Header

NI NINI BIBLIA INAFUNDISHA KUHUSU MAMBO YA MWISHO.

 

Utangulizi.

 

Katika kijitabu hiki tutajifunza ni nini Biblia inafundisha kuhusu mambo ya mwisho.  Tunapojifundisha kuhusu mambo ya mwisho, kuna mambo mawili muhimu sana ambayo tunaangalia: Mambo haya mawili ni kifo na kurudi kwa Bwana Yesu Kristo.  Kwa hivyo kijitabu hiki kimengawanywa katika sehemu mbili.  Katika sehemu ya kwanza tutajifundisha kuhusu kifo na katika sehemu ya pili, tutajifundisha kuhusu kurudi kwa Yesu Kristo duniani.

 

Sehemu ya Kwanza, ni nini Biblia inafundisha kuhusu kifo.

 

Funzo la kwanza, Warumi 5:12-17, Wafilipi 1:20-26.  Jinsi Biblia inafundisha kuhusu kifo.

 

Katika funzo hili tunaangalia vifungu viwili muhimu sana ambavyo Mtume Paulo aliandika, yaani Warumi 5:12-17 na Wafilipi 1:20-26.  Tafadhali hakikisha umesoma vifungu hivi kabla ya kuendelea na somo hili.  Hivi vifungu viwili vinatufundisha mambo manne kuhusu kifo.

 

1. Kifo kiliingia duniani kwa sababu ya hukumu wa Mungu.

 

Paulo anasema, “Kwa hivyo kama vile dhambi ilivyoingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja na kupitia dhambi hii, mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote wamefanya dhambi” (Warumi 5:12).  Paulo anafundisha hapa kwamba wakati Mungu aliwaumba Adamu na Hawa, hakuwaumba ili miili yao iwe ni ya kufa.  Kama Adamu na Hawa hawangefanya dhambi, wao pamoja na wajukuu wao wangeishi maisha ya milele duniani.  Lakini walifanya dhambi na kwa hivyo Mungu akawahukumu, na sehemu moja ya hukumu hii ni kwamba miili yao haitaishi milele bali itakufa, “Kwa jasho la uso utakula chakula chako hadi utakaporudi ardhini, kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo, kwa kuwa wewe ni mavumbi na mavumbini wewe utarudi” (Mwanzo 3:19).

 

Hii ndiyo sababu kifo ni shida kubwa sana kwa kila mwanadamu.  Kila wakati mtu akifa tunajua ndani mwetu kwamba jambo fulani baya limefanyika, tunajua kwamba jambo fulani baya limetendeka ambalo hatukutarajia litendeke.  Hii ndiyo sababu hatuwezi kuona kifo kuwa jambo la kawaida.  Mara mingi utasikia jamii ambayo imewapoteza wapendwa wao wanne au watano kwa mwaka.  Kila wakati mtu anapokufa katika jamii hiyo kunakuwa na kilio sana.  Haiwezekani kwamba baada ya mtu wa kwanza na wa pili kufa basi jamii hiyo itazoea mambo ya kifo na hawatakuwa wanahuzunika wanapofiwa.  Wanadamu wamekuwa katika dunia hii kwa miaka maelfu sasa lakini hawajazoea kifo, kifo ni shida kubwa sana kwa kila mmoja wetu.  Hivi sivyo Mungu alipanga wakati aliumba mwandamu.  Kifo kiliingia duniani  kwa sababu ya dhambi ya mwanadamu na kila wakati kifo kinatukumbusha kwamba tumefanya dhambi mbele za Mungu na kwamba tuko katika hukumu wa Mungu.

 

2. Kristo Yesu alishinda kifo kwa kufa na kufufuka.

 

Paulo anaandika, “Kwa maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mtu mmoja, yaani, Yesu Kristo” (Warumi 5:17).  Wakati Biblia inasema kwamba Kristo Yesu alishinda mauti kwa kifo chake msalabani, huwa inamaanisha mambo mawili.

 

(i) Kwanza, inamaanisha kwamba Bwana Yesu alishinda kifo cha kiroho kwa kifo chake mwenyewe.  Wakati Adamu na Hawa walifanya dhambi katika bustani la Edeni, wao walikufa kiroho, yaani walitengana na Mungu.  Wakati Mungu aliwaumba, wao walikuwa watoto wake na walikuwa na ushirika naye.  Lakini wakati walifanya dhambi, walianza kijificha ili Mungu asiwaone, hii ni kwa sababu walikuwa wametengana na Mungu na sasa walikuwa wamekufa kabisa kiroho.  Hii ndiyo hali ambayo kila mtoto wa Adamu na Hawa aliyomo, yaani tumezaliwa tukiwa tumekufa kiroho (Waefeso 2:1).  Sisi sote tunazaliwa tukiwa  hatuna Kristo, bila tumaini, wala Mungu humu duniani (Waefeso 2:12).  Wakati Bwana Yesu Kristo alining’inia msalabani alikuwa ametengana na Mungu kwa niaba yetu ili tusiendelee kutengana na Mungu.  Yesu Kristo  alilia, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” (Mathayo 27:46), ili sisi tusiwahi kuachwa na Mungu bali tupatanishwe naye milele.

 

(ii) Pili, inamaanisha kwamba Bwana Yesu alishinda uoga wa kifo kupitia kufa na kufufuka kwake.  Kabla Yesu hajakufa msalabani, watu wote wa dunia walikuwa katika utumwa wa kuogopa mauti (Waebrania 2:15).  Lakini kupitia kwa kifo chake na kufufuka kwake, Bwana Yesu Kristo ameshinda kifo na akaondoa uoga wa kifo kwa watu wake.  Kifo hakingeweza kumzuilia, Yeye ametoa nguvu za kifo ili kisiweze kuwazuia watu wake kwa uoga.

 

Sababu kuu ya watu kuogopa kifo ni kuwa hawajui ni nini kinafanyika baada ya mtu kufa.  Kwa wale ambao hawajaokoka, hakuna  ulinzi na hakuna faraja baada ya kufa, hii ndiyo sababu wanaogopa kifo sana na watafanya chochote ili waweze kuepuka kifo.  Lakini kwa wale ambao wameokoka kifo kwao siyo tisho.  Wao wanajua kwamba wameokoka na  kwamba wamesamehewa dhambi zao kwa hivyo watakapokufa wataenda mbinguni.  Wale ambao wameokoka na wanaogopa kifo cha mwili wanapaswa kufikiria sana kuhusu kifo cha Bwana Yesu na jinsi alivyoangamiza uoga wa kifo na kuwahakikishia watu wake wokovu wa milele.  Wale wote ambao wameokoka, kifo kwao ni mlango wa kuingia kwa Mungu (Wafilipi 1:20-26).  Hii ndiyo sababu Biblia inasema, “Kifo cha watakatifu kina thamani machoni pa Bwana” (Zaburi 116:15).  Kifo  cha  mtu ambaye ameokoka kina thamani sana machoni pa Mungu kwa sababu kinamtoa mtoto wake mpendwa kutoka kwa ulimwengu huu wa dhambi na kumpeleka kuwa naye milele.

 

Hii inamaanisha kwamba mtu ambaye ameokoka mawazo yake kuhusu kifo ni tofauti kabisa na mtu ambaye hajaokoka.  Mtu ambaye hajaokoka hapendi kufa na kwa hivyo ataogopa hata kutaja neno kifo.  Lakini mtu ambaye ameokoka yeye si hivyo.  Wakati Paulo aliwaandikia barua wafilipi, alikuwa karibu kufa, na hivi ndivyo alisema, “Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo na kufa ni faida.  Kama nitaendelea kuishi katika mwili, hii ni kwa ajili ya matunda ya kazi.  Lakini sijui nichague lipi?  Mimi sijui!  Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi” (Wafilipi 1:21-23).  Paulo hakuogopa kifo, bali alikuwa anatamani kufa kwa sababu alitarajia kuwa naye Kristo.  Hivi ndivyo mkristo anafaa kuwaza kuhusu kifo.  Mkristo hafai kuogopa kifo ama kuogopa kuzungumza kuhusu kifo.  Hawazi kwamba akiongea kuhusu kifo, atakufa.  Tunapaswa kuwa tayari kufa ikiwa ni  mapenzi ya Bwana Yesu.

 

3. Mungu pekee ndiye anathibiti kifo.

 

Katika kitabu cha Wafilipi 1:19-20 Paulo anaandika kuhusu maisha yake akiwa korokoroni.  Anasema katika mistari hii kwamba kuna uwezekano kwamba atauawa kwa  sababu ya imani yake.  Katika kifungu hiki chote Paulo anaeleza wazi kwamba ikiwa atauawa ama ataendelea kuishi, yote yatakuwa mapenzi ya Mungu na haitakuwa mpango wa mtu mwingine yeyote.  Anasema kwamba ikiwa yeye ataendelea kuwa hai basi itakuwa faida kwa watu wa Mungu hapa ulimwenguni na hiyo ndiyo sababu alikuwa na tumaini kwamba ataendelea kuishi (Mstari 25 ).  Paulo hasemi, “Mimi ninataka kuendelea kuishi duniani, lakini shetani anao watu wake wengi na wataniua hata kama Mungu anataka niendelee na  kuishi.”  Hili ni jambo muhimu sana kwetu sisi watu wa Mungu.  Kuna watu wengi sana hapa nchini mwetu ambao wanaamini kwamba ikiwa ajali limetokea, ama wakati mtu fulani amekufa kwa sababu ya ugonjwa, basi ni shetani ambaye anasababisha mambo hayo ya kifo.  Watu hawa watasema kwamba Mungu  hakuwa anataka kifo hicho kitokee lakini shetani amekisababisha.  Hii ni kama kusema kwamba Mungu hakuwa na nguvu za kumzuia shetani kusababisha kifo hicho.  Hii si kweli.  Mungu ndiye anatawala mbinguni na duniani, na chochote kinachofanyika humu duniani huwa kinafanyika kwa mapenzi ya Mungu.  Ikiwa Mungu  hataki jambo fulani lifanyike, basi jambo hilo haliwezi kufanyika kamwe, hata shetani ama mwanadamu akijaribu namna gani.  Kifo cha mtu ambaye ameokoka na kifo cha mtu ambaye hajaokoka, vyote vinathibitiwa na Mungu mwenyewe.  Ni Mungu pekee anaamua ni lini mtu fulani atakufa.

 

4. Kifo ndiyo mwisho wa shughuli zote kabisa za mwanadamu duniani.

 

Katika kitabu cha Wafilipi 1:23 Paulo anasema, “Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo.”  Ni wazi  hapa kwamba wakati mtu anakufa anaondoka kutoka duniani na anamaliza shughuli zake zote hapa duniani.  Kuna watu wengi ambao wanaamini kwamba mtu akifa, roho yake huwa inarudi duniani na kuwa na ushawishi kwa wale walio hai ulimwenguni.  Hii ndiyo sababu watu wengi wako makini sana kupeleka mwili wa yule amekufa nyumbani na kufanya mambo fulani ya kimila, halafu kuuzika mwili kwa njia ya utaratibu fulani.  Watu hawa wanaamini kwamba ikiwa hautamfanyia kimila vizuri mtu ambaye amekufa basi roho yake, yaani yule ambaye amekufa itarudi katika hiyo jamii na kuanza kutatiza jamii hiyo.  Biblia haifundishi kitu chochote kama hiki.  Biblia inasema wazi kwamba mtu akifa huwa anamaliza shughuli zake zote za hapa duniani.  Unaweza kuuzika mwili wake mahali popote unataka jinsi wewe mwenyewe unaona inafaa, hii haiwezi kuleta mabadiliko kwako ama kwa jamaa waliofiwa.

 

Funzo la pili,  Luka 16:19-31, Biblia hapa inafundisha ni nini kinafanyika baada ya mtu kufa.

 

Tafadhali hakikisha umesoma  kitabu cha Luka 16:19-31 kabla hujaendelea na somo hili.  Katika mfano huu tunaona funzo muhimu na la kushangaza kuhusu ni nini kinafanyika wakati watu wanakufa.  Tunasoma mambo haya katika kifungu hiki:

 

1. Mtu anapokufa, mwili na nafsi zitengana.

 

Tunasoma katika mfano huu, “Yule tajiri naye akafa na akazikwa.  Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake” (mistari 22-23).  Yule tajiri alikufa na akazikwa lakini alienda jahanum.  Je, hii ilifanyika namna gani?  Jibu ni kwamba mwanadamu anazo sehemu mbili, yaani mwili na nafsi.  Wakati wa kifo, mwili ndiyo unakufa.  Wakati wa kufa, nafsi huwa inatengana na mwili, kwa hivyo mwili unazikwa ndani ya udongo na unaoza lakini nafsi inaendelea kuishi milele.

 

2. Nafsi ya mtu ambaye ameokoka inaenda kuishi na Bwana Yesu Kristo.

 

Hivi ndivyo Biblia inamaanisha wakati inasema kuhusu kukaa pamoja na Abrahamu.  Lazaro ambaye alikuwa maskini sana alikufa na akaenda mbinguni punde tu alipokufa.  Nafsi ya mtu ambaye ameokoka haiendi mahali fulani ambapo hapajulikani bali inaenda mbinguni.  Hii ndiyo  sababu Paulo alisema, “Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo” (Wafilipi 1:23).  Hii ndiyo sababu Bwana Yesu Kristo alimwambia mwizi msalabani, “Leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso” (Luka 23:43).  Kuna mambo mawili muhimu sana hapa ambayo tunafaa kukumbuka.

 

(i) Biblia inafundisha kwamba wokovu unapatikana kwa imani pekee ndani ya Kristo pekee.  Lazaro alienda mbinguni kwa sababu alikuwa na imani ndani ya Kristo pekee, siyo kwa sababu alikuwa maskini.  Kuna watu ambao wanaamini kwamba, mtu akifa bila msamaha wa dhambi zake, kuna mahali ambapo atapelekwa kwa muda fulani ili ahukumiwe, na baada ya muda huo, Mungu atamchukua na kumingiza mbinguni.  Hii si kweli.  Ukweli ni  kwamba ikiwa mtu hajaokoka, mtu huyo hawezi kuingia mbinguni, awe aliishi maisha ya umaskini ama maisha ya ugonjwa kila wakati hapa ulimwenguni.  Ni wale tu ambao wameokoka ndiyo wataingia mbinguni.

 

(ii) Pili, kumbuka mtu anaweza kuwa na mali nyingi hapa duniani, lakini hiyo haimaanishi kwamba mtu huyo amepata baraka za Mungu.  Yule alikuwa tajiri katika mfano huu, “Alivaa nguo za rangi ya zambarau na katani safi, ambaye aliishi kwa anasa, kila siku” (mstari 19).  Chakula alichokula kila siku kilikuwa kizuri sana kwamba huyu maskini Lazaro alitamani tu kula kile ambacho kilianguka kutoka mezani kwa sababu kilikuwa kizuri kuliko kile chake alichokuwa anakula kila siku.  Hii yote haimaanishi kwamba huyu tajiri alikuwa na baraka za Mungu, hii haimaanishi kwamba Mungu alipendezwa na maisha ya tajiri huyu na ndiyo sababu alimbariki na mali nyingi.

 

Ukweli ni kwamba tajiri huyu alikuwa hajaokoka na kwa hivyo  ghadhabu ya Mungu ilikuwa juu yake.  Hii ndiyo sababu baada ya kufa alienda mahali pa  mateso milele.  Mtu anawezakuwa tajiri sana akiwa hapa ulimwenguni lakini hiyo haimaanishi kwamba anazo baraka za Mungu.  Lazaro naye alikuwa maskini sana, lakini hiyo haimaanishi kwamba alikuwa amelaaniwa na Mungu.  Lazaro alikuwa na baraka sana kwa sababu alikuwa ameokoka na hiyo ndiyo sababu wakati alikufa alienda mbinguni.  Funzo ambalo tunapata hapa ni wazi, kwamba hatuwezi kujua hali y akiroho ya mtu kwa kuangalia jinsi alivyo katika maisha yake hapa ulimwenguni.  Tumeona tajiri ambaye alifurahia maisha ya anasa na ghadhabu ya Mungu ilikuwa juu yake na baada ya kufa alienda jahanum.  Yule ambaye alikuwa maskini wa kuomba-omba ambaye maisha yake hapa duniani yalijawa na matatizo mengi alikuwa ameokoka na alikuwa na baraka za Mungu, kwa hivyo baada ya kufa alienda mbinguni.

 

3. Nafsi ya mtu ambaye hajaokoka inaenda mahali pa mateso milele baada ya kufa.

 

Kama vile nafsi ya mtu ambaye ameokoka huwa inaenda mbinguni akifa, vivyo hivyo nafsi ya  mtu ambaye hajaokoka inaenda jahanum wakati anakufa.  Tunaelezwa wazi katika kifungu hiki, “Yule tajiri naye akafa na akazikwa.  Kule kuzimuni alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, “naye Lazaro alikuwa karibu naye (mstari 22-23).  Kuna mafundisho mawili ambayo tunafundishwa hapa kuhusu huyu tajiri.

 

(i) Tunafundishwa kwamba punde tu mtu ambaye hajaokoka amekufa huwa anaenda jahanum, na hakuna njia hata moja anaweza kuingia mbinguni.  Yule tajiri alimwuliza Abrahamu  kama Lazaro anaweza kumletea maji.  Abrahamu alimjibu, “Kati yetu nanyi huko, kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu” (mstari 26).  Kuna mamilioni ya watu hapa duniani leo ambao wamefundishwa kwamba watu wa jamii zao, ama marafiki wao ambao walikufa wako mahali ambapo ni pa kutakasa dhambi zao, na kwa hivyo wakiwaombea ama wakipeana pesa kwa kanisa ili ibada maalum ifanywe kwa ajali yao, basi wataachiliwa kutoka mahali pa kutakasia dhambi na kuingia mbinguni.

 

(ii) Tunafundishwa hapa kwamba mtu hawezi akabeba mali yake aliyokuwa nayo hapa duniani na kuondoka nayo wakati anakufa.  Huyu tajiri, “Aliishi kwa anasa, kila siku” (Msitari 19), hii inamaanisha alikuwa anakula chakula kizuri sana na kunywa vizuri kinywaji alichotaka.  Lakini alipokuwa jahanum, hakuwa hata na tone la maji na alimsihi Ibrahimu amtume Lazaro ili amletee tone moja la maji.  Mali yake yote aliyokuwa nayo hapa ulimwenguni haingeweza kumsaidia. Alikuwa anahitaji kubwa sana lakini mali yake haingemsaidia hata kidogo: Biblia inasema, “Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu” (1 Timotheo 6:7).

 

4. Mtu ambaye hajaokoka hawezi akaona faida ya kuokoka hadi baada ya kufa.

 

Huyu tajiri aliishi maisha ya dhambi hapa ulimwenguni, hakujali kutubu dhambi zake na kupata wokovu wa Yesu Kristo.  Aliupenda ulimwengu huu  na vitu vilivyomo ulimwenguni na alifurahia sana mambo ya anasa.  Kuna watu wengi sana leo hii kama huyu tajiri.  Wanajua kweli kwamba Mungu anawaita waje kwake ili wapate wokovu, lakini wanapenda dhambi zao sana, na wanaupenda ulimwengu huu na hawataki kamwe kuacha anasa za ulimwengu na kwa hivyo wanaendelea na maisha yao bila kuokoka.  Baada ya huyu tajiri kufa, alijua jinsi alivyokuwa mjinga.  Alijua kwamba alifurahia anasa za dunia hii za dhambi kwa muda mfupi na sasa anaishi milele katika mateso makali sana.  Tajiri huyu hakujua mambo haya hadi alipofariki na hangeweza kufanya chochote kwa sababu muda haukuwepo.

 

Hivi ndivyo watu wale ambao hawajaoka walivyo, hawajui umuhimu wa wokovu hadi wakati wamekufa.  Wanafurahia anasa za dhambi maishani mwao mwote wakitumaini kwamba Mungu atawakubali waingie mbinguni wakifa.  Huu ni ujinga.  Ikiwa hujaokoka, basi hutaingia mbinguni kwa sababu ungali uko katika dhambi zako.  Unahitaji kutubu dhambi zako na uje kwa Yesu leo.  Ukikataa kutubu na kuja kwa Yesu, basi kama huyu tajiri utateseka jahanum milele.

 

Sehemu ya pili, ni nini Biblia inafundisha kuhusu kurudi mara ya pili duniani kwa Yesu Kristo.

 

Funzo la Tatu, 2 Wathesalonike 2:1-12, ishara za kurudi kwa Bwana Yesu Kristo.

 

Bwana Yesu Kristo alisema wazi katika mafundisho yake kwamba hakuna mtu yeyote anajua siku ya kurudi kwake humu duniani (Mathayo 24:36), lakini kuna mambo ambayo yatafanyika hapa ulimwenguni kabla ya Yesu Kristo kurudi.  Mambo haya tunayasoma katika kifungu hiki.  Sababu kuu ya mtume Paulo kuandika kifungu hiki ni kwamba kulikuwa na watu katika kanisa la Thesalonike ambao walikuwa wakisema kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwepo (mstari 2).  Kwa hivyo Paulo aliwaandikia akiwaeleza kwamba hivyo si kweli, na kwamba siku ya kuja kwa Bwana haitafanyika hadi mambo fulani yatendeke.

 

1.  Uasi utatokea kwanza (mstari 3).

 

Paulo anaandika, “Mtu ye yote na asiwadanganye kwa namna yo yote kwa maana siku ile haitakuja mpaka uasi utokee kwanza.”  Paulo hasemi jambo lingine kuhusu jambo hili, anasema tu, “Mpaka uasi utokee.”  Neno “uasi” ambalo Paulo anatumia linamaanisha “kafiri” ama “Mtu ambaye amejiondoa katika mambo ya Mungu.”  Inaonekana kwamba kile Paulo anasema ni kwamba watu wengi watasikia injili ya Yesu Kristo na kudai kwamba wameokoka na kumwamini Bwana Yesu Kristo, lakini wengi hawatakuwa wakristo wa kweli.  Wengi wao watadanganyika kwamba wao ni wakristo na wengine watawadanganya watu wa Mungu kuwa wameokoka.  Kabla ya Bwana Yesu Kristo kurudi watu hawa wataacha kabisa kudai kuwa wao wameokoka na wataacha kabisa mambo ya Yesu Kristo.  Mtume Yohana aliandika kuhusu watu hawa, “Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu hasa.  Kwa maana kama wangelikuwa wa kwetu, wangelikaa pamoja nasi, lakini kutoka kwao kulionyesha kwamba hakuna mmoja wao aliyekuwa wa kwetu” (1 Yohana 2:19 ).

 

2.  Mtu wa kuasi atadhihirishwa kwanza (mstari 3-8).

 

Paulo anaandika, “Mtu ye yote asiwadanganye kwa namna ye yote kwa maana siku ile haitakuja mpaka uasi utokee kwanza na yule mtu wa kuasi adhihirishwe.”  Paulo hasemi mambo mengi kuhusu tukio hili, anasema tu, “Mpaka uasi utokee kwanza na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa” (mstari 3).  Inaonekana kulingana na kifungu hiki kwamba siku moja kuna mtu atadhihirishwa ambaye Biblia inamwita “Mtu wa uasi.”  Tunahitaji kujua kwamba huyu atakuwa mwanadamu kamili.  Katika kifungu hiki Paulo anatueleza mambo matatu kuhusu huyu mtu wa uasi.

 

(i) Katika mstari wa nne Paulo anatueleza ni nini mtu huyu atafanya: “Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.”  Huyu mtu wa uasi atakataa mamlaka yote, hasahasa mamlaka ya Mungu Mmoja wa kweli aliye hai.  Yeye mwenyewe atajitunikia mamlaka na heshima ambayo inafaa kupewa Mungu pekee, na kwa sababu yeye ni mwasi wa Mungu atawatesa watu wa Mungu na wale wote wamwabuduo Mungu wa kweli.

 

(ii) Katika mstari 5-7 Paulo anatueleza kwamba huyu mtu wa uasi atadhihirishwa, “Yule anayezuia ataendelea kufanya hivyo mpaka atakapoondolewa.”  Je, ni nani huyu ambaye anayezuia uasi na ataendelea kufanya hivi mpaka aondolewe?  Jibu rahisi na la kweli kabisa ni kwamba hatujui ni nani.  Paulo alikuwa amewafundisha watu wa kanisa la Thesalonike jambo hili tena na kwa hivyo hapa haelezi mambo mengi.  Inaonekana kwamba hapa Paulo anaeleza kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu inayoendelea hapa ulimwenguni.  Roho Mtakatifu hakuja tu kuwadhihirishia watu wa Mungu dhambi zao na kuwaokoa, bali pia anahakikisha kwamba kuna mpangilio mzuri wa haki unaendelea ulimwenguni.  Hii ni neema ya Mungu ambapo anahakikisha kwamba viongozi wa mataifa wanaongoza kwa haki na kwa uaminifu na kwamba watu wanafuata sheria ya nchi.  Wakati wa kuja kwa Yesu Kristo kutakapokaribia, Yule anayezuia nguvu za uasi ataregeza kazi yake ya kuzuia huyu mtu wa uasi na kwa hivyo sheria itavunjwa na mtu wa uasi atapata nguvu na kujulikana sana.

 

(iii) Katika mstari wa nane, Paulo anaeleza kuhusu kuangamizwa kwa mtu huyu wa uasi, “Ambaye Bwana Yesu atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa ufunuo wa  kuja kwake.”  Ufunuo wa kuja kwa Bwana Yesu Kristo utamwangamiza kabisa huyu mtu mwasi.  Uwepo mtakatifu wa Mungu ni hali ya kutisha sana kwa wale wote wafanyao maovu na ni lazima wote watoroke.  Huyu mtu wa uasi ataondoka baada ya kuona kwamba Bwana Yesu Kristo amekuja.

 

3.  Injili itahubiriwa kwa mataifa yote.

 

Bwana Yesu Kristo aliongea kuhusu jambo hili katika kitabu cha Mathayo 24:14 aliposema, “Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni pote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote.  Ndipo ule mwisho utakapokuja.”  Bwana Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake wahubiri injili ulimwenguni kote, na Biblia inaeleza wazi kwa Bwana Yesu hatarudi hadi watu wake wote waokolewe kutoka kwa dhambi zao na kuletwa ndani ya ufalme wake (2 Petro 3:9).  Hii ndiyo sababu kazi ya kuhubiri injili inahitajika kufanywa kwa haraka na kwa bidii.

 

Funzo la nne, Mathayo 24:42-25:46, Jinsi tunafaa kuishi tukitanzamia kurudi kwa Bwana Yesu Kristo.

 

Katika kifungu hiki, Bwana Yesu anafundisha kuhusu kurudi kwake duniani mara ya pili na jinsi sisi watu wake tunafaa kuwa tayari kwa tukio hili.  Kuna mifano minne katika kifungu hiki.

 

1. Tunapaswa kuwa wafanyikazi waaminifu na wenye hekima hadi mwisho (24:42-51).

 

Katika kifungu hiki tunasoma kuhusu mfanyakazi ambaye ni mwovu (mstari 48-51).  Hii ni habari ya mtu mmoja tajiri ambaye alikuwa na nyumba kubwa na wafanyakazi wengi.  Tajiri huyu  alikuwa anaenda safari, na kwa hivyo akamwacha mfanyakazi mmoja kuwasimamia watumishi wengine.  Kazi ya huyu msimamizi ilikuwa kuhakikisha kwamba wale wengine wamefanya kazi yao inavyostahili na kuwalipa mishahara yao.  Kwanza huyu mtumishi alifanya kazi yake kwa uaminifu.  Lakini baada ya muda akaanza kuwaza, “Bwana wangu atakawia muda mrefu,” na kwa hivyo “akaanza kuwapiga watumishi wenzake na kula na kunywa pamoja na walevi” (mstari 48-49).  Lakini siku moja, bwana wa huyu mtumishi akaja siku ambayo mtumishi hamtarajii na akampata anaishi maisha ya dhambi na akamkatakata vipande vipande (mstari 51).

 

Lengo kuu la mfano huu ni kuwahimiza wale wote ambao wameokoka kuwa waaminifu katika kufanya kazi ya Bwana Yesu.  Wale ambao wamechaguliwa kuwa wachungaji na viongozi kama huyu mtumishi wanapaswa kuwa waaminifu katika kazi zao.  Kana huyu mtumishi, kuna wengi ambao wanaanza kazi yao vizuri sana wakimwa makini na waaminifu.  Lakini wanapoendelea wanasahau kwamba siku moja Bwana Yesu atarudi na kwamba wataeleza jinsi waliishi maisha yao na vile walimtumikia Bwana Yesu.  Ni jambo mbaya sana kwa watumishi wa Yesu kuvutwa na tamaa ya pesa na mamlaka.  Jambo hili linawafanya wasiwe wafanyakazi waaminifu, kwa sababu wanaanza kuishi  maisha ya  dhambi badala ya kuwa wafanyikazi waaminifu kwa Bwana.  Wachungaji hawa uanza kuharibu vyeo vyao na pesa ambazo wamepewa kama tu huyu msimamizi alivyofanya.  Mtu kama huyu hataingia mbinguni kwa sababu yeye hajaokoka: Bwana Yesu atamwita mtu huyu mnafiki na atamhukumu jahanum milele (mstari 51).  Mfano huu unatukumbusha kwamba ni wale tu ambao watavumilia hadi mwisho ndiyo wataokoka (Mathayo 24:13).

 

2.  Tunapaswa kuwa tayari hadi mwisho tukigojea kuja kwa Bwana Yesu (25:1-13).

 

Katika kifungu hiki tunasoma kuhusu karamu ya arusi.  Inaonekana kwamba mila za wakati wa Yesu alipokuwa duniani bwana arusi alikuwa anaenda kwa bibi arusi, akifika mlangoni alikuwa anakutana na marafiki wake ambao wanamwongoza katika karamu ya arusi.  Pia inaonekana wakati wa karamu ya arusi hii bwana arusi alichelewa na kwa hivyo marafiki wa bibi arusi walihitaji kuwa na mafuta ya taa wanapomgoja.  Walikuwa wanawali kumi waliokuwa wanamgoja bwana arusi.  Wote walikuwa na taa zao zikiwa na mafuta, lakini ni watano tu walikuwa na mafuta ya akiba.  Bwana arusi alichelewa sana hadi saa sita usiku (mstari 6).  Wakati alipokuja wanawali walihitajika kuwakisha taa zao na kumkaribisha bwana arusi.  Wale watano ambao walikuwa na mafuta ya akiba walikuwa tayari, lakini wale wengine watano hawakuwa tayari kumkaribisha bwana arusi kwa sababu hawakuwa na mafuta ya taa zao.  Wale watano waliokuwa tayari ndiyo walikaribishwa na kuingia na bwana arusi katika karamu ya arusi, wale wengine watano waliambiwa, “Siwajui ninyi” (mstari 12).  Bwana Yesu alimalizia mfano huu kwa kusema, “Kwa hivyo kesheni, kwa sababu hamjui siku wala saa” (mstari 13).

 

Mfano huu unatufundisha kwamba ni lazima tuwe waangalifu na tuwe tayari kungoja kuja kwa Bwana Yesu.  Wale ambao wameokoka watakuwa waangalifu na wataakuwa tayari kwa sababu Mungu anaendelea kufanya kazi ndani mwao na atahakikisha kwamba wao wako tayari kumgojea Kristo.  Wale ambao wanadai kuwa wameokoka na bado hawajaokoka kwa kweli wako kama hawa wanawali watano wajinga.  Hawa wanawali walikuwa katika karamu ya kumkaribisha bwana arusi lakini wao wenyewe hawakuwa tayari.  Kuna watu ambao wanadai kuwa wameokoka na kwamba wao ni wa jamii ya ufalme wa Mungu hapa duniani, na wanamgojea Bwana Yesu arudi.  Lakini Bwana Yesu atakaporudi, itadhihirika kwamba hawatakuwa tayari kwa sababu hawatakuwa wameokoka.

 

 

3. Tunapaswa kuhakikisha kwamba tunatumia vipawa vyetu kwa kufanya kazi ya Mungu (25:14-30).

 

Katika kifungu hiki tunasoma kuhusu mfano wa talanta.  Hii ni hadithi ya mfanyi biashara mmoja ambaye alisafiri na kuacha mali yake kwenye uangalizi wa watumishi wake watatu.  Aliporudi alipata kwamba watumishi wake wawili walifanyisha kazi ile mali aliwapa na wakamletea faida, lakini yule mtumishi wa tatu hakuifanyia kazi ile mali alipewa bali aliichimbia shimo ardhini na kuificha.  Huyu bwana alifurahishwa sana na wale watumishi wawili waliotumia mali yake vizuri,  lakini alimtupa nje kwenye giza yule mtumishi mwovu na mvivu.

 

Biblia inatueleza wazi kwamba sisi sote tumepewa vipawa na Mungu (Warumi 12:4-8, 1 Wakorintho 4-11, Waefeso 4:7-13).  Ni wazi katika vifungu hivi kwamba Mungu anawapa watu hivi vipawa tofauti tofauti kwa neema na bila malipo yoyote.  Biblia pia inaeleza wazi kwamba tuna jukumu la kutumia vipawa vyetu na hatufai kuzificha.  Mfano huu unatuonyesha kwamba watu ambao wanadai kuwa wameokoka na hawafanyi kazi yoyote ya ufalme wa Mungu hao hawajaokoka.  Wao ni kama huyu mtumishi ambaye alitupwa nje kwenye giza ambako kuna kilio na kusaga meno (mstari 30).  Hii inaonyesha umuhimu wa kila mkristo kujichunguza ili ajue kipawa chake na akitumie kwa utukufu wa Mungu.  Hii pia inaonyesha umuhimu wa wachungaji kuwasaidia washirika wao ili wajue vipawa vyao na kuwasaidia wakue.  Mchungaji ambaye hawaruhusu washirika wake wafanye kazi yoyote kanisani lakini anawaruhusu watu wachache tu kutumika katika kanisa, yeye si mchungaji mwaminifu.

 

4. Tunapaswa kutenda mema humu duniani ili tudhihirishe kwamba imani yetu ni hai (25:31-46).

 

Katika kifungu hiki tunasoma kuhusu kondoo na mbuzi.  Tunaposoma mfano huu ni lazima tujue kwamba hautufundishi kwamba tunapata wokovu wetu kwa kufanya mambo mazuri.  Bwana Yesu mwenyewe alifundisha kwamba kazi zetu nzuri haziwezi kutupeleka mbinguni (Luka 18:9-14), Pia katika sehemu zingine Biblia inaeleza jambo hili wazi (Warumi 3:20-22, Wagalatia 2:15-16, Waefeso 2:8, Wafilipi 3:9).  Tunafaa kukumbuka kwamba tumeokolewa kwa imani pekee ndani ya Yesu Kristo.

 

Biblia pia inatufundisha kwamba mtu ambaye ameokoka ako na imani ambayo ni hai na si imani ambayo imekufa (Yakobo 2:14-26).  Hii inamaanisha kwamba imani yake itamfanya kuwa na upendo kwa wengine na kutamani kuwasadia wengine walio na mahitaji.  Ikiwa mtu hatamani kufanya hivi bali anajijali yeye mwenyewe basi ni wazi kwamba yeye hajui upendo wa Mungu na mtu huyo hajaokoka: “Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo?  Watoto wangu wadogo, tusipende kwa maneno tu, au kwa ulimi bali kwa tendo na katika kweli” (1 Yohana 3:17-18).

 

Mfano wa kondoo na mbuzi unatufundisha kwamba tunapaswa kufanya kazi zetu nzuri kwa kuwasaidia dada zetu na ndugu zetu wakristo.  Hivi ndivyo bwana Yesu anasema kwa watu wake, “Amin amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea Mimi” (mstari 40).  Biblia inasema, “Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio” (Wagalatia 6:10).  Ikiwa mkristo anataka kuwasaidia watu, kwanza anafaa awasaidie wakristo wenzake.  Kwa kufanya hivi yeye anaonyesha kweli imani yake ni imani hai na kwamba ataingia mbingu wakati Bwana Yesu atarudi duniani.

 

Funzo la tano, Yohana 5:28-29; Mathayo 24:36-41.

 

Wakati wa Bwana Yesu kurudi duniani.

 

Swala la kuhusu kurudi kwa Bwana Yesu duniani ni jambo ambalo watu wengi wanalipenda sana, ni swala ambalo watu wengi wametofautiana sana.  Katika funzo hili, tutaangazia katika vifungu viwili, Yohana 5:28-29 na Mathayo 24:36-41.  Katika kila moja ya vifungu hivi tunapata mafundisho ya Yesu mwenyewe.  Tafadhali hakikisha kwamba umevisoma vifungu hivi kabla hujaendelea na funzo hili, na pia hakikisha kwamba unavisoma vifungu hivi pamoja na vingine ambazo vimetaja kwa uangalifu sana.  Haya ndiyo mambo tunayoyasoma katika vifungu hivi.

 

1. Bwana Yesu alisema, “Hakuna ajuaye siku wala saa, hata malaika mbinguni hawajui wala Mwana, ila Baba peke yake.  Kama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.  Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia kwenye safina, nao hawakujua lolote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote.  Hivi ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu” (Mathayo 24:36-39).  Kuna mambo matatu muhimu sana amabayo tunapaswa kukumbuka katika kifungu hiki.

 

(i) Kifungu hiki kinatueleza kwamba hakuna mtu hata mmoja ajuaye siku ya kuja kwa Bwana Yesu Kristo.  Hii inamaanisha kwamba ikiwa mtu anasema kwamba amefanya hesabu fulani kulingana na Biblia, ama ameonyeshwa na Bwana Yesu mwenyewe siku ya kuja kwake, mtu huyo anadanganya, kwa sababu hakuna mtu ajuaye siku wala saa

 

(ii) Wakati Yesu atakaporudi, wengi watapatwa ghafla.  Watu watakuwa wakifanya mambo ya kawaida kama kula na kunywa.  Na kama ilivyokuwa wakati wa Noa, watu watapatwa bila kutarajia.

 

(iii) Siku ile Bwana Yesu atakaporudi wenye dhambi wataondolewa na wenye haki watabaki. Wakristo wengi wamechanganyikiwa sana na jambo hili siku hizi.  Ikiwa tutachunguza Biblia kwa makini, tutapata kwamba mafundisho ya Bwana Yesu Kristo kuhusu jambo hili ni wazi kabisa. Bwana Yesu alisema, “Kama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.  Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia kwenye safina, nao hakujua lolote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote.  Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu.  Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mwingine ataachwa.  Wanawake wawili watakuwa wanasanga pamoja, mmoja atatwaliwa mwingine ataachwa” (Mathayo 24:37-41).

 

Tukisoma kifungu kwa makini, tunaona kwamba katika siku za Noa, wenye dhambi ndiyo walihukumiwa kwa maji ya gharika lakini wenye haki walibaki kuendelea kujaza dunia tena.  Hivi ndivyo itafanyika wakati Bwana Yesu atarudi duniani: kwamba wenye dhambi wataondolewa na wenye haki watabaki.

 

2. Wakati Yesu atakaporudi wale wote walio makaburini watafufuliwa na kupewa miili ya ufufuo.

 

Bwana Yesu alisema, “Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake.  Nao watatoka nje, wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima wa milele na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe” (Yohana 5:28-29).  Katika kifungu hiki Bwana Yesu anasema kwamba siku ile atarudi wale wote ambao wako makaburini watafufuliwa na kupewa miili mipya.  Nafsi ambayo ilitengana na mwili wakati mtu alipokufa itarudishwa tena kuungana na mwili mpya wa ufufuo.  Katika kitabu cha 1 Wakorintho 15:42 mtume Paulo anaeleza kuhusu mwili, “Ule mwili wa kuharibika uliopandwa utafufuliwa usioharibika.”  Mwili ambao tuko nao wakati huu ni mwili wa kuharibika, hii inamaanisha kwamba huu mwili unazeeka, unapatwa na udhaifu na unakufa.  Mwili wa ufufuo utakuwa ni mwili usioharibika, usio dhaifu na hautakufa bali utaishi milele.  Wale ambao walikufa wakiwa wenye dhambi pia watapewa miili ya ufufuo, wao watakuwa milele jahanum wakiwa na miili ambayp haikufi na inahisi uchungu na mateso.  Hii ndiyo sababu mateso ya jahanum ni ya milele, ni kwa sababu wale watakuwa jahanum miili yao haitakufa lakini itapata mateso milele.

 

3. Wale wote watakuwa hai wakati Yesu atarudi watabadilishwa ghafla.

 

Tumeona kwamba wakati Yesu atakuja wale waliokufa watafufuliwa na kupewa miili ya ufufuo.  Je, wale walio hai tayari watafanywa nini Yesu atakaporudi?  Mtume Paulo aliandika, “Sote hatutalala, lakini sote tutabadilishwa ghafla, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho  itakapolia, kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa” (1 Wakorintho 15:51-52).  Kifungu hiki kinaeleza wazi kwamba wale watu watakaokuwa hai siku ya kuja kwa Yesu Kristo watabadilishwa ghafla ili wao pia wapate miili ya ufufuo isiyoharibika.

 

4. Kila mtu atahukumiwa na Bwana Yesu Kristo.

 

Bwana Yesu alifundisha kuhusu jambo hili katika Yohana 5:28-29 aliposema, “Wale waliotenda mema watafufuliwa wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuliwa wahukumiwe.”  Bwana Yesu Kristo alikuja mara ya kwanza kuwaletea watu wake wokovu, na aturudi kuhukumu ulimwengu wote.

 

Funzo la sita, ufunuo 20:11-15, Hukumu wa mwisho.

 

Katika kifungu hiki, tunasoma kuhusu kuja kwa Bwana Yesu duniani na pia tunasoma kuhusu hukumu wa mwisho.  Kuna mafundisho matatu muhimu ambayo tunajinza hapa.

 

1. Ni nani atakayekuwa hakimu siku ya hukumu.

 

Biblia inaeleza wazi kwamba yule atakayekuwa ameketi kwenye kiti kikubwa cha enzi cheupe (mstari 11) atakuwa ni Bwana Yesu Kristo.  Bwana Yesu mwenyewe alisema kwamba Baba alimpa mamlaka yote ya kuhukumu (Yohana 5:27).  Kuna sababu mbili muhimu sana kwa nini Bwana Yesu Kristo ndiye hakimu siku ya hukumu.

 

(i) Kwa sababu wokovu unapatikana kwa imani ndani ya Yesu Kristo pekee.  Biblia inatueleza kwamba, hatupati wokovu kwa sababu ya matendo yetu mazuri bali tunaokolewa kwa imani ndani ya Kristo Yesu pekee (Warumi 3:21-22, Wagalatia 2:16).  Mtu ambaye akija kwa imani ndani ya Yesu Kristo, Roho Mtakatifu atambadilisha ili siku ile Bwana Yesu  atakuja, yeye atafanana na Kristo. Hii ndiyo sababu Bwana Yesu atakuwa hakimu, bali si malaika ama mwanadamu:  Yeye atakuja kuwaokoa watu wake, ambao wanafanana naye.

 

(ii) Kwa sababu ni wale tu walio wakamilifu kama Kristo  ambao wataokolewa.  Watu wengu wanafikiria kwamba wokovu ni  kama kufanya mtihani.  Wanafikiria kwamba ikiwa utafanya bidii sana kuishi maisha mazuri basi utaingia mbinguni.  Lakini Biblia inafundisha kwamba siyo wale wanafanya bidii sana kuishi maisha mazuri na kujaribu sana wataingia mbinguni, bali ni wale ambao wamemwamini Bwana  Yesu Kristo, wale wamepata haki ya Bwana Yesu ndiyo wataingia mbinguni.  Ni wale ambao wamepata ukamilifu wa Bwana Yesu pekee ndiyo wataingia mbinguni. Hii ndiyo sababu Bwana Yesu Kristo atakuwa hakimu wa ulimwengu, na ni wale tu ambao wako wakamilifu kama Yeye ndiyo wataingia mbinguni.  Tunaweza kuwa wakamilifu kama Yeye ikiwa tutaokolewa naye katika imani ndani yake pekee.

 

2. Ni nani watakaohukumiwa.

 

Biblia inaeleza wazi kabisa kwamba jambo la kwanza ambalo Bwana Yesu atafanya wakati atarudi ni kuwakusanya watu wote mbele zake. Halafu awatenganisha wale ambao wameokoka na wale ambao hawajaokoka, “kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi” (Mathayo 25:32).  Bwana Yesu atawapokea walio wake ili wawe naye, halafu atawahukumu wenye dhambi.  Kifungu hiki katika kitabu cha ufunuo kinaeleza kuhusu hukumu ya wale ambao hawajaokoka.  Tunajua huu ndiyo ukweli kwa sababu wanaitwa “wafu”, hili linamaanisha kwamba hawakuwa wamezaliwa mara  ya pili.  Pia tunaelezwa kwamba, “mauti na kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake.”  Hizi ni nafsi za wale walikufa wakiwa hawajaokoka na ambao wanawekwa jahanum wakingojea siku ya Bwana Yesu kurudi duniani.

 

Kwa hivyo Biblia inafundisha kwamba wale walio katika dhambi zao watahukumiwa.  Kila mtu alioko duniani atasimama mbele za Bwana Yesu na atahukumiwa.  Kila mtu, wale wanaishi Afrika na wale  wanaishi ulaya, wale wanaishi Marikani na wale wanaishi Asia, hawa wote watasimama mbele za Bwana Yesu na kuhukumiwa.  Wale waliodai kuwa wakristo na wale waliofuata dini ziangine  za ulimwengu huu watahukumiwa.  Wale wote ambao walikuwa wamesoma sana, matajiri na viongozi wa mataifa watahukumiwa.  Pia wale ambao ni maskini, bila elimu yoyote watahukumiwa.

 

Hakuna hata mmoja ataepuka hukumu wa Mungu.  Wale ambao walisikia neno la Mungu na walikataa kuja kwa Bwana Yesu ili awaokoe, bali waliendelea kuishi maisha yao ya dhambi watahukumiwa kwa sababu ya dhambi zao.  Biblia inasema kuhusu siku  hiyo, kwamba wengi wataiita milima na miamba ili ziwaangukie na kuwaficha kutokana na ghadhabu ya Mwana-kondoo (Ufunuo 6:15-17).

 

Kifungu hiki kinafundisha wazi kwamba wale ambao hawajaokoka watahukumiwa wakati Bwana Yesu atakaporudi.  Pia inafaa tukumbuke kwamba wale ambao wameokoka wataeleza Bwana Yesu jinsi waliishi maisha yao hapa duniani baada ya kuokoka.  Wale ambao wameokoka hawatahukumiwa kwa sababu dhambi zao zimeoshwa kwa damu ya Yesu Kristo (Yohana 1:7) .  Biblia inasema, “Sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu” (Warumi 8:1).  Lakini tukumbuke kwamba Mungu anataka tuishi  maisha matakatifu na tutumie vipawa vyetu kumtumikia katika ufalme wake na kumletea utukufu na heshima hapa ulimwenguni.  Kwa hivyo inafaa tujue kwamba tutahitajika siku ya hukumu kueleza ni namna gani tuliishi maisha yetu hapa ulimwenguni baada ya Yesu Kristo kutuoka.  Hii ndiyo sababu Paulo anasema, “Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya” (2 Wakorintho 5:10).

 

Ni lazima pia tukumbuke kwamba wale  walitumika kama wachungaji na walimu wa neno la Mungu wataeleza jinsi walivyofanya kazi yao.  Biblia inasema, “Ndugu  zangu, msiwe walimu wengi, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi” (Yakobo 3:1).  Hii inamaanisha kwamba wale wanafundisha neno la Mungu watahukumiwa jinsi walivyoishi maisha yao wakiwa wakristo na jinsi walifanya huduma wao wa kufunza neno la Mungu.  Ikiwa hawakufundisha neno la Mungu kwa uaminifu basi wataeleza siku hiyo.

 

3. Jinsi Bwana Yesu atawahukumu wale ambao hawajaokoka siku ya  hukumu.

 

Yohana anasema, “Hao wafu wakahukumiwa sawa sawa na matendo yao  kama yaliyoandikwa ndani ya hivyo vitabu” (Ufunuo 20:12).  Biblia inatueleza hapa kwamba kuna vitabu mbinguni ambavyo vimeandikwa matendo yote ya wale ambao hawajaokoka.  Pia Biblia inatueleza kwamba  kuna kitabu cha uzima ambacho kimeandikwa majina ya wale wameokoka.  Kuhusu hukumu ya wale ambao hawajaokoka, Biblia inafundisha mambo yafuatayo.

 

(i) Matendo yote ya  wale ambao hawajaokoka yatahukumiwa: “Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao.”  Kila jambo ambalo wale ambao hawajaokoka wamewahi kufanya maishani mwao yote yataletwa katika hukumu.  Dhambi ambazo wengi wao waliwaza kuwa dhambi dogo na sisizo na maana zitahukumiwa.  Dhambi ambazo mtu alifanya akiwa mtoto na hata hawezi kuzikumbika pia zitahukumiwa.  Mungu atahukumu dhambi zote za wale ambao hawajaokoka.

 

(ii) Maneno yote ya wenye dhambi yatahukumiwa.  Bwana Yesu alisema, “Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu  watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena.  Kwa maana kwa maneno yako hutahesabiwa haki na kwa maneno yako hutahukumiwa” (Mathayo 12:36-37).  Tunaopaswa kuelewa kwamba hatufanyi dhambi tu kwa matendo pekee, bali pia katika maneno yetu tunafanya dhambi.  Tunaposema maneno ambayo si ya upendo na tunapodanganya, tunafaa kukumbuka hizi ni dhambi kubwa sana mbele za Mungu.  Biblia inatufundisha wazi kwamba wote wale wanaosema uogo wataenda jahanum (Ufunuo 21:8).  Hii ndiyo sababu sisi sote tunapaswa kuwa waangalifu sana kuhusu maneno tunayoongea, tukumbuke kwamba yote yameandikwa na Mungu na atawahukumu wenye dhambi kwa sababu ya maneno  yao.

 

(iii) Siri zote za wale ambao hawajaokoka zitahukumiwa.  Biblia inasema, siku hiyo Mungu atazihukumu siri za mioyo ya wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo(Warumi 2:16).  Kuna dhambi nyingi ambazo tunafanya katika mioyo yetu na ambazo hakuna mtu anajua.  Mwanaume anaweza kuwa na  mawazo ya dhambi baada ya kuona  mwanamke mrembo, pia mtu fulani anaweza kumchukia mwenzake moyoni mwake.  Hizi ni baadhi ya dhambi  ambazo tunafanya lakini hakuna mtu  anatuona, lakini Mungu anaziona na anaziandika  na atawahukumu wenye dhambi kwa sababu ya hizi dhambi za siri.

 

Hivi ndivyo Biblia inafundisha kuhusu siku ya hukumu.  Biblia inatueleza kwamba Bwana Yesu Kristo siku hiyo atawauliza wote ambao wameokoka kueleza jinsi waliishi maisha yao hapa ulimwenguni kutoka wakati ule waliokoka, na pia Bwana Yesu Kristo atazihukumu kazi zote na maneno yote na mafikira yote ya wale ambao hawajaokoka.

 

Ni jambo muhimu kufahamu kwamba katika kifungu hiki cha Ufunuo 20:11-15 kwamba wokovu ni kazi ya Mungu wala si matendo mazuri ya mtu.  Wale ambao hawajaokoka watahukumiwa kulingana na kazi zao ambazo Mungu  ameziandika katika kitabu chake.  Wale ambao wameokoka  hawataingia mbinguni kwa sababu ya matendo yao mazuri, bali ni kwa sababu majina yao yameandikwa katika kitabu cha  uzima.  Hawa wameokoka kwa sababu Mungu alipanga wokovu wao toka milele na kwamba Mungu aliwahakikishia wokovu wao kupitia kifo cha Bwana Yesu msalabani.

 

Funzo la saba, Mathayo 25:46, Hukumu wa milele.

 

Mstari ambao tunaangazia hapa uliandikwa baada ya mfano wa kondoo na mbuzi kupeanwa.  Bwana Yesu Kristo anasema hivi kuhusu wenye dhambi, “Ndipo watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”  Kuna mafunzo mengi ambayo tunasoma katika kifungu hiki kuhusu hukumu wa milele.

 

1.Hukumu wa milele unaanza punde tu baada ya Bwana Yesu kurudi duniani.

 

Biblia inatufundisha jinsi mambo yatakavyofuatana wazi kabisa: kwamba Bwana Yesu atatokea ghafla na atawakusanya watu wote.  Yaani wale ambao wameokoka na wale hawajaokoka, wote watapewa miili mipya na kusimama mbele zake.  Bwana Yesu atawatenganisha wanadamu wote katika makundi mawili, wale ambao wameokoka na wale hawajaokoka.  Bwana Yesu atawakaribisha wale wameokoka kwake na hatawahukumu wale hawajaokoka jahanum milele.  Hii inatufundisha kwamba wakati Bwana Yesu atarudi tena, mara moja atawatuma jahanum wote wale hawajaokoka.

 

2. Hukumu wa milele inamaanisha kutenganishwa na Mungu milele.

 

Bwana Yesu anasema katika mstari huu, “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele.”  Hili ndilo jambo mbaya zaidi kuhusu jahanum, kwamba ni kutenganisha kabisa na Mungu.  Watu wote sasa hapa duniani wako chini ya ulinzi na upendo wa  Mungu.  Hata wale ambao wamekataa kuokoka na hawamwamini Mungu na wanafuata dini za uongo, wote wako katika ulinzi wa neema ya Mungu (Mathayo 5:44-45).  Hii ndiyo sababu wale ambao hawajaokoka wanaishi maisha ya  starehe hapa duniani.  Hii haimaanishi kwamba Mungu anapendezwa nao, lakini ni kwa sababu Mungu amewapa neema yake.  Jahanum hakuna neema ya Mungu.  Jahanum ni mahali ambapo pametayarishwa na Mungu pa kuwaadhibu wenye dhambi.  Neema ya upendo wa Mungu na ulinzi wa Mungu haupo jahanum, na hii inamaanisha kwamba uko watu wanaishi maisha ya dhambi kabisa bila kuzuiliwa na kujizuia.  Hapa duniani, watu ambao hawajaokoka wanaweza kuonyesha huruma na ukarimu kwa wenzao kwa sababu ya neema ya Mungu.  Jahanum hakuna huruma wala ukarimu, ni mahali pa dhambi na giza, na neema ya  Mungu haijulikani huko.

 

3. Jahanum ndiyo mwisho wa wote  ambao hawajaokoka.

 

Wakati watu wale ambao hawajaokoka watatumwa jahanum, hatuna njia yoyote wanaweza kutoka nje.  Hapo ndipo mahali ambapo Mungu amewatayarishia na hapo ndipo wataishi milele.  Kuna watu wengi ambao wanafikiria kwamba baada ya kufa ikiwa hakuwa ameokoka anaweza akapata fursa ya kuokoka na kuingia mbinguni.  Huu ni uongo mtupu.  Ikiwa utakufa kabla hujaokoka, utaenda jahanum milele.

 

4.  Jahanum ni mahali ambapo mateso yake yanafahamika na yule atakayeadhibiwa.

 

Ni lazima tuelewe kwamba jahanum ni mahali ambapo Mungu mwenyewe alitengeneza, na kwamba alitengeneza mahali hapo kwa kusudi la kuwaadhibu wenye dhambi.  Hivi ndivyo Bwana Yesu atawaambia wale hawajaokoka, “Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye  moto wa milele alioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake” (Mathayo 25:41).  Bwana Yesu Kristo anasema kwamba hapa ni mahali ambapo pameandaliwa.  Hii inamaanisha kwamba Mungu aliandaa mahali hapa akiwa na lengo fulani: yaani lengo la kuwaadhibu wenye dhambi.  Biblia inafundisha kwamba Jahanum ni mahali pa mateso na adhabu kwa wenye dhambi.

 

Bwana Yesu alisema kwamba Jahanum ni, “Mahali ambako kutakuwa na kulia na kusaga meno” (Mathayo 24:51), na ni “Mahali ambako funza wake hawafi, wala moto hauzimiki” (Marko 9:48).  Mtume Yohana anaeleza jahanum kuwa ziwa la moto na kiberiti (Ufunuo 20:10;14).  Mistari hii yote inatufundisha kwamba wale wote watakuwa jahanum watapata mateso kwa sababu ya dhambi zao.  Hapa ni mahali ambapo Mungu ameandaa ili awaadhibu wenye dhambi.

 

5. Jahanum ni ya milele.

 

Mtu anapopata shida wakati ako hapa duniani kwa sababu ya ugonjwa ama umaskini, anaweza kufikiria moyoni mwake na kuwaza, “Haijalishi, siku moja nitatoka katika umaskini huu ama ugonjwa huu.”  Lakini hakuna mawazo kama hayo kwa wale watakuwa Jahanum.  Funza wake hawafi wala moto wake hauzimiki (Marko 9:48).  Jahanum ni mahali pa mateso ambayo yanaendelea bila kufika kikomo.

 

Tunaweza kuona sasa ni kwa sababu gani watu wengi hawapendi kuamini mambo ya jahanum hata kufikiria kama jahanum iko.  Mafundisho ya Biblia kuhusu jambo hili ni wazi na yanatisha sana.  Haya si mambo ambayo watu wengi wanapenda kuyafikiria.  Lakini ni lazima tuelewe kwamba Jahanum iko na kwamba wale wanakufa katika dhambi zao wataishi Jehanum milele.  Kwa hivyo njia mzuri ya kushughulikia mafundisho ya Biblia kuhusu Jahanum si kukataa ama kupuuza bali ni kuhakikisha kwamba tumeokoka.  Bwana Yesu anawaalika watu wote waje kwake waokolewe.  Biblia inaeleza  wazi kwamba njia ya wokovu ni kupitia kwa Yesu Kristo.  Wote wale ambao watatubu dhambi zao na kumwamini Bwana Yesu pekee wataokolewa kutoka kwa dhambi zao.  Baada ya kuokoka hawataongopa Jahanum.

 

Funzo la nane, Ufunuo 21:1-5, Mbingu  mpya na nchi mpya.

 

Katika kifungu hiki tunaona ni nini Biblia inafundisha kuhusu makao ya wale wameokoka.  Watu wengi wanafikiria kwamba wale wameokoka wataishi mahali mbali sana paitwao mbinguni ambapo watakuwa na mavazi meupe na kukaa katika mawingu.  Lakini Biblia haifundishi jambo hili.

 

1.Bwana Yesu Kristo ataifanya upya nchi na kamilifu.

 

Katika kifungu hiki cha Ufunuo 21:1-5, mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita na kwamba kutakuwa na mbingu mpya na nchi mpya.  Hivi ndivyo Bwana Yesu atafanya wakati atarudi.  Atatengeneza kila kitu chote kiwe jinsi kilivyokuwa kabla dhambi  kuingia duniani.  Mwanzo Mungu aliumba mbingu na nchi zikiwa mahali pazuri pa mwanadamu kuishi.  Nchi ambayo Adamu na Hawa walimoishi ilikuwa ni nchi kamilifu kabisa bila kasoro yoyote.  Lakini wakati Adamu na Hawa walifanya dhambi Mungu aliilaani ardhi (Mwanzo 3:17).  Mungu ni wa neema na huruma, kwa hivyo hakumwacha mwanadamu aangamie katika dhambi zake.  Mungu alianza mpango wake alioupanga zamani wa kumkomboa mwanadamu na viumbe vyote kutoka kwa matokeo ya dhambi.  Mpango huu wa Mungu hukuwa wa kumwokoa mwanadamu pekee kutoka kwa laana ya dhambi, lakini pia ulikuwa ni mpango wa kukomboa viumbe vyote kutoka kwa laana ya dhambi.  Viumbe vyote vinangojea jambo hili (Warumi 8:20-21).  Kwa hivyo wakati Bwana Yesu atakaporudi, ataondoa laana ambalo Mungu alilaani ardhi na ataifanya nchi hii kama vile ilikuwa   kabla Adamu kufanya dhambi, itakuwa nchi kamilifu na maridadi sana.

 

2. Watu wa Mungu wataishi duniani milele.

 

Biblia inasema katika kifungu hiki, “Nikaona Mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe” (Ufunuo 21:2).  Ni wazi kwamba huu Mji mtakatifu ni kanisa la Mungu, yaani watu wa Mungu wale ambao wameokoka.  Biblia inasema kwamba huu Mji mtakatifu utashuka kutoka mbinguni na kwa Mungu kuishi duniani.  Biblia inafundisha hapa kwamba wote wale walikufa wakiwa wameokoka, ambao sasa wako mbinguni na Kristo watarudishwa hapa duniani na wataishi duniani milele.  Mungu  alipomuuba Adamu na hawa, aliwaumba waishi katika ardhi milele, na hivyo ndivyo itafanyika wakati Kristo atarudi ili akamilishe kazi yake ya wokovu.  Hii dunia itakuwa mahali pakamilifu, bila dhambi na mahali pazuri sana.  Biblia inatueleza vile mambo yatakavyokuwa wakati huo:

 

“Mbwa ataishi pamoja na mwana kondoo, chui atalala pamoja na mbuzi, ndama, mwana simba na ng'ombe aliyenona wa mwaka mmoja watalishwa pamoja, naye mtoto mdogo atawaongoza.  Ng'ombe na dubu wataishi pamoja, watoto wao watalala pamoja na simba atakula majani makavu kama maksai, mtoto mdogo atacheza karibu na shimo la nyoka mwenye sumu kali, naye mtoto  mdogo ataweka mkono wake kwenye kiota cha nyoka mwenye sumu.  Hawatadhuru wala kuharibu juu ya mlima wangu mtakatifu wote, kwa kuwa duniani itajawa na kumjua Bwana kama maji yajazavyo bahari” (Isaya 11:6-9).

 

Hivi ndivyo ardhi itakuwa baada ya Bwana Yesu Kristo kurudi duniani.  Itakuwa ni mahali pakamilifu, mahali pa kupendeza sana na mahali ambapo watu wa Mungu wataishi milele.

 

3.  Mungu ataishi na watu wake milele.

 

Yohana anasema, “Nami nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, 'Tazama, makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao.  Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao” (Ufunuo 21:3).  Mungu alipowaumba Adamu na Hawa alikuwa na ushirika wa karibu sana nao.  Lakini wakati Adamu na Hawa walianguka dhambini, huu ushirika wao na Mungu ulikatika.  Bwana Yesu Kristo atakaporudi duniani, ataifanya hii dunia kuwa kamilifu tena na ataishi na watu wake milele.  Hili ndilo jambo mzuri sana kuhusu nchi mpya, kwamba Mungu mwenyewe atakuwa na watu wake milele kila wakati.  Mungu hatawaacha watu wake kamwe bali atakuwa nao kila wakati.

 

Hii ndiyo sababu katika kifungu hiki Biblia inaeleza kuhusu mbingu mpya na nchi mpya.  Katika hayo maisha mapya, mbingu na nchi hazitengani bali zitakuwa kitu kimoja.  Wakati huu tunaweza kusema kwamba Mungu ako mbinguni na sisi tuko hapa duniani.  Hii ni kwa sababu ya matokeo ya dhambi.  Lakini wakati dhambi na laana yake zitaondolewa, mbingu na nchi zitaungana na kuwa kitu kimoja: mahali Mungu anaishi na pia mahali mwanadamu anaishi.  Hali ya kuwa pamoja na Mungu kila wakati itatuletea furaha na kutosheka.  Ulimwengu na vitu vilivyomo haviwezi kututosheleza, ni Mungu  pekee ambaye anaweza kutujaza, kututosheleza na kutupatia furaha ya milele.

 

4. Hakutakuwa na dhambi katika nchi mpya.

 

Biblia inasema, “Atafuta kila chozi, kutoka katika macho yao.  Mauti haitakuwepo  tena, wala maombolezo,  wala kilio,  wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.” (Ufunuo 21:4).  Biblia inatueleza kwamba wakati dhambi iliingia duniani ilileta mauti na ilifanya maisha kuwa magumu kama tunavyohisi leo.  Biblia inatueleza hivi sivyo Mungu aliumba nchi iwe, haya mambo magumu yalitokea kwa sababu ya dhambi.  Lakini wakati Yesu atakaporudi, atatengeneza nchi hii iwe katika ile hali ilikuweko kabla ya dhambi kuingia.  Hii inamaanisha kwamba mambo kama mauti na maombolezi, maumivu na kilio zitaondolewa milele.  Sisi wale ambao tumeokoka tutapewa miili mipya ya ufufuo ambayo haizeeki, haigojeki ama kufa.  Hii nchi itakuwa mpya na hakutakuwa na njaa ama mafuriko au shida yoyote.

 

Kumbuka wakati Mungu alimuuba Adamu alimpatia kazi afanye (Mwanzo 2:15), na hivi ndivyo tutafanya katika nchi mpya.  Mungu hakumwambia mwanadamu afanye kazi kama hukumu kwa sababu alifanya dhambi bali kazi ni kitu kitakatifu ambacho Mungu alimpatia mwanadamu kufanya.  Kazi ilianza kuwa ngumu kwa mwandamu baada ya dhambi kuingia duniani (mwanzo 3:17-19).  Wakati Mungu ataondoa dhambi ulimwenguni,  kazi itaanza kuwa kitu cha kufurahia sana.

 

Ukweli kwamba Mungu atafanya kila kitu kuwa kipya ni ahadi ya kupendeza sana.  Hii inatuonyesha kwamba wokovu ni jambo kuu sana. Tunapata msamaha wa dhambi zetu zote na tunaungana na jamii ya Mungu.  Zaidi ya haya yote, tumehaidiwa nchi mpya kamilifu ambalo tumetengenezewa na tutaishi na Mungu kila wakati.