Header

Kuhusu kijitabu hiki

 

Mafunzo haya yanahusu Biblia.  Kusudi la mafunzo haya ni kukusaidia kuelewa Biblia ni nini, ili uweze kuisoma na uielewe na ufaidike.  Kuna watu wengi nchini mwetu leo ambao wanasoma Biblia kila siku lakini hawafaidiki kwa sababu hawaisomi kwa makini.  Biblia inasema kwamba kuna watu ambao, “Wanasikiliza sana, lakini hawaelewi; wanatazama sana, lakini hawaoni” (Isaya 6:9), na kuna wengi kama hawa nchini mwetu leo.  Wanasikiliza mahubiri na kusoma Biblia lakini huwa hawafaidiki.  Hii ni kwa sababu hawaelewi Biblia ni nini.  Katika kijitabu hiki, tutajaribu kuelewa Biblia ni nini.

 

Mafunzo haya yamegawanyishwa kwa aina saba:

 

Funzo la Kwanza:    Je, Biblia ni nini?

Funzo la Pili:    Je, kuna nini ndani ya Biblia?

Funzo la Tatu:    Je, ujumbe mkuu katika Biblia ni gani?

Funzo la Nne:    Je, ni nani waliyeandika Biblia na ni kwa nini waliiandika?

Funzo la Tano:   Je, tunasomaje na tunajifunzaje Biblia?

Funzo la Sita:   Je, tutafafanua Biblia aje?

Funzo la Saba:   Je, tutahubiri aje na kufunzaje Biblia?

 

Funzo la Kwanza: Biblia ni nini?

 

Tukitaka kujibu swali hili, ni lazima tutazame vifungu viwili.

 

Kwanza kabisa tutatazama 2 Timotheo 3:14-17

 

Katika kifungu hiki Paulo anasema, “Bali wewe ukae katika mambo yale ulivyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.  Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”

 

Katika kifungu hiki Paulo anatufunza mambo manne kuhusu Biblia.

 

1. Biblia ni neno la Mungu.

 

Paulo anasema, “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu.”  Hii inamaanisha kwamba ni Mungu mwenyewe ambaye alitupatia Biblia.  Hili ni jambo la muhimu sana.  Fikiria juu ya barua ambayo unaweza kupata kutoka kwa mzee ambaye wewe mwenyewe unamheshimu sana.  Katika barua hiyo awe amekupatia maagizo fulani ambayo unafaa kufuata.  Je, utafanya nini kuhusu barua hiyo?  Je, utapuuza barua hiyo?  Jibu ni wazi kwamba utafanya kila uwezalo kutii maagizo hayo kwa sababu yametoka kwa mtu ambaye unamheshimu sana.

 

Biblia ni neno la Mungu; na hii inamaanisha kwamba ni Mungu mwenyewe ambaye aliandika Biblia.  Kila neno katika Biblia limetoka kwa Mungu mwenyewe.  Paulo anasisitiza jambo hili kwa kusema, “Kila andiko,” akimaanisha kila neno katika Biblia limetokana na Mungu mwenyewe.  Hii inamaanisha kwamba kuna mambo matano tunafaa kufanya.

 

(i) Ni lazima tusome Biblia kila siku.  Biblia iliandikwa na Mungu mwenyewe kwa hivyo ndiyo kitabu cha maana ulimwenguni kote.  Kwa mfano, siku moja unapata kitabu ambacho kimeandikwa na raisi wa Amerika.  Huwezi kusahau kitabu hiki kwani kila mahali utakapoenda utakuwa nacho.  Biblia iliandikwa na Mungu na ametupatia kitabu hiki: hatuwezi kupuuza kitabu hiki, ni lazima tukisome kila siku.

 

(ii) Ni lazima tujifunze Biblia.  Kuna tofauti kati ya kusoma na kujifunza Biblia.  Tunaposoma Biblia, tunasoma kifungu na kuwaza jinsi kifungu hicho kinatuzungmzia na kufanya yale ambayo kifungu hicho kinaeleza.  Lakini kujifunza Biblia ni kufanya zaidi ya hayo.  Baadaye katika somo hili tutajifunza jinsi tunavyofaa kujifunza Biblia.  Watu wengi nchini mwetu ambao wameokoka huwa hawajifunzi Biblia.  Wanawaza kwamba hawana uwezo wa kujifunza Biblia kwa sababu wao siyo wachungaji na wanawaza kwamba ni wachungaji pekee ambao wako na uwezo wa kujifunza Biblia.  Pia wanawaza kwamba Biblia ni kitabu kigumu sana kujifunza.  Lakini tunafaa kujua kwamba jambo hili silo la ukweli.  Siyo ukweli kwamba ni wachungaji pekee ndiyo wanaweza kuelewa Biblia, na pia siyo ukweli kwamba Biblia ni kitabu kigumu sana na watu hawezi kukielewa.  Ni jukumu la kila mkristo kujifunza Biblia.

 

(iii) Ni lazima tuamini kile Biblia inafunza.  Ukweli ni kwamba mambo fulani ambayo Biblia inafunza siyo rahisi kuamini.  Kwa mfano, watu wengi nchini mwetu wanawaza kwamba watoto ni malaika wadogo ambao hawana dhambi yoyote.  Haya ni mawazo ambayo ni ya kawaida nchini mwetu leo na hii ndiyo sababu makanisa mengi hayawafunzi watoto kwamba ni wenye dhambi ambao wanahitaji kutubu dhambi zao.  Je, ni ukweli kwamba watoto ni malaika ambao hawana dhambi?  Je, hivi ndivyo Biblia inavyofunza?  Ukweli ni kwamba Biblia inafunza watoto wamezaliwa na dhambi mioyoni mwao na pia wanatenda dhambi tangu wanapokuwa watoto.  Biblia inasema, “Waovu wamepotoka tangu kuzaliwa kwao, waongo hao, wamekosa tangu walipozaliwa” (Zaburi 58:3).  Haijalishi ni vipi tunawawazia watoto, hivi ndivyo Biblia inavyofunza na hivi ndivyo inafaa tuamini.

 

Jambo la kuhuzunisha ni kwamba watu wengi ambao wameokoka hawaelewi ni nini Biblia inafunza kuhusu mambo muhimu, kama vile Mungu ni nani, ni kwa nini Yesu alikuja ulimwenguni, kwa nini alikufa, kwa nini alifufuka, kwa nini Roho Mtakatifu alikuja, jinsi tunavyookolewa, inamaanisha nini kuokoka na nini itatendeka wakati Kristo atakaporudi.  Haya ni mambo ambayo watu wengi ambao wameokoka hawaelewi; kwa hivyo wanaamini mambo ambayo wanaambiwa badala ya kuamini Biblia.  Wanashikilia mafunzo ambayo hayako katika Biblia kabisa lakini kwa sababu waliyajua tangu utotoni mwao au kutoka kwa marafiki wao au wachungaji wao ambao pia hawajifunzi Biblia.  Wakati mwingine unapowaeleza ukweli watu hawa, watasema, “Ninajua Biblia inasema hivyo, lakini hivi ndivyo nimefunzwa na hivi ndivyo ninavyoamini.”  Hivi sivyo tunafaa kumtukuza Mungu.  Biblia ni neno la Mungu; na ni lazima tuisome na tujifunze na tuiamini.

 

(iv) Ni lazima tutii Biblia.  Mtu anaweza kusoma Biblia kila siku, na ajifunze kwa makini sana, na kuamini kila neno.  Lakini hadi atakapotii Biblia hawezi kufaidika kamwe.  Jinsi tunavyomwabudu na kumheshimu Mungu ni kumtii.  Mtoto ambaye anakosa kutii wazazi wake anakosa kuwaheshimu.  Hadi mtoto atakapotii maagizo ya wazazi wake ndipo atakuwa akiwaheshimu.  Kwa njia hiyo hiyo mtu anaweza kuenda kanisani kila Jumapili na kuimba nyimbo za injili na kuomba maombi marefu na kusikiliza neno la Mungu, lakini hadi atakapotii neno la Mungu, mtu huyu hamwabudu Mungu.  Hatuwezi kumwabudu Mungu kwa vinywa vyetu tu na tukose kumtii katika maisha yetu.  Huu ni unafiki, dhambi ambayo Mungu anachukia sana.

 

(v) Ni lazima tufunze Biblia.  Kwa sababu Biblia ni neno la Mungu, ni jukumu letu kubwa kwamba watu wanasikia na kuelewa ni nini inasema.  Ni jukumu la kila mkristo kufunza Biblia.  Siyo lazima sisi sote tufunze kwa madhabahu.  Ukiwa wewe ni mzazi ni lazima uwafunze wanao neno la Mungu.  Ukiwa na majirani, basi unafaa kuwaalika katika nyumba yako na uwafunze Maandiko Matakatifu.  Biblia inawaamuru wanawake ambao wamekomaa katika imani kuwafunza wanawake wengine (Tito 2:3-5).  Hili ndilo jukumu ambalo tumepewa katika Maandiko Matakatifu: ni lazima tufunze neno la Mungu.

 

2. Biblia ilipeanwa ili tupate hekima ya wokovu.

 

Paulo anasema, “Maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.”  Mungu alitupatia Maandiko ili atuonyeshe njia ya wokovu.  Biblia inatuambia kwamba mwanadamu amepotea kwa sababu ameanguka katika dhambi.  Hii inamaanisha kwamba mwanadamu ako katika hatari kubwa sana.  Kuna sababu mbili kwa nini mwanadamu ako katika hatari kubwa sana:

 

(i) Kuna hatari kwamba mwanadamu atapotea milele.  Fikiria juu ya mtoto ambaye anaishi katika mji mkubwa na siku moja anapotea.  Anaenda mahali ambapo hajawahi kuwa na mahali huko kuna watu wengi na anapotea njia.  Mtoto huyu huenda apotee kabisa kama mtu yeyote hatajitokeza amsaidie.  Kwa njia hiyo hiyo mwanadamu amepotea kwa ajili ya dhambi.  Bwana Yesu alitupatia mifano kama ule wa kondoo aliyepotea na shilingi iliyopotea akituonyesha ukweli huu, yaani tumepotea (Luka 15:1-10).  Hii ndiyo sababu alisema, “Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea” (Luka 19:10).  Kama Mungu hangetupatia Biblia, tungebaki tukiwa tumepotea na mwishowe tungepelekwa jehanum.

