikulenga Musa pekee, lakini alikuwa mmoja wa wale ambao walikuwa watupwe majini; na angekufa iwapo Mungu hangeingilia kati.  Kwa njia hiyo hiyo Herode alitoa amri kwamba watoto wote wa kiume wauliwe katika mji wa Bethlehemu na vitongoji vyake (Mathayo 2:16-18).  Hili lilikuwa jaribio la shetani kukatisha kazi ya Kristo akiwa mdogo.

 

(ii) Pili, mara nne Farao alijaribu kumwongelesha Musa kwamba anaweza kuwaachilia waende lakini warudi.  Katika kutoka 8:25 Farao alimwambia Musa, “Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii.”  Alikuwa tayari kuwaacha Waisraeli wamtolee Mungu dhabihu, lakini hakuwa tayari kuwaachilia waende kabisa.  Katika sura ya 8:28 Farao anasema, “Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mchinjie dhabihu Bwana, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana.”  Katika sura 10:11 Farao anasema, “Sivyo; endeni ninyi mlio watu wazima, mkamtumikie Bwana kwa kuwa ndilo jambo mtakalo.”  Mwisho katika sura ya 10:24 Farao anasema, “Haya, nendeni, mkamtumikie Bwana; kondo zenu na ngombe zenu tu na waachwe; watoto wenu nao na waende pamoja nanyi.”  Kwa ufupi Farao anamwambia Musa, “Nitawaacha mwende mfanye jinsi Mungu wenu anavyotaka, lakini siko tayari kuwaachilia kutoka katika nchi, ni lazima mbaki mkiwa watumwa.”  Kwa njia hiyo hiyo shetani alijaribu pia kumwongelesha Yesu ili asifanye kile Mungu alitaka afanye.  Mfano mwema kabisa ni ule ambao Kristo alikuwa jangwani akifunga siku 40.  Shetani alijua kwamba Yesu alikuwa apewe mamlaka yote na kila kitu kiwe chini yake ulimwenguni kote; kwa hivyo alimwonyesha Yesu Kristo utajiri wa ulimwenguni kote na akasema, “Hivi vyote nitakupa kama ukipiga magoti na kuniabudu” (Mathayo 4:9).

 

(iii) Tatu, vile Farao alivyoshindwa kabisa kabisa, hivyo hivyo Yesu Kristo msalabani alishinda shetani na akamfungia.  Biblia inasema kwamba Yesu alikuwa mwanadamu kamili, “Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao.  Alifanya hivyo ili, kwa njia ya kifo chake, amwangamize ibilisi ambaye ana mamlaka juu ya kifo, na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu ya kifo” (Waebrania 2:14-15).  Biblia inatuambia kwamba kupitia kwa kazi yake msalabani, Bwana Yesu alimshinda shetani ili asiendelee kuwadanganya watu wake (Ufunuo 20:2-3).  Hii ndiyo sababu wakati alifufuka aliwatokea wanafunzi wake akawaambia, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.  Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu” (Mathayo 28:18-19).  Kulikuwa na wakati ambapo shetani alikuwa mwenye nguvu na alikuwa amewadanganya watu wote na kuwaweka katika giza la dhambi (Matendo ya Mitume 14:16).  Lakini wakati Bwana Yesu alikufa msalabani, alipigana na shetani, na akamshinda na akamfunga (Mathayo 12:29).  Mataifa ya ulimwengu ni urithi wake Yesu (Zaburi 2:8), na atawaita watu wake kutoka mataifa haya.

 

2. Pili, tunajifunza jinsi Mungu alivyoufanya moyo wa Farao kuwa mgumu.  Tumeambiwa mara mingi katika kitabu hiki kwamba Farao alikataa kuwaachilia Waisraeli kwa sababu Mungu aliufanya moyo wake kuwa mgumu.  Ilikuwa mpango wa Mungu kwamba Farao akatae neno la Mungu hata wakati neno lilikuwa wazi kwake; hata baada ya kuonyeshwa kwa mapigo kwamba Mungu ni mwenye nguvu.  Farao aliona muujiza baada ya muujiza wakati wa mapigo ambayo yalionyesha kwamba Mungu wa Waisraeli anadhibiti kila jambo mikononi mwake.  Lakini hata baada ya kuona haya, alikataa kuwaachilia Waisraeli waende kwa sababu Mungu alikuwa ameufanya moyo wake kuwa mgumu.  Je, Mungu aliufanya moyo wa Farao kuwa mgumu vipi?  Tunaposoma sura hizi ambazo zinaeleza kuhusu mapigo, tunapata mambo machache kuhusu vipi Mungu alivyofanya jambo hili.

 

(i) Kwanza, Mungu aliwakubali wale waganga wa Farao kufanya miujiza ambayo Musa alifanya. Tunaposoma vifungu hivi tunapata kwamba miujiza tatu ya kwanza ya Musa waganga hawa waliweza kuifanya pia.  Tunasoma kwamba fimbo ya Haruni iligeuka ikawa nyoka, halafu maji ya mto yaligeuka yakawa damu, na vyura vingi vilijaa nchi ya Misri.  Inawezekana kwamba baada ya mapigo haya matatu, Farao angewaachilia Waisraeli waende kwa sababu aliona nguvu za Mungu.  Lakini Mungu hakutaka Farao awaachilie Waisraeli waende wakati huo huo, kwa hivyo Mungu aliwawezesha waganga wa Farao wafanye pia miujiza hii mitatu.  Kwa hivyo Farao alifikiria kwamba Mungu wa Waisraeli hana nguvu kuliko miungu wake na kwa hivyo moyo wake ulikuwa mgumu zaidi.  Hivi ndivyo Mungu aliufanya moyo wake kuwa mgumu.  Biblia inasema kwamba huruhusu maadui wake wabaki katika upotevu (2 Wathesalonike 2:11).

 

(ii) Pili, baada ya muujiza wa nne, waganga wa Farao walimwambia, “Hii ni kazi ya mkono wa Mungu” (Kutoka 8:19).  Lakini sasa moyo wa Farao ulikuwa mgumu sana kusikia.  Hii ni onyo kali sana kwa kila mtu ambaye analisikiza neno la Mungu lakini anakosa kulitii.  Tukifanya mioyo yetu kuwa migumu dhidi ya neno la Mungu, wakati utafika ambapo mioyo yetu itakuwa migumu sana hadi kiwango cha kwamba hatuwezi kulitii tena hata tukiambiwa ukweli waziwazi (Waebrania 10:26-31).

 

(iii) Tatu, wakati pigo la nne lilikuja, Farao alianza kujua kwamba Mungu wa Waisraeli ako na nguvu kuliko yeye na waganga wake.  Lakini bado aliendelea na kusitasita kuwaachilia Waisraeli akiwaambia kwamba wanaweza kumtolea dhabihu Mungu wao mahali popote katika nchi ya Misri.  Labda alijiwazia kwamba lingemfurahisha Mungu.  Tunaona jambo hili pia wakati Farao anasema kwamba Waisraeli wanaweza kuenda kumtolea dhabihu Mungu wao lakini siyo mahali mbali sana; halafu pia wakati anasema kwamba wanaume peke yao waende, na baadaye wakati anasema wanyama wabaki nyuma.  Mambo haya yote yanaonyesha kwamba Farao hakuwa tayari kuwaachilia Waisraeli.  Mambo haya yalikuwa ya kuonyesha kwamba alijaribu kukubaliana na mapenzi ya Mungu.  Hii ni hali ya mtu ambaye amefanya moyo wake kuwa mgumu dhidi ya Mungu; atafanya haya yote akijidanganya kwamba amefanya yale yote Mungu alitaka afanye.

 

Ni jambo la kutilia manani kwamba hata kama Mungu aliufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, haimaanishi kwamba Farao hakufaa kuajibika.  Hawezi kusema kwamba, “Siyo makosa yangu moyo wangu kuwa mgumu, ni Mungu aliyeufanya uwe mgumu.”  Hata kama yeye ni chombo mikononi mwa Mungu, bado anafaa kuajibika machoni pa Mungu kwa ajili ya dhambi zake.  Hii ndiyo sababu katika vifungu hivi mara mingi jukumu limepewa Farao.  Tunaambiwa pia kwamba ni Farao ambaye aliufanya moyo wake kuwa mgumu.

 

3. Tatu, Mungu huwalinda watu wake wakati wako katika majaribu makali.  Tunaambiwa kwamba pigo la ng'ombe kufa, mvua ya mawe, na pigo la giza, haya yote hayakuwafikia Waisraeli.  Mapigo haya yalikuwa yamelenga Wamisri, watu wa Mungu walindwa kutokana na mapigo haya.  Mungu huwa hatulindi kotokana na kila jaribu au matatizo.  Si ukweli kusema kwamba wakati tunaokoka tunakuwa huru kutoka kwa matatizo yote.  Waisraeli baada ya kutoka Misri walikumbana na matatizo mengi jangwani.  Lakini kifungu hiki kinatuonyesha kwamba katika matatizo Mungu bado hutulinda.

 

 

 

 

Funzo la Nane: Tafadhali soma kitabu cha Kutoka sura ya 11 hadi 14

 

Sura hizi katika kitabu cha Kutoka zinafafanua hukumu ya Mungu juu wa Wamisri na ukombozi wa Waisraeli kutoka Misri.  Tunafunzwa mafunzo matatu muhimu sana.

 

1. Kwanza, tunajifunza kwamba Mungu ni mtakatifu.  Katika sura hizi tunasoma jinsi Mungu mwenyewe alishuka Misri.  Alisema kwamba, “Usiku wa manane nitapita ndani ya Misri” (Kutoka 11:4).  Kusudi lake lilikuwa awahukumu Wamisri kwa sababu ya kuabudu sanamu.  “Usiku huo, nitapita nchi ya Misri na kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Misri, watu kwa wanyama.  Nitaadhibu miungu yote ya Misri.  Mimi ndimi Mwenyezi Mungu” (Kutoka 12:12).  Ni muhimu sana kuelewa kwamba sababu ya Mungu kupita katika nchi ya Misri usiku huo na kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Wamisri si kwa sababu alitaka amlazimishe Farao awaachilie Waisraeli au kwa sababu alitaka kumwonyesha Farao kwamba alikuwa na nguvu mingi; ilikuwa kwa sababu Mungu ni Mtakatifu na mwenye haki, yaani ndani mwake hamna dhambi yoyote.  Wamisri walikuwa wakiabudu sanamu na jambo hili machoni pa Mungu ni dhambi mbaya sana.  Kwa hivyo Mungu alipita katika nchi ya Misri usiku ili awahukumu Wamisri kwa sababu ya dhambi zao.

 

Utakatifu wa Mungu ni jambo ambalo wengi wetu hatutaki kuwaza juu yake.  Tunajua kwamba tumetenda dhambi dhidi ya Mungu na sisi ni wenye hatia mbele yake.  Kwa hivyo jambo hili la Mungu kuwa Mtakatifu na mwenye haki linatuogopesha sana; na ukweli ni kwamba hatuwezi kuepuka jambo hili.  Hatuwezi kusema kwamba dhambi zetu hazijalishi au Mungu atazipuuza.  Hadi tutakapo kubali kwamba sisi ni wenye dhambi na Mungu ni mtakatifu, hatuwezi kamwe kuokoka.  Tutakapokubali hali yetu ndipo tutakuja kwa Yesu naye atatuokoa.

 

2. Pili, tunajifunza kwamba Mungu amejawa na huruma na neema.  Tunasoma kwamba usiku huo wakati Mungu alipita nchini Misri ni wazaliwa kwanza wa Wamisri ndiyo walikufa tu.  Wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli hawakuguzwa.  Sababu ya jambo hili siyo kwa sababu Waisraeli walikuwa watakatifu.  Biblia inasema wazi kwamba wakati Waisraeli walikuwa Misri walianguka katika dhambi mbaya sana ya kuabudu sanamu na walikuwa na hatia ya kuabudu sanamu kama tu Wamisri.  Miaka mingi baadaye nabii Ezekieli anaeleza jinsi mambo ilivyokuwa Misri wakati Mungu alipojionyesha kwa Waisraeli.  “Siku hiyo niliwaapia kwamba nitawatoa nchini Misri na kuwaongoza mpaka kwenye nchi niliyowashghulia, nchi inayotiririka maziwa na asali na nchi nzuri kuliko nchi zote.  Niliwaambia: 'Tupilieni mbali machukizo yote mnayoyapenda, msijitie najisi kwa sanamu za miungu ya Misri, kwa maana mimi ni mwenyezi Mungu, Mungu wenu” (Ezekieli 20:6-7).

 

Hii ni sababu Yoshua aliwaambia,  “Acheni kabisa miungu ile ambayo wazee wenu waliabudu ng'ambo ya mto Eufrate na nchini Misri.  Mtumikieni Mwenyezi Mungu” (Yoshua 24:14).  Sababu kwa nini wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli hawakuuliwa siku ile Mungu alipita katika nchi ya Misri na kuwahukumu Wamisri siyo kwa sababu Waisraeli walikuwa watakatifu, bali ni kwa sababu Mungu ni mwenye neema na huruma kwa wale ambao amewachagua.  Hii ndiyo sababu aliwapatia Waisraeli maagizo ambayo walifaa wafuate kikamilifu.  “Chagueni kila mmoja wenu, kulingana na jamii yake, mwanakondoo na kumchinja kwa siku kuu ya pasaka.  Mtachukua majani ya husopo na kuyachovya katika damu ndani ya birika na kupaka vingitini na miimo yote miwili ya milango ya nyumba zenu.  Mtu yeyote asitoke nje ya nyumba usiku huo hadi asubuhi.  Maana mimi Mwenyezi Mungu nitapita kuwaua Wamisri.  Lakini nitakapoona damu iliyopakwa kwenye vingiti na miimo ya nyumba zenu, nitazipita na wala sitamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwaua” (Kutoka 12:21-23).

 

Kwa neema na huruma wake Mungu alitengeza njia kwa Waisraeli ili wasihukumiwe kwa sababu ya dhambi zao: walikuwa wamuue mwanakondoo wa pasaka na wapake damu yake kwa miima ya milango yao.  Jambo hili lilifanywa kwa ajili ya kuwaanda watu wa Mungu kwa siku yenyewe ya Mwanakondoo wa pasaka ambaye ni Kristo Yesu.  Hadithi yote katika kitabu cha Kutoka imeandikwa kwa ajili ya kutuonyesha kwamba Mungu ni nani na jinsi anatuokoa kutoka kwa dhambi zetu.  Hapa tunaona kwamba sisi ambao tumeokoka hatukuwa bora kuliko wale ambao hawajaokoka.  Waisraeli na Wamisri walikuwa wote wakiabudu masanamu.  Lakini Waisraeli walikuwa watu ambao wamechaguliwa na Mungu na kwa hivyo aliwatengenezea njia ya kuepuka hukumu.  Kwa njia hiyo hiyo wale wote ambao wameokoka tumechaguliwa na Mungu.  Alituchagua ili tuokoke kabla ya kuumba chochote ambacho kimeumbwa (Waefeso 1:4; 2 Wathesalonike 2:13), na kwa njia hiyo alitutengezea njia ya kuepuka hukumu kupitia kwa Kristo Yesu ambaye ni Mwanakondoo wa Pasaka: “Maana, Kristo, pasaka yetu amekuisha tolewa kuwa sadaka” (1 Wakorintho 5:7).

 

3. Tatu, Mungu anaokoa watu wake kwa njia ya miujiza.  Kitabu cha Kutoka ni moja wapo wa vitabu vya Biblia ambavyo viko na miujiza mingi katika Biblia.  Tunapotazama miujiza yote katika kitabu cha Kutoka tunaona kwamba yote ilikuwa kwa ajili ya kuwakomboa Waisraeli kutoka Misri. Kwanza kuna miujiza ambayo Musa na Haruni walifanya ili kuwashawishi wazee wa Waisraeli kwamba walikuwa wametumwa na Mungu (Kutoka 4:1-7; 4:29-31).  Pia kuna miujiza ambayo Musa na Haruni walifanya mbele ya Farao na waganga wake (Kutoka 7:8-13).  Halafu kulikuwa na mapigo kumi (Kutoka 8:14-11:10).  Pia kulikuwa na muujiza wa kutenganisha bahari ya Shamu (Kutoka 14:21-22).  Halafu kulikuwa na muujiza wa upeanaji wa maji na chakula katika jangwa.  Baadaye, kulikuwa na muujiza wa kushinda Wameleki (Kutoka sura ya 16 na 17).  Miujiza hii yote ilikuwa iwaonyeshe Waisraeli kwamba kukombolewa kwao kutoka kwa utumwa kule Misri ilikuwa kazi ya ajabu ya Mungu.  Mambo haya yote yanatufunza kwamba ukombozi wetu kutoka kwa dhambi zetu ni kazi ya ajabu na miujiza ya Mungu.  Ni jambo la kuhuzunisha kwamba watu leo hawaelewi wokovu ni nini.  Mtu anajiwazia kwamba, “Nitaokoka” akimaanisha kwamba “Nitaacha dhambi zangu fulani na nitaanza kuishi maisha mazuri ya kwenda kanisani.”  Huyu ni mtu ambaye anafanya mabadiliko machache hapa na pale maishani mwake.  Mtu huyu hajaokoka na hataingia mbinguni kwa sababu ya mabadiliko yake.

 

Wokovu siyo kazi ya mwanadamu, bali ni kazi ya Mungu; “Wokovu ni wa Bwana Mungu” (Yona 2:9), na ni kazi ya miujiza ya Mungu.  Kabla mtu aokoke yeye amekufa katika dhambi (Waefeso 2:1).  Kwa hivyo kazi ya kwanza ya muujiza wa Mungu ni kumfanya awe hai kiroho.  Jambo hili Mungu anafanya kwa njia ya Roho Mtakatifu (Yohana 3:8).  Mtu ambaye hajaokoka amejawa na dhambi na ni adui wa Mungu.  Mungu anafanya kazi nyingine ya muujiza kwa kumleta kwa Kristo akitubu dhambi zake kwa imani.  Mtu huyu anaokolewa na kufanywa mwana wa Mungu.  Hata baada ya haya yote mtu huyu bado ako na dhambi ndani mwake na dhambi hizo zinahitaji kuondolewa.  Kwa hivyo Mungu anaendelea na kazi yake ya miujiza ya kumbadilisha mtu huyo kutoka ndani mwake.  Mungu anafanya kazi ndani ya mtu huyu ili mtu huyu aweze kufanya yale ambayo Mungu mwenyewe anataka afanye (Wafilipi 2:13).  Kwa hivyo wokovu ni kazi ya miujiza ya Mungu.  Wokovu siyo matamshi ya mwanadamu au kujaribu kwa mtu au kurudia maombi fulani ambayo inaonekana kama inamfurahisha Mungu.  Wokovu ni kazi ya Mungu pekee yake; kazi yetu wanadamu ni kuhubiri ukweli ambao unapatikana katika neno la Mungu.

 

 

 

Funzo la Tisa, Tafadhali soma kitabu cha Kutoka sura ya 15 hadi 18

 

Katika sura hizi kwanza tunasoma kuhusu wimbo wa Musa na Miriamu baada ya kukombolewa kwa Waisraeli kutoka kwa utumwa katika nchi ya Misri (sura ya 15).  Halafu tunasoma kuhusu Waisraeli wakiwa mlimani Sinai.  Kuna mafundisho muhimu manne katika sura hizi.

 

1. Kwanza, Mungu anafanya kila kitu ili viumbe vyake vyote vikamsifu.  Katika sura ya 15 tunasoma kwamba baada ya Waisraeli kuvuka bahari ya Shamu, waliimba wimbo wa kumsifu Mungu kwa sababu ya kuwakomboa na kuaangamiza Wamisri.  Wimbo huu ni muhimu sana katika kitabu hiki kwa sababu ni wimbo wa kumsifu Mungu.  Kiini cha wimbo ni sifa kwa Mungu kwa sababu kazi yake ajabu ya kuwakomboa Waisraeli.  Sababu ya Mungu ya kumwokoa mtu yeyote ni aweze kupata sifa na kutukuzwa.  Hili ni jambo ambalo tunafaa kutilia maanani sana.  Mtu anapookoka anapata baraka nyingi kutoka kwa Mungu, na mara mingi mtu huyu huwaza kwamba sababu Mungu alimwokoa ni aweze kumbariki.  Lakini jambo hili siyo la ukweli.  Hata kama tunapata baraka nyingi kutoka kwa Mungu wakati tumeokoka, sababu kubwa kwa nini Mungu hutuokoa ni apate kusifiwa na kutukuzwa.  Katika kitabu cha Waefeso 1:3-14 tunasoma kuhusu kazi kubwa ya wokovu.  Katika ujumbe huu Paulo anatueleza jinsi Mungu alivyotuchagua kabla ya kuumbwa kwa ulimwenguni (Waefeso 1:4), jinsi Kristo alivyotuokoa kwa damu yake (Waefeso 1:7), na jinsi Roho Mtakatifu anatulinda hadi siku ya kurudi kwake Yesu (Waefeso 1:14).  Tunapoangalia kifungu hiki kwa makini, tunaona kwamba kuna maneno ambayo imerudiwa: “Tuusifu utukufu wake” (Waefeso 1:6,12,14).  Hapa kile Paulo anatuambia ni kwamba Mungu Baba alituteua ili apate utukufu wote, Bwana Yesu alituokoa kwa damu yake ili Mungu aweze kupata utukufu na Roho Mtakatifu anakuja na kuishi ndani mwetu ili Mungu aweze kupata utukufu wote.  Sababu kuu ya wokovu wetu ni Mungu apate utukufu wote.  Mungu alipanga wokovu wetu kwa makini sana ili mtu ambaye ameokoka asije akajisifu (Warumi 3:27; Waefeso 2:8-9).  Mtu ambaye anajisifu jinsi alivyookoka mtu huyu hajaelewa wokovu wake kabisa.  Sababu kuu Mungu anatuokoa ni tuweze kumpa utukufu wote bali siyo tusijisifu kwa yale tumefanya.

 

2. Pili, Mungu ndiye anayewalinda na kuwalisha watu wake maishani mwao mwote. Tunasoma katika kifungu hiki kwamba baada ya Waisraeli kuvuka bahari ya Shamu, waliingia katika jangwa (Kutoka 15:22).  Wakati huu wote Mungu aliwalisha na kuwanywesha.  Pia wakati huu walivamiwa na Wameleki, na Mungu aliwaokoa kwa kujibu maombi ya Musa (Kutoka 17:8-15).  Wakati ambao Waisraeli walikuwa jangwani, ni kama maisha yetu wakristo hapa ulimwenguni.  Kama Waisraeli, sisi tumekombolewa kutoka kwa utumwa, kama wao tuko njiani kuenda katika nchi ya ahadi, na pia kama wao tuko na safari ndefu ambayo inahitaji ujasiri kabla tufike huko.  Kwa hivyo maisha ya Waisraeli katika jangwa ni maisha ya kutuhimiza sisi.  Kuna mambo matatu ambayo tunafaa kujifunza kutokana na mambo haya.

 

(i) Mungu alitosheleza mahitaji yao yote.  Aliwapatia chakula chao cha kila siku na kuwalinda kutokana na maadui wao.  Kwa hiyo hiyo Mungu ameahidi kutulinda na kutosheleza mahitaji yetu tunavyoendelea kuishi maisha ya ukristo hapa ulimwenguni.

 

(ii) Mungu aliwahitaji wajitahidi.  Kwa mfano tunasoma kwamba wakati walivamiwa na Wamelaki, walihitajika kupigana.  Hawakufaa kukaa tu na kungoja kuona jinsi Mungu anayowapigania na kuaangamiza maadui wao.  Walihitajika kupigana.  Kwa njia hiyo hiyo Mungu anatuhitaji tujitahidi katika ukristo wetu kila siku.  Tunafaa kufanya kazi ili tupate chakula badala ya kuwategemea wengine.  Tunafaa kutumia vipawa vyetu katika kanisa la Mungu badala ya kungoja mchungaji afanye kila kitu.  Pia tunafaa kutoroka dhambi na tuishi maisha ya utakatifu. Haya ni majukumu ambayo tumepewa tuifanye na hatufai kuipuuza hata kidogo.

 

(iii) Mungu aliwahitaji wawe na imani ndani yake kwa maisha yao ya kila siku.  Kitabu cha Waebrania kinazungumza kuhusu watu ambao walitoka Misri na Musa kwamba walikosa imani. “Maana habari njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale.  Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani” (Waebrania 4:2).  Bila imani hatuwezi kuokolewa na bila imani hatuwezi kuishi maisha ya ukristo.  Tukikosa imani, kama wengi wa Waisraeli jangwani tutaangamia bila kufika nchi ya ahadi.

 

3. Tatu, Mungu ni mwenye huruma na mvumilivu kwa watu wake wakati wako wadhaifu katika imani yao.  Tumeona kwamba Mungu anataka watu wake watembee naye kwa imani.  Lakini anajua kwamba mara mingi imani yetu ni dhaifu na kwamba tunakumbwa na mashaka.  Katika sura hizi ambazo tunasoma tunaona kwamba mara mingi Waisraeli walilalamika kwa Musa na Mungu.  Tunasoma mistari kama hii; “Basi, watu wote wakalalamikia Musa wakisema, 'Sasa tutakunywa nini?'  Jangwani Waisraeli wote waliwalalamikia Musa na Haruni.  Waisraeli waliwaambia, 'Laiti Mwenyezi Mungu angetuua tulipokuwa nchini Misri ambako tulikaa, tukala nyama na mikate hata tukashiba.  Lakini nyinyi mmetuleta huku jangwani kuiua jumuiya hii yote kwa njaa!'; Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?” (Kutoka 15:24; 16:3; 17:3).

 

Waisraeli hawakulalamika tu dhidi ya Musa na Mungu, pia walikosa kutii neno la Mungu.  Katika sura ya 16 tunaambiwa kwamba Mungu aliwapa mkate kutoka mbinguni na maagizo kwamba mtu yeyote hakufaa kuuweka mkate huo hadi siku ambayo ilifuata kwa sababu hata siku iliyofuata Mungu bado angewapa mkate.  Lakini tunasoma kwamba, “Watu hamkumsikia Musa.  Baadhi yao walijibakizia chakula mpaka asubuhi.  Lakini asubuhi chakula hicho kikawa kimeoza na kuwa na mabuu” (Kutoka 16:20).  Pia walipewa maagizo kwamba siku ya Sabato hawafai kwenda na kukusanya mkate kwani ule ambao walikuwa wamekusanya jana yake ulikuwa uwe wa siku mbili.  Lakini hata baada ya haya, “Mnamo siku ya saba watu kadhaa walitoka kwenda kutafuta chakula, lakini hawakukipata” (Kutoka 16:27).  Walimjaribu Mungu kwa malalamishi yao na kutotii kwao; lakini Mungu hakuwaangamiza.  Alikuwa mvumilivu kwao na aliendelea kuwatosheleza kwa neema yake.  Biblia inasema kwamba kulalamika na kutotii Mungu ni dhambi na ni lazima tuhakikishe kwamba hatuzifanyi.

4. Nne, Mungu huwapatia watu wake viongozi.  Katika sura ya 18, tunasoma kumhusu baba mkwe wa Musa ambaye alimtembelea.  Alipoona Musa peke yake akiwa kiongozi wa watu hawa wote, Yethro alisema, “Unavyofanya si vizuri!  Chagua miongoni mwa watu wote, watu wanaostahili, watu wanaomcha Mungu, waaminifu na wanaochukia kuhongwa.  Wape mamlaka, wawe na jukumu la kuwasimamia watu katika makundi ya watu elfu, mia, hamsini na kumikumi” (Kutoka 18:17,21).  Musa alijua kwamba huu ulikuwa ushauri wa maana sana na kwa hivyo alifanya jinsi alivyoambiwa.  Aliwachagua watu wengine ambao walimsaidia katika kazi yake.

 

Huu ni mfano mwema wa kufuatwa leo na watu wote wa Mungu.  Mara mini wachungaji wanaweza kuwaza kwamba ni hao tu ambao wanaweza kuwatumikia watu wa Mungu na pia kwamba ni hao tu ambao wako na vipaji na uwezo wa kuhubiri na kufunza neno la Mungu.  Jambo hili si la ukweli.  Ukweli ni kwamba ni jambo la hatari sana mtu mmoja kwa kiongozi wa kanisa kwa sababu mtu huyu hataajibika kwa yeyote kuhusu jinsi anavyofanya kazi.  Jambo la kuhuzunisha ni kwamba kuna wachungaji wengi wa aina hii na wametumia mamlaka yao kujifaidisha.  Ni wazi wakati tunasoma Biblia kwamba kanisa linafaa kuwa na wachungaji kadhaa ambao wanawalisha kondoo wa Mungu neno la Mungu, bali siyo mchungaji mmoja ambaye hana mtu wakuajibika kwake.  Paulo na Barnaba waliwachagua wachungaji bali siyo mchungaji kwa kila kanisa ambalo walipanda wakati wa safari yao ya kwanza wakihubiri (Matendo ya Mitume 14:23).  Kitabu cha Matendo ya Mitume sura 20:17 tunasoma kwamba kanisa la Waefeso lilikuwa na wachungaji bali siyo mchungaji, na walikuwa wachunge katika kanisa hili (Matendo ya Mitume 20:28).  1 Petro 5:1-4, Petro anaandikia wachungaji bali siyo mchungaji mmoja.  Katika kila kifungu hapa ni waziwazi kwamba kila kanisa litawachagua wazee kulingana na 1 Timotheo 3:1-7, na hawa wazee wote watakuwa wachungaji wa kanisa.  Hakuna mahali popote katika Agano Jipya ambapo tunafunzwa kwamba kanisa litakuwa na wazee na mchungaji, na huyu mchungaji atakuwa na mamlaka juu ya wazee.

 

 

Funzo la Kumi; Tafadhali soma kitabu cha Kutoka sura za 19 na 20.

 

Hili ndilo funzo la mwisho katika kijitabu hiki.

 

1. Kwanza, Mungu aliingia katika Agano na watu Waisraeli.  Agano ni uhusiano ambao watu wawili wako na jukumu la kufanya.  Hapa tunaona Mungu mara ya kwanza akiingia katika Agano na taifa la Uisraeli.  Hadi wakati huu Agano lake lilikuwa kati yake na Ibrahimu, Isaka na Yakubu. Alimwambia Musa awaambie watu wa taifa la Uisraeli, “Sasa basi, kama mkitii sauti yangu na kulishika Agano langu, mtakuwa watu wangu wateule kati ya mataifa yote, maana dunia yote ni yangu.  Mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.  Hayo ndiyo maneno utakayowaambia Waisraeli” (Kutoka 19:5-6).  Tunaona hapa Agano hili kati ya Waisraeli na Mungu linamaanisha nini.  Uisraeli itakuwa taifa teule takatifu, watu watakuwa watu wake.  Mungu ndiye mwenye dunia na kila kitu kiko mikononi mwake na anakidhibiti, lakini alilichagua Uisraeli kama taifa lake.  Atawapenda Waisraeli, atawajali, atawalisha na kuwalinda.  Kwa upande wa Waisraeli walikuwa wanahitajika kumtii Mungu kabisa na kutembea kwa uaminifu.  Kwa maneno haya uhusiano kati ya Mungu na Waisraeli ulikuwa umefanyika.  Jambo hili lilikuwa kama ndoa.

 

Kwa ndoa watu wawili wakisha hapa kuwa bibi na bwana; mambo mawili yanatendeka.

 

(i) Watu hawa wawili wanaanza kuishi pamoja.

 

(ii) Watu hawa wawili wanaamua juu ya sheria ambayo itawasaidia kuishi pamoja.  Watu hawa hawawezi tena kuishi kama walivyokuwa wakiishi wakiwa peke yao.  Sasa wameoana na wako na jukumu kwa kila mmoja wao.  Sasa ni lazima waamue ni jinsi gani wataishi; wapi wataishi, nani ataishi nao, kama watahitaji mfanyakazi na ni pesa ngapi wanafaa kumlipa, ni wakati gani wanafaa kula chakula cha mchana au cha usiku, ni chakula cha aina gani wanafaa wale, nini watakuwa wakifanya kila Jumamosi, kanisa gani wanafaa kuwa wakienda, watoto wangapi watakuwa nao na mambo mengine.  Sababu kubwa sana kwa nini ndoa inakumbwa na matatizo mapema ni kwa sababu wale ambao wameoana hawajazungumza kuhusu mambo haya.  Unakuta kwamba mke anahitaji mumewe awe nyumbani kila jioni naye, lakini unakuta kwamba mumewe yeye wakati huo ako na marafiki wake wakitazama mpira au wakizungumza.

 

Baada ya Agano kati ya Mungu na Uisraeli kutengenezwa, mambo haya mawili yalijadiliwa.  Kwanza kabisa Mungu alisema atafanya jambo ambalo hajawahi kufanya; alisema kwamba atakuja na aishi miongoni wao.  Hii ndiyo sababu katika sura zingine za kitabu hiki cha Kutoka, Waisraeli walipewa maagizo ya kujenga hema.  Katika hema hii kulikuwa na mahali ambapo palikuwa patakatifu pa watakatifu.  Mahali hapa palikuwa mahali ambapo uwepo wa Mungu ulikuwa.

 

Pili, baada ya Agano kutengenezwa Mungu aliwapatia Waisraeli Sheria.  Tunapotazama Sheria takatifu ya Mungu katika Agano la Kale, ni wazi kwamba kuna kanuni ya aina mbili ambazo walihitajika kufanya.

 

(i) Kuna sheria ambazo zilipeanwa kwa ajili ya kuwaongoza Waisraeli; kwa mfano kama Sheria Kumi za Mungu.

 

(ii). Kuna sheria ambazo zilipeanwa ili zirejeshe uhusiano kati ya Mungu na Waisraeli wakati Waisraeli walianguka katika dhambi; kwa mfano sadaka ambazo walikuwa wakipeana katika kitabu cha Walawi.  Sheria hii ya kutoa sadaka ilipeanwa kwa sababu Mungu alielewa moyo wa mwanadamu na pia alijua kwamba Waisraeli wangekosa kutimiza mambo haya.  Kwa hivyo kulihitajika kuwa na njia ambayo ingewawezesha Waisraeli kuoshwa dhambi zao na kuletwa tena katika uhusiano mwema na Mungu.

 

Katika Agano Jipya Mungu mwenyewe amekuja kuishi miongoni mwa watu wake lakini mara hii kwa njia tofauti.  Bwana Yesu mwenyewe ambaye ni Mungu kamili alikuja na kuishi hapa ulimwenguni kwa miaka kama 30 miongoni mwa watu.  Baadaye wakati alipopaa mbinguni alimtuma Mungu Roho Mtakatifu ambaye leo anaishi ndani na miongoni mwa watu wake.  Hii ndiyo sababu Agano Jipya halisisitizi kuhusu mijengo.  Yesu alimwambia mwanamke msamaria, “Niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wale kule Yerusalemu....lakini wakati waja, tena umekwisha wasili, ambapo wenye kuabudu wa ukweli watamwabudu Baba katika roho na ukweli.  Maana Baba anawataka watu wanaomwabudu namna hiyo” (Yohana 4:21,23).

 

2. Pili, tunaona kwamba Mungu aliwapatia watu wake Sheria Kumi.  Katika kitabu cha Kutoka sura ya 20, tunasoma kuhusu Sheria Kumi zikipeanwa mara ya kwanza; na mara ya pili zilipeanwa katika sura ya 5 ya kitabu cha Kumbukumbu la Torati.  Kuna sababu tatu muhimu kwa nini Mungu alipeana sheria.

 

(i) Sababu ya kwanza ni sheria inatuonyesha utakatifu wa Mungu.  Biblia inatueleza kwamba Mungu ni mtakatifu na tunapotazama Sheria ya Mungu tunaona utakatifu wake.  Tunaona kwamba utakatifu wa Mungu unagusia kila sehemu ya maisha: uhusiano wetu naye na uhusiano wetu na wanadamu wengine.  Katika mafunzo ya Kristo katika kitabu cha Mathayo sura ya 5 hadi 7 anasema kwamba Sheria ya Mungu inahusu hata yale ambayo yanatendeka katika mioyo yetu na mawazo yetu, hata mawazo yetu mabaya yanahukumiwa.  Mungu anashughulika na kila sehemu ya maisha yetu.  Yeye siyo kama mwajiri ambaye anashughulika tu na wafanyakazi wake wakati wamekuja afisini kwa wakati ufaao na wako na tabia mzuri.  Mungu anashughulikia kila jambo ambalo linaendelea maishani mwetu.  Sheria hizi pia zinaonyesha kwamba utakatifu wa Mungu haupunguki wakati wowote.  Mungu anatarajia tuwe watakatifu kila wakati.  Hasemi kwamba, “Mjaribu sana kuishi maisha ya utakatifu, na mkifanya makosa hapa na pale haijalishi sana.”  Bali anasema, “Ninatarajia muwe watakatifu kila wakati na msipungukiwe na utakatifu.  Mkipungikiwa na utakatifu basi nyinyi ni wenye dhambi.”

 

(ii) Sababu ya pili kwa nini Mungu alipeana Sheria yake ni kuonyesha dhambi za mwanadamu. Sisi sote tunapenda kujiwazia vizuri na tunapenda kusema, “Mimi siyo mtu mbaya sana.  Ninajua kwamba mimi sijakamilika, lakini pia mimi siyo mtenda dhambi mbaya sana.”  Lakini Sheria ilipeanwa ili tujue kwamba sisi ni watenda dhambi wabaya sana.  Ilipeanwa ili kutuonyesha kwamba tumepungikiwa na utukufu wa Mungu.  “Kazi ya sheria ni kumwonyesha mtu kwamba ametenda dhambi” (Warumi 3:20).

 

(iii) Sababu ya tatu kwa nini sheria ilipeanwa ni kutuongoza kwa Kristo Yesu.  Paulo anasema, “Basi, hiyo sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya amani tufanywe waadilifu mbele yake Mungu” (Wagalatia 3:24).  Kuna watu wengi ambao wanafikiria kwamba sheria ya Mungu ilipeanwa ili ituwezeshe kuenda mbinguni. Wanajiwazia kwamba wakijaribu kuzishika Sheria Kumi za Mungu, Mungu ataona kwamba wamejaribu sana na atawaruhusu waingie mbinguni.  Sheria haikupeanwa ili ituokoe.  Sheria ilipeanwa ili ituonyeshe kwamba hatuwezi kujiokoa.  Ilipeanwa kutuonyesha jinsi tulivyoanguka katika dhambi sana na kupungukiwa na utukufu wa Mungu na kwamba juhudi zetu wenyewe haziwezi kutuokoa.  Ilipeanwa kutuonyesha hitaji letu la mwokozi ambaye ni Kristo Yesu aliyetumwa na Mungu.  Kwa hivyo sheria ni kama kwenda hospitalini na kutolewa damu ili daktari aweze kukudhibitishia nini unaugua.  Uchunguzi ambao unafanywa hauwezi kukupa afya bora.  Huwezi kusema kwamba, “Nimefanyiwa uchunguzi kwa hivyo nitaishi muda mrefu.”  Kusudi la uchunguzi huo ilikuwa ni kukudhibitishia ni ugonjwa gani uko nao na uweze kwenda kwa matibabu.  Kusudi la sheria siyo kuleta wokovu, bali ni kutuonyesha kwamba sisi ni watenda dhambi wabaya sana.  Sheria inatuonyesha kwamba tuko na ugonjwa mbaya sana ambao unatupeleka jehanum milele.  Sheria imewekwa ili ituongoze kwa Kristo Yesu ambaye ndiye mwokozi wa nafsi zetu; Kristo Yesu atatusamehe wakati tunaenda kwake kwa imani na kumwomba msamaha wa dhambi zetu.  Hizi ndizo sababu kuu kwa nini sheria ilipeanwa.

 

 

 

 

Mafunzo machache kuhusu Utatu wa Mungu.

 

Kama vile tumeona katika kitabu cha Kutoka, tunasoma mengi kumhusu Mungu kwa sababu Mungu anajionyesha kwetu katika kitabu hiki cha Kutoka.  Mambo mengi ambayo tunafaa kujua kuhusu Mungu yanapatikana katika kitabu hiki.  Kuna jambo fulani kuhusu Mungu ambalo halipatikani katika kitabu hiki cha Kutoka, na jambo hilo ni Utatu wa Mungu.  Katika mafunzo haya machache tutajifunza jambo hili.

 

1. Mafunzo machache kuhusu Utatu wa Mungu.

 

Mafunzo ya Utatu wa Mungu yanaweza kuelezwa hivi kwa ufupi:

 

“Mungu anaishi milele kwa Utatu, yaani, Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu.  Kila Mmoja wao ni Mungu kamili ambaye amekuwepo na ataendelea kuishi milele na kuna Mungu Mmoja.”

 

Kwa akili zetu ndogo sisi wanadamu tunapata kwamba jambo hili la Utatu wa Mungu si jambo rahisi kuelewa.  Je, inawezekanaje kwamba kuna Watatu ambao kila Mmoja ni Mungu kamili na anaishi milele na kuna Mungu Mmoja?  Hili swali ambalo limewachanganya wakristo wengi kwa muda mrefu na ni moja wapo ya mambo ambayo walimu wa uongo watatumia kuwapinga wakristo.  Kwa mfano wale walimu wa uongo wanasema kwamba tunaabudu Mungu watatu.  Lakini jambo hili siyo la ukweli.  Tunamwabudu Mungu Mmoja ambaye anaishi kwa Utatu.  Hatuwezi kuelewa jambo hili kabisa lakini hatuwezi pia kulikataa; kwani Mungu ni Mungu na sisi ni wanadamu tu, kwa hivyo siyo jambo la kushangaza kwamba hatumwelewi Mungu kabisa.  Pia tukiabudu mungu na kumtumikia mungu ambaye tunaelewa kabisa, basi kuna uwezekano kwamba tunamwabudu mungu ambaye siyo wa ukweli bali ni sanamu ambayo sisi wenyewe tumeumba.  Ukweli ni kwamba tunapenda na tunamtumikia Mungu Mmoja ambaye anaishi milele kwa Utatu.  Hatumwelewi kabisa lakini tunampenda na tunamtumikia kwa sababu Yeye ndiye mwokozi wetu na Bwana wetu.

 

2. Je, Biblia inafunza kuhusu Mungu wa Utatu?

 

Hatujaandika hapa kila mstari katika Biblia kuhusu mafunzo haya ya Mungu wa Utatu lakini kuna mistari michache tutaangazia kutoka kwa Biblia.  Mtu yeyote ambaye anasoma Biblia kwa makini ataona kwamba Biblia inafunza jambo hili kwa ukweli.

 

(i) Kuna Mungu Mmoja.  Haya yanatokana na maneno ya Mungu alipozungumza na Musa: “Basi, msikilizeni enyi Waisraeli!  Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni Mwenyezi Mungu Mmoja. Mpendeni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa moyo wenu wote, kwa roho yenu yote na kwa nguvu zenu zote” (Kumbukumbu la Torati 6:4-5).

 

(ii) Baba ni Mungu.  Mara tano katika Agano Jipya anaitwa Mungu Baba: (Yohana 6:27; Tito 1:4; 1 Petro 1:1-2; 2 Petro 1:17 na Yuda 1:1-2).

 

(iii) Mwana ni Mungu.  Kuna mistari katika Agano Jipya ambayo inasema kwa wazi kwamba Bwana Yesu Kristo ni Mungu: (Yohana 1:1; Warumi 9:5; Wafilipi 2:5-8; 9-11; 1 Wathesalonike 3:13; Tito 2:13).

 

(iv) Roho Mtakatifu ni Mungu: Zaburi 139:7-8; Matendo ya Mitume 5:3-4 ni wazi kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu.

 

Hii ndiyo sababu tunaamini kwamba kila Mmoja wa Hawa ni Mungu na kuna Mungu Mmoja.

 

3. Makosa ambayo wakristo wamefanya kuhusu Mungu wa Utatu.

 

Kwa miaka mingi wakristo wamejaribu kuelewa jambo hili la Utatu wa Mungu, lakini katika juhudi zao wamefanya makosa makubwa sana.  Makosa mengine kati ya yale wamefanya bado yako nasi hadi leo.  Kwa hivyo tunastahili kuyatazama makosa haya.

 

(i) Wakristo wengine wamesema kwamba Hawa katika Utatu hawako sawa.  Wamesema kwamba Baba na Mwana hawako sawa na kwamba Roho Mtakatifu ni aina ya nguvu fulani lakini siyo Mungu.  Hivi sivyo Biblia inavyofunza.  Ukweli ni kwamba kila Mmoja ni Mungu kamili anayeishi milele na Wote Watatu wako sawa.

 

(ii) Wakristo wengine wamesema kwamba Mungu haishi katika Utatu.  Kwa hivyo wanasema kwamba katika Agano la Kale alijitokeza kama Baba, katika vitabu vya Injili (Mathayo, Marko, Luka na Yohana) amejitokeza kama Mwana na katika kitabu cha Matendo ya Mitume na leo amejitokeza kama Roho Mtakatifu: ni Mmoja lakini amejitokeza kwa njia tatu tofauti.  Jambo hili si la ukweli hata kidogo.  Mungu ni wa milele habadiliki.  Kwa hivyo Baba ni Mungu kamili, na hatawahi kubadilika: Yeye ni wa milele; Mwana ni Mungu kamili, na hatawahi kubadilika: Yeye ni wa milele; Roho Mtakatifu ni Mungu kamili, na hatawahi kubadilika; Yeye ni wa milele.

 

(iii) Wakristo wengine wanasema kwamba Mwana aliacha kuwa Mungu wakati alipokuja hapa ulimwenguni.  Wanasema kwamba alichukua mwili wa mwanadamu na akaacha kuwa Mungu kabisa.  Siyo rahisi kwetu kuelewa kabisa kwamba Kristo ni Mungu kamili na mwanadamu kamili; lakini Biblia inatueleza kwamba Yeye ni yote mawili kwa hivyo ni lazima tuamini jambo hili.  Wakati Yesu Kristo alikuja hapa ulimwenguni alikuwa mwanadamu kamili na pia alikuwa Mungu kamili.