 

(ii) Kuna hatari kwamba mwanadamu anatafuta njia ambayo ni mzuri kwake, lakini siyo mzuri machoni pa Mungu.  Fikiria tena juu ya mtoto ambaye amepotelea katika mji.  Anapokuwa anatafuta njia anakuja kwa njia ambayo anafikiria ni mzuri; maduka kwa njia hii ni kama yale ambayo yako nyumbani kwao.  Kwa hivyo anafuata njia hii.  Lakini hii siyo njia mzuri, kwa sababu inamwongoza mahali pabaya.  Hii ndiyo hatari ambayo watu ambao wamepotea wanakumbana nayo.  Wanapata njia ambayo inaonekana kuwa mzuri na kwa hivyo wanafuata njia hii.  Biblia inasema, “Mtu anaweza kuona njia yake kuwa sawa, lakini mwishowe humwongoza kwenye kifo” (Methali 16:25).  Kuna mamilioni ya watu ulimwenguni leo ambao huwaza kwamba njia ya wokovu ni matendo yao mema.  Wanawaza kwamba njia ya kufika mbinguni ni kujaribu sana kwa juhudi zao jinsi wawezavyo kuishi maisha mema na kutii Amri Kumi za Mungu na kuenda kanisani kila Jumapili.  Wanajiwazia kwamba wakifanya mambo haya yote, Mungu atafurahishwa na juhudi zao na atawapatia nafasi mbinguni kama zawadi kwao.  Hii ni njia ambayo kwa mwanadamu inaonekana mzuri, lakini njia hii haielekei mbinguni, bali inaelekea jehanum.  Biblia inasema kwamba, “Tunajua kwa hakika kwamba mtu hawezi kufanywa mwadilifu kwa kuitii sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo” (Wagalatia 2:16).  Hii ndiyo sababu Paulo anasema katika kifungu cha 2 Timotheo 3:14-17 kwamba Maandiko Matakatifu yanaweza kumfanya mtu awe na hekima ya wokovu kupitia kwa imani ndani ya Yesu Kristo.

 

Kwa hivyo Biblia ilipeanwa kawa sababu mwanadamu alikuwa amepotelea kwa dhambi na alikuwa hana uwezo wowote wa kujisaidia kurudi kwa Mungu.  Kwa huruma wake na uzuri wake, Mungu anatuonyesha njia ya kuenda mbinguni kupitia kwa neno lake.  Bila neno la Mungu tutapotea milele.

 

3. Biblia ilipeanwa ili tuwe watakatifu.

 

Paulo anasema katika kifungu hiki kwamba, “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki.”  Biblia ilipeanwa ili tuwe na hekima ya wokovu, pia Biblia ilipeanwa ili itufunze ukweli, ituonye, itusahihishe makosa na ituongoze katika maisha ya utakatifu.  Kwa ufupi ni kwamba Biblia ilipeanwa ili tuwe watakatifu.  Biblia inatueleza kwamba wakati tunaokoka, bado tunakuwa na dhambi ndani mwetu.  Siyo hali kwamba wakati tunapookoka kila dhambi inatuondokea kabisa.  Bado tuko na dhambi ndani mwetu ambazo tulikuwa nazo kabla ya kuokoka.  Dhambi hizi zinahitaji kuondolewa ndani mwetu na kazi hii ni ya muda mrefu hadi wakati tutakapokufa.  Baada ya kuokoka, Mungu anaanza kazi ndani mwetu ya kuondoa dhambi hizi; na njia ile anatumia ni neno lake.  Hii ndiyo maana Paulo anasema kwamba Kristo atalitakasa kanisa lake kwa njia ya kuoshwa na neno lake (Waefeso 5:25).

 

4. Biblia inatosheleza mahitaji yetu yote.

 

Kwa uangalifu tazama kile Paulo anasema hapa; “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho...ili mtu wa Mungu awe KAMILI, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”

 

Kuna watu leo nchini mwetu ambao wanakubali kwamba Biblia ni neno la Mungu, lakini hawakubali kwamba Biblia ni ufunuo tosha kutoka kwa Mungu.  Wanaamini kwamba Mungu bado anazungumza leo kwa kupitia njia zingine kando ya Biblia, kama unabii, maono na ndoto.  Wanaendelea kusema kwamba, “Ndiyo ninajua Biblia inasema hivi, lakini pia kuna ufunuo mpya kutoka kwa Mungu, na ni lazima tuufuate ufunuo huo.”  Jambo hili ni la uongo.  Biblia ilipeanwa ili mtu wa Mungu (yaani wale wote ambao wameokoka) akamilike na awe tayari kufanya kila kazi njema.  Kila kitu ambacho tunahitaji ili tuokoke na kila kitu ambacho tunahitaji ili tuishi maisha matakatifu inapatikana katika Biblia.

 

Kila kitu ambacho Mungu anataka kutuambia kiko katika Biblia.  Hakuna ufunuo mwingine mpya au ambao unakuja, Mungu amesha zungumza nasi kupitia kwa neno lake.  Maneno ya mwisho kwa Biblia ni haya: “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu yeyote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki” (Ufunuo 22:18).

 

Tukiwaza kuhusu jambo hili kwa uangalifu sana, tutaona jinsi ilivyo hatari sana tukiendelea kuwaza kwamba Mungu bado anazungumza leo kwa njia nyingine yoyote ile au kwa watu fulani.  Tutazame mfano wa kijana mmoja kanisani ambaye anatafuta kazi mjini.  Mchungaji wa kanisa anakuja kwake na kusema, “Mungu amenizungumzia kwamba unafaa kuendelea ukitafuta kazi hapa mjini na utapata kazi hiyo karibuni.”  Mchungaji kutoka kanisa nyingine anakuja kwake na kumwambia, “Mungu amenizungumzia kwamba unahitaji kurudi mashambani na ufanye kazi huko.  Mungu atakubariki ukifanya hivyo.”  Je, kijana huyu atafanya nini?  Je atafuata yule wa kwanza au wa pili?  Wacha tuwaze zaidi kwamba atabaki mjini na aendelee kutafuta kazi; lakini baada ya miezi awe hana kazi.  Je, atahitajika kufanyia nini yule ambaye alimwambia abaki mjini na atapata kazi?  Je, ni Mungu ambaye alinena kupitia mchungaji huyu?  Na kama Mungu alizungumza kupitia mchungaji huyu, mbona kijana huyu hakupata kazi?  Je, kati ya Mungu na mchungaji huyu ni nani mwongo?  Ni huyu mchungaji ni mwongo, kwa sababu, “Mungu si mtu, aseme uongo” (Hesabu 23:19), na huyu mchungaji hafai kuitwa mchungaji kwa sababu yeye ni mwongo.

 

Haya ni mambo tunasikia na kuona kila siku katika makanisa mengi.  Watu huzungumza kwa jina la Mungu na kuahidi watu mambo mengi ambayo hayatimiki.  Mambo haya huwaacha wakristo wakiwa wamechanganyikiwa sana na wale ambao siyo wakristo wanaanza kusema kwamba imani ya kikristo haiwezi kutegemewa.

 

Haya ndiyo mambo manne tunapata katika kifungu hiki cha 2 Timotheo 3:14-17; Biblia ni neno la Mungu, Biblia ilipeanwa ili tuwe na hekima ya wokovu, Biblia ilipeanwa ili tuwe watakatifu na Biblia inatosheleza.

 

Pili tutatazama 2 Petro 1:21

 

Mstari huu unasema, “Kwa maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.”

 

Katika mstari huu Petro anapozungumza kuhusu “unabii” anamaanisha Biblia kwa ujumla, siyo tu vitabu fulani vya Biblia kama vile ambavyo vinaitwa vitabu vya unabii.  Anatufunza funzo muhimu kuhusu jinsi Biblia ilivyoandikwa.

 

Petro anatufunza kwamba kuandikwa kwa Biblia kulishirikisha Mungu na mwanadamu.

 

Petro anasema kwamba Biblia iliandikwa na wanadamu ambao waliongozwa na Roho Mtakatifu. Hii inamaanisha kwamba ni wanadamu ambao waliandika Biblia wakiwa chini ya uongozi na ushawishi wa Roho Mtakatifu.  Anasema, “Kwa maana unabii hakuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu.”  Kwa ufupi ni kwamba Biblia haikuandikwa kwa sababu wanadamu fulani waliamua kuiandika: ujumbe wake hautokani na matakwa ya wanadamu.  Bali neno la Mungu lilikuja wakati Roho Mtakatifu aliwatumia wanadamu kuliandika.  Hili ni jambo ambalo tunahitaji kuelewa vizuri.  Biblia ni neno la Mungu na ni maandiko ya wanadamu.  Kwa mfano waraka wa 1 Wakorintho, Paulo alikuwa katika mji wa Waefeso wakati alipata habari kuhusu kanisa la Korintho na matatizo ambayo yalikuwemo kanisani.  Kwa hivyo alitengeneza orodha ya matatizo yote na baadaye akaandika waraka wa 1 Wakorintho.  Ni yeye ambaye alipanga jinsi atakavyoandika lakini ni Mungu ambaye alimtumia kuandika yale aliandika.  Roho wa Mungu alimwongoza Paulo kuandika waraka huu ili liwe neno la Mungu.  Lakini hii haimaanishi kwamba Biblia iko na makosa.  Kwa kawaida mwanadamu anapoandika kitabu, kitakuwa na makosa fulani fulani kwa sababu yule ambaye aliandika kitabu hicho hajui kila kitu; na kwa sababu yeye ni mwanadamu atafanya makosa.  Lakini Biblia ni neno la Mungu.  Liliandikwa chini ya uongozi na ushawishi wa Roho Mtakatifu.  Kila neno ndani mwake ni neno la Mungu.  Kwa hivyo neno hili halina makosa yoyote au mafunzo ya uongo.

 

Jambo hili kwamba Biblia ni kazi ya mwanadamu ni muhimu sana wakati tunafafanua Biblia.  Wakati tunasoma kifungu fulani cha Biblia na kutaka kukielewa, tunatumia njia sawa na ile tunatumia tukifafanua maandiko ya mtu yeyote.  Fikiria juu ya barua ambayo unapata kutoka kwa rafiki wako mjini, na ndani ya hiyo barua kuna kifungu ambacho huelewi.  Utasoma barua yote kutoka mwanzoni ili uone ni nini barua inasema na ni jinsi gani imeandikwa.  Halafu utasoma tena kifungu hicho ambacho huelewi ili uone kama utakielewa ukikilinganisha na barua yote.  Hivi ndivyo tunafaa kufafanua Biblia na kuielewa.  Kuna watu wengi nchini mwetu leo ambao wanachukua mstari mmoja na kuanza kuhubiri bila kuelewa ni nini Biblia inasema kwa ujumla katika kifungu hicho.

 

Muhtasari wa Funzo la Kwanza

 

Katika funzo hili tumeuliza swali, “Biblia ni nini?”  Tukianganzia kujibu swali hili tumetazama vifungu viwili kutoka kwa Biblia: 2 Timotheo 3:14-17 na 2 Petro 1:21.  Kutoka kwa vifungu hivi viwili, tumejifunza mambo matano kuhusu Biblia:

 

1. Biblia ni neno la Mungu.

2. Biblia ilipeanwa ili tupate hekima ya wokovu.

3. Biblia ilipeanwa ili tuwe watakatifu.

4. Biblia inatosheleza mahitaji yote.

5. Kuandikwa kwa Biblia kulishirikisha Mungu na mwanadamu.

 

 

Funzo la Pili:  Kuna nini ndani ya Biblia?

 

Katika funzo hili tutatazama yale yaliomo katika Biblia.  Biblia ni kitabu kikubwa ambacho kiko na mambo mengi.  Tukikisoma kwa uangalifu kitatusaidia kujua yale ambayo yako ndani.

 

1. Kuna vitabu 66 katika Biblia.

 

Miongoni mwa vitabu hivi kuna vile ambavyo ni vifupi sana na viko na sura moja pekee; na vingine ni virefu sana.  Wale ambao wanafunza Biblia wanahitajika kujua majina ya kila kitabu cha Biblia bila kuyasoma.  Hii siyo kazi ngumu hata kidogo.  Unaweza kila siku kushika majina ya vitabu vitano na kwa siku chache utajua majina yote ya vitabu hivi.

 

2. Kuna Agano mbili katika Biblia; Agano la Kale na Agano Jipya.

 

Wakristo wengi huwa hawatofautishi kati ya Agano hizi mbili.  Kuna watu wengi ambao huamini kwamba katika Agano la Kale watu walikuwa wanaokoka kwa sababu ya matendo yao mema na kutii Sheria ya Musa.  Jambo hili si la ukweli hata kidogo.  Katika kitabu cha Warumi sura ya 4 tunaambiwa kwamba watu kama Abrahamu na Daudi waliokolewa kwa sababu ya imani yao.  Watu katika Agano la Kale waliokolewa jinsi tunavyookolewa katika Agano Jipya au sasa, yaani kwa imani pekee kwa sababu Mungu habadiliki.

 

Agano la Kale ni wakati kabla ya kuja kwa Yesu hapa ulimwenguni akiwa mwanadamu.  Agano hili linazungumza jinsi ulimwengu ulivyoumbwa, jinsi dhambi ilivyokuja hapa ulimwenguni na jinsi Mungu alivyopanga mpango wa kuwaokoa watu wake kutoka kwa dhambi.

 

Kwa hivyo Agano la Kale lilitayarisha njia ya Agano Jipya.  Ni kama vile mtu anavyojenga nyumba; anatayarisha mahali ambapo atajenga kwa kununua kila kifaa ambacho kitahitajika kwa kazi hiyo.  Baada ya kumaliza matayarisho, basi kazi yenyewe ya kujenga inaanza.  Mungu alipanga kujenga ufalme wake hapa ulimwenguni ambao utakuwa na watu kutoka kwa kila taifa.  Agano la Kale ni hadithi ya jinsi alivyofanya kazi yake ya kutayarisha ufalme huu hapa ulimwenguni na Agano Jipya ni hadithi jinsi Bwana Yesu Kristo mwenyewe alianza kujenga ufalme huu.

 

Agano Jipya linatuambia kwamba Bwana Yesu Kristo alianza kazi hii na baadaye akamtuma Roho Mtakatifu ambaye alikuja kuendelesha kazi hii.  Roho Mtakatifu bado anafanya kazi katika ulimwengu akiendelea kujenga ufalme huu.

 

3. Kuna aina tofauti tofauti ya vitabu katika Biblia.

 

Ni muhimu sana kwetu kuelewa kwamba Biblia inajumlisha vitabu vingi kama maktaba.  Unapoingia katika maktaba utapata aina mingi ya vitabu: kuna vitabu vya hadithi tu, kuna vitabu vya kihistoria, kuna vitabu vya ushairi, vitabu vya siasa, vitabu kumhusu Mungu na vitabu vingine.   Hivi ndivyo Biblia ilivyo; kwani iko na vitabu 66 na vya aina tofauti tofauti.  Katika Biblia tunapata vitabu vya kihistoria, vitabu vya methali na vitabu vya unabii.  Tunapata pia barua ambazo zinaeleza kuhusu mafunzo fulani muhimu sana na barua ambazo ziliandikwa kwa kusudi la kutatua mambo fulani katika kanisa.  Haya ni baadhi ya mambo ambayo tunapata katika Biblia.  Tunaweza kuweka vitabu vya Biblia katika vikundi tofauti tofauti kama hivi:

 

Agano la Kale

Maandishi ya Musa au vitabu vya Sheria (Mwanzo hadi Kumbukumbuku la Torati).

Historia ya Agano la Kale (Yoshua hadi Esta).

Vitabu vya Ushairi (Yobu hadi Wimbo uliyo bora).

Vitabu virefu vya Manabii (Isaya hadi Danieli).

Vitabu vifupi vya manabii (Hosea hadi Malaki).

 

Agano Jipya

Vitabu vya Injili (Mathayo hadi Yohana).

Kitabu cha Historia (Matendo ya Mitume).

Barua za Paulo (Warumi hadi Filemoni).

Barua za ujumla (Waebrania hadi Yuda).

Kitabu cha Ufunuo (Ufunuo).

 

Kwa nini ni jambo muhimu kwetu kuelewa kwamba Biblia iko na vitabu tofauti?  Ni kwa sababu wakati tunapokuwa tunafafanua Biblia tunatumia njia tofauti kwa kila kitabu kulingana na mtindo wa uandishi wa kitabu hicho.  Kwa mfano unaingia katika maktaba na kupata kitabu ambacho kimeandikwa kuhusu mashetani.  Unatambua kwamba mwandishi aliandika kuonyesha ubaya wa pombe akitumia mfano wa mashetani.  Halafu pia unapata kitabu kingine ambacho mwandishi ameandika kuhusu historia ya Kenya tangu kupata uhuru.  Unapata kitabu cha tatu na unapata kwamba hiki kinahusu ushairi, mila na methali ambazo hupatikana mahali tofauti tofauti nchini Kenya.  Sasa unajua kwamba vitabu hivi vitatu ni tofauti kabisa.  Katika kitabu cha kwanza mwandishi haandiki kuhusu mashetani ya ukweli, anatumia mfano huu kuonyesha jinsi pombe ilivyo mbaya sana.  Kwa hivyo tunaposoma kifungu katika kitabu hiki, ni lazima tukumbuke kitabu kinahusu nini na tukifafanue kama inavyotakikana.  Kwa njia hiyo hiyo unaposoma shairi au methali, ni lazima ujue ni maandishi ya aina gani kama unataka kuyafafanua vyema.

 

Hivi pia ndivyo ilivyo na Biblia.  Katika Biblia tunapata vitabu vingine ni vya kihistoria, vingine ni vya ushairi na methali, vingine viliandikwa kwa kanisa fulani au kwa mtu fulani.  Haya yote ni maandishi tofauti na ni muhimu kukumbuka jambo hili tunapofafanua Biblia.

 

Muhtasari wa Funzo la Pili

 

Katika mafunzo haya tumetazama swali hili, “Ni nini iko katika Biblia?” na tumetazama mambo matatu:

 

1. Kuna vitabu 66 katika Biblia.

2. Kuna Agano mbili katika Biblia : Agano la Kale na Agano Jipya.

3. Kuna vitabu tofauti tofauti katika Biblia.

Funzo la Tatu: Je, ujumbe mkuu katika Biblia ni gani?

 

Katika somo la kwanza tulianza kwa kuangalia ni nini iliyomo katika Biblia.  Tumeona kwamba ni kitabu ambacho kiko na vitabu 66, na kiko na Agano mbili na kiko na vitabu ambavyo vimeandikwa tofauti tofauti.  Tunafaa kukumbuka kwamba hata kama kuna vitabu 66 katika Biblia, hiki ni kitabu kimoja na kiko na ujumbe moja mkuu.  Kwa hivyo Biblia siyo kama maktaba.  Katika maktaba tunapata vitabu vingi na vyote viko na ujumbe tofauti.  Hatuwezi kuwaza kwamba vitabu vyote katika maktaba viko na ujumbe moja.  Lakini Biblia iko na ujumbe moja.

 

Katika somo hili tutaangazia ujumbe muhimu ambao Biblia inafunza kwa kusoma Luka 24:25-27.  Kabla ya kuendelea na somo hili tafadhali soma Luka 24:13-35.  Katika kifungu hiki tunasoma kuhusu wanafunzi wawili wa Yesu ambao walikutana na Yesu wakati alipokuwa amefufuka wakiwa njiani wakielekea Emmau.  Tunasoma kwamba hawakuwezeshwa kumjua Kristo wakati huo.  Wakati moja kwa mazungumzo Yesu aliwaambia, “Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii!” (mstari wa 25).  Aliwaambia hivi kwa sababu hawakuelewa ujumbe muhimu wa Biblia.  Labda walikuwa wamesoma maandiko mara mingi, lakini kama watu wengi leo hawakuwa wamejua ujumbe muhimu ambao unapatikana katika Biblia.  Jambo hili si la kushangaza kamwe kwa sababu Biblia ni kitabu kikubwa ambacho kimeandikwa na watu wengi ambao walikuwa chini ya ushawishi na uongozi wa Mungu.  Siyo rahisi kuelewa kwamba Biblia iko na ujumbe moja.

 

Katika nchi yetu labda mafunzo ya kawaida ni haya: “Wakati Mungu alipoumba Adamu na Hawa, alidhani kwamba wataishi maisha matakatifu na kumtii milele.  Lakini siku moja Mungu alishitukia kwamba Adamu na Hawa walikuwa wameanguka dhambini na kumwasi.  Kwa hivyo baada ya Adamu kuanguka dhambini, Mungu alianza kupanga mpango ya wokovu.  Hakutaka watu wote waende jehanum, alitaka awaokoe.  Kwa hivyo baada ya kuanguka kwa Adamu dhambini, Mungu alianza kupanga mpango jinsi atakavyookoa mwanadamu.  Kwanza kabisa aliwapatia sheria takatifu, lakini watu hawakuweza kutii sheria yake.  Kwa hivyo aliamua kumtuma Mwanawe katika ulimwengu huu afe kwa ajali ya watu wote na anaendelea kuwaita watu wote waje kwake Yesu awaokoe.”  Hivi ndivyo watu wengi wanavyowaza kuhusu Biblia.  Hii ndiyo sababu watu hawasomi na kujifunza Agano la Kale kwa makini.  Kwao Agano la Kale ni hadithi ambayo inaonyesha kwamba mpango wa Mungu haukufaulu.  Wanakubali kwamba Agano hili liko na hadithi nyingi nzuri, lakini hawaoni ni wapi Agano hili linamzungumzia Kristo au mpango wa Mungu wa wokovu.

 

Ni muhimu kwetu kuelewa kwamba mawazo ya aina hii ni ya uongo kabisa.  Biblia ni wazi kwetu kwamba Mungu alipanga wokovu wetu kupitia kwa kifo na kufufuka kwa Yesu kabla ya kuumba ulimwengu.  Biblia inatuambia kwamba Mungu aliwachagua wale wote ambao wataokoka kabla ya kuumba ulimwengu (Waefeso 1:3-4).

 

Tunaposoma Luka 24:25-27, tunaona mambo matatu.

1. Biblia iko na hadithi moja.

 

Tunaposoma Biblia tunaona kwamba ni kitabu ambacho kiko na vitabu vingi ndani mwake na inaonekana kwamba vitabu hivi viko na ujumbe tofauti tofauti.  Kwa mfano tunaweza kuwaza kwamba Agano la Kale limejumlisha tu hadithi nzuri kama ile ya Nuhu, Yusufu, Musa na Daudi, na kwamba hadithi hizi hazina uhusiano na nyingine kabisa.  Kuwaza hivi ni makosa makubwa sana.  Njiani wakielekea Emmau, Yesu Kristo alianza kuzungumza kumhusu Musa, na manabii, na alitumia mifano ya hawa watu kuzungumza juu ya ujumbe muhimu ambao unapatikana katika Biblia.  Biblia ni hadithi moja ambayo iko na mwanzo na mwisho.  Tunaona jambo hili katika sura za kwanza za kitabu cha Mwanzo na sura za mwisho za kitabu cha Ufunuo.  Biblia inaanza na Mungu akiumba dunia na mbingu na inamalizika na dunia mpya na mbingu mpya.  Katika kitabu cha Mwanzo kuna paradiso, yaani mahali ambapo Mungu anatembea na mwanadamu, na katika kitabu cha Ufunuo, mwanadamu ako katika ushirika kamili na Mungu tena.  Kwa ufupi hadithi ya Biblia ni hii: kwanza Mungu aliumba kila kitu kizuri.  Halafu dhambi iliingia na kuharibu kila kitu.  Baadaye, mpango wa Mungu wa kuwaokoa watu wake ambao aliupanga kabla ya kuumba ulimwengu aliutekeleza kwa kuja kwake Yesu hapa ulimwenguni.  Mpango wa Mungu ni “kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo” (Waefeso 1:10).  Roho Mtakatifu anaendelea na kazi yake ya kuwaokoa watu wake, kazi ambayo atakamilika wakati Yesu atakaporudi.

 

2. Biblia inazungumza kumhusu Kristo kila mahali.

 

Kristo ndiye ujumbe muhimu katika Biblia.  Tunaambiwa jinsi Yesu alipozungumza na hawa wanafunzi walipokuwa wanaenda Emmau: “Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Musa hadi manabii wote” (mstari 27).  Tazama kwamba Yesu hapa anaanza na kuzungumza kumhusu Musa akisema kwamba maandiko yote yalikuwa yanamhusu Yesu.  Tunaposoma Agano la Kale lazima tutilie maanani kwamba ujumbe muhimu katika Agano hili ni Kristo Yesu.  Katika kitabu cha Mwanzo 3:15, baada ya mwanadamu kuanguka dhambini, Mungu alimwambia nyoka, “Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, kati ya uzawa wako na uzawa wake, yeye atakiponda kichwa chako.”  Haya ni maneno ya Mungu kwamba siku moja atamtuma Mwanawe katika ulimwengu na Yeye atamshinda shetani na kurejesha viumbe vyake katika hali ambayo Mungu aliviumba viwe katika utukufu wake.  Katika kitabu cha Mwanzo 12:3 Mungu alimwambia Abrahamu, “Kwako wewe, nitayabariki mataifa yote ya dunia.”  Hapa kuna tangazo kwamba Yesu atakapokuja atajenga ufalme wake hapa ulimwenguni ambao utajumlisha  watu wa kila taifa.  Agano la Kale lote ni hadithi kuhusu jinsi Mungu alivyotayarisha njia kwa kuja kwake Kristo.

 

Tunaposoma Agano la Kale, tunafaa kila wakati kukumbuka kwamba liliandikwa kutuongoza kwa Kristo Yesu.

 

 

3. Biblia yote inahusu kazi yake Kristo Yesu.

 

Yesu aliwaambia wanafunzi ambao walikuwa wakielekea mji wa Emmau kwamba, “Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii!  Je!  Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?”  Kwa ufupi ni kwamba kama wanafunzi hawa wawili wangeelewa maandiko ya Agano ya Kale, hawangeshangaa kuona Kristo akiteswa na kufa msalabani.  Hata wangetarajia kufufuka kwake kwa sababu Agano la Kale linaeleza kwamba ataingia, “katika utukufu wake” (mstari wa 26).  Kuna njia nne ambazo Agano la Kale linatuongoza kwake Kristo.

 

(i) Kwanza, Agano la Kale linatuonyesha jinsi mwanadamu alivyoanguka katika dhambi mbaya sana na hawezi kujiokoa.  Agano la Kale linahusu taifa la watu ambao walikuwa wamebarikiwa sana na Mungu lakini watu hawa waliendelea katika dhambi.  Mungu alikuwa ameingia katika agano na Ibrahimu, Mungu alikomboa taifa la Uisraeli kutoka kwa utumwa katika nchi ya Misri kwa nguvu zake, Mungu alipatia Waisraeli sheria yake, uwepo wa Mungu ulikuwa pamoja nao, Mungu aliwapatia viongozi ambao wengi wao walikuwa wamejitolea kumtumikia Mungu, Mungu aliwapatia nchi ambayo ilikuwa ikitiririka na asali na maziwa, Mungu aliahidi kuwalinda na kuwalisha na pia aliwapatia manabii ambao waliwahubiria neno la Mungu na kuishi maisha ambayo yalikuwa ya kumtii Mungu.  Hizi ni baraka ambazo hakuna taifa lolote ulimwenguni limeshawahi kuwa nazo.  Hata baada ya baraka hizi mingi taifa la Uisraeli liliendelea katika dhambi hata baada ya kuadhibiwa na Mungu, walirudi katika dhambi.  Jambo hili linatufunza kwamba ugonjwa wa dhambi ni ugonjwa ambao uko na mizizi.  “Moyo wa mtu ni mdanganyifu kuliko vitu vyote” (Yeremia 17:9).  Agano la Kale linatuonyesha kwamba hata taifa likiwa na baraka mingi na kupewa miaka mingi ili lijaribu kuishi maisha matakatifu, halitaweza.  Jambo hili linatuonyesha kwamba uovu wa mwanadamu ni mbaya sana na unahitaji mwokozi ambaye ametumwa na Mungu.

 

(ii) Pili, Agano la Kale linatuonyesha kwamba Mungu anahitaji sadaka takatifu ya dhambi zetu.  Katika kitabu cha Walawi, tunasoma kuhusu sadaka ambazo watu wa Mungu walikuwa wakitoa kwa ajili ya dhambi zao.  Mnyama alikuwa awe hana kasoro yoyote.  Jambo hili linatuonyesha kwamba matendo yetu hayawezi kutuokoa kwa sababu hayako huru kutoka kwa dhambi.  Sadaka yoyote ile tutawahi kuleta kwa ajili ya dhambi zetu haitawahi kukubaliwa kwa sababu kwa asili sisi ni wenye dhambi.  Kama tutaokolewa basi sadaka hiyo lazima iwe, “Damu ya thamani ya Kristo, ambaye alikuwa kama mwanakondoo asiye na dosari wala doa” (1 Petro 1:19).

 

(iii) Tatu, Agano la Kale linatueleza kwamba sadaka hii ingetoka kwa Mungu mwenyewe.  Kuhani katika Agano la Kale alikuwa aingie mahali patakatifu kila mwaka na damu ya mnyama, kuonyesha kwamba kazi ya kuhani huyu haingewahi kuisha hadi sadaka bora ipeanwe.  Manabii wa Agano la Kale, ikizingatiwa Isaya sana, walizungumza wazi kabisa kuhusu yule ambaye “Angejeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu, kuumizwa kwa sababu ya maovu yetu.  Kwa kuadhibiwa kwake sisi tumepata uhai; kwa kupigwa kwake sisi tumepona.  Lakini Mwenyezi Mungu alimtwika adhabu, ambayo sisi wenyewe tuliistahili” (Isaya 53:5-6).

 

(iv) Nne, Agano la Kale linatueleza kuhusu Masia ambaye angeshinda vita na kuuleta ufalme wake wa amani.  Linatueleza kuhusu mmoja ambaye, “Naye ataleta amani miongoni mwa mataifa; utawala wake utaenea toka bahari hata bahari, toka mto Eufrate hata miisho ya dunia” (Zekaria 9:10).  Hakuna mfalme wa Yuda au Uisraeli ambaye aliweza kuleta amani katika dunia.  Kuna vita vingi katika Agano la Kale ambavyo vinatufanya kumtamani mwokozi ambaye Mungu atamtuma kuja kuleta amani kwa viumbe vyake.

 

Yesu aliwaita wanafunzi wake ambao walikuwa wakielekea mji wa Emmau “wasiofahamu” kwa sababu hawakuwa wamesoma maandiko ya Agano la Kale vizuri.  Je, ni wangapi leo katika ulimwenguni kote ambao wako kama wanafunzi hawa: hawaoni ujumbe muhimu wa Biblia ambao ni Kristo Yesu na kazi yake.

 

Je, jambo hili linatuzungumzia kwa njia gani?

 

Kwa sababu Biblia ni kitabu kimoja ambacho kinazungumzia ujumbe mmoja, ni lazima tuwe waangalifu jinsi tunavyokisoma.  Wakati tunaposoma Biblia, lazima tujue kwamba kila mstari au kifungu ni mojawapo ya ujumbe wote wa Biblia.  Kwa hivyo kila wakati tunaposoma kifungu kimoja lazima tujiulize, “Je, kifungu hiki kinaingianaje na ujumbe wa Biblia nzima?”  Katika Agano la Kale pole pole Mungu anatufunulia mpango wake na nia yake kwa maisha yetu.  Wale wote ambao wako katika huduma wa kuhubiri na kufunza neno la Mungu lazima wajue jambo hili kila wakati wanapojitayarisha kuwafunza na kuwahubiria watu wa Mungu.  Wakati tunasoma kifungu kwa kusudi la kukifunza au kukihubiri, swali letu lisiwe, “Je, nitawaambia watu nini kutokana na kifungu hiki,” bali swali letu linafaa liwe, “Je ujumbe huu unaingianaje na ujumbe mzima wa Biblia?”  Tunapoelewa, basi tutaona jinsi kifungu kinatueleza jinsi tunavyofaa kuishi kulingana na mafunzo hayo.

 

Muhtasari wa Funzo la Tatu

 

Katika somo hili tumetazama swali hili, “Je, ujumbe muhimu wa Biblia ni gani?”  Tumesoma kitabu cha Luka 24:25-27 na tumejifunza mambo matatu.

 

1. Biblia iko na hadithi moja.

 

2. Biblia inazungumza kumhusu Kristo kila mahali.

 

3. Biblia yote inahusu kazi yake Kristo Yesu.

 

 

Funzo la Nne:  Je, ni nani waliviandika vitabu

vya Biblia na ni kwa nini waliviandika?

 

Katika Funzo la Kwanza tuliona kwamba Biblia ni neno la Mungu na ni Mungu mwenyewe aliyeiandika.  Tuliona katika funzo hilo kwamba Biblia pia ni kazi ya wanadamu; kwamba wakati Mungu aliandika Biblia aliwatumia wanadamu.

 

Katika funzo hili tutazingatia wanadamu waliotumiwa na Mungu kuandika Biblia.  Ni muhimu sana kwetu kujua mambo kuwahusu watu hawa ambao waliandika Biblia; kwa sababu mambo haya yatatusaidia kufafanua Biblia vyema.  Katika mafunzo haya tutajiuliza maswali kadhaa na kutafuta majibu ya maswali hayo.

 

1. Je, ni watu wangapi ambao Mungu aliwatumia kuandika Biblia?

 

Kwa sababu hatujui waandishi wa vitabu vyote vya Biblia, hatuwezi kupeana jibu sahihi kwa swali hili.  Kile tunajua ni kwamba walikuwa watu karibu 40 ambao Mungu aliwatumia kuandika Biblia.  Idadi kamili ya watu hawa hatuijui kabisa, kile tunajua walikuwa karibu 40.

 

2. Je, watu hawa waliishi lini?

 

Watu ambao waliandika vitabu vya Biblia waliishi miaka mingi iliyopita.  Musa ambaye aliviandika vitabu vitano vya kwanza aliishi kama miaka 3,500 iliyopita.  Mtume Yohana ambaye aliandika kitabu cha Ufunuo aliishi kama miaka 1,900 iliyopita.  Tunaweza kujifunza mambo mawili kutoka kwa haya:

 

(i) Kwanza kabisa tunaona kwamba Biblia ni kitabu cha zamani sana.  Si kitabu ambacho kiliandikwa miaka michache iliyopita, kwani miongoni mwa vitabu vya Biblia, vingine viliandikwa zamani sana kuliko vingine.  Tunafaa kuwa waangalifu sana kuhusu jambo hili wakati tunafafanua Biblia.  Watu ambao waliandika Biblia waliishi enzi ambazo mambo yalikuwa tofauti sana na sasa. Mila zao zilikuwa tofauti sana, na jinsi walivyoishi maisha yao ilikuwa tofauti kabisa.  Lakini Biblia ni neno la Mungu na kwa hivyo lazima kila mwanadamu aitii bila kujali mila.  Kwa hivyo lazima tuwe waangalifu wakati tunafafanua kifungu, ni lazima tuhakikishe kwamba tunaelewa ni nini ilikuwa ikitendeka wakati kitabu fulani kiliandikwa.

 

(ii) Pili tunaona kwamba ilichukua miaka mingi ndipo Biblia iandikwe.  Baada ya Musa kuandika kitabu cha Mwanzo, miaka 1,600 ilipita kabla ya Yohana kuandika kitabu cha Ufunuo.  Hii inamaanisha kwamba Biblia iko na hadithi mingi za kihistoria.  Siyo kitabu tu ambacho kinazungumza kuhusu miaka michache ya kihistoria, ni kitabu ambacho kinazungumza kuhusu miaka  mingi ya kihistoria wakati mambo mengi yaliwatendekea watu wa Mungu.

 

3. Je, waandishi wa Biblia walikuwa akina nani?

 

Kitu cha ajabu ni mchanganyiko wa watu ambao waliiandika Biblia.  Kwa kawaida hakuna kitabu hapa ulimwenguni ambacho kimeandikwa na watu 40.  Pengine tunaweza kupata kitabu ambacho kiliandikwa na watu watano au sita.  Lakini siyo jambo rahisi kupata kitabu ambacho kimeandikwa na watu 40 ambao waliishi kwa muda wa miaka 1,600 na walikuwa tofauti kabisa.  Ukitazama wale wote ambao walihusishwa kwa kuandika Biblia utaona jambo hili likiwa la ukweli.  Musa ambaye aliandika vitabu vya kwanza vitano alilelewa katika nyumba ya mfalme wa Misri na baadaye aliishi katika jangwa miaka 40 akiwachunga kondoo na baadaye aliwaongoza Waisraeli kutoka Misri.  Paulo ambaye aliandika barua 13 katika Agano Jipya alitoka katika mji wa Tarso ambao haukuwa katika nchi ya Uisraeli, alipata mafunzo yake kule Yerusalemu na alikuwa mtu ambaye alishikilia sana dini ya Kiyahudi kabla ya kuokoka kwake akiwa njiani akienda Damasko.  Petro naye alikuwa mvuvi wa samaki kwa bahari ya Galilaya ambaye alitembea na Yesu wakati alipokuwa hapa ulimwenguni.  Baadaye alimkana Yesu, lakini baadaye alisamehewa na siku ya Pentekote alihubiri na watu 3,000 wakaokoka.  Daudi ambaye aliandika Zaburi alikuwa kijana mdogo ambaye alikuwa akichunga kondoo wa babake na baadaye alikuwa mfalme wa Uisraeli.  Alipigana vita nyingi za Mungu na pia alianguka katika dhambi mbaya sana ya uzinzi na uuaji.  Amosi ambaye aliandika kitabu kimoja kati ya manabii, alikuwa mchunga kondoo na Mathayo alikuwa mtoza ushuru ambaye alikuwa akishirikiana na watenda dhambi (Mathayo 9:9-13).  Hawa ni baadhi ya wale watu karibu 40 ambao waliandika Biblia.

 

Kuna mafunzo mawili ya kujifunza kutokana na haya:

 

(i) Tunajifunza kwamba watumishi wa Mungu ni watu wa kawaida.  Ukweli ni kwamba, kwa kawaida hakuna kitu cha maana kutoka kwa Petro, Yakobo na Mathayo.  Walikuwa watu wa kawaida ambao waliishi Uisraeli na waliitwa na Mungu kufanya kazi kubwa.  Pia Daudi alikuwa mchungaji wa wanyama wa kawaida na huenda kama Mungu hangemwita angeendelea kuwa mchungaji wa mifugo maishani mwake mwote.  Mara mingi sisi huwaza kwamba mtu akitaka kuwa mtumishi wa Mungu lazima awe mtu ambaye anajulikana ulimwenguni na pia amesoma sana.  Lakini jambo hili si la ukweli.  Mungu huwaita watu wa kawaida na kuwatumia kwa utukufu wake.

 

(ii) Tunajifunza kwamba Biblia ni kitabu ambacho kiko na vitabu tofauti tofauti kwa sababu kimeandikwa na watu tofauti tofauti.  Kila mtu atakayesoma Biblia atapata kwamba iko na kitu cha kumfaidi.  Mtu ambaye amesoma sana akisoma Biblia atapata maandishi ya Paulo yakiwa ya manufaa sana na ambayo yatampa changamoto katika maisha yake.  Mtu ambaye ameanguka katika dhambi mbaya sana akisoma Biblia, atapata katika Zaburi za Daudi himizo kubwa sana na ni jinsi gani mtu huyu anaweza kusamehewa na Mungu.  Kama mtu anahitaji maagizo kuhusu jinsi gani anaweza kuishi maisha matakatifu katika ulimwengu atapata mengi kutoka katika kitabu cha Petro ambaye aliishi maisha ya kawaida katika ulimwengu kabla hajaokoka.

4. Je, ni kwa nini watu hawa waliandika Biblia?

 

Hili ni swali muhimu sana kwetu kwa sababu linatusaidia katika kufafanua Biblia.  Tunajua kwamba Musa aliandika kitabu cha Mwanzo, Luka aliandika Matendo ya Mitume, Paulo aliandika 2 Timotheo na Yohana aliandika Ufunuo.  Swali ni kwa nini?  Kwa nini Paulo aliandikia Timotheo barua?  Kwa nini Musa aliandika Mwanzo wakati Waisraeli walikuwa katika jangwa?  Kuna sababu tano muhimu kwa nini vitabu vya Biblia viliandikwa.

 

(i)  Vitabu vingine viliandikwa ili kuwafunza watu wa Mungu.  Kitabu cha Mwanzo kiliandikwa kuwafunza Waisraeli kwamba Mungu ambaye aliwaokoa kutoka Misri kwa utumwa Yeye si sanamu ambayo haina nguvu yoyote kama zile sanamu za Wamisri; kwani Yeye ni muumba wa dunia na mbingu.  Na pia kwamba hayuko mbali, bali alikuwa na agano na mababu zao na hii ndiyo sababu aliwaokoa kutoka Misri.  Musa aliandika kitabu hiki cha Mwanzo kufundisha kwamba Mungu alikuwa na mpango wa kuwaokoa watu wake na hii ndiyo sababu alikuwa na agano na Abrahamu.  Kitabu cha Warumi kiliandikwa kufafanua jinsi mwanadamu mwovu machoni pa Mungu Mtakatifu anaweza kufanywa mwenye haki mbele yake; na kitabu cha Waebrania kiliandikwa kuonyesha kwamba Agano Jipya ni bora kuliko Agano la Kale kwani Kristo ndiye msingi wa Agano Jipya.

 

(ii) Kuna vitabu vingine katika Biblia ambavyo viliandikwa kuwasaidia wakristo wakati wako na matatizo.  Kanisa la Korintho lilikuwa na matatizo mengi katika maisha yao ya kila siku na pia walikuwa na mambo mengi ambayo walikuwa wamechanganyikiwa nayo.  Wakati Paulo alisikia mambo haya, aliandika waraka wa 1 Wakorintho kwa minajili ya kutatua matatizo hayo walikuwa wakikumbana nayo.  Jambo hili pia ni la ukweli kwa barua ya Wagalatia na Wakolosai.

 

(iii) Kuna vitabu vingine katika Biblia ambavyo maisha ya mkristo yamezungmziwa kuwahimiza  wakristo wengine.  Mfalme Suleimani aliishi maisha ambayo yalijawa na mafunzo makubwa kwa wakristo wote.  Kwa hivyo aliongozwa na Roho Mtakatifu kuandika vitabu kama vile Methali na Mhubiri.  Vitabu hivi vimejawa na maagizo kwetu jinsi tunavyofaa kuishi maisha yetu hapa ulimwenguni na jinsi tunafaa kufanya wakati tuko katika hali ngumu.  Zaburi pia ziliandikwa na watu ambao walikuwa katika hali ngumu za maisha na walimwita Mungu na aliwasikia na kuwapa msaada wake.

 

(iv) Kuna vitabu vingine katika Biblia ambavyo Mungu anapeana maagizo fulani kwa watu wake.  Kwa mfano, katika kitabu cha Walawi watu wa Mungu wanaambiwa jinsi wanafaa kumwabudu Mungu.  Hili pia ni kweli kwa vitabu vyote vya Unabii.  Manabii walitumwa na Mungu na maagizo fulani kwa watu wake: kuwa watu walifaa kutubu dhambi zao na kumrudia Mungu (Yeremiah 25:1-5).

 

(v) Kuna vitabu vingine katika Biblia vya historia ambavyo viliandikwa ili watu wa Mungu wajue matendo ya ajabu ya Mungu wao ambayo aliyatenda siku za kale.  Hivi vitabu vimeandikwa ili tupate mwelekeo, kuhimizwa na kuonywa.  Vitabu vingi vya kihistoria katika Agano la Kale na kile cha Matendo ya Mitume vyote viko katika kikundi hiki.  Vitabu vinne vya injili (Mathayo, Marko, Luka na Yohana) pia vinazungmza kuhusu matendo na mafunzo ya Yesu Kristo kama himizo na mwelekeo wa maisha ya wakristo.

 

Hizi ni sababu tano kuu kwa nini waandishi wa Biblia waliiandika vitabu hivi.  Tunapotaka kufafanua kifungu fulani katika Biblia, swali la kwanza tunafaa kujiuliza ni, “Kwa nini mwandishi aliandika kitabu hiki?”  Hii ni kwa sababu kusudi la mwandishi litamwongoza msomaji kufafanua.  Msomaji hawezi kufafanua kile ambacho mwandishi hakukusudia kusema.  Hili ni jambo la kawaida siku za leo kwani watu wengi wanafafanua kile mwandishi hakukusudia kuandika.  Unapopata barua na kuisoma na kujaribu kufahamu ni nini inasema, ni lazima ujiulize ni kwa nini umetumiwa?  Ukifafanua kile ambacho mwandishi hakusudia, utakuwa umefanya makosa makubwa.  Kwa njia hiyo hiyo ni lazima tujiulize kwanza, “Ni nini mwandishi anasema hapa na ni nini anamaanisha hapa?”

 

5. Je, ni lugha gani ambazo zilitumiwa kuandika Biblia?

 

Biblia iliandikwa katika lugha tatu; na kwa lugha hizi hakuna lugha ambayo bado inatumika.  Karibu Agano la Kale lote liliandikwa kwa lugha ya Kiebrania.  Kuna vifungu vitatu katika Agano la Kale ambavyo havikuandikwa katika lugha ya Kiebrania bali viliandikwa katika lugha ya Aramaiki: Ezra 4:6-8,18; Ezra 7:11-26 na Danieli 2:4-7:28.  Agano Jipya liliandikwa katika lugha ya Kigiriki.

 

Muhtasari wa Funzo la Nne

 

Katika funzo hili tumetazama maswali matano ambayo yalikuwa yatusaidie kuelewa ni nani aliyeandika Biblia na ni kwa nini iliandikwa.  Maswali ambayo tumetazama ni haya:

 

1. Je, ni watu wangapi ambao Mungu aliwatumia kuandika Biblia?

 

2. Je, watu hawa waliishi lini?

 

3. Je, watu hawa ambao waliandika Biblia walikuwa akina nani?

 

4. Je, ni kwa nini watu hawa waliandika Biblia?

 

5. Je, ni lugha gani ambazo zilitumiwa kuandika Biblia?

 

 

 

Funzo la Tano: Je, tutasoma na kujifunza Biblia aje?

 

Maswali haya mawili ndiyo muhimu sana ambayo mtu yeyote anaweza kuuliza. Tangu tuanze mafunzo haya ninajua kwamba hadi sasa tumejifunza mambo mengi kuhusu Biblia.  Kuna mambo mengi kuhusu Biblia ambayo unajua sasa.  Lakini akili hii yote ni bure kama hutasoma na kujifunza Biblia mwenyewe.  Kuna watu wengi nchini mwetu ambao husema kwamba wao ni wakristo lakini watu hawa huwa hawasomi na kujifunza Biblia.  Katika mafunzo haya tutatazama jinsi tunafaa kufanya mambo haya.

 

1. Kusoma Biblia kibinafsi.

 

Kuna mambo fulani unafaa kufanya ili ufaidike kutokana na kusoma Biblia yako.

 

1. Soma Biblia kwa maombi.  Kumbuka kwamba ni neno la Mungu na tunaweza kulifahamu kama tutapata usaidizi kutoka kwa Mungu mwenyewe.  Kabla hujaanza kusoma, omba kwamba Mungu atakufunza kutoka kwa neno lake na pia kwamba atakupatia uwezo wa kutii yale ambayo unasoma.

 

2. Soma Biblia kila siku.  Usiwe mtu ambaye anasoma kifungu kimoja cha Biblia siku moja halafu uache kusoma kwa siku kadhaa.  Hakikisha kwamba una wakati wa kusoma Biblia kila siku.  Njia mwafaka ya kusoma Biblia ni kutenga muda kila siku kwa ajili ya kusoma Biblia, labda asubuhi au wakati wa mchana au jioni.  Usisome Biblia wakati umechoka.  Utakapoendelea kufanya hivi kila siku utazoea na hii itakuwa tabia ya kawaida kwako.

 

3. Soma kitabu kimoja bila kurukaruka.  Watu wengine wanasoma kifungu kutoka kwa Injili ya Yohana leo na kesho watasoma kifungu kingine kutoka kwa kitabu cha Yoshua.  Usifanye hivi kwani wewe hutafaidika kabisa.  Jambo la maana ni kusoma Biblia yote kitabu kwa kitabu.  Hakikisha uko na kitabu na kalamu na uandike mahali yale mambo ambayo umejifunza au yale ambayo huelewi ili umwulize mtu ambaye ataweza kukusaidia.  Utapata kwamba unavyosoma Biblia kila mwaka kufahamu kwako kutaongezeka.

 

4. Soma Biblia kwa hekima.  Kuna watu ambao wanapenda tu vitabu kama kile cha Danieli na Ufunuo.  Kwa hivyo kila mara wanaposoma Biblia wanasoma tu vitabu hivi.  Hili silo jambo la hekima.  Vitabu vya Danieli na Ufunuo ni mojawapo wa vile vitabu vigumu katika Biblia.  Kuna vitabu ambavyo ni rahisi kuelewa katika Biblia.  Anza kusoma vitabu vya injili kama kile cha Marko.  Pia siyo jambo la busara kusoma Biblia jinsi vitabu vinavyofuatana.  Usianze na kitabu cha Mwanzo, halafu Kutoka, halafu Walawi, halafu Hesabu na tena Kumbu Kumbu la Torati.  Bali njia mwafaka ya kusoma Biblia ni kuhakikisha unasoma vitabu vya aina tofauti tofauti za Biblia. Kama ndipo umemaliza kusoma kitabu cha Mwanzo itakuwa vyema kusoma kitabu kingine kama kile cha Wafilipi, halafu 1 Samweli halafu Hagai unapoendelea kusoma.

 

5. Soma Biblia na moyo ambao umenyenyekea na uko tayari kufunzwa.  Shida kubwa sana ambayo tuko nayo leo katika nchi yetu ni jinsi watu wanavyosoma Biblia.  Kuna maelfu ambao wanasoma Biblia kila siku, lakini wanaisoma kwa njia isiyofaa.  Hawasomi neno la Mungu kwa moyo mnyenyekevu na ambao uko tayari kufunzwa.  Wanasoma Biblia kama mioyoni mwao wameshikilia mambo yao ambayo wanaamini hata kama Biblia haisemi hivyo; hawasomi Biblia wakitaka kufunzwa.  Watu wa aina hii wameamua kwamba yale wanaamini ni ya ukweli na hawako tayari kujua kama mawazo yao ni uongo.  Hii ni njia mbaya sana ya kusoma neno la Mungu.   Biblia ilipeanwa ili itufunze na kwa hivyo tunahitaji kusoma Biblia tukitazamia kufunzwa.  Ikiwa Biblia haikubaliani na mawazo yetu, basi lazima tuwe tayari kuacha mawazo yetu na kufuata Biblia pekee.

 

2. Kusoma Biblia na jamii yako.

 

Kama uko na jamii, basi unahitaji pia kusoma Biblia nao.  Hili ni jukumu ambalo kulingana na Biblia limepewa baba.  Biblia inasema, “Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana” (Waefeso 6:4).  Hapa kuna maelezo kuhusu ni jinsi gani unaweza kusoma Biblia na jamii yako.

 

1. Someni Biblia kila siku.  Msisome Biblia na jamii yako siku moja halafu mwache kwa siku kadhaa halafu msome tena.  Hivi hamtaweza kufaidika kabisa.  Hakikisheni kwamba mnasoma Biblia kila siku.

 

2. Someni Biblia kama jamii kwa maombi.  Mwanzeni na maombi kwa Mungu awasaidie mwelewe neno lake na pia baada ya kumaliza masomo ombeni.

 

3. Chagueni wakati mzuri wa masomo haya.  Msikae hadi kuwe usiku sana kwani watoto watachoka na watalala.  Kumbuka kwamba jukumu la kufunza watoto wenu ni amri ambayo imetoka kwa Mungu na kwa hivyo ni lazima izingatiwe sana.  Siyo vyema kusema kila wakati, “Niko na kazi mingi kwa hivyo siwezi kuwafunza.”  Ikiwa Mungu ametuamrisha kufanya jambo fulani, mambo mengine maishani mwetu ni lazima yafanyike baada ya kufanya kile Mungu ameamuru.

 

4. Chagueni kitabu kimoja cha Biblia na mkisome hadi mwisho.  Msisome tu kifungu kimoja kutoka kwa kitabu fulani na kesho msome kifungu kingine kutoka kwa kitabu kingine.  Watoto wako wanahitaji kujua kwamba kila kitabu cha Biblia kiliandikwa kwa kusudi na kina ujumbe muhimu.  Anza na kitabu ambacho siyo kigumu kuelewa kama kitabu cha Marko na msome kifungu kutoka kwa kitabu hiki kila siku.  Hakikisha kwamba kila mtu wa jamii yako ako na Biblia na wanafuata jinsi unavyosoma. Ukiwa na watoto ambao ni wakubwa na wanaweza kusoma, waulize pia wasome wakati mko pamoja kama jamii.

 

5. Kuwa na hekima wakati unafunza jamii yako.  Usianze kuhubiri kwa muda mrefu baada ya kusoma kifungu.  Ni muhimu pia kuuliza maswali na kujadiliana kwa yale ambayo mmesoma.  Ukihubiri kwa muda mrefu watoto wako wanaweza kuchoka ikizingatiwa kwamba ni wadogo au wanaenda shuleni; na pia mjue kwamba wanaweza kuchukua masomo haya kama jukumu bali siyo njia ya kujifunza Biblia ambayo ni neno la Mungu.

 

3.Kujifunza Biblia.

 

Kujifunza Biblia ni tofauti na kusoma Biblia.  Kwa kusoma Biblia kila siku unaweza kusoma sura moja.  Kwa kujifunza Biblia unaweza maliza muda mwingi katika kifungu kimoja cha Biblia ukitaka kuelewa mafunzo ambayo yaliyomo na jinsi unaweza kukifunza.  Hapa kuna jinsi unaweza kujifunza Biblia.

 

1. Chagua kitabu kimoja cha Biblia ambacho unataka kujifunza kwa siku kadhaa au miezi kadhaa. Kama ni wakati wako wa kwanza kufanya hivi chagua kitabu kifupi ambacho kinaeleweka haraka. Kwa mfano kitabu cha Wafilipi au 1 Wathesalonike kwa sababu vitabu hivi ni rahisi kuelewa na ni vifupi.

 

2. Kwanza kabisa soma kitabu chote ukiandika chini yale mafunzo ambayo unapata.  Hii itakusaidia kujua ni nini kitabu hiki kinasema na ni nini Mungu anasema.

 

3. Ikiwa unaweza, jaribu kusoma vitabu vingine kuhusu kitabu cha Biblia ambacho unataka kujifunza.  Unaweza kupata kamusi ya Biblia ambayo inaweza kukusaidia sana.

 

4. Anza kusoma kitabu hicho cha Biblia kifungu kwa kifungu.  Pia unaweza gawa vifungu hivyo; kwa mfano: Wafilipi sura 1:1-2 salamu za mwandishi; mistari ya 3-11 maombi ya Paulo kwa ajili ya kanisa la Wafilipi, na mambo mengine.  Kwa njia hii unaweza kugawa kitabu kulingana na jinsi kilivyoandikwa kikigusia mambo tofauti tofauti.  Tazama kifungu chote kwa maombi, ukitaka kujua ni nini mwandishi alikuwa akisema, na ni vipi kinakuzungumzia wewe.

 

Utapata kwamba mara ya kwanza unapojifunza kitabu kimoja hutaelewa kila kitu.  Usiache jambo hili likutatize.  Kumbuka kwamba ni kupitia kwa kusoma kitabu hiki mara kwa mara ndipo utaelewa ni nini Biblia inasema.

 

4. Mafunzo zaidi kuhusu kusoma na kujifunza Biblia.

 

1.  Ni vyema kujijua kwamba unaweza kusoma kiasi gani.  Kuna watu ambao wanasoma sura nne au tano kwa siku na kwa njia hii wanaweza kusoma Biblia nzima kwa mwaka mmoja.  Kama unaweza kufanya hivi, hilo ni jambo zuri sana.  Lakini kama huwezi usisome kiasi kikubwa ambacho huwezi kuelewa kwa sababu hutafaidika.  Ukipata kwamba wewe unaweza kusoma sura moja kwa siku, basi fanya hivyo: bora uelewe ni nini unasoma.  Kumbuka kwamba unasoma Biblia ili ufaidike kiroho.  Kwa njia hiyo unaposoma Biblia na jamii yako, usiwaze kwamba ni lazima usome sura moja kila siku.  Utapata kwamba kwa mistari michache kuna mambo mengi, na ni vyema kusoma mistari michache kuliko mingi na ukose kufahamu chochote.

 

2. Tenga wakati mwema na uzingatie.  Kusoma Biblia kila siku ni tabia ambayo tunahitaji kujifunza.  Usipozoea tabia hii hutawahi kusoma Biblia kila siku.  Njia moja ya kuzoea tabia fulani ni kufanya jambo moja kila siku wakati sawa.  Baada ya muda mchache utapata kwamba umezoea tabia hiyo na kuifanya bila kusukumwa.  Kwa njia hiyo hiyo hakikisha kwamba masomo ya Biblia ya kila siku katika jamii yako inakuwa mazoeo.  Chagua wakati ambao watoto hawajachoka na uwe wakati ambao kila siku ndiyo utakuwa wakati wa masomo ya Biblia.  Na pia lazima uwe wakati ambao hamtasumbuliwa na marafiki wenu.

 

3.Tafuta aina ya Biblia ambayo ni mzuri kwa kusoma na kujifunza.  Ukienda kwa maktaba ya kikristo utapata kwamba kuna aina nyingi za Biblia.  Tafuta moja ambayo imetafsiriwa vizuri na lugha yake unaielewa vyema.  Biblia ambayo imetafsiriwa na Union Version ndiyo tafsiri mzuri, lakini tafsiri ya Habari Njema ni rahisi kuelewa.  Lakini usitumie ile ya dhehebu la MASHAHIDI WA YEHOVAH (JEHOVAH'S WITNESSES), au wale wanajiita MORMONS.  Kwani, kitabu chochote kile ambacho hakiambatani na mafunzo ya Biblia hakifai kusomwa.

 

4. Tafuta usaidizi kutoka kwa vitabu vingine.  Sisi wakristo tumebarikiwa sana kwa sababu kuna vitabu vingi vizuri ambavyo vinaweza kutusaidia kusoma na kufafanua Biblia.  Kuna vitabu ambavyo vitakuwezesha kuelewa Biblia kwani vimeandikwa vikifafanua kitabu kwa kitabu katika Biblia.  Kuna pia vitabu vingine ambavyo vimeandikwa vikifafanua kila mstari wa Biblia.  Vitabu hivi vitakusaidia kuelewa Biblia unapoisoma.  Lakini ni lazima uwe mwangalifu wakati unatumia vitabu vingine, kwa sababu siyo vitabu vyote vinaweza kukusaidia.  Kuna vitabu vingi ambavyo vinafundisha mafunzo mabaya.  Kwa hivyo hakikisha kwamba unasoma vitabu ambavyo vinakujenga kiroho.

 

5. Tafuta wakristo wengine wa kusoma nao Biblia.  Ni jambo la muhimu sana kusoma Biblia na wakristo wengine.  Kwa hivyo ukiwa na marafiki na majirani ambao wameokoka na wanapenda kusoma neno la Mungu, panga mkusanyike pamoja ili msome neno la Mungu.

 

Muhtasari wa Funzo la Tano

 

Katika somo hili tumetazama mambo manne kuhusu jinsi gani tunaweza kusoma na kujifunza Biblia.

 

1. Kusoma Biblia kibinafsi

 

2. Kusoma Biblia na jamii yako

 

3. Kujifunza Biblia

 

4. Mafunzo zaidi kuhusu kusoma na kujifunza Biblia

 

 

Funzo la Sita: Je, tunawezaje kufafanua Biblia?

 

Tumeona kwamba Biblia ni neno la Mungu.  Hii inamaanisha kwamba ni lazima tuwe waangalifu sana wakati tunaifafanua.  Hili ni neno la Mungu kwa mwanadamu, na kwa hivyo ni muhimu kwamba tunalielewa.  Tukikosa kuwa waangalifu katika kufafanua kwetu, makosa mengi yatapatikana katika ufafanuzi wetu.  Watu watachanganyikiwa kuhusu mambo ya wokovu, pia kuhusu maisha ya utakatifu na jinsi wanafaa kukumbana na dhambi.

 

Tukitaka kufafanua Biblia kuna maswali matano tunafaa kuzingatia sana.  Maswali haya yatatusaidia sana kufafanua Biblia kwa njia inayofaa.

 

1. Je, ni nini mwandishi alitaka kusema wakati aliandika kifungu hiki?

 

Kumbuka kwamba katika Funzo la Kwanza tulitazama swali “Biblia ni nini?” tuliona kwamba Biblia iliandikwa na Mungu akishirikisha wanadamu.  Kwa ufupi ni kwamba wanadamu ambao waliandika Biblia walihusishwa na Mungu katika kazi hii.  Kwa hivyo tunapokuwa tunafafanua maandiko yoyote, kanuni ambayo tunafaa kuzingatia ni kifungu kinafaa kufafanuliwa jinsi mwandishi alivyomaanisha.  Kwa hivyo tusifafanue kinyume na kusudi la mwandishi.  Kwa hivyo swali la kwanza tunafaa kujiuliza ni, “Je, mwandishi alikusudia nini wakati aliandika kifungu hiki?”  Hii ndiyo sababu ni muhimu sana kwetu kuelewa kusudi la mwandishi alipoandika kitabu chake.   Tukijua ni kwa nini kitabu fulani kiliandikwa, tutaweza kujua kwa nini kifungu fulani katika kitabu kile kiliandikwa.

 

2. Je, mwandishi alipanga kitabu chake vipi?

 

Hili ndilo swali ambalo linafaa kufuata lile la kwanza.  Ili uweze kufafanua kifungu vyema, unahitaji kujua ni kwa nini mwandishi aliandika kifungu hicho, ni kwa nini aliandika kitabu hicho na ni kwa nini amefuata mpangilio fulani wa uandishi katika kitabu chake.  Kwa mfano, Warumi 4:1-5, tunasoma kifungu hiki na tunaona kwamba hapa Paulo anazungumza kumhusu Abrahamu.  Je, ni nini Paulo alikuwa anawaambia Warumi?  Ili tuweze kujibu swali hili ni lazima tujiulize maswali mengine mawili: ni kwa nini Paulo aliwaandikia Warumi kitabu hiki?  Mpangilio wa kitabu hiki ni upi?  Wakati tunajifunza kitabu hiki, tunaona kwamba kiliandikwa kwa ajili ya kuwaeleza wakristo ambao walikuwa katika mji wa Roma kwamba mtu anafanywa mwenye haki kwa kupitia kwa imani pekee ndani ya Kristo.  Paulo aliandika kitabu hiki akieleza kwamba tunaokolewa si kwa matendo yetu mazuri bali ni kwa imani pekee ndani ya Kristo Yesu.

 

Baada ya kujibu swali hilo la kwanza tunaweza sasa kujibu lile la pili, je, mpangilio wa Paulo ni upi?  Tunapotazama kitabu hiki tunaona kwamba baada ya utangulizi katika mistari 17 ya kwanza, Paulo anaonyesha jinsi kizazi chote cha mwanadamu kimeanguka katika dhambi mbaya sana machoni pa Mungu (Warumi 1:18-3:20).  Tunaona tena akituonyesha kwamba jibu la Mungu kwa dhambi za mwanadamu ni mafunzo muhimu, yaani tunaokolewa kwa imani pekee (Warumi 3:21-31).  Baadaye katika sura ya 4 anaanza kuongea juu ya Abrahamu na Daudi.  Kwa nini?  Jibu ni kwamba anataka kutuonyesha kwamba watu wa Mungu katika Agano la Kale hawakuokolewa kwa sababu ya matendo yao mazuri, lakini kwa imani pekee.  Hii ndiyo sababu ananukuu kitabu cha Mwanzo 15:6 katika kitabu cha Warumi 4:3.

 

Kwa hivyo tunaona kutokana na haya kwamba maswali haya mawili yanaenda pamoja: ni nini mwandishi alitaka kutufundisha na ni vipi alipanga kitabu chake?  Baada ya kuona sababu ya kitabu kuandikwa, na jinsi kitabu kimepangwa, tunaweza kujua ni nini mwandishi alitaka kusema katika kila kifungu.

 

3. Je, ni nini mwandishi anasema katika kifungu hiki?

 

Baada ya kuona ni nini mwandishi anataka kusema katika kifungu, tunahitaji kusoma kifungu kwa makini ili tujue kabisa kile anasema.  Kuna mambo mawili tunahitaji kufanya ili tujue kabisa ni nini mwandishi anasema.

 

(i) Tazama kwa makini yale maneno ambayo anatumia.  Sisi sote tunajua kwamba maneno yako na umuhimu na kwa hivyo ni vyema kujua kabisa ni nini kila neno linamaanisha katika kifungu hicho. Bila kufanya hivi hatutawahi kujua ni nini mwandishi anasema.

 

(ii) Kwa makini tazama lugha ya mifano ambayo anatumia.  Kwa mfano, katika kitabu cha 2 Timotheo 2:4, Paulo anasema, “Mwanajeshi vitani hujiepusha na shughuli za maisha ya kawaida, ili aweze kumpendeza mkuu wa jeshi.”  Tunajua kwamba Paulo hakuwaandikia barua hii kwa wanajeshi ambao walikuwa vitani, bali alikuwa anawaandikia wakristo.  Katika mstari huu anatumia lugha ya mifano mara tatu:  mwanajeshi ni mkristo, mkuu wa jeshi ni Kristo na mambo ya kawaida ni yale ambayo ni ya ulimwengu huu.  Biblia imejawa na lugha ya aina hii na ni lazima tuwe waangalifu sana wakati tunafafanua Biblia.

 

4. Je, vifungu vingine katika Biblia vinahusikaje na kifungu hiki?

 

Biblia ni kitabu kikubwa na kimejaa mafunzo mengi sana kwa kila mwanadamu.  Kwa hivyo wakati tunafafanua kifungu chochote, ni lazima tutilie maanani vifungu vingine ili tusije tukafafanua vibaya.  Kwa mfano, mfano wa kondoo na mbuzi katika kitabu cha Mathayo 25:31-46.  Unaposoma bila kuwa makini, ni rahisi kusema kwamba mfano huu unafunza kwamba mtu anaweza kuokolewa kwa kufanya matendo mazuri.  Kwa sababu inaonekana kwamba mfano huu unasema kwamba wale ambao walifanya matendo mazuri kama kuwalisha maskini, kuwavalisha wale waliokuwa uchi na kuwatembelea wagonjwa watapata nafasi mbinguni kwa sababu ya matendo yao mazuri.  Lakini tunafaa kuelewa kwamba Biblia haifunzi hivi.  Biblia ni wazi kuhusu wokovu kwamba ni kwa imani pekee ndani ya Kristo watu huokoka, na kwamba wakati tumeokolewa, matendo mazuri ni hakikisho ya wokovu wetu.  Kwa hivyo ufafanuzi wa mfano huu siyo kwamba matendo mazuri yatafanya tuokolewe na tuingie mbinguni, bali wale ambao wameokolewa na Kristo watafanya matendo haya kama hakikisho ya wokovu wao kwamba ni wokovu wa kweli.

 

Kwa sababu tunafaa kutilia maanani Biblia yote wakati tunaifafanua, ni lazima tuielewe Biblia vyema kabisa.  Mtu ambaye amepewa kipaji cha kufunza na kuhubiri Biblia anahitaji kujua mafunzo ya Biblia kabisa ili asije akafanya makosa.

 

5. Je, kifungu hiki kinasema nini kutuhusu leo, na tunafaa kufanya nini kutokana na ukweli ambao uko katika kifungu hiki?

 

Tazama kwamba maswali haya ni ya mwisho.  Ni tabia ya watu wengi wakati wanaposoma Biblia, kujiuliza kwanza, “Je, ni nini Mungu anasema kunihusu?”  Hili ni swali muhimu lakini siyo swali tunafaa kujiuliza kwanza.  Ni lazima kwanza tufafanue kifungu vyema ndipo tujiulize swali hili.  Kwa mfano, sisi sote tunajua mfano wa msamaria mwema katika kitabu cha Luka 10:30-37.  Kwa hivyo tunajua mfano huu unasema nini kutuhusu leo kwa sababu Yesu anasema, “Nendeni na mfanye hivyo” (mstari wa 37).  Je, ni vipi tunafaa kutii baada ya kupata ukweli huu?  Katika mfano huu tunaelezwa kuhusu mtu ambaye alikuwa amevamiwa na wezi na kupigwa vibaya sana na alikuwa akilala barabarani.  Watu wawili, yaani kuhani na yule kutoka katika kabila la walawi, walimpita bila kumsaidia.  Labda kuhani aliwaza kwamba angefanyika mchafu kulingana na dini yake kwa kumgusa kwa sababu mtu yule alionekana kama amekufa.  Labda yule wa kabila la walawi alitoa sababu kwamba alikuwa anahitajika katika hekalu.  Lakini msamaria mwema alikuja na akamsaidia mtu yule.  Tunapotazama kwa nini Yesu alipeana mfano huu,  tunapata kwamba alikuwa akijibu swali “Ni nani jirani yako?”  Biblia inatuambia tuwapende jirani zetu, lakini jirani yangu ni nani?  Kifungu hiki kinatupatia jibu kwamba jirani ni mtu yeyote ambaye anahitaji msaada wetu.  Hatufai kutoa sababu za kikabila au kidini au za kijamii au za kirafiki.  Fikiria juu ya mchungaji wa kanisa moja ambaye ako njiani kuenda kanisani na yeye ni kabila fulani na anapatana na mtu ambaye anatoka katika dhehebu la kiislamu na ako na hitaji.  Je, mchungaji anafaa kufanya nini?  Je, anafaa kusema, “Sitamsaidia, mimi niko njiani kuenda kanisani kuhubiri!”  Je, anafaa kujiwazia, “Mtu huyu siyo wa kabila langu na pia yeye ni muislamu.  Je, ni kwa nini nimsadie?”  Jibu ni kwamba hafai kuwaza hivi.  Anafaa kumsaidia yule mtu haijalishi kabila wala dini au kitu chochote kile.  Huu ndiyo ufafanuzi wa mfano huu kwetu leo.

 

Muhtasari wa Funzo la Sita

 

Katika somo hili tumejifunza jinsi ya kufafanua Biblia.  Tumeona kwamba ili tufafanue Biblia vyema, ni lazima tujiulize maswali matano.

 

1. Je, mwandishi alitaka kusema nini wakati aliandika kifungu hiki?

2. Je, mwandishi alipanga kitabu chake vipi?

3. Je, ni nini mwandishi anasema katika kifungu hiki?

4. Je, vifungu vingine katika Biblia vinahusikaje na kifungu hiki?

5. Je, kifungu hiki kinasema nini kutuhusu leo, na tunafaa kufanya nini kutokana na ukweli ambao uko katika kifungu hiki?

 

 

Funzo la Saba: Je, ni jinsi gani tutaihubiri Biblia?

 

Katika somo hili tutaangazia jinsi tunafaa kuhubiri Biblia.  Kuhubiri Biblia ndilo jukumu kubwa zaidi ambalo Mungu amewapatia watumishi wake.  Mhubiri ako na jukumu la kuwaambia watu ni nini Mungu anasema kupitia kwa neno lake na ni jinsi gani neno hilo linazungumza juu ya maisha yao.  Hana uhuru wa kusema jinsi anavyofikiria.  Mhubiri ni mtumishi ambaye anafaa kusema yale Bwana wake amemwambia aseme kwa watu wake.

 

Jambo tunafaa kukumbuka ni kwamba njia mzuri ya kuhubiri au kufunza Biblia ni kuhubiri kitabu kimoja kutoka mwanzo hadi mwisho.  Mara mingi mhubiri anajipata kwamba anahubiri katika kitabu kimoja Jumapili hii na katika kitabu kingine Jumapili ijayo.  Kuhubiri kwa aina hii hakuwezi kuwafaidi watu sana.  Ni vyema kama mhubiri anahubiri katika kitabu kimoja toka mwanzo mwa kitabu hicho hadi mwisho wake.

 

Kuna mambo manne ambayo mhubiri anafaa kufanya  ili aweze kuhubiri neno la Mungu vyema kwa watu.

 

1. Ni lazima tufafanue vyema kifungu ambacho tunaenda kuhubiri.

 

Kama tulivyoona katika Funzo la Kwanza, hili ni jambo muhimu kwa sababu mhubiri lazima ajue ni nini Mungu anasema katika kifungu hicho.  Hadi atakapojua ni nini Mungu anasema kwa neno lake, hawezi kamwe kuhubiri ukweli.  Fikiria juu ya mfanyabiashara ambaye anamtuma ajiri wake na ujumbe fulani.  Ajiri lazima ahakikishe kwamba anaelewa vyema ujumbe kabla hajaenda.  Kwa sababu yeyote ile asipoelewa ujumbe ule basi hawezi akaupeleka kwa kuwa haelewi ni nini ametumwa kufanya.  Lazima amwulize mwajiri wake amweleze vizuri ujumbe ule ili aweze kupeleka ujumbe ambao ameelewa.  Kwa njia hiyo hiyo wahubiri ni watumishi wa Mungu ambao wanafaa kuhubiri neno la Mungu jinsi alivyowatuma.  Ikiwa hawahubiri neno la Mungu basi siyo Mungu ambaye amewatuma.  Hatuwezi kuhubiria watu wa Mungu mawazo yetu badala ya ukweli ambao unapatikana katika neno la Mungu.  Kufanya hivi ni dhambi kwani hatuhubiri kile ambacho Mungu mwenyewe ametuamuru tuhubiri bali tunahubiri mawazo yetu na kujifaidisha.

 

2. Ni lazima tuwe na mpangilio wakati tunaandaa mahubiri yetu.

 

Watu wa Mungu ni lazima wahubiriwe kwa njia ambayo wakienda nyumbani wanaweza kukumbuka yale ambayo wamefunzwa.  Ni lazima tuwe waangalifu katika mpangilio wetu ili mtu anapoulizwa ni nini amehubiriwa awe anaweza kukumbuka.  Kwa kawaida wanadamu hukumbuka mambo ambayo yamewekwa katika mpangilio fulani.  Kama mhubiri atazungumza tu kwa muda wa dakika 40 kuhusu jambo fulani, itakuwa vigumu sana kwa watu kukumbuka yale aliyosema.  Lakini kama mhubiri atakuwa na mpangilio mzuri wa ujumbe wake basi itakuwa rahisi kwa watu kuelewa na kukumbuka ujumbe wake.  Kwa ujumbe mwema utakuwa na mada na mpangilio mwema ambao watu wanaweza kuelewa kwa urahisi.

 

Kwa mfano Wakolosai 1:13-14, kifungu hiki kinasema kwamba, “Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi.  Kwake Yeye tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.”  Mtu ambaye anahubiri katika kifungu hiki ni lazima afafanue kifungu kwanza ili ajue kifungu hiki kinasema nini, kuwa kinazungumza kuhusu nini Mungu alifanya wakati alituokoa.  Kwa hivyo atapanga ujumbe wake kwa njia hii:

 

Mada: Ni nini Mungu alifanya wakati alituokoa.

Kwanza: Alituokoa kutoka kwa nguvu za giza.

Pili: Alituleta katika ufalme wa Mwanawe.

Tatu: Alituokoa kutoka kwa dhambi kupitia Kristo.

Nne: Alitusamehe dhambi zetu kupitia Kristo.

 

Mwishowe ni lazima watu wajue ni jinsi gani wataishi kulingana na mafunzo haya.

 

3. Ni lazima tuhubiri Kristo Yesu.

 

Kumbuka kwamba Kristo ndiye ujumbe mkuu katika Biblia na hakuna mtu yeyote atawahi kuokolewa hadi atakapokuja kwa Yesu amsamehe dhambi zake.  Kwa hivyo mahubiri yetu lazima yaelekeze watu kwa Kristo Yesu.

 

4. Ni lazima tuhubiri kwa makini na kwa uangalifu sana.

 

Mhubiri anapomaliza kufafanua kifungu na kutayarisha ujumbe wake, basi anabakia na kazi muhimu ya kuhubiri ujumbe huo.  Kusimama mbele ya umati na kuhubiri ni kazi muhimu sana na siyo kazi ambayo tunafaa kukosa kufanya kwa makini.  Mhubiri anafaa kufikiria sana juu ya mavazi ambayo anavaa na jinsi anavyoongea.  Mhubiri hafai kuwa na tabia ambayo itafanya neno la Mungu likashifiwe; anafaa kufanya kila awezalo kuhakikisha kwamba neno la Mungu linahubiriwa kwa uaminifu na kwa uangalifu sana kwa watu wa Mungu.

 

Kumbuka kwamba kila wakati ni lazima tumwombe Mungu atuongoze na atusaidie kuwa wajasiri na tuweze kueleweka wakati tunapohubiri; kwa sababu ni neno lake siyo letu.

 

Muhtasari wa Funzo la Saba

 

Katika somo hili tumeona kwamba njia mzuri ya kuhubiri neno la Mungu ni kuhubiri kitabu kwa kitabu badala ya kuhubiri mstari moja hapa na mwingine pale.  Kuna njia nne ya kuhubiri Biblia.

 

1. Lazima tufafanue vyema kifungu ambacho tunafunza.

2. Lazima tupange mafundisho yetu kwa njia ambayo watu watatuelewa wakati tunafunza.

3. Lazima tuhubiri Kristo akiwa ujumbe mkuu wa Biblia.

4. Baada ya haya yote, tuhubiri ujumbe huo kwa watu wa Mungu